Mambo Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha How to Think like Leonardo da Vinci: Jinsi ya Kufikiri Kama Leonardo da Vinci

Habari ya leo rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri.

Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya 45 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi wa vitabu mbalimbali kwa ajili ya kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako uyatumie kubadilisha kila sekta ya maisha yako.

Makala hizi za uchambuzi wa vitabu zimekuwa zikikufikia kila wiki kwa kadri ambavyo napata muda wa kukushirikisha kile ninachojifunza kutoka kwenye vitabu vya maarifa mbalimbali. Ni matarajio yangu kuwa muda ninaotumia kukushirikisha uchambuzi wa vitabu umekuwa wa msaada mkubwa kwako katika kubadilisha maisha yako.

Hata hivyo, mtandao huu unahitaji maoni/ushauri au shuhuda kwa namna ambavyo umekuwa wa msaada kwako (tuma maoni/ushauri/ushuhuda wako kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com).

Unaweza kujiunga na mtandao huu, KWA KUBONYEZA BONYEZA HAPA na kujaza fomu kisha bofya “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.

Kitabu cha wiki hii ni “How To Think Like Leonardo da Vinci” kutoka kwa mwandishi Michael J. Gelb. Mwandishi anatumia kitabu hiki kwa ajili ya kutushirikisha kanuni ambazo Leonardo da Vinci alizitumia katika maisha yake. Leonardo da Vinci alikuwa ni Muitalino ambaye aliishi miaka 67 kati ya mwaka 1452 hadi 1519. Katika kipindi cha umri wake Leonardo aliishi maisha ya mafanikio ambayo yalijengwa juu misingi na kanuni mbalimbali.

Kanuni hizi zilimfanya da Vinci kuwa mtu mwenye mafanikio makubwa kwenye fani mbalimbali kama vile uvumbuzi, uchoraji, uchongaji, usanifu, sayansi, muziki, hisabati, uhandisi, fasihi, jeolojia, sayansi ya anga, botani, fasihi, historia, na ramani.

Mara nyingi da Vinci amekuwa akijulikana kama baba wa teknolojia na usanifu na kama mmoja wa wachoraji na mtu mwenye akili sana wa wakati wote. Wakati mwingine hujulikana kutokana na uvumbuzi wa parachute, helikopita na tanki.

Karibu tujifunze machache kutoka kwa da Vinci kati ya mengi ambayo tumeshirikishwa katika kitabu hiki:

1. Ubongo wako una akili/uwezo wa hali ya juu kuliko unavyodhania. Mwandishi anatushirikisha kuwa kumekuwepo na upotoshaji mkubwa wa aina mbili juu ya akili ya mwanadamu. Upotoshaji wa kwanza ni ule unaodai kuwa akili ya mwanadamu inategemea jeni (genes) wakati wa kuzaliana na akili hiyo haiwezi kuongezeka katika umri wa mwanada. Mwandishi anatushirikisha kuwa tafiti zinaonesha kuwa jeni zinachangia asilimia 48 tu ya akili na asilimia 52 iliyobaki inapatikana kupitia malezi, elimu na mazingira ambayo mwanadamu anapitia kipindi chote cha maisha yake.

2. Upotoshaji wa pili ni ile dhana ya kwamba ujuzi wa hoja za hisabati na uwezo wa lugha kuwa unaweza kupimwa kwa kipimo cha IQ (kipimo cha akili). Tafiti zinaonesha kuwa kila mmoja wetu ana angalau uwezo wa akili ambao umegawanyika katika sehemu tofauti saba. Na kila mmoja anaweza kufanikiwa katika sehemu zote hizo saba na zaidi kama ambavyo da Vinci alifanikiwa. Sehemu hizo na mifano ya watu waliofanikiwa ni pamoja na;
*     Mantiki (logic) – uwezo wa hisabati, mfano, Isaac Newton, Marie Curie;
*     Lugha (verbal) – uwezo wa lugha, mfano, William Shakespeare;
*     Makenika – mfano, Buckerminster Fuller;
*     Muziki;
*     Mwili – uwezo wa matumizi ya viungo vya mwili, mfano, Mohamed Ali;
*     Uwezo kujali wengine kwenye matendo ya kijamii – mfano, Nelson Mandela; na
*     Uwezo wa binafsi – mfano, Mother Teresa.

3. Siyo kweli kwamba mtu akizeeka na ubongo wake ndivyo unazeeka. Mwandishi anatushirikisha kuwa ubongo wa kawaida unakuwa bora zaidi kadri umri unavyoongezeka kama endapo mhusika ameweka jitihada za kuendeleza ubongo wake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba ubongo una nuroni (neurons) ambazo zina uwezo wa kutengeneza muunganiko wa vitu vipya au mazingira mapya katika kipindi chote cha mwanadamu.

4. Kama ambavyo makinda ya ndege anaiga mbinu za kukabiliana na maisha kutoka kwa mama yao, binadamu pia anao uwezo wa kuiga mambo mazuri katika maisha yake. Kufanikiwa katika kila sekta ya maisha yako unahitaji kuwa na walimu kwenye sekta hizo ambao kwa namna moja au nyingine walifanikiwa kwa kiasi kikubwa. Kwa maana nyingine unahitaji kuwa na ‘role models’. Mfano, kama unahitaji kuwa kiongozi bora huna bora kujifunza kutoka viongozi maarufu kama J.K Nyerere, Nelson Mandela na Winston Churchill. Kama unahitaji kufanikiwa kwenye uvumbuzi huna budi kujifunza kutoka kwa Leonardo da Vinci, Albert Einsten na wengineo.

5. Historia ya mwanadamu imepitia kwenye mabadiliko mbalimbali ambayo kila kizazi kinachoingia kinakuja na maboresha ya namna ya kurahisisha utendaji kazi pamoja na kuboresha njia bora za mawasiliano. Mabadiliko haya ni lazima yawe na athari chanya/hasi kwa kila binadamu ambaye bado anaishi pasipo kujali utashi wake. Kiwango cha athari chanya/hasi kitategemea na jinsi mwanadamu ambavyo amejiandaa kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko yanayotokea. Uwezo wa mwanadamu katika kujifunza na kukabiliana na mabadiliko kwa kutumia mfumo wa fikra huru ni nyenzo pekee ya kumuokoa dhidi ya mabadiliko ya kila aina. Leonardo aliishi kwenye matazamo wa namna hii na alitabiri juu ya mabadiliko haya katika historia ya mwanadamu.

6. Kwa ufupi historia ya maisha ya Leonardo da Vinci inaonesha kuwa mama yake alikuwa mkulima wa kawaida na alimzaa kwa baba ambaye alikuwa hajafunga nae ndoa. Baba yake alikuwa ni mhasibu, hata hivyo, kwa vile Leonardo alikuwa ni mtoto wa nje ya ndoa alilelewa na babu yake mpaka pale ambapo alifikia umri wa kujitegemea. Pamoja na changamoto zote hizo bado hazikuwa kikwazo kwa da Vinci kufikia mafanikio makubwa kimaisha na kitaaluma. Mpaka anakufa katika umri wa miaka 67 bado da Vinci alikuwa na uwezo wa kuendelea kujifunza na aliomba msamaha kwa “Mungu na wanadamu” kutokana na kuacha kazi nyingi ambazo zilikuwa hazikamilika wakati umauti unamfikia.

Kanuni saba za Leonardo da Vinci (Seven da Vincian Principles)

7. Kanuni ya kwanza: Udadisi. Kanuni hii da Vinci aliitumia kwa ajili ya kuwa na kiu ya kujifunza mara zote katika maisha yake. Kanuni hii ilisimama kama kanuni namba moja katika maisha yake kwa kuwa hamu ya kufahamu, kujifunza au kukua inatakiwa kuwa kipaumbele namba moja kwa ajili ya kuwa na maisha yenye ujuzi, hekima na ubunifu kwenye kila sekta. Leonardo tokea akiwa mtoto alikuwa na kiu ya kujifunza mambo mengi zaidi ya yale aliyofundishwa na walimu wake. Katika kujifunza huko mara zote hakuwa tayari kukubali neno NDIYO au HAPANA kama jibu la kujitosheleza.

8. Akili kubwa ni lazima mara zote iulize maswali makubwa. Maswali haya ni lazima yahusishe mfumo mzima wa fikra na yajikite kwenye mazingira yanayotuzunguka pamoja na uzoefu tulionao kwenye kila sekta ya maisha yetu. Hapa unahitaji kuwa na fikra huru kwa ajili ya kuuchunguza ulimwengu huu na hatimaye kuweza kupanua uelewa wako dhidi ya watu na vitu vinavyo kunzunguka. Kufanikisha zoezi hili ni lazima kwanza ujenge tabia ya kutembea na kijitabu kidogo kwa ajili ya kuhifadhi fikra zinazokujia pamoja na kuwa na muda wa kutafakari mawazo/fursa mbalimbali.


9. Kanuni ya pili: Vitendo. Kanuni hii ni maalamu kwa ajili ya kutafsili ujuzi unaojifunza kwenye vitendo kwa kutumia uzoefu, uvumilivu na utayari wa kujifunza kutokana na makosa. Hakuna sababu ya kujifunza vitu ambavyo havitumiki katika maisha yako. Ni kutokana na msingi huu da Vinci mara zote alitafsili kila alichojifunza kwenye vitendo bila kujali kama ujuzi huo unaenda kinyume na mazoea au mtazamo wa watu kwa nyakati hizo. Hivyo, mara zote da Vinci aliamini kuwa makosa ni sehemu ya kujifunza na hii ilimfanya aamini kuwa uzoefu una nafasi kubwa katika mafanikio ya mwanadamu. 

10. Kamwe hauwezi kuwa mtu wa vitendo kama wewe ni mtumwa wa fikra/mtazamo wako. Mwandishi anatushirikisha kuwa sio mitazamo yote tuliyonayo ni sahihi, Leonardo da Vinci alijaribu fikra/mitazamo yake kwa vitendo. Pale ambapo aligundua kuwa hakuwa sahihi alikiri makosa na hatimaye kutumia makosa hayo kama msingi wa kujisahihisha na kuboresha kwenye hatua zinazofuata. Hapa unahitaji kufanya tathimini juu ya ukweli kwenye fikra, mtazamo na imani ulizonazo kwenye kila sekta ya maisha yako. Tafuta vyanzo na malengo ya imani au mitazamo husika katika kipindi chote cha maisha yako.

11. Jifunze kutokana na makosa ya watu wengine. Mwandishi anatushirikisha kuwa mbinu nyingine ya kujifunza ni kuwa na “role model” wa uongo. Hii ina maana kuwa unatafuta mtu ambaye amefanya makosa kwenye kile unachohitaji kufanya na hatimaye unachambua makosa yake kwa ajili ya kuboresha zaidi.

12. Kanuni ya tatu: Hisia. Milango yote ya fahamu ina mchango mkubwa katika uzoefu tulionao kwenye maisha yetu ya kila siku. Leonardo da Vinci aliamini kuwa siri ya kuwa mtu wa vitendo inatokana na matumizi ya milango ya fahamu hasa mfumo wa macho. Tunahitaji kufahamu namna ya kuona vitu/watu wanaotuzunguka. Tunaweza kujifunza mengi kwa kutumia macho kwani ni kupitia macho haya tunaweza kuhoji maswali mengi juu ya yale tunayo tazama. Ni kutokana na mtazamo huu da Vinci aliamini kuwa yeyote anayepoteza uwezo wa kuona anakuwa amepoteza mwonekano wa ulimwengu. Macho yanabeba uzuri wote wa ulimwengu huu hivyo ni wajibu wetu kuyatumia vyema.

13. Baada ya kuona mlango mwingine wa fahamu unaofuatia kwa umuhimu kulingana na da Vinci ni kusikia. Hapa ndipo tunaona kuwa da Vinci pamoja na kuwa mchoraji mzuri (kutumia mlango wa kuona) alikuwa pia ni mwimbaji mzuri. Hivyo, aliona kuwa muziki una nafasi kubwa katika kufundisha au kupotosha jamii. Kwa ujumla wake da Vinci aliamini kuwa milango yote ya fahamu (kuona – macho, kusikia – masikio, kugusa – ngozi, kunusa – pua na radha/kuongea – ulimi) ina nafasi kubwa ya kumfanya mhusika atambue nafasi yake na muumba wake kwa maana ya muunganiko wa roho na mwili.

14. Tengeneza uhusiano kati ya mlango wa fahamu wa kugusa na mfumo wa hisia. Leonardo alishangaa sana kuona kuwa kuna watu wanagusa vitu pasipo kuwa na hisia juu ya kile wanachogusa. Siri kubwa ya mlango wa fahamu wa kugusa ni kutambua kuwa unaweza kujifunza kutafsili kila kitu kwa kutumia mikono na mwili mzima. Chochote unachogusa tengeneza hisia kana kwamba ndo mara ya kwanza unakigusa.

15. Kanuni ya nne: Kabiliana na giza. Kanuni hii inalenga kwenye utayari wa kukabiliana na mazingira, vitendo au hatua zenye utata, utayari wa kutegeua vitendawili kwenye maisha au utayari wa kuchukua hatua sehemu ambazo huna uhakika. Kadri unavyoendelea kudadisi na kutenda kwa kutumia uzoefu na milango yako ya fahamu unatafikia sehemu ambayo uelewi kilichopo mbele yako au ni hatua zipi unatakiwa kuchukua. Katika hali kama da Vinci alihakikisha anaruhusu fikra huru katika kichwa chake kwa ajili ya kuchukua hatua zaidi ambazo wakati mwingine zinaweza kuwa hatarishi. Kanuni hii inapima ujasiri wetu wa kuchukua hatua katika mazingira mapya.  

16. Kuwa na muda wa kupumzika kwa ajili ya kutafakari juu ya yale ambayo unaona ni magumu kwako kwa wakati huo. Mwandishi anatushirikisha kuwa tafiti zinaonesha kuwa watu wengi wanapata majibu ya changamoto zinazowakabili wakati wa mapumziko. Hivyo, ambapo unaona kuwa kichwa kimegoma kusonga mbele pata muda kwa ajili ya kupumzika ili utafakari kwa kina.

17. Kanuni ya tano: Sanaa/Sayansi. Kanuni hii inalenga kuhakikisha unakuwa na mlinganyo kati ya sayansi na sanaa au kati ya mantiki na mawazo. Hii ina maana kwamba unahitaji kushughulisha ubongo wako kwa kuhusisha ujuzi kutoka pande zote pindi unapofikri. Tafiti zinaonesha kuwa ubongo wa mwanadamu unagawanyika katika sehemu mbili ambazo ni, sehemu ya kushoto ambayo inajihusisha na fikra za kichambuzi (analytical thinking) na sehemu ya kulia ambayo inajihusisha na kufikiri kwa mapana (big picture thinking). Sehemu ya kushoto inajihusisha na kufikri kwa uchambuzi wa hatua kwa hatua kwa maana nyingine ni sehemu inayojihusisha na sayansi wakati sehemu ya kulia inajihusisha na kufikiri kwa mapana juu ya mada husika na hivyo ni sehemu inayojihusisha na sanaa. Leonardo da Vinci anatufundisha kuwa mara zote tunahitaji kutumia sehemu zote za ubongo katika kutatua changamoto za maisha yetu ya kila siku. Hii ni kutokana na ukweli kwamba ni vigumu kusema kuwa da Vinci alikuwa msanii kwa maana ya sanaa zake za michoro au kusema alikuwa mwanasayansi kwani sehemu zote mbili alizitumia katika kazi zake.

18. Kama mzazi au mwajiri unahitaji kutambua watu wako ambao wanatumia ubongo wa kulia na wale ambao wanatumia ubongo wa kushoto. Mfano, kama wewe ni mzazi husioneshe kupendelea mtoto ambaye anafanya vizuri zaidi kwenye masomo ya sayansi ukilinganisha na yule ambaye labda anafanya vizuri kwenye masomo ya sanaa. Unahitaji kutambua tofauti zilizopo katika yao na hivyo kama mzazi hakikisha wote unawapa mlinganyo sawa.

19. Kanuni ya sita: Ujasiri na utimamu wa mwili. Hapa mwandishi anatushirikisha kuwa kanuni hii da Vinci aliitumia kwa ajili ya kuwa na afya bora iliyotokana na mazoezi ya viungo. Hali hii ilimfanya da Vinci kuwa mtu hodari kwenye kutembea bila kuchoka, kuogelea, kuendesha bike au mazoezi mengine ya viungo. Leonardo aliamini kuwa kuzeeka kwa kasi ni matokeo ya mwili kukosa mazoezi ya kutosha na hivyo alihakikisha anatumia viungo vya mwili wake kwa ajili ya kuwa imara zaidi. Mfano, katika kuchora michoro yake alihakikisha anatumia mikono yote miwili kama sehemu ya kuimarisha sehemu zote za mwili wake.

20. Jifunze kutunza afya yako. Leonardo aliamini kuwa tunapaswa kukubali majukumu yetu kama sehemu ya kuimarisha au ustawi wa afya zetu. Mtazamo wake juu ya ugonjwa ulikuwa ni “ugonjwa unasababishwa na hali ya kupingana kwa ‘seli’ za mwili ambako usababishwa na mhusika na hivyo njia ya pekee ya kupona ugonjwa husika ni mhusika kuondoa hali hiyo katika mwili wake”. Baadhi ya njia ambazo da Vinci alihamasisha kama sehemu ya kuepuka magonjwa ni mazoezi mepesi, vyakula sahihi, pendelea mboga za majani, tumia vinjwaji sahihi na usinywe pombe kama haujala kitu, jifunike vizuri wakati wa usiku, epuka kuwa na hasira/manunguniko, epuka matumizi mengi ya sukari na chumvi, pendelea vyakula vya asili ambavyo vimepikwa kiasili zaidi (epuka viungo), kuwa na muda wa kupuzika, nenda chooni mara kwa mara na tafuna chakula vya kutosha. Binafsi nimezipenda hizi sijui wewe nipe mrejesho wako……..

21. Kanuni ya saba: Uhusiano. Kanuni hii da Vinci aliitumia kwa ajili ya kutambua na kuheshimu uhusiano wa vitu/matukio yote ili kutoa nafasi sawa kwa pande zote. Kanuni hii inahusisha umuhimu wa kufikiri kimfumo zaidi badala ya kujikita kwenye kitu/tukio moja na kuacha vitu/matukio mengine. Kila kitu au kiumbe kwenye mazingira yanayotuzunguka kina umuhimu wake kwa ajili ya ustawi wa vitu au viumbe wengine. Kila kiungo kwenye mwili wako kina uhusiano mkubwa na viungo vingine kwenye mwili wako. Hapa ndipo da Vinci alisoma uhusiano wa viungo vya mwili kama kiungo kimoja au aliheshimu mazingira kutokana na kila kitu kilichopo ndani yake.

Haya ni machache ambayo nimeweza kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.


Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link). Nakutakia mapambano mema.

Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.

Born to Win ~ Dream Big 

Augustine Mathias Bilondwa

Namba ya Simu:      +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com

Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com

onclick='window.open(