Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa upo vizuri na mapambano
yanazidi kushika kasi katika kipindi hiki ambacho tunamalizia robo ya kwanza ya
mwaka 2017. Ikiwa ni wiki ya kumi na mbili tokea nianze kukushirikisha uchambuzi
wa kitabu kimoja kila wiki ni matarajio yangu kuwa uchambuzi wa vitabu hivi
umekusaidia kwa kiasi flani katika kipindi hiki cha robo ya kwanza ya mwaka.
Kama mpaka sasa haujafanikiwa kujifunza
kitu chochote katika makala hizi za uchambuzi wa vitabu nakushauri ni vyema
husiendelee kupoteza muda wako na badala yake ufanye mambo ambayo umeyazoea. Hii
ni kutokana na ukweli kwamba uchambuzi wa vitabu kupitia kwenye mtandao wa
fikra za kitajiri unalenga uwasaidie wale wenye kiu ya kubadilisha maisha yao kupitia
usomaji wa vitabu ikiwa ni pamoja na kutumia mbinu na maarifa tunayojifunza
kwenye vitabu hivi katika kuboresha maisha yetu.
Kujiunga na mtandao wa fikra za
kitajiri BONYEZA HAPA na
ujaze fomu ili uendelee kunufaika na mwaliko huu ambao unakulenga wewe mwenye
kiu ya kutimiza ndoto za maisha yako. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata
makala za mtandao wa fikra za kitajiri moja kwa moja kwenye barua pepe yako.
Kitabu
cha wiki hii ni “The Art of Power” kutoka kwa mwandishi na Mtawa wa Kibuddha Thich Nhat Hanh. Mwandishi wa kitabu hiki
amekuwa ni mpenda amani kwa muda mrefu kiasi cha kutumia muda wake mwingi
katika kusuruhisha sehemu zenye vita ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wahanga wa
vita.
Kwa
ujumla mwandishi anatushirikisha kuwa kwa maumbile kila mmoja wetu amezaliwa na
nguvu ya madaraka ndani mwake na nguvu hii inaanza kutumika ipasavyo pale
muhusika anapotambua yeye ni nani na ameumbwa ili atimize nini katika ulimwengu
huu. Pia katika kitabu hiki mwandishi anatushirikisha umuhimu wa kutumia vizuri
nguvu ya madaraka yetu kwa kutambua kuwa madaraka uliyonayo ndani mwake kuna
nguvu ya kuyaangamiza pale yanapotumiwa vibaya.
Karibu
tujifunze wote machache niliyojifunza kutoka kwenye kitabu hiki:
1. Madaraka
halisi kwa kila mtu chimbuko lake ni kuishi maisha yenye furaha kwa wakati
uliopo, maisha yasiyo na hofu, ulevi, ubaguzi, hasira na upumbavu wa kila aina.
Hii ndio haki ya kuzaliwa ambayo kila mtu amezaliwa nayo hata kama yeye
mwenyewe hajatambua haki hiyo. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wengi katika
jamii wameishi kwenye msingi wa uongo wa kuwa madaraka yanatokana na elimu, utajiri,
mafanikio, ukubwa wa vyombo vya jeshi, umaarufu, kipaji na nguvu au nafasi ya
kisiasa. Hii ni kinyuma kabisa na maana halisi ya madaraka ambayo mwandishi
anatushirikisha hapa kutokana na ukweli kwamba madaraka yanatakiwa yaanzie
kwenye mfumo wa fikra wa kila mtu pasipo kujali nafasi au elimu yake.
2. Kutaka
kuwa tajiri, maarufu au mafanikio ya namna yoyote ile sio jambo baya endapo
tunatafuta vitu hivi kama msingi wa kutusaidia kuendelea kuishi maisha yenye furaha
ya kweli katika nafsi zetu na wale tunaowapenda au jamii inayotuzunguka kwa
ujumla. Kama vitu hivi vinapelekea madaraka ambayo yana athari kwa watu wengine
na nafsi zetu basi vyote hivi havifai katika maisha yetu.
3. Madaraka
ya kweli ni lazima yazingatie mambo yanayotokea ndani na nje ya mhusika. Kwa maana
hii mwandishi anatushirikisha kuwa madaraka ambayo kila mtu amerithishwa
kupitia uumbaji ni lazima yazingatie mahitaji ya nafsi kupitia mfumo wa fikra
lakini pia mahitaji ya watu wanaokuzunguka. Madaraka ya namna hii yanajengwa
katika msingi wa kufurahia kazi unayofanya ambayo pia ni lazima iwe inawasaidia
watu wanaokuzunguka kutambua na kutumia vyema madaraka yao. Hii ni kwa mtu yeyote
yule kuanzia kwa mfanyabiashara, mkulima, msanii, mwanasiasa au mfanyakazi. Kila
mmoja katika makundi haya ni vyema kutanguliza lengo kubwa la kuwasaidia watu
kupitia kazi yake na hatimaye mafanikio mengine yafuate.
4. Madaraka
ya kweli ni yale yanayoongozwa na furaha kwa nafsi yako na watu wako wa karibu
katika kila hatua unayopiga. Hapa mwandishi anatushirikisha kuwa ni muhimu
kuishi maisha ya furaha kila iitwapo leo kana kwamba kesho hatutakuwepo. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba wengi wetu tumekuwa tukisubirisha furaha ya maisha
yetu kwa kutegemea kuwa tutafurahi siku tukimiliki vitu flani lakini hata pale
tunapofanikiwa kuvipata tunajikuta bado hatuna furaha rohoni mwetu. Ili kuondokana
na hali kama hii mwandishi anatushauri kuishi leo kwa vile hakuna mwenye
uhakika wa kwamba kesho atakuwepo.
5. Msingi
wa madaraka tuliyonayo au tunayoyataka ni lazima uwe ni mapenzi ya dhati kwa
familia zetu, wenza na watoto wetu, jamii inayotuzunguka. Ili kufanikiwa katika
msingi huu ni lazima tusikubali kuruhusu maisha yetu yatawaliwe na yale
tunayoyafanya kiasi cha kusahau kuwa karibu na wapendwa wetu. Daima tunakiwa
kufahamu kuwa kuna furaha nje ya hayo tunayokimbizana nayo kila siku na furaha
hiyo haipo sehemu nyingine zaidi ya kuwa na muda wa kufurahi na familia zetu.
6. Hata
kama wewe ni tajiri mkubwa au maarufu kiasi gani ni lazima utambue kuwa hakuna
furaha kama hauna mapenzi yanayoongozwa na hamasa ya ndani mwako bila kufahamu
hili ni dhahiri kuwa yote unayofanya ni sawa na bure. Mwandishi anatushirikisha
kuwa utajiri au mafanikio ya namna yoyote ile ni lazima yatokane na misingi ya
kiroho ambayo ni upendo kwa nafsi zetu na wengine, huruma na kuepuka kiburi.
7. Madaraka
ya kweli ni lazima yajengwe kwenye msingi wa imani kwani tunafahamu kuwa hata
maandiko matakatifu yanasema kuwa kwa imani ndogo mtu anaweza kuhamisha milima.
Katika hili ni lazima tutambue imani ni kuwa na uhakika pamoja na uhaminifu
katika mambo yanayotarajiwa. Hivyo imani ni kufuata njia ambayo inakupeleka
kwenye uhuru, wokovu au ukombozi na yenye uhakika wa kukutoa kwenye kila aina
ya mateso. Hii ndiyo imani ya kweli ambayo kwa undani wake utagundua kuwa ndiyo
msingi wa madaraka ambayo mwandishi anatufundisha kupitia kitabu hiki.
8. Madaraka
ya kweli yanatokana na mwendelezo wa bidii zako pasipo kurudi nyuma au kutafuta
njia ya mkato. Njia rahisi ya kufanikiwa katika siri hii ni kujenga tabia ya
utulivu wa akili katika kila jambo unalofanya na kuhakikisha unatenga muda wa
kuongea na nafsi yako kila siku. Pia, mwandishi anatushirikisha kuwa mafanikio
ya zoezi hili ni muhimu yapate baraka za wanafamilia. Hata hivyo mwandishi
anatushirikisha kuwa ni muhimu kujenga tabia ya kupenda kufanya
tajuhudi/tafakari (meditation) kama njia ya kutuwezesha kuwa na utulivu wa
akili.
9. Mfumo
wa ubongo wetu umejengwa katika namna ambayo unahifadhi mbegu za mema na
mabaya. Kadri utakavyomwagilia mbegu za mema kupitia fikra zako ndivyo utapata
matokeo mema na kinyume chake ni kwamba utapata matokeo mabaya kwa kutoa nafasi
ya mawazo hasi katika fikra zako. Hivyo kuanzia sasa fahamu kuwa hasira, chuki,
wivu, hofu, roho ya visasi, kutokujiamini na mengine mengi ambayo yamekusumbua
kwa muda ni matokeo ya mbegu hasi ambazo umekuwa ukizimwagilia katika mfumo
wako wa fikra. Hili kuepuka fikra hasi mwandishi anatushirikisha kuwa hatuna
budi ya kuendelea na fikra hizo hadi zikajidhihirishe kwenye vitendo na badala
yake tunatakiwa kubadilisha fikra hasi kwa fikra chanya.
10. Jifunze kutumia nguvu ya utulivu wa
akili katika kila hali inayokuzunguka. Mwandishi anatufundishwa kuwa utulivu wa
akili ni dhana pekee ya kumwezesha mtu kufikia mafanikio makubwa katika
ulimwengu wa roho na mwili. Dhana hii imejengwa kwenye siri ya kuhakikisha
akili yako kila wakati inatambua ni kipi kinatakiwa kufanyika kwa wakati huo na
kipi hakipaswi kupewa nafasi. Mfano, kama unatembea badala kuwaza makosa yako
ya nyuma au uoga wa maisha ya baadae unatakiwa akili yako yote iwe kwenye kila
hatua ya mguu wako na hivyo utajikuta unapata furaha kwenye tendo la kutembea
vivyo hivyo kwenye shughuli nyinginezo. Kwa kuishi msingi wa nguvu hii
utafanikiwa kuepuka kufanya makosa na madhara mengi ya kiafya na hivyo kufanikiwa
kuishi maisha yenye furaha muda wote.
11. Jifunze kufanya vitu kwa ukamilifu. Hapa
mwandishi anatushirikisha kuwa hakuna mwenye uhakika kuwa kesho atakuwepo kwani
yawezekana leo upo vizuri lakini kesho ukaaga dunia kwa ajili au tukio lolote
lile. Hivyo ni muhimu kuishi maisha ya ukamilifu kwa kila jambo unalofanya. Kama
umetenga muda wa kuwa na mwenzi wako kuwa naye kana kwamba hautakuwa na muda
mwingine wa kukaa naye. Kwa ujumla tunafundishwa kuepuka kusubirisha jambo
lolote kwa kutegemea kuwa litafanywa baadae.
12. Fahamu kuwa madaraka na vitu vyote
tulivyo navyo katika dunia hii ni vya muda tu na hivyo umiliki wake sio wa
kudumu. Hii inajumuisha maisha yetu. Wapendwa wetu na umiliki wa mali
tulizonazo katika dunia hii. Mwandishi anatushirikisha kuwa unapotambuwa kuwa
kila ulichonacho una umiliki wa muda itakuwa rahisi kwako kuhakikisha unapata
furaha ya kutosha wakati huu kikiwa bado kwenye miliki yako. Mwandishi anatushirikisha
kuwa kwenye msiba sio wote wanalia kwa sababu ya kupoteza mpendwa wao bali
wengi wao wanalia kwa kujutia kuwa kwa muda ambao wameishi na marehemu
hawakupata muda wa kumtumia vizuri na hivyo ameondoka kabla hawajafaidi uwepo
wake.
13. Tumia madaraka uliyonayo vizuri ili
uepuke kuumiza watu wa chini yako. Kama wewe ni mwalimu, baba/mama, kiongonzi
au mwajiri hakikisha unatumia madaraka yako vizuri pindi unapowakanya watu wa
chini yako ili kuepuka kuumiza nafsi yako au wale waliopo chini yako. Hapa mwandishi
anatushauri kuwa muda wote tunatakiwa kutumia madaraka yetu vizuri ili
tuwasaidie watu wa chini wafikie malengo yao pasipo kuwa na msongo wa mawazo au
maumivu ya roho. Kiongozi bora ni yule anayetanguliza upendo, busara, huruma na
hasiye na majivuno kwa watu wake kwa kuhakikisha anaishi hisia za machungu
wanayopata watu wake.
14. Cheo hakitoi madaraka ya kweli bali
madaraka ya kweli yanapatikana kutokana na juhudi za muhusika kujifunza mbinu
za uongozi wa kweli. Madaraka ya kweli yanaanzia kwanza kwa muhusika kujifunza
na kutumia mbinu za utulivu wa akili. Utulivu wa akili ni chanzo cha furaha,
amani, upendo na busara na vyote hivi ndo nyenzo muhimu za madaraka ya kweli. Hii
ni kutokana na ukweli kwamba unapokuwa na vitu hivi ni rahisi wafuasi wako kukusilikiliza
kile unachoongea na hivyo nguvu ya madaraka yako itakufuata pasipo kutumia
nguvu nyingi. Hapa tunajifunza kuwa viongozi wengi wamekuwa wakitumia nguvu
nyingi ili waonekane kuwa wana madaraka makubwa.
15. Viongozi wengi wametumia nguvu nyingi
na hivyo kuwanyanyasa watu wengi kupitia maamuzi yao. Hii inasababishwa na
kushindwa kutambua kuwa madaraka waliyonayo yana nguvu ya roho mtakatifu ndani
mwake hivyo kama kiongozi ni lazima uwe tayari kuongozwa na vipaji vya roho
mtakatifu kuliko kuongozwa na maono binafsi. Maono haya mara nyingi yamejaa
majivuno, kiburi na visasi. Kwa kutambua kuwa wewe hapo ulipo tayari ni
kiongozi kwa madaraka uliyonayo kuanzia sasa mfanye roho mtakatifu akuongoze
katika matendo yako yote. Mwandishi anamalizia kwa kusema kuwa viongozi
watapata upinzani kutoka kwa wafuasi wao endapo watatumia madaraka yao vibaya
na pale wanapotumia madaraka yao vizuri kwa kuongozwa na nguvu ya roho
watafanikiwa kufanya vitu vikubwa pasipo kupata changamoto nyingi.
16. Pesa na vyeo vya siasa vyote vinaweza
kukupa nguvu ya madaraka lakini vyote hivi hakuna hata kimoja ambacho
kitakuhakikishia furaha ya kweli endapo hujajua jinsi za kuvitumia. Kwa pesa
unaweza kununua kila kitu, unaweza kununua mtu yeyote yule au kwenda mahali
popote japo bado kuna muda utajikuta kwenye sononeko la roho kutokana na
matendo yako ambayo yanawaumiza watu wengi.
17. Pesa na umaarufu kama vyenyewe havina
ushetani ndani yake bali ushetani unakuja pale ambapo unashindwa kuvitumia kama
inavyotakiwa. Unaweza kutumia pesa na umaarufu wako kwa ajili ya kuwanyanyasa
watu wengine unaweza kutumia vyote hivyo kwa ajili ya kuwainua watu wengi
zaidi. Kwa ujumla ni kwamba ufanisi katika vyote ni lazima uongozwe na roho
mtakatifu. Wote ni mashahidi kuwa pamoja na kwamba Marekani ni taifa kubwa
duniani lakini Marekani haipo hata kati ya mataifa kumi yenye watu wenye furaha
zaidi. Hivyo ni muhimu kujifunza kuwa furaha ya kweli inatokana ndani mwetu
pasipo kujali magumu au mema tuliyonayo.
18. Furaha ya kweli haitokani na ukubwa wa
akaunti zetu za benki bali furaha ya kweli inatokana jinsi tunavyochukulia
mazingira yetu ya kila siku. Kwa ujumla furaha ya kweli inatokana na kuwa na uhuru,
huruma, upendo, busara na kuridhika na kile tulichonacho kwa sasa. Hapa tunakiwa
kufahamu kuwa furaha hainunuliwi kwa wingi wa mali kwani wapo matajiri wakubwa
lakini bado wanaishi maisha yenye huzuni rohoni mwao.
19. Kila mtu ameumbwa kuishi maisha yenye
furaha hapa duniani na hivyo kila mtu amepewa mamlaka ya kuishi maisha hayo. Pamoja
na mamlaka hayo kila mmoja amezungukwa na nguvu zinazomsukuma kutoka kwenye
maisha hayo ya furaha. Nguvu hizi zinajumuisha maisha ya kutimiza hanasa za
mwili ambazo mara nyingi zinajikita kwenye furaha ya muda mfupi na baada ya
hapo ni majonzi na huzuni ya roho.
20. Njia pekee ya kumpenda mwenza wako au
watu wanaokuzunguka kwanza kabisa unatakiwa kuuona uzuri na ukweli ndani mwako
na baada ya hapo unaweza kuuona uzuri na ukweli katika watu wengine. Mwandishi
anatukumbusha kile ambacho maandiko matakatifu yanatueleza kuwa “mpende jirani
yako kama unavyojipenda mwenyewe”. Kwa maana hii hauwezi kuwapenda watu wako wa
karibu kama wewe mwenyewe hauoni uzuri ndani mwako. Kama wewe hujipendi
hutaweza vipi kuwapenda wenzio? Kama wewe mwenyewe hujitambui, ujielewi au
hujikubali utaweza vipi kuwakubali/kuwaelewa watu wengine?
21. Njia rahisi ya kukuza upendo kwa watu
wako wa karibu ni kuhakikisha wana uwepo wako wa kiakili na kimwili pale
wanapokuhitaji. Ni mara nyingi kukuta wazazi au mtu na mwenza wake wanamezwa na
kazi kiasi ambacho kila mmoja anahitaji uwepo wa mwingine pasipo mafanikio. Pia,
katika hali kama hii watoto nao wanakosa vitu muhimu kutoka kwa wazazi. Mwandishi
anatushirikisha kuwa kama unataka kukuza upendo wako huna budi ya kuhakikisha
una muda wa kukaa karibu na uwapendao kwa ajili ya kushirikishana mambo muhimu.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba upendo haukuzwi kwa zawadi za vitu bali upendo
unaboreshwa kwa kufarijiana.
22. Kiongozi mwenye mafanikio ni yule
anayesikiliza na kutatua matakwa ya wafusi wake. Ni lazima kama kiongozi uwepo
kwa ajili ya watu wako ili ufahamu changamoto zinazowakabili na hatimaye uwe
tayari kuzifanyia kazi kwa maslahi ya wafuasi wako na wewe pia.
23. Kama mfanyabiashara jifunze kufanyia
kazi vitu ambavyo sio lazima vichangie kwenye biashara yako. Somo hapa ni
kwamba hatupaswi kumezwa na shughuli za kutafuta faida au shilingi kila wakati
kwani vitu mambo mengine ambayo tunapaswa kufanya kwa kuongozwa na utu wetu. Hapa
tunatakiwa kuishi kwa kuongozwa na sheria ya asili ya uwili kinzani katika kila
tunalofanya. Kwa maana hii tunatakiwa kutambua kuwa kama kuna faida pia hasara
ipo, kama kuna tajiri pia masikini yupo, kama kuna kupanda pia kuna kushuka n.k.
Hivyo muhimu ni kuhakikisha kila tunalofanya tufanye kwa wastani pasipo kuumiza
wenzetu kwa kisingizio cha kutafuta shilingi.
Haya ni machache kati ya mengi ambayo mwandishi
ametushirikisha kupitia kitabu hiki. Kama ni asilimia basi nilichokushirikisha
hapa ni kama asilimia 20 tu katika mafundisho yaliyopo ndani ya kitabu hiki. Mafundisho
haya yanagusia maisha ya kiroho, kijamii, kisiasa na kiuchumi hivyo nakushauri
upate muda wa kusoma kitabu hiki kwa ajili ya kubadilisha maisha yako. Kupata
nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com