Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa Fikra za Kitajiri.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Naamini kuwa rafiki yangu unaendelea
vizuri na mapambano ya kila siku kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Kama
kawaida yangu, leo katika uchambuzi wa vitabu kupitia mtandao wa Fikra za
Kitajiri nakushirikisha uchambuzi wa kitabu cha wiki hii.
Kama bado hujajiunga kwenye mfumo wetu
wa kupokea makala za uchambuzi wa vitabu, tafadhali fanya hivyo KWA KUBONYEZA BONYEZA HAPA
na
kujaza fomu kisha bofya “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu. Ni
fursa ya bure ambayo utaendelea kupata uchambuzi wa vitabu kwa lugha rahisi
kupitia barua pepe yako.
Kitabu
cha wiki hii ni “A Gift To My Children” ambacho
kimeandikwa na mwandishi Jim Gogers. Mwandishi ametumia kitabu hiki
kutushirikisha uzoefu wake wa maisha pamoja na uwekezaji. Uzoefu
anaotushirikisha umetokana na maisha aliyoishi kama baba wa familia lakini pia
kama mwekezaji kwenye upande wa fedha. Ikumbukwe pia kuwa Rogers ni mtu wa
kwanza kuweka rekodi za dunia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzunguka mabara
sita (Dunia) kwa kutumia pikipiki.
Karibu
ushirikiane nami kujifunza machache kati ya mengi ambayo mwandishi
anatushirikisha katika kitabu hiki:
1. Maisha unayoishi ni yako
mwenyewe hivyo kumbuka kutegemea sana akili yako pindi unapofanya maamuzi
muhimu katika maisha yako. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika maisha kuna
watu wanatuzunguka ambao wapo tayari kutoa ushauri hata kama hawajaombwa
kufanya hivyo. Mara nyingi washauri hawa wengi wao huwa wanashauri hata kwenye
masuala ambayo hawana uelewa mpana. Jifunze kwa mapana juu ya changamoto
inayokukabili ili kuwa na uelewa wa kutosha kuliko washauri wanaokuzunguka. Kumbuka
wewe ndo wa kuchagua namna unavyotaka maisha yako yawe kabla ya kutegemea
wengine wakusaidie kufanya hivyo.
2. Mtu akidharau wazo lako au
mipango yako ya mafanikio itazame hali hiyo kama deni lako la kufanikiwa zaidi.
Mwandishi anatushirikisha kuwa ni wewe pekee mwenye uhakika na wazo au mipango
yako ya mafanikio na kutambua hivyo husijali pale ambapo mtu au kundi la watu
wanashindwa kukuelewa. Husikabali kutoka kwenye mstari wako wa mafanikio
kutokana na maneno ya watu. Muhimu ni kuhakikisha una uelewa wa kutosha kwenye
kile ambacho umekusudia kutekeleza katika safari ya maisha yako.
3. Husifanye manunuzi ya vitu au
starehe za hanasa kwa sababu ya kwamba una uwezo badala yake hakikisha kila
unachoamua kinafanyika kwa kuongozwa na fikra za ndani mwako. Hapa mwandishi
anatushirikisha kuwa tusipende kuishi maisha ya kuigiza bali kila tunachofanya
kiongozwe na macho ya ndani mwetu. Kumbuka kuwa badala ya kuwekeza katika kununua
vitu vya gharama na hanasa ili kutafuta umaarufu wa nje tuwekeze tulichonacho kwa
ajili ya kuwa na maisha ya baadae kuliko tuliyonayo sasa.
4. Husikubali umri wako uwe
kizuizi cha kutimiza ndoto yako. Mwandishi anatushirikisha kuwa pale
unapochagua nini unataka kutimiza katika maisha yako moja kwa moja unatakiwa
kuanza kufanyia kazi machaguo yako pasipo kutazama umri wako au nafasi
uliyonayo kwa wakati husika. Muhimu katika kila hatua ni kufanya kufanya kufanya
kufanya...... bila kikomo kuliko kuendelea na maneno yasiyokuwa na utekelezaji.
5. Njia
rahisi ya kufanikiwa ni kufanya kazi ya tamanio la roho yako na kuhakikisha
unawekeza jitihada/bidii ya kutosha kwa ajili kazi hiyo kuwa bora kila siku.
Mwandishi anatushirikisha kuwa katika maisha hasa katika ukuaji utafanya kazi
nyingi lakini katika zote chagua kazi ambayo ni tamanio la moyo wako na
kuhakikisha unaweka bidii ya kutosha. Hata hivyo, unatakiwa kulenga kuikuza
kazi hiyo kutoka kwenye hali yake ya sasa ili kila siku iwe bora. Kumbuka kuwa
hata husipofanikiwa kuwa tajiri kupitia kazi hiyo utakuwa na furaha katika
maisha yako ya kila siku na utafanikiwa kukamilisha kazi iliyokuleta duniani
humu.
6. Kuwa
makini katika kila taarifa unayopata. Mwandishi anatushikisha kuwa siri kubwa
inayotofautisha waliofanikisha maisha na watu wengine ni kuchukulia kila
taarifa kwa umakini wake. Hii ni muhimu kutokana na ukweli kwamba kuwa taarifa
ndizo zinachambuliwa kwa ajili ya kufanyiwa kazi iwe kwenye uwekezaji au
mahusiano na watu wanaokuzunguka. Hivyo, ni muhimu kujenga utamaduni wa kufanya
tafiti za kina juu ya taarifa zinazokufikia kabla ya kuzifanyia maamuzi. Tafiti
hizi zinatakiwa kuongozwa na bidii ya kutaka kujua zaidi hasa juu ya kile
ambacho umeamua kufanyia kazi katika maisha yako.
7. Hakikisha
unaishi maisha yenye ndoto tena ndoto kubwa ambayo inakuogopesha. Mwandishi
anatushirikisha kuwa katika kufanya kazi ya matanio ya moyo wako ni lazima uwe
na ndoto ambayo ni chachu kwako kuendeleza kufanya makubwa katika maisha. Kadri
unavyoendelea kuifanyia kazi ndoto yako utagundua kuwa kukamilika kwa ndoto
hiyo ni mwanzo wa ndoto nyingine tena kubwa ambazo hukuwahi kuzitarajia katika
maisha yako.
8. Kumbuka
sio kweli kuwa kila jibu unaloambiwa ni HAPANA kweli ni hapana na kila
unachoambiwa NDIYO kweli ni ndiyo. Mwandishi anatushirikisha katika safari
ndefu ya maisha hatutakiwi kukubaliana na mitazamo ya watu moja kwa moja na
badala yake ni lazima tuwe na kanuni zinazotuongoza ambazo hata hivyo sio
lazima zikubaliwe na watu wanaotuzunguka.
9. Tembea
na kuona mapana ya dunia na kujifunza mengi kwenye kila nchi unayotembelea.
Mwandishi anatushirikisha kuwa ili kufanikiwa kimaisha unahitaji kujifunza
tamaduni mbalimbali zaidi ya eneo ambalo umekulia. Hata hivyo, unatakiwa
kutumia tamaduni hizo katika kufanikisha safari yako ya uwekezaji au mafanikio
ya maisha kwa ujumla. Ni kupitia kutembea utaweza kujijua vyema na pia kuweza
kuifahamu vyema nchi yako kwa kulinganisha na mazingira ya nchi nyingine. Ni
katika kutembea pia utajifunza kuwa watu wote ni sawa na hivyo unaweza kuishi
mahali popote na kutengeneza maisha unayotaka.
10. Kuwa muwazi kwa watu wote bila kujali
tamaduni, asili au rangi zao. Mwandishi anatushirikisha kuwa siri ya kufanikiwa
kimaisha ni kuhakikisha watu watu wote unawapa uzito sawa. Siri hii itakufanya
uishi na watu wa aina mbalimbali hata kama upo kwenye mazingira ya ugenini.
11. Wekeza kwenye nchi au maeneo ambayo
hayana ubaguzi wa rangi. Mwandishi anatushirikisha kuwa uwepo wa ubaguzi wa
rangi hasa kwenye baadhi ya nchi zilizoendelea imesababisha uwepo wa machafuko
mengi katika maeneo hayo. Hii ni pamoja na kuendelea kukua kwa matukio ya
ugaidi ambayo chanzo chake kikubwa ni mwendelezo wa chuki baina ya watu wa
asili au imani tofauti.
12. Katika hatua zote za ukuaji kuwa na
fikra uhuru na jitahidi kuwa raia wa mataifa au dunia kwa ujumla wake.
Mwandishi anatushirikisha kuwa kizazi cha sasa kipo kwenye zama za fikra huru
na chenye nafasi kubwa ya kuishi kidunia zaidi kuliko vizazi vilivyotangulia.
Hii ni kutokana na kukua kwa teknolojia ya mawasiliano ambayo imerahisisha
upatikanaji wa taarifa kutoka pande zote za dunia. Ukiwa na fikra uhuru za
namna hii utaishi maisha yenye furaha hasa kwenye kile ambacho umeamua kufanya
katika maisha yako na hii ndio itakufanya uwe uhuru kuishi na watu wa asili
tofauti. Kumbuka kuwa kama kila mtu angeishi kama raia wa dunia, dunia hii
ingekuwa ni mahali pazuri na salama kwa kila kiumbe kuishi.
13. Kumbuka kuwa vita haijawahi kuwa na
manufaa kwa mtu au hata nchi inayoshinda. Katika hatua za ukuaji na uwekezaji
jitahidi kukwepa nchi ambazo zinapigana vita mara kwa mara. Hii ni pamoja na
kuwa mmoja kati ya majeshi ya nchi na badala yake jitahidi kufanya kazi ambayo
itakuwa ni mapenzi kutoka moyoni mwako lakini pia inakufanya uwe na fikra uhuru
na pana katika maisha yako yote kwenye ulimwengu huu.
14. Jifunze falsafa (philosophy) kwani
kupitia elimu hiyo utaweza kujitambua na kufikiri kwa kujitegemea. Mwandishi anatushirikisha
kuwa njia ya kwanza ya kukamilisha hitaji lolote la maisha yako ni kujitambua
kwanza na elimu pekee ambayo inaweza kufanikisha hilo ni kupitia falsafa. Katika
elimu hiyo ya falsafa hautaji kuzama sana ili ufanikishe hilo bali unahitaji
kujikita kwenye kipengele cha kujitegemea kifikra au fikra huru. Hapa unahitaji
kujifunza kufikiri nje boksi kwa maana ya kufikiri nje ya mazoea, kweli, imani au
tamaduni zilizojengeka katika jamii unayoishi.
15. Kuna njia mbili za kufikiri na mwisho
kufanya maamuzi. Njia ya kwanza ni kufikiri kwa kutegemea uchunguzi au
mwonekano/uhalisia wa jambo husika. Njia ya pili ni kufikiri kwa kutegemea
nadharia (evidence) za kweli ambazo tayari zimewekwa wazi juu jambo husika
(kufikiri kwa mantiki). Mwandishi anatushirikisha kuwa hakuna njia ambayo ni
bora kuliko nyingine kati ya hizi njia mbili za kufikiri. Hivyo, unahitaji
kujifunza kuzitumia njia zote ili kuwa na mfumo msawazo wa kufikiri (balanced
way of thinking).
16. Jifunze historia ya ulimwengu kwa
mapana na tumia historia hii kujua mwenendo wa ulimwengu na vilivyomo ndani
yake. Katika historia hii unahitaji kupata picha kubwa ya namna ambavyo mabadiliko
mbalimbali yametokea katika Dunia hii na hivyo utumie matukio hayo kwa ajili ya
kukadiria matukio yanayokuja siku zijazo. Ni kupitia historia hii utajifunza
kuwa kilichosahihi leo hii kwenye mitazamo ya watu yawezekana baada ya miaka 10
au 20 hakitakua sahihi tena. Ni kupitia historia ya tamaduni au nchi mbalimbali
utafahamu ni sekta ipi unaweza kuwekeza kwa mafanikio.
Soma: Mambo Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha A Brief History of Humankind (Historia Fupi ya Mwanadamu)
17. Hakuna jipya chini ya jua. Mwandishi anatushirikisha
kuwa matukio yote yanayotokea katika ulimwengu wa sasa yamewahi kuwepo siku za
nyuma bali kinachofanyika matukio hayo yanawasilishwa kwa njia zenye ubunifu
tofauti lakini asili yake ni ya tokea enzi hizo. Katika safari ya maisha yako
unahitaji kuongozwa na kanuni ya kwamba yanayotokea katika ulimwengu wa sasa
yamewahi kuwepo na yatatokea katika ulimwengu wa baadae. Hii ndiyo siri kubwa
ya kutumia historia kwa ajili ya mafanikio yako hasa katika ulimwengu wa
uwekezaji.
18. Jifunze lugha mbalimbali lakini kama
utaweza hakikisha unajifunza kichina na kingeleza. Mwandishi anatushirikisha
kuwa katika ulimwengu wa uwekezaji mwenyekujua lugha ya sehemu husika ana
nafasi kubwa ya kufanikiwa kuliko yule ambaye hajui. Lugha ambazo zinakuwa kwa
kasi ni kichina pamoja na kingeleza hivyo katika kujifunza lugha ambazo sio za
asili yako hakikisha lugha hizo mbili zinakuwa sehemu ya malengo yako. Kumbuka kuwa
ukweli unajionesha wazi kuwa sasa ni karne ya China kuwa taifa kubwa kiuchumi,
kisiasa na kijamii duniani.
19. Jitambue wewe ni nani na muhimu zaidi
tambua madhaifu yako ikiwa ni pamoja na namna unavyokabiliana na makosa unayofanya.
Mwandishi anatufundisha kuwa njia pekee ya kujifunza kutokana na makosa yetu
katika ulimwengu wa uwekezaji au maisha ya kila siku kwanza ni kukubali kuwa
tumekosea. Kama haukubali kuwa unakoseaga kamwe hauwezi kujifunza kitu na mara
zote utaendelea kufanya makosa yaleyale.
20. Jifunze saikolojia. Mwandishi anatushirikisha
kuwa pamoja na kujifunza historia, falsafa pamoja na lugha unahitaji zaidi
kujifunza saikolojia. Katika ulimwengu wa uwekezaji unahitaji kufahamu zaidi
saikolojia ya watu kwa kuwa hii ndio inasababisha mabadiliko ya soko. Ni kutokana
na mabadiliko hayo watu wengi wanapaniki kiuwekezaji na hivyo kupelekea kuuza
kile walichowekeza kutokana na kuongozwa na hisia. Ni lazima uwe tayari kutumia
paniki za watu kwa ajili ya mafanikio yako.
21. Tambua mabadiliko mbalimbali
yanayotokea kwenye jamii na yatumie kwa faida yako. Mwandishi anatushirikisha
kuwa msingi mkuu wa uchumi unatokana na “kusambaza bidhaa – supply” na “mahitaji
ya bidhaa husika – demand”. Mabadiliko yoyote kati ya mahitaji au kusambaza
yanaweza kuathiri uchumi wan chi au mtu binafsi endapo hajajua kucheza
kulingana na mabadiliko katika soko.
22. Fanya utafiti wa kutosha kwenye sekta
ambayo kila mtu anakimbia. Mwandishi anatushirikisha kuwa kutokana na kuongozwa
na hisia watu wengi wanakimbia fursa kwa kuongozwa na maneno ya kusikia. Kama unahitaji
kuwa mwekezaji makini unahitaji kufanya tafiti zako mwenyewe na wekeza bila
kujali kuwa wengi wanakimbia sekta husika. Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa
mara zote unahitaji kuwekeza kwenye kitu kipya.
23. Fanyia kazi ndoto yako na kamwe
husikubali kukatiza ndoto hiyo kwa vyovyote vile. Mwandishi anatushirikisha
kuwa watu wengi wanakatiza ndoto zao kwa vile wanakubali kuyumbishwa na mawimbi
wanayokutana nayo njiani. Unahitaji kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha
kuwa unatimiza ndoto yako.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link). Nakutakia
mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com
|