Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri.
Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa
FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa
ni wiki ya 6 katika kipindi cha mwaka 2018 naendelea kukushirikisha uchambuzi
wa vitabu mbalimbali vyenye mafundisho tofauti katika kila sekta ya maisha
yako.
Makala hizi za uchambuzi wa vitabu
zimekuwa zikikufikia kila wiki kwa kadri ambavyo napata muda wa kukushirikisha
kile ninachojifunza kutoka kwenye vitabu hivi. Ni matarajio yangu kuwa muda
ninaotumia kukushirikisha uchambuzi wa vitabu umekuwa wa msaada mkubwa kwako
katika kubadilisha maisha yako.
Unaweza kujiunga na mtandao huu, KWA KUBONYEZA BONYEZA HAPA
na
kujaza fomu kisha bofya “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu.
Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja
kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “The Craving Mind” kutoka kwa mwandishi Judson Brewer. Mwandishi
Judson ametumia kitabu hiki kuelezea namna ambavyo mwanadamu ni kiumbe mwenye
uwezo wa kutumia ubongo wake kujifunza mambo yenye kila aina ya ubunifu ikiwa
ni pamoja na uwezo wa kutumia ubongo huu katika kuamua hatma ya maisha ya
mhusika.
Watu
wengi katika maisha wanaishi kwenye aina ya uteja/ulevi wa kila aina, wapo
ambao ulevi wao ni sigara, pombe, mitandao ya kijamii, madawa ya kulevya, ubinafsi,
tamaa ya mwili kwenye kila kitu au ulevi wa kudharau nafsi zao kupitia fikra
hasi.
Katika
hali kama hii, mwili unakuwa unaitikia vichocheo pasipo kushirikisha ubongo kwani
tayari uteja/ulevi huo ulishakuwa sehemu ya vitu ambavyo havihitaji kujadiliwa
na ubongo ili vifanyike. Mfano, kama umegusa waya ya umeme haraka utatoa mkono
kwa vile hali hatarishi zote zilishakuwa sehemu ya ubongo.
Mwandishi
ametumia uzoefu wake katika tasnia ya sayansi ya ubongo pamoja na mafundisho ya
budha ambayo amekuwa akiyaishi kwa muda mrefu kutushirikisha namna ambavyo kila
mtu anaweza kutumia “utulivu wa akili” kukabiliana na kila aina ya ulevi/uteja
ambao umekuwa sehemu ya maisha yetu kwa muda mrefu.
Karibu
tujifunze machache kati ya mengi ambayo mwandishi anatushirikisha katika kitabu
hiki:
1. Ulevi/uteja wa tabia yoyote
unatengenezwa kwa kurudia tabia mara kwa mara na hatimaye kujenga mazoea. Mwandishi
anatushirikisha kuwa unavyotumia kitu mara ya kwanza kuna ujumbe unatumwa
kwenye ubongo juu ya kitu husika. Ujumbe huu unahifadhiwa na kazi ya ubongo ni
kukumbusha mara kwa mara juu ya tabia husika na matokeo yake ni mazoea/ulevi
uliopitiliza juu ya tabia husika. Mfano, mvuta sigara mara kwa mara akili yake
inamkumbusha kuvuta akihisi kuwa kwa kufanya hivyo mwili utajisikia vizuri na
matokeo yake ni ulevi wa sigara.
2. Uteja/ulevi wa tabia yoyote
unatengezwa kupitia mzunguko wa Kichocheo ambacho kinaleta tabia na tabia
inaleta matokeo au zawadi. Hizi sehemu tatu ambazo zinatumiwa na wanyama au
binadamu katika kujifunza tabia mpya. Pale tabia inapokuwa imekolea kiasi cha
kumwendesha mtu ndipo tunasema kuwa flani ni teja/mlevi (addicted) wa tabia
flani.
3. Kadiri unavyojifunza tabia mpya
ndivyo tabia husika inaambatana na mabadiliko ya akili ambayo pia yanapelekea
mabadiliko ya mwili. Hali hii inapelekea mwili na akili/ubongo kupelekeshwa na
tabia husika kila unapokutana na mazingira ya yabayoendana na tabia hiyo. Katika
hatua hii ndipo unajikuta umekuwa teja/mlevi wa tabia husika. Mfano, kama
umezoea kunywa soda kila baada ya kula, utajikuta kwenye uhitaji wa soda kila unapomaliza
kula kama tulizo la nafsi yako.
4. Mwili
wa binadamu unaitikia vichocheo kulingana na mazoea yaliyopita. Tunaweza kuitikia
vichocheo vya upande chanya au kuachana na vichocheo vya upande hasi. Katika upande
chanya mara nyingi unapelekea kwenye tulizo la nafsi wakati upande hasi mara
zote unapelekea kwenye hali ambazo si nzuri kwa mhusika. Hata hivyo tulizo la
upande chanya kama umekuwa teja wa tabia flani huwa ni la muda mfupi na matokeo
yake ni kujikuta kwenye magonjwa ambayo chimbuko lake ni tabia za awali. Mfano,
unapenda kula sana bila kufanya mazoezi ya kutosha, matokeo yake unajikuta
kwenye magonjwa kama presha na sukari.
5. Mwandishi
anatushirikisha kuwa njia pekee ya kuisha maisha ya ukamilisho/furaha ni kuwa
na utulivu wa akili kwenye kila tukio tunalojihusisha nalo kwa wakati husika
ikiwa ni pamoja na kushiriki tukio hilo kwa ukamilifu wake. Utulivu wa akili
pia unahusisha tafakari ya kwa nini unafanya kile unachofanya kwa wakati husika
pamoja na udhibiti wa hisia/maamuzi yanayoegemea upande mmoja katika kila hali
au tukio husika. Hivyo, utulivu wa akili unajumuisha kuona kwa mapana, kuhusika
na kufurahia yale tunayokutana nayo katika miili na akili zetu. Kadiri tunavyofanya
hivi kwa kila tukio ndivyo tunagundua tabia mbaya na kuamua kuachana nazo.
6. Tunashutuka
kuwa tupo kwenye ulevi/uteja wa tabia flani wakati ambao tayari athari hasi
zimeonekana kwenye mwili/akili zetu. Hali hii inatuingiza kwenye gharama kubwa
za kiafya wakati wa kukabiliana na athari husika. Pia ni muhimu kufahamu kuwa
uteja/ulevi unasababishwa na tabia ya kupenda raha au faraja ya muda mfupi. Mfano,
mtu anakunywa pombe kali kwa kisingizio cha kupoteza mawazo wakati pombe hizo
mwisho wake zina madhara makubwa kiafya.
7. Watu
wengi wanapoteza mahusiano na watu wa karibu nao kutokana na kuwa mateja/walevi
wa vitu flani. Mfano, watu wengi wamekimbiwa na wapenzi wao kutokana na tabia
ya ulevi wa pombe au uteja wa madawa ya kulevya. Pia, uteja huu unaongeza
msalaba kwa serikali katika kugharamia watu walioathirika.
8. Uteja/ulevi
wa tabia yoyote mhusika anaweza kuachana nao endapo yupo tayari
kushinda vichochoe vinavyomsukuma kwenye tabia husika. Mwandishi anatushirikisha
kuwa kuna wakati teja wa tabia yoyote ile anakuwa kwenye mazingira ambayo
hayampi nafasi ya kufanya tabia ambayo amezoea, mfano, kama ni mvutaji wa
sigara, huwezi kuvuta sigara wakati upo kwenye basi au usafiri wa ndege. Katika
mazingira kama hayo mhusika anapata vichocheo vya tabia husika lakini
anavipotezea. Hii ni mbinu ambayo kila mtu anaweza kuitumia kushinda vichochoe
vya uteja alionao.
9. Njia
nyingine ya kuachana na uteja/ulevi ni kutumia hatua hizi; i) tambua ni
kichocheo cha tabia ipi kinachotawala akili yako kwa wakati husika; ii)
kubaliana na uwepo wa kichocheo husika kwenye akili yako – kwa maana
husipambane na kichocheo hicho; iii) chunguza mwitikio wa mwili, hisia na fikra
– jiulize maswali kama “ni nini kinaendelea ndani ya mwili na akili yangu?” na iv)
elewa hali ulinayo kwa wakati husika. Hatua hizi kwa ujumla wake zitaunganisha
mwili wako na akili katika kuelewa sababu zinazopelekea vichocheo vya tabia
husika na hivyo kuchukua hatua stahiki dhidi ya vichocheo hivyo.
10. Watu wengi wamekuwa watumwa/mateja wa mitandao
ya kijamii (facebook, instangram) bila kujua kuwa utumwa huo unachochewa na
yale wanayofanya kila wanapokuwa kwenye mitandao hii. Uteja huu wa mitandao
unajengeka kwa kufuata hatua zile tatu (angalia point ya pili juu), mfano, kila
unapowaza facebook unakuwa umetengeneza kichocheo ndani ya akili yako; kila
unapowaza ‘kupost’ picha au kitu chochote unakuwa tayari umejenga tabia ya
kutaka kila mara ‘upost’ vitu kwenye mtandao. Hata hivyo, baada ya kupost
unasubilia kuona mwitikio wa marafiki zako kwenye mtandao husika kupitia ‘likes’
na ‘comment’ zao. Kadiri likes zinavyokuwa nyingi ndivyo tunashawishika
kuendelea kutumia mitandao ya kijamii.
11. Uteja wa mitandao ya kijamii ni uteja sawa
na uteja wa madawa ya kulevya au uvutaji wa sigara. Uteja huu unaendelea
kutengeneza kizazi ambacho kinafikiria zaidi nafsi zake kuliko nafsi za
wengine. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kila mtu kwenye mitandao hii
anatafuta kukubalika zaidi kwa marafiki zake. Hivyo, kila mara anafanya vitu
ambavyo vitawavutia marafiki zake. Pia, mitandao hii imekuwa ni sehemu ya kukuza
umbea jambo ambalo ni uteja mbaya.
12. Uteja mwingine ambao unamtesa mwanadamu
wa kizazi hiki ni ule wa kufikiria hatima ya nafsi yake kuliko kitu chochote
kile. Uteja huu unapelekea mwanadamu kuwa na mawazo finyu/uongo juu ya ulimwengu
kutokana na mtazamo wake juu ya jinsi anavyotaka ulimwengu uwe kuliko ukweli
ulivyo. Hali hii inapelekea kuwa mtazamo wa uongo na hivyo kujikuta tunaishi kulingana
na kipimo cha mtazamo wetu kuliko uhalisia wa uwezo wa ulimwengu. Pia, uteja
huu umepelekea watu wengi kuishi kwenye maisha ya mashindano kwa vile kila
mmoja anaiona nafsi yake ni bora kuliko mwenzake.
13. Matumizi ya simu hasa simu janja
yameanzisha aina nyingine ya uteja kwa watumiaji. Watu wengine wameshindwa
kujidhibiti kwenye matumizi ya simu kiasi ambacho wanatumia muda mwingi kwenye
simu kuliko yale waliyopanga kutekeleza ndani ya muda husika. Uteja huu
unapelekea watu waathirika washindwe kutulia kwenye kazi wanayofanya na hivyo
kujikuta kila mara wanawaza kushika simu kwa ajili ya mawasiliano. Hii ni
pamoja na matumizi ya simu hata kwenye kazi ambazo zinahitaji utulivu wa akili
kama vile kuendesha vyombo vya moto.
14. Uteja mwingine ambao unawatesa watu
bila ya ufahamu wao ni uteja wa kufikiri ambao pia ni chimbuko la uteja wa kufikiria
nafsi zao zaidi. Mwandishi anatushirikisha kuwa kama hauwezi kudhibiti fikra
zako unakuwa upo kwenye hatari kubwa ya kundeshwa na fikra. Katika hali kama
hii mhusika anafanya vitu kwa kutegemea maamuzi binafsi ambayo mara nyingi
yanatokana na historia ya mafanikio yake. Mara nyingi mafanikio yanapumbuza
watu, hali ambayo inapelekea waone kuwa hakuna jipya zaidi ya kile walichofanikisha.
15. Tunaweza kudhibiti fikra kwa kufanya
tajuhudi (meditation). Mwandishi anatusshirikisha kuwa tafiti zinaonesha kuwa
watu ambao wamezoea kufanya tajuhudi wana uwezo mkubwa wa kutuliza fikra zao
kwenye tukio moja ikilinganishwa na wengine.
16. Upo uteja mwingine ambao watu wanaingia
bila ufahamu nao si mwingine bali ni uteja wa mapenzi. Katika uteja huu,
mhusika anajikuta katika hali ambayo kila analofanya anaona haliwezi kukamilika
pasipo uwepo wa mwenza wake ambaye kwa pamoja wapo kwenye dimbwi la penzi zito.
Ni katika hali hii unajikuta kila mara unamuwazia yule ambaye umempenda na haupo
tayari kusikiliza jambo lolote baya juu yake kutoka kwa watu wa karibu yako.
Zifuatazo
ni njia za kukabiliana na aina yoyote ile ya uteja;
17. Uwezo wa kutuliza akili bila kuruhusu
mwingiliano wa kitu chochote kile ni muhimu kwa ajili ya kufanikisha jambo
lolote. Hii ni pamoja na mafanikio kwenye biashara, kazini au kiroho. Njia pekee
ya kutuliza akili ni kuwa na muda kwa ajili ya kufanya tajuhudi. Hii ni pamoja
na kujenga hali ya kujiamini katika kila hali unayokutana nayo.
18. Mafundisho ya kibudha ni njia nyingine ya
kukabiliana na uteja. Mfano, moja ya mafundisho ya kibudha ni namna mtu
anavyotakiwa kuwa na mtazamo juu ya furaha na mateso. Yapo matukio yanayoonekana
kuwa ni ya furaha lakini katika mafundisho ya kibudha yanaonekana kuwa ni
mateso. Vivyo, hivyo yapo matukio ambayo yameaminishwa kuwa ni mateso lakini
katika mafundisho ya kibudha yanaonekana kuwa ya kifuraha.
19. Mara zote katika kila hali jitahidi
kuwa mwema au wastani. Hii ni pamoja na kuepuka kukaa kwenye hali ya msongo wa
mawazo. Hali hii itakusaidia kukabiliana na uteja wa mapenzi pamoja na uteja wa
kutanguliza nafsi yako kuliko kitu chochote.
20. Jenga tabia ya kuwa na huruma. Huruma ni
ile hali ya kuelewa na kuwa na mguso dhidi ya matatizo ya watu wa karibu yako. Hali
hii inavunja tabia ya kujifikiria sisi pekee na kuona kuwa kuna watu wenye
kuhitaji uwepo wetu katika kila hali.
21. Jenga mazoea ya kutokubaliana na
vichocheo vya uteja ulionao, hii ni pamoja na kuepuka mazingira yanayokusuma
kwenye hali ya kuhitaji kurudia tabia yako.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link). Nakutakia
mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com
|