Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri.
Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa
FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa
ni wiki ya 3 katika kipindi cha mwaka 2018 naendelea kukushirikisha uchambuzi
wa vitabu mbalimbali vyenye mafundisho tofauti katika kila sekta ya maisha
yako.
Makala hizi za uchambuzi wa vitabu
zimekuwa zikikufikia kila wiki kwa kadri ambavyo napata muda wa kukushirikisha
kile ninachojifunza kutoka kwenye vitabu hivi. Ni matarajio yangu kuwa muda
ninaotumia kukushirikisha uchambuzi wa vitabu umekuwa wa msaada mkubwa kwako
katika kubadilisha maisha yako.
Hata hivyo, mtandao huu unahitaji
maoni/ushauri au shuhuda kwa namna ambavyo umekuwa wa msaada kwako (tuma
maoni/ushauri/ushuhuda wako kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com).
Unaweza kujiunga na mtandao huu, KWA KUBONYEZA BONYEZA HAPA
na
kujaza fomu kisha bofya “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu.
Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja
kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kijitabu
cha wiki hii ni “Ultimate Trading Systems” kutoka kwa mwandishi David Jenyns.
Katika kijitabu hiki mwandishi anatushirikisha mbinu mbalimbali za ukuaji wa
kibiashara.
Karibu
tujifunze machache kati ya mengi ambayo mwandishi Robert Kiyosaki
anatushirikisha katika kitabu hiki:
1. Ili ufanikiwe kibiashara ni
lazima uwe na msukumo/hamasa kubwa ya kwanini unataka kufanikiwa kibiashara. Mwandishi
anatushirikisha kuwa ukiwa na sababu kubwa za kwanini unahitaji kufanikiwa
kibiashara ni rahisi kupenya kwenye changamoto zote za kibiashara. Jiulize kwa
nini unataka kuwa mfanyabiashara.
2. Mafanikio ya kibiashara hayana
ubaguzi wa aina ya rangi, sehemu unayotoka, kiwango cha elimu wala historia ya
maisha yako bali kila mtu anaweza kufanikiwa kibiashara endapo atafuata mbinu
za mafanikio ya biashara na mbinu hizi zipo wazi kwa kila mtu.
3. Takwimu
zinaonyesha kuwa watu wengi wanapoteza fedha katika biashara na hivyo kupelekea
kuanguka kibiashara. Hali hii imepelekea watu wengi kuogopa kuanzisha biashara
kwa vile wanahisi watapoteza fedha. Ukweli ni kwamba kama unafahamu mbinu za
kibiashara na kuzitumia mbinu husika kwenye biashara yako nafasi ya kufanikiwa
kibiashara ni kubwa sana.
4. Kama
haujifunzi kutoka kwa wengine waliofanikiwa kibiashara au kuwa na mwalimu wako
kwenye masuala ya biashara daima utaendelea kurudia makosa yale yale. Hii ina
maana kuwa kufanikiwa kibiashara itakuwa na ndoto kwako.
5. Saikolojia
ya mafanikio ya kibiashara ndio sababu pekee inayotofautisha watu wenye
mafanikio na watu wa kawaida. Mwandishi anatushirikisha kuwa saikolojia katika
mafanikio inachukua asilimia 60 ikifuatiwa na udhibiti wa pesa ambao ni
asilimia 30 na asilimia kumi iliyobaki ni inategemea mfumo wa biashara au
mazingira ya kazi. Kutokana utafiti huu, katika biashara kwanza kabisa ni
lazima ujiweke sawa kisaikolojia. Na saikolojia inabeba hisia zako zote kwenye
mazingira yanayokuzunguka.
6. Muda
wote katika biashara mfanyabiashara ni lazima ulenge kuongeza faida pamoja na
kupunguza hali hatarishi katika uwekezaji wako. Hata hivyo, lengo hili linaweza
lisifikiwe kutokana na hisia zako kama vile matumaini, uoga, hofu, ubinafsi,
uchoyo au wivu wa kibiashara. Mara zote watu wanaofanya maamuzi kwa kuongozwa
na hisia uishia kupata matokeo ya ovyo.
7. Hofu
ya kupoteza inawafanya wafanyabiashara wengi kupoteza fursa ambazo ni sawa na
mara mbili ya kile wanachohofia kupoteza. Mfano, kama ulihitaji kuwekeza
shilingi milioni moja na mwisho ukashindwa kufanya hivyo kwa sababu ya hofu,
matokeo yake ni kwamba umepoteza fursa yenye thamani ya mara mbili ya shilingi
milioni moja. Somo kubwa hapa ni kwamba hisia zako zina nafasi kubwa ya kuamua
mafanikio yako ya biashara.
8. Nidhamu
ndo dawa pekee ya kutibu maamuzi ya kihisia. Kwanza kabisa ni lazima uwe na
nidhamu binafsi ambayo itakuongoza kukabiliana na maamuzi ya kihisia. Pia,
unahitaji kuwa na nidhamu ya kujifunza mara kwa mara – kamwe husiridhike na
mafanikio uliyonayo.
9. Kufanikiwa
kibiashara ni lazima uwe ni kanuni na sheria za kibiashara ambazo umejiwekea
mwenyewe katika maisha yako ya kila siku.
Kanuni na sheria hizi ndo zinatakiwa kuwa mwongozo wako katika maamuzi yote
ya kibiashara.
10.
Nidhamu kwa ajili ya kudhibiti hisia zako
kibiashara ni muhimu kuliko kitu chochote kile. Hii ni kutokana na ukweli
kwamba tabia mbaya ambazo utazifanya kwenye biashara zitadhibitiwa na soko
husika na matokeo yake zitakurudia katika mfumo wa kupoteza faida au kupoteza
mtaji wako.
11.
Kila mfanyabiashara aliyefanikiwa ni
lazima awe na mfumo au njia ambazo zimepelekea afanikiwe kibiashara. Mfumo huu
unakuwa ni siri ya mafanikio yake na kupitia mfumo huo anaendelea kufanikisha
hatua zaidi. Unaweza kujifunza mifumo kutoka kwa watu wengine ikafanya kazi
kwako au pengine ikashindwa kukufikisha kwenye hatua unazotamani. Muhimu ni
kutengeneza mfumo wako wa mafanikio ya biashara na kuutumia mfumo husika katika
masoko ya biashara.
12.
Katika kutengeneza mfumo wako wa
kibiashara ni lazima uzingatie mfumo ambao unaupenda kutoka rohoni na mfumo huu
uwe na uwezo wa kuongeza ukauaji wako wa biashara badala ya kuwa mfumo
kandamizi. Njia bora ya kufanikisha katika kutengeneza mfumo wako wa biashara
ni kupitia tathimini ya malengo yako ya biashara.
13.
Mfumo wako wa biashara ni lazima
uendane na jitihada/bidii zako za kila siku katika kufikia mafanikio ya
kibiashara. Hii ina maana kwamba mfumo wako wa kibiashara ni lazima uzingatie
namna ambavyo umejipanga kuweka bidii kwa ajili ya mafanikio. Hakuna mfumo
ambao utafanya kazi wenyewe bila jitihada/bidii zako.
14.
Ili ufanikiwe kibiashara ni lazima
kwanza uchague soko sahihi na bidhaa sahihi kwa wakati sahihi. Mwandishi
anatushirikisha kuwa watu wengi wanaanguka kibiashara kwa vile wanashindwa
kuoanisha bidhaa, soko pamoja na nyakati husika. Kuna bidhaa ambayo itafanya
vyema kwenye soko moja na ishindwe kufanya vyema katika soko jingine vivyo
hivyo kuna bidhaa ambayo ilikuwa inafanya vyema siku za nyuma lakini kwa sasa
haifai tena. Pia, hapa ni muhimu kuuza bidhaa moja kwenye soko kuliko
kuchanganya kila kitu.
15.
Daima kwenye soko unatakiwa kufanya
biashara kwa kigezo cha kwamba haujui hali ya soko kwa nyakati zijazo. Kupanda
na kushuka kwa mahitaji ya bidhaa au thamani ya hisa ni kawaida sana katika
soko lolote, japo ni vigumu sana kwa mfanyabiashara kutabiri hali ya soko kwa
siku zijazo. Hapa ndipo unatakiwa kuwa makini katika maamuzi yako ili
yasiendeshwe na mazoea.
16.
Ili ufanikiwe katika kufanya maamuzi
kwa mazoea unatakiwa uwe na mpango wa kibiashara yako (trading plan). Maamuzi
yako yote yanatakiwa yafanywe kwa kuzingatia mpango wako wa biashara. Mpango
huu unatumika kama dira ya kukuongoza katika kipindi chote cha biashara bila
kujali kupanda na kushuka kwa soko.
17.
Unapotengeneza mpango wa kibiashara ni
lazima uzingatie mfumo wa biashara yako. Mpango wa biashara ni lazima uendane
na mfumo wa biashara na hivyo ni rahisi kupenya kwenye soko kwa kutumia vitu
hivi viwili bila kujali mawimbi ya soko.
18.
Mpango wako wa ufanyaji biashara ni
lazima uwe na kipengele cha udhibiti wa fedha. Mwandishi anatushirikisha kuwa
kama mfanyabiashara kitu pekee ambacho unaweza kudhibiti katika soko ni fedha
zako. Hapa ni unatakiwa kuwa makini na dili za kibiashara ambazo unafanya.
Daima epuka dili ambazo tija yake ni ndogo au zitasababisha hasara kubwa. Kwa
ujumla katika udhibiti wa fedha ni lazima utengeneze kanuni ambazo
zitakuongezea nafasi ya kushinda kifedha huku zikikusaidia kupunguza nafasi za
kupoteza fedha zako.
19.
Chagua mtandao sahihi au mfumo wa
kompyuta sahihi kwa biashara yako. Mwandishi anatushirikisha kuwa siku mambo
mengi yanaendeshwa kwa mfumo wa kompyuta, hivyo hakuna namna utaweza kuendesha
biashara yenye mafanikio bila kutumia mfumo wa kompyuta.
20.
Pale inapobidi chagua wakala bora
kwenye biashara unayofanya. Mfano, kama ni kwenye uwekezaji wa hisa ni vyema
ukachagua wakala ambaye anaonekana kufanya vyema ili awe kiungo sahihi kati
yako na soko.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link). Nakutakia
mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com
|