Habari ya leo rafiki na
msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Rafiki nakupongeza kwa kumaliza mwaka
2017 salama na hatimaye umefanikiwa kuuanza mwaka 2018 ukiwa na hamasa kubwa
kwa ajili ya kufikia mafanikio ya ndoto yako.
Kama ambavyo wengi wetu
tumezoea kuanza mwaka mpya kwa hamasa huku tukiwa na malengo mengi ya
kukamilisha; nina imani kuwa na wewe kwa sasa una hamasa kama hiyo kwa ajili ya
kuendelea kufanyia kazi malengo ya ndoto zako katika kipindi cha mwaka 2018.
Mara nyingi watu wamekuwa
wanaanza mwaka kwa kuweka malengo mengi lakini kadri siku zinavyosogea wengi
wanasahau malengo waliyojiwekea na hatimaye wanaanza kuishi maisha yale yale.
Tunapouanza mwaka 2018
ningependa nikushirikishe machache ambayo nilijifunza kutokana na malengo
niliyokusudia kufanya katika kipindi chote cha mwaka 2017.
Kabla
ya kukushirikisha niliyojifunza mwaka 2017, kwanza niombe radhi kwa kutokuwa
hewani kwa kipindi chote cha mwezi wa Desemba, 2017. Hali hii ilitokana na kazi
zangu ambazo zilinifanya niwe field kwa wiki mbili kabla ya kwenda likizo
kijijini kwa wiki mbili. Katika kipindi hiki chote nilikuwa kwenye maeneo
ambayo mtandao wa internet na umeme vilikuwa shida kiasi ambacho sikuweza
kusoma vitabu na kuwashirikisha kwenye mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com kama
ambavyo nilikuwa nafanya hapo awali.
Karibu nikushirikishe
machache;
1. Mafanikio
yanaanzia kwenye fikra. Mwaka 2017 nilijifunza kuwa kila jambo
ambalo unahitaji kulifanikisha ni lazima kwanza ubadilishe fikra zako. Hakuna
changamoto hata moja ambayo itakuzuia kufikia mafanikio unayohitaji. Mfano,
nilianza mwaka 2017 nikiwa na hasara ya 1.8m kama mkopo ambao hata hivyo
sikufanikiwa kuupokea kwani mtumaji aliibiwa akiwa benki wakati anajiandaa
kunitumia. Baada ya tukio hili nilijikuta nikiwa kwenye nguvu kubwa kifikra
kiasi ambacho nilijiapiza kuwa zilizoibiwa ni fedha lakini bado nina nguvu na
afya kwa ajili ya kutengeneza fedha zaidi kuliko fedha ambazo nimewahi
kutengeneza katika kipindi cha maisha yangu. Namshukuru Mungu kuwa kauli hii
ilinipa nguvu zaidi kipindi cha mwaka 2017 huku nikifanikisha malengo mengi
ambayo nilijiwekea kwa upande wa sekta ya fedha kuliko miaka yote iliyopita.
2. Unapoamua
kufanya jambo, lifanye ndani ya muda muafaka. Mwaka 2017
nimejifunza kufanya jambo kwa wakati bila kujali maandalizi yaliyopo. Kila fursa ina wakati wake na kamwe
hakuna siku ambayo utasema kuwa sasa najitoshereza kwa kila kitu. Hivyo
unahitaji kuanza mara moja kwa kutumia kile ulichonacho kwa wakati huo. Baada
ya kuibiwa fedha nilizotaja hapo juu, kwa haraka nilifanya tathimini ya nini
nifanye kwa ajili ya kutimiza lengo lililokusudiwa na ndipo nikagundua kuwa
naweza kutumia akiba yangu niliyokuwa nimekusanya kupitia uwekezaji wa vipande
vya Mfuko wa Umoja (UTT). Kwa kufanya hivi nilifanikiwa kununua biashara
niliyokusudia kwa kutumia fedha zangu tofauti na awali nilivyopanga kukopa
fedha kutoka kwenye microfinance kupitia kwa rafiki yangu.
3. Hakuna
changamoto ambayo haina mlango wa kutokea. Katika kipindi chote
cha mwaka 2017 nimekumbana na chanagamoto ambazo pengine kama ningekuwa ni mtu
wa kukata tamaa ningenyosha mikono. Changamoto hizi zilijumuisha fitna kutoka
kwa wapinzani wangu wa kibiashara, changamoto za wasaidizi wangu wa kazi pamoja
na changamoto za wizi. Mara zote, nimekuwa mtu wa kusimama imara katika kila
aina ya changamoto kwa kuhakikisha kwanza najiuliza ni kipi naweza kujifunza
kutokana na changamoto husika. Hali hii imenifanya kwenye kila changamoto nijiulize
nimehusika vipi (yapi makosa yangu) kwenye changamoto husika.
4. Mafanikio
ni zao la matumizi bora ya muda. Ufanisi kwenye jambo lolote
ni lazima kwanza pawepo matumizi bora ya muda. Pia, ufanisi huo ni lazima uwe
unaongozwa na msukumo imara wa kwa nini unahitaji mafanikio kwenye jambo
husika. Hii ina maana kwamba ili ufanikiwe kwenye sekta yoyote ile ni lazima
uwe na sababu za msingi ambazo zinakusukuma kupata mafanikio hayo. Mwaka 2017
niliweka lengo la kusoma vitabu 12 kwa maana ya kitabu kimoja kwa mwezi, lakini
nikajikuta kuwa sikuwa na msukumo imara wa kutekeleza lengo hili kwa vile
niliona kama vile sina muda wa kutosha kuniwezesha kusoma kitabu kizima ndani
ya mwezi mmoja. Haraka haraka kabla ya kumaliza mwezi Januari, 2017, ilinibidi
nijiunge na kundi la “Tanzania Voracious Readers” ambapo kupitia kundi hili
kila mwanakundi anatakiwa kusoma kitabu kimoja ndani ya wiki moja na
kuwashirikisha wengine. Kwa hatua hii nilijikuta nasoma vitabu zaidi ya 40
katika kipindi chote cha mwaka 2017 ikilinganishwa na vitabu 12 ambavyo
nilikusudia awali.
5. Jilipe
kwanza kwenye kila shilingi inayoingia mikononi mwako. Kanuni
ya kujilipa kwanza ni moja kati ya kanuni ambazo zinaendelea kutofautisha
masikini na matajiri. Matajiri mara zote wanatenga asilimia ya pato lao kwa
ajili ya uwekezaji na masikini mara zote wanatumia pesa zote wanazopata pasipo
kutenga hata shilingi moja kwa ajili ya uwekezaji. Mwaka 2017 nimeendelea
kujilipa kwanza kwa kuhakikisha natenga asilimia kumi (10%) ya kila pesa
inayoingia mkononi mwangu kwa ajili ya uwekezaji. Fedha hizi zinatengwa kwa
ajili ya uwekezaji wa muda mrefu kupitia uwekezaji wa hisa na vipande vya mfuko
wa umoja. Unahitaji nidhamu ya hali ya juu kufanikisha zoezi hili kwani mara
zote fedha huwa haitoshi kukamilisha mahitaji ya wakati husika.
6. Weka
malengo ambayo yanakuogopesha. Mwaka 2017 nilijiwekea
malengo ambayo kwa ujumla yalinifanya niogope kama kweli nitaweza kuyafikia.
Pamoja na uoga huo, nimefanikiwa kufikia malengo hayo kwa zaidi ya asilimia 70.
Hapa nimejifunza kuwa mara nyingi tunajinyima wenyewe kwa kuwa tunaruhusu fikra
finyu zitawale maisha yetu. Ili ufanikiwe kwenye kila sekta ni lazima uwe na
fikra chanya ambazo zinatakufanya uone ushindi kwenye kila lengo hata kama ni
kubwa kiasi gani.
7. Kamwe
usiseme hapana/siwezi kwenye fursa inayojitokeza. Mbinu
hii nilifundishwa na mwandishi Robert Kiyosaki kwenye kitabu chake cha “Rich Dad Poor Dad”. Mara nyingi
tunakutana na fursa nyingi ambazo pengine ni nzuri sana kwa ajili ya
kukamilisha ndote zetu japo tumekuwa na uoga wa kuulizia bei au hata baada ya
kuuliza bei tunakimbia moja kwa moja. Kiyosaki alinifundisha kuwa unapopata
fursa muhimu kwako unachotakiwa ni kufanya makubaliano ya kibiashara na muuzaji
kiasi ambacho ataridhishwa na ushawishi wako na hatimaye mfike bei ya kuuziana.
Baada ya hapo unachotakiwa kufanya ni kupeana ahadi ya lini mkamilishe biashara
husika ili wewe katika kipindi hicho ujipange kwa ajili ya kutafuta fedha
husika hata kama kwa kipindi hicho hauna pesa hiyo. Mbinu hii nimeitumia
kipindi chote cha mwaka 2017 na imezaa matunda chanya.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi niliyojifunza mwaka 2017. Karibu twende pamoja katika kipindi chote cha mwaka 2018. Kujiunga na mtandao wa
fikra za kitajiri BONYEZA HAPA .
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com
|