Mambo Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha Screw It, Let’s Do It: Lessons in Life (Nadharia ya Mafundisho ya Maisha Kupitia Kuthubutu)

Habari ya leo rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea vizuri na mapambano ya kuyaboresha maisha yako yanendelea. Wiki hii ikiwa ni wiki ya kumi na nne tokea nianze kukushirikisha uchambuzi wa kitabu kimoja kila wiki ni matarajio yangu kuwa uchambuzi wa vitabu hivi umekusaidia kubadilisha maisha yako kwa kiasi flani. 

Kama mpaka sasa haujafanikiwa kujifunza kitu chochote katika makala hizi za uchambuzi wa vitabu nakushauri husiendelee kupoteza muda wako na badala yake ufanye mambo ambayo umeyazoea. Lengo kuu la mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI ni kuona unakubadilisha wewe kifikra na hatimaye kivitendo kupitia usomaji wa vitabu na makala mbalimbali.

Kujiunga na mtandao wa fikra za kitajiri BONYEZA HAPA na ujaze fomu ili uendelee kunufaika na makala za mtandao wa fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala za mtandao wa fikra za kitajiri moja kwa moja kwenye barua pepe yako.

Kitabu cha wiki hii ni “Screw It, Let’s Do It” kutoka kwa mwandishi Richard Branson. Richard Branson ni miongoni mwa wanamafanikio ambao wameishi maisha ya kutokuridhika na jinsi maisha yalivyo badala amekuwa mtu wa kuhakikisha kila siku anafikiri na kujipa changamoto kwa ajili ya kufanikisha ndoto zake.

Katika kitabu hiki mwandishi anatushirikisha siri ambazo amekuwa akitumia yeye mwenyewe kwenye maisha yake kwa ajili ya mafanikio makubwa aliyonayo. Siri hizi zipo wazi na zinaweza kufanya kazi kwa kila mmoja ambaye yupo tayari kuzitumia kwa ajili ya kutimiza ndoto zake.

Karibu tujifunze wote machache niliyojifunza kutoka kwenye kitabu hiki:

1. Mwanzo ni hatua muhimu ya kutekeleza kazi yoyote kwa ufasaha. Hauwezi kufikia hatua kumi kama bado haujaanzisha hatua ya kwanza. Kwa maana hii hatua ya kwanza ni muhimu sana kwani hatua nyingine zote zinategemea hatua hii. Mwandishi anatushirikisha umuhimu wa kuanza kutekeleza mara moja kitu unachowaza pasipo kuogopa changamoto ambazo unaziona mbele yako.


2. Siku zote kubali kuwa HAPANA haimaanishi kuwa HAIWEZEKANI. Jifunze kutumia neon hapana kwa ajili ya kutafuta njia mbadala za kufanikisha yale ambayo watu wengi wanadhania kuwa hayatekelezeki. Fikria nje ya boksi kwa ajili ya kufanikisha ndoto zako na muda wote hakikisha hautumii mfumo uliopo kama kigezo cha kusingizia kushindwa kusonga mbele.

3. Tengeneza lengo kubwa na tafuta kila njia kwa ajili ya kutimiza lengo hilo. Mwandishi anatushirikisha kuwa mara zote ni vyema kuwa na lengo kubwa ambalo pengine hata wewe mwenyewe linakuogopesha na hatimaye anza mara moja kutekeleza lengo lako hatua kwa hatua. Daima husikubali kushindwa kusonga mbele kwa visingizio vya changamoto kwani changamoto zipo kwa ajili ya kupata fundisho la kusonga mbele zaidi. Mara zote zifanye changamoto kuwa sababu ya kukufanya uendelee kusonga mbele mpaka pale utakapofanikiwa.

4. Tumia kanuni ya kuanza kidogo na hatimaye tanuka zaidi. Mara nyingi watu wengi wameshindwa kutekeleza ndoto zao kwa vile wanawaza kuanzia katika viwango vya juu zaidi na kudharau kuthamini kanuni ya kuanza na kidogo. Ni lazima tutambue kuwa hakuna mafanikio ambayo yanakuja kwa muda wa siku moja kwani mafanikio yanatengenezwa katika tukio la maisha yako. Kwa kifupi mafanikio yako ni majumuisho ya fikra na matendo yako yote katika muda wa kipindi chote cha maisha yako.

5. Siri pikee ya kuwa na mafanikio ya kila aina ni kujiamini kuwa unaweza na kufanya kazi kwa bidii. Ushindi wa kila aina unaanzia kwenye nafsi ya mhusika kwa maana ya kwamba ni lazima muhusika ajione mshindi na ndipo mafanikio mengine yanafuata. Baada ya kujiamini katika nafsi yako kuwa unaweza kitu chochote ni lazima uwe tayari kutoa sadaka ambayo si nyingine bali ni jitihada za kuweka bidii ya akili na mwili kuhakikisha kuwa unafikia lengo lako.

6. Fanya kazi ambayo inakupa furaha na amani rohoni. Daima katika ulimwengu wa mafanikio husifanye makosa ya kwamba utaishi maisha yenye furaha na amani pindi ukiwa na mafanikio. Mara nyingi watu wa aina hii wanajikuta kwenye maisha ya msongo wa mawazo pamoja na kwamba wana kila aina ya mafanikio ya ndoto zao. Mwandishi anatushirikisha kuwa ni muhimu kuishi maisha yenye ukamilifu wa furaha na amani kila siku ya maisha yako. Ukifanikiwa maisha ya namna hii ni wazi kuwa pesa zitakufuata kwenye yale unayofanya.

7. Kuwa macho muda wote kwa ajili ya kuona fursa mpya. Mwandishi anatushirikisha kuwa kila sehemu unayotembelea hakikisha unatafuta fursa mpya kwa ajili ya kutimiza ndoto zako. Kufanikisha zoezi hili ni muhimu kuhakikisha unatembea na kijitabu kidogo kwa ajili kuorodhesha fursa mpya. Pia, unatakiwa kutumia kijitabu hicho kwa ajili ya kuandika mawazo mazuri yanaojengeka akilini mwako.

8. Tumia hobi (interest) yako kufikia mafanikio makubwa sana. Kama una hobi ya musiki unaweza tumia hobi hiyo kwa ajili ya kufikia mafanikio makubwa kwenye ulimwengu wa musiki. Kama hobi yako ni mapishi vilevile unaweza tumia hobi hiyo kwa ajili ya kufikia mafanikio makubwa sana kwenye ulimwengu wa mapishi. Kwa ujumla tumia hobi yako kufanya vitu ambavyo vinakupa uhakika wa furaha maishani mwako.

9. Epuka michezo ya kamari na badala kuwa tayari kubeba hatari yenye makadirio ya kimahesabu (calculated risk). Mara zote uwekezaji ni sawa na kamari japo uzuri wa kamari hii ikilinganishwa na nyingine yenyewe ni rahisi kutabiri ushindi wako. Ili ufanikiwe zaidi ni lazima uwe tayari kufahamu upana wa hatari (risk) katika eneo unaloenda kuwekeza na hatimaye wekeza muda/fedha zako kwa kuongozwa na taarifa sahihi.

10. Simama imara katika yale unayofanya bila kuruhusu kuondolewa kwenye biashara kutokana na fitina za wapinzani wako. Mwandishi anatushirikisha jinsi ambavyo alifanikiwa kuanzisha kampuni imara ya usafiri wa anga japo mwanzoni alikumbana na fitina za mpinzani wake mkubwa British Air Ways.

11. Mara nyingi watu wa karibu yako watakuambiwa kuwa sio rahisi kufanikiwa katika yale ambayo utawashirikisha kuwa unakusudia kufanya. Mwandishi anatushirikisha kuwa ili ufanikiwe ni lazima uwe tayari kufahamu kwa kina juu ya uwekezaji unaokusudia kuanzisha na baada ya kujiridhisha kuwa faida ni kubwa kuliko hasara anza mara moja pasipo kuruhusu maneno ya watu.

12. Timiza ahadi yako kwa kadri unavyoweza. Ukiahidi hakikisha unatekeleza tena pengine zaidi ya kile ulichoahidi. Hii ni siri kubwa ambayo itakutambulisha kwa watu wengi hatimaye kufanikiwa kupata wateja wengi kwenye biashara/huduma zako. Njia pekee ya kufanikiwa katika siri hii ni kuhakikisha muda wote unafahamu lengo kubwa katika kile ulichoahidi.

13. Kumbuka kuwa kuna wakati utashinda na kuna wakati utashindwa. Unaposhinda shukuru kwa hatua hiyo na pale unaposhindwa chukulia kama sehemu ya kujifunza badala ya kuhuzunika. Pia, hapa tunashirikishwa umuhimu wa kutoangalia historia ya nyuma kwa manunguniko na badala yake tutumie matukio yetu ya nyuma kama sehemu ya kujifunza kuboresha zaidi katika siku zijazo.

14. Muda wote jipe changamoto za kimafanikio. Kadri unavyojipa changamoto na kuzifanyia kazi ndivyo unavyozidi kukua zaidi kimafanikio. Husikubali kukaa na kuridhika na hali iliyopo na badala yake pigana sana kwa ajili ya kutatua changamoto zilizopo mbele yako.

15. Njia mbili za changamoto unazotakiwa kuwa nazo moja ni kutumia bidii zako zote kwa ajili ya kufanya kazi zako na mbili ni kuangalia fursa mpya kila sehemu unapokuwa. Fanya kazi kwa bidii kama sehemu ya starehe yako na pale unapokuwa kwenye sehemu za mapumziko au safari tumia nafasi hiyo kuangalia fursa mpya ambazo hazijafanyiwa kazi katika sehemu husika.

16. Unaweza kufanikiwa katika jambo lolote lile endapo utaweka juhudi za kutosha. Mafanikio katika jambo lolote ni lazima yatanguliwe shauku pamoja na juhudi binafsi zinalolenga kufanikisha jambo husika. Ili ufanikiwe ni lazima kwanza uwe na shauku yenye nia thabiti na baada ya hapo weka jitihada za kuhakikisha unafanikisha jambo husika.

17. Mafanikio yanaanzia kwenye nafsi yako. Kama unajiamini kuwa unaweza kufanikiwa daima hakuna wa kukuzuia kufikia ndoto zako. Hata hivyo ni lazima utambue kuwa mafanikio ya aina yoyote ile wewe ndo muhusika mkuu wa kuyafanikisha. Hii ni kutokana na ukweli kwamba hakuna muujiza wala njia ya mkato bali mafanikio yanaandaliwa katika kila tukio la maisha yako.

18. Zungumza maendeleo ya miradi yako mbele ya wanafamilia wote ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha watoto wako yale unayofanya. Biashara nyingi hasa kwa Afrika huwa ni zinaendeshwa na mtu mmoja hasa baba. Katika mazingira kama haya unakuta mama na watoto hawajui namna ambavyo biashara inaendeshwa na matokeo yake inapotekea baba hayupo biashara inakufa moja kwa moja. Hivyo ni muhimu kuwakuza watoto wako katika misingi ambayo hata kama wewe haupo biashara hisiyumbe.

19. Ishi maisha ya sasa. Mwandishi anatushirikisha umuhimu wa kuisha maisha yasiyokuwa na manunguniko ya makosa yaliyofanyika siku za nyuma wala maishaa yenye hofu ya maisha yajayo. Kuishi maisha yenye manunguniko na hofu ya maisha ya baadae ni chanzo kikubwa kutofanikiwa kwa yale unayofanya. Pia, maisha ya namna hiyo kamwe hayawezi kuwa maisha yenye furaha.

20. Ithamini familia yako pamoja na washirika wako wa kibiashara bila kusahau wafanyakazi wako. Kila aina ya mafanikio uliyonayo ni lazima utambue kuwa umefikia hatua hiyo kutokana na mchango wa watu wengine. Hakikisha kila mmoja kwenye timu unampa thamani sawa ili uendelee kunufaika na mchango wake.

Haya machache ambayo niweza kukushirikisha kati ya mengi niliyojifunza kutoka kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.

Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.

Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.

Born to Win ~ Dream Big 

Augustine Mathias Bilondwa

Namba ya Simu:      +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com


onclick='window.open(