Mambo Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha Winning The Loser’s Game: Mikakati ya Uwekezaji Wenye Mafanikio

Habari ya leo rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri.

Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya 7 katika kipindi cha mwaka 2018 naendelea kukushirikisha uchambuzi wa vitabu vyenye mafundisho tofauti katika kila sekta ya maisha yako.

Makala hizi za uchambuzi wa vitabu zimekuwa zikikufikia kila wiki kwa kadri ambavyo napata muda wa kukushirikisha kile ninachojifunza kutoka kwenye vitabu hivi. Ni matarajio yangu kuwa muda ninaotumia kukushirikisha uchambuzi wa vitabu umekuwa wa msaada mkubwa kwako katika kubadilisha maisha yako.

Unaweza kujiunga na mtandao huu, KWA KUBONYEZA BONYEZA HAPA na kujaza fomu kisha bofya “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.

Kitabu cha wiki hii ni “Winning the Loser’s Game” kutoka kwa mwandishi Charles D. Ellis. Mwandishi huyu ametumia kitabu kutushirikisha mbinu mbalimbali ambazo zinatumiwa na wawekezaji wakubwa kufanikiwa kiuwekezaji. Mwandishi anasisitiza kuwa katika uwekezaji ni muhimu mwekezaji kuwa msimamizi mkuu na kuhakikisha anafuatilia kila aina uwekezaji alionao. Hii ni pamoja na kufikiri na kuchukua hatua za kivitendo kwenye kila za uwekezaji ulizonazo. Epuka sana kutegemea mawazo ya washauri katika uwekezaji kwani mara nyingi wengi wao hawana uzoefu juu ya kile wanachoshauri.

Katika uwekezaji kuna aina makundi mawili ya wawekezaji, kundi la kwanza ni wawekezaji ambao kwa namba ni wachache lakini wako macho katika kuhakikisha wanaboresha masoko. Hawa ndio wanafanya vitu vinaonekana kwenye soko kwani wapo tayari kuwekeza muda na akili kwa ajili ya ubunifu mpya katika soko. Kundi la pili ni wawekezaji ambao kwa namba ni wengi sana lakini hawajishughulishi kutengeneza mazingira ya soko la uwekezaji. Hawa hawawekezi kwenye rasimali au elimu kwa ajili ya kuboresha mazingira ya soko bali wanategemea kutumia mazingira yaliyopo kwenye soko husika.

Karibu tujifunze machache kati ya mengi ambayo mwandishi anatushirikisha katika kitabu hiki:

1. Katika uwekezaji wa aina yoyote kinachoamua ushindi ni matendo sahihi ya mwekezaji na kinachoamua kushindwa ni maamuzi ya kimakosa yanayofanywa na mwekezaji. Kutokana na ukweli huu tunajifunza kuwa kwenye kila aina ya uwekezaji ili ushinde ni lazima uwe na ufahamu sahihi. Hivyo kwenye uwekezaji kuna waliobobea na hawa ndio wanapata pointi za ushindi ikinganishwa na wale wanaosindikiza.

2. Kwenye uwekezaji ni muhimu kutambua kuwa mbinu za ushindi zinabadilika kulingana na nyakati. Hapa tunajifunza kuwa ili tufanikiwe kiuwekezaji ni muhimu kuboresha mbinu zetu kulingana na nyakati zilizopo. Mwandishi anatushirikisha kuwa wengi wanashindwa kupata mafanikio kwenye soko kwa kuwa wanaendelea kutumia mbinu zilizopitwa na wakati.

3. Katika mchezo wa fedha ni lazima utambue kuwa ushindi unachangiwa na namna ambavyo unapoteza fedha kidogo kwenye soko na hivyo kubakiza sehemu kubwa ya fedha kama ushindi wako. Hii ni kanuni ambayo inatumika kuamua ushindi kwenye mchezo wowote ule. Mfano, mshindi wa tenisi anapatika kulingana na pointi nyingi anazokusanya ikilinganishwa na zile anazopoteza.

4. Katika mchezo wa uwekezaji/fedha mara zote unahitaji kuhakikisha unamridhisha mteja. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mteja anaporidhika wewe kama mwekezaji unapata uhakika wa kuwekeza zaidi. Wateja ni njia pekee ambayo itaendelea kukuweka sokoni endapo umetekeleza mahitaji muhimu ya uwekezaji.

5. Soko la uwekezaji hasa uwekezaji wa hisa limepitia kwenye mabadiliko makubwa ambayo kwa ujumla wake yanatofautisha wawekezaji kwenye soko. Wawekezaji ambao wameendelea kuwekeza kwa kutumia mbinu zile zile wameendelea kupotea kwenye soko kwa kasi kubwa kuliko wale ambao wanabadilisha mbinu kulingana na mabadiliko yaliyopo. Muhimu ni kuwa na taarifa sahihi kuhusu soko kila wakati.

6. Wawekezaji wote wana sifa zinazofanana kama vile kuhitaji kufanya vyema kwenye soko (kutengeneza faida). Sifa hii ndio inamfanya kila mwekezaji kuwa na uhuru wa kuchagua wapi awekeze fedha zake katika soko. Hata hivyo, kinachotofautisha wawekezaji hawa katika soko ni pamoja na: rasilimali wanazomiliki, mitaji, majukumu ya matumizi, elimu ya biashara, uwezo wa kuvumilia hatari za uwekezaji na uzoefu wa soko. Tofauti hizi ndizo zinaonesha kuwa wawekezaji hawa ili wafanye vyema kwenye soko ni lazima pawepo msaada wa kielimu au mawazo.

7. Njia pekee ya wawekezaji makini kuendelea kufanya vyema kwenye soko ni kutumia makosa yanayofanywa na wawekezaji makini wa ngazi zao. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika uwekezaji kosa moja kwa mwekezaji ni baraka kwa mpinzani wake wa karibu. Njia hii imekuwa ikiamua mwenendo wa makampuni katika soko, hivyo, kama mwekezaji unahitaji kufahamu mbinu hii ili kuepuka makosa ya kiuwekezaji lakini pia kuitumia kwa ajili ya kufaidi makosa ya wawekezaji wengine.

8. Ili kuepuka makosa ya kiuwekezaji kwenye soko ni lazima ujitoe kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya kulifahamu soko, kuwa na taarifa sahihi na elimu sahihi ya soko husika. Njia hizi ndizo zinatumiwa na wawekezaji makini kwa ajili ya kuepuka makosa ya kiuwekezaji. Mfano, katika uwekezaji wa hisa unahitaji kulifahamu soko kwa nyakati husika, kuchagua hisa sahihi kwa wakati husika na kufahamu ni lini mabadiliko na yanaweza kutokea kwenye soko na hivyo yakaathiri thamani za hisa. Mwekezaji ambaye amefanikisha kufahamu yote haya ni rahisi kwake kufanya vyema kwenye soko kwani ana uwezo wa kununua hisa pale ambapo thamani hisa imeshuka (wakati ambao kila mtu anauza) na kuuza hisa zake pale ambapo thamani ya hisa imepanda (wakati ambao kila mtu ananunua).


9. Njia nyingine ya kufanya vyema kwenye soko la hisa ni kuwa uelewa wa kina hisa za makampuni yaliyoorodheshwa kwenye soko la hisa. Mwandishi anatushirikisha kuwa wawekezaji makini wanachagua hisa ambazo thamani ya beiza hisa iliyotangazwa kwenye soko ni ya chini kuliko thamani halisi ya hisa husika. Na hii ndio inaamua nyakati zipi wawekezaji makini wanunue au kuuza hisa wanazomiliki.

10. Wawekezaji makini ni wale ambao mara zote wanatafuta fursa mpya za kiuwekezaji. Wawekezaji hawa mara zote wanaandaa njia kwa ajili ya wengine kufuata njia husika na wanaacha njia hii pale ambapo kila mtu ameingia kwenye njia husika. Hii ni kutokana na ukweli kwamba nyakati ambazo kila mtu anatumia njia husika ni nyakati ambazo soko limefurika na hivyo faida inakuwa ni ndogo matokeo yake mwekezaji makini anatakiwa kutafuta njia mpya.

11. Kama mwekezaji unahitaji kufahamu nguvu za soko na thamani ya vitu/bidhaa katika soko. Mwandishi anatushirikisha kuwa soko mara zote lina kelele nyingi ambazo upelekea mabadiliko ya thamani ya bidhaa/kampuni kwa nyakati tofauti. Mabadiliko haya mara nyingi yanasababishwa na taarifa za uongo na hivyo yanapelekea kupanda na kushuka kwa thamani/bei ya bidhaa. Kama mwekezaji makini hautakiwi kuendeshwa na miemko/kelele za soko ambazo mara nyingi huwa ni za muda mfupi bali unatakiwa kujikita kwenye malengo/sera ya uzalishaji/uwekezaji wa muda mrefu wa kampuni yako.

12. Mara nyingi katika kukabiliana na kelele za soko wawekezaji makini wanatumia mantiki (logic) badala ya kuongozwa na hisia. Mwandishi anatushirikisha kuwa kinachosababisha mabadiliko makubwa kwenye soko ndani ya muda mfupi ni kutokana na soko kutawaliwa na wawekezaji wasio makini. Wawekezaji hawa wanaongozwa na hisia ambazo zinawafanya wapaniki kutokana na hofu ya kupoteza kile walichowekeza. Hali hii inawafanya wauze kwa haraka au kununua kwa pupa na matokeo yake ni kushuka/kupanda kwa thamani ya bidhaa/hisa.


13. Kama ilivyo michezo mingine, mchezo wa uwekezaji nao pia unaundwa na timu yenye watu mbalimbali na timu hii ndio inaamua ushindi au kukosa ushindi. Mwandishi anatusirikisha kuwa uwekezaji mitaji unahitaji timu makini kwa ajili ya kuamua ushindi wa wawekezaji. Hii inaanzia kwa wamiliki wa soko kama taasisi inayoendesha soko, mfano, kwa hapa Tanzania Dar es salaam Stock Exchange (DSE) ni lazima soko liwe na wataalamu wa kila kada zote za fedha za uchumi kwa ajili ya kufanikisha ukuaji wa soko husika.

14. Katika kuwekeza unahitaji kuwa makini na hatari za uwekezaji. Hii ni pamoja na uhakika wa kulinda mtaji wako kutokana na ukweli kwamba kuna nyakati ambazo unaweza kujikuta unapoteza kila kitu ulichowekeza. Hali inatokea pale ambapo kuna mabadiliko ya kudumu katika soko ambayo mara nyingi yanapelekea upotevu wa thamani ya bidha/hisa kiasi ambacho thamani haiwezi kurudi kwenye hali yake soko. Inapotokea hali kama hii unaweza kujikuta unaharibu maisha yako yote kiuwekezaji na kiroho pia.

15. Mojawapo ya makosa yanayopelekea wawekezaji kuangukia kwenye shimo la upotevu wa pesa ni hali ya kujiamini kuwa wanafahamu zaidi kuliko watu wengine katika soko husika. Hali inapelekea wengi kuwekeza mitaji yao kwa kuongozwa na taarifa ambazo hazina uhalisia wa soko. Hali hii pia inachangiwa na tabia kukimbilia matokeo ya muda mfupi ambayo kiuwekezaji hayana tija.

16. Uvumilivu ni njia mojawapo ya kukuwezesha kudumu katika soko. Mwandishi anatushirikisha kuwa wawekezaji makini mara nyingi katika kuepuka miemko ta soko mara nyingi wanajitahidi kuwa wavumilivu kwa ajili ya kusubilia mapito ya upo wa soko. Kama sio mvumilivu unaweza kujikuta unapoteza mtaji ambao umekusanywa kwa kipindi kirefu na kujikuta unaanza upya.

17.  Hatari za uwekezaji zinaweza kuepukwa kwa; kupunguza makosa ya kiuwekezaji hasa yanayosababishwa na miemko ya hisia, kuwa na malengo ya uwekezaji ambayo mwekezaji ameweka mwenyewe, kuwa na mkakati wa uwekezaji unaotekeleza katika kipindi cha muda mrefu (long term investment strategy) na kuendelea kujikita kwenye mpango wako wa muda mrefu bila kujali kelele za soko ambazo mara nyingi zinasabishwa na watu kuwa na hofu ya kutopoteza au tamaa ya kupata zaidi katika soko husika.

18. Mafanikio yako kama mwekezaji yanatemea nguvu yako kwenye elimu ya uwekezaji na uwezo wa kudhibiti hisia zako. Katika uwezo wa kielimu tunaangalia uwezo wako wa kudhibiti fedha (zinazoingia na kutoka), uwezo wako wa kutumia taarifa zilizopo kuhusu soko, na uwezo wa kuchambua hisa za makampuni mbalimbali kwa ajili ya kuchagua hisa sahihi. Katika upande wa hisia tunaangalia uwezo wa kuwa mtulivu na imara hasa nyakati ambazo kuna kelele nyingi katika soko.  

19. Mchezo wa uwekezaji hasa kwenye masoko ya mitaji kama hisa, hatifungamani, dhamana au mifuko ya pamoja ni mchezo ambao kila mshiriki (mwekezaji) ana nafasi sawa ya kushinda. Siri ya kwanza katika kushinda kwenye uwekezaji wa mitaji ni kuepuka kupelekeshwa na miemko/kelele za soko. Siri ya pili ni kila mwekezaji kwa utashi wake kuandaa sera ya uwekezaji ambayo anaona inamfaa kwa ajili ya kutumia sera hiyo kukamilisha malengo ya uwekezaji wa muda mfupi na muda mrefu.

20. Uwekezaji wa aina yoyote ile ni lazima uwe na msingi imara kama ilivyo kwenye uhandisi ujenzi. Kwenye uwekezaji pia mwanzoni ni lazima ujiulize kama yale unayofanya kwa sasa yanatosha kukupa msingi imara kwa ajili ya miaka 10, 20, au 30 ijayo. Kama umejiweka sawa kiuwekezaji kwa sasa ni rahisi sana kufanikiwa kiuwekezaji katika miaka ijayo.


Haya ni machache ambayo nimeweza kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.

Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link). Nakutakia mapambano mema.

Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na mwisho.

Born to Win ~ Dream Big 

Augustine Mathias Bilondwa

Namba ya Simu:      +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com

PATA UCHAMBUZI WA KITABU CHA THE RULES OF MONEY ( KANUNI ZA PESA)
 
Mwandishi Richard Templar katika kitabu hiki ametushirikisha kanuni 107 ambazo kila mtu anaweza kuzitumia kutengeneza pesa na hatimaye kuwa tajiri. Uchambuzi wa kina wa kanuni zote (107) umeandaliwa kwa mfumo wa pdf na unapatikana kwa gharama ya Tshs. elfu tano tu (5,000/=). Kanuni zote zimechambuliwa na kuandaliwa kijitabu kidogo chenye kurasa 39 ambazo unaweza kusoma kwenye simu ya mkononi (smart phone) au kwenye kompyuta (pc).

Kupata uchambuzi wa kanuni zote tuma pesa yako kwa njia ya M-pesa au Airtel Money kupitia namba zifuatazo:-

M – Pesa tumia namba: 0763 745 451 (Majina ni Augustine Mathias)
Airtel Money tumia namba: 0786 881 155 (Majina ni Augustine Mathias)

Baada kutuma pesa hiyo nitumie ujumbe kwenye namba ya airtel (0786 881 151 451) ukiwa na barua pepe yako ili nikutumie uchambuzi wa kanuni hizi moja kwa moja kwenye mtandao wako.

UTAJIRI NI HAKI YAKO YA KUZALIWA "BEING RICH IS YOUR BIRTH RIGHT"





onclick='window.open(