Habari ya leo rafiki
na msomaji wa mtandao wa Fikra za Kitajiri.
Kama bado hujajiunga
na mfumo wetu wa kupokea makala za uchambuzi wa vitabu, tafadhali fanya hivyo KWA KUBONYEZA HAPA na
kujaza fomu kisha bofya “jiunge/subscribe”. Ni fursa ambayo itakuwezesha kupata
uchambuzi wa vitabu kwa lugha rahisi kupitia barua pepe yako.
Ni matumaini yangu
kuwa unaendelea kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Ni mwisho wa wiki
tena na kwa majaliwa ya Mwenyezi Mungu nipo tayari kukushirikisha mambo muhimu niliyojifunza
kutoka kwenye kitabu cha “Be Rich & Happy” kutoka kwa Mwandishi maarufu Robert Kiyosaki. Kiyosaki
ni Mwandishi, Mhamasishaji na Mwekezaji mwenye mafanikio makubwa. Moja ya kazi
yake ambayo imebadilisha maisha ya mamilioni ya watu duniani ni Kitabu chake cha
“Rich Dad Poor Dad – Baba Tajiri Baba Masikini” ambacho ameeleza changamoto
mbalimbali hasa jinsi gani mfumo wa elimu, malezi ya watoto na mfumo wa ajira
vinavyosababisha watu wengi kuendelea kuwa masikini.
Robert Kiyosaki amejichanganua kama mwanamapinduzi
wa mfumo wa elimu ambapo anatamani kuona elimu ya fedha inafundishwa mashuleni.
Hii ni pamoja na wazazi kuhakikisha wanawafundhisha watoto wao mbinu mpya
kuhusiana na pesa badala kuendelea kutumia mbinu za zamani. Mfano, katika jamii
tumezoea kusikia kauli kama vile “nenda shule, mwanangu soma kwa bidii, ili
upate kazi nzuri ambayo itakuwezesha uishi maisha mazuri”. Kwa Kiyosaki kauli
zote hizo ni kizamani kwa kuwa hazina uhalisia katika maisha ya sasa.
Katika kitabu cha Be Rich & Happy (Kuwa
Tajiri na Mwenye Furaha), Kiyosaki anatushirikisha kuwa muda umefika ambapo
mfumo wa elimu unahitaji kubadilishwa ili kuondoa makundi ya kutenga wanafunzi
katika madaraja ya wenye akili na wasiyo na akili kwa kutumia kigezo kimoja tu cha
ufaulu wa darasani.
Mfumo huu umendelea kupoteza vipaji vingi kwa
vile watoto wengi wakishaambiwa kuwa hawana akili wanapoteza ubunifu ambao kila
mtoto anazaliwa nao. Mbaya zaidi ni kwamba baada ya kumaliza masomo hata wale
ambao walionekana wana akili darasani linapokuja suala la mafanikio ya fedha
hali zao ni mbaya zaidi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba watoto hawa walikalilishwa
mambo mengi ambayo hayana tija katika maisha yao. Kumbe kuna kila sababu ya
kuhakikisha mfumo wa elimu unabadilishwa ili uendane na uhalisia wa maisha.
Karibu ushirikiane nami kujifunza machache
kati ya mengi ambayo mwandishi anatushirikisha katika kitabu hiki:
1. Mbegu
za kutofanikiwa zinapandwa katika maisha yetu tangu enzi za utoto wetu. Mfano,
katika hatua mbalimbali za ukuaji tumeambiwa mara kadhaa kama vile: (a)
mwanangu unapaswa kuwa mtoto mwema; (b) tekeleza unachoambiwa; (c) hapana,
haupo sahihi, sio kweli; (d) hili ndilo jibu sahihi; (e) ukifanya vyema shuleni
una uhakika wa kufanikisha maisha. Kauli zote hizi zinapunguza uwezo wa mtoto
katika kubuni, kuthubutu, kujaribu mambo mapya na mbaya zaidi ni pale ambapo
hata baada ya kukua kauli hizi zinaendelea kutumika katika jamii inayomzunguka.
Matokeo yake ni kwamba ile nguvu kubwa ambayo kila mmoja anarithishwa wakati wa
kuzaliwa inadumazwa kiasi ambacho haiwezi kuzaa matunda.
2. Mfumo
wa elimu wa sasa unawazadia wale wanaofanya vyema shuleni na kuwahadhibu wale
ambao hawafanyi vyema. Wale ambao uwezo wao wa kujifunza ni wa kawaida (kasi
ndogo) wanaonekana hawana akili na pengine wanafukuzwa au kulazimishwa kukalili
darasa. Hali hii inadumaza akili ya mtoto kwa kujiona kuwa yeye hana akili.
Ukweli ni kwamba kila mtu ana akili hila uwezo wetu unatofautiana kulingana
sekta moja kwenda nyingine. Mfano, katika jamii inayotuzunguka utagundua kuwa
ukilinganisha wafanyabiashara na wafanyakazi (mfumo wa ajira rasmi) utagundua
kuwa wafanyabiashara wengi waliofanikiwa kifedha ni wale ambao darasani
waliambiwa kuwa hawana akili kwa maana hawakufahulu mtihani wa darasa saba au
kidato cha nne. Hali hii inatoa fundisho kuwa kushindwa hesabu au historia
haina maana kuwa mtoto hawezi kufanikiwa katika maisha. Mzazi una wajibu mkubwa
wa kuhakikisha unamuandaa mwanao kufanikiwa kimaisha bila kujali uwezo wake
darasani.
3. Uoga
wa kufanya makosa ambao tumefundishwa shuleni unaendelea kuandama maisha yetu
hata katika kipindi ya utu uzima. Mfumo wa elimu uliopo unamtaka mwanafunzi
kuepuka kufanya makosa na matokeo yake wale wanaoenda kinyume na majibu yalipo
kwenye orodha ya majibu katika vitabu wanaambiwa wamekosea au hawana akili.
Hali hii inamlazimisha mtoto kukalili majibu yaliyopo kitabuni na hivyo kushindwa
kufungua uelewa wake kulingana na mazingira yanayomzunguka. Matokeo yake mtoto
anaendelea kuamini kuwa katika maisha hautakiwi kufanya makosa. Hata hivyo,
ukweli ni kwamba katika maisha ya kila siku makosa ni sehemu ya kujifunza na
hivyo kama haupo tayari kukosea maana yake ni kwamba haupo tayari kujaribu kitu
kipya katika maisha yako.
4. Katika
maisha ya mafanikio unahitaji kuwa na uelewa kiasi kwenye kila sekta ya maisha
yako. Mfano kwa kutaja tu baadhi, unahitaji kuwa na uelewa kwenye misingi ya elimu
ya fedha, uelewa kwenye sekta ya kiroho, historia, sayansi, jiografia, uchumi,
afya, mazingira unayoishi (viumbe hai na visivyo hai), jamii, uelewa wa kanuni
za asili na uelewa wa siasa. Katika kila sekta hizo unapaswa kufahamu ni jinsi
gani zinaathiri maisha yako katika upande chanya au hasi. Mfumo, wa elimu ya
sasa unamtaka mwanafunzi kujitikita kwenye vitu vichache ili awe mbobevu katika
hivyo. Matokeo yake ni kwamba tuna wasomi wengi ambao hawa mbinu za misingi
muhimu ya maisha yao. Mfano, asilimia kubwa ya wasomi ndio wanaoongoza kuchukua
mikopo hisiyo na tija au matumizi makubwa kuliko pato lao hali ambayo inatokana
na kukosekana kwa elimu ya pesa.
5.
Mfumo wa elimu ya sasa unakandamiza uwezo wa mwanafunzi kuuliza maswali. Kama
ambavyo tumeona hapo juu kuwa mwanafunzi anatakiwa kutoa majibu sawa na yale
yaliyopo kitabuni, matokeo yake ni kwamba uwezo wa kuuliza maswali nje ya
yaliyopo kitabuni unakufa. Hali hii haishii katika enzi za kusoma kwani hata
baada ya kumaliza masomo katika mifumo ya Serikali au kazini tunaambiwa
kutokwenda kinyume na misingi iliyopo. Matokeo yake ni kwamba yule anayeuliza
maswali nje ya mfumo ataonekana mkorofi, mtukutu, msaliti na wakati mwingine
mwenda wazimu.
6.
Mfumo wa elimu uliopo unahamasisha jamii kuwa wabinafsi kuliko kupendana na
kusaidiana. Darasani kila mwanafunzi anapambana awe namba moja kwenye kila
somo. Hali hii inatokana na ukweli kwamba wale wanaofanya vizuri wanaonekana
ndo vichwa vya darasa japo kwenye uhalisia wa maisha ni kinyume chake. Katika
hali kama hiyo tokea enzi za utotoni tunafundishwa kutanguliza nafsi zetu
kuliko maslahi mapana ya wanaotuzunguka. Kama mzazi una wajibu wa kuhakikisha
unamfunda mwanao kwenda kinyume na mfumo huu ili mbegu ya upendo na kusaidiana
iendelee kukua na kuongezeka ndani mwake.
7.
Kutokana na elimu ya pesa kukosekana katika mfumo wa elimu na hata katika
malezi ya watoto kutoka kwa wazazi – jamii inaendelea kuwa na idadi kubwa ya watumishi
au wafanyakazi ambao kila mwezi wanasubiria tarehe ya mshahara kwa hamu. Ukweli
ni kwamba wale ambao walionekana kuwa vichwa darasani baada ya kuajiriwa
wanajikuta kwenye wakati mgumu wa kifedha. Mfano, ukitaka kugundua kuwa hali
hii inaendelea katika jamii yetu tembelea taasisi za kibenki hasa NMB kuanzia
tarehe 23 hadi 25 ndipo utagundua kuwa wafanyakazi wengi mshahara hauungi. Tatizo
hili sio tu kwa wafanyakazi bali linaendelea kutengeneza idadi kubwa ya
masikini katika jamii. Jamii ina idadi kubwa ya watu ambao wanafanya kazi ili wapate
kula na siku wakiachishwa kazi hata kwa mwezi mmoja maisha yao yanakuwa
hatarini.
8. Mshahara
haujawahi kutosha na ndio maana wafanyakazi kilio chao kikubwa ni nyongeza ya
mshahara ya kila mwaka au kupandishwa vyeo. Mwandishi anatushirikisha kuwa
hauwezi kuwa tajiri kwa mshahara bali unafanya nini kupitia mshahara huo ndicho
kitakufanya uwe tajiri. Pamoja na kwamba waajiriwa ni kati ya wanafunzi
waliofanya vyema darasani, maisha yao yanakumbwa na msongo wa mawazo unaosababishwa
na uhaba wa fedha kwa ajili ya mahitaji ya kila siku. Kumbe kinachokosekana kwa
jamii hii ya watu ni kukosekana kwa elimu ya fedha ambayo ndio msingi mkuu wa
kuwezesha fedha kidogo wanazopata kuandaa maisha yao ya baadae yenye uhuru wa
kifedha.
9. Njia
bora ya kuepukana na kuishi kwa kutegemea mshahara (maisha ya mshahara kwa
mshahara) ni kuwa na vyanzo vingi vya mapato. Mwandishi anatushirikisha kuwa
mshahara sio chanzo halisi ya mapato kutokana na ukweli kwamba unapata mshahara
kulingana na uwepo wako kazini. Mfano, ikitokea ukapata matatizo ya kiafya kiasi
ambacho utapoteza uwezo wa kufanya kazi – hakuna mwajiri ambaye ataendelea
kukulipa mshahara. Unalipwa kutokana na kazi unayofanya kazi.
10.
Changamoto za kifedha zinazotukabili katika maisha yetu zinatokana na maamuzi
yetu kuhusu matumizi ya fedha zinazoingia mikononi mwetu. Mwandishi anatushirikisha
kuwa katika jamii watu wengi wanawaza kuwa ili uwe tajiri ni lazima upate
muujiza wa kupata fedha nyingi ili zitumike kama mtaji. Ukweli ni kwamba mtaji
wa kuanzisha biashara unayofikiria upo mikononi mwako. Ni suala la kuweka mpangilio
wa matumizi ya fedha sambamba na kuhakikisha unajilipa kwanza kwenye kila
shilingi inayoingia mkononi mwako.
11. Hakuna
jibu pekee ambalo ni sahihi katika changamoto zinazokukabili. Mwandishi
anatushirikisha kuwa mfumo wa maisha tunaoishi kwa sasa ni wa kujikita kwenye
jibu moja ambalo ni sahihi. Hali hii inapunguza uwezo wa kufikiria kuhusu mbinu
mbadala katika kila changamoto inayokukabali kwa maneno mengine inapunguza
ubunifu katika jamii zetu.
12. Maana
halisi ya kazi yenye usalama/nzuri ni: (a) kufanya kazi pale unapotaka kufanya
kazi sambamba na kuchagua mtu wa kufanya nae kazi; (b) kuwa huru kutofanya
chochote ambacho kipo nje ya utashi wako; (c) kuwezesha kupata chochote
unachotaka bila kuathiri maisha yako; (d) yenye uwezo wa kuongeza au kupunguza
pato lako muda wowote ule unaotaka wewe; (e) yenye uhuru wa kifedha kwa ajili
kukidhi mahitaji ya kifedha; (f) kukuwezesha kuwa na uhuru wa kuishi sehemu yoyote
ile unayotaka; na (g) kukuwezesha kusafiri sehemu yoyote kwa gharama zako bila
kuwa na wasiwasi. Hapa tujiulize kama kazi tunazofanya zina usalama tulioambiwa
na jamii yetu. Mfano katika hatua mbalimbali za ukuaji utakuwa ulizoea kuambiwa
kauli kama “kazana na masomo ili upate kazi nzuri na yenye usalama Serikalini”
lakini kiuhalisia kama ulifanikiwa kupata kazi hiyo Serikalini au kwenye
mashirika yasiyo ya Serikali utakuwa tayari umegundua kuwa kazi hiyo siyo
salama kama ulivyodhania. Hiki ni kilio cha waajiriwa walio wengi na ndio maana
kila siku vilio vya nyongeza ya mshahara vinasikika kila kona sehemu za kazi.
13. Mwandishi
anatushirikisha kuwa kuna njia tatu za kujifunza ambazo ni:
(a) Kujifunza
kwa kutumia akili – njia hii inahusisha kujifunza kwa kujaza akili ya muhusika kupitia
kukalili ukweli ambao tayari umewekwa kwenye mifumo ya kumbukumbu;
(b) Kujifunza
kwa vitendo – njia hii inahusisha sehemu zote za mwili na akili katika kupata
maarifa mapya; na
(c)
Kujifunza kwa kutumia hisia na fahamu – njia hii inamwezesha mhusika kujihisi
furaha, amani, huzuni, hofu, huruma na upendo.
Hata hivyo, mfumo wa elimu ya sasa unajikita
kwenye njia ya kwanza pekee na kuachana na njia nyingine mbili. Hali hii
inapelekea kuwa na jamii ambayo uwezo wake wa kufikiri ni mdogo kwa vile ni zao
la kukalili majibu ambayo mara nyingi hayana tija katika uhalisia wa maisha.
14. Kujifunza
kunahusisha hatua nne ambazo ni:
(i) Hatua
ya kutokuwa na ufahamu na uwezo – katika hatua hii unakuwa na hamu ya kujifunza
kitu kipya (tumia mfano wa kuendesha baiskeli) lakini kwa kuwa hujawahi kufanya
kitu hicho (kuendesha baiskeli) haujui ni misingi ipi unatakiwa kujifunza;
(ii) Hatua
ya kuwa na ufahamu lakini hauna uwezo – tayari unatambua misingi ipi unatakiwa
kujifunza lakini kivitendo bado hauna uwezo (mfano tayari umepanda kwenye
baiskeli lakini kwa vile haujui mbinu za kuendesha kila ukijaribu kuendesha
unaanguka);
(iii) Hatua
ya kuwa na ufahamu pamoja na uwezo – katika hatua hii kupitia makosa na
kurekebishwa kwa makosa hayo sasa unajua kuendesha baiskeli na unaweza kuendesha
baada ya kujua tatizo lilokuwa linakukwamisha;
(iv)
Kutokuwa na ufahamu lakini una uwezo – hatua hii sasa tayari wewe ni mbobevu wa
kuendesha baiskeli na unaweza kufanya hivyo bila hata kufikiria kila hatua
katika uendeshaji. Maarifa sasa yamekuwa sehemu ya akili yako na yanatekelezeka
moja kwa moja bila kushirikisha mfumo wako wa akili.
Mwandishi anatushirikisha kuwa kwa bahati
mbaya sana, elimu ya sasa hairuhusu mwanafunzi kutumia hatua zote hizo za
kujifunza. Hii ni kuanzia elimu ya msingi hadi elimu ya juu kwani hakuna
mwanafunzi anayefurahia kujifunza maarifa mapya kwa vile mfumo wa elimu umekuwa
ni wakupeana presha. Athari hii haishii shuleni bali inaenda hadi kwenye mfumo
wa utendaji kazi. Kama mzazi, wajibu wako ni kuhakikisha unatumia hatua hizo
katika kuwafundisha watoto wako maarifa mapya katika maisha yao.
15. Mfumo
wa elimu ya sasa unasababisha asilimia kubwa ya watu (zaidi ya asilimia 80)
kuendelea kuridhika na hali waliyonayo (hali ya umasikini, huzuni na msongo wa
mawazo). Ukweli ni kwamba ni lazima wawe katika hali hiyo kwa kuwa
wamefundishwa kuepuka kufanya makosa katika maisha tokea enzi za utoto wao. Mfano,
kinda la ndege likiwa bado halijaweza kuruka likiridhika kukaa kwenye kiota
litaendelea kuishi humo milele na milele. Lakini pale linapoamua kuruka kwa
mara ya kwanza litapitia kwenye changamoto zinazotokana na kutojua misingi
sahihi ya kuruka angani. Baada ya kurudia makosa hayo mara kwa mara litajifunza
misingi hiyo na kufanikisha kuruka kwa usahihi. Mwandishi anatushirikisha kuwa
na maisha ya mwanadamu yapo hivyo lakini kwa kuwa amefundishwa kuogopa kufanya
makosa matokeo yake anaendelea kuishi kwenye kiota chake kipindi chote cha maisha
yake. Mwisho wa maisha yake anaondoka Duniani akiwa bado hajatumia uwezo halisi
aliopewa na Mungu. Wachache wanaothubutu (chini ya asilimia 20) ndio wanaitwa majiniasi
au wenye mafanikio makubwa sana.
16. Kutojifunza
kutokana na makosa kunasababishwa na tabia nne za mwanadamu ambazo kwa asilimia
kubwa amejifunza kutokana na mfumo wa elimu nazo ni:
(a) Kutokukubali
kuwa umetenda kosa – pale unapotenda kosa haupo tayari kujitokeza na kusema
nimekosea;
(b) Kutafuta
sehemu, mtu au mazingira ya kusingizia kuwa ndo yamepelekea kosa husika
lifanyike – kila mmoja anatafuta namna ya kujinasua kwenye kosa husika;
(c) Kukubaliana
na kosa hilo badala ya kujifunza kutokana na kosa husika – mfano katika hali
ukata wa fedha badala ya kutafuta kwa nini hali hiyo ni changamoto kwa mhusika
utasikia ajisemea kauli kama vile “fedha sio hitaji la msingi katika maisha”;
na
(d) Kuendelea
kujipa adhabu kutokana na makosa yaliyopita – katika tabia hii mhusika
anaendelea kuona kuwa kila analofanya hawezi kufanikisha kutokana na makosa
aliyofanya siku za nyuma. Mwandishi anatushirikisha kuwa ili ujifunze kutumia
makosa yako kwa faida ni lazima uepukane na tabia zote nne katika maisha yako
ya kila siku.
17. Athari
za kutaka kuwa sahihi katika kila kitu ni pamoja na:
(a)
Kushindwa kuona yajayo – mtu ambaye anajiona kuwa yupo sahihi mara nyingi huwa
anakomaa na taarifa/ujuzi wa zamani ambao pengine hauna nafasi au siyo sahihi
tena katika nyakati zilizopo au zijazo. Ili kujifunza kutokana na makosa kamwe
hatupaswi kusema kuwa wazo hilo siyo sahihi badala yake tunakiwa kuchukua muda
wa kulitafakari na kuelewa mazuri na mabaya yaliyopo ndani mwake;
(b)
Kushindwa kuongeza utajiri hasa utajiri wa maarifa/ujuzi. Mwandishi anatushirikisha
kuwa mtu ambaye anajiona yuko sahihi mara zote hana muda wa kujifunza vitu
vipya katika maisha yake. Na mara nyingi watu wa aina hiyo ni wabishi kwa kila
wazo jipya;
(c) Kuongezeka
kwa migogoro – mtu anayejiona kuwa sahihi yupo tayari kufanya lolote
kudhihirisha kuwa upande wake ndio sahihi. Mfano, angalia migogoro kati ya
dhehebu moja na jingine au kati ya Wakristu na Waislamu;
(d) Kipato
kilichodumaa – katika sehemu nyingi za biashara au kazini watu wanalipwa au
kupandishwa vyeo kutokana na kile wanachojua hasa ujuzi au maarifa mapya sehemu
ya kazi/biashara. Watu wanaojiona kuwa sahihi nyakati zote hawana muda wa
kujifunza maarifa mapya matokeo yake ni kuendelea kuwa na pato duni;
(e) Giza
nene katika maisha ya baadae – watu wengi katika kundi la “nipo sahihi au hilo
siyo kweli” hawana uhakika wa maisha yao ya baadae kutokana na kushindwa kuona
fursa mpya katika maisha. Matokeo yake ni kuongezeka kwa msongo wa mawazo; na
(f)
Kuongezeka kwa upofu wa maono ya fursa zinazowazunguka – mwandishi anatushirikisha
kuwa Dunia ipo jinsi tunavyoiona ilivyo na kadri tunavyobadilisha mtazamo wetu
kuhusu Dunia ndivyo tutaona mengi ambayo hatujawahi kuyaona; na
(g)
Kushindwa kuendana na nyakati – adhabu ya kutoenda na wakati ni kuadhibiwa na
ulimwengu na hivyo kushindwa kupata kile ambacho mhusika alikusudia katika
maisha.
Mwisho Mwandishi anatushirikisha kuwa KWELI au
SIYO KWELI ni mtazamo tu ambao jamii imekubaliana lakini haina maana kuwa kila
unachoambiwa ni KWELI au SIYO KWELI ni sahihi katika uhalisia wa maisha. Kuwa
tayari kufanya makosa kwa kasi na kwa kadri uwezavyo ili kupitia makose
ujifunze masomo mengi katika maisha yako.
18. Kama
tunahitaji kubadilisha mfumo wa elimu uliopo ni lazima kwanza tuache kutumia hofu
kama nyenzo muhimu ya kuwalazimisha wanafunzi wajifunze. Wote ni mashahidi kuwa
mfumo wa elimu wa sasa unatumia hofu ambayo inatengenezwa na mzazi/mwalimu
dhidi ya mwanafunzi. Mwanafunzi analazimika kusoma sana tena kwa kukalili ili
afanye vyema kwenye mitihani ya darasani na hatimaye afanikiwe kupata kazi
nzuri yenye malipo bora. Mwandishi anatushirikisha kuwa badala ya kutumia hofu
tunatakiwa kutumia mbinu ambazo zitamfanya mwanafunzi aone kujifunza ni sehemu
ya furaha. Katika kila anachojifunza atumie njia zote 3 kama zilivyo ainishwa
kwenye pointi ya 13 katika makala hiii. Hivyo, wewe mzazi kuanzia sasa
unatakiwa kuwa wa kwanza kuachana na kutumia mfumo wa hofu kama nyenzo ya kumlazimisha
mtoto wako kujifunza na badala yake tumia mbinu ambazo mtoto atafurahia
kujifunza kwa kutumia akili, mwili na hisia.
19. Watoto
wanahitaji kufundishwa elimu ya pesa sawa na ilivyo kwenye masomo au malezi
mengine. Mwandishi anatushirikisha kuwa sababu ya elimu ya pesa kuendelea kuwa tatizo
gumu kwa jamii ni kutokana na elimu hii haifundishwi kwa watoto toka enzi za
ukuaji. Si wazazi au walimu ambao wapo tayari kufundisha elimu ya pesa kwa
watoto, matokeo yake watoto wanaifahamu pesa katika kipindi ambacho
walishachelewa kuitumia kubadilisha maisha yao. Mara nyingi katika ukuaji
tumezoea kuambiwa kuwa mtoto anayependa pesa atakuwa mwizi, mara mchoyo, mara
ukipenda pesa utashindwa kufanya vyema kimasomo na mengine mengi. Kauli zote
hizi zinadumaza akili ya mtoto kuhusiana na sekta ya pesa katika maisha yake. Kumbe,
kama mzazi kuanzia sasa utambue kuwa una wajibu mkubwa wa kuhakikisha unakuwa
mwalimu wa somo la pesa kwa mwanao. Mshirikishe mambo muhumi kuhusiana na pesa;
mfundishe kwa nini pesa ni muhimu katika maisha ya mwanadamu; mfundishe namna
ya kutengeneza pesa kwa njia huru, halali na haki; mfundishe kuhusu uwekezaji
akiwa bado mdogo; na mfundishe kila kitu kuhusiana pesa.
20. Kama
unahitaji kuwa tajiri ni lazima ufikirie utajiri unaoutaka katika maisha yako
kama mti wa matunda au mbao. Ili upate matunda ya mti ni lazima kwanza mti huo
uoteshwe, umwagiliwe na kuondolea matawi ambayo hayafai mpaka ukomae kufikia
umri wa kuzaa matunda. Na utajiri pia unatengenezwa kwa njia hizo hizo, ni
lazima uoteshe mbegu, imwagiliwe, ipaliliwe na kukingwa dhidi ya wadudu au moto
hadi pale ambapo mbegu itazaa matunda. Tatizo lililopo katika jamii ni kwamba
walio wengi wanaweza kupanda mti wa matunda na wakavumilia hadi pale utakapozaa
matunda lakini linapokuja suala la mti wa utajiri wengi wanaanza kula mbegu,
mizizi, majani na hivyo mti wa utajiri unashindwa kukomaa hadi kufikia hatua ya
kuzaa matunda.
21. Ili
uwe tajiri ni lazima:
(a) Uanze
kuwekeza muda na fedha zako kwa ajili ya uwekezaji badala ya kutumia ovyo
kwenye mambo yasiyo na tija. Kumbuka kuwa pesa uliyonayo sasa pamoja na muda
wako ndio mbegu muhimu ya kutengeneza mti wa utajiri. Mara zote katika maisha
yako tumia kanuni hii “Matajiri wanawekeza wakati masikini wanatumia”.
(b) Anzisha
biashara ambayo utaifanya kwa mapenzi ya dhati katika kipindi chote cha maisha
yako. Mwandishi anatushirikisha kuwa inachukua kipindi cha kati ya miaka 5 hadi
10 kutengeneza biashara yenye mafanikio. Hakikisha biashara unayoanzisha iwe
sehemu ya kukamilisha mahitaji muhimu kwenye kila sekta ya maisha yako.
(c)
Hakikisha wewe pamoja na familia yako mnajinyima katika kipindi chote cha
kutengeneza utajiri wako. Ajenda ya kutengeneza utajiri ni lazima iwe ajenda ya
familia na sio ajenda yako pekee. Hakikisha kila mmoja ndani ya familia
anafahamu kuwa mnaishi kwa kunyima katika kipindi maalumu na baada ya hapo hali
ya maisha itakuwa sawa.
Haya ni machache kati ya mengi yaliyopo ndani
ya kitabu hiki ambacho mwandishi Kiyosaki ametushirikisha. Jiunge na mtandao wa
Fikra za Kitajiri kwa KUBONYEZA HAPA.
Endelea
kusambaza makala hizi kwa kadri uwezavyo ili ndugu, jamaa na marafiki wanufaike
kwa kujifunza maarifa mbalimbali kutoka kwa waandishi wa vitabu. Kumbuka
umepata makala hii bila malipo yoyote hivyo hakikisha na wewe unaisambaza bure.
(Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share
link). Nakutakia mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe: fikrazatajiri@gmail.com
|