Habari ya leo rafiki
na msomaji wa mtandao wa Fikra za Kitajiri. Naamini unaendelea vyema kiafya,
kiroho na kiakili kwa ajili ya kuboresha Dunia hii kuwa mahala pazuri pa
kuishi. Karibu tena katika makala ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii.
Kama bado hujajiunga
na mfumo wetu wa kupokea makala za uchambuzi wa vitabu, tafadhali fanya hivyo KWA KUBONYEZA HAPA na
kujaza fomu kisha bofya “jiunge/subscribe”. Ni fursa ambayo itakuwezesha kupata
uchambuzi wa vitabu kwa lugha rahisi kupitia barua pepe yako.
Kitabu cha wiki hii ni
“An
Hour to Live, An Hour to Love” kutoka kwa mwandishi Richard Carlson na
Kristine Carlson. Katika kitabu hiki tunashirikishwa umuhimu wa kuishi kwa
upendo wa dhati kama familia. Aidha, tunashirikishwa kuwa yapo matukio mengi ambayo
kama familia yakifanyika yanasaidia kukuza upendo tena bila gharama yoyote.
Katika kitabu hiki Kristine anakumbuka upendo
wa kweli kutoka kwa mwandishi mwenza Richard Carlson (mme wake) kwa jinsi
ambavyo katika siku za maisha yake ameacha alama kubwa katika familia yake. Pamoja
na kwamba Richard ameondoka mapema lakini bado anaishi ndani ya familia yake. Hivyo,
kitabu hiki ni muhimu kwa wale ambao wana familia au wanakusudia kuwa na familia
bora katika maisha yao.
Karibu ushirikiane nami kujifunza machache
kati ya mengi ambayo tunashirikishwa katika kitabu hiki:
1. Mara
nyingi baada ya ukomo wa maisha yako hapa duniani hautakumbukwa kwa yale
uliyokamilisha katika maisha bali kwa namna gani kila ulichofanya ulitekeleza kwa
upendo katika enzi za maisha yako. Upendo ni zawadi ya kipekee ambayo tumepewa
kama kiungo muhimu cha kutuunganisha katika jamii. Hivyo, haijalishi
unajishughulisha na nini au nini umefanikisha katika maisha, kama yote hayo hakuna
upendo ndani mwake, hakika hauwezi kuwa na furaha ya kweli katika maisha yako.
2. Maisha
ni fumbo ambalo hakuna anayejua tukio linalokuja katika maisha yake ya baadae. Ni
kutokana na ukweli huu, kila muda wa saa unaoishi unapaswa kujiuliza katika
muda huu ni nani napaswa kuwasiliana nae na mawasiliano yetu yajikite kwenye
mada ipi. Mfano, katika maisha mara nyingi tunakuwa mbali na familia zetu – ni
katika kipindi hicho tunaweza kuendelea kuwa pamoja kwa kuwasiliana kwa simu na
wote mkaunganishwa na neno moja – upendo. Aidha, neno moja linalonenwa kwa
upendo wa dhati linaweza kuwa alama ya kukumbukwa kipindi chote cha maisha ya
mhusika.
3. Katika
nyakati ambapo mauti yanakaribia binadamu anakuwa na mfadhahiko kwa kujutia
yale ambayo hakufanikiwa kutenda katika maisha yake. Mwandishi anatushirikisha
kuwa mara nyingi yale ambayo wengi wanajutia yanakuwa ni mambo madogo madogo
ambayo yalikuwa ndani ya uwezo wao. Wengi wanashindwa kukamilisha vitu vidogo japo
ni viungo muhimu vya pendo la dhati kwa kuwa wanachukulia maisha kana kwamba
mwisho wake bado. Hivyo, mwandishi anatushirikisha kuwa ni muhimu kupanga
mipango yetu kwa ukamilisho kana kwamba kesho hatutakuwepo duniani hapa.
4. Jiulize swali kuwa katika kipindi ambacho
mauti yanakunyemelea na ikatokea ukaambiwa kuwa una dakika sitini za kuishi, Je
ungetamani kumpigia nani simu au kuomba uongee na nani? Je katika kipindi hicho
utatamani kuongea na: Wapangaji wako? Mshauri wako wa masuala ya uwekezaji? Meneja
wa Benki? Mwanasheria wako? Hakika utagundua kuwa hao wote nyakati kama hizo
sio wa msaada tena.
5. Asilimia
kubwa katika nyakati hizo watahitaji kuongea au kuonana na wenza wao (mme/mke),
watoto, wazazi au ndugu kwa ujumla (familia). Pia, asilimia kubwa ya maongezi
yao huwa ni kujutia yale ambayo hawakukamilisha katika enzi za maisha yao. Hivyo,
wengi wanaishia kuomba msamaha au kutoa nasaha kwa wale ambao wanabaki duniani.
Mwandishi anatushirikisha kuwa yale ambayo wengi wanajutia ni kati ya majukumu/wajibu
waliotakiwa kukamilisha enzi za maisha yao. Kumbe, somo kubwa hapa ni kwamba
katika maisha tunatakiwa kuishi kana kwamba tupo kwenye saa moja ya mwisho wa
maisha yetu.
6. Lengo
kubwa katika kila tunalofanya kwenye maisha ni lazima lijumuishe umuhimu wa kuwa
na huruma, unyenyekevu, upole, fadhira, faraja na mengine yote yanayokamilisha
maisha ya upendo. Hakika yote haya yanaleta faraja kwa mtu yoyote katika
kipindi cha mhusika kupigania siku za mwisho wa maisha yake. Pia, ni matendo
hayo yanaacha alama kwa kila aliyeguswa katika siku za maisha yake hata baada
ya ukomo wa siku za maisha yako.
7. Ili
kuishi maisha ya ukamilisho katika kila saa ya maisha yetu ni lazima
tuisikilize roho iliyopo ndani mwetu kuliko kuishi kwa kufuata akili zetu au
matakwa ya mwili. Mwandishi anatushirikisha kuwa mara nyingi maisha ya
mwanadamu yanatawaliwa na matendo ya kimwili hasa kutokana na kujipenda zaidi
kuliko jamii inayozunguka. Ni kutokana na tabia hii kusikiliza matakwa ya mwili
kunapelekea wengi wajutie maisha waliyoishi katika nyakati za mwisho wa maisha
yako. Kumbe, tunakiwa kuishi kwa kutanguliza maslahi mapana ya wale
wanaotuzunguka ili katika kutimiza maslahi yao na sisi tunakamilisha kusudi la
maisha yetu.
8. Unahitaji
kutenga muda wa kukaa pamoja kama familia. Mwandishi anatushirikisha kuwa
watoto ni zawadi ambayo wazazi wanapewa na Mwenyezi Mungu. Na kila zawadi ina
sifa zake za kipekee. Kumbe, kama mzazi ili utambue sifa za kipekee zilizopo
ndani ya wanao ni lazima uwe na muda wa kutosha kukaa nao. Katika muda huo
unatakiwa kuwaonesha umuhimu wa kuishi maisha ya upendo kati yao kwa wao na
jamii wanakoishi sambamba na kuwapa mwongozo sahihi katika kila hatua ya maisha
yao.
9. Hakika
haupaswi kujutia kusema hapana kwa kiongozi wako wa kazi au kwa mtu yeyote ile
kama hapana hiyo ni kwa ajili ya kulinda maslahi mapana ya mwenza wako au
watoto wako. Mwandishi anatushirikisha kuwa chochote unachofanya ni lazima utangulize
maslahi ya wapendwa wako (mke/mme na watoto). Ni lazima uwe tayari kusimama
imara kwa ajili ya kuwatimizia matakwa yao ambayo kubwa zaidi ni upendo wako
dhidi yao. Nyakati nyingine inaweza kuwa ngumu lakini hakuna siku utajutia
kufanya hivyo kwa kuwa hao ndipo moyo wako unatakiwa kuwa kwani kila
unachofanya ni kwa ajili yao.
10. Furaha
ndo kila kitu katika maisha ya mwanadamu. Katika kila dakika unayoishi unatakiwa
kutafuta furaha hiyo sambamba na kuhakikisha wanafamilia wanapata furaha. Njia rahisi
ya kukuza furaha kati yenu kama familia ni kila mmoja kumwambia mwenza wake
upekee alionao kwake. Mfanye mwenza wako ajione kuwa na thamani kwa kuhakikisha
kila mara unamwelezea juu uthamani wake kwako. Wanao pia wanastahili kusikia
kutoka kwako kwa namna walivyo watoto wa kipekee hapa Duniani. Kwa kufanya
hivyo unaongeza uwezo wao wa kujihamini katika mazingira yanayowazunguka.
11.
Hakikisha maisha yako unayafanya kuwa filamu yenye matukio ya kuvutia ili hata
katika nyakati za kupigania uhai wa maisha yako kwenye ukomo wa maisha ujisikie
raha katika kila tukio unalokumbuka. Kumbuka kuwa maisha yako yanaundwa na matukio
ya wanafamilia. Kama kila tukio lililofanyika linakufanya utamani kulirudia
basi hakuna shaka kuwa umefanikiwa kuishi maisha yenye furaha ikilinganishwa na
maisha ya uzuni.
12. Nyakati
ngumu katika maisha hazikwepeki lakini hakikisha nyakati hizo zinatumika kuwa
nyakati muhimu za maisha yako. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika maisha
kuna kupanda na kushuka. Kama familia mnatakiwa kuwa na umoja pamoja na
kuhakikisha mnalinda upendo ili kuvuka katika nyakati hizo ngumu mpate kuvuka
salama.
13. Katika
kila mwanamme mwenye mafanikio nyuma yake kuna mwanamke shupavu. Mwandishi anatushirikisha
kuwa wanawake wana nguvu kubwa ya kuhamasisha wenza wao japo ni wanaume
wachache ambao wamefanikiwa kutumia nguvu hiyo. Nguvu hiyo inahusisha uwezo wao
katika kusimamia maamuzi ya familia, kushauri, kutimiza wajibu, upendo wa kweli
sambamba na kufanya kazi kwa bidii. Hata hivyo, ni wanaume wachache sana ambao
wamevuna matunda ya wake zao. Kumbe, tunatakiwa kuwapa nafasi stahiki wake zetu
au wake watarajiwa ili tupate kuvuna nguvu ya ushindi iliyopo ndani mwao.
14.
Uchoyo wa mafanikio unapelekea kupoteza kusudio la maisha kwa kuwa unapelekea
kupoteza upendo ndani mwetu. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika kila
tunachofanya tunatanguliza malipo kuliko lengo zima la kusaidiana kimaisha. Mbaya
zaidi ni kwamba hakuna anayeridhika na kile anachopata na matokeo yake kila
siku ni kujikita kwenye matukio ya kuridhisha nafsi zetu kuliko nafsi za wanaotuzunguka
(familia kwanza). Hakika tunapoishi kwa mtazamo huu (mtazamo wa kuridhisha
mwili) hakika katika nyakati za ukomo wa maisha yetu tutajikuta tuna pengo
kubwa ambalo tumeshindwa kulitimiza katika siku za maisha yetu.
15. Kuwa
tayari kumfariji mwenza wako katika nyakati za huzuni katika kipindi cha maisha
yenu. Mwandishi anatushirikisha kuwa matukio yanayohuzunisha ni sehemu ya
maisha ya wanafamilia. Katika nyakati kama hizo ni lazima utambue wajibu wako
ili kumsaidia mwenza wako kuepuka maumivu yanayomkabili mapema iwezekanavyo. Tumia
maneno yenye faraja kwa kadri uwezavyo ili kupunguza mawazo na maumivu yake. Nyakati
ngumu katika maisha zinawezakuwa: kufiwa na mpendwa au ndugu; kufukuzwa kazi;
kupata ajali; magonjwa; kufilisika au kufungwa jela.
16. Hakikisha
unajenga utamaduni wa kusikiliza zaidi kuliko kuongea. Mwandishi anatushirikisha
kuwa upendo wa familia unajengwa kwa kusikiliza zaidi wenza wako na hatimaye
kutatua changamoto kwa pamoja. Hata hivyo, katika jamii wazazi wengi hawana
muda wa kusikilizana wao kwa wao au kuwasikiliza watoto. Kumbuka kuwa bila
kusikilizana ni vigumu kutambua changamoto mnazopitia kama wanafamilia. Kumbe wewe
baba hakikisha unamsikiliza mke wako mpenzi sawa na ilivyo yeye kwako. Pia,
hakikisha wote kwa pamoja mnakuwa kimbilio la watoto pale ambapo wanahitaji msikie
sauti yao.
17. Maisha
yanakuwa na mafupi na yasiyo na furaha kwa kuwa muda mwingi tunabanwa na
majukumu ya kila siku. Ukweli ni kwamba kila siku tunaikimbiza furaha kwa
kufanya kazi kwa bidii tukitegemea kuwa kesho itakuwa ya furaha zaidi kuliko
sasa. Hata hivyo, baada ya kuifikia kesho na kilele cha yale tuliyojibidisha
nayo jana tunajikuta katika hali ya kuhitahiji kukamilisha zaidi na zaidi katika
ziku zijazo. Haya ndio maisha ya mwanadamu na ndio maana tuna msemo kuwa kila
kukicha ni bora zaidi ya jana. Mwandishi anatushirikisha kuwa maisha haya ni
sawa na mbio za panya ambazo mara nyingi zinaishia ukutani. Kumbe ili kuepukana
na maisha ya namna hii mwandishi anatushauri kuwa furaha ya kweli inatengenezwa
katika kila tukio tunalofanya kwenye kila dakika ya maisha yetu. Kwa maana
nyingine, tunatakiwa kuishi katika sasa badala ya kuishi kulingana na jana au
hofu ya kesho.
18. Kitu
pekee ambacho kila mwanadamu anaweza kufanikisha katika maisha ni kuhakikisha
anatekeleza kila jambo kwa kadri ya uwezo wake japo kwa mapendo ndani yake. Mama
Theresa aliliweka hili sawa kuwa “hatuwezi kufanya mambo makubwa katika uso huu
wa Dunia bali tunachoweza kufanya ni mambo madogo kwa pendo la dhati ndani yake”.
Kumbe vitu vidogo vinaweza kuwa vitu vikubwa katika kukamilisha furaha yetu
pale tu tunapohakikisha roho zetu zinakuwepo katika kila tunachofanya. Mfano,
unaweza kuunganishwa kwa upendo na mwenza wako kwa matembezi tu cha msingi muwe
mmekusudia kufanya hivyo. Katika matembezi hayo kila mmoja atajikuta kwenye
muunganiko wa penzi la dhati.
19. Kusudi
kubwa la msingi wa uwepo wetu hapa Duniani ni kuwatumikia wengine na kumtumikia
Mungu. Malipo ya kazi hii yanadumu milele hata baada ya ukomo wa maisha yako. Hii
ni kutokana na ukweli kuwa msingi huu unajengwa na upendo, dhamira, ukaribu,
upole, ukarimu na huruma kwa wengine. Hivyo, wote tunatakiwa kutafuta
ukamilisho wa msingi huu kwani mengine ni yote ni ziada.
20. Kuna
neema katika nyakati za kilio. Mwandishi Kristine kama mwandishi mwenza wa
sehemu ya pili ya kitabu hiki anatushirikisha namna ambavyo baada ya kifo cha
mme wake aliweza kugundua kusudio la maisha yake katika nyakati za maombolezo. Pale
unapoomboleza kifo cha mtu wako wa karibu hasa ambaye mmeishi katika penzi kwa
muda mrefu kuna mengi ya kujifunza. Mengi kati ya hayo yanaweza kuwa mlango
muhimu wa kubadilisha mtazamo wa maisha kwa ajili ya maisha bora ya baadae.
Haya ni machache niliyojifunza kutoka katika
kitabu hiki, nimeona nikushirikishe kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Jiunge
na mtandao wa Fikra za Kitajiri kwa KUBONYEZA HAPA.
Endelea
kusambaza makala hizi kwa kadri uwezavyo ili ndugu, jamaa na marafiki wanufaike
kwa kujifunza maarifa mbalimbali kutoka kwa waandishi wa vitabu. Kumbuka
umepata makala hii bila malipo yoyote hivyo hakikisha na wewe unaisambaza bure.
(Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share
link). Nakutakia mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe: fikrazatajiri@gmail.com
|