Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri.
Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa
FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa
ni wiki ya 5 katika kipindi cha mwaka 2018 naendelea kukushirikisha uchambuzi
wa vitabu mbalimbali vyenye mafundisho tofauti katika kila sekta ya maisha
yako.
Makala hizi za uchambuzi wa vitabu
zimekuwa zikikufikia kila wiki kwa kadri ambavyo napata muda wa kukushirikisha
kile ninachojifunza kutoka kwenye vitabu hivi. Ni matarajio yangu kuwa muda
ninaotumia kukushirikisha uchambuzi wa vitabu umekuwa wa msaada mkubwa kwako
katika kubadilisha maisha yako.
Unaweza kujiunga na mtandao huu, KWA KUBONYEZA BONYEZA HAPA
na
kujaza fomu kisha bofya “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu.
Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja
kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “Powerful Skills” kutoka kwa mwandishi Heather Hansen. Mwandishi
wa kitabu hiki ni mtaalamu wa masuala ya mawasiliano na amekuwa msaada kwa watu
wengi kitaifa na kimataifa katika kuboresha mawasiliano yao katika masuala ya
mahusiano, biashara na kazini. Kitabu hiki mwandishi ametushirikisha mbinu
muhimu kwa ajili ya kutengeneza marafiki wengi, kudumisha mahusiano sehemu za
kazini au na watu wako wa karibu.
Karibu
tujifunze machache kati ya mengi ambayo mwandishi anatushirikisha katika kitabu
hiki:
1. Ili uwe na mafanikio katika
kuwasiliana/mahusiano na wengine ni muhimu kujifunza sifa za watu wenye mafanikio
katika mawasiliano/mahusiano. Sifa hizi ni pamoja na kujiamini na kuwa na
uhakika juu ya kile anachoongea, wanajua kuvuta hisia za wasilikilizaji/watu
wao wa karibu, wanaongea ukweli na wanajivunia jinsi walivyo, wanajiheshimu na
kuwaheshimu wengine na mara zote wanakuwa na mawazo chanya – sifa hizi kwa
pamoja zinawavuta watu pamoja na fursa kwa ajili ya mafanikio zaidi.
2. Jinsi ulivyo katika mawasiliano
au mahusiano na watu wengine ni matokeo ya majumuisho ya michango mbalimbali
kutoka kwa watu ambao umekutana nao katika vipindi tofauti vya maisha yako. Hawa
wanaweza kuwa ni walimu, wazazi, walimu wa kiroho, majirani au watu wa karibu
na wewe kwa ujumla wake. Watu hawa wanatoa athari (chanya/hasi) kwenye uwezo
wako wa kuongea/kujieleza na hivyo mahusiano yako na watu wengine kwa ujumla
wake. Wazazi/walezi wana mchango mkubwa kutokana na ukweli kwamba hawa ni watu
wanaoongoza watoto wao toka enzi wakiwa wadogo.
3. Katika
mahusiano kuna vitu vitatu vya kuzingatia; moja, kukubalika – kila mtu kwenye
mahusiano anahitaji kuwa na uhakika wa kukubalika na wenzake, mbili, faraja – kwenye
mahusiano kila mtu anapenda apate faraja au aone watu wake wa karibu wanamjali/kumpenda,
na tatu, nguvu ya kuamua – katika kila hali kwenye mahusiano kila mtu angependa
awe na uhuru wa kuamua mambo muhimu juu yake pamoja na mazingira yanayomzunguka.
Nguvu hii inatakiwa iwe kwenye mlinganyo kati ya wote waliyopo kwenye mahusiano
kwa kuzingatia sheria au taratibu walizojiwekea.
4. Katika
mahusiano ni lazima kwanza mhusika atambue mahitaji yake binafsi na hatimaye
atambue wengine wanahitaji nini kutoka kwake. Hii ni pamoja na kutambua watu wa
rika mbalimbali kutoka sehemu tofauti pasipo kujali rangi au utaifa wanahitaji
nini kutoka kwako. Kama unafanya kazi au biashara ambayo wateja wako ni watu
tamaduni tofauti ni lazima uwe tayari kujifunza namna ya kuwasiliano nao kwa
mafanikio.
5. Jifanyie
tathimini binafsi pale unapoenda kuingia kwenye mahusiano mapya au pale unapotegemea
kukutana na watu wapya. Ni kawaida sana watu kuogopa wenzao hasa pale
wanapokutana kwa mara ya kwanza. Mwandishi anatushirikisha kuwa kabla ya
kuingia kwenye mahusiano na watu wapya ni muhimu kujitathimini kwa kujiuliza
maswali kama vile, Je ningekuwa wao ningependa kujisikiliza kile ninachoenda
kuwasilisha? Je ningekuwa upande wao ningefanya biashara hii? Je nina uhakika
na ninachowasilisha, na Je najipenda mwenyewe?
6. Kinachowafanya
watu wengi washindwe kuwa na mahusiano bora na watu wengine ni kutokana na
tabia ya kuingia kwenye mahusiano wakiwa na matazamio hasi dhidi ya wale
wanaoingia nao kwenye mahusiano. Katika hali
kama hiyo ni vigumu kujenga mahusiano ya muda mrefu kwa vile hakuna uaminifu.
7. Tabia
ndio msingi mkuu katika mahusiano. Tabia ni maamuzi ya mhusika kwani unaweza
kuamua kuwa na tabia njema au mbaya. Tabia uliyonayo ndiyo itakuwa mwamuzi
dhidi ya watu kuvutika kuja kwako au kukimbia dhidi yako. Mfano, katika
mahusiano na watu wengi tabia za kichoyo, ubinafsi, kukosa uvumilivu, hasira na
kukosa heshima haziwezi kukufikisha kwenye mahusiano mema na wanaokuzunguka.
8. Unahitaji
kuepuka hali hizi katika kuboresha tabia yako. Kundi la kwanza ni kukosa muda
wa kutosha kwa ajili ya usingizi, hii ni changamoto dhidi ya tabia yako katika
mahusiano na watu wengine – unapokosa muda wa kusinzia inakuwa vigumu kufikiri
vyema na matokeo yake muda wote unaonekana umechoka. Hali hii inawakimbiza watu
wengi dhidi yako.
9. Kundi
la pili ni msongo wa mawazo, matatizo binafsi na kushindwa kujiamini. Unapokuwa
na msongo wa mawazo pamoja na kuchanganya matatizo binafsi unakuwa na hali ya
hasira dhidi ya watu wa karibu yako. Pia, kushindwa kujiamini ni chanzo cha
kukimbiwa na watu wengi kwani kama haujiamini mwenyewe ni vigumu kuaminiwa na
watu.
10. Kundi la tatu ni kuwa na hisia kali. Mwandishi
anatushirikisha kuwa hisia ni chanzo cha kuona kuwa wewe ni bora kuliko wengine
na hivyo hali kama hii inasababisha mhusika kuwa na majivuno. Unapokuwa na
mahusiano na watu wengine mara zote unapaswa kujitahidi kudhibiti hisia zako.
11. Ili ujiamini ni lazima mtazamo wako wa
nje uwe vizuri. Hii ni pamoja na kujisitiri kwa mavazi mazuri yanayoendana na
tamaduni za sehemu ulipo. Hata hivyo muda wote unapaswa kuwa na uso wa furaha
ili kuepuka sura ya kuogepesha. Hali hii itakusaidia kupendwa na watu zaidi
katika shughuri zako hasa wale wanaoendana na hadhi yako.
12. Jitahidi kuonesha nafsi yako halisi pale
unapokutana na watu wapya. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wanahitaji
kuingia kwenye mahusiano ya undugu au urafiki na watu ambao ni wa kweli na
wanasimama kwenye misingi ya maisha yao. Katika mawasiliano na watu unatakiwa
kuepuka kuwa na sura mbili ili uweze kuaminiwa na watu. Hii ni muhimu pia
kwenye mahusiano ya kibiashara – watu hawapo tayari kufanya biashara na wewe
kama una sura ya kutoaminika.
13. Epuka kuwa mtu wa maneno bila vitendo. Tumezoea
kusikia msemo wa kuwa ‘video haiendani na audio’ kwenye tasnia ya muziki. Ndivyo
ilivyo hata kwenye mawasiliano na watu, watu wanakupima kile unachoongea
kupitia matendo yako. Kama matendo yako ni kinyume na maneno yako utawekwa
pembeni. Mara zote hakikisha maneno, sauti na vitendo vyako vinaendana.
14. Mara zote epuka kuoongelea umaarufu,
kipato, cheo, mali unazomiliki, hisitoria yako na mambo mengine kama hayo pale unapokutana
na watu wapya. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu tuna mitazamo na tafsiri
tofauti, unaweza kudhani kuwa kuongelea mafanikio uliyonayo kama chachu ya
kuvuta watu kwako kumbe ukatafisiriwa kama vile unaringa au una majivuno.
15. Kumbuka kuwa hauwezi kupendwa na kila
mtu kwenye makundi ya watu unayokutana nayo. Kadri unavyokutana na makundi ya
watu wapya usilazimishe kutafuta umaarufu ili upandwe na watu wote kwani
kufanya hivyo unaweza kushusha heshima zako na kujikuta unadharauliwa.
16. Tafuta sehemu muhimu ambazo
zinakuunganisha na watu pale unapokutana na watu wapya. Sehumu hizi zinaweza
kuwa vitu ambavyo wote mnafahamu, hobi ambazo wote mnazo, wote mmetokea sehemu
moja (kijiji, wilaya, mkoa, taifa au bara) au fani zenu zinafanana. Baada ya
zoezi hili, sasa unahitaji kutumia sehemu hizi muhimu kwa ajili ya kuanzisha
mazungumzo na yule au kundi la watu ambao umekutana nao kwa mara ya kwanza. Kumbuka
kujizuia ili husionekana kuwa kiongozi wa maongezi husika badala yake maongezi
yawe ya pande zote.
17. Jifunze kusikiliza kutoka kwa wenzako
ili uelewe mada kwa mapana. Mwandishi anatushirikisha kuwa usikivu ni nyenzo
muhimu katika kutengeneza marafiki wapya. Hii ni kutokana na ukweli kwamba
kadri unavyosikiliza ndivyo unapata uelewa na hisia zaidi juu ya mada husika. Katika
kusikiliza unapaswa kudhibiti hisia zako ili kuepuka kuwa na majibu, maamuzi au
mawazo yanayotokana na hisia binafsi.
18. Baadhi ya makosa ambayo yanafanywa na
watu kwenye usikivu ni pamoja na; i) tabia ya kufanya maamuzi – hapa watu
wanajiona kuwa bora kuliko wenzao. Tabia hii inawafanya washindwe kufungua
akili yao kwa ajili ya kusikiliza wenzao; ii) tabia ya kumalizia mawazo ya
wengine – hapa pindi mtu anao wewe unatafuta namna bora ambayo unaweza kuelezea
mada inayowasilishwa na matokeo yake unakosa pointi muhimu kutoka kwa
mwasilishaji; na iii) tabia ya kuweka hisia zako mbele – unapokubali hisia zikutawale
moja kwa moja unakuwa umezuia muunganiko wewe na yule anayeongea.
19. Matumizi ya lugha ya mwili ni nyenzo
muhimu ya kumuunganisha msikilizaji na mtoa mada. Mwandishi anatushirikisha
kuwa unaposikiliza ni muhimu kutumia lugha ya mwili kama vile kutikisa kichwa
ili mtoa mada afahamu kuwa mko pamoja.
20. Ukiwa katika kutoa mada jitahidi sana
kutumia sauti inayoendana na kile unachowasilisha. Mfano, kama unawasilisha
mada ya furaha ni muhimu kutumia sauti ambayo itawafanya wasikilizaji wapate
mguso wa furaha. Hali kadharika kama unawasilisha mada ya uzuni, tumia sauti ya
uzuni. Hali hii inaleta muunganiko wa hisia kati ya msikilizaji na mtoa mada.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link). Nakutakia
mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com
|