Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri.
Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa
FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa
ni wiki ya 30 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi
wa vitabu mbalimbali kwa ajili ya kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako
kuyatumia ili ubadilishe kila sekta ya maisha yako.
Ni matumaini yangu kuwa makala hizi
zimekuwa na msaada mkubwa kwako kwa kadri ambavyo umekuwa ukichukua hatua za
kubadilisha maisha yako. Hata hivyo, makala hizi haziwezi kubadilisha chochote
kama umekuwa mtu wa kusoma na kutokufanyia kazi yale unayojifunza.
Ili uendelee kunufaika na makala za
mtandao huu BONYEZA HAPA na
ujaze fomu kisha bonyeza “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao wa
fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa
humu moja kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “Power of Motivation” kutoka
kwa mwandishi Michael Bolduc. Mwandishi ni muhamasishaji na mzungumzaji
maarufu ambaye amekuwa mstari wa mbele kuwaongoza watu ili waishi maisha ya
mafanikio ya ndoto zao. Kupitia kitabu hiki mwandishi anatushirikisha mbinu
ambazo zinaweza kutumiwa na kila mtu kwa ajili ya kufikia mafanikio
anayoyatamani kwenye kila sekta ya maisha yake.
Mwandishi
alipata msukumo wa kuandika kitabua hiki mara baada kuona kuwa taarifa za jinsi
gani kila mtu anaweza kufanikiwa zipo kila mahali na zinapatikana kwa urahisi
lakini watu wenye mafanikio bado ni wachache. Pamoja na kwamba watu wanafahamu
ni kipi wanatakiwa kufanya ili wafanikiwe lakini watu hawa bado hawafanyi kile
wanachotakiwa kufanya kwa ajili ya mafanikio yao. Kutokana na hali hii ndipo
mwandishi aligundua kuwa njia pekee ya kumwezesha mtu kufanya kile anachohitaji
kufanya kwanza ni kuwa na msukumo/hamasa.
Karibu
tujifunze wote machache niliyojifunza kwenye hiki:
1. Watu
wengi wanahitaji mafanikio lakini ni wachache ambao wapo tayari kubadilisha
tabia zao. Mwandishi anatushirikisha kuwa kutaka mafanikio ni hatua moja lakini
hatua muhimu ni ile ya kujiuliza swali hili “ili nifakiwe natakiwa kubadilisha nini katika maisha niliyozoea?”. Hapa ndipo panakuwa pagumu kwa watu wengi
kwani ni wachache ambao wapo tayari kubadilisha tabia zao. Kupata mafanikio ni
lazima kwanza ujikane na uwe tayari kufanya kazi kwa bidii japo cha kushangaza
ni kwamba watu wanahitaji kupata mafanikio lakini hawahitaji kufanya chochote
ambacho kitawapa mafanikio ya ndoto zao.
2. Sio
kweli kwamba hauna maarifa na ndio maana haujafanikisha ndoto zako bali
haujafakisha ndoto zako kwa kuwa umekosa nguvu ya hamasa/msukumo binafsi kwa
ajili ya kufanya kile ambacho watu wenye mafanikio wamefanya. Ili ufanikiwe ni
lazima kwanza ukubali kupata maumivu kabla ya kutimiza malengo yako. Ili ufanikiwe
ni lazima kwanza uwe tayari kudhibiti hisia za maumivu na starehe. Kama wewe
unaona kufanya kazi kwako ni maumivu basi tambua kuwa mafanikio utaishia
kuyaimba tu. Pia kama wewe unatawaliwa na hisia za kujirusha kwenye starehe kwa
kila shilingi au muda unaopata kamwe husitegemee kupata mafanikio.
3. Matamanio
ni nguzo muhimu katika kufanikisha kila sehemu ya maisha ya muhusika. Kama una
matamanio ya chini utaishia kupata mafanikio ya chini na kama una matamanio ya
juu ni lazima utapata mafanikio makubwa. Kumbuka kuwa kupata mafanikio ya matamanio
yako ni lazima uwe tayari kuzishinda hofu zako. Pia, mara zote unatakiwa
kutambua kuwa kila unaposhindwa kufikia malengo ni matokeo ya kuruhusu matamanio
ya chini yatawale matamanio ya juu. Mfano ni kawaida watu kushindwa kuchukua
hatua kwa vile wanahisi hatua husika zitapelekea maumivu ya mwili na hivyo
wanajisemea rohoni kuwa hawapo tayari kuumia na matokeo yake ni kuendelea
kuishi maisha yao ya kawaida.
4. Mara
zote tunasindwa kuchukua hatua kwa vile tunashindwa kudhibit hofu zetu juu ya
hatua tunazokusudia kuchukua. Hofu inaweza kutudidimiza au kutuinua kwa
kutegemea hofu yetu ipo katika kundi lipi. Kundi la kwanza ni lile ambalo hofu
inatuzuia kuchukua hatua; hapa ndipo nguvu ya hamasa/msukumo inapofanya kazi ya
kutuangamiza. Kwa vile hatuamini uwezo wetu matokeo yake tunashindwa kuchukua
hatua kwa vile tunaogopa kushindwa.
Kundi la pili ni
pale ambapo hofu inatusukuma kuchukua hatua. Mfano kama unaogopa njaa utafanya
jitihada za kuhakikisha unalima ili upate akiba ya chakula. Kutokana na ukweli
huu kumbe tunaweza kuitumia hofu kwa ajili ya faida badala ya kuwa na hofu ya
kutuzuia kuchukua. Hivyo, kadri unavyotambua kuwa hofu inaweza kutumiwa kwa
faida yako ndivyo utaitumia kwa ajili ya kufanikisha ndoto zako. Kubali
kuitumia hofu kwa faida yako na sio hofu ikutumie wewe.
5. Tangeneza
sababu ambazo ni msukumo wako wa kufanikiwa kwenye kila sekta husika. Mwandishi
anatushirikisha kuwa kama hauna sababu ambazo zinakusukuma kuhitaji
ushindi/mafanikio kamwe hauwezi kufanikiwa. Hivyo, unahitaji kujiliuza maswali
kama endapo nitashindwa kufanikiwa ni athari zipi ambazo zitanipata. Mfano,
sababu moja ambayo inaweza kuwa msukumo wa kupata uhuru wa kifedha ni yale
mahitaji muhimu ya kifedha katika maisha yako ya kila siku kama vile mahitaji
ya chakula, maradhi, ada za nyumba, ada za watoto kwa ajili ya kwenda shule
n.k. Hapa unahitaji kutengeneza orodha ya visababishi vikuu vya kwanini
unahitaji kufanikiwa katika kila sekta ya maisha yako.
6. Fahamu
kuwa mafanikio ni zao la muunganiko wa mahusiano kati ya shauku ya mafanikio
uliyonayo na hisia zako juu ya kuumiza/kuupa raha mwili wako. Muunganiko huu ni
kazi ya ubongo wa kila mwanadamu ambao ufanya kazi ya kutafsiri fikra na
hatimaye mwili unaitikia kwa ajili ya vitendo. Habari njema ni kwamba kila
mwandamu anaweza kudhibiti fikra zake ili mara zote ubongo ufanyie kazi zenye
manufaa pekee na kuachana na fikra za hovyo. Hapa ndipo utagundua kuwa tofauti
kubwa kati ya watu wenye mafanikio na watu wa kawaida ni utashi wa kukamilisha
kile kinachotakiwa kufanyika kwa ajili ya kufanikiwa katika sekta huska. Watu wenye
mafanikio wanafanya hatua za ziada ambazo kwa watu wa kawaida wanaona hatua
hizo ni kujitesa au kujibana. Mfano, kama unahitaji kupunguza mwili ni lazima
uwe tayari kufanya mazoezi na kudhibiti mfumo wako wa chakula na si vinginevyo.
7. Kila
mmoja anahitaji maisha yenye furaha na ili uishi maisha ya furaha kwa sasa ni
lazima uwe na tumaini kuwa kesho na kesho kutwa itakuwa bora kuliko leo. Hii ndio
sababu ya kila mtu kutaka kuendelea kuishi vinginevyo kama mtu angetegemea
kesho hali kuwa mbaya zaidi ya leo hakuna ambaye angetamani kuendelea kuishi. Kutokana
na ukweli huu ili ufanikiwe ni lazima uwe na tumaini ndani mwako kuwa kesho na
kesho kutwa utakuwa na mafanikio bora kwenye kila sekta ya maisha yako ikilingwanishwa
na sasa. Hii ndio injini ya mafanikio kwani ukishakuwa na tumaini la namna hii
unaanza kujibidisha kuchukua hatua kwa ajili ya kuboresha maisha yako.
8. Furaha/huzuni
utengenezwa na kila mtu kulingana na matendo yake ya kila siku. Kutokana na
ukweli huu watu wanaotaka kuwa na maisha ya furaha wanachagua kufanya matendo
ambayo yanaleta furaha na wale ambao wanaishi maisha ya huzuni ni matokeo ya
matendo yao ya kila siku. Hapa tunatakiwa kutofautisha furaha na starehe; furaha
ni kuridhika kwa roho/nafsi kwa muda mrefu wakati starehe ni ile hali
kujiridhisha kwa muda na mara nyingi uambatana na tamaa/hanasa za kuridhisha
mwili.
9. Hisia
zote za mwanadamu zinaweza kugawanjwa katika makundi mawili ambayo ni hisia za upendo
na hisia za hofu. Kuumia, huzuni, hasira, visasi, kinyongo, kukata tamaa,
kutojiamini au msongo wa mawazo zote hizi ni chimbuko la hisia za hofu. Mtu mwenye
hisia za mapenzi mara nyingi anatawaliwa na matendo ya furaha, hamasa, kusaidia
wengine, amani na faraja. Kwa ujumla hisia za mapenzi zinamfanya mhusika
ajisikie mwenye faraja na mwenye kutamani aendelee kuishi siku zote. Hivyo, ili
tufanikiwe ni lazima tuwe na hisia za upendo huku tukiongozwa na matarajio
chanya ya baadae. Pia, unatakiwa kufahamu kuwa kama unaitazama kesho yako kwa
maono hasi itakuwa vigumu kwako kupata mafanikio.
10. Kila mwanadamu anapitia kwenye nyakati
za juu na nyakati za chini. Nyakati za juu zina kila aina ya mafanikio kulingana
na juhudi za mhusika na nyakati za chini mara nyingi zimejaa kila aina ya
dalili za kukatishwa tamaa na kushindwa. Ushindi kwa kila mtu unategemea na
nguvu aliyonayo katika kukabiliana na nyakati ngumu. Kama mtu atakubaliana na
hali ya nyakati za chini basi mara zote maisha yake yote yatazungukwa na
nyakati ngumu na hivyo kwake ni vigumu kupata mafanikio anayotamani maishani
mwake. Njia pekee ya kujikwamua kwenye nyakati ngumu ni kufanya matendo mema
ambayo yanapingana na nyakati hizo na matokeo yake ni faraja na furaha kwenye
kila sekta ya maisha yetu.
11. Njia pekee ya kuendelea kuelea kwenye
nyakati za chini ni kuacha kujifunza. Mwandishi anatushirikisha kuwa ni kupitia
kujifunza vitu vipya kila mtu anaweza kujikwamua kutoka kwenye nyakati za chini.
Hata hivyo, katika kila hatua unahitaji kuongozwa na Roho Mtakatifu na ndio
maana kila mtu anahitaji kuwa na imani thabiti ambayo ndio mwongozo wa pekee katika
nyakati anazopitia. Pia, unahitaji kukumbuka kuwa njia pekee ya kuishi maisha
ya faraja na furaha ni kuendelea kuzungukwa na matendo ya nyakati za juu.
12. Hamasa inagawanyika katika makundi
mawili ambayo ni hamasa ya kibiolojia (hamasa kutoka ndani mwetu) na hamasa ya
kijamii (hamasa ya nje). Hamasa ya ndani ndio msingi wa kufahamu kwa nini watu
wanafanya yale wanayofanya na kwa nini watu wengine hawafanyi kile
wanachohitaji kufanya. Hapa ndipo tunahitaji kufahamu kuwa hamasa ya ndani ndio
inawaongoza watu kufanikiwa na kadri wanavyofanikisha hatua moja hamasa hii
inawapeleka kwenye mahitaji ya juu zaidi. Mara nyingi hamasa hii ya ndani
inaongozwa na ile hali ya kuhitaji kujikomboa kwenye hali ngumu ya maisha. Kadri
tunavyohusianisha furaha ya maisha itokanayo na ushindi wa yale tunayotamani
kufanya ndivyo tunakuwa na nafasi kubwa kufanikisha matamanio yetu. Hamasa ya
nje inajumuisha yale tunayotamani katika maisha yetu kutokana na mafanikio ya
watu ambao wamefanikiwa katika sekta hizo.
13. Kujenga picha akilini juu ya kile
ambacho unahitaji kukamilisha ni njia ya haraka na uhakika wa kumwezesha mhusika
kufanikisha ndoto yake. Njia hii ndio inamfanya mtu kuwa na maono chanya juu ya
maisha yake ya baadae na hivyo inawatofautisha watu wenye mafanikio na wale wenye
maisha ya kawaida. Kwa ujumla mwandishi anatushirikisha kuwa sisi ni zao la
yale tunayoyajaza na kuyajengea picha katika akili zetu kwa muda mrefu. Kutokana
na ukweli huu maisha yetu yanadhihirisha kile ambacho tunawaza mara kwa mara
katika akili zetu.
14. Mfumo wa kuweka malengo kwa muda mrefu
umeongelewa kila mahali kama njia ya kufanikisha ndoto za mhusika. Hata hivyo, asilimia
kubwa ya watu wanaoweka malengo huwa hawatimizi kama walivyokusudia. Makosa ambayo
watu wanafanya na hatimaye kuwafanya washindiwe kufikia malengo ni pamoja na (1)
kushindwa kujiwekea malengo ya kila siku – ni muhimu kujipima kila siku kama
unatekeleza malengo yako (2) kujiwekea malengo magumu ambayo siyo rahisi
kuyaamini – kama lengo hauliamini katika akili yako kamwe hauwezi kulitekeleza na
(3) kujiwekea malengo ambayo hayakupi hamasa – lengo ni lazima liwe na msukumo
wa kukutaka uchukue hatua ya ziada.
15. Kama unahitaji kuwa na furaha maishani
mwako kamwe hauwezi kukwepa kuweka sawa malengo yako ya kifedha. Unahitaji kutengeneza
mpango wako wa masuala ya fedha ili utumike kama njia ya kukuelekeza kwenye
uhuru wa kifedha. Njia pekee ya kufanikisha uhuru wa kifedha ni kuhakikisha
matumizi yako yanakuwa chini ikilinganishwa na kipato chako na hatimaye hakikisha
unawekeza salio ili lizae faida na wekeza faida hiyo kwa ajili ya kukuza
utajiri wako. Na hii ndio njia ya kuifanya pesa itufanyie kazi badala ya sisi
kufanya kazi kwa ajili ya kupata pesa. Tatizo ambalo limelepekea watu wengi
kuwa masikini ni kuruhusu matumizi yao yawe juu kuliko pato lao na matokeo yake
ni kuendelea kufanya kazi ili wapate pesa.
16. Hakuna njia ya mkato ya kuwa tajiri
bali unahitaji kutumia hamasa kwa mujibu wa mafundisho ya kitabu hiki
kutengeneza utajiri wa ndoto yako. Mwandishi anatushirikisha hatua nane ambazo
kila mtu anaweza kutumia kwa ajili ya kutengeneza utajiri wa ndoto yake (1) furahia
hatua unazochukua kwa ajili ya kutimiza ndoto zako – hapa unahitaji kufurahia
hatua zako za kujidhibiti ili matumizi yako yawe chini ya pato lako (2) tengeneza
mpango wa uhakika kwa ajili ya kukuza kipato chako – epuka udanganyifu wa
kupata fedha za haraka bila mpango (3) epuka maisha ya kuridhika – ainaisha tabia
ambazo zimekufikisha hapo ulipo na anza kukabiliana nazo mara moja (4) kuwa
makini na sehemu unazowekeza – wekeza sehemu ambayo uhakika wa kupata faida upo
juu (5) ongeza mifereji ya fedha na punguza gharama za uendeshaji (6) fuatilia
kwa makini maendeleo ya uwekezaji wako (7) endelea kuwa na msukumo/hamasa ya
kuendelea kutengeneza kipato zaidi, na (8) tafuta timu ya wataalamu washauri
katika uwekezaji wako.
17. Hauwezi kuwa na maisha yenye hamasa na
furaha kama mwili wako hauna nguvu au unasumbuliwa na magonjwa. Unahitaji kutengeneza
mpango wako wa kiafya kwa ajili ya kukuongoza kwenye afya ya mwili wako. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba nguvu ndo injini ya kila unalofanya, kama hauna nguvu
moja kwa moja na uzalishaji wako utakuwa chini. Afya ya mwili inategemea na
tabia zako kwenye vitu vitatu (a) chakula – vyakula/vinywaji unavyotumia vina
nafasi kubwa ya kuamua hali ya afya yako, (b) mfumo wa maisha yako – hii inajumuisha
ratiba zako kuanzia shughuli unazofanya na namna unavyofanya mazoezi ya viungo
na (c) kuzingatia kanuni muhimu za afya – unahitaji kuhakikisha unahishi kwenye
mazingira safi, unavuta hewa safi, unatumia maji safi, unapumzika muda wa
kutosha n.k.
18. Ufunguo pekee wa mafanikio ni mhusika
kuwa na kiu ya mafanikio kuliko kitu chochote kile hata kuliko maisha yenyewe. Na
hapa ndipo tunapata hatua nne za kufikia mafanikio tunayotamani (1) kwanza
unahitaji kutambua ni kipi unahitaji kwa ajili ya kukamilisha ndoto zako (2)
unahitaji kuchukua hatua thabiti kwa ajili ya kufikia kile unachohitaji – kuwa mtu
wa vitendo (3) tambua ni njia ipi inafanya kazi na ipi haifanyi kazi na
hatimaye tuliza akili zako kwenye njia ambazo zimedhihirisha ufanisi wa matokeo
bora na (4) badilisha mbinu mpaka pale utakapo kuwa umefanikiwa – epuka kuendelea
kurudia njia ile ile huku ukitegemea kupata matokeo tofauti.
19. Kila mtu kwa asili ya uumbaji amepewa
mamlaka makubwa ya kuumba na kuharibu vitu. Na hivyo katika ulimwengu watu wote
wamegawanyika katika makundi mawili ya waumbaji na watu wanao haribu vitu
vilivyoumbwa na wengine. Watu ambao kwa asili ni waumbaji muda wote wanasukumwa
na hamasa ya kufanikisha ndoto zao na hivyo wanakuwa ni wabunifu. Watu ambao
kazi yao ni kuharibu muda wote wao ni wanakatisha tamaa, wanalalamika na ni
wakosoaji wenye nia mbaya ili mradi tu wawaharibie wengine.
20. Furaha kwenye maisha haipaswi kupimwa
kwa mizani vitu unavyomiliki. Hapa mwandishi anatushirikisha kuwa kila hatua ya
maisha yetu ni muhimu kwa ajili ya ukamilisho wa kusudi la maisha yetu hapa
duniani. Kukamilisha safari yetu kwa mafanikio makubwa ni lazima tutambue kuwa
furaha ipo kwenye matendo yetu ya kila siku na hivyo hatupaswi kusema nitakuwa
na furaha pindi nikapata mme/mke, nikiwa na fedha, nikimaliza masomo n.k. Hapa
tunafundishwa umuhimu wa kuishi leo kana kwamba kesho haitokuwepo.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com