Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri.
Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa
FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa
ni wiki ya 7 katika kipindi cha mwaka 2018 naendelea kukushirikisha uchambuzi
wa vitabu vyenye mafundisho tofauti katika kila sekta ya maisha yako.
Makala hizi za uchambuzi wa vitabu
zimekuwa zikikufikia kila wiki kwa kadri ambavyo napata muda wa kukushirikisha
kile ninachojifunza kutoka kwenye vitabu hivi. Ni matarajio yangu kuwa muda
ninaotumia kukushirikisha uchambuzi wa vitabu umekuwa wa msaada mkubwa kwako
katika kubadilisha maisha yako.
Unaweza kujiunga na mtandao huu, KWA KUBONYEZA BONYEZA HAPA
na
kujaza fomu kisha bofya “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu.
Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja
kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “Winning the Loser’s Game” kutoka kwa mwandishi Charles D. Ellis.
Mwandishi huyu ametumia kitabu kutushirikisha mbinu mbalimbali ambazo
zinatumiwa na wawekezaji wakubwa kufanikiwa kiuwekezaji. Mwandishi anasisitiza kuwa
katika uwekezaji ni muhimu mwekezaji kuwa msimamizi mkuu na kuhakikisha anafuatilia
kila aina uwekezaji alionao. Hii ni pamoja na kufikiri na kuchukua hatua za
kivitendo kwenye kila za uwekezaji ulizonazo. Epuka sana kutegemea mawazo ya
washauri katika uwekezaji kwani mara nyingi wengi wao hawana uzoefu juu ya kile
wanachoshauri.
Katika
uwekezaji kuna aina makundi mawili ya wawekezaji, kundi la kwanza ni wawekezaji
ambao kwa namba ni wachache lakini wako macho katika kuhakikisha wanaboresha
masoko. Hawa ndio wanafanya vitu vinaonekana kwenye soko kwani wapo tayari
kuwekeza muda na akili kwa ajili ya ubunifu mpya katika soko. Kundi la pili ni
wawekezaji ambao kwa namba ni wengi sana lakini hawajishughulishi kutengeneza
mazingira ya soko la uwekezaji. Hawa hawawekezi kwenye rasimali au elimu kwa
ajili ya kuboresha mazingira ya soko bali wanategemea kutumia mazingira
yaliyopo kwenye soko husika.
Karibu
tujifunze machache kati ya mengi ambayo mwandishi anatushirikisha katika kitabu
hiki:
1. Katika uwekezaji wa aina yoyote
kinachoamua ushindi ni matendo sahihi ya mwekezaji na kinachoamua kushindwa ni maamuzi
ya kimakosa yanayofanywa na mwekezaji. Kutokana na ukweli huu tunajifunza kuwa kwenye
kila aina ya uwekezaji ili ushinde ni lazima uwe na ufahamu sahihi. Hivyo kwenye
uwekezaji kuna waliobobea na hawa ndio wanapata pointi za ushindi ikinganishwa
na wale wanaosindikiza.
2. Kwenye uwekezaji ni muhimu
kutambua kuwa mbinu za ushindi zinabadilika kulingana na nyakati. Hapa tunajifunza
kuwa ili tufanikiwe kiuwekezaji ni muhimu kuboresha mbinu zetu kulingana na
nyakati zilizopo. Mwandishi anatushirikisha kuwa wengi wanashindwa kupata
mafanikio kwenye soko kwa kuwa wanaendelea kutumia mbinu zilizopitwa na wakati.
3. Katika mchezo wa fedha ni
lazima utambue kuwa ushindi unachangiwa na namna ambavyo unapoteza fedha kidogo
kwenye soko na hivyo kubakiza sehemu kubwa ya fedha kama ushindi wako. Hii ni
kanuni ambayo inatumika kuamua ushindi kwenye mchezo wowote ule. Mfano, mshindi
wa tenisi anapatika kulingana na pointi nyingi anazokusanya ikilinganishwa na
zile anazopoteza.
4. Katika
mchezo wa uwekezaji/fedha mara zote unahitaji kuhakikisha unamridhisha mteja. Hii
ni kutokana na ukweli kwamba mteja anaporidhika wewe kama mwekezaji unapata
uhakika wa kuwekeza zaidi. Wateja ni njia pekee ambayo itaendelea kukuweka
sokoni endapo umetekeleza mahitaji muhimu ya uwekezaji.
5. Soko
la uwekezaji hasa uwekezaji wa hisa limepitia kwenye mabadiliko makubwa ambayo
kwa ujumla wake yanatofautisha wawekezaji kwenye soko. Wawekezaji ambao wameendelea
kuwekeza kwa kutumia mbinu zile zile wameendelea kupotea kwenye soko kwa kasi
kubwa kuliko wale ambao wanabadilisha mbinu kulingana na mabadiliko yaliyopo. Muhimu
ni kuwa na taarifa sahihi kuhusu soko kila wakati.
6. Wawekezaji
wote wana sifa zinazofanana kama vile kuhitaji kufanya vyema kwenye soko
(kutengeneza faida). Sifa hii ndio inamfanya kila mwekezaji kuwa na uhuru wa
kuchagua wapi awekeze fedha zake katika soko. Hata hivyo, kinachotofautisha
wawekezaji hawa katika soko ni pamoja na: rasilimali wanazomiliki, mitaji,
majukumu ya matumizi, elimu ya biashara, uwezo wa kuvumilia hatari za uwekezaji
na uzoefu wa soko. Tofauti hizi ndizo zinaonesha kuwa wawekezaji hawa ili
wafanye vyema kwenye soko ni lazima pawepo msaada wa kielimu au mawazo.
7. Njia
pekee ya wawekezaji makini kuendelea kufanya vyema kwenye soko ni kutumia
makosa yanayofanywa na wawekezaji makini wa ngazi zao. Mwandishi
anatushirikisha kuwa katika uwekezaji kosa moja kwa mwekezaji ni baraka kwa
mpinzani wake wa karibu. Njia hii imekuwa ikiamua mwenendo wa makampuni katika
soko, hivyo, kama mwekezaji unahitaji kufahamu mbinu hii ili kuepuka makosa ya kiuwekezaji
lakini pia kuitumia kwa ajili ya kufaidi makosa ya wawekezaji wengine.
8. Ili
kuepuka makosa ya kiuwekezaji kwenye soko ni lazima ujitoe kufanya kazi kwa
bidii kwa ajili ya kulifahamu soko, kuwa na taarifa sahihi na elimu sahihi ya
soko husika. Njia hizi ndizo zinatumiwa na wawekezaji makini kwa ajili ya
kuepuka makosa ya kiuwekezaji. Mfano, katika uwekezaji wa hisa unahitaji
kulifahamu soko kwa nyakati husika, kuchagua hisa sahihi kwa wakati husika na
kufahamu ni lini mabadiliko na yanaweza kutokea kwenye soko na hivyo yakaathiri
thamani za hisa. Mwekezaji ambaye amefanikisha kufahamu yote haya ni rahisi
kwake kufanya vyema kwenye soko kwani ana uwezo wa kununua hisa pale ambapo thamani
hisa imeshuka (wakati ambao kila mtu anauza) na kuuza hisa zake pale ambapo
thamani ya hisa imepanda (wakati ambao kila mtu ananunua).
9. Njia
nyingine ya kufanya vyema kwenye soko la hisa ni kuwa uelewa wa kina hisa za makampuni
yaliyoorodheshwa kwenye soko la hisa. Mwandishi
anatushirikisha kuwa wawekezaji makini wanachagua hisa ambazo thamani ya beiza
hisa iliyotangazwa kwenye soko ni ya chini kuliko thamani halisi ya hisa
husika. Na hii ndio inaamua nyakati zipi wawekezaji makini wanunue au kuuza
hisa wanazomiliki.
10. Wawekezaji makini ni wale ambao mara
zote wanatafuta fursa mpya za kiuwekezaji. Wawekezaji hawa mara zote wanaandaa
njia kwa ajili ya wengine kufuata njia husika na wanaacha njia hii pale ambapo
kila mtu ameingia kwenye njia husika. Hii ni kutokana na ukweli kwamba nyakati ambazo
kila mtu anatumia njia husika ni nyakati ambazo soko limefurika na hivyo faida
inakuwa ni ndogo matokeo yake mwekezaji makini anatakiwa kutafuta njia mpya.
11. Kama mwekezaji unahitaji kufahamu nguvu
za soko na thamani ya vitu/bidhaa katika soko. Mwandishi anatushirikisha kuwa
soko mara zote lina kelele nyingi ambazo upelekea mabadiliko ya thamani ya
bidhaa/kampuni kwa nyakati tofauti. Mabadiliko haya mara nyingi yanasababishwa
na taarifa za uongo na hivyo yanapelekea kupanda na kushuka kwa thamani/bei ya
bidhaa. Kama mwekezaji makini hautakiwi kuendeshwa na miemko/kelele za soko ambazo
mara nyingi huwa ni za muda mfupi bali unatakiwa kujikita kwenye malengo/sera
ya uzalishaji/uwekezaji wa muda mrefu wa kampuni yako.
12. Mara nyingi katika kukabiliana na
kelele za soko wawekezaji makini wanatumia mantiki (logic) badala ya kuongozwa
na hisia. Mwandishi anatushirikisha kuwa kinachosababisha mabadiliko makubwa
kwenye soko ndani ya muda mfupi ni kutokana na soko kutawaliwa na wawekezaji
wasio makini. Wawekezaji hawa wanaongozwa na hisia ambazo zinawafanya wapaniki kutokana
na hofu ya kupoteza kile walichowekeza. Hali hii inawafanya wauze kwa haraka au
kununua kwa pupa na matokeo yake ni kushuka/kupanda kwa thamani ya bidhaa/hisa.
13. Kama ilivyo michezo mingine, mchezo wa
uwekezaji nao pia unaundwa na timu yenye watu mbalimbali na timu hii ndio inaamua
ushindi au kukosa ushindi. Mwandishi anatusirikisha kuwa uwekezaji mitaji
unahitaji timu makini kwa ajili ya kuamua ushindi wa wawekezaji. Hii inaanzia
kwa wamiliki wa soko kama taasisi inayoendesha soko, mfano, kwa hapa Tanzania Dar
es salaam Stock Exchange (DSE) ni lazima soko liwe na wataalamu wa kila kada
zote za fedha za uchumi kwa ajili ya kufanikisha ukuaji wa soko husika.
14. Katika kuwekeza unahitaji kuwa makini
na hatari za uwekezaji. Hii ni pamoja na uhakika wa kulinda mtaji wako kutokana
na ukweli kwamba kuna nyakati ambazo unaweza kujikuta unapoteza kila kitu
ulichowekeza. Hali inatokea pale ambapo kuna mabadiliko ya kudumu katika soko
ambayo mara nyingi yanapelekea upotevu wa thamani ya bidha/hisa kiasi ambacho
thamani haiwezi kurudi kwenye hali yake soko. Inapotokea hali kama hii unaweza
kujikuta unaharibu maisha yako yote kiuwekezaji na kiroho pia.
15. Mojawapo ya makosa yanayopelekea
wawekezaji kuangukia kwenye shimo la upotevu wa pesa ni hali ya kujiamini kuwa
wanafahamu zaidi kuliko watu wengine katika soko husika. Hali inapelekea wengi
kuwekeza mitaji yao kwa kuongozwa na taarifa ambazo hazina uhalisia wa soko. Hali
hii pia inachangiwa na tabia kukimbilia matokeo ya muda mfupi ambayo
kiuwekezaji hayana tija.
16. Uvumilivu ni njia mojawapo ya
kukuwezesha kudumu katika soko. Mwandishi anatushirikisha kuwa wawekezaji
makini mara nyingi katika kuepuka miemko ta soko mara nyingi wanajitahidi kuwa
wavumilivu kwa ajili ya kusubilia mapito ya upo wa soko. Kama sio mvumilivu
unaweza kujikuta unapoteza mtaji ambao umekusanywa kwa kipindi kirefu na
kujikuta unaanza upya.
17. Hatari za uwekezaji zinaweza kuepukwa
kwa; kupunguza makosa ya kiuwekezaji hasa yanayosababishwa na miemko ya hisia, kuwa
na malengo ya uwekezaji ambayo mwekezaji ameweka mwenyewe, kuwa na mkakati wa
uwekezaji unaotekeleza katika kipindi cha muda mrefu (long term investment strategy)
na kuendelea kujikita kwenye mpango wako wa muda mrefu bila kujali kelele za
soko ambazo mara nyingi zinasabishwa na watu kuwa na hofu ya kutopoteza au tamaa
ya kupata zaidi katika soko husika.
18. Mafanikio yako kama mwekezaji yanatemea
nguvu yako kwenye elimu ya uwekezaji na uwezo wa kudhibiti hisia zako. Katika uwezo
wa kielimu tunaangalia uwezo wako wa kudhibiti fedha (zinazoingia na kutoka),
uwezo wako wa kutumia taarifa zilizopo kuhusu soko, na uwezo wa kuchambua hisa
za makampuni mbalimbali kwa ajili ya kuchagua hisa sahihi. Katika upande wa
hisia tunaangalia uwezo wa kuwa mtulivu na imara hasa nyakati ambazo kuna
kelele nyingi katika soko.
19. Mchezo wa uwekezaji hasa kwenye masoko
ya mitaji kama hisa, hatifungamani, dhamana au mifuko ya pamoja ni mchezo ambao
kila mshiriki (mwekezaji) ana nafasi sawa ya kushinda. Siri ya kwanza katika
kushinda kwenye uwekezaji wa mitaji ni kuepuka kupelekeshwa na miemko/kelele za
soko. Siri ya pili ni kila mwekezaji kwa utashi wake kuandaa sera ya uwekezaji
ambayo anaona inamfaa kwa ajili ya kutumia sera hiyo kukamilisha malengo ya uwekezaji
wa muda mfupi na muda mrefu.
20. Uwekezaji wa aina yoyote ile ni lazima
uwe na msingi imara kama ilivyo kwenye uhandisi ujenzi. Kwenye uwekezaji pia
mwanzoni ni lazima ujiulize kama yale unayofanya kwa sasa yanatosha kukupa
msingi imara kwa ajili ya miaka 10, 20, au 30 ijayo. Kama umejiweka sawa
kiuwekezaji kwa sasa ni rahisi sana kufanikiwa kiuwekezaji katika miaka ijayo.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link). Nakutakia
mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com
|