Mambo Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha Se Habla Dinero: Mwongozo wa kila siku wa kufanikiwa kifedha

Habari ya leo rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri.

Kwanza niombe radhi kwa kushindwa kukushirikisha usomaji wa kitabu kwa takribani wiki 2 zilizopita kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu.

Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya 11 katika kipindi cha mwaka 2018 naendelea kukushirikisha uchambuzi wa vitabu vyenye mafundisho tofauti katika kila sekta ya maisha yako.

Kama ambavyo, makala hizi za uchambuzi wa vitabu zimekuwa zikikufikia kila wiki kwa kadri ambavyo napata muda wa kukushirikisha kile ninachojifunza kutoka kwenye vitabu hivi. Ni matarajio yangu kuwa muda ninaotumia kukushirikisha uchambuzi wa vitabu umekuwa wa msaada mkubwa kwako katika kubadilisha maisha yako.

Unaweza kujiunga na mtandao huu, KWA KUBONYEZA BONYEZA HAPA na kujaza fomu kisha bofya “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.

Kitabu cha wiki hii ni “Se Habla Dinero ~ Pesa zinaongea” kutoka kwa mwandishi Lynn Jimenez.

Neno “FEDHA” limekuwa ni kitendawili ambacho kila mtu anatoa majibu kulingana na mazoea yake kwenye ulimwengu wa fedha. Wapo wanaosema fedha kamwe haiwezi kutosha, fedha hazitunziki, fedha hazitakiwi kuongelewa au fedha zipo chache na kwa watu wachache ambao ni wateule. Ni kutokana na mtazamo huu watu wengi linapokuja suala la kuwa na uhuru wa kifedha maswali mengi yanakuwa; nitaweza vipi kutengeneza pesa? Naweza vipi kuitunza pesa isipotee? Nawezaje kuifurahia pesa yangu kwa sasa huku nikiendelea kutengeneza pesa kwa ajili ya siku zijazo?

Mwandishi katika kitabu hiki anatushirikisha mbinu muhimu za kufanikiwa kifedha na hatimaye kuwa na uhuru wa kifedha. Hii ni pamoja na mbinu za uwekezaji, namna ya kukopa kwa mafanikio na jinsi ya kudhibiti matumizi ya fedha zako. Hivyo, kupitia kitabu hiki tunapata majibu ya namna ya kutengeneza pesa, kutumia pesa na kuiwekeza kwa ajili ya kupata fedha zaidi.

Karibu tujifunze machache kati ya mengi ambayo mwandishi anatushirikisha katika kitabu hiki:

1. Mafanikio kwenye kitu chochote kile ni matokeo ya imani ulijiwekea. Katika sekta ya fedha kila mtu ana imani yake, wapo wanao amini kuwa pesa ni mbaya au nzuri. Mwandishi anatushirikisha kuwa pesa ni nyenzo tu kwa ajili ya kufanikisha baadhi ya majukumu tulionao. Ubaya au uzuri wa pesa unategemea na namna tunavyoitumia katika kukamilisha hayo majukumu. Endapo imetumiwa vyema fedha itakusaidia kukamilisha majukumu yote muhimu katika maisha yako ya kila siku.

2. Endapo fedha itatumiwa vibaya itamfanya mhusika kukosa uhuru wa kuwa karibu na watu wake wa karibu na hata kukosa mahitaji muhimu ya maisha. Pia, fedha inapotumiwa vibaya mhusika anaweza kuingia kwenye madeni makubwa ikiwa ni pamoja na kukosa uhuru wa maisha yake. Jambo muhimu la kujifunza ni kwamba unatakiwa kuidhibiti fedha na usipofanya hivyo itakudhibiti yenyewe. Njia bora ya kudhibiti pesa yako ni kuwa na vipaumbele vya namna ya kuitumia kutekeleza matakwa yako muhimu bila kupoteza utu wako.

3. Kama mzazi unahitaji kuwafundisha watoto wako kuhusu fedha wakiwa bado wadogo na njia rahisi ya kufanya hivyo ni kuruhusu wote kuongelea fedha. Hii ni pamoja na kuongelea mapato na matumizi ya fedha za familia kila mara na namna fedha hizo jinsi zinavyopatikana kutoka kwenye mifereji mliyonayo.

4. Unapokuwa na hela ambayo unahitaji kuiwekeza kwa ajili ya baadaye ni muhimu kuhakikisha fedha hizo inawekezwa sehemu salama. Kwenye kuifadhi fedha kila mtu ana sehemu anazohifadhia fedha zake. Wapo ambao wanahifadhi benki, wapo wanaohifadhi chini ya godoro au kwenye kibuyu. Mwandishi anatushirikisha kuwa unapohifadhi fedha ni muhimu kujihakikishia juu ya usalama wa fedha hizo dhidi ya wezi, wadudu/panya au majanga ya moto. Pia, ni muhimu kuhifadhi sehemu ambayo fedha inaongezeka kwa siku za baadae kupitia ongezeko la riba (compounding interest).

5. Fahamu umuhimu wa ongezeko la riba katika kuwekeza pesa zako. Unapowekeza fedha kwenye benki ambayo ongezeko la riba mfano ni 5% kwa mwaka ina maana kuwa baada ya mwaka mmoja fedha hizo zitaongezeka kwa 5% na baada ya mwaka wa pili ongezeko litakuwa ni 5% ya kiasi kilichokuwepo baada ya ongezeko la mwaka wa kwanza. Hivyo, hivyo mpaka miaka kumi na kuendelea na hivyo ndivyo fedha zako zinatengeneza fedha zaidi wakati wewe ukiwa umepumzika.

6. Kama huhitaji kutumia fedha zako ndani ya muda mfupi unaweza kuwekeza fedha hizo kwenye ‘fixed account’ ambapo utafanikiwa kupata ongezeko la riba kulingana na utaratibu wa benki uliweka fedha zako. Pia, mwandishi anatushauri kufungua akaunti ya uwekezaji (saving account) badala ya akaunti ya kutunzia fedha (deposite account). Katika akaunti ya uwekezaji, pesa inayowekezwa inaongezeka kila mwaka kwa kutegemea riba inayotolewa na benki.

7. Mifumo ya kuweka au kutoa pesa kwenye akaunti yako ya benki siku hizi imerahisishwa kwa kutumia mfumo wa mtandao. Siku hizi unaweza kufanya huduma zote za kibenki ukiwa kwenye umekaa Ofisini au nyumbani kwako kwa kutumia simu yako au kompyuta mpakato. Hata hivyo, mwandishi anatukumbusha umuhimu wa kuhakikisha mifumo hii hisiwe sehemu ya kurahisisha matumizi ya hovyo ya fedha zako.

8. Kipindi cha muda unaotakiwa ili pesa inayowekezwa itumike kwa siku za baadae ndicho kinaamua njia ipi ya uwekezaji itumike kwa ajili ya kuwekeza peza zako. Hii ina maana kwamba kama unategemea pesa unayowekeza uitumie ndani ya wiki mbili zijazo au mwezi hauwezi kuiweka kwenye akaunti ya akiba ukitegemea kufaidika kupitia ongezeko la riba. Lakini kama pesa hiyo ipo kwenye mipango ya mwaka mmoja na kuendelea huna budi kuiwekeza kwenye sehemu ambayo fedha itaongezeka kupitia ongezeko la riba au kupitia gawio.

9. Watu wengi wanashindwa kutenga fedha kwa ajili ya uwekezaji ili kukidhi mahitaji ya fedha kwa siku za baadae lakini kamwe hawajahi kukosa fedha kwa ajili vitu visivyo vya lazima kama vile kununua kila toleo la nguo zinazoingia au fedha za vocha kwa ajili ya vifurushi. Mwandishi anatushirikisha kuwa ili kuwa na uhuru wa kifedha ni lazima mhusika awe tayari kwa ajili ya kujibana kwenye matumizi yasiyo ya lazima na fedha hizo zitengwe kwa ajili ya uwekezaji.

10. Katika uwekezaji unahitaji kutenga fedha kwa ajili ya mahitaji muhimu kwenye uzee wako au fedha kwa ajili ya kustaafu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kama kiumbe hai kila siku unaongezeka umri na kadri unavyoongezeka umri ndivyo uwezo wa kufanya kazi unavyozidi kupungua. Matokeo yake kuna kipindi ambacho hautakuwa na uwezo wa kufanya kazi wakati mahitaji ya fedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji muhimu ya maisha yatakuwa yako palepale.

11. Ili uwe uhuru wa kifedha ni lazima utumize hatua mbili ambazo ni kudhibiti matumizi ya fedha na kuhakikisha unajilipa kwanza. Hatua hizi zinategemeana kutokana na ukweli kwamba unapodhibiti matumizi ya fedha unaokoa fedha ambazo unatakiwa kuziwekeza kwa ajili ya kukuza fedha zako (kujilipa kwanza). Hii ndio siri ya kuwa tajiri na ili ufanikishe siri hii unatakiwa kuanza sasa kwa kuhakikisha kila mara unapopata fedha utenge fedha kwa ajili ya kuwekeza kabla kufanya matumizi mengine. Kwa maana uwekezaji uwe kipaumbele namna moja.

12. Katika kudhibiti matumizi ya hovyo unahitaji kuwa na bajeti ya fedha zako na bajeti hii inatakiwa kuwa mwongozo katika manunuzi/matumizi ya kila mara. Bajeti hii inatakiwa kuwa mahitaji yote muhimu ambayo yanatakiwa katika maisha yako ya kila siku bila kusahau fedha za uwekezaji. Hii ni pamoja na fedha ambazo huwa unatoa kama msaada kwa ndugu na jamaa pamoja na gharama za afya, sadaka, mavazi, chakula na vinywaji.

13. Siri nyingine ambayo mwandishi anatushirikisha katika kitabu hiki ni kuhakikisha matumizi yanakuwa kidogo ukilinganisha na mapato. Hii inakuafanya ujibane kwa ajili ya kuishi maisha ya hadhi yako. Watu wengi katika maisha wanaishi maisha ya maigizo na matokeo yake matumizi yao yanakuwa makubwa kuliko mapato walinayo jambo linalopelekea maisha ya kuunga kuunga. Mfano, mtu analazimika kula kwenye hoteli kila siku wakati ana uwezo wa kununua chakula na kupika chakula ambacho ni bei nafuu ukilinganisha na cha hotelini.

14. Punguza/epuka madeni yasiyo ya lazima kwa ajili ya kuokoa fedha ambazo utawekeza kwa matumizi ya baadae. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wengi wanakandamizwa na madeni ambayo mara nyingi yanalipwa na riba juu. Na madeni yaliyo mengi wakopaji wanachukua mkopo kabla kufanya tathimini ya namna mkopo husika unatakiwa kutumika kuzalisha faida kama sehemu ya kulipia riba ya mkopo na faida. Mkopo mzuri ni ule ambao unakopa kwa ajili ya kupanua biashara ambayo tayari unafahamu changamoto zake. Epuka mkopo kwa ajili ya kununua gari, kujenga jina baa na kununua vyakula.

15. Kuna tofauti kubwa kati ya kuwa tajiri na kuonekana tajiri. Watu wengi wanakazana kwa ajili ya kuonekana matajiri na hivyo wanaishi maisha ya kuigiza mifumo ya maisha ya matajiri na matokeo yake wanashindwa kuufikia utajiri wa kweli (uhuru wa kifedha). Mfano, mtu anataka aonekane anaendesha gari kali wakati hata uwezo wa kulihudumia kwake ni tatizo. Ili uwe tajiri ni lazima ukazane kununua vitu ambavyo thamani yake inaongezeka kadri siku zinavyoongezeka.

16. Husikazane kwa ajili ya kumiliki gari kubwa au nyumba kubwa ambayo ipo nje ya uwezo wako. Watu wengi wanapambana kwa ajili ya vitu ambavyo vinahitaji gharama kubwa na matokeo yake wanashindwa kukamilisha miradi hiyo au hata pale wanapokamilisha wanakuwa kwenye madeni makubwa. Pigania kile ambacho ukamilishwaji wake hautakuchia pengo kubwa kiuchumi.

17. Hakikisha una uhakika wa kutosha kuhusu biashara unayokusudia kufanya kabla ya kuchukua mkopo wa biashara. Hii ni pamoja na kufahamu gharama za uendeshaji wa biashara husika kwa kipindi cha mwaka. Hata hivyo, mwandishi anatushirikisha kuwa kabla ya kuchukua mkopo unatakiwa uwe umefanikiwa kuwekeza fedha zako mwenyewe kwa ajili ya gharama zinazohusiana na uanzishwaji wa biashara. Gharama hizi ni zile zisizo husika moja kwa moja kwenye utengenezaji wa faida katika biashara unayokusudia kufanya.

18. Utunzaji wa kumbukumbu ni muhimu katika ufanisi wa uendeshaji wa biashara. Takwimu muhimu kama vile bidhaa zinazoingia na kutoka pamoja na mtiririko wa fedha ni muhimu katika ustawi wa biashara. Takwimu hizi ndizo zinaonesha kama biashara inakua au imedumaa. 

19. Uwekezaji wenye tija ni pale pesa inapotumika kuzalisha pesa zaidi. Kama mwekezaji unatakiwa kuhakikisha kila shilingi unayowekeza inatumika kuzalisha pesa kwa ajili ya ukuaji wa fedha zako. Hapa ndipo unahitaji kufahamu miujiza ya ongezeko la riba kwenye pesa unayowekeza katika kipindi cha muda maalum. Na ili uwe mwekezaji mwenye mafanikio ni lazima uwe tayari kutenga asilimia flani ya fedha kwa ajili ya uwekezaji kutoka kwenye kila shilingi inayoingia kwenye mkono wako.

20. Ili ufanikiwe katika uwekezaji ni lazima uwe na lengo kubwa la nini hasa unahitaji kufanikisha kupitia uwekezaji wako. Lengo hili ndilo linatakiwa kuwa chachu kwako kwa ajili ya kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kufanikisha ndoto zako za uwekezaji. Na hapa ni lazima uwe tayari kubeba hatari za kiuwekezaji ambazo zinaweza kujitakeza katika safari yako ya uwekezaji.

21. Katika uwekezaji unatakiwa kufahamu nguvu ya mfumuko wa bei. Unapowekeza unatakiwa kujiuliza kama kiwango cha ongezeko la riba kinacholipwa kupitia fedha unazowekeza kama kipo juu ya kasi ya ukuaji wa mfumuko wa bei. Mfano, kama kiwango cha riba ni asilimia nne kwa kila shilingi uliyowekeza kwa mwaka na wakati huo huo kasi ya ukuaji wa mfumuko wa bei ni asilimia nne kwa mwaka, maana yake ni kwamba pamoja na fedha ulizowekeza zimeongezeka kwa asilimia tatu kwa mwaka lakini ongezeko hilo halina maana yoyote kwenye soko. Kanuni muhimu katika uwekezaji ni kuhakikisha unawekeza sehemu ambayo asilimia ya ongezeko la riba ni kubwa kuliko kiwango cha mfumuko wa bei.

22. Baada ya kufanikiwa kutengeneza utajiri kupitia uwekezaji mbalimbali sasa unatakiwa kuhakikisha unalinda fedha zako dhidi ya wezi, wajanja na kodi zisizo za lazima. Hii ni kutokana na ukweli kwamba ili uwe tajiri inahitaji miaka kadhaa lakini kupoteza pesa ulizokusanya kwa kipindi kirefu ni kitendo cha sekunde chache. Hivyo, mwandishi anatushirikisha umuhimu wa kuwa makini katika kulinda utajiri wako.

Haya ni machache ambayo nimeweza kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.

Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link). Nakutakia mapambano mema.

Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na mwisho.

Born to Win ~ Dream Big 

Augustine Mathias Bilondwa

Namba ya Simu:      +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com

PATA UCHAMBUZI WA KITABU CHA THE RULES OF MONEY ( KANUNI ZA PESA)
 
Mwandishi Richard Templar katika kitabu hiki ametushirikisha kanuni 107 ambazo kila mtu anaweza kuzitumia kutengeneza pesa na hatimaye kuwa tajiri. Uchambuzi wa kina wa kanuni zote (107) umeandaliwa kwa mfumo wa pdf na unapatikana kwa gharama ya Tshs. elfu tano tu (5,000/=). Kanuni zote zimechambuliwa na kuandaliwa kijitabu kidogo chenye kurasa 39 ambazo unaweza kusoma kwenye simu ya mkononi (smart phone) au kwenye kompyuta (pc).

Kupata uchambuzi wa kanuni zote tuma pesa yako kwa njia ya M-pesa au Airtel Money kupitia namba zifuatazo:-

M – Pesa tumia namba: 0763 745 451 (Majina ni Augustine Mathias)
Airtel Money tumia namba: 0786 881 155 (Majina ni Augustine Mathias)

Baada kutuma pesa hiyo nitumie ujumbe kwenye namba ya airtel (0786 881 151 451) ukiwa na barua pepe yako ili nikutumie uchambuzi wa kanuni hizi moja kwa moja kwenye mtandao wako.

UTAJIRI NI HAKI YAKO YA KUZALIWA "BEING RICH IS YOUR BIRTH RIGHT"





onclick='window.open(