Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri.
Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa
FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa
ni wiki ya 35 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi
wa vitabu mbalimbali kwa ajili ya kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako
kuyatumia ili ubadilishe kila sekta ya maisha yako.
Ni matarajio yangu kuwa makala hizi
zimekuwa na msaada mkubwa kwako kwa kadri ambavyo umekuwa ukichukua hatua za
kubadilisha maisha yako. Ili uendelee kunufaika na makala za mtandao huu BONYEZA HAPA na
ujaze fomu kisha bonyeza “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu.
Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja
kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “Rising A Positive
Kid in A Negative World” kutoka
kwa mwandishi na mhamasishaji mahiri Zig
Ziglar. Zig Ziglar ameandika vitabu vingi vikiwemo vya masuala ya ukuaji wa
mwanadamu, uongozi, mauzo, kiroho, familia na mafanikio kwa ujumla. Baadhi ya
vitabu vingine vya Ziglar ni pamoja na See
You at the Top, Courtiship After Marriage, Secrets of Closing the Sale, Success
for Dummies na Confessions of a
Grieving Christian. Vitabu hivi pamoja na audio zake vimekuwa vikifanya
vyema kwenye soko na vimetafsiliwa katika lugha nyingi kwenye nchi tofauti
tofauti.
Katika
kitabu hiki mwandishi anatushirikisha namna kumkuza mtoto katika mtazamo chanya
japo anazungukwa na ulimwengu uliojaa maovu. Mwandishi anatushirikisha kuwa
mtazamo chanya na tumaini jema ni msingi mkuu wa maisha kwani maisha bila misingi
hii ni sawa na mhusika amekufa. Ni kutokana na tumaini ili jema tunasema kuwa
watoto ni taifa la kesho. Hata hivyo, ili watoto hawa wawe na matunda bora kwa
taifa la kesho ni lazima wazazi watambue wajibu wao katika hatua mbalimbali za
ukuaji wa mtoto.
Wajibu
wa kwanza ambao mzazi anatakiwa kutimiza ni kuwa na mtazamo chanya au matumaini
mema dhidi ya mtoto wake mdogo hata kama bado ni mdogo kwa umri. Kila mzazi
anapaswa kumtazama mwanae mdogo kwa maono ya kuwa mtoto bora, mbunifu, mtiifu
au mwenye bidii ya mafanikio kwenye kila sekta ya maisha yake pindi atakapokuwa
mtu mzima. Hivyo sisi kama wazazi tunapaswa kwa ujasiri (a) kuona picha ya watoto
wetu mdogo akikuwa kupitia hatua zote za ukuaji na hatimaye kuwa mtu mzima
kiroho na kimwili; na (b) kuhakikisha mtoto huyu anafundwa ili mtu mzima mwenye
mtazamo chanya.
Kwa
ujumla malezi ya mtoto yanajumuisha viungo muhimu ambavyo ni haki ya mtoto
kutoka kwa wazazi wake, viuongo hivi vinajumuisha upendo, nidhamu, kusamehe na
furaha. Viungo hivi kwa ujumla wake vinahitaji mzazi awe tayari kumtunza,
kumjali na kumfariji kwa ajili ya hustawi bora wa mtoto wake.
Karibu
tujifunze wote machache niliyojifunza kwenye hiki:
1. Kila mtoto ndani yake kuna upendo, tumaini, akili, utu, uaminifu na sifa
nyinginezo. Mzazi ana jukumu kubwa la kumtazama mwanae kwa jicho la ndani ili
afanikiwe kutambua sifa hizi kwa mwanae na hatimaye amwongoze mtoto huyu katika
kuendeleza sifa hizi kwenye kila hatua ya maisha yake. Kwa bahati mbaya sana
katika ulimwengu wa sasa wazazi wengi wanakosa muda wa kutosha kwa ajili ya
kugundua kalama za watoto wao ili waziendeleze kwa manufaa ya maisha ya baadae
ya watoto wao.
2. Kuna kanuni mbili ambazo kila mzazi anaweza
kuzitumia kumkuza mtoto wake katika mtazamo chanya; Moja, upo jinsi
ulivyo na sehemu ulipo kutokana na yale
ambayo umekuwa ukiingiza kwenye ubongo wako (mfumo wa fikra) na unaweza
kubadilisha jinsi ulivyo na sehemu ulipo kama utabadilisha yale yanayoingia
kwenye fikra zako. Fikra zao zina athari ya moja kwa moja kwenye utendaji
kazi wako. Mbili, maisha siyo
rahisi kama inavyodhaniwa – ni magumu, magumu sana. Na hii ni sahihi kwa
kila mtu pasipo kujali nafasi yake kiuchumi au kijamii. Ili kuwa na mafanikio
katika maisha, watoto na wazazi wao ni
lazima waishe kwenye ulimwengu huu mgumu. Ili kuuishinda ulimwengu huu mgumu ni
wote kwa pamoja waisha maisha yenye nidhamu na uadilifu dhidi ya nafsi zao. Kama
una nidhamu binafsi muda wote katika maisha yako itakuwa rahisi kufanikisha
jambo lolote. Mzazi ana wajibu wa kumfunda mwanae ili awe na nidhamu binafsi
tokea akiwa na umri mdogo kinyume chake ni kwamba atafunzwa na ulimwengu.
3. Mafanikio
hayaji kirahisi ni lazima uweke utaratibu ambao utaufuata kwa nidhamu ya hali
ya juu katika kipindi cha maisha yako. Mwandishi anatushirikisha kuwa kila
mzazi anatamani mwanae awe na kila ya mafanikio katika maisha yake. Hata hivyo,
ni wazazi wachache ambao wapo tayari kuwekeza kwa ajili ya kukuza talanta za
watoto wao. Matokeo yake ni kwamba watoto wanafundwa na ulimwengu ambao mara zote
hauna njema dhidi yao. Kumbe tunakiwa kufajifunza kuwa kama unahitaji kuwa baba/mama
bora ni lazima uwe tayari kujifunza mbinu muhimu zitakazokuwezesha kufikia nia
yako.
4. Epuka
maongezi hasi dhidi ya mwanao na dhidi ya nafsi yako. Mwandishi anatushirikisha
kuwa hatua ya kwanza ya kumfunda mwanao katika mazingira chanya, mzazi mara
zote unatakiwa kuepuka kauli hasi. Hata hivyo, kauli hasi zimekuwa ni sehemu ya
mazingira na jamii tunayoishi kutokana na ukweli kwamba hata misamihati mingi
au majina ya baadhi ya vitu/watu wana maana hasi.
5. Tofauti
na zamani ulimwengu wa sasa umejaa kila aina ya maovu. Maovu haya ni pamoja na ubakaji,
madawa ya kulevya, ulevi, mauaji, wizi, mapenzi ya jinsia moja, ulafi, ufisadi,
picha za ngono na vibaka. Haya ni maovu ya dunia ambayo kama mzazi unatakiwa
kumlinda mwanao ili hasije akaharibiwa na walimwengu.
6. Uovu
mkubwa wa dunia ya sasa umekuwa ukisambazwa kupitia miziki na filamu ambazo zinauzwa
katika maeneo mengi ya jamii. Mwandishi anatushirikisha kuwa maneno yanamfanya
mtu ajenge picha kwenye mfumo wa akili yake na hatimaye kusukumwa kutekeleza
yale ambayo amesikia au kuona kwenye mziki au filamu. Mbaya zaidi wazazi
wamekuwa wakiwapata watoto wao fedha kwa ajili ya kununua CD za miziki au
filamu pasipo kuwapa mwongozo juu ya miziki/filamu zipi wanatakiwa
kusikiliza/kuona na zipi hazifai kwa ajili ya maadili mema. Hii ni kutokana na
ukweli kwamba mziki una nafasi kubwa ya kutawala ulimwengu kuliko kitu chohote
kile.
7. Uwepo
wa TV katika familia nyingi pia ni chanzo cha kueneza maovu ya ulimwengu wa sasa
kwa watoto wadogo. Familia nyingi zimekuwa na utaratibu wa kuwaacha watoto wao
waangalie vipindi vya TV vinavyorushwa bila ya wazazi kudhibiti ni vipindi
watoto hawatakiwi kuviangalia. Mbaya zaidi vipindi vingi vya TV vinarushwa muda
ambao wazazi pengine hawapo karibu na watoto wao. Matokeo yake watoto wanaanza
kuiga yale wanayoona kwenye michezo mbalimbali ya TV. Pia, TV imekuwa ni chanzo
cha kupoteza muda kwa watoto wetu ambavyo muda huo ungetumika kwa ajili ya
kuwekeza kwenye mbinu za kuongeza motisha binafsi ya mtoto au mzazi, ubunifu wa
akili pamoja na kuwekeza kwenye maisha ya watu wengine.
8. Wazazi
wanahitaji kutenga muda kuwafariji watoto wao pale ambapo watoto kwa bahati
mbaya wanaangukia kwenye maovu ya dunia hii. Katika kipindi kama hicho wazazi
wanatakiwa kuwa karibu na watoto wao huku wakionesha huruma waliyonayo kwa
matatizo yanayowakumba watoto wao. Katika kipindi kama hiki wazazi wanahitaji
kuwasikiliza watoto wao ili watambue ni hasa mahitaji yao kwa ajili ya kurudi
kwenye maadili mema. Hivyo kama mzazi unatakiwa kujipanga kwa ajili ya kutoa
msaada wa kimawazo, kimalezi na kiuchumi.
9. Muda
wote wazazi wanapaswa kulenga kuwa na mafanikio yaliyojikikta kwenye kila sekta
ya maisha yao. Mafanikio haya yanapaswa yalenge ukuaji wa kiroho, kijamii
(maadili bora ndani ya familia) na kiuchumi. Haina maana kama mtu atasema
amefanikiwa kiuchumi au kitaaluma huku watoto wake wakiwa wezi, mateja, walevi,
machangudoa au vibaka. Kwa ujumla hapa tunahitaji kutambua kuwa kama wazazi
pamoja na majukumu ambayo tunaangaika nayo kila siku ni lazima tutenge muda kwa
ajili ya kuwa karibu na watoto wetu. Hii itasaidia kutambua nyakati wanazopia
watoto wetu kwenye kila hatua ya maisha yao.
10. Wazazi ni nguzo namba moja ya kufunda watoto
wao kuliko kundi lolote lile katika jamii. Hii ni kutokana na ukweli kwamba
mtoto ana muda mwingi wa kukaa na wazazi kuliko muda anaotumia kukaa na walimu
wake. Hivyo mzazi ni mtu wa kwanza wa kulaumiwa pale mtoto anapokuwa na tabia
mbaya katika jamii inayomzunguka.
11. Jenga msingi imara wa maadili mema kwa
mwanao tokea akiwa bado mdogo. Njia rahisi ya kufanya hivi ni kuhakikisha mzazi
unaishi kile ambacho kila mara unawahubiria watoto wako. Kama unahitaji wanao
wawe na maadili mema lakini wewe hauna maadili hayo itakuwa vigumu sana watoto
hawa kufuata kile unachofundisha. Mfano, kama kila mara unawafundisha watoto
wako kuwa waaminifu lakini pale inapotekea mtu anagonga mlangoni unawaambia
wamwambie kuwa baba/mama katoka, hii inawafanya watoto wajenge picha ya kuwa
waongo dhidi ya wazazi wao na jamii inayowazunguka.
12. Familia ni kiwanda cha malezi na makuzi
bora kwa watoto na sehemu inayobakia inajaziliziwa na taasisi za elimu/dini. Kwa
maana hii wazazi ndani ya wanapaswa kuwapa watoto msingi imara wa maadili mema.
Hata hivyo, mwandishi anatushirikisha kuwa taasisi za elimu zina wajibu mkubwa
wa kudhibiti nidhamu ya wanafunzi pamoja na kwamba taasisi hizi zimeshidwa
kutekeleza wajibu huu katika siku za karibuni. Hali hii inamfanya mzazi
aendelee kupambana kuboresha nidhamu ya mwanae pasipo kujali ngazi ya elimu
aliyopo (kuanzia elimu ya msingi hadi elimu ya chuo). Hii ni pamoja na kujenga
sifa ya uaminifu kwa watoto hawa tokea wakiwa wadogo.
13. Mtoto mwenye mtazamo chanya ni lazima afundishwe
tabia ya kukubali majukumu. Tabia hii mtoto anatakiwa afundishwe toka akiwa
bado mdogo hasa kupitia kazi za kila siku nyumbani kuanzia usafi wa
nyumba/mazingira na maandalizi ya chakula. Kila mtoto ndani ya familia
anatakiwa kufahamu majukumu yake ni yapi kila iitwapo leo na pale ambapo
anashindwa kutekelezwa akumbushwe. Bahati mbaya ni kwamba vijana wengi siku
hizi wamelelewa katika mazingira ambayo yanawafanya wakwepe majukumu muhimu ya
maisha yao na hivyo wanasubiria msaada kutoka nje kwa ajili ya kufikia hatua
wanazokusudia. Hali hii imefanya makundi mengi ya vijana kuwa tegemezi na walalamikaji.
14. Mtoto afundishwe umuhimu wa kujenga
jina lake kupitia nidhamu, uadilifu na uaminifu. Mwandishi anatushirikisha kuwa
mtoto anapofundishwa umuhimu wa kukuza thamani ya jina lake hasa kupitia uaminifu
wa kila anachofanya inamjenga kiakili na hatimaye mtoto huyu anakuwa kwenye
nafasi ya kutambua kuwa majina yetu yanakuwa na thamani kupitia matendo yetu ya
kila siku. Hivyo, mtoto anatakiwa kujengewa nidhamu, uadilifu na uaminifu toka
akiwa bado mdogo kwenye masuala ya shule, kijamii na kiuchumi.
15. Mara nyingi sifia mambo mema
yanayofanywa na watoto wako. Kumsifia mtoto pale anapofanya vyema ni jambo ambalo
linaacha alama ndani ya mtoto husika kutamani aendelee kufanya vyema. Hii ni
njia pekee ambayo imeonesha kujenga hamasa ndani ya watoto. Hapa mzazi
anahitaji kuwa msikilizaji ili aweze kutambua mambo mema kutoka kwa watoto
wake.
16. Kama mzazi ili uwaze watoto wako katika
mtazamo chanya wewe binafsi unapaswa uwe na hamasa/msukumo pamoja na fikra
chanya. Unahitaji kutambua kuwa hamasa pamoja na fikra chanya ni lazima viwe sehemu
ya maisha yako ya kila siku na wala sio suala la kuhamasika au kuwa na fikra
chanya kulingana na matukio. Hamasa pamoja na fikra chanya vinahitaji kuwa
sehemu ya maisha yako kuanzia kwenye mfumo wa fikra, matendo yako na kufanya
hivyo utapa faida wewe mzazi pamoja na familia yako kwa ujumla. Hii ni kutokana
na ukweli kwamba fikra chanya zitakuwezesha kufanya vitu katika ubora wa hali juu
kwenye kazi zako za kila siku.
17. Fikra chanya na fikra hasi kamwe
haziwezi kufanya kazi kwa wakati mmoja. Ni lazima aina moja ya fikra ipite
nyingine na hatimaye fikra hizo zitapelekea matokeo hasi au chanya kulingana na
wapi mhusika anawekeza muda mwingi kufikria.
18. Hamasa ni kitu ambacho kama mzazi
unatakiwa kutambua kuwa watu wengi wanapata hamasa kwa muda na baadae kurudia
kwenye hali yao ya awali. Mwandishi anatushikisha kuwa ili uendelee kuhamasika
mara kwa mara unahitaji kujifunza kutoka kwa watu wanao kuhamasisha kutokana na
historia ya maisha yao au mafanikio yao. Kazi ya hamasa ni kukupa nguvu ya
kuendelea kusonga mbele, kuhitaji kufanikiwa zaidi na kukupa tumaini jipya la
kufanikisha malengo yako.
19. Wajengee hamasa na motisha wanao kwa
kuwaulizia yale ambayo watoto wanapenda zaidi. Mara nyingi wazazi huwa wana
tabia ya kuwauliza watoto wao yale ambayo yamejiri kwa muda ambao hawakuwa
pamoja. Hata hivyo wengi huwa wanapendelea kuulizia yale ambayo wanahisi ni ya
muhimu kwao na hivyo kusahau mtoto amefurahishwa na yapi katika matukio ya siku
nzima. Hivyo, badala kuulizia wamefundishwa nini shuleni, mzazi unaweza kuuliza
ni kipi mtoto amependa zaidi kati ya yale aliyofundishwa katika siku husika. Hii
inamfanya mtoto awe na hamasa/motisha ya kuhitaji kuendelea kujifunza zaidi.
20. Zoezi la kumfundisha mtoto kuwa na
mtazamo chanya linapaswa kuanza tokea mtoto akiwa bado mtoto mdogo. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba watoto wanajifunza vitu vingi katika umri mwako ziro
mpaka miaka mitano. Hata hivyo, katika umri wowote ule mzazi husichoke
kumfundisha mwanao kwani hakunaga msemo wa nimechelewa pale unapolenga
kutekeleza jambo jema.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
|
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com