Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa
ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI
kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya 19 katika
kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi wa vitabu nikiwa na
lengo kubwa la kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako kuyatumia ili ubadilishe
kila sekta ya maisha yako.
Uamzi wa kubadilisha maisha yako upo
mikononi mwako na hivyo kama mpaka sasa haujajifunza kitu chochote katika
makala hizi nakushauri husiendelee kupoteza muda wako na badala yake ufanye
mambo ambayo umeyazoea.
Ili uendelee kunufaika na makala za
mtandao huu BONYEZA HAPA na
ujaze fomu utakuwa umejiunga na mtandao wa fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na
mtandao huu utapata makala zinazochapishwa na mtandao wa fikra za kitajiri moja
kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “Strong Fathers,
Strong Daughters” kutoka
kwa mwandishi Meg Meeker, M.D. Mwandishi Meg Meeker ni daktari wa binadamu na
mzungumzaji/mhamasishaji mashuhuri kwenye masuala ya afya pamoja na uhusiano
kati ya wazazi na watoto. Dr. Meg Meeker ni mama wa watoto watoto watatu ambapo
kati yao wawili ni wa kike na mmoja ni wa kiume. Mwandishi ana uzoefu wa maisha
ya ndoa kwa vile amefanikiwa kuishi na mme wake kwa zaidi ya miaka 30.
Kwa
ujumla mwandishi Dr. Meg Meeker anatumia nafasi yake kutushirikisha kuwa kama
baba una nafasi kubwa ya kubadilisha maisha ya mtoto wako wa kike ikiwa ni
pamoja na mtazamo wake juu ya wanaume wote. Wewe ni chujio namba moja na kubwa
kuliko chujio zote ambazo zinaweza kuchuja tabia za mwanao wa kike. Pamoja na
nguvu kubwa uliyonayo katika kumkuza vyema mwanao wa kike ni lazima kwanza
utambue kuwa mwanao wa kike anahitaji ukaribu wako wa karibu. Pia, ni lazima
utambue kuwa mtazamo na meneno unayonena kila mara kwake juu ya wanaume ndo yanamjenga
kwa ajili ya kuwa mtoto bora wa kike na hatimaye kuwa mama bora au kinyume
chake.
Karibu
tujifunze wote machache niliyojifunza kutoka kitabu hiki:
1. Wewe
ni mfano na mwakilishi wa wanaume wote kwa mwanao wa kike. Mwandishi anatushirikisha
kuwa mtoto wa kike katika enzi zake za ukuaji mwanaume wa karibu yake ni baba
yake mzazi. Kama baba una tabia mbaya kwa mke wako itapelekea mwanao wa kike
ajenge sura mbaya dhidi ya wanaume wote jambo ambalo litamfanya awe na msingi
mbaya wa maisha yake ya baadae. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wewe kama baba
ni mwanamme wa kwanza wa kuwa karibu nae katika enzi za utoto wake. Kwa maana
hiyo kama wewe ni mkalimu mwanao atakuwa na picha ya kuwa wanaume wote ni
wakalimu, kama wewe ni mwenye upendo vivyo hivyo atategemea wanaume wote kuwa
na upendo na kama una tabia mbaya ndivyo atakavyojenga hisia juu ya wanaume
wote.
2. Kila
siku unaporudi nyumbani hakikisha unamuona binti yako ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha unajidhirisha na mwonekano wake kwa siku hiyo. Hapa mwandishi
anatushirikisha kuwa kila unapokuwa na binti yako hakikisha unatumia muda huo
kumfundisha ujuzi wowote ikiwa ni pamoja na makuzi na tamaduni bora ambazo
atazitumia kama mwongozo katika ukuaji wake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba
kila muda binti yako atakuwa anajifunza mengi kutoka kwako hivyo ni muhimu
kuhakikisha kila siku unampa muda wa kuwa naye. Katika muda huu ni lazima
utambue kuwa majibu yako kwake ndo yataamua kiwango cha uwezo wa kujiamini na
kujiona kuwa yuko vizuri kwenye jamii na kazi zake kwa ujumla.
3. Muda
wote unatakiwa kutambua kuwa wewe na binti yako mnaunganishwa na upendo wa baba
na mwana. Kwa mantiki hii ni lazima utambue kuwa kadri utakavyoonesha upendo
kwake kama baba ndivyo ataendelea kutambua kuwa wanaume ni watu wenye wema,
upendo, busara, hekima na wapole. Hii itakuwa ni mchango mkubwa katika maisha
yake ya ndoa kwani ataanza maisha haya akiwa na mtazamo mzuri kwa mwenza wake.
4. Binti
yako muda wote anakuona shujaa wake katika kila hali anayokutana nayo. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba muda wote mwanao anakuona wewe ni mkubwa na mwenye
nguvu kuliko kitu chochote kile au mtu yeyote yule. Ile aendelee kukuona shujaa
ni lazima uhakikishe unalinda heshima yako kwake ikiwa ni pamoja na kuwa
mwanifu katika ahadi zako. Kwa kufanya hivyo utamfanya binti yako ajione mwenye
amani, furaha na upendo. Hata hivyo wengi wameshindwa kuwa shujaa kwa binti zao
kwa kudhania kuwa ili uwe shujaa ni lazima uwe na akili sana au uwe na pesa
nyingi jambo ambalo ni potofu. Ushujaa pia unategemea na jinsi ambavyo unazuia
jazba zako pale mwanao anapokwenye kinyuma na taratibu.
5. Katika
jamii imekuwa ni kawaida wanaume kupenda watoto wa kiume kuliko watoto wa kike.
Hii ni pamoja na kuhitaji watoto wa kiume wafanye vyema kwenye masomo ya
sayansi ikilinganishwa na watoto wa kike. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika
jamii ya sasa ni muhimu kuhakikisha binti yako unamuandaa kwa ajili ya kufanya kazi
yoyote ile inayoonekana ni nzuri kwa watoto wa kiume. Mfano, muandae binti yako
kwa ajili ya kufanya vyema kwenye masomo ya sayansi, sanaa au biashara. Njia bora
ya kumjengea uwezo binti yako ili afanikiwe sawa na watoto wa kiume ni kumshirikisha
mara kwa mara kwenye kazi zako au kufanya kazi zako akiwa anashuhudia jinsi
unavyotekeleza majukumu yako. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kadri
unavyomuhusisha kwenye zako ndivyo anatambua thamani yako kwake na wanafamilia
wengine. Hata hivyo ni muhimu kutambua kuwa watoto wa kike wanapenda wanaume
wachapa kazi hivyo ni muhimu kama baba ufahamu ukweli huo na ujitahidi kufanya
kazi kwa bidii kwa manufaha ya familia yako.
6. Binti
yako anaona wewe ndo kiongozi bora na mwenye uzoefu kuliko mtu yeyote yule. Kwa
mantiki hii mwanao anahitaji kujifunza kutoka kwako mbinu za uongozi na wewe
kama baba una wajibu mkubwa kuhakikisha unakuwa kiongozi bora wa familia. Katika
karne ya sasa unaweza kujifunza vitu vingi kwa kutumia simu yako, hivyo ni
muhimu kutumia muda wako kujifunza namna ambavyo unaweza kuwa baba na mwanaume
bora katika familia yako na jamiii inayokuzunguka. Hapa ni lazima ukubuke kuwa
kiongozi bora anatoa viongozi bora pia, hivyo, kama utakuwa na misingi ya
uongozi bora katika familia yako ndivyo utafanikiwa kuwalea wanao kwenye
misingi ya uongozi bora.
7. Watoto
wa kike wanahitaji kupendwa na kujali. Mwandishi anatushirikisha kuwa kama baba
ni lazima utambue kuwa kila mara binti yako anahitaji upendo wako katika kila tukio
la maisha yake. Hivyo ni muhimu kutenga muda wa kumpongeza pale anapofanya
vizuri na pale anapoenda kinyume na taratibu tafuta namna bora ya kumkanya ili
hasiojione mnyonge wa nafsi. Unapofanya matendo ya kuonesha kuwa unamjali na
kumpenda moja kwa moja anatambua kuwa ndani ya nafsi kuna nafasi kwa ajili yake
ajambo ambalo linampa nguvu ya kufanya vyema zaidi.
8. Tofauti
na upendo wa binti kwa mama yake, mtoto wa kike anajua kuwa upendo wa baba
kwake unatafutwa. Mwandishi anatushirikisha kuwa watoto wa kike akilini mwao
wanajua kuwa upendo wa mama upo muda wote ikilingaishwa na upendo wa baba. Kutokana
na ukweli huu baba una wajibu wa kuhakikisha unaonyesha matendo ya upendo kwa
wanao ili ufanikiwe kupata upendo wao kama ilivyo kwa mama. Hii ni pamoja na
kumwambia mwanao kwa nini unampenda kwa maana unatakiwa utumie mbinu ambazo zitaonesha
kuwa thamani yake kwako haina kipimo wal ukomo.
9. Wewe
ni wa kipekee kwa mwanao wa kike. Mwandishi anatushirikis kuwa kila mara binti
yako anavyokuona moja kwa moja anaona sifa tofauti na zile anazoziona kutoka
kwa mama yake. Hii ni kuanzia kwenye sauti, ngozi, ndevu, nywele na mwonekano
wako kwa ujumla. Kwa mantiki hii binti yako anategemea apate matendo ya kujali
kutoka kwako kuliko ilivyo kwa mama yake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba
mtoto wa kike anapokuwa mikononi mwa baba yake anajisikia mwenye amani kuliko
akiwa na mama yake. Upendo huu wa baba na binti yake hauna ukom o hata pale
ambapo atakuwa ameolewa bado nafasi ya baba yake itakuwepo kwenye nafsi yake. Japo
unatakiwa kutambua kuwa nafasi hiyo itakuwepo endapo tu ulimpenda katika enzi
za utoto wake, kinyume chake ni kwamba kama ulimfanya akuchukie katika enzi hizo,
chuki hiyo itakuwepo enzi za maisha yake yote.
10. Mfundishe binti yako tabia ya kujithamini,
unyenyekevu na heshima kwa jamii inayomzunguka. Mwandishi anatushikisha kuwa
jukumu la kuhakikisha mtoto wa kike anaishi maisha yenye tabia njema lipo
mikononi mwa baba. Hii ni kutokana na ukweli kuwa binti ambaye amelelewa katika
misingi ya kujithamini na unyenyekevu anaweza kufanya vyema katika mazingira
yoyote yale pasipo kutegemea uwepo wa wazazi wake. Sifa pekee mtoto mnyenyekevu
ni kutambua kuwa yeye sio bora kuliko wengine na wala wengine sio bora au
wabaya kuliko yeye. Kwa mantiki hii mtoto mnyenyekevu ana sifa ya kuishi na
watu wa kila aina kwenye jamii.
11. Tambua kuwa kila unalofanya binti yako
yupo pembeni kujifunza au kuigiza matendo yako. Mwandishi anatushirikisha kuwa
kama baba unatakiwa kuwa makini kwa kila tukio unalofanya mbele ya mwanao. Kwa ujumla
mwanao ana shauku kubwa ya kujifunza kutoka kwako hivyo kama haupo makini na
matendo yako atajifunza tabia mbaya ambazo zitaharibu maisha yake kwa ujumla. Kutokana
na ukweli huu ni kawaida katika jamii kukuta mtoto anafanya vyema kwenye
taalamu au tasnia ya baba yake kwa vile alikuwa anafuatilia kwa makini shughuli
za baba yake. Vivyo hivyo, mwanao anahitaji ajifunze sifa za kujithamini,
unyenyekevu na heshima kutoka kwako. Kama wewe hauna sifa hizo moja kwa moja mwanao
nae atafuata nyayo zako.
12. Kumbuka kuwa kama wa baba hakuna kazi
ngumu kama kumfanya mtoto afanye au awe na tabia zile ambazo wewe unazitaka. Mara
nyingi katika jamii ya sasa utandawazi umetawala kiasi cha kuvuruga akili ya
watoto wa jinsia zote. Kama baba unatakiwa ufahamu kuwa una wajibu kuhubiri na
kusimamia tabia njema kwa mwanao mpaka pale ambapo utaona amefikia viwango
unavyovitaka. Kama baba unahitaji kuhakikisha binti yako anafikia viwango vya
kuwa binti mwenye kupendeza, kujitambua, kujiamini, ana akili ya maisha,
mcheshi na mwenye hekima, busara na heshima. Njia bora ya kufikia viwango hivi
ni kuboresha ukweli na uwazi kati ya baba na binti yake, na katika kila hatua
ya makuzi unayomfundisha mwanao hakikisha inakuwa sehemu ya furaha, upendo na
amani kati yenu wawili.
13. Fahamu kuwa wewe una nguvu kubwa ya
kumlinda binti yako dhidi ya maovu mengi ambayo yanaendelea kuitawala jamii ya
sasa. Mwandishi anatushirikisha kuwa kinachozuia akina baba wengi kuwalea vyema
binti zao ni kutawaliwa na hofu ambayo inawafanya kuona mauvu ya dunia ya nguvu
kubwa kuliko wao. Hili ni kosa kubwa kwani unapokili udhaifu huu haitakuwa kazi
rahisi kusikilizwa na binti yako. Ni lazima utambue kuwa una mamlaka yenye
nguvu ya kila aina ya kumlinda binti yako ili aishi maisha unayoyataka wewe. Kama
baba hakikisha unatimiza wajibu wako na sehemu nyingine mshirikishe Mwenyezi
Mungu katika kuhakikisha binti yako anakuwa kwenye misingi imara.
14. Kumbuka kuwa binti yako anapitia katika
nyakati toafauti za ukuaji wake. Kuna nyakati ambazo fikra zake zitakuwa
zimetawaliwa na namna gani anaweza kuwavutia vijana wa kiume wa umri wake na
hivyo atawekeza nguvu nyingi kwenye jinsi gani anaweza kuwa mdada mrembo. Kama baba
unapaswa utambue kuwa katika nyakati kama hizo unapaswa kumpa mwongozo wa namna
ambavyo anatakiwa awe makini na matendo yake. Mfundishe zaidi juu ya tabia za
wanaume na tumia nafasi hiyo kumfundisha namna ambavyo anaweza kuvaa nguo zenye
heshima na ambazo hazitawatamanisha wanaume. Kwa kufanya hivyo utamlinda mwanao
dhidi ya vishawishi vingi kutoka kwa wanaume. Hata hivyo katika kipindi hiki
unatakiwa kuzidisha ukaribu wako kwa binti yako ili uendelee kufahamu ni nini
nahitaji kwa wakati huo.
15. Kumbuka kuwa nyakati zimebadilika. Zamani
ilikuwa binti hawezi kufanya tendo la kujamiana mpaka pale atakapoolewa. Lakini
siku hizi watoto wadogo wanaingia kwenye mahusiano wakiwa bado shule za
msingi/sekondari na mara nyingi mahusiano ya namna hii hayadumu. Mwandishi anatushirikisha
kuwa kama baba una nguvu kubwa ya kumuongoza binti yako katika kipindi hiki
kigumu. Hii ni pamoja na kuhakikisha unajenga ukuta imara wa msimamo wake juu
ya ngono. Hata hivyo, baba wengi wamekuwa ni waoga kwa binti zao linapokuja
suala la kuwafundisha juu ya mahusiano ya ngono katika umri mdogo. Hali hii
imepelekea watoto wa kike waharibu usichana wao na hatimaye kujikuta kwenye
wakati mgumu na hapa ndipo baba zao wanashutka wakati wameshachelewa.
16. Akina baba wengi wanaishi kwa wasiwasi
juu ya watoto wao wa kike katika umri wa elimu ya sekondari au elimu ya juu. Wasiwasi
huu unatokana na hofu ya binti wao kubeba mimba, kujiingiza kwenye makundi
mabaya au kuanzisha ulevi na uvutaji wa bangi. Mwandishi anatushirikisha kuwa
njia pekee ya kumkinga mwanao dhidi ya makundi haya ya kidunia kumfundisha
namna ya kupanua uwezo wake wa kufikri kwa kina. Katika zoezi hili unatakiwa umfundishe
atambue ni kwa nini anaamini katika misingi flani na kisha awe tayari kudumu
katika misingi hiyo pasipo kusimamiwa na mtu yeyote. Misingi hii ni lazima
ijikite kwenye viwango vya mila na desturi, kiakili, kihisia na kiroho. Na vyote
kwa pamoja ni lazima vilenge kumwezesha binti yako atambue kusudi la maisha
yake.
17. Jenga tabia ya kuingilia kati pale mambo
yanapokuwa magumu kwa binti yako. Hii ni kutokana ukweli kwamba katika akili ya
binti wako yeye anafahamu kuwa wenye ni mwelevu na mwenye nguvu kuliko mtu
yeyote yule. Hiyo kutokana na mtazamo wake pale unapoingilia kwa ajili ya
ushauri, moja kwa moja anatumia ushauri huo kwa mapana yake. Hata hivyo ni
lazima umfundishe binti yako kuhakikisha anatumia neon HAPANA pale inawezekana.
Katika mazingira yote umfundishe binti yako kusimama imara katika kila aina ya
changamoto inayomkabili.
18. Kuna tofauti kubwa kati ya mwanamke na
mwanaume kwa namna wanavyokabiliana na changamoto. Mwanaume anapokutana na
changamoto hatua ya kwanza kabisa ni kufikiria chanzo chake na hatimaye
kutafuta suluhisho la changamoto husika. Mwanamke mara baada ya kukutana na changamoto
cha hatua ya kwanza kabisa anaanza kutafuta nani wa kumlahumu kutokana na
tatizo husika na mara nyingi hataki kujishughulisha kutafuta suluhisho lake. Uwezo
huu wa kipekee wa kukabiliana na changamoto pasipo kuathirika kihisia ni nyenzo
muhimu kwa baba katika kumsaidia binti yake kwenye changamoto zinazomkabili. Pia
unaweza kutumia uwezo huu kutambua hali inayomkabili binti yako ambayo pengine
mwenza wako hajaweza kuitambua.
19. Ishi sifa zote za mwanaume ambaye
unataka amuoe binti yako. Mwandishi anatushirikisha kuwa baba ana nafasi kubwa
ya kumfanya binti yake achague sifa za mwanaume bora kwa kuangalia sifa za baba
yake. Hapa tunajifunza kwamba ni muhimu sana kuishi maisha yenye kila aina ya
upendo kwa mwenza wako ili binti yako ajifunze kutokana na uimara wa ndoa yenu.
20. Mpe binti yako mwongozo wa namna ya
kumpata mwenza wake ambaye atadumu naye. Hii ni kutokana na ukweli kwamba baba
ana uwezo kuona vitu vingi kwa mtu ambaye anataka kumuoa binti yake tofauti na
binti yake anavyoweza kumtazama mwenza wake mtarajiwa. Mwandishi anatushirikisha
kuwa katika enzi kuingia kwenye uchumba mabinti wengi wanatawaliwa na hisia juu
ya mwenza wake badala ya kuangalia sifa muhimu ikiwa ni pamoja na kumchunguza
kwa undani mwenza wake. Kwa mantiki hii, baba ana jukumu kubwa la kumchunguza
kijana anayetaka kuingia kwenye mahusiano na binti yake na pale inapobidi
atumie mbinu bora kumshawishi binti yake kufanya maamuzi sahihi.
21. Kumbuka kumlea mtoto wa kike inahitaji
uvumilivu na ubunifu wa hali ya juu. Mwandishi anatushirikisha kuwa kumlea
mtoto wa kike ni sawa na moyo wako utolewe na uwe unatembea nao mikononi mwako.
Ni lazima utumie mbinu zote kuhakikisha unalinda moyo wako ili watu wasije
wakauharibu. Vivyo hivyo ndivyo ilivyo kwa mtoto wa kike, kadri anavyozidi
kukua na kupendeza ndivyo anavyotolewa macho na kila mtu. Wapo wenye nia nzuri
lakini mara nyingi wengi wao ni waharibifu na hivyo unahitaji kuwa karibu sana
na binti yako kwa ajili ya kumsaidia kama baba.
22. Jifunze kuwa na maonge magumu na binti
yako juu ya ngono, imani, Mungu na kifo. Mwandishi anatushirikisha kuwa hizi ni
kati ya sekta ngumu ambazo baba anatakiwa kumfundisha binti yake na hatimaye wote
kwa pamoja wakawa na uelewa mmoja. Pamoja na ugumu wake baba ni lazima uwe
tayari kuhakikisha binti yako anapata dozi ya kutosha kwenye kila sekta husika.
Wote tunafahamu kuwa endapo atapa dozi ya kutosha kwenye kumjua Mungu itakuwa
kubadilisha mtazamo wake kwenye sekta nyingine za maisha yake.
23. Akina baba wengi wameshindwa
kuwafundisha binti zao juu ya Mungu kwa vile hawaamini juu ya uwepo wa Mungu au
hawatambui umuhimu wa Mungu. Hata hivyo wengi katika nyakati ngumu za maisha
yao au maisha ya wapendwa wao huwa wanakili juu ya uwepo wa Mwenyezi Mungu. Kwa
maana hii baba unatakiwa kumfundisha mwanao wa kike kuwa Mungu yupo na miujiza
yake inafanya kazi ndani mwetu kila iitwapo leo. Hii ni njia pekee ya kumkuza
mwanao katika misingi ya imani na kadri atavyoimarika katika misingi hii ndivyo
itakuwa ni mwongozo katika maisha yake ya baadae.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Ukurasa wetu wa facebook: Fikra za Kitajiri: Fikri na Kutenda Kitajiri: Elimika na Tajirika
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com