Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri.
Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa
FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa
ni wiki ya 2 katika kipindi cha mwaka 2018 naendelea kukushirikisha uchambuzi
wa vitabu mbalimbali vyenye mafundisho tofauti katika kila sekta ya maisha
yako.
Makala hizi za uchambuzi wa vitabu
zimekuwa zikikufikia kila wiki kwa kadri ambavyo napata muda wa kukushirikisha
kile ninachojifunza kutoka kwenye vitabu hivi. Ni matarajio yangu kuwa muda
ninaotumia kukushirikisha uchambuzi wa vitabu umekuwa wa msaada mkubwa kwako
katika kubadilisha maisha yako.
Hata hivyo, mtandao huu unahitaji
maoni/ushauri au shuhuda kwa namna ambavyo umekuwa wa msaada kwako (tuma
maoni/ushauri/ushuhuda wako kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com).
Unaweza kujiunga na mtandao huu, KWA KUBONYEZA BONYEZA HAPA
na
kujaza fomu kisha bofya “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu.
Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja
kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “Rich Kid Smart Kid” kutoka kwa mwandishi Robert Kiyosaki. Kitabu
hiki ni maalumu kwa ajili ya mzazi yeyote mwenye kuhitaji kumkuza mtoto katika
ulimwengu wa mafanikio ya kifedha.
Mwandishi
anatushirikisha kuwa zama zimebadirika, zamani ilikuwa ni kawaida kumwambia
mtoto nenda shule soma kwa bidii kwa ajili ya kufaulu masomo ili upate kazi
nzuri. Nasaha hizi kwa watoto enzi hizo wengi walifanikiwa kupitia taaluma zao
lakini zama hizi mambo yamekuwa kinyume kwani ufaulu wa masomo haumaanishi kuwa
ndio tiketi ya kufaulu maisha.
Katika
kipindi hiki cha mapinduzi ya teknolojia ya habari mtoto anahitaji kufundishwa umuhimu
wa kujifunza vitu vingi zaidi ya kile alichosomea. Zaidi wazazi pia wanahitaji
kufahamu kuwa wao ni walimu namba moja hivyo watoto wanahitaji kujifunza
kupitia matendo yao. Pia wazazi wanapaswa kutambua kuwa elimu inayotolewa
haijitoshelezi kwa ajili ya kufanikisha maisha. Hivyo, mtoto anahitaji
kufundishwa misingi muhimu ya maisha ya mafanikio ikiwa ni pamoja na elimu ya
fedha ambayo haifundishwi kwenye mitaala ya shule zetu.
Karibu
tujifunze machache kati ya mengi ambayo mwandishi Robert Kiyosaki
anatushirikisha katika kitabu hiki:
1. Katika ulimwengu wa sasa ambao
usalama wa kazi umeendelea kuwa mdogo siku hadi siku, mtoto ni vyema akafundishwa
elimu ya pesa kwa ajili ya kulinda taarifa zake za kifedha. Elimu hii
itamsaidia kuwa na msingi wa usalama wa kifedha katika kipindi cha maisha yake ikiwa
ni pamoja na ufahamu wa kuwa mara zote pesa inatakiwa kumfanyia kazi badala
yeye kuifanyia kazi. Ni misingi hii ya elimu ya pesa ambayo itamuwezesha mtoto
kuwekeza fedha kidogo anazopata kutoka kwenye kazi/biashara yake kwa ajili ya
maisha yake ya baadae.
2. Watoto wote wanazaliwa wakiwa
tajiri na akili nyingi. Mwandishi anatushirikisha kuwa kadri mtoto anavyokuwa
ndivyo anazidi kujifunza kuwa masikini au kujiona kuwa hana akili
ikilinganishwa na watoto wengine. Haya ni matokeo ya mtoto kukosa miongozo
sahihi kutoka kwa wazazi wake juu ya uwezo alionao kwenye ulimwengu wa utajiri
na kiakili. Kumbe kama mzazi unahitaji kumfunda mwanao kwenye mihimili muhimu
ya uhuru wa kifedha na fikra sahihi juu ya uwezo wake kiakili.
3. Katika
ukuaji mtoto anatakiwa afundishwe umuhimu wa kufahamu kuwa katika maisha hakuna
jibu sahihi. Jibu la HAPANA au NDIYO yote ni majibu sahihi ikitegemewa na namna
muhusika anavyosimama kutetea jibu lake. Hii ni elimu ambayo mtoto ataipata kwa
wazazi pekee kwani elimu ya sasa inalenga kwenye kutambua watoto wanaoweza
kutoa majibu sahihi na kuwafanya wengine waonekana hawana uwezo. Hii ni pamoja
na umuhimu wa kutambua kuwa katika maisha maamuzi unayofanya ni lazima yawe na
athari nzuri au mbaya kwa baadae.
4. Akili
ya pesa inapimwa pale mtu pesa alizonazo zinaweza kumfanyia kazi na wakati huo
huo yeye akiendelea kufurahia maisha yake kupitia uwekezaji wake. Kwa maana
nyingine ni lazima uwe na furaha juu ya mifereji inayokuingizia pesa na kupitia
mifereji hiyo uwe na uhuru wa kifedha kwenye maisha. Hii ni elimu ambayo watoto
wengi wanaikosa kwa vile wengi wanafundishwa kuifanyia kazi pesa. Kwa kifupi
akili ya pesa kwa kila mtu inapimwa na kiasi cha fedha ambacho mhusika
anatengeneza na kwa namna gani pesa hizo zinampa uhuru wa kifedha na furaha katika
maisha yake kwa ujumla.
5. Mtoto
anahitaji kufundishwa kwa vitendo. Elimu ya sasa inajikita zaidi kwenye nadharia
kuliko vitendo, elimu hii imepelekea kuzalisha vijana wengi ambao darasani wanafaulu
kwa viwango vya hali juu japo katika maisha mafanikio yao ni ya kawaida. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba elimu ya sasa inazalisha watu ambao wanaweza kuelezea
kwa kina mbinu mbalimbali za mafanikio lakini wao hawajawahi kutumia mbinu husika
kwa ajili ya mafanikio yao.
6. Kuna
aina tofauti za ‘ujiniasi’ japo jamii inachukulia majiniasi kuwa ni wale wanaofanya
vyema kwenye masomo hasa wenye uwezo mkubwa wa lugha na hesabu. Hali hii
inapelekea watoto wengi kupoteza kalama zao hasa wale ambao ujiniasi wao upo
kwenye matumizi ya mwili kama vile muziki, wachezaji wa mpira na kikapu au
wasanifu wa vitu. Kama mzazi unahitaji kutambua ujiniasi wa mwanao upo katika
maeneo yapi na kuhakikisha unamsaidia katika kila hatua ya ukuaji wake ili afikie
malengo yake.
7. Elimu
ya kweli inaanzia pale mtoto anapomaliza masomo yake. Mtoto anahitaji
kuandaliwa kwa ajili ya kuendelea kujifunza katika kipindi chote cha maisha
yake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba watoto wengi wanapomaliza masomo yao
wanaona kuwa ndo mwisho wa kujifunza. Hali hii inapelekea watoto wengi
waliokuwa wanafanya vyema shuleni/vyuoni kushindwa kufanikiwa katika maisha kwa
vile wanashindwa kujifunza mbinu za mafanikio katika kimaisha.
8. Mtoto
anahitaji kufundishwa toka akiwa mtoto kuwa ana uwezo wa kila aina kwa ajili ya
kuwa tajiri – anaweza kupata fedha za ndoto zake kwani fedha zinatengenezwa
kutoka kwenye mawazo na si kweli kwamba ili utengeneze pesa ni lazima uwe na
pesa. Matajiri wanaendelea kuwa tajiri kwa kuwa wana mawazo ya kitajiri na
masikini wanaendelea kuwa masikini kwa kuwa wana mawazo ya kimasikini. Na masikini
wengi wanajifunza kuhusu pesa kutoka kwa wazazi wao ambao pia wana matatizo ya
kipesa. Hivyo kama unahitaji mwanao awe tajiri ni lazima umpe nguvu ya utajiri
ambayo si nyingine bali ni elimu ya namna jinsi fedha zinavyotengenezwa.
9. Kati
ya umri wa miaka 9 hadi 15 ndipo mzazi anatakiwa kuwa makini kwenye mwenendo wa
mtoto wake katika kuchagua maisha yake ya baadae. Katika kipindi hiki ndipo
mzazi anahitaji kujua ni vipaji vipi mtoto alivyonavyo kwa ajili ya kusaidia kuendeleza
vipaji husika. Hapa ndipo mazazi
anapaswa kuwa makini kwa ajili ya kumsaidia mtoto apitie kwenye njia sahihi
ambazo kwa baadae zitakuwa na msaada katika kufanikisha ndoto za mtoto.
Hata hivyo, katika
jamii zetu kwa wazazi walio wengi ni katika kipindi hiki mtoto anaweza
kuonekana mkorofi kwa vile anaenda kinyume na mahitaji ya wazazi wake. Hali hii
inatokea pale mzazi analazimisha mtoto kutumia kanuni za maisha ambazo zinaenda
kinyume na matamanio ya mtoto. Mfano, mtoto anapenda kucheza mpira lakini mzazi
anamlazimisha kukaa darasani kwa ajili ya masomo.
10. Mtazamo juu ya nafsi yako ndio nguzo
kuu ya kufanikisha kila jambo katika maisha. Jukumu kubwa la mzazi ni
kuhakikisha mtoto anafundishwa msingi wa kuwa na mtazamo chanya juu ya nafsi
yake katika kila aina ya matukio ambayo atakutana nayo katika maisha yake. Mtoto
anahitaji akuzwe katika mazingira ya ya na mtazamo kuwa anaweza kufanikisha
jambo lolote.
11. Kinachotofautisha watu kiuchumi sio malipo
ya kazi wanazofanya bali kile wanachofanyia pesa wanazolipwa. Kwa maana
nyingine, hatuwezi kupima utajiri wa mtu kwa kuangalia mshahara wake. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba mtu anaweza kulipwa mshahara mkubwa lakini akawa
anatumia pesa zote kwenye mambo ambayo hayana msingi wa kumwezesha kuwa na uhuru
wa kifedha. Mtu huyu pindi akiacha kazi ataishi maisha ya msongo wa mawazo kwa
sababu ya mahitaji ya kifedha. Kipato/mshahara uwe mdogo au mkubwa ni lazima
ujenge nidhamu ya kuwekeza kwa ajili ya maisha ya baadae.
12. Utajiri unaanzia kwenye vitu vidogo ambavyo
vinafanyiwa kazi kwenye muda wa ziada nje ya muda wako wa kazini. Je muda wako
wa ziada unautumia kufanya nini? Huu ni muda maalum ambao ukitumiwa vizuri
utakuwa na manufaa kwako na watoto wako kwa ujumla. Hii ni kutokana na ukweli
kwamba katika muda wa ziada ni rahisi kufanya kazi ambazo unaweza
kuwashirikisha watoto kwa vitendo au wenyewe kuona kazi unazofanya na hivyo
inakuwa rahisi kuiga kazi zako.
13. Mtoto katika ukuaji wake afundishwe
kuwa ili ufanikiwe kimaisha ni lazima utengeneze mifereji mingi ya vipato. Kadri
unavyokuwa ni mifereji mingi ya kipato ndivyo unaongeza nafasi ya kuwa na uhuru
wa kifedha. Hivyo katika ukuaji mtoto anatakiwa kufundishwa misingi mikuu
mitatu kwa ajili ya mafanikio. Msingi wa kwanza ni elimu ya fedha, msingi wa
pili ni umuhimu wa kujifunza kila mara katika kila sekta ya maisha yake
(kiroho, kijamii na kiuchumi) na msingi wa mwisho ni namna ya
kukua/kujiendeleza kwenye kada ambayo atachagua.
14. Mzazi/mlezi daima ujitahidi kuepuka
maneno ambayo yanamfanya mtoto ajione wa tofauti badala yake unatakiwa utamke
maneno ambayo yanamjenga au yana baraka ndani mwake. Epuka kutamka maneno kama
mjinga wewe, mpumbavu, mtundu, mkorofi na badala yake jitahidi kutamka meneno
kama mwanangu wewe ni wa kipekee, wewe ni jiniasi, una akili sana mwanangu na
mengine kama hayo.
15. Nyakati zimebadilika kwani zamani
ilizoeleka kuwa kadri unavyozeeka ndivyo thamani yako inavyoongezeka. Siku hizi
katika zama hizi za taarifa mambo yamebadilika kwani kadri unavyozeeka ndivyo
na thamani yako inavyopungua. Siku hizi suala la uzoefu halina nafasi kubwa
badala yake muda wote wanatakiwa kuwa na taarifa au maarifa sahihi. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba taarifa/maarifa yanabadilika kila mara na hivyo mtoto
anatakiwa kufundishwa juu ya mabadiliko hayo ili aishi maisha yanayoendana na nyakati
zilizopo.
16. Zama hizi hazina nafasi kwa mtoto
anayemaliza na maksi nzuri bali zinahitaji mtoto anayemaliza akiwa na ujuzi
sahihi kwenye uzalishaji au utendaji kazi. Ni katika zama hizi tunaona wale
waliokuwa wanafanya vibaya mashuleni/vyuoni ndo wanaongoza kwenye mafanikio. Hizi
ni zama za kutumia ujuzi ulionao kwa ajili ya kubuni vitu vipya. Ni katika zama
hizi watoto wadogo kabisa wanakuwa mamilionea tofauti na zamani ilivyozoeleka
kuwa hadi kuwa milionea ni lazima uwe mzee.
17. Zama hizi sio za kumfundisha mtoto kuwa
nenda shule usome kwa bidii kwa ajili ya kupata kazi nzuri. Katika zama
tulizopo na tunakoelekea nafasi za ajira zinazidi kupungua kutokana na ukweli
kwamba kwa sasa kazi nyingi zinafanywa na kompyuta badala ya kufanywa na watu. Hizi
ni zama sahihi za kumfundisha mtoto kwa ajili ya kujiajiri au kuzalisha ajira
zaidi kwa ajili ya wengine.
18. Kila jambo linalofanywa iwe kujifunza au
kitu chochote kile ni lazima kiwe na kinaongozwa na msukumo wa kiroho. Msukumo huu
ndio unaosababisha mwili upate nguvu ya kutenda vitu mbalimbali. Ni msukumo huu
ambao daima unaendelea kutukumbusha sisi ni nani na tumeubwa kwa ajili ya
kutimiza makusudi maalum katika ulimwengu huu. Kama mtu amekosa msukumo huu
kamwe hawezi kufanikiwa katika maisha yake.
19. Watoto wengi wanamaliza masomo kabla ya
kujiandaa kwenye ulimwengu wa maisha baada ya shule. Watoto hawa wanamaliza
masomo wakiwa na shauku ya usalama wa kazi pasipo kufahamu kuwa kazi salama
inatatoka ndani mwao. Matokeo yake ni kwamba vijana hawa wanaishia kuzunguka na
baasha wakitafuta kazi miaka hadi miaka. Hapa kuna tatizo la kimalezi, kama
wazazi wangetimiza wajibu wa kuwafundisha vijana hawa mbinu za kujitegemea na
kukubali kutimiza wajibu tusingeona wimbi kubwa la vijana wanaosubilia
kuajiriwa.
20. Kupandishwa mshahara si suluhisho la
matatizo ya kifedha. Mwandishi anatushirikisha kuwa mfumo wa elimu ya sasa
unamfanya mtoto afahamu kuwa kadri anavyopandishiwa mshahara ndivyo anamaliza
matatizo yake ya kifedha. Ukweli ni kwamba kadri Serikali inavyopandisha
mshahara ndivyo na mfumuko wa bei unavyoongezeka na matokeo yake mambo yanarudi
kwenye mlinganyo. Pia, kama hauna elimu ya fedha kadri kipato chako
kinavyoongezeka ndivyo na matumizi yanavyoongezeka mara dufu.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link). Nakutakia
mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com
|