Mambo Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha Strong Mothers, Strong Sons: (Mama Bora, Mtoto wa Kiume Bora; Mwongozo kwa Akina Mama katika Kuwakuza Vyema Watoto wa Kiume)

Habari ya leo rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya 23 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi wa vitabu nikiwa na lengo kubwa la kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako kuyatumia ili ubadilishe kila sekta ya maisha yako.

Uamzi wa kubadilisha maisha yako upo mikononi mwako na hivyo kama mpaka sasa haujajifunza kitu chochote katika makala hizi nakushauri husiendelee kupoteza muda wako na badala yake ufanye mambo ambayo umezoea.

Ili uendelee kunufaika na makala za mtandao huu BONYEZA HAPA na ujaze fomu utakuwa umejiunga na mtandao wa fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa na mtandao wa fikra za kitajiri moja kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.

Kabla ya kuendelea kushirikisha uchambuzi wa kitabu cha leo nitumie muda huu kuomba radhi kwa kuchelewa kukutelea uchambuzi huu ndani ya wiki iliyoisha jana. Hii imetokana na sababu zilizo nje ya uwezo wangu kwa kuwa mazingira niliyopo kwa sasa hayana nishati ya umeme ya uhakika.

Kitabu cha wiki hii ni Strong Mothers Strong Sonskutoka kwa mwandishi Meg Meeker, M.D. Mwandishi Meg Meeker ni daktari wa binadamu na mzungumzaji/mhamasishaji mashuhuri kwenye masuala ya afya pamoja na uhusiano kati ya wazazi na watoto. Dr. Meg Meeker ni mama wa watoto watoto watatu ambapo kati yao wawili ni wa kike na mmoja ni wa kiume. Mwandishi ana uzoefu wa maisha ya ndoa kwa vile amefanikiwa kuishi na mme wake kwa zaidi ya miaka 30. Dr. Meg Meeker pia ni mwandishi wa Kitabu cha Strong Fathers, Strong Daughters ambacho anashirikisha nafasi ya baba katika kumuandaa mwanae wa kike ili awe mtoto bora na hatimaye mama bora kwa familia yake.


Mwandishi anatushirikisha kuwa shauku kubwa ya kuandika kitabu hiki ilitokana na uzoefu wake katika jamii kuwa akina mama wengi na watoto wao wa kiume wameingia kwenye mahusiano mabaya ya kutoelewana kwa vile hawatambui wajibu wao katika malezi ya watoto wa kiume. Mwandishi anatushirikisha kuwa mara nyingi akina mama wamekuwa na hasira na jinsia ya kiume kutokana na matendo maovu au manyanyaso ambayo wamewahi kutendewa na wanaume katika maisha yao. Hali hii imewafanya kupitisha hasira zao kwa watoto wao wa kiume pasipo wao kuelewa na matokeo yake watoto wanaanza kubadilika na kuwachukia mama zao. Hii inapelekea mtoto kubadilika kitabia kiasi ambacho hataki kusikiliza ushauri wa mama au baba.

Mtoto wa kiume anapokuwa katika hali kama hii inakuwa ni hatari zaidi kwake kutokana na ukweli kwamba; watoto wa kiume wana uwezekano wa kuwa na ulemavu wa kujifunza (kushindwa kujifunza) mara sita zaidi ikilinganishwa na watoto wa kike, ni mara tatu zaidi ya kujiunga kwenye vikundi vya madawa ya kulevya na mara nne zaidi ya kutambuliwa kama watoto wenye msongo wa mawazo.

Pia, watoto wa kiume wapo kwenye hatari kubwa ya kutawaliwa na tabia za wizi, ngono, ulevi, kukojoa kitandani, kujihusisha na makosa ya jinai na wapo kwenye asilimia kubwa ya kukumbwa na ajali za barabarani.  Yamkini ni akina mama wachache ambao wanafahamu kuwa wao ni nguzo namba moja katika kumkinga mwanae wa kiume dhidi ya tabia chafu na hatimaye kumkuza mwanae katika ili awe baba bora wa familia. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mama ana muda mwingi wa kuwa karibu na mtoto ikilinganishwa na baba. Katika kitabu hiki mwandishi anatoa mwongozo kwa akina mama kwa ajili ya kufanikisha malezi bora kwa watoto wa kiume.

Karibu tujifunze wote machache niliyojifunza kutoka kitabu hiki:

1. Wewe ni mtu wa kwanza wa kumuonyesha upendo. Mara nyingi ni kawaida kuona kuwa upendo wa mama kwa mtoto wake wa kiume haupimiki kwani mwanae ni zaidi ya mme wake. Ni kutokana na ukweli huu, katika kipindi cha ukuaji wa mtoto wa kiume, mama ana wajibu wa kuonesha kila aina ya upendo kwa mwanae na pengine akina mama wengi huwa wanatamani kuwa upendo huo uwe wa milele japo kutokana na maumbile ya kisayansi mtoto wa kiume anapopata mwenzi wake upendo wake kwa mama huwa unapungua. Katika kipindi hiki cha ukuaji mtoto wa kiume mara zote anaendelea kujifunza kutoka kwa mama yake ikiwa ni pamoja kuhitaji kila aina na faraja, furaha, hamasa na amani kutoka kwa mama yake. Hali hii inampa msingi bora katika maisha yake ya baadae dhidi ya mwenza wake na wanawake wote kwa ujumla na kinyume chake ni sahihi. Hii inatokana na ukweli kwamba akina mama wana muunganiko wa hisia mkubwa kwa watoto wao ikilinganishwa na akina baba.   

2. Mama hakikisha unampenda mwanao hata katika kipindi ambacho unaona tabia zake haziridhirishi. Mwandishi anatushirikisha kuwa mama ana nafasi ya kumrudisha mwanae wa kiume katika misingi ya tabia njema kama ataendelea kuonesha hali ya upendo kwa mwanae. Mara zote katika kumlea mtoto wa kiume mama unatakiwa kufahamu kuwa watoto wa kiume siyo wepesi wa kuzungumza matatizo yanayowakabili hivyo njia ya pekee ni kuhakikisha unamfahamu mwanao kwa undani zaidi. Wazazi wengi wameharibikiwa na watoto wao wa kiume kwa vile wametekeleza pindi wanapoona wamejiingiza katika makundi ya tabia mbaya. Kumbe wazazi wanasahahu kuwa katika kipindi hiki mzazi hasa mama anatakiwa kuonyesha upendo wa hali ya juu kwa mwanae wa kiume ikiwa ni pamoja na kumsaidia kuepukana na tabia mbaya au changamoto zinazomkabili. Hapa unatakiwa kukumbuka kuwa upendo wa mama kwa mwanae haupimiki wala kulinganishwa kulingana na hali iliyopo. Hii ndio njia pekee ya mtoto wako kuona kuwa anapendwa na ana wajibu wa kulipa upendo huo kwa wazazi wake kwa gharama yoyote.

3. Mama anapaswa kumfundisha mwanae misingi mitano ya fadhila ambayo ni (i) ujasiri – uwezo wa kufanya kitu kwa haki pasipo kujali wengine wanasema nini juu yake (ii) kiasi – uwezo wa kufanya vitu kwa kiasi pasipo kutawaliwa na tamaa za mwili (iii) haki – kufanya vitu pasipo kuvunja sheria au kuwaumiza wengine (iv) busara – uwezo wa kuishi maisha ya staha na tahadhari katika matendo, na (v) hekima – kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi makini pale inapotakiwa. Hivi ni vipaji ambavyo kila mama anapaswa kuhakikisha mwanae wa kiume anavipata kwani vipaji hivyo ni msingi wa mtoto kutambua yeye ni nani hasa katika kuishi maisha ya usafi wa moyo pamoja na kutambua kusudi la maisha yake. Na kadri mtoto atavyofundishwa vipaji hivi akiwa bado mdogo ndivyo atakuwa katika maisha ya furaha. Na hapa mtoto anatakiwa kufundishwa juu ya upendo kwa wengine kwa maana ya kwamba baada ya kupendwa na yeye anatakiwa kutambua wajibu wa kupenda wenzake na jamii kwa ujumla.

4. Mama mara zote kumbuka kuwa maneno mabaya unayonena kwa mwanao yaanacha makovu yasiyoponyeka. Kama ambavyo tumezoea kusikia sentensi ya “maneno uumba”, ndivyo mwandishi anatushirikisha kuwa endapo mtoto mara nyingi ataambiwa misamihati mibaya kama vile wewe ni mkorofi, mgomvi, mwizi, mchoyo, mjinga, mpumbavu na mengineyo ndivyo atakuwa akiamini kuwa hizo ndizo tabia zake halisi. Kutokana na ukweli huu mama ana nafasi ya kumjenga mtoto wa kiume kutoka kwenye tabia hasi kwa kumnenea misamihati yenye kumtia moyo mtoto ili abadilishe tabia zake kwa kadri anavyoongezeka umri.

5. Mama unahitaji kukumbuka kuwa una wajibu wa kumfundisha mwanao wa kiume misamihati ya hisia. Hapa tunafundishwa kuwa mama ana nafasi kubwa ya kutambua hisia za mtoto wa kiume kuliko ilivyo kwa baba mtoto. Hii ni pamoja na kutambua nyakati za furaha, hasira, msongo wa mawazo, huzuni au kuumizwa ambazo mwanae anapitia. Kutokana na ukweli huu, mwandishi anatushirikisha kuwa mama anapaswa awe mwalimu kwa mwanae wa kiume katika kumfundisha namna bora ya kutumia misamihati ya hisia. Hii ni pamoja na kumfundisha mwanae kutambua hisia zinazomkabili, jinsi ya kuonesha/kukabiliana na hisia husika pamoja na kumfundisha hatua zipi achukue kwa kila hisia pasipo kuumiza nafsi yake na jamii inayomzunguka. Mtoto ambaye amefundwa katika misingi hii ana nafasi kubwa ya kukabiliana na misukosuko ya mazingira yanayomkabili bila kukata tamaa.

6. Mama una nafasi kubwa ya kutatua hisia za mwanao wa kiume hasa ambazo zinapelekea aishi maisha ya huzuni unaosababishwa na historia ya maisha ya familia. Katika familia nyingi ni kawaida kukuta watoto wanateseka hasa kutokana na matendo ya wazazi wao ambayo pengine huwa yanapelekea wazazi kutalikia. Mwanandishi anatushirikisha kuwa watoto wa kiume mara nyingi huwa wanaumizwa na matendo ya baba zao kutokana na tabia mbaya za baba kiasi ambacho huwa wanaishi katika maisha ya upweke pamoja na kutokujiamini. Mama ana nafasi kubwa ya kuwajengea uwezo wa kukabiliana na tabia hii kwa kutumia maongezi ya mara kwa mara na mtoto wake. Katika maongezi haya mama anatakiwa afahamu chanzo halisi cha hisia zinazomkabili mwanae na hatimaye aanze kumsaidia kuepukana nazo kwa kadri awezavyo. Zoezi hili unatakiwa kulifanya mtoto angali bado mdogo.

7. Mara zote epuka kumkanya mwanao kwa kumpiga na badala yake unatakiwa umpe uelewa wa kwa nini hatakiwi kurudia makosa aliyofanya. Unapomuelewesha mtoto kwa njia hii inamsaidia kutambua kuwa alichofanya sio sahihi na hakikubaliki katika jamii. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mtoto wa kiume katika umri mdogo anakuwa hana uwezo wa kujidhibiti dhidi ya hisia zake kama vile hasira ambazo mara nyingi huwa zinamfanya apigane na wenzake. Hivyo, ili kuachana na tabia hii mtoto anahitaji kufundishwa kuwa anaweza kuishi na wenzake kwa upendo na anapotambua hili huwa inamjenga kisaikolojia na hivyo inakuwa sio rahisi kurudia makosa yake.

8. Tofauti kati ya mtoto wa kiume na mtoto wa kike ni kwamba watoto wa kike ni wazungumzaji wazuri wakilinganishwa na watoto wa kiume. Kutokana na ukweli tunashirikishwa kuwa watoto wa kiume ni wasiri wa matatizo yanayowakabili jambo ambalo hupelekea kugundua matatizo waliyonayo wakati yamekuwa sugu. Mwandishi anatushirikisha kuwa mama ana nafasi kubwa ya kutambua matatizo anayopitia mwanae wa kiume kwa kuhakikisha amejenga utaratibu wa kufanya mahojiano na mwanae mara kwa mara. Ili kufanikisha zoezi hili mama anatakiwa kujifunza kuwa msikilizaji badala ya kuwa mwongeaji. Kadri atakavyomsikiliza mwanae ndivyo atamfahamu kwa undani na hatimaye pindi mwanae anapokuwa katika hali tofauti inakuwa rahisi kumgundua mapema.

9. Ulimwengu umebadilika kiasi ambacho kuna kila aina ya uozo kama vile mapenzi ya jinsia moja kwa wanaume. Mwandishi anatushirikisha kuwa watoto wengi wa kiume wameangukia kwenye uozo wa namna hii kwa vile wazazi wengi hawana utaratibu wa kuwafahamu kwa undani watoto wao. Hali hii imepelekea watoto kugunduliwa wakati ambao tayari wameshaharibiwa. Kama mama ni lazima ufahamu kwa undani mwanao anapendelea michezo ya aina gani, sehemu anazopendelea kwenda, mapito yake wakati wa kwenda au kutoka shule pamoja na kuwafahamu kwa undani marafiki zake. Pia, mara nyingi unatakiwa kufahamu kuwa mtoto atabadilisha hobi kwa kadri siku zinavyoongezeka hivyo kadri anavyobadilisha hobi zake ndivyo unatakiwa kufahamu hobi zake mpya. Kwa ufupi; mama kwa kushirikiana na baba mna wajibu wa kumlinda mtoto dhidi ya maovu ya dunia hii na njia pekee ya kufanya hivyo ni kufahamu yapi anapendelea na yapi hapendelei.

10. Mambo ambayo yanakwamisha ukaribu wa mtoto na mama yake ni pamoja na ubize wa kufuatilia TV, kuchati kwenye mitandao ya kijamii, kuwa mkali pindi mtoto anapohitaji kuwa karibu na wewe au kumkatisha mtoto wakati anapokueleza jambo flani. Mwandishi anatushirikisha kuwa mama unahitaji kufahamu kuwa kadri mtoto wa kiume anavyokatishwa au kukosa muda wa kuwa karibu na wewe ndivyo itakuwia vigumu kumfahamu mwanao. Kama kweli unahitaji kuwa mama bora kwa mwanao wa kiume huna budi kuhakikisha unatenge muda wa saa moja kila siku kwa ajili ya mazungumzo na watoto wako hasa wa kiume. Saa moja au dakika chache kila siku zinaweza kubadilisha maisha ya mwanao kwa ujumla endapo umezitumia bila ya kuwa na mwingiliano wa majukumu mengine.

11. Kumbuka kuwa aibu kwa mwanao ni chanzo cha kutofahamu matatizo yanayomkabili. Mwandishi anatushirikisha kuwa kadri mtoto wa kiume anavyoongezeka umri ndivyo anapitia mabadiliko makubwa ya kimwili na tabia ikiwa ni pamoja na kuingia kwenye mahusiano. Muda huu mama unahitaji kuwa shupavu kumweleza ukweli juu ya mahusiano na watoto wa kike ili atambue mahusiano yapi yanamfaa. Hata hivyo ni akina mama wachache wenye ujasili wa kuzungumza na watoto wao wa kiume masuala ya kimahusiano hasa kwa kuzingatia tofauti za jinsia. Pamoja na tofauti hizo bado mama unatakiwa kutafuta lugha nzuri ya kumfunda mwanao kwenye masuala ya mahusiano pamoja na undani wa mapenzi.

12. Mama mpe hamasa mwanao kushiriki mazoezi ya viungo. Mazoezi ni njia nzuri ya kumfanya mwanao wa kiume hasiwe na muda wa kufanya au kuangalia vitu vya hovyo kwenye mtandao wa intaneti. Mwandishi anatushirikisha kuwa kadri kijana wa kiume anavyokaa bila mazoezi ya viungo ndivyo anavyokuwa anatengeneza nguvu ambazo ni sawa na bomu ambalo litalipuka wakati wowote. Na mara nyingine bomu hilo huwa linalipuka kwenye matumizi mabaya ya nguvu zake ikiwa ni pamoja na kujihusisha kwenye masuala ya ngono, ulevi au madawa ya kulevya. Kutokana na ukweli huu mama huna budi ya kuhakikisha mwanao ana ratiba ambayo haimpi muda wa kukaa kizembe pasipo kuwa na shughuli anayojihusisha nayo.   

13. Kuna muda ambao mama mwanao wa kiume atakutangazia uadui kati yake na wewe. Mara nyingi ugomvi huu huwa unaanza katika kipindi cha kubarehe kwa vile mtoto anakuwa katika hali ya kulinda maovu yake ili yaonekane ni kitu cha kawaida kwa mama yake. Hii inatokana na mabadiliko ya tabia anayopitia katika ukuaji wake. Hata hivyo, katika nyakati hizi mama hautakiwi kukata tamaa dhidi ya mwanao kwani ndani ya uadui huo kuna tumaini ndani yake endapo hautanyosha mikono dhidi ya mwanao. Katika hali hii, mama unatakiwa kwanza ufahamu mazingira anayopitia mwanao ikiwa ni pamoja na kutambua kuwa hata kama akisema kuwa hufahi kuwa mama yake bado haina maana kuwa ameondoa penzi lako kwake.

14. Watoto wa kiume wana tofauti ya kimaumbile na kimajukumu ikilinganishwa na mama zao. Mama anatakiwa kutambua kuwa mtoto wa kiume anafahamu tofauti iliyopo dhidi ya mama yake hata akiwa na umri mdogo wa miaka miwili. Kutokana na tofauti hizi kadri mtoto wa kiume anavyoongezeka umri ndivyo ukaribu wake na mama unavyozidi kupungua. Matokeo yake ni kwamba kadri umri unavyoongezeka ndivyo mtoto wa kiume anahitaji afanye maamuzi yake pasipo kuingiliwa na mama yake akidhania kuwa yeye ni mwanaume na anaweza kufanya jambo lolote bila ya ridhaa ya mtu mwingine. Kutokana na ukweli mama unahitaji kutambua tofauti hizi za asili na kuhakikisha unatafuta njia nzuri za kuendelea kumfunda mwanao katika hali tulivu.

15. Kuna umri ambao mama unahitaji kumfanya mwanao aondoe hisia zake kwako. Mara nyingi tumezoea kusikia msemo wa “mtoto wa mama”, hapa ndicho mwandishi anatushirikisha kuwa kama mtoto wa kiume ataendeleza hisia zake kwa mama itamuwia vigumu kudumu na mwenza wake katika maisha yake ya baadae. Hivyo, kama mama unatakiwa kumuongoza mwanao katika kipindi hicho cha mpito kwa ajili ya kufanikisha maisha yake ya baadae ili hatimaye mwanao awe baba bora wa familia yake.

16. Mama ni faraja kwa mwanae wa kiume. Hii haijalishi mwanao ana umri gani kwani katika kila hatua mtoto wa kiume anahitaji faraja kutoka kwa mama yake. Hata katika nyakati ambazo atakuwa ameoa bado mtoto wa kiume anahitaji faraja ya mama yake. Hii inatokana na ukweli kwamba katika ukuaji, mtoto wa kiume kuna mambo mengi ya kipekee ambayo uyapata kutoka kwa mama kiasi ambacho hawezi kuyapata sehemu yoyote ile. Kwa ufupi ni kwamba mama afananishwi na mtu mwingine na hivyo huu ni muunganiko tosha wa faraja ya mama kwa mtoto wa kiume katika kipindi chote cha maisha ya wawili hawa.

17. Wewe ni sehemu pakee ambayo mwanao wa kiume atapa msingi/mizizi imara. Kumbuka kuwa kama nyumba imejengwa juu ya msingi imara daima itadumu na kinyume chake ni kwamba kama nyumba imejengwa juu ya msingi dhaifu haiwezi kudumu. Pia, tunaweza kusema kuwa mama ni mhusika mkuu wa kuandaa mizizi imara ya mwanae wa kiume. Kumbuka kuwa kama mmea hauna mizizi imara hauwezi kustawi wakati wa dhoruba kama jua kali au wakati wa upepo mkali. Mwandishi anatushirikisha kuwa mama ni muhusika mkuu wa kumuandaa mwanae wa kiume ili apate kila aina ya mafanikio katika jamii inayomzunguka pasipo kujali changamoto atakazokabiliana nazo.

18. Mama ana nafasi kubwa ya kumfanya mtoto wa kiume atambue kusudi la maisha yake. Kumbuka kuwa watu wengi wapo jinsi walivyo kutokana na mchango mkubwa wa makuzi na malezi waliyopata katika enzi za ukuaji wao. Kwa maana hii, mama ana nafasi kubwa ya kumuongoza mwanae ili atambue wajibu wake katika ulimwengu huu. Mara nyingi baba huwa ni rahisi kumuongoza mwanae katika kazi zile ambazo sana sana zinahusisha matumizi ya nguvu ambazo pia utegemea majukumu ya baba. Lakini kwa upande wa mama wewe una nafasi kubwa ya kumuandaa mwanao katika ulimwengu wa kiakili, kiroho na kijamii. Hii haimaanishi kuwa baba hapaswi kujihusisha katika kumuandaa mwanae katika sekta hizi bali ukweli huu unatokana na maumbile ambayo akina mama wamejaliwa kuwa na hisia nyingi ikilinganishwa na akina baba. Hivyo mama una wajibu wa kutumia hisia zako kuhakikisha unamfunda mwanao kuwa hakuja duniani humu kwa bahati mbaya bali amekuja kukamilisha kazi ya wito wake. Hivyo kama mama bora hakikisha unamsaidia mwanao atambue vipaji vyake na namna ya kutumia vipaji hivi ili maisha yake yawe na msaada kwa jamii inayomzunguka.

19. Mfundishe mwanao misingi ya maisha kama vile kukubalika, kusamehe na kuvumilia. Kama ambavyo tunafahamu kuwa katika ulimwengu huu siku zote mambo hayawezi kwenda kama tunavyotarajia kwani kuna nyakati mambo yataenda kinyuma na matarajio. Mama unahitaji kumfunda mwanao wa kiume ili siku zote afahamu wazi juu ya ukweli huu na hatimaye abadilike kulingana na hali iliyopo. Hii ni pamoja na kumfundisha mwanao kuwa na roho ya kusamehe na kusahau kwa ajili ya kutoa nafasi ya kuanza upya katika maisha yake.

20. Mfundishe mwanao wa kiume kuwa kuna nguvu kubwa kuliko viumbe vyote kwa maana ya elimu ya dini. Mwandishi anatushirikisha kuwa mtoto wa kiume anahitaji kujifunza juu ya uwepo wa Mungu kutoka kwa mama yake. Mfanye mwanao aisome sura ya Mwenyezi Mungu kutoka kwenye uso wako. Kama wewe ni furaha muda wote mtoto atajua kuwa Mwenye Mungu ni mwingi wa furaha na hatimaye mtoto huyu naye atatamani kuwa na furaha kama Mungu alivyo. Kumbuka kuwa kama wewe unabadilika badilika mara kwa mara ndivyo mwanao atatafsri kuwa na Mungu yupo katika hali kama hiyo. Hapa una jukumu la kumfundisha mwanao kadri atavyokuwa anaoongezeka umri juu ya ukamilifu wa Mungu.

21. Kadri mwanao anavyoongezeka umri unahitaji kumsaidia kujibu maswali juu ya uwepo wa Mwenyezi Mungu. Kutokana na asili ni kawaida kukuta kuwa watoto wanauliza hivi Mungu yupo? Je Mungu anafanana je? Je mungu anapenda watoto? Mungu anakaa wapi? Haya ni baadhi ya maswali ambayo mara nyingi kila mtoto anatamani kufahamu kwa ajili kumfahamu Mungu kwa undani. Kama mzazi unahitaji kutumia muda wako kumpa majibu ya maswali kwa kadri atakavyokuwa anakuuliza. Majibu ya maswali haya yanamjengea msingi imara mwanao kwenye misingi ya imani na hatimaye kumfahamu na kumtumikia Mwenyezi Mungu.


Haya ni machache ambayo nimeweza kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.

Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.

Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.

Born to Win ~ Dream Big 

Augustine Mathias Bilondwa

Namba ya Simu:      +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com

Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com
onclick='window.open(