Mambo Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha The Warren Buffet Way (Njia za Warren Buffet: Mwenkezaji na Bilionea wa Siku Nyingi)

Habari ya leo rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri.

Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya 33 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi wa vitabu mbalimbali kwa ajili ya kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako kuyatumia ili ubadilishe kila sekta ya maisha yako.

Ni matarajio yangu kuwa makala hizi zimekuwa na msaada mkubwa kwako kwa kadri ambavyo umekuwa ukichukua hatua za kubadilisha maisha yako. Hata hivyo, makala hizi haziwezi kubadilisha chochote kama umekuwa mtu wa kusoma na kutokufanyia kazi yale unayojifunza.  

Ili uendelee kunufaika na makala za mtandao huu BONYEZA HAPA na ujaze fomu kisha bonyeza “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao wa fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.

Kitabu cha wiki hii ni The Warren Buffet Waykutoka kwa mwandishi Robert G. Hagstrom. Kitabu hiki nit oleo la pili na kimeandikwa kuelezea maisha ya bilionea Warren Buffett. Mwandishi anatumia kitabu hiki kutushirikisha mbinu ambazo mwekezaji bilionea Warren Buffet amekuwa akizitumia kukuza utajiri wake. Kwa kifupi kama ni mara yako ya kwanza kusikia jina la Warren Buffet unachotakiwa kufahamu ni kwamba bilionea huyu ni mwekezaji ambaye amewahi kuwa tajiri namba moja wa dunia kwa kipindi kirefu na amekuwa kati ya matajiri watano wanaoongoza kwa muda sasa.

Warren Buffet amekuwa tajiri kupitia uwekezaji katika kampuni yake ya Berkshire Hathaway ambayo inajihusisha na uwekezaji kwenye biashara tofauti. Mwandishi anatumia uzoefu aliopata kupitia ripoti mbalimbali juu ya kampuni ya Berkshire Hathaway na maongezi na watu wa karibu na Warren Buffet kutushirikisha mbinu ambazo zimekuwa zikutumiwa na Warren Buffett kupata mafanikio kiuwekezaji. Kwa ufupi ni kwamba Warren Buffet amekuwa ni mtu ambaye anachukua hatua mapema kama tahadhari dhidi ya nyakati zinazokuja na hivyo nyakati hizo (mbaya au nzuri) zinapowadia zinamkuta ameshajiandaa kiuwekezaji.

Karibu tujifunze wote machache niliyojifunza kwenye hiki:

1. Tofauti na mabilionea wengine Warrant Buffet ni bilionea ambaye amepata utajiri wake kupitia kwenye uwekezaji wa hisa na uwekezaji kwenye makampuni ya bima. Mabilionea wengine katika orodha ya matajiri wakubwa duniani wametengeneza utajiri wao kupitia teknolojia ya computa pamoja na teknolojia ya mtandao. Mfano, wa matajiri hawa ni kama Bill Gates na Mark Zuckerberg. Kupitia kitabu hiki tutajifunza mambo mengi muhimu kuhusu uwekezaji wa hisa. Warren Buffet tunaambiwa kuwa baba yake alikuwa ni dalali wa hisa (stock broker) na huu ulikuwa msingi kwa Warren kuhamasika kwenye uwekezaji wa hisa. Hamasa yake iliongezeka zaidi baada ya kusoma kitabu cha The Intelligent Investor cha Benjamin Graham kiasi ambacho alishawishika kuomba kozi katika Chuo ambacho Profesa Graham alikuwa anafundisha ili aweze kujifunza mengi kutoka kwake. Hii inatufundisha kuwa kama unahitaji kufanikiwa katika sekta uliochagua husichoke kujifunza maarifa mapya kwa njia yoyote ile.

2. Katika kununua hisa za kampuni, Warren Buffett amekuwa akinunua kwa bei ya chini hisa za kampuni ambazo ni rahisi kukadiria ukuaji wa uchumi wake kwa siku zinajazo. Kwa kufanya hivi imekuwa rahisi kwake kununua hisa za kampuni kwa bei ya chini na baada ya muda hisa hizo zinaongezeka thamani na hatimaye anapata faida kutokana na hisa anazomiliki kwenye kampuni husika. Sifa nyingine aliyonayo Buffet katika uwekezaji ni kwamba kamwe hawekezi kwenye biashara ambayo hana uzoefu nayo au haifahamu kwa undani.

3. Uwekezaji wenye tija ni ule ambao kupitia tathimini ya kina unaridhisha uhakika wa mwendelezo wa mtaji/kianzio na uhakika wa faida inayoridhisha.  Huu ni maana ya uwekezaji kutoka kwa Benjamin Graham ambayo Warren Buffett amekuwa akiitumia kuchagua biashara za kuwekeza. Maana hii ina sehemu kuu mbili ambazo katika sehemu ya kwanza unatakiwa kufanya tathimini ya kina dhidi ya kampuni ambayo unahitaji kuwekeza fedha zako – kwa maana unatahiji kuwa na taarifa sahihi za kampuni husika. Sehemu ya pili inakutahadharisha kuwa kabla ya kufanya uwekezaji wowote unatakiwa kujiridhisha kuwa sehemu unayotaka kuwekeza itakuwa salama dhidi ya kianzio/mtaji wako na uhakika wa faida kwa ajili ya kuongeza thamani kile ulichowekeza.

4. Njia nzuri ya kuitathimini kampuni kwa kina ni kuangalia taarifa za kampuni za kifedha kwa kipindi kisichopungua miaka mitano. Kama mapato ya kampuni yamekuwa mara tano au zaidi ya matumizi yote ya mwaka katika kipindi chote cha miaka mitano basi mwekezaji ana uhakika juu ya usalama wa fedha zake.

5. Kwa mujibu wa mafundisho ya Benjamin Graham kuhusu uwekezaji kuna sheria mbili; sheria ya kwanza “kamwe husipoteze” na sheria ya pili kamwe “husisahau sheria ya kwanza”. Kwa kifupi ni kwamba wekeza sehemu ambayo una uhakika na usalama wa fedha zako.

6. Thamani ya uwekezaji inapatikana kutokana mtiririko wa pesa (net cash flows) unaotegemewa kuzalishwa katika kipindi chote cha uwekezaji na mtiririko huo wa fedha ukipunguzwa kwa asilimia ya kiwango cha riba. Hapa kuna vitu viwili vya kujifunza; moja: umuhimu wa mtiririko wa fedha ili ya kutambua thamani ya sasa na ya baadae ya kampuni husika. Kwa upande wa uwekezaji wa hisa njia ya haraka ya kutambua mtiririko wa fedha wa kampuni husika ni kuangalia kiasi cha gawio kwa wanahisa katika kipindi kilichopita. Kwa ufupi ni kwamba hisa ni ya thamani kulingana na kiasi cha gawio ambacho utakipata kwa kila mwaka. Mbili: umuhimu wa kupunguza kiasi cha mtiririko wa fedha ili kutoa nafasi ya hatari (risk) ambazo zinawekuikumba kampuni husika.

7. Muda mzuri wa kununua hisa ni pale wengi wanapouza hisa zao na kuuza pale wengine wanaponunua. Hii ni kutokana na ukweli kwamba katika soko la hisa nyakati ambazo kila mtu anauza ni nyakati ambazo hisa zinauzwa kwa bei ya chini kuliko thamani halisi ya kampuni. Mara nyingi hii huwa inasababishwa na mabadiliko ya ghafla kwenye uchumi. Nyakati kama hizo kwenye soko la hisa wawekezaji wanazitumia kununua hisa za kampuni kwa bei ya chini na baadae kuziuza kwa bei ya juu.  

8. Siri ya mafanikio kibiashara ni rahisi na hii si nyingine bali ni lazima fedha zinazoingia ziwe nyingi kuliko zinazotoka. Mwandishi anatushirikisha kuwa hii ni kanuni ambayo ilimwezesha Warren Buffett kufanikiwa kupitia kampuni zake za bima chini ya umiliki wa kampuni ya Berkshire Hathaway.

9. Biashara ya bima ni kati ya biashara chache ambazo watu wapo tayari kufanya. Warren Buffett ametumia nafasi kumiliki makampuni ya bima kiasi ambacho amefanikiwa kukuza thamani ya kampuni yake Berkshire Hathaway kwenye. Hii inatufundisha kuwa kama unataka kufanikiwa ni lazima uwe tayari kufanya vitu ambavyo sio kila mtu anafanya. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kadri unavyofanya vitu vya kipekee ndivyo unapunguza wapinzani wa bidhaa unayozalisha kwenye soko.
               
10. Kwake Warren Buffett kununua kampuni au kununua hisa za kampuni yoyote vyote ni vinachukuliwa kwa nidhamu sawa kwani kila uamzi unamfanya kuwa mmiliki kamili au sehemu ya wamiliki wa kampuni husika. Kutokana na msimamo huu, tahadhari anazochukua wakati wa kununua kampuni ni zile zile wakati wa kununua hisa kwenye kampuni nyingine. Hata hivyo, kipaumbele chake ni kukunua kampuni pale fursa inapojitokeza ili impe nafasi ya kudhibiti mtaji wa kampuni husika. Pia, pale ambapo hisa zinajitokeza zikiwa na thamani nzuri kiuwekezaji Warren Buffett amekuwa akiwekeza kwenye kampuni zinazomilikiwa na umma kupitia mfumo wa ununuaji wa hisa.

11. Pamoja na kwamba Warren Buffett amekuwa akiwekeza kwenye kampuni nyingi kupitia kampuni yake ya Berkshire Hathaway mara zote vigezo vyake ni vile vile: kuwekeza kwenye biashara rahisi na inayoeleweka, yenye uhakika wa kutengenaza faida, yenye uwezekano wa kufanya vyema kwenye soko la hisa, isiyo na madeni makubwa na ambayo tayari uongozi imara unaoendesha biashara husika. Hizi ini sifa ambazo Warren Buffet anatumia kufanya tathimini kwa kila kampuni ambayo ipo sokoni. Muda wote Warren Buffett anaamini kuwa haina maana yoyote kuwekeza kwenye kampuni au kiwanda ambacho haujui uendeshaji wake. Kwani kwa kufanya hivyo hautaweza kufahamu thamani ya kampuni/kiwanda husika na hivyo kushindwa kufahamu maenedeleo ya kampuni/kiwanda.   

12. Warren Buffett anaamini kuwa biashara bora ya kumiliki ni ile ambayo kwa muda inaweza kuwekeza mtaji mkubwa na kusambaa maeneo mengi huku ikizalisha faida kubwa ikilinganishwa na mtaji uliowekezwa. Ni kutokana na sifa hii, Warren Buffet alishawishika kuwekeza kwa kununua hisa za kampuni ya vinjwaji vya Coca – cola ambayo mpaka sasa imesambaa katika nchi zaidi 195.

13. Unapoenda kuwekeza kwenye hisa nenda na wazo la kumiliki biashara husika. Dhana hii itakufanya kabla ya kuwekeza ufanye upembuzi yakinifu dhidi ya uendelevu wa kibiashara kwa kampuni ambayo unahitaji kununua hisa zake. Warren Buffett amekuwa akitumia msingi huu na hivyo kila kampuni anayonunua hisa zake ni lazima ajione kama yeye ndo mmiliki mkuu wa kampuni husika na hivyo imani yake ni kwamba kuna muunganiko mkubwa kati ya mmiliki wa hisa za kampuni na mwenye kampuni.

14. Mtazamo wa Warren Buffett kwenye mafanikio ya wawekezaji ni “kadri mwekezaji anavyokuwa na taarifa/ufahamu sahihi kwenye biashara aliyowekeza ndivyo alivyo na nafasi kubwa ya kupata mafanikio makubwa kwenye uwekezaji husika. Hapa tunafundishwa kuwa kamwe usikimbilie kuwekeza sehemu ambayo hauna taarifa sahihi au kwenye biashara ambayo hauna ufahamu wa kutosha jinsi ya invyoendeshwa. Pia, unatakiwa kabla ya kuwekeza kwenye kampuni ujiridhishe kuwa kampuni husika itaendelea kufanya vyema kibiashara kwa muda mrefu.

15. Daima husikimbilie kununua hisa au kampuni ambayo inaonekana kufanya vyema kwa muda mfupi badala yake angalia uimara wa kampuni kwa siku za baadae. Mwandishi anatushirikisha kuwa Warren Buffett huwa hanunui hisa/kampuni kwa vile zinafanya vyema kwenye soko kwa wakati huo bali anaangalia mwenendo wa kampuni kibiashara kupitia taarifa za kifedha na matarajio ya kukua kwa kampuni kwa siku za baadae.  Huu ni msingi ambao unamfanya awe na sifa za kipekee kwenye uwekezaji kwani watu wengi huwa wanaongozwa na hisia (hasa tamaa kufanikiwa haraka) kwenye uwekezaji wa hisa. Watu wengi wananunua hisa/kampuni ambazo zinafanya vyema kwenye soko kwa wakati huo wakidhani kwa kufanya hivyo watapata mafanikio ya haraka. na tamaa ya kufanikiwa haraka

16. Kabla ya kuwekeza kwenye kampuni kwa mfumo wa hisa au kununua kampuni husika unahitaji kutathimini umakini wa watendaji wanaoiendesha kampuni kwa wakati huo. Buffett amekuwa na nidhamu ya kuhakikisha kila kampuni ambayo anawekeza fedha zake ni lazima iwe na uongozi imara ambao unatekeleza majukumu yake ipasavyo. Buffet anapenda watendaji ambao wapo tayari kujiona kama wamiliki wa kampuni badala ya kujiona kama waajiriwa tu. Kabla ya kuwekeza kwenye kampuni yoyote Buffet huwa anajiuliza maswali matatu juu uongozi unaoendesha kampuni husika;
     i.  Je uongozi uliopo una uadilifu pamoja weledi/uwezo wa kuchanganua mambo haraka? Hasa matawanjo sahihi wa mtaji kwa ajili uendelevu wa biashara.
    ii.  Je uongozi una uaminifu dhidi ya kampuni pamoja na wateja wa kampuni? na
   iii.  Je uongozi upo tayari kwenda na kasi ya mabadiliko ya soko?

Haya ni maswali ambayo mwandishi anatushirikisha kwa ajili ya kuyatumia katika maamuzi tunayofanya kabla ya kuamua kuwekeza kwenye kampuni yoyote.

17. Njia mojawapo ya kufahamu thamani ya kampuni ni kwa kuangalia mrejesho wa mapato kwa kila hisa uliyowekeza kwenye kampuni husika. Hapa Warren Buffett anachoangalia ni kiasi ambacho kila mwekezaji anapata kutoka kwenye kila hisa aliyowekeza kwenye kampuni husika. Ili kamouni iweze kuwa ni mrejesho wa mapato kwa kila hisa ni lazima kampuni husika isiwe na madeni mengi. Tunachotakiwa kujifunza hapa ni kwamba sio tu kununua hisa za kampuni bali tunatakiwa kabla ya kununua tujiridhishe kiasi kinachotolewa na kampuni husika kama gawio kwa kila hisa inayowekezwa.

18. Uwekezaji mzuri ni ule ambao kila shilingi inayozalishwa na kampuni inaweza kutasiliwa kwenye angalau thamani ya shilingi moja kwenye soko. Maana yake ni kwamba kama kila shilingi inayozalishwa ina thamani ya angalau shilingi moja katika soko tafsili yake ni kwamba thamani ya kampuni husika katika soko inaongezeka kwa kila shilingi inayozalishwa. Somo muhimu ni kwamba kama una biashara unapaswa kuhakikisha kila shilingi ya ziada inayozalishwa na biashara husika ni lazima iwekezwe sehemu ambapo itazalisha thamani shilingi nyingine au zaidi na matokeo yake ni kuongezeka kwa thamani ya uwekezaji wako katika soko. Hakikisha shilingi inazaa shilingi.

19. Bei ni kile unacholipia na thamani inapatakana kwenye kile unachopata. Kwa maana nyingine ni kwamba sio mara zote bei inaonyesha thamani ya kile unachopata. Thamani ya hisa za kampuni zinaweza kubadilika mara kwa mara kwani zinaongozwa na tamaa au hofu ya watu kwenye soko la hisa. Kama mwekezaji unahitaji kuangalia thamani ya kampuni na uzalishaji wake kuliko unavyoangalia thamani ya hisa zake kwenye soko. Watu wa kawaida wanauza au kununua hisa kwa kuangalia bei na thamani ya hisa za kampuni husika. Wawekezaji makini kama Buffett wanachoangalia ni kabla ya kununua ni:
     i.  Kutambua thamani halisi ya kampuni husika pamoja na uzalishaji wake badala ya kuangalia thamani ya hisa zake kwenye soko; na
    ii.  Kununua pale ambapo biashara inauzwa kwa bei punguzo kuliko thamani yake halisi.

20. Warren Buffet amekuwa akinunua hisa, dhamana (bonds) au kampuni katika bei ya punguzo na kusubilia mpaka pale bei inapokuwa imepanda anaziuza kwa faida. Hii imenfanya kuwa mwekezaji mkubwa kuliko wote katika uso huu wa duniani kwa kipindi kirefu. Hapa tunachojifunza ni kuhakikisha tunakuwa macho muda wote kwa ajili ya kuchangamkia fursa zinazojitokeza.

21. Kila mwekezaji ana staili yake ya uwekezaji kwani wapo ambao wananunua hisa za kila kampuni ambayo inaonekana kufanya vyema kwenye soko. Warren Buffet staili yake ni kutuliza rasilimali zake kwenye kampuni chache ambazo zinaonesha kuwa na matarajio ya kudumu kwenye biashara kwa muda mrefu na zinaendeshwa na watendaji wenye weledi wa kutosha kwenye tasnia ya biashara na uwekezaji kwa ujumla.

Haya ni machache ambayo nimeweza kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.

Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.

PATA UCHAMBUZI WA KITABU CHA THE RULES OF MONEY ( KANUNI ZA PESA)
 
Mwandishi Richard Templar katika kitabu hiki ametushirikisha kanuni 107 ambazo kila mtu anaweza kuzitumia kutengeneza pesa na hatimaye kuwa tajiri. Uchambuzi wa kina wa kanuni zote (107) umeandaliwa kwa mfumo wa pdf na unapatikana kwa gharama ya Tshs. elfu tano tu (5,000/=). Kanuni zote zimechambuliwa na kuandaliwa kijitabu kidogo chenye kurasa 39 ambazo unaweza kusoma kwenye simu ya mkononi (smart phone) au kwenye kompyuta (pc).

Kupata uchambuzi wa kanuni zote tuma pesa yako kwa njia ya M-pesa au Airtel Money kupitia namba zifuatazo:-

M – Pesa tumia namba: 0763 745 451 (Majina ni Augustine Mathias)
Airtel Money tumia namba: 0786 881 151 451 (Majina ni Augustine Mathias)

Baada kutuma pesa hiyo nitumie ujumbe kwenye namba ya airtel (0786 881 151 451) ukiwa na barua pepe yako ili nikutumie uchambuzi wa kanuni hizi moja kwa moja kwenye mtandao wako.

UTAJIRI NI HAKI YAKO YA KUZALIWA "BEING RICH IS YOUR BIRTH RIGHT"


Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.

Born to Win ~ Dream Big 

Augustine Mathias Bilondwa

Namba ya Simu:      +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com


onclick='window.open(