Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri.
Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa
FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa
ni wiki ya 34 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi
wa vitabu mbalimbali kwa ajili ya kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako
kuyatumia ili ubadilishe kila sekta ya maisha yako.
Ni matarajio yangu kuwa makala hizi
zimekuwa na msaada mkubwa kwako kwa kadri ambavyo umekuwa ukichukua hatua za
kubadilisha maisha yako. Hata hivyo, makala hizi haziwezi kubadilisha chochote
kama umekuwa mtu wa kusoma na kutokufanyia kazi yale unayojifunza.
Ili uendelee kunufaika na makala za
mtandao huu BONYEZA HAPA na
ujaze fomu kisha bonyeza “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao wa
fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa
humu moja kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “Uongozi Wetu na
Hatima ya Tanzania” kutoka
kwa ambacho kiliandikwa na hayati Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere. Linapotajwa jina la Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere katika ardhi ya Tanzania ni wazi kuwa kila mmoja anafahamu na kuheshimu
mchango wake katika maendeleo na ustawi wa taifa uhuru, lenye amani na
mshikamano la Tanzania. Wote tunafahamu mchango wa Mwalimu Nyerere katika Muungano
wa Tanzania na Zanzibar. Hii ni kutokana Mwalimu Nyerere kuwa na fikra pevu
ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa hata katika kipindi
ambacho yeye kwa sasa ametangulia mbele za haki.
Kitabu
hiki Mwalimu alikiandika mwaka 1994 katika kipindi ambacho taifa lilikuwa
linapitia wakati mgumu hasa juu ya uendelevu wa Serikali ya Muungano katika
mfumo wake pamoja na suala zima la Zanzibar kutaka kujiunga na Umoja wa Nchi za
Kiislamu (OIC). Pia ni katika kipindi hiki ambacho mwaka mmoja baadae taifa kwa
mara ya kwanza lilikuwa linaingia kwenye uchaguzi wa Rais wa awamu ya tatu
chini ya Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa.
Hivyo
kutokana na hali hii ambayo taifa lilikuwa linapitia Mwalimu aliona vyema
kutumia kijitabu hiki kama wosia wake au honyo kwa viongozi waliokuwa na
dhamana ya uendeshaji wa Serikali ya awamu ya pili chini ya Rais Ali Hassan
Mwinyi.
Karibu
tujifunze wote machache niliyojifunza kwenye hiki:
1. Hoja
ya kwamba muundo wa muungano uwe wa Serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume
ya Nyalali haikuwa hoja ya kuu ya wananchi. Mwalimu Nyerere alikuwa anashangaa namna ambavyo hoja ya muundo wa
Serikali ya Muungano ulivyoibuliwa na kupewa kipaumbele na uongozi wa wakati huo
wakati sehemu ya taarifa ya tume ya Nyalali inasema kuwa ni wananchi 49 tu
waliozungumzia muundo wa Serikali tatu kati ya wanachi 36,299 waliojitokeza
kwenye Tume kutoka Bara na Visiwani. Kwa mujibu wa Mwalimu Nyerere kuendelea
kujadili muundo wa Serikali ya Muungano lilikuwa ni shinikizo la watu wachache
ambao walikuwa na ajenda zao hasa za ukabila, udini na tamaa ya uongozi. Kutokana
na hali hii alishindwa kunyamaza kwani hakuwa tayari kuona Muungano aliouhasisi
ukielekea kuvunjika.
2. Pamoja
na kwamba demokrasia alisaidia kuleta utaratibu wa kupokezana madaraka kwa
mfumo wa kupigiwa kura, utaratibu huu ulikuja na matakwa mengi ya kikoloni
ambayo wao walikuwa hawayatekelezi. Mfano, Malkia wa Uingireza anapatikana kwa mfumo
wa kurithishana kwa mujibu wa utashi wa Malkia anayemaliza muda wake. Baada ya
uongo wa demokrasia kuingia katika nchi za ki-Afrika, nchi nyingi ziliachana na
tamaduni zao na kufuata tamaduni zilizoenezwa na Wakoloni. Hata hivyo, katika
nchi ili kuendeleza demokrasia ya kupokezana madaraka ndipo demokrasia ya vyama
vingi ilitakiwa na kuungwa mkono na wanachi wengi katika Tume ya Nyalali.
3. Mabadiliko
ya mfumo kutoka chama kimoja kwenda vyama vingi vya siasa yaliambatana na
ulazima wa kubadilisha baadhi ya vifungu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Tume ya Mark Bomani ilipewa jukumu la kutafuta maoni ya wananchi
kwenye vifungu vilivyotakiwa kuboreshwa. Mojawapo ya majukumu ilikuwa ni
kupendekeza namna ya kumpata makamu wa rais ili kuachana na mfumo wa kuwa na Makamu
wa Rais wa wawili kwa maana ya Makamu wa Rais wa upande wa Bara na wa upande wa
visiwani. Kamati hii ilipendekeza mfumo unaotumika sasa wa “mgombea mwenza” ili
endapo mgombea wa Urais akishinda mgombea mwenza wake awe ni Makamu wa Rais. Na
endapo mgombea wa nafasi ya Rais ametoka Bara basi mgombea mwenza wake
anatakiwa atokee upande wa visiwani na kinyume chake ni sahihi.
4. Kupitia
kitabu hiki pia Mwalimu Nyerere anaelezea umuhimu wa kuhakikisha Rais wa taifa
la Tanzania anakuwa madarakani kwa muda wa vipindi viwili. Hii ilitokana na
msukumo kutoka kwa baadhi ya viongozi wa chama ambao walikuwa wameanza mchakato
wa chini chini wenye nia ya kuleta hoja ya Rais wa wakati huo (Mzee Mwinyi)
kuongezewa muda ili aendelee kuwa madarakani. Hivyo mnamo mwezi Desemba, 1992,
Mwalimu Nyerere alikaribishwa kwenye Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM
na ndipo alilisisitiza umuhimu wa kuendelea kuheshimu ukomo wa madaraka ya Rais
na kuwataka kuwa ni vyema ukomo huu uendelee kufahamika hivyo kwenye katiba ya
nchi ili uheshimiwe na watu wote.
5. Myunani
wa kale, Plato, alipendekeza kuwa wanafalsafa ndio wanaofaa kuwa watawala wa
nchi kwa kuwa wana sifa mbili: kwanza, wana uwezo wa kutawala na pili,
hawapendi kutawala. Hivyo, katika Jamhuri ya Plato walitakiwa kulazimishwa
kutawala kwa zamu na mtu zamu yake ya kutawala inapoisha atafurahi sana kwa
vile anarudi kwenye kazi zake za falsafa kwani ndizo anazipenda zaidi. Tofauti ya
viongozi wetu na wanafalsafa wa Plato, nchi zetu zinatawaliwa na wanasiasa wa
kawaida ambao wanapenda sana kutawala hata kama hawana uwezo wa kutawala; na
ambao wapo tayari kuonga kwa ajili ya kuchaguliwa kuwa watawala na
wakishakuchaguliwa hawatoki bila kulazimishwa. Kutokana na ukweli huu, Mwalimu
Nyerere aliona suala la ukomo wa madaraka ya Rais lisiwe swala la kuacha ili
liamuliwe na busara ya Rais na Washauri wake na bali liwe suala la Katiba ya
nchi.
6. Mwalimu
Nyerere yeye aliona suala la Zanzibar kujiunga na OIC lilikuwa ni kinyume na
katiba ya nchi hata alishangaa kuona kuwa viongozi wa wakati huo walikuwa na
uoga wa kukemea suala hili. Hali hii ilichochea wabunge wa Tanzania Bara
maarufu kama kundi la G55 kutaka kuleta hoja ya Bungeni ya kuhitaji kudai upya
taifa la Tanganyika. Hii ilimfanya Mwalimu Nyerere kusimama kidete kukemea
suala hili kwa kuainisha msimamo wake wenye mambo makuu manne: moja, Zanzibar
ijiondoe kwenye OIC; mbili, Makamu wa Rais apatikane kwa mujibu wa mapendekezo
ya Tume ya Mark Bomani; na tatu, Hoja ya Serikali tatu ipingwe na viongozi wote.
7. Mwalimu
Nyerere anasema sababu ya kuunda mfumo wa Serikali ya Muungano yenye Serikali
Mbili badala ya Serikali Tatu (Serikali ya Zanzibar, Tanganyika na Shirikisho)
ulitokona na sababu kuu ya “udogo wa Zanzibar na ukubwa wa Tanganyika. Kipindi Muungano
huu unaanzishwa kipindi hicho Zanzibar ilikuwa na idadi ya watu laki tatu huku Tanganyika
ikiwa na watu milioni kumi na mbili. Kuwa na muundo wa Serikali tatu kungepelekea Zanzibar kumezwa na Tanganyika
na pia kuisababishia Tanganyika kubeba mzigo mkubwa wa kuendesha serikali mbili
ambazo ni gharama za uendeshaji wa Serikali ya Tanganyika pamoja na zile za
uendeshaji wa Serikali ya Shirikisho. Hii ingesababisha minong’ono kutokana pande
zote za muungano na hivyo kuhatarisha kudumu kwa muungano.
8. Uongozi
ili uwe imara ni lazima uwe tayari kuishi misingi ya uongozi na sio kufuata tu
au kuyumbishwa na upepo. Kulingana na hali ilivyokuwa inaelekea taifa lilikuwa
linayumbishwa na matakwa ya watu wachache ambao walitumia udhahifu wa uongozi
wa wakati huo. Hali hii ilikuwa inapelekea kuligawa taifa na matokeo yake ikawa
endapo ingevumiliwa basi taifa la Tanzania lilikuwa linasambaratika jambo
ambalo Mwalimu Nyerere hakuwa tayari kulishuhudia katika uhai wake. Kuongoza ni
kuonesha njia na endapo kiongozi anashindwa kuonesha njia ni bora akipisha
wengine wenye uwezo wa kuonesha njia na yeye akawa mfuasi.
9. Kiongozi
mkuu anapokosa msimamo taifa zima kwa ujumla linapoteza mwelekeo. Mwalimu Nyerere
kupitia kijitabu hiki anasikitika kuona namna maamuzi ya Kamati Kuu ya Chama
yalivyokuwa yanashindwa kutete na Serikali Bungeni na badala ya kufanya hivyo
viongozi wa Serikali ndio walikuwa wa kwanza kupindua maamuzi Kamati Kuu hasa
kwenye suala Utanganyika kupitia kilemba cha Serikali tatu. Kama ni kiongozi wa
kweli daima utaendelea kuishi misingi ya uongozi bora hata kama hauna cheo cha
mamlaka. Hii inaoneshwa wazi na namna ambavyo Mwalimu Nyerere aliendelea kukemea
hoja ya utanganyika hata pale ambapo alizungukwa na uongozi uliokuwa
madarakani.
10. Goigoi uzaa goigoi na legelege uzaa
legelege. Hiki ndicho kilikuwa kinaendelea katika taifa la Tanzania miaka 1992
mpaka 1994 kwani Chama kilishindwa kuisimamia Serikali na Serikali nayo
ikashindwa kusimamia misingi ya Chama. Kama muasisi wa Chama na muasisi wa
taifa, Mwalimu Nyerere alishindwa kukaa kimyaa badala yake alisimama imara
kupinga kilichokuwa kinaendelea ndani ya Chama na Serikalini kwa ujumla.
11. Kiongozi unatakiwa kuongoza kwa
kusikiliza maoni ya waliokuweka madarakani. Mwalimu Nyerere pamoja na kwamba
alitumia jitihada kubwa za kuulinda muungano kwa kukataa hoja za Utanganyika na
Unzanzibar hatimaye aligundua kuwa viongozi waliokuwa madarakani walikuwa na
ajenda zao za kutaka kulazimisha uwepo wa Serikali tatu bila ya ridhaa ya
wananchi walio wengi. Kiburi cha viongozi hawa pia kiliambatana na dharau za
wazi dhidi ya Kamati Kuu ya Chama.
12. Ushupavu wa kiongozi unategemeana na
uwezo wa viongozi washauri wanaomzunguka. Katika kundi la washauri wa Rais
Waziri Mkuu anatakiwa kuwa na msimamo thabiti kwani yeye ndiye kiongozi wa
shughuli za Serikali Bungeni. Mwalimu Nyerere alishangaa kuona Waziri Mkuu wa
wakati huo alizidiwa nguvu viongozi wenzake. Na hii ilitokana na hali yake ya
kutokuwa na msimamo juu ya hoja iliyokuwa inalazimishwa. Tunachojifunza hapa ni
kwamba kama kiongozi unahitaji kuwa na weledi mkubwa dhidi ya wale
wanaokuzunguka.
13. Pale ambapo kiongozi unashindwa
kutekeleza majukumu yako ipasavyo ni vyema ukawajibika kwa maslahi ya umma
kabla ya kuwajibishwa. Mwalimu Nyerere analiweka wazi hili kutokana na baadhi
ya Mawaziri kuendelea na hoja ya Utanganyika. Waziri mkuu wa kipindi hicho
katika kutekeleza majukumu yake alitakiwa aitishe Kabineti ya Mawaziri kwa
ajili ya kuweka msimamo wa pamoja wa kuzima hoja ya Utanganyika. Lakini kimakosa
Waziri Mkuu alishindwa kutimiza wajibu wake. Katika hali ya kawaida Mawaziri
waliokuwa wamebeba hoja ya Utanganyika kabla hawajawajibika kwa maslahi ya
umma; Waziri Mkuu alitakiwa kuachia ngazi kwa kushindwa kumshauri vyema Rais wa
Jamhuri ya Muungano.
14. Rais hawezi kutikiswa na nchi
hisitikisike. Cheo cha Rais kilivyo ni taasisi ambayo imeshikilia mihimili yote
ya nchi (Bunge, Serikali na Mahakama). Kutokana na makosa yote ya wazi ambayo
yalisababishwa na udhaifu wa Rais wa wakati huo, bado Mwalimu Nyerere hakuona
ni vyema kumshambulia Rais kama alivyofanya kwa Waziri Mkuu na viongozi wengine.
Kwake yeye aliamini kuwa kumshambulia Rais kungepelekea kulitikisa taifa
jambalo hakuwa tayari kulishuhudia. Hata hivyo, makosa ya Rais yalikuwa wazi
ikiwa ni pamoja na kushindwa kuweka wazi msimamo wake juu ya hoja ya Utanganyika
tukiachilia mbali yale ya Zanzibar kujiunga na OIC.
15. Katika nafasi ya uongozi wa juu kama Rais
hautakiwi kuwa na upole uliopitiliza. Hapa Mwalimu Nyerere anatushikirisha namna
ambavyo alikerwa na kitendo cha Rais kushindwa kumwajibisha Waziri Mkuu pamoja
na Katibu Mkuu wa Chama kutokana na hali ya nchi ilivyokuwa kutokana na kukua
kwa hoja ya uchochezi wa Utanganyika. Rais ana mamlaka ya kusafisha makosa ya
washauri wake pale wanapoenda kinyume na matakwa ya kazi zao na njia pekee ya
kusahihisha makosa hayo pale nchi inapoelekea kwenye anguko ni kuwawajibisha
wahusika mara moja na pale asipofanya hivyo makosa ya watu washauri wake
yanakuwa ya kwake.
16. Pale kiongozi mkuu unapokuwa mpole/mdhaifu
ndivyo watu wako wa chini wanavyotumia upole/udhaifu huo kutimiza ajenda zao. Hiki
ndicho ambacho kilikuwa kinaendelea katika taifa letu mpaka kufikia hatua ya
kushindwa kujua nani ni mwenye mamlaka ya juu kati ya Rais au Waziri Mkuu ndani
ya Serikali au kati ya Rais na Katibu Mkuu ndani ya Chama.
17. Serikali ili isonge mbele ni uongozi
uliopo madarakani ufanye kazi kama timu moja na timu hiyo iongozwe na dira
chini ya uongozi wa rubani mashuhuri. Hiki ni kitu ambacho kilikosekana kipindi
mwandishi anaandika kijitabu hiki. Mwandishi anatueleza wazi kuwa kwa kipindi
hiki Uongozi wa Serikali ulikuwa na uhalali wa kisheria wa kuendelea kuwa
madarakani kwa vile tu iliingia madarakani kwa mujibu wa sheria japokuwa haikuwa
uhalali wa uwezo wa kuiongoza nchi.
18. Mkusanyiko wa Mawaziri bila
dira/mwelekeo, bila dira, bila mshikamano na bila uongozi kila Waziri ni
atafanya yake anayoyaona ni muhimu kwake. Mawaziri wa aina hii kamwe hawawezi
kuitwa Serikali. Katika hali kama hii kila mmoja anacheza ngoma yake matokeo
yake ni hatari kwa maendeleo ya nchi kwani mambo muhimu ya nchi hayawezi
kujadiliwa wala kushughulikiwa. Hivi ndivyo ambavyo Tanzania ilikuwa inaendeshwa
kipindi mwandishi anaandika kitabu hiki.
19. Tanzania ni nchi kipekee kabisa
ukilinganisha na nchi nyingine za Africa kwani nchi pekee ambayo haikukubali
kukumbatia mipaka ya Wakoloni. Suala la Zanzibar kuungana na Tanganyika na zote
kuwa nchi moja ni jambo la kifahari katika historia ya nchi yetu. Muungano wa Tanganyika
na Zanzibar ni wakihistoria kwani kabla ya Wakoloni nchi hizi kwa asili
zilikuwa ni moja. Mwali Nyerere anashangaa anapoona watu wanahoji uhalali wa
Muungano na kusahau kuwa nchi hizi zilitenganishwa na Wakoloni kwa kutumia
mtutu wa bunduki.
20. Malengo ya kuwa na Muungano wa Nchi
hizo mbili chini ya uongozi wa Chama cha Mapinduzi ambacho ni zao la Muungano
wa TANU na ASP ilikuwa ni siku moja kuwa na nchi moja yenye Serikali Moja chini
ya uongozi wa Rais Mmoja. Mwalimu anamtazama mtu ambaye anaibua hoja ya Tanganyika
ni kutaka kurudisha nyuma nia ya waasisi wa Muungano. Hii ni kutokana na ukweli
kwamba ukifufua Tanaganyika unaua Tanzania. Kwa mtazamo huu, Sera ya Chama juu
ya Muungano ni Serikali Mbili na ni matarajio Chama kikibadilisha Sera yake, Sera
mpya itakuwa ni Serikali Moja.
21. Sifa ya kiongozi makini ni kupenda kupata
heshima kutoka kwa wananchi wenzake lakini kamwe hapendi kuogopwa na wananchi
hao. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kuogopwa ni sifa na ada ya madikteta
ambao ni mfumo husiokuwa na nafasi katika taifa uhuru la Tanzania. Hata hivyo,
kwa watawaliwa kujenga utaratibu wa kutii kila kitu hata kama ni cha hovyo ni
dalili ya woga na hatua za kukaribisha udikteta. Mwalimu Nyerere hakuwa tayari
kuwa sehemu ya uoga huo na ndio maana alitushirikisha kitabu hiki ili taifa
lifahamu kilichokuwa kinaendelea nyuma ya pazia na alikuwa tayari kupinga
katika ngazi zote za Chama hata kama angeoonekana mwasi au msaliti.
22. Mwalimu Nyerere kwa maono yake wakati
ule kulikuwa bado hakijapatikana chama makini ambacho kingeweza kuitikisa CCM
ili Chama hicho kiwe Mkombozi kwa Taifa ambalo lilikuwa linaelea. Hali ambayo
ilikuwa inaendelea ndani ya Chama ambayo mpaka sasa inakitesa aliita kuwa ni
Kansa ya Uongozi ndani ya Chama. Kwa yeye aliona fursa ya kipekee katika
kulikomboa taifa ni kuzaliwa kwa Chama kipya chenye itikadi makini ili kiwe
mbadala wa CCM na ndio maana alipendekeza mfumo wa vyama vingi vya siasa hapa
nchini. Maneno yake ni kwamba bila demokrasia halisi ndani ya Chama na bila
chama makini cha upinzani nje ya CCM, CCM itaendelea kudidimia chini ya uzito
wa uongozi mbovu.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri
uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
|
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com