Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri.
Ni muda mrefu tangu nimekushirikisha
makala za vitabu ninavyosoma kila wiki hali ambayo ilisababishwa na kushiriki
mafunzo maalumu ya kazi yangu ambayo yaliniweka nje ya mtandao kwa muda.
Pamoja na hayo bado ni nina hali ya
kuendelea kukushirikisha yale ninayojifunza ili kwa pamoja tuendeleze jitihada
za kuboresha maisha yetu. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI kwa
uchambuzi wa kitabu cha wiki hii.
Kujiunga na mtandao huu, KWA KUBONYEZA BONYEZA HAPA
na
kujaza fomu kisha bofya “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu.
Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja
kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “Everything I Know About Sales
Success” kutoka kwa mwandishi Gerhard Gschwandtner. Kupitia kitabu hiki mwandishi
anatushirikisha mbinu muhimu ambazo zimetumiwa na watu mbalimbali waliofanikiwa
kwenye tasnia ya mauzo ya bidhaa/huduma za kampuni zao. Watu hawa wengi wao
walianzia ngazi ya chini na pengine bila kusomea kozi ya mauzo lakini kupitia
nia na dira maalumu walifanikiwa kufikia ngazi za juu kabisa.
Karibu
tujifunze machache kati ya mengi ambayo mwandishi anatushirikisha katika kitabu
hiki:
1. Mwandishi anatushirikisha kuwa
siri kubwa katika mauzo ni kufahamu kuwa unafanikiwa kimauzo pale tu
unapowasaidia watu kupata kile wanachohitaji au kutatua matatizo yao. Kwa ufupi
tunaweza kusema ni kuwaridhisha wateja kwa kupata kile wanachotaka. Na hapa
ndipo mwandishi anatushirikisha kuwa mafanikio ya kimauzo hayapimwi kwa
kuangalia mauzo tu bali kwa kuangalia mahusiano muhusika alionayo na wateja
wake au jamii inayomzunguka kwa ujumla.
2. Taarifa sahihi na kwa wakati
sahihi ni nyenzo muhimu ambayo muuzaji bora anatakiwa kuwa nayo. Nyenzo hii
inahusisha taarifa muhimu za masoko mapya, taarifa za uendeshaji wa
biashara/kampuni, taarifa za teknolojia mpya au taarifa za kiubunifu kwenye
uzalishaji wa bidhaa/huduma mpya. Siri hii imetumiwa na makampuni mengi kutumia
teknolojia mpya au masoko mapya katika nchi zinazoendelea kufikia mafanikio makubwa.
3. Tengeneza timu ya watu wenye
uchu wa kufanikiwa kimauzo. Mwandishi anatushirikisha kuwa mauzo yanategemea
timu ya watu hivyo kama ni kampuni hakikisha unazungukwa na watu wenye uchu wa
kufanikiwa kimauzo. Hii ni pamoja na kuwa na timu ya wafanyakazi ambao ni
waaminifu kwa kampuni ikiwa ni pamoja na kila mmoja kwenye kampuni husika
kumiliki hisa za kampuni. Pale mfanyakazi anapomiliki hisa za kampuni anakuwa
ni sehemu ya wamiliki wa kampuni jambo ambalo litapelekea afanye kazi kwa
weledi ili kufanikisha maendeleo ya kampuni. Kwa ujumla unahitaji kuwa na timu
ya watu ambao wapo tayari kujiongoza katika majukumu yao na kufanya kazi kwa
ubunifu na weledi.
4. Safari ya mafanikio kimauzo
inaanza na maneno ya kukatishwa tamaa kutoka watu/jamii inayokuzunguka.
Mwandishi anatushirikisha kuwa wote waliofanikiwa wamepitia kwenye hali ambayo
kila mmoja wetu ambaye anathubutu kufanikiwa kimauzo. Silaha muhimu ambazo
unatakiwa kuwa nazo ni kufahamu nini unataka kupata na kwa muda gani (lini).
Unahitaji kuchora mstari wako wa mafanikio ya kimauzo na kuanza kuutekeleza
mara moja. Hapa unahitaji kuwa na sifa ya uvumilivu, bidii ya kazi, uchu wa
kusonga/kupata zaidi na kuendelea kwenye imani ya kile unachoamini katika
kufikia ngazi ya mafanikio ya ndoto zako.
5. Dhibiti
kila shilingi inayoingia na kutoka katika biashara yako. Uhai wa biashara
yoyote unategemea namna ambavyo fedha inayoingia na kutoka inavyodhibitiwa. Mwandishi
anatushirikisha kuwa ni lazima kudhibiti fedha zinatoka hasa pale ambapo
tunafanya manununizi/matumizi kwa ajili ya biashara lakini pia kuhakikisha kuwa
fedha inayoingia kwenye biashara kupitia mauzo inakuwa na thamani zaidi ya ile
iliyowekezwa. Kwa ufupi ni kwamba ni lazima uwe tayari kununua na kuuza kwa
faida ikiwa ni pamoja na kudhibiti matumizi yasiyo na mpangilio.
6. Mafanikio
ya mauzo yanaanzia kwenye kuwekeza muda wa kutosha kwa ajili ya maandalizi na
kupanga mipango ya baadae. Ili uuze ni lazima uwe na bidhaa au huduma ambayo
wewe mwenye unaridhika nayo. Mwandishi anatushirikisha kuwa kama unahitaji
kuongeza mauzo ni lazima ujiulize maswali haya: Je kila siku natenga muda kiasi
gani kwa ajili ya kuandaa mauzo ya siku inayofuata? Je kila siku unajiwekea
malengo kwa ajili ya mauzo ya siku husika ikiwa ni pamoja na kuandaa orodha ya
majukumu ya siku husika? na Je una mkakati maalum kwa ajili ya kuwa na
bidhaa/huduma bora zaidi kuliko wapinzani wako kibiashara? Kwa ujumla utagundua
kuwa maswali haya yote yanakuhitaji kuwekeza muda wa kutosha kwa ajili ya
kuboresha biashara yako.
7. Kufanikiwa
kimauzo ni lazima uwe na sifa kuu tatu ambazo ni: shauku ya kufanikiwa; ufahamu
wa watu/jamii unayofanya nayo kazi; na ufahamu wa kutosha juu ya huduma au
bidhaa ambayo unauza. Hizo ni sifa kuu tatu za kufanikiwa kimauzo ambazo
mwandishi anatushirikisha kutoka kwa mwanamafanikio nguli Donald Trump ambaye
kwa sasa ni rais wa Marekani. Jiulize je una shauku na bidhaa/huduma ya
biashara yako?; je upo tayari kubadilisha mfumo wa mauzo kwa kutegemea aina ya
watu unaofanya nao kazi? na Je unaweza kubuni njia mbadala kwa ajili ya
kuboresha bidhaa au huduma yako?.
8. Katika
ulimwengu wa mauzo ni lazima utambue kuwa hakuna njia moja sahihi au ya kipekee
ya kufikia lengo. Kutokana na ukweli huu ni lazima kila siku uwekeze kwenye
kutafuta mawazo mapya kwa ajili ya kuboresha mfumo wako wa mauzo. Kuwa tayari
kufuta mifumo ya zamani ambayo yanaonekana kutokwenda na nyakati. Kwa ujumla
tambua kuwa hakuna njia sahihi au hisiyo sahihi ya kufikia lengo lako la
kimauzo.
9. Kufanikiwa
kimauzo unatakiwa kutambuwa kuwa kukataliwa ni sehemu ya kukujenga na hivyo
kadri unavyokataliwa ndivyo unakua zaidi katika ulimwengu wa mauzo. Hapa
unahitaji kuachana na roho ya kukatishwa tamaa na badala yake wekeza muda wako kusonga
mbele zaidi. Pia, unahitaji kutambua kuwa nyakati ngumu kimauzo hazitakiwi
kukuzuia kuendelea kufikiria kwa mapana zaidi. Fikiria kufanikiwa zaidi,
kufikiria kufanya maamuzi sahihi na fikiria kuwa bora zaidi.
10. Ubunifu wa mara kwa mara ni injini ya
kukuza mauzo katika biashara. Ubunifu huu ni lazima ujikite kwenye uboreshaji
wa bidhaa/huduma zinazotolewa kwa wateja kulingana na nyakati husika. Mwandishi
anatushirikisha kuwa biashara bila ubunifu wa mara kwa mara kamwe haiwezi
kuendelea na badala yake itadumaa siku zote na mwisho wake ni kushuka kwa mauzo.
Hili ni tatizo kubwa ambalo linakumba wafanyabiashara wa kati walio wengi
katika mazingira yanayotuzunguka.
11. Mara zote katika biashara lenga
kuzalisha/kuendesha biashara kwa gharama ya chini ili uingie sokoni kwa bei nafuu.
Hata hivyo, pamoja na kuzalisha au kujiendesha kwa gharama nafuu unatakiwa
kulinda ubora wa bidhaa/huduma zako. Mwandishi anatushirikisha kuwa kadri
unavyozalisha kwa gharama nafuu ndivyo unavyomfikia mteja kwa gharama ambazo
hazimuumizi sana. Na hii ni nyenzo muhimu ya kuwashinda wapinzani wako
kibiashara.
12. Kuwa na utamaduni wa kusikiliza
mrejesho wa wateja dhidi ya bidhaa au huduma zako. Mwandishi anatushirikisha
kuwa mauzo hayaishii pale unapouza bidhaa/huduma yako kwa mteja bali pale mteja
anaporidhika na bidhaa/huduma yako. Lazima uwe tayari kutenga gharama kwa ajili
ya kurekebisha au kubadilisha bidhaa ambazo zimeingizwa sokoni zikiwa chini ya
ubora. Hii ni pamoja na kuweka muda wa uhakika (warranty/guarantee) kwa mteja
kutumia bidhaa kwa kipindi flani pasipo kupata hitilafu yoyote ya kiufundi. Pia,
unaweza kuweka utaratibu wa huduma ya simu ya bure kwa wateja ili kupata
mrejesho wao dhidi ya bidhaa/huduma zako.
13. Kama mtendaji mkuu wa biashara au
kampuni yako, kazi kubwa ulionayo ni kuhakikisha unaonesha mwelekeo wa malengo
ya kampuni au biashara husika. Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa kila mmoja ndani
ya timu yako anafahamu mwelekeo wako na hatimaye hakikisha kuwa wote wanafanya
kazi kufikia mwelekeo husika.
14. Hizi ni baadhi ya sifa za kufanikiwa
kimauzo ambazo mwandishi anatushirikisha kutoka kwa mwanamafanikio Arnold Schwarzenegger:
Kwanza kabisa ni lazima uchore mstari wako wa mafanikio – tambua ni wapi
unataka kufikia kimafanikio; mbili, kataa kila aina ya vikwazo – kuwa na imani
hisiyo kuwa na chembe ya shaka juu ya ndoto yako ya mafanikio na hivyo kuwa
tayari kukataa kila aina ya vikwazo mbele ya safari yako; tatu, lenga kuwa bora
kuliko wote katika kile ambacho umekusudia kufanya; nne, kumbuka ni lazima
kujitoa kwa nguvu zako zote – husitegemee vitu kutokea kama muujiza bali ni
lazima ujione kuwa wewe ndio mhusika mkuu wa kufanya miujiza hiyo itokee; tano,
husikubali k ushindwa – tambua kuwa kuna kupanda na kushuka katika safari yako hivyo
mara zote nyakati za kushuka zikufundishe kitu kwa ajili kupanda juu zaidi; sita,
tumia ushawishi/kukubalika kwako ajili ya kwenda hatua ya ziada – Arnold baada
ya kuona amefanikiwa kwenye tasnia ya filamu alihamia kwenye siasa ambako nako
alifanikiwa kuchaguliwa kama Gavana wa California; na mwisho waoneshe watu kuwa
kila unapoweka malengo ya juu huwa unayafikia kupitia matendo yako.
15. Kufanikiwa kimauzo ni lazima uwe tayari
kudhibiti hisia zako. Kumbuka kuwa tasnia ya mauzo inakuunganisha na watu
mbalimbali tena wenye mitazamo taofauti. Katika kila hali ni lazima ukubali
kuruhusu mantiki (logic) itumike badala ya hisia (feelings) katika kila maamuzi
unayofanya. Unahitaji kujifunza kusikiliza zaidi kuliko kuwa mzungumzaji mkuu –
kuwa tayari kuhimili hisia za wateja/jamii inayokuzunguka tena kwa busara na
hekima ya hali ya juu.
16. Kuongeza idadi ya mteja ni lazima
uhakikishe kila mtu unamchukulia kama mteja tarajiwa wa bidhaa/huduma zako. Mwandishi
anatushirikisha kuwa kila unapokutana na watu wapya katika maisha hakikisha
unaongea nao kana kwamba unaongea na wateja wako au wateja tarajiwa. Hapa unahitaji
kuwa na nyuso za furaha na tabasamu kila mara unapokutana na watu wapya.
17. Kumbuka kurejesha kwenye jamii. Mwandishi
anatushirikisha kurudhisha kwenye jamii ni sehemu ya kukua kimauzo kutokana na
ukweli kwamba kadri unavyojiweka karibu na jamii ndivyo biashara zako
zinavyopendwa zaidi. Hapa unahitaji kutenga sehemu ya faida yako kwa ajili
kuwekeza kwenye shughuli za kijamii. Tenga sehemu ya faida yako kwa ajili ya
wahitaji katika jamii kama vile watoto yatima, wajane na wazee wenye mahitaji
maalumu.
18. Mafanikio kwenye mauzo bila kusahau
yanatokana na kuwa na timu bora ya wanyakazi na wewe kama Mtendaji Mkuu
unatakiwa kuhakikisha watu hawa wanapewa malipo na marupurupu ya kutosha. Mwandishi
anatushirikisha kuwa kadri unavyopanuka kibiashara ndivyo watu wanaokuzunguka
kiutendaji wanatakiwa kupanuka kwenye vipato vyao. Hali hii itakusaidia kuwa na
wafanyakazi ambao wana morali ya kazi.
19. Kufanikiwa kimauzo unahitaji kuhimili
figusufigisu au fitina kutoka kwa wapinzani wako wakubwa. Kuna fitina ambazo
kama haupo imara zinaweza kukutoa kabisa kwenye ulimwengu wa biashara. Unahitaji
kuwa imara katika kukabiliana na fitina hizo na pengine pale ambapo umetolewa
nje ya mstari na wapinzani wako kibiashara inabidi uwe tayari kulipanga upya
jeshi lako kwa ajili ya mapambano mapya katika soko.
20. Kuwa na uelewa mpana wa bidhaa/huduma
yako na jiandae vya kutosha pale ambapo una mikutano ya kuwashawishi wateja
tarajiwa kufanya biashara na wewe. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wengi
wanakataliwa kukubaliwa kutokana na kukosa maandalizi ya kutosha juu ya kile
ambacho wanakusudia kuuwauzia wateja tarajiwa. Njia pekee ya kufanikiwa kwenye
eneo hili ni kuwa na uelewa wa kutosha kwenye bidhaa/huduma yako kuliko mteja
unayemshawishi. Husikubali mteja tarajiwa afahamu bidhaa/huduma husika kuliko
wewe kwani kufanya hivyo ni hatua ya kwanza kwako kufeli.
21. Tangeneza mpango mzuri wa kuzalisha,
kufunga, kusambaza, kutangaza na kuuza bidhaa/huduma zako. Ngazi zote hizi
katika uzalishaji zinahitaji ubunifu ambao umejikita kwenye kupunguza gharama
za uzalishaji au uendeshaji. Hata hivyo, katika ngazi zote unatakiwa kukumbuka
kuwa jambo la muhimu ni mteja aridhike na huduma au bidhaa zako. Na hapa
unahitaji kuhakikisha unatimiza ahadi kwa mteja ndani ya muda husika.
22. Hakikisha fanikio moja linazaa
mafanikio zaidi kwa ajili ya kufikia malengo mapana zaidi. Mwandishi anatushirikisha
kuwa kadiri unavyofanikiwa ndivyo sifa zako zinavyojitangaza zaidi na hivyo
kufanya mafanikio yakufuate zaidi. Kumbuka pale unapotengeneza jina kuna
gharama za kuhakikisha unalinda jina lako kibiashara zaidi.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link). Nakutakia
mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com
|