Habari
ya leo rafiki yangu na msomaji wa mtandao wa Fikra za Kitajiri. Ni matumaini yangu
kuwa una afya njema na mapambano yanaendelea kwa ajili ya kuifanya kesho yako iwe
bora zaidi ya leo. Leo hii katika makala za kila wiki nakuletea makala maalumu kwa
ajili yakufikisha nasaha zangu kwa wanafunzi wote waliojiunga na vyuo mbalimbali
kwa ajili ya masomo yao ya elimu ya juu. Wewe kama unafuatilia mtandao huu na sio
mlengwa wa makala hii naomba tu unisaidie kuisambaza kwa walengwa kwa kadri unavyoweza.
Kabla
ya kuanza barua yangu ningependa nianze kwa kujitambulisha ili ifahamike kuwa anayeandika
makala hii ni nani. Kwa majina anaitwa Augustine
Mathias Bilondwa, ni mwajiriwa na mjasiliamali, ambaye alihitimu elimu yake
ya uzamili (Masters Degree) katika Chuo Kikuu cha Sokoine mwaka 2015 ambako pia
alihitimu elimu yake ya digrii ya kwanza mwaka 2011 katika fani ya sayansi ya misitu.
Baada
ya kumfahamu japo kidogo nina ni huyu anayekuandikia barua hii ya wazi sasa angependa
akushirikishe machache ambayo roho yake inamsukuma afikishe ujumbe huu kwako kwa
ajili ya kupanua ufahamu wako katika safari yako yote uwapo unaitafuta elimu ya
juu.
Nianze
kwa kuweka wazi kuwa barua hii ya wazi haitoi mwongozo wa namna gani unatakiwa kuhishi
kwa ajili ya kufaulu masomo ya elimu yako la hasha. Lengo la barua hii ni kukuongoza
namna gani unatakiwa kuishi kwa ajili ya kufanikiwa kimaisha nyakati zote ukiwa
Chuoni na hata maisha baada yachuo.
Kwa
ufupi nahitaji utambue kuwa namna unatavyoishi
kwa mafanikio kwenye haya nitakayo kushirikisha ndivyo utakuwa umeweka msingi imara
wa maisha yako na hata baada ya kumaliza chuo msingi huu hautayumbishwa na mawimbi
ya aina yoyote ile katika maisha yako yote.
Rafiki
kazana na masomo yako ambayo umejiunga nayo lakini nisaidie kutekeleza haya kwa
ajili ya ufanisi wa maisha yako na jamii kwa ujumla:-
Moja, wekeza sana kuitafuta elimu ambayo
inalenga kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii yetu. Rafiki,
uwapo Chuoni utakutana na mazingira ambayo yatakufanya usome kwa ajili ya kujibia
mitihani badala ya kusoma kuelewa. Nakusihi sana kila unachojifunza jitahidi kujiuliza
ni namna gani unaweza kutumia elimu yake kwenye mazingira ya jamii inayo kuzunguka.
Katika kufanya hivyo unahitaji kuwa na picha ya familia yako ambayo umeiacha nyumbani
pamoja na picha ya changamoto zilizopo kwenye jamii yako. Picha hiyo iwe chachu
ya kujifunza na kuelewa na hatimaye kutafsiri elimu husika kwa vitendo. Tumia elimu
hiyo kwa ajili ya kutatua changamoto za umasikini, maradhi na magonjwa, tumia elimu
hiyo kwa ajili ya kuboresha mbinu za uzalishaji na hata kuboresha mbinu za
mawasiliano. Kwa ujumla jamii inahitaji kupata kitu cha ziada kutoka kwako hivyo
huna budi kuwa mfano bora kupitia yale unayojifunza na kuyatafsiri kwa vitendo.
Mbili, jilipe kwanza kwenye kila shilingi
inayoingia mikononi mwako kupitia ‘Boom’
au chanzo chochote halali. Hapa
namaanisha uwekezaji kwa kila shilingi inayoingia mikononi mwako. Husikubali kutumia
hela yote unayopata bila kutenga asilimia yake kwa ajili ya uwekezaji. Kwa
bahati mbaya sana elimu hii ya uwekezaji kwa maana ya elimu ya pesa pengine hujawahi
kufundishwa mahali popote na ni mategemeo yangu kuwa hata katika masomo uliyo chagua
hakuna sehemu ambayo utafundishwa elimu hii kwa ufasaha. Hii ni kutokana na ukweli
kuwa mitahala ya elimu yetu na hata nchi nyingi haijaweza kufundisha elimu hii kama
inavyotakiwa. Kutokana na elimu hii kutofundishwa kwa
ufasaha tumekuwa tukifanya maamuzi yenye makosa katika suala zima la utawala wa
fedha (financial management) na hivyo kuendelea kuwa kwenye mzunguko wa
umasikini pasipo kujali kiwango cha elimu tulichonacho.
Rafiki
yangu katika kujilipa kwanza nahitaji uwe na utamaduni wa kutenga asilimia 10
au 20% ya kila fedha inayoingia mikononi mwaka kwa ajili ya uwekezaji wa muda
mfupi na muda mrefu. Unaweza ukafungua akaunti maalumu benki kwa ajili ya
kuwekeza fedha hizo au ukanunua hisa za makampuni yanayofanya vizuri kwenye
soko au ukafungua akaunti ya Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja (Mf. Mfuko wa Umoja)
au ukanunua Dhamana za Serikali (Government Bonds). Kumbuka, katika yote hakikisha
unawekeza fedha zako sehemu ambapo zitaongezeka kwa muda kupitia ongezeko la
riba.
Rafiki
kama maneno haya yamekuwa magumu kwako jitahidi sana kuyapa nafasi katika muda
wako wa ziada ili kuhakikisha unachimba kwa undani ili uyafahamu kwa kina. Kumbuka
ni kupitia uwekezaji utafanikiwa kuwa na maisha yenye uhuru wa kifedha (financial
freedom) ambao naamini kuwa ndio ndoto yako kubwa.
Tatu, husikubali kuwa mtumwa wa
teknolojia ya mawasiliano. Rafiki bahati nzuri
sana umeingia Chuoni wakati ambao mapinduzi ya teknolojia ya mawasiliano yapo
kwenye kilele chake na pengine bado uvumbuzi wa teknolojia hii unakuja zaidi ya
sasa. Rafiki natambua kuwa ni katika kipindi hiki utahitaji kumiliki simu janja
hata kama hukuwahi kuimiliki hapo nyuma. Nakuomba sana rafiki ufahamu kuwa simu
janja hizi zimewafanya watu wengi kuwa watumwa kiuchumi, kiakili, kifikra na
hata kiutamaduni. Rafiki fahamu kuwa watu hawa wamekuwa watumwa bila ya wao
kutambua kuwa ni watumwa.
Utumwa
huu unatokana na mitandao ya kijamii waliojiunga nayo kwenye simu zao. Mitandao
hii kwa kutaja tu michache ni kama WhatsApp, Facebook, Insta na mingineyo. Rafiki
ni katika mitandao hii unakuta watu hawa wana makundi zaidi ya kumi na yote
hakuna hata moja ambalo linajadiri mambo ya maana hisipokuwa ni udaku tu. Rafiki
kuwa unapokuwa na simu janja chagua makundi yanayoendana na vipaumbele vya
maisha yako na sio tu kujiunga na makundi ya umbea na kusambaza picha na video
sizizo kuwa na maana.
Rafiki
kumbuka kuwa makundi haya si tu yanakupotezea muda kutokana na kushabikia
meseji zisizokuwa na maana bali yanasababisha kuwa na bajeti kubwa ya
mawasiliano na mtandao. Hii inatokana na ukweli kwamba kadri unavyofungua video
au ujumbe wenye mb 200 ndivyo na kifurushi
chako ulichojiunga kupitia simu yako kinavyopungua mb 200 hizo hizo.
Soma: BARUA YANGU YA WAZI KWA WAHITIMU WA VYUO
Soma: BARUA YANGU YA WAZI KWA WAHITIMU WA VYUO
Nne, kuwa na vipaumbele vyako
husikubali kupelekeshwa na makundi ya marafiki wapya. Rafiki nimekuwa Chuoni kwa muda wa miaka mitano na
katika kipindi hicho chote nimeona vijana wengi wanaokuja wakiwa vijana wazuri
na wapenda dini kulingana na imani zao. Hata hivyo, baada ya miezi michache
vijana hawa waliangukia kwenye mikono ya Dunia hisiyo mizuri kwa vile
walishindwa kuchagua marafiki wema. Rafiki kumbuka kuwa sasa wewe ni mtu mzima kwa
maana sasa unajua ni kipi bora na kipi sio bora katika maisha yako na hapa
ndipo tunasema kuwa tayari unajitambua. Rafiki kama bado hauna vipaumbele vya
maisha yako nachelea kusema kuwa bado hujafikia hatua ya kuwa mtu mzima.
Rafiki
kipindi chote uwapo Chuoni unahitaji kuwa na vipaumbele vya maisha yako na
kuhakikisha kila siku unaishi kulingana na vipaumbele hivyo. Rafiki hapa ndipo
unahitaji kukubali kuwa tofauti na wenzako ili mradi tu uwe kwenye mstari
sahihi. Kamwe husikubali kujiunga kwenye kundi ambalo unaona ni kinyume na
vipaumbele vyako kwa vile tu umeshawishiwa na marafiki. Kamwe husikubali
kufanya au kushiriki kwenye matukio ya aina yoyote ambayo ni kinyume na
vipaumbele vyako kwa vile tu umeona wenzako wanafanya hivyo. Daima kubali
kujitofautisha na wenzio hakika rafiki utafika mbali.
Tano, tenga muda wa kujisomea kwa ajili
ya maarifa ya ziada nje ya kozi unayosoma. Rafiki
nakusihi sana utenge muda wa kujisomea vitabu vya maarifa mbalimbali. Kama ambavyo
nimekusisitiza kwenye umuhimu wa kujitambua, rafiki hauwezi kujitambua kama
hauna muda wa kuboresha ubongo wako. Rafiki kumbuka kuwa ubongo wa mwanadamu ni
kiungo ambacho kinahitaji kuendelezwa kwa
kupata maarifa mbalimbali.
Hivyo,
rafiki katika muda wako wa elimu ya juu unahitaji kuwa na muda wa kujisomea
vitabu vya maarifa mbalimbali. Hii ni pamoja na kujisoma vitabu kuhusu
mwanadamu kwa ujumla wake (mahusiano, kazi na historia), vitabu vya biashara,
vitabu vya dini na vitabu falsafa mbalimbali. Hakika kama utafanikiwa kwenye
hili utakuwa umeweka msingi imara katika maisha yako na kamwe ubongo wako
hautazeeka.
Sita, lenga kuzalisha ajira zaidi
kuliko kulenga kujiariwa hata mara baada ya kumaliza masomo. Kujiajiri ni bora zaidi kuliko kuajiliwa kwa vile
kujiajiri kunakuweka huru zaidi katika fani ambayo umechagua kufanya. Rafiki najua
kwa sasa umeingia Chuoni ukiwa na ndoto kuwa pindi utakapomaliza masomo yako
utapata ajira kwa ajili ya kupata mahitaji yako muhimu. Vilevile natambua kuwa
umechagua kozi hiyo kwa kujua kuwa kozi hiyo ndo yenye uhakika wa ajira au
pengine kozi uliyochagua unajihisi kuwa umekosea unajutia kuwa sehemu ya
wanafunzi wanaosoma kozi hiyo.
Rafiki ukweli ni kwamba ajira kwa sasa
zimepungua kwa fani zote ukilinganisha na miaka ya nyuma. Hii ni kutokana na
idadi ya vyuo kuongezeka ambayo imepelekea kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi
wanaomaliza. Rafiki katika miaka
yako yote Chuoni fikiria kujiajiri na kutengeneza ajira kwa wengine kwani
uzoefu unaonesha kuwa hata waliopo kwenye ajira hawana uhuru wa kifedha.
Rafiki
namalizia kwa kukuombea uwe na afya njema katika masomo yako. Pia, nakuombea
upate roho wa kukuongoza kusoma barua hii ya wazi mara kwa mara ili kadri
unavyoisoma uitafakari kwa macho ya ndani.
Karibuni kwenye Fikra za Kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com
|