Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri.
Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa
FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa
ni wiki ya 32 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi
wa vitabu mbalimbali kwa ajili ya kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako
kuyatumia ili ubadilishe kila sekta ya maisha yako.
Ni matumaini yangu kuwa makala hizi
zimekuwa na msaada mkubwa kwako kwa kadri ambavyo umekuwa ukichukua hatua za
kubadilisha maisha yako. Hata hivyo, makala hizi haziwezi kubadilisha chochote
kama umekuwa mtu wa kusoma na kutokufanyia kazi yale unayojifunza.
Ili uendelee kunufaika na makala za
mtandao huu BONYEZA HAPA na
ujaze fomu kisha bonyeza “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao wa
fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa
humu moja kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “How Successful
People Think” kutoka
kwa mwandishi John C. Maxwell. John C. Maxwell ni mwandishi mahiri ambaye
vitabu vyake vimefanya vyema kwenye soko kiasi cha kuwa muuzaji bora wa vitabu
kwenye jarida la New York Times. Mwandishi
anatumia kitabu hiki kutushirikisha namna ambavyo watu wenye mafanikio
wanavyofikiri na jinsi ambavyo kila mmoja anaweza kubadilisha fikra zake kwa
ajili ya kubadilisha maisha yake kwa ujumla.
Kitabu
hiki kinatoa mafundisho ambayo yanatuweka wazi juu ya umuhimu wa kudhibiti
fikra zetu kwani wale ambao wanaweza kumudu fikra zao ndio wanaweza kufanikiwa
katika kila sekta ya maisha yao. Kwa kifupi ni kwamba fikra ni nyenzo pekee
inayotofautisha watu wenye mafanikio na watu wa kawaida. Habari njema ni kwamba
kila mmoja anaweza kujifunza namna ambavyo watu wenye mafanikio wanavyofikiria
katika maisha yao ya kila siku.
Karibu
tujifunze wote machache niliyojifunza kwenye hiki:
1. Kama
unahitaji kuwa kati ya watu ambao wanadhibiti fikira zao na hatimaye kufanikiwa
kwenye kila sekta ya maisha yako mwandishi anatushirikisha njia sita za kufuata
kwenye maisha yako ya kila siku. Moja,
tumia muda mwingi kuwekeza kwenye mambo ya msingi. Mwandishi anatushirikisha
kuwa watu wanaodhibiti fikra zao wanafahamu fika kanuni ya asili ya kuvuna
kulingana na kile ulichopanda. Ndivyo ilivyo kwenye fikira kadri unavyotumia
muda wako kuwaza mambo ya msingi kwenye maisha yako ndivyo unapata matokeo
mazuri ya fikra zako. Hapa unahitaji kutumia muda wako kwa kusoma vitabu, kusikiliza
vitabu vilivyosomwa (audio books), kusoma majarida ya biashara au kubadilishana
mawazo na watu wenye mafanikio.
2. Mbili, tumia
muda mwingi na watu wema. Kama ambavyo tumezoea kuwa ndege wanaofanana uruka
pamoja ndicho mwandishi anatushirikisha kuwa kama utatumia muda mwingi na watu
wenye uwezo wa kudhibiti fikra zao ndivyo na wewe utaongeza uwezo wako wa
kufikiri. Tumia muda wako kukaa na watu ambao wanaweza kukupa changamoto za
kimaendeleo na sio watu ambao wamekata tamaa wenye kutumia muda wao kulalamikia
watu/vitu ambavyo vipo nje ya uwezo wao.
3. Tatu, kuwa na nidhamu
binafsi kwenye vipaumbele vya fikira zako. Mwandishi anatushirikisha kuwa ili
mfikiriaji mzuri ni lazima uwe na nidhamu binafsi ambayo ni nyenzo ya
kukuongoza katika kupanga vipaumbele vya vitu vipi uvipe nafasi kwenye mfumo wa
fikra zako. Muda wote jiweke kwenye mazingira ambayo hayatakuhamisha vipaumbele
vya fikira zako.
4. Nne, fanyia kazi fikra
zako nzuri. Mwandishi anatushirikisha kuwa ni muhimu kuhakikisha kuwa kuna
muunganiko wa fikra na vitendo vyako katika maisha yako ya kila siku. Mawazo ni
ya muda mfupi hivyo kama hayatafsiliwi kwenye vitendo yanakuwa hayana maana
yoyote. Hapa unatakiwa kuhakikisha unafanyia kazi fikra zako kabla hazijapotea
kwenye mfumo wa ubongo.
5. Tano, ruhusu hisia zako
kuendelea kutengeneza fikra nzuri. Mwandishi anatushirikisha kuwa mfumo wa
fikira hauwezi kutenganishwa na mfumo wa hisia. Vyote vinategemeana kutokana na
ukweli kwamba hisia zinashawishi fikra na fikra kwa upande mwingine zinaamsha
hisia za mwili. Ili uendelee kudhibiti fikra zako ni lazima mfumo wa hisia
ulishe ubongo ili na ubongo nao ufanyie kazi vichocheo vya hisia. Hapa ni
lazima ukumbuke kuchuja aina ya hisia ambazo zinatakiwa kuingia kwenye mfumo
wako wa fikra.
6. Sita, rudia zoezi la kudhibiti
hisia mara kwa mara. Mwandishi anatushirikisha kuwa zoezi la kujikita kwenye
fikra nzuri sio la muda mfupi bali unahitaji kufanya jitihada za kurudia hatua
zote hizi mara kwa mara katika maisha yako ya kila siku. Hapa unahitaji kujenga
utamaduni wa kurudia kufikiria mawazo mema muda mwingi huku ukiendelea
kuyafanyia kazi kwa vitendo. Kwa maana hii kadri inavyokuwa na utamaduni wa
nidhamu ya kufikiri vyema ndivyo unakuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa katika
kila sekta ya maisha yako.
7. Fikri
katika mapana ya picha kubwa (big – picture thinking) kwani ndo njia ambayo
itakupa ufanisi wa fikra zako. Sifa kubwa waliyonayo watu wanaofikiri kwa
mapana ya picha kubwa ni kwamba daima huwa hawaridhiki na mazingira/hali
inayowakabili bali muda wote wanakuwa macho kwa ajili ya fursa mpya. Watu hawa
wanajifunza kila mara kutoka kwa watu wengine na hivyo wanafanya kazi kwa bidii
na ubunifu katika shughuli zao kila siku. Watu hawa wanatambua nguvu kubwa
iliyopo kwenye usikivu kutoka kwa wengine kuliko kuwa wazungumzaji wakubwa.
Pia, watu hawa muda wote wanatazama nje ya boksi kwa ajili ya kupata fursa
mpya.
8. Jenga
mtazamo wa fikra pana kwa ajili ya kuwa kiongozi bora. Mwandishi
anatushirikisha kuwa sifa kubwa ya kiongozi bora ni kuwa na uwezo wa kuona vitu
kwa mapana yake kuliko watu anaowaongoza. Uwezo huu unajumuisha ubunifu katika
kutafsiri hali ya sasa na makadirio ya matukio yanayokuja – kutafsili matukio
yajayo kutokana na matukio yaliyopita au yaliyopo. Faida nyingine ya kufikira
kwa mapana ya picha kubwa ni kuwa na uwezo wa kuona vitu ambavyo watu wengine
wanaviona. Uwezo huu ni nyenzo muhimu katika yale unayofanya kwani ni kupitia
uwezo huu utaweza kuboresha bidhaa/huduma kwa wateja wako.
9. Zifuatazo
ni mbinu ambazo zitakufanya ufikiri katika mapana ya picha kubwa;
i. Kubali
kuwa tofauti kwenye mitazamo ya mazoea ya wengi – kuna nyakati utahitaji
kupingana na ukweli uliozoeleka katika mazingira yako kwa ajili ya kudhihirisha
kuwa ukweli huo ulikuwa ni uongo;
ii. Jifunze
kutoka kwenye kila tukio unalokutanalo katika maisha yako ya kila siku – hii ni
kwa matukio yote jema au baya ni lazima ujiulize fundisho gani unajifunza
kutokana na tukio husika;
iii.
Jifunze kwa kadri uwezavyo kutoka kwa
watu wengine – watu wenye fikra pana wantambua kuwa wao sio wakamilifu kwa kila
kitu hivyo muda wote wanajifunza kutokana na uzoefu wa watu wengine; na
iv.
Fungua milango ya boksi linalokufunika
ili ufanikiwe kuitawala dunia – jamii imezoea kuishi kwa mazoea na hatimaye
kuhisi kuwa milango ya mafanikio imefungwa. Watu wengi wanahitaji usalama na majibu/kazi
nyepesi na hivyo kuishia kupata matokeo mepesi.
10. Jifunze kuwa na utulivu wa fikra
(focused thinking). Kama unahitaji kuboresha mfumo wako wa fikra huna budi ya
kujenga nidhamu ya utalivu wa akili. Hapa ni lazima uwe tayari kufanya
tathimini ya mara kwa mara juu ya yale unayowaza kwa wakati husika. Utulivu wa
akili ni njia pekee ya kukuwezesha kuondoa mwingiliano wa fikra hasi pamoja na
vikwazo vyote kwenye akili yako. Pia, njia ya utulivu wa akili inakupa nguvu na
hamasa zaidi kwa ajili ya kutekeleza fursa zinazojitokeza. Kwa ujumla ni kwamba
kadri changamoto ilivyo kubwa ndivyo unahitaji kuongeza utulivu wa akili kwa
ajili ya kutatua changamoto husika.
11.
Zifuatazo ni njia ambazo zitakusaidia
kuboresha utulivu wa akili kwa yale unayofanya;
i. Ondoa
vikwazo vyote ambavyo huwa vinakuhamisha kutoka kwenye kazi unayofanya – hapa
unahitaji kuhakikisha unafanya kazi kwa mtiririko wa vipaumbele. Yale ya
umuhimu zaidi yape kipaumbele kwanza. Pia, hakikisha unaondoa mwingiliano wa
vifaa vya mawasiliano kama vile simu, barua pepe na mitandao ya kijamii n.k;
ii. Tenga
muda maalumu katika siku kwa ajili ya utulivu wa akili pasipo mwingiliano
wowote – muda huu unaweza kuwa kabla ya kulala au asubuhi na mapema wakati kuna
utulivu wa kutosha;
iii.
Kuwa na orodha ya sehemu kwenye sekta
ya maisha yako ambayo inahitaji kuwekewa kipaumbele; na
iv.
Weka malengo na yapitie mara kwa mara
kwa ajili kujitathimini – hakikisha malengo unayojiwekea yanapimika na
kutekelezeka.
12. Tengeneza orodha ya vitu au tabia
ambazo upo tayari kuachana nazo kwa ajili ya utulivu wa akili. Mwandishi
anatushirikisha kuwa hakuna mafanikio bila kuwa tayari kupoteza baadhi tabia
ambazo zimekuwa kandamizi kwako. Kwa maana nyingine hakuna mafanikio pasipo
kuwa tayari kutoa sadaka, sadaka hiyo inaweza kuwa kwenye vitu ambavyo upo
tayari kupoteza au mazingira mapya ambayo unahitaji kuyaishi. Ndivyo ilivyo
hata kwenye mafanikio ya utulivu wa akili. Hapa unahitaji kuandaa orodha ya
tabia, mila au tamaduni ambazo zimekufanya husiwe na utulivu wa akili kwa
kipindi kirefu na hatimaye uzifanyie kazi kwa ajili ya kujirekebisha.
13. Tumia hazina ya ubunifu kwa ajili ya
kuboresha mfumo wa fikra zako (creative thinking). Kufikiri kwa ubunifu ni
hazina pekee ambayo imeendelea kutenda maajabu katika kubadilisha dunia hii
kuwa mahala pazuri pa kuishi. Ni kupitia hazina hii ulimwengu umeendelea kubadilika
kila kukicha. Ili uwe mbunifu kwenye fikra zako unahitaji kujifunza yafuatayo;
i. Ni
lazima husiwe mtu wa kuogopa kushindwa – watu wenye fikra za ubunifu kamwe
hawaogopi kushindwa kwani ubunifu wenyewe ni sawa na kushindwa kutokana na
ukweli kwamba unabuni kitu ambacho hauna uhakika na uwepo wake;
ii. Ni
lazima uwe tayari kuongeza thamani kwenye kila unachojihusisha nacho – watu
wenye fikra za ubunifu muda wote wanaongozwa na macho ya kuongeza thamani kwa
ajili ya manufaa yao na jamii inayowazunguka; na
iii. Utulivu
wa akili unasaidia mhusika kujifunza zaidi – hii ni kutokana na ukweli kuwa
hatuna majibu ya mambo yote tunayokutana nayo katika maisha yetu.
14. Ili uwe kati ya watu wenye fikra za
ubunifu unahitaji kuondoa vikwazo vyote ambavyo vimekuwa kizuizi kwako muda
mrefu. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wengi wameshindwa kuwa na fikra za
ubunifu kutokana na imani ambazo wamekuwa wakinena juu ya nafsi zao. Baadhi ya
kauli kandamizi ni kama vile: mimi siwezi kuwa mbunifu hata siku moja, mimi
nafuata sheria zilizopo siwezi kwenda kufanya lolote nje ya sheria hizo, hakuna
jipya katika dunia hii, mimi sio mtu wa kuuliza maswali n.k. Pia, ili uwe na
fikra bunifu ni lazima uchague watu kutumia muda mwingi na watu wenye fikra
bunifu.
15. Tengeneza utamaduni wa kufikiria katika
hali halisi ya nafsi yako (realistic thinking) – husiwe mwongo wa nafsi katika
fikra zako. Faida mojawapo ya kufikiri katika hali yako halisi ni kwamba
kufanya hivyo inakusaidia kubadilisha tabia zile ambazo unaona zipo kinyume na
mahitaji ya maisha yako. Pia, kadri unavyokuwa mkweli katika fikra zako ndivyo
unajijengea uadilifu na uaminifu kwenye jamii inayokuzunguka. Kwa kufanya hivyo
itakusaidia kuvuta watu wengi na hivyo kuongeza ufanisi katika huduma zako.
16. Jifunze utamaduni wa kufikiri kimkakati
(strategic thinking). Mwandishi anatushirikisha kuwa kufikiri kimkakati ni pale
ambapo mhusika anaweza kutumia fikira kutengeneza na hatimaye kuuishi mkakati
wa maisha yake. Mkakati wa maisha unahusisha mpangilio wa matukio ya maisha ya
mhusika katika kila siku ya maisha yake. Kutokana na maana hii mtu mwenye
mkakati wa maisha anatambua matukio ya maisha yake kwa siku zilizopo na siku
zijazo. Fikra zinakuongoza kutengeneza mkakati wa maisha yako lakini pia ni
kupitia fikra hizo hizo unaweza kuuishi mkakati wa maisha yako.
17. Ruhusu fikra zenye uwezekano
(possibility thinking). Mwandishi anatushirikisha kuwa watu waliofanikiwa huwa
wanatanguliza uwezekano wa kukamilisha jambo lolote kabla ya kuangalia vikwazo
vilivyopo. Kadri unavyoruhusu fikra wezeshi ndivyo inakuwa rahisi kuona
uwezekano wa kutatua changamoto zilizopo mbele yako na kinyume chake ni kwamba
kama hauna fikra wezeshi muda wote mfumo wako wa fikra unatafsiri vikwazo na matokeo
yake ni kushindwa kuchukua hatua. Pale unapoamini kuwa unaweza kutekeleza jambo
gumu ni mwisho wake ukafanikiwa kulitekeleza unaruhusu milango mingi katika
mfumo wako wa fikra kwa ajili ya kutekeleza magumu mengi unayokutana nayo. Pia,
fikra wezeshi zinakusaidia kuwaza vitu kwa mapana yake na hivyo zinamfanya
mhusika hasiwe mtu wa kawaida.
18. Jifunze kurudia fikra zako mara kwa
mara kutokana na mafanikio au makosa unayopitia. Mwandishi anatushirikisha kuwa
matukio mengi yanayotokea katika maisha yetu yanatokana na mafanikio au makosa
yetu ya siku za nyuma. Watu wenye mafanikio wanafahamu juu ya msingi huu na
hivyo mara kwa mara wanakuwa muda wa kufikiria juu ya mafanikio au makosa yao. Kadri
unavyokuwa na muda wa kufikiria juu ya matukio yaliyopita ndivyo unaongeza
nafasi ya kufanya maamuzi sahihi katika nyakati zilizopo. Kutokana na umuhimu
wa kurudia matukio ya maisha yako, mwandishi anatushirikisha kuwa ni muhimu
kutenga muda katika siku hasa kabla ya kulala kwa ajili ya kurudia matukio ya
siku nzima.
19. Jifunze kujiuliza maswali dhidi ya
fikra ambazo zimezoeleka (popular thinking) katika mfumo wako wa fikra. Mwandishi
anatushirikisha kuwa binadamu ni kiumbe ambaye ameumbwa kwa ajili ya kuleta
mabadiliko mema katika mazingira yanayomzunguka. Hata hivyo binadamu wengi
wameshindwa kuleta mabadiliko chanya kutokana na ukweli kuwa wanaishi ndani ya
minyororo ya mila na imani ambazo wamewekewa toka enzi za utoto wao. Ili ufanikiwe
kudhibiti fikra zako ni lazima uwe na utaratibu wa kuhoji juu ya mila au
desturi. Kwa kufanya hivi inakuwa rahisi kwako kubuni mawazo mapya ambayo yataboresha
maisha yako. Hii ni kutokana na ukweli kwamba fikra ambazo zimezoeleka huwa
zinaleta matokeo ya kawaida hivyo ni lazima utafute fikra mpya kwa ajili ya
matokeo makubwa.
20. Jifunze kunufaika na thamani ya fikra
za wengine. Mwandishi anatushirikisha kuwa tunaishi katika ulimwengu wenye
mabadiliko ya kasi hivyo kwenda kutegea fikra zako pekee kamwe hauwezi kwenda
sambamba na kasi ya mabadiliko ya ulimwengu huu. Kadri unavyothamini fikra za
wengine ndivyo na wewe unaongeza nafasi ya kuwa na ubunifu zaidi katika mipango
ya maisha yako. Hapa unahitaji kuondoa fikra za kishindani katika mfumo wako wa
fikra na kuingiza fikra za kushirikiana zaidi na wenzio kwa ajili ya kuboresha maisha
yako na jamii inayokuzunguka. Pia, unatakiwa kuondoa dhana ya “mimi” na
kuingiza mtazamo wa “sisi”.
21. Jibidishe kuwa na fikra zisizokuwa na
uchoyo (unselfish thinking). Mwandishi anatushirikisha kuwa hakuna kitu
kinawanyima mafanikio watu wengi kama uchoyo kwani uchoyo una tabia ya kufunga
milango ya mafanikio. Hivyo, katika maisha jifunze kuwasaidia binadamu wengine
wanafanikiwe ili na wewe ufanikiwe zaidi kupitia wao. Pia, kadri unavyowasaidia
wengine ndivyo na wewe thamani yako inaongezeka na hatimaye unafakiwa kuacha
alama katika maisha yako.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
|
|
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com