Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa Fikra za Kitajiri.
Naamini kuwa rafiki yangu unaendelea
vizuri na mapambano ya kila siku kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Leo hii
pia katika uchambuzi wa vitabu kupitia mtandao wa Fikra za Kitajiri
nakushirikisha uchambuzi wa kitabu cha wiki hii.
Kama bado hujajiunga kwenye mfumo wetu
wa kupokea makala za uchambuzi wa vitabu, tafadhali fanya hivyo KWA KUBONYEZA BONYEZA HAPA
na
kujaza fomu kisha bofya “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu. Ni
fursa ya bure ambayo utaendelea kupata uchambuzi wa vitabu kwa lugha rahisi
kupitia barua pepe yako.
Kitabu
cha wiki hii ni “How to Build a Multi – Billion
Dollar Business in Africa” ambacho kimeandikwa na mwandishi Strive Masiyiwa. Kupitia kitabu hiki tunashirikishwa namna
ambavyo kila mtu anavyoweza kuanzisha biashara yenye mafanikio makubwa katika
Bara la Afrika na kuweza kuwa utajiri mkubwa sana (bilionea). Ikumbukwa kuwa
Strive ni mwekezaji mkubwa katika bara la Africa ambaye ni Mzimbabwe na
amewekeza kwa mafanikio kwenye mitandao ya simu na vyombo vya habari.
Karibu
ushirikiane nami kujifunza machache kati ya mengi ambayo mwandishi
anatushirikisha katika kitabu hiki:
1. Misingi mikuu ya mafanikio
katika biashara yoyote ni kuanza na kidogo ulichonacho, kuweka bidii ya kazi,
kuwekeza sehemu ya faida unayopata ili hatimaye uweze kufanya mambo makubwa
kiuwekezaji. Somo kubwa la kujifunza hapa ni kwamba kamwe husisubilie nyakati
sahihi zifike kwani wakati ulio sahihi wa kuanzisha biashara ya matamanio yako
ni sasa kwa kutumia kidogo ulichonacho. Somo jingine ni kwamba unahitaji
kufanya kazi kwa bidii na mwisho ni nidhamu ya fedha hasa kwenye faida
unayotengeneza.
2. Kukua kwa biashara ya aina
yoyote ile ni matokeo ya kudhibiti fedha. Fedha ndo kila kitu, hapa mwandishi
anatushirikisha kuwa kabla ya kuwekeza kwenye mradi wowote unatakiwa
kujiridhisha kwenye uimara wa mradi huo katika kipengele cha fedha zinazoingia
na kutoka. Namba ndo kila kitu – fahamu ni namba zipi zipo juu kati ya zile
zinazohusu fedha inayotoka na zile zinazohusu fedha inayoingia.
3. Kuna fursa nyingi za kuzalisha
mitaji kupitia mikopo na misaada inayotolewa ajili ya kuendeleza wajisiliamali
wadogo hasa katika Bara la Africa. Je umejiandaa vipi kwa ajili ya kufanikiwa
kupata mikopo au misaada hiyo. Kumbuka namba ndo kila kitu, je, una mpango wa
biashara yako ambao ndio dira kuu ya kuombea mikopo au misaada husika?
4. Katika jitihada zako za kukuza
mtaji au kukuza biashara yako unahitaji kutambua kuwa Mungu ndio jibu kuu. Anajibu
pale husipotegemea hivyo wajibu wako ni kumuomba kwa kumaanisha juu ya nia
unayohitaji. Unatakiwa kubakia kwenye nia hivyo bila kuyumbishwa na mawimbi ya dunia
ambayo yanaweza kuwa na tivisho vikali kwa nyakati unazopitia.
5. Simama
imara katika nyakati ngumu hasa pale unapokutana na vikwazo ambavyo vinakwamisha
njia yako ya mafanikio. Mwandishi anatushirikisha kuwa kuna kipindi ambacho
unajikuta kwenye nyakati ambazo unaona kuwa mradi wa ndoto yako hauwezi
kutekelezeka labda kutokana na mazingira ya kisheria. Masiyiwa yeye binafsi
alipitia kwenye nyakati hizo kipindi ambacho alikuwa kwenye hatua za awali za
kuanzisha kampuni ya mawasiliano ya simu nchini Zimbabwe. Kwa nguvu za Mwenyezi
Mungu alisimama imara mpaka kufanikiwa kutatua vikwazo vya kisheria vilivyokuwepo
dhidi yake.
6. Uaminifu
ni mtaji kuliko hata fedha zenyewe. Mwandishi anatushirikisha kuwa moja ya
nyenzo muhimu pale unapopambana kukuza biashara ni uaminifu. Unahitaji kuwa
mwanifu kwa wadeni wako hata nyakati zile ambazo unajikuta upo kwenye wakati
mgumu wa kurejesha madeni yako kwa wakati.
7. Katika
nyakati ngumu za vikwazo vya kisheria pamoja na rushwa hasa katika nchi
zinazoendelea unahitaji kuzungukwa na Wanasheria makini. Mwandishi anatushirikisha
kuwa pale ambapo unajikuta umekwama kisheria huna budi kuwa na timu ya
wanasheria makini na watiifu ambao sio tu wanahitaji kupata pesa zako bali
wanahitaji kufanikiwa kupitia utatuzi wa changamoto ulizonazo kwa wakati husika.
Kufanikiwa kupata Wanasheria makini kama hao huna budi kuwashirikisha historia
ya changamoto ulizonazo au pale inapobidi endelea kutumia timu ile ile kwa nyakati
tofauti ili kuwa na uelewa wa ndani wa biashara/kampuni zako.
8. Unapokuza
biashara yako ni lazima uwe tayari kuzungukwa na timu ya wataalam wenye weledi
na uzoefu wa kutosha. Kwa kifupi ni kwamba katika kukua kwa biashara ni lazima
uepuke washirika au wataalam wa bei nafuu kwani hawa ni chanzo cha kuua
biashara. Tafuta watu wenye uzoefu na kaliba ya utendaji kazi ya hali ya juu. Watu
hawa wawe na mchanganyiko wa taaluma, uzoefu wa taasisi tofauti na kutoka
sehemu mbalimbali ndani au nje ya nchi.
9. Katika
nyakati za kukuza mtaji wa biashara yako ni lazima uwe tayari kuuza mpango wako
wa kibiashara kwa wafadhili/wawekezaji mbalimbali. Kumbuka kuwa ili ufanikiwe
kupata ufadhili au kuwavutia wawekezaji wakubwa ni lazima mpango wako wa
kibiashara uwe na uhalisia hasa kwenye mpango wa mauzo.
10. Katika kukuza biashara yako ni lazima
uwe tayari kupanua wigo wa biashara kwa kufungua masoko mapya katika sehemu
mbalimbali. Mwandishi anatushirikisha kuwa biashara nyingi zinashindwa kupanuka
kwa vile zinaendelea kutegemea masoko yaleyale wakati kuna fursa nyingi katika
nchi zilizoendelea au zinazoendelea. Unahitaji kuifanya biashara yako isafiri
sehemu mbalimbali za dunia hii kwa kufungua masoko mapya ndani na nje ya mipaka
ya nchi yako ya awali.
11. Je unaona nini? Mwandishi anatushirikisha
kuwa kila mjasiliamalia anatakiwa awe tayari kuona fursa ambazo watu wengi
hawazioni. Hapa ndipo unatakiwa kuwa na makadirio chanya (projections) ya
ukuaji wa biashara yako ambayo hakuna hata mmoja anayeamini kuwa unaweza
kutimiza makadirio hayo. Kumbuka kuwa katika kila hatua ya ukuzaji wa biashara
yako ni lazima ufikirie kwa mapana.
12. Jifunze kuwekeza. Mwandishi anatushirikisha
kuwa kama hauna utamaduni wa kuwekeza fedha zote unazopata zitapitiliza na
mwisho wake hautajua zimepotelea wapi. Kumbuka kila mtu ana fedha za kuwekeza
pasipo kujali kiasi cha pesa alichonacho, anza kuwekeza ukiwa na hiki hiki
kidogo ulichonacho kwa ajili ya kujijengea utamaduni wa kuwekeza. Hapa ndipo
unatakiwa kujifunza kuhusu kuwekeza kwenye masoko ya hisa (stock markets) au
mifuko ya pamoja (mutual funds).
13. Je unawekeza wapi muda wako? Mwandishi anatushirikisha
kuwa kama unataka kuwa mwekezaji mzuri ni lazima uwe tayari kuwekeza muda wa
kutosha kwa ajili ya kufanya tafiti za uwekezaji. Unahitaji kusoma vitabu au
magazeti yanayohusu uwekezaji hasa kwenye uwekezaji wa hisa kwa ajili ya kujua
ni hisa za kampuni zipi ambazo zinafanya vyema kwenye soko kulingana na
historia ya kampuni husika. Kama ambavyo maandiko matakatifu yanasema kuwa “watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa”
ndivyo ilivyo kwenye ulimwengu wa uwekezaji. Watu wengi wanashindwa kuwa
wawekezaji wazuri kutokana na kushindwa kujifunza mbinu za uwekezaji.
14. Tekeleza majukumu yako ya kila siku kwa
mpangilio. Hakikisha unaanza na yale yenye umuhimu wa kukamilishwa kwanza kabla
ya kuanza yale ambayo si lazima yakamilishwe kwa wakati huo. Mwandishi anatushirikisha
kuwa kama unahitaji kuwa tajiri ni lazima utambue kutumia muda wako vizuri
kwani kinyume na hilo hautoweza kupiga hatua.
15. Jifunze miundo ya kampuni kubwa
zilizofanikiwa na namna ambavyo kampuni hizi zinaongozwa kwa ufanisi. Mwandishi
anatushirikisha kuwa kuna kampuni ambazo zina wafanyakazi wengi kuliko hata wafanyakazi
wa Serikali kwa baadhi ya nchi za Africa. Lakini kampuni hizi zinaongozwa na
mtu mmoja akisaidiwa na wasaidizi wake. Hivyo, kama unahitaji kumiliki na
kuendesha kampuni kubwa kiabiashara ni lazima uwe tayari kujifunza. Anza kujifunza
namna ya kuongoza wafanyakazi wako hata kwa biashara ndogo unayomiliki kwa
sasa. Lenga kupanua biashara hiyo mpaka kufikia kwenye viwango vya biashara
kubwa kimauzo katika soko.
16. Sifa ya mjasiliamali mzuri ni yule
ambaye anaweza kuanzisha, kukuza na kuongoza biashara yake kwa ufanisi hata
katika kipindi ambacho biashara hiyo imepanuka mpaka viwango vya kimataifa. Biashara
zilizo nyingi zinashindwa kupanuka mpaka kwenye viwango vya kimataifa kwa vile
wamiliki wanashindwa kuwa na ubunifu katika yale wanayofanya. Mwandishi
anatushirikisha kuwa kila biashara inaweza kutanuka na kufikia viwango vya
kimataifa bila kujali inajihusisha na nini au ndogo kiasi gani. Jambo la muhimu
ni kuhakikisha kuwa kila unapoitazama biashara yako uitazame kwa mapana ya
kimataifa na kuhakikisha kila mara unaweka mipango ya ukuaji kwa ajili ya
kufikia viwango hivyo.
17. Katika kukuza biashara yako unahitaji
kuwa makini katika kuchagua jina la biashara yako. Chagua jina ambalo ni rahisi
kulitangaza na linaweza kupenya nje mipaka ya sehemu ulipo na bado likaendelea
kukubalika kwa wateja. Jina linahitaji kuwa fupi, kipekee na lenye maana halisi
ya kile unachofanya. Biashara za kampuni zinatangazwa kupitia jina la kampuni. Pia,
mwandishi anatushirikisha kuwa ni muhimu kuhakikisha unatenga bajeti kwa ajili
ya kujitangaza kibiashara.
18. Epuka kuendesha biashara peke yako badala
yake jifunze njia mpya na za kisasa zinazotumika kuendesha biashara kupitia watu
mbalimbali ambao wapo tayari kufanya kazi kwa ajili yako. Mwandishi anatushirikisha
kuwa biashara nyingi ndogo katika maeneo mengi zinashindwa kuendelea kutokana
na kuendeshwa na mtu mmoja na pale inapotokea mtu huyo akakosekana basi na biashara
inakuwa ndo mwisho wake. Hapa ndipo unahitaji kuhakikisha unakuwa unatamaduni
wa kurudisha sehemu ya faida kwa ajili ya kuendeleza kupanua biashara husika
ili kila mara biashara hiyo iendelee kupanuka zaidi.
19. Upofanya maamuzi ya kifedha hakikisha
kuwa ni maamuzi sahihi. Mwanidishi anatushirikisha kuwa njia pekee ya kukuza
biashara ni kupitia maamuzi sahihi ya matumizi ya fedha ulizonazo kwa ajili ya
biashara. Ukifanya maamuzi ambayo sio sahihi matokeo yake ni kudumaza biashara
au kufilisika kwa ujumla. Kipo bora cha namna gani unafanya maamuzi sahihi ya
kifedha ni matokeo ya kifedha juu ya maamuzi uliyofanya. Kumbuka maamuzi sahihi
ya kifedha watu hawazaliwi na kuwa nayo bali taaluma ambayo kila mtu anaweza
kujifunza, hivyo, unahitaji kuwekeza muda wako kujifunza zaidi. Kumbuka maamuzi
sahihi ya kifedha yanaanzia kwenye fedha ulizonazo kwa wakati husika bila
kujali uchache au wingi wake na bila kujali umri ulionao.
20. Tambua nyakati zipi biashara
inajiendesha kwa kuzalisha pesa au bila kuzalisha pesa. Mwandishi anatushirikisha
kuwa katika uendeshaji wa biashara kuna kipindi ambacho unaweza kuwa na mauzo
makubwa lakini kumbuka kuwa wingi wa mauzo sio kwamba biashara inajiendesha kwa
faida. Ni wajibu wako kama mmiliki wa biashara kufanya maamuzi sahihi ya
kifedha kulingana na nyakati husika kwenye biashara.
21. Kila mchezo una sheria zake na ndivyo
ilivyo hata kwenye biashara. Sheria moja wapo ambayo mwandishi anatushirikisha
ni kwamba pale unapotaka kuingia kwenye ushirika wa biashara hakikisha
unamfahamu vyema mshirikia wako kabla ya kushirikiana nae kibiashara. Pia,
mwandishi anatushirikisha kuwa kama unahitaji kukua kibiashara huna budi kuunganisha
nguvu na washirika mbambali japo kabla ya kufanya hivyo kumbuka ni lazima
uwatambue vyema.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link). Nakutakia
mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com
|