Mambo Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha Automatic Millionaire: A Powerful One-step Plan to Live and Finish Rich (Utajiri wa Moja kwa Moja: Mwongozo wa Kuishi Maisha ya Utajiri).


Habari ya leo rafiki na msomaji wa mtandao wa Fikra za Kitajiri.

Rafiki naamini kuwa unaendelea kupambana kwa ajili ya kuhakikisha kesho yako inakuwa bora zaidi ya sasa. Ni lazima upambane kwa maana ya kufanya kazi kwa ubunifu na weledi ili kuhakikisha unatimiza ndoto za maisha yako.

Naendelea kutimiza ahadi yangu kwako ya kuhakikisha kila ninapopata muda nakushirikisha kile ninachojifunza kupitia uchambuzi wa vitabu ninavyosoma. Ni mategemeo yangu kuwa Makala hizi za uchambuzi wa vitabu zimekuwa msaada mkubwa kwako katika kubadirisha sekta mbalimbali za maisha yako. Naomba kupata shuhuda sambamba na maoni juu ya makala hizi zilivyogusa maisha yako namna ambavyo kwa pamoja tunaweza kupanua wigo na kufikia wanufaika wengi zaidi.

Kama bado haujajiunga na mtandao huu, BONYEZA HAPA na jaza fomu kisha bofya “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja kwenye barua pepe.

Kitabu ninachokushirikisha leo hii ni Automatic Millionairekutoka kwa mwandishi maarufu David Bach. Mwandishi anatumia kitabu hiki kutushirikisha namna ambavyo kila mmoja anaweza kutengeneza utajiri katika maisha yake hapa duniani. Mwandishi anatushirikisha kuwa kitabu hiki kinalenga kumsaidia msomaji kutengeneza njia/mpango wa moja kwa moja (Automatic) wa kuwa milionea.

Lengo kubwa ambalo mwandishi anakusudia kupitia kitabu hiki ni kuhakikisha msomaji anapata elimu muhafaka kuhusu “fedha” kwani elimu hii imekosekana kwa watu wengi. Hii ndio sababu asilimia kubwa katika jamii ni masikini kwa kuwa hawana msingi sahihi kuhusu somo la fedha hasa namna ya kuitengeza na namna ya kuitumia kutengeneza fedha zaidi.

Hata hivyo mwandishi anatoa tahadhari kuwa “siri/misingi ya kuwa tajiri ipo wazi kwa kila mmoja” na pengine hata wewe unayesoma makala hii unafahamu misingi hiyo. Pamoja na kwamba siri hizo zipo wazi lakini wengi wameshindwa kufikia utajiri wa ndoto zao kwa vile hawatumii misingi hiyo katika maisha yao ya kila siku. Hivyo, kitabu hiki sio kwa wale wanaotaka utajiri wa haraka haraka kwa maana kulala masikini na kuamka tajiri bali kinalenga kuweka mfumo wa moja kwa moja (automatic) wa kufikia UHURU WA KIFEDHA AU UTAJIRI WA KWELI.

Kwa ufupi, kitabu hiki kimejengwa juu ya falsafa kuwa:-
  • Kuwa tajiri sio lazima uwe na pesa nyingi;
  • Sio lazima uwe na nidhamu juu ya fedha zako (najua hii itakuchanganya kama mimi maana tunafahamu kuwa siri mojawapo ya kuwa tajiri ni kuwa na nidhamu ya fedha);
  • Sio lazima ujiajiri mwenyewe ili kuwa tajiri kwani unaweza kuendelea kuajiriwa na ukawa milionea;
  • Kwa kutumia kile mwandishi anachokiita “The Latte Factor”, unaweza kutengeneza pesa nyingi kupitia pesa kidogo ulizonazo;
  • Matajiri wanaendelea kuwa matajiri kwa kuwa wana utaratibu wa kujilipa kwanza;
  • Wamiliki wa nyumba za biashara wanaendelea kuwa matajiri wakati wapangaji wanaendelea kuwa masikini; na
  • Zaidi ya yote unahitaji mfumo wa moja kwa moja (automatic system) ili husikwame katika kufikia utajiri wa ndoto zako.

Karibu ushirikiane nami kujifunza machache kati ya mengi ambayo mwandishi anatushirikisha katika kitabu hiki:

1. Njia pekee inayokuhakikishia kufikia utajiri wa ndoto zako ni kuweka mfumo wa moja kwa moja wa mipango yako yote ya kifedha. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika maisha kuna majukumu mengi ambayo kila siku mhusika anajishughulisha nayo. Ni kutokana na majukumu hayo watu wengi wanashindwa kufikia mipango waliyojiwekea kwa vile pengine wanasahau au wanashindwa wajigawe vipi. Kumbe, mwandishi anatushirikisha kuwa kupitia mfumo wa moja kwa moja (automatic system) unakuwezesha kupata muda wa kuendelea na majukumu yako bila ya kuwa na wasiwasi juu ya pesa yako.  Hivyo, mfumo huu unafaa kwa vile utakufanya husiwe na msongo wa mawazo na hivyo utakuwa na maisha halisi unayotamani kuwa nayo kwa maana ya maisha yenye furaha.

2. Watu wengi wanaigiza maisha ya utajiri wakati maisha waliyonayo ni ya kimasikini. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika jamii watu wanaishi maisha ambayo watu wanaowazunguka wanadhania kuwa wana maisha mazuri kumbe ukitembelea akaunti zao hazina kitu na wala hawana kitega uchumi chochote ambacho kina uhakika. Kumbe, kama unahitaji kuwa tajiri wa moja kwa moja unapaswa kuishi maisha yako bila kujali mtazamo wa jamii inayokuzunguka. Fanya kile ambacho kipo kwenye mpango wako wa utajiri bila kujali macho/maneno ya wanaokuzunguka.

3. Kama unahitaji kuwa tajiri hakikisha unajilipa kwanza katika kila shilingi inayoingia mikononi mwako. Somo kubwa hapa ni kwamba ni lazima uweke mfumo wa moja kwa moja ambao utawezesha kila shilingi inayoingia mkononi mwako inawekezwa kwa ajili ya kesho yako. Hivyo, kabla ya kufanya mgawanyo wa kila fedha unayopata kupitia vyanzo mbalimbali ni lazima ujilipe kwanza kwa kutenga asilimia flani ya pato lako kwa ajili ya uwekezaji. Na hapa ndipo mwandishi anatushirikisha kuwa ni vyema ukafungua akaunti maalum ya uwekezaji ili asilimia flani ya pesa unayopata iingie moja kwa moja kwenye akaunti hiyo hata kabla ya kuingia mikononi mwako. Hali hii itakuwezesha kugawanya kiasi cha pesa kinachoingia mikononi mwako bila kugusa kiasi kilichowekezwa kwenye akaunti ya uwekezaji.


4. Siri nyingine ya kuwa tajiri nikutofanya manunuzi ya aina yoyote ile kwa mkopo. Katika siri hii una chaguzi mbili ambazo ni kununua kwa pesa taslimu (cash) au kutonunua kabisa. Pamoja na siri ni kuhakikisha unanunua bidhaa iliyotumika lakini ikiwa bado ina ubora badala ya kununua bidhaa mpya – mfano kununua gari kutoka kwa mtu badala ya kwenda kununua “show room”.  Pale unaponunua kwa mkopo unajiweka kwenye hatari ya kuingilia matumizi ya pato lako kabla hata halijaingia mkononi mwako. Pia, unaponunua kwa mkopo kuna hatari ya kupandishiwa bei zaidi ya ile ambayo ungelipa kwa fedha taslimu. Aidha, unaponunua bidhaa iliyotumika inakuwezesha kupata punguzo katika bei ikilinganishwa na bei halisi ya bidhaa husika dukani.

5. Kama unahitaji kuwa tajiri ni lazima uipende pesa yako kwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima. Hii ni pamoja na kuhakikisha pesa ambayo ingetumika kwenye matumizi ya ovyo inatumika kufanya mambo ya maana kwa maana yale yanayochangia kukuza utajiri wako. Na ni siri hii mwandishi ndiyo anatushirikisha kuwa unahitaji kutumia “The Latte Factor” kwa maana pesa ambayo ungetumia katika matumizi yasiyo ya lazima; moja kwa moja inatumika kukuza utajiri wako (angalia pointi Na. 8). Kumbe unahitaji kutambua kuwa sio pato lako linalokufanya uwe tajiri bali nini ufanya kutokana na pato lako bila kujali kama una kipato kikubwa au kidogo kiasi gani. Utajiri ni maamuzi ambayo yapo akilini mwako yanasubiria uchukue hatua.

6. Unatahitaji kuwa na mfumo wa moja kwa moja na siyo kuwa na nidhamu ya pesa. Mwandishi anatushirikisha kuwa hakuna kitu kigumu kama kuwa na nidhamu juu ya matumizi ya pesa ambayo ipo mikononi mwako kutokana na vishawishi katika ulimwengu wa sasa. Ili kufanikisha siri hii, mwanishi anatushirikisha kuwa ili uepukane na matumizi ya ovyo ni lazima utengeneze mfumo wa moja kwa moja ambao utakufanya husiwe na pesa mkononi kwa ajili ya matumizi ambayo hayana tija katika kufikia utajiri wa ndoto zako. Kumbe siri zote hizi zinatukumbusha nguvu ya maamuzi na umuhimu wa kuchukua hatua stahiki katika maisha ya kila siku. Hakika hauwezi kufa masikini endapo umezitendea haki siri hizo.

7. Je unahitaji kuwa tajiri? Naamini jibu lako ni ndio kama ndo hivyo basi mwandishi anatushirikisha kuwa ni lazima uhakikishe matumizi yako yanakuwa madogo ikilinganishwa na kipato. Kumbuka kuwa baada ya kutoa asilimia kwa ajili ya uwekezaji (kujilipa) matumizi yako ni lazima yaendane na kiasi kinachobakia. Kama matumizi yanazidi kipato chako hakika utajiri utakuwa ni ndoto kwako. Mwandishi anatushirikisha kuwa kama unahitaji kuwa tajiri unahitaji kutenga angalau asilimia 15 hadi 20 kwa ajili ya kujilipa kwanza kabla ya kuanza kulipa matumizi mengineyo. Watu wengi wanashindwa kuwekeza kwa vile wanapoteza fedha ambayo inaonekana kuwa ni ndogo katika vitu vidogo vidogo ambavyo si vya muhimu katika maisha ya kila siku. Kumbe, unahitaji kutambua kuwa katika safari ya utajiri hakuna pesa ndogo kwani unayoiona kuwa ndogo ikutumiwa vyema thamani yake inaongezeka.


8. Je upo tayari kuwa tajiri? Kama jibu ni ndiyo basi angalia ni matumizi yapi ya fedha ambayo kila siku unafanya lakini si ya lazima au yanaweza kupunguzwa kwa kununua kwa bei pungufu. Baada ya kutambua sehemu ambazo unaweza kuokoa pesa basi hakikisha unajiwekea utaratibu wa kuwekeza hicho kiasi kidogo cha pesa kila siku ya maisha yako bila kuacha kufanya hivyo. Hakika utaona maajabu ndani ya mwaka wa kwanza. Maajabu haya yanatokana na muujiza wenye nguvu unaoitwa ongezeko la riba (interest) kwa kila shilingi inayowekezwa. Mfano, kama umewekeza 1,000/= kila siku kwenye benki ambayo ongezeko la riba ni asilimia 10. Baada ya mwaka mmoja kiwango ulichowekeza kitakuwa ni 1,000X30X12+1,000X0.1X30X12 = 396,000.00. Bila kuongeza uwekezaji wowote hela hii ambayo kitaani inaitwa “buku” iliyowekezwa kwa mwaka mmoja tu katika kipindi cha miaka 10 itakuwa imeongezeka kama ifuatavyo: 396,000.00+396,000.00X0.1X10 = 792,000.00. Fikiria kama umeendelea kuweka buku kila siku ndani ya miaka 10 utakuwa na shilingi ngapi kwani hapo tumepigia hesabu ya buku ile ya mwaka wa kwanza tu ikiwekezwa kwa kipindi cha miaka 10. Naamini mpaka hapo rafiki yangu umeona nguvu ya buku halisi kuliko ile ambayo umekuwa ukiambiwa na muhindi. Unaweza kupunguza matumizi kwenye vocha, soda, sigara, chakula, bia, mishikaki, bodaboda, chips n.k hizo nimekusaidia tu baadhi.

9. Mfumo wa bajeti sio njia sahihi ya kukuwezesha kuwa tajiri. Mwandishi anatushirikisha kuwa ni mara nyingi tumeambiwa kuwa ili uwe tajiri ni lazima uishi kwa kuzingatia bajeti. Ukweli ni kwamba ni vigumu mno kuishi kwa bajeti na nyakati nyingine inaweza kusababisha ugomvi ndani ya familia kwa sababu mmoja anaweza kumdu kuishi kwa bajeti husika wakati mwenza wake hawezi kabisa. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wengi wanashindwa kutumia pesa kulingana na mahitaji ya bajeti yao kwa kuwa mfumo huu wa bajeti unamfanya mhusika kuwa mtumwa na hivyo anakosa uhuru. Kumbuka kuwa tunatafuta utajiri ili kuwa na maisha yenye furaha zaidi ya tuliyonayo sasa na maisha utumwa kamwe hayawezi kuwa na furaha ndani mwake. Kumbe suruhisho la bajeti ni kuhakikisha wewe mwenyewe unaidhibiti pesa yako na sio pesa ikuchanganye kiasi cha kufanya matumizi ambayo hayana uhalisia. Bila kujali pesa ipo mfukoni au benki haupaswi kuitumia kwenye vitu ambavyo havina tija na badala yake fanya manunuzi pale ambapo umekusudia kufanya hivyo.

10. Unaweza kupata utajiri kwa njia sita tofauti ambazo ni: (a) unaweza kushinda kupitia mchezo wa bahati na sibu; (b) unaweza kuoa au kuolewa na tajiri; (c) unaweza kushinda kesi ambayo itakufanya uwe tajiri – kama ipo; (d) unaweza ukarithi utajiri wa ndugu zako; (e) unaweza kuishi kwa bajeti – japo tumeona ni kazi ngumu; na (f) unaweza kupata utajiri kwa kujilipa kwanza. Kati ya njia zote hizo mwandishi anatushirikisha kuwa utajiri wa kweli ambao unatangenezwa na mhusika, njia ya kujilipa kwanza ndio njia sahihi ambayo itakufikisha sehemu unayotaka kufika. Hata hivyo, njia hii sio njia mpya kwani kama ni msomaji wa vitabu au mhudhuriaji wa semina utakuwa umeisikia mara kwa mara. Sasa jiulize maswali haya: a) Je unajua kiasi gani unatakiwa kujilipa kwanza? b) Je unatambua ni sehemu ipi sahihi ya kuwekeza pesa hiyo unayojilipa? c) Je ni kweli kwa sasa unajilipa kwanza? na d) Je una mfumo wa moja kwa moja wa kujilipa kwanza?

11. Mwandishi anatushirikisha kuwa kama majibu ya maswali yote hapo juu ni NDIYO basi unastahili hongera kwa kuwa tayari upo kwenye safari ya kuwa tajiri. Kama majibu yako baadhi au yote ni HAPANA basi na wewe husikate tamaa kwa kuwa ndio maana unasoma makala kama hii kwa ajili ya kubadirisha mfumo wa maisha yako. Ukweli ni kwamba watu wengi hawajilipi kwanza japo wanahitaji kuwa matajiri jambo ambalo ni gumu mno labda kama utajiri huo waupate kwa zari tu. Maana halisi ya kujilipa kwanza ni kuhakikisha kila shilingi inayoingia mkononi mwako unatenga asilimia yake kulingana na mpango wako wa kufikia utajiri na pesa hiyo unaiwekeza kwenye akaunti maalumu ya uwekezaji. Mwandishi anatushirikisha kuwa kama unahitaji kuwa tajiri hakikisha unajilipa asilimia 15 hadi 20 ya pato lako. Kama kiasi hicho ni kikubwa kwa kuanzia unaweza kuanza na asilimili 5 kwa ajili ya kujijengea nidhamu ya kujilipa kwanza.

12. Tunapima masaa halisi unayofanyia kazi kwa ajili yako na wategemezi wako kwa kuangalia kiasi unachowekeza kwa kujilipa kwanza. Mwandishi anatushirikisha kuwa kila tunachofanya iwe kazini au kwenye biashara ni kwa faida ya mhusika mwenyewe na wategemezi wake. Je ni kwa kiasi gani unatumia muda mwingi kufanya kazi kwa ajili yako na wategemezi wako? Majibu ya swali hili yanapatikana kwa kugawanya kiwango ulichojilipa kwanza dhidi ya masaa uliyofanya kazi. Mfano, chukulia ndani ya mwezi mmoja una masaa 240 ya kazi na umejilipa 50,000. Hivyo, masaa ambayo umefanya kazi kwa faida yako na wategemezi ni sawa na 50,000/240 ambayo kwa kukadiria ni masaa 208 ndani ya mwezi mmoja. Kumbuka kama haukutenga chochote ni sawa na kwamba mwezi mzima umeupoteza bila kujilipa wewe na wategemezi wako.
                                               
13. Fikiria kati ya makundi haya na chagua moja ambalo linakufaa: (a) husijilipe kwanza, tumia zaidi ya pato lako, kopa hela kwa ajili ya matumizi na endelea kuishi kwa mshahara husiyounga mwezi hadi mwezi. Kwa dalili hizo wewe ni mtu ambaye kila siku utakuwa umepinda kiuchumi na msongo wa mawazo juu; (b) njia ya umasikini – endelea kusoma kuhusu kujilipa kwanza bila kuchukua hatua, endelea kutumia kila kinachoingia mikononi mwako bila kuwekeza chochote huku ukiendelea kujisemea ipo siku ntakuwa tajiri bila kuweka mpango wowote; (c) njia ya kuwa mtu wa pato la kawaida – jilipe kwanza kati ya asilimia 5 hadi 10 ya pato lako; (d) Njia ya kuwa mtu mwenye kipato cha juu – jilipe kwanza kati ya asilimia 10 hadi 15; (e) njia ya utajiri – jilipe kwanza kati ya asilimia 15 hadi 20; na (f) njia ya utajiri kiasi kwamba unaweza kustaafu umri wako ukiwa mdogo – jilipe kwanza angalau asilimia 20 na kuendelea. Njia zote zipo kwa ajili yako na hivyo kuwa masikini wa kupindukia au tajiri/milionea ni maamuzi yaliyopo mkononi mwako. 

14. Weka mfumo wa moja kwa moja wa kujilipa kwanza. Mwandishi anatushirikisha kuwa baada ya kuamua kujilipa kwanza kwenye kila shilingi inayoingia mkononi mwako sasa unahitaji kutengeneza mfumo wa moja kwa moja wa kujilipa ili pesa hiyo husishawishike kuipangia matumizi pale inapoingia mikononi mwako. Mwandishi ametushirikisha mbinu mbalimbali ambazo tunaweza kuzitumia kwa ajili ya kuwa na mfumo wa makato wa moja kwa moja kwa kiasi ambacho tumeamua kujilipa kwanza. Hata hivyo, njia hizo nimeona kuwa katika mazingira ya nchi yetu yawezekana hazipo hasa kwa wale ambao wamejiajiri. Somo, kubwa ni kwamba iwe umeajiriwa au umejiajiri utaratibu wa kujilipa kwanza unawezekana kabisa katika mazingira yetu. Kubwa ni kuwa na nidhamu ya kutekeleza kile ambacho umekusudia kujilipa katika pato lako. Kwa yule ambae yupo tayari kufanya hivyo nitafungua group la WhatsApp la “JILIPE KWANZA”. Tuma ujumbe kwenye namba +255 786 881 155 ukiomba kuunganishwa kwenye kundi hilo na nitakupa masharti ya kundi.

15. Kumbuka hakuna kesho, mwaka kesho au nyakati zilizo bora zaidi ya sasa. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wengi wanafanya makosa kwa kujisemea kuwa kwa sasa mambo yangu hayajakaa sawa hivyo ngoja kwanza yakikaa sawa ndo nitaanza kutenga asilimia ya kujilipa kwanza. Ukweli ni kwamba kama unahitaji kuwa tajiri ni lazima ufanye maamuzi magumu na wakati sahihi wa kufanya maamuzi hayo ni sasa. Anza sasa na hakikisha kila mwezi unatenga asilimia uliyojipangia kwa ajili ya kujilipa kwanza. Pia, hakikisha kila shilingi inayoingia mkononi mwako unajilipa kwanza bila kujali ni nyingi au kidogo. Hakika kwa kufanya maamuzi hayo hautojutia hata siku moja.

16. Wekeza pesa unayojilipa kwenye akaunti au ambayo ina ongezeko la riba. Mwandishi anatushirikisha kuwa sifa kubwa ambayo matajiri wanayo ni kuifanya pesa iwafanyie kazi badala ya wao kuifanyia kazi. Hata nyakati ambazo wanakuwa wamelala pesa yao inakuwa inawafanyia kazi – huo ndio utajiri wa kweli. Njia mojawapo wa kufanikisha hilo ni kuwekeza pesa sehemu ambayo ina ongezeko la riba au thamani. Mfano, unaweza kuwekeza kwenye dhamana za serikali (Government bond), Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja (UTT), fixed account au kununua hisa. Lengo la kuwekeza katika sehemu hizo ni kwa ajili ya kupata muujiza wa uwekezaji unaotokana na “Ongezeko la Riba”. Kumbuka kuwa njia ya utajiri inayotafutwa hapa sio ya kulala masikini na kuamka tajiri bali ni njia ya kutafuta utajiri kwa mpango maalum ambao ni wa muda mrefu. Ni kutokana na muda huo ndipo utashangaa maajabu ya “ongezeko la riba” (angalia Na. 8).

17. Unaweza kuwekeza pesa unayojilipa kwenye mchanganyiko wa makundi haya ya uwekezaji: (a) fedha taslimu (cash); (b) dhamana za serikali; (c) hisa za makampuni (stocks); (d) uwekezaji wa mapato (miradi mbalimbali); na (e) ukuaji wa uwekezaji (kujikta kwenye uwekezaji mkubwa zaidi). Hata hivyo, mchanganyiko huo wa uwekezaji utategemea nyakati mbalimbali ambazo unapitia kama vile: (i) kipindi cha maandalizi (kukusanya mtaji); (ii) kipindi cha kutengeneza pesa; (iii) kipindi cha maandalizi ya kustaafu; na (iv) kipindi cha kustaafu. Katika kila kipindi mahitaji yako na malengo ni tofauti hivyo unahitaji mchanyiko mzuri wa makundi tofauti ya uwekezaji. Pia, mchanganyiko huo wa makundi ya uwekezaji (fedha taslimu, dhamana za serikali na hisa) utategemea na umri wako kwa wakati huo. 

18. Mchanganyiko wa uwekezaji unaouchagua (angalia Na. 17) unatakiwa kuzingatia hatari za uwekezaji. Hivyo, uwekezaji wako unapaswa kuwa katika muundo wa umbo la piramidi (pembe tatu iliyogeukia juu). Kwa maana kuanzia chini ya piramidi kwenda juu yake hatari za uwekezaji zinaongezeka zaidi. Hii inamaanisha kuwa katika kipindi cha maandalizi (kukusanya mtaji) unahitaji kuwekeza pesa unayojilipa kwenye sehemu yenye usalama zaidi ambayo katika umbo la piramidi inakuwa ni kama msingi wa umbo. Mfano, kwa hapa kwetu unaweza kuwekeza kwenye Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja au kwenye Akaunti Maalum ya Uwekezaji – saving account). Kadri mtaji unavyoongezeka ndivyo unahitaji kuchukua hatari zaidi kiuwekezaji kwa kupanda ya piramidi. Lengo la kuwa na mchanganyiko wa uwekezaji ni kuepuka kuweka mayai yote katika kapu moja.


19. Baada ya kujilipa kwanza sasa unatakiwa kutenga hela kwa ajili ya dharura. Mwandishi anatushirikisha kuwa hakuna mwenye uhakika na matukio ya baadae katika maisha yake. Ni kutokana na ukweli huo kama “Automatic Millionaire” unatakiwa utenge fedha kwa ajili ya dharura. Lengo la kufanya hivyo ni kulinda fedha unazojilipa zisijekutumika kwa ajili ya dharura katika maisha yako ya baadae. Mwandhishi anashauri kuwa kiasi unachotenga kinatakiwa angalau kiwezeshe kukidhi mahitaji yako yote katika kipindi cha kuanzia miezi mitatu na kuendelea. Fedha hizi ni kwa ajili ya dharura kama vile kufukuzwa kazi, umepata uremavu, magonjwa au kuunguliwa na nyumba. Baada ya kuchagua kiasi unachotakiwa kutenga kwa ajili ya dharura sasa unatakiwa kukiwekeza kwenye akaunti maalum ambayo pia ina ongezeko la riba na kama unaweza hakikisha kinaingizwa kwenye mfumo wa makato ya moja kwa moja.

20. Miliki nyumba na hakikisha haidaiwi kodi kwa maana kodi ya Serikali. Mwandishi anatushirikisha kuwa hatua kubwa katika safari ya kuelekea kwenye utajiri ni kuhakikisha unamiliki nyumba unayoishi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba pesa unayotoa kwa ajili ya kulipia kodi hakuna siku hata moja ambayo itakuwezesha umiliki nyumba yako. Hii ni pesa ambayo ni lazima kila mwisho wa mwaka au mwezi uitoe kwa mwenye nyumba na mwisho wa pango haumiliki chochote. Mfano, kama unakaa kwenye nyumba ambayo kodi ni Tshs. 200,000.00 kwa mwezi. Kwa mwaka ni Tshs. 2,400,000.00 ambayo katika kipindi cha miaka kumi ni Tshs. 24M. Pesa hii ni nyingi kiasi kwamba ingekuwezesha kumiliki nyumba yako bila kujali ukubwa wake.

21. Wekeza kwenye nyumba za biashara kama njia ya kutengeneza utajiri zaidi. Mwandishi anatushirikisha kuwa baada ya kumiliki nyumba unayoishi sasa unatakiwa kumiliki nyumba za biashara ili pesa yako ianze kukufanyia kazi. Kubwa ni kwamba nyumba ya biashara ni: (a) uwekezaji ambao mtaji wake uonaongezeka thamani kila kukicha; (b) unapata faida kutokana na uwepo wa wapangaji – malipo ya kodi; na (c) unaweza kuitumia kama dhamana kwa ajili ya kupata fedha za wengine zikufanyie kazi. Faida hii ya tatu inahusiana na kukopa benki ambapo unapewa fedha za wateja wengine ili uzitumie kwa ajili ya kuwekeza zaidi.

22. Hakikisha unamaliza madeni yasiyo na faida kama tayari unayo. Hii ni sambamba na kuhakikisha unakimbia mikopo yote ya hasara ambayo umekuwa ukifanya bila kutambua athari ya mikopo hiyo kwenye safari yako ya utajiri. Unahitaji kubadirisha tabia ya kununua kwa mkopo bila kujali ukubwa wa mkopo husika. Mwandishi anatushirikisha kuwa mikopo mingi huwa inasababishwa na wahusika kuishi maisha ya kuigiza kwa kutaka waonekane wapo vizuri kuliko uhalisia wa kipato chao. Kumbe, baada ya kufahamu kuhusu siri hii unachotakiwa kufanya ni kuishi kulingana na uwezo wa pato lako. Matajiri huwa hawaishi maisha ambayo hayapo kwenye akaunti zao. Katika jamii wengi ambao unadhania kuwa ni matajiri ukiuliza wanamiliki nini kwenye akaunti utagundua kuwa hawana chochote zaidi ya nguo, viatu au gari la kifahari wanalotembelea.

23. Kumbuka kurudisha kwa jamii. Mwandishi anatushirikisha kuwa mbinu zote zilizoshirikishwa hapa zinalenga kukusanya utajiri ambao kila mmoja anatamani kuwa nao. Hata hivyo, maisha mengine ni lazima yaendelee kwa maana haupaswi kuwa mchoyo kwenye jamii inayokuzunguka. Kumbuka unabarikiwa zaidi kadri unavyotoa kwa wale wenye uhitaji. Tunahitaji kutambua kuwa tunatafuta utajiri si tu kwa ajili ya kuwa na uhuru wa kifedha bali kwa ajili ya kuendelea kuishi maisha yenye furaha ambayo yanaguswa na maisha ya jamii inayotuzunguka. Kumbe, kuwa tajiri kisiwe kigezo cha kutokuwa na hisia dhidi ya maisha ya wale ambao hawajabahatika kuwa matajiri badala yake tumia utajiri wako kuifikia jamii zaidi kwa kadri uwezavyo. Utajiri wako uwe nyenzo ya kubadirisha dunia hii kuwa mahala pazuri pa kuishi kwa viumbe vyote.


Haya ni machache ambayo nimebahatika kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.

Kwa ambao wamehamasika ushauri wangu ni kwamba husiishie kuhamasika bila kuchukua hatua. Hakikisha unachukua hatua ya kwanza kwa kuanzisha mpango wa kujilipa kwanza. KARIBU KWENYE KUNDI LA “JILIPE KWANZA” ambapo kwa pamoja tutaianza safari ya kuwa MILIONEA.

Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na mwisho.

Born to Win ~ Dream Big 

Augustine Mathias Bilondwa

Namba ya Simu:      +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com

PATA UCHAMBUZI WA KITABU CHA THE RULES OF MONEY ( KANUNI ZA PESA)
 
Mwandishi Richard Templar katika kitabu hiki ametushirikisha kanuni 107 ambazo kila mtu anaweza kuzitumia kutengeneza pesa na hatimaye kuwa tajiri. Uchambuzi wa kina wa kanuni zote (107) umeandaliwa kwa mfumo wa pdf na unapatikana kwa gharama ya Tshs. elfu tano tu (5,000/=). Kanuni zote zimechambuliwa na kuandaliwa kijitabu kidogo chenye kurasa 39 ambazo unaweza kusoma kwenye simu ya mkononi (smart phone) au kwenye kompyuta (pc).

Kupata uchambuzi wa kanuni zote tuma pesa yako kwa njia ya M-pesa au Airtel Money kupitia namba zifuatazo:-

M – Pesa tumia namba: 0763 745 451 (Majina ni Augustine Mathias)
Airtel Money tumia namba: 0786 881 155 (Majina ni Augustine Mathias)

Baada kutuma pesa hiyo nitumie ujumbe kwenye namba ya airtel (0786 881 151 451) ukiwa na barua pepe yako ili nikutumie uchambuzi wa kanuni hizi moja kwa moja kwenye mtandao wako.

UTAJIRI NI HAKI YAKO YA KUZALIWA "BEING RICH IS YOUR BIRTH RIGHT"





onclick='window.open(