Mambo Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha Procrastinte on Purpose: 5 Permissions to Multiply Your Time (Hailisha kwa Makusudi; Ruhusa 5 za Kuongeza Muda Wako)


Habari ya leo rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri.

Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya 29 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi wa vitabu mbalimbali kwa ajili ya kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako kuyatumia ili ubadilishe kila sekta ya maisha yako.

Ni matumaini yangu kuwa makala hizi zimekuwa na msaada mkubwa kwako kwa kadri ambavyo umekuwa ukichukua hatua za kubadilisha maisha yako. Hata hivyo, makala hizi haziwezi kubadilisha chochote kama umekuwa mtu wa kusoma na kutokufanyia kazi yale unayojifunza.  

Ili uendelee kunufaika na makala za mtandao huu BONYEZA HAPA na ujaze fomu kisha bonyeza “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao wa fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.

Kupata uchambuzi wa kitabu cha The Rules of Money (Kanuni 107 za Kutengeneza pesa na kuwa tajiri) BONYEZA HAPA

Kitabu cha wiki hii ni Procrastinate on Purposekutoka kwa mwandishi Rory Vaden.  Rory Vaden ni mwanaharakati wa mafanikio ambaye anaongozwa na nidhamu binafsi na uadilifu katika kutimiza majukumu yake. Mwandishi huyu ni mkufunzi (kocha), mzungumzaji wa kimataifa na mshauri ambaye amejikita kwenye maono ya kuwaongoza watu ili waishi maisha yaliyojikita kwenye msingi wa nidhamu binafsi. Mwandishi anatumia uzoefu alionao katika biashara zake kuwashirikisha mamia ya watu ili wafikie mafanikio ya ndoto zao.

Muda ni rasilimali ambayo watu wotu wote tumepewa sawa. Yaani kila mtu kwa siku anapewa masaa 24 ambayo ni sawa na dakika 1,440 ambazo ni sawa na sekunde 86,400. Hivyo, kila kukicha kila mmoja ambaye yu hai anapewa sekunde hizo ndani ya masaa 24 na yeye ndo mwamuzi mkuu wa nini afanye katika kila sekunde.

Tunasema muda ni rasilimali kutokana na ukweli kwamba yale tunayofanya katika kila sekunde ya maisha yetu ndiyo yanaamua nafasi ya mafanikio yetu. Kutokana na muda kutumiwa visivyo katika makundi ya watu kwenye jamii ndio maana tunaweza kutofautisha mafanikio ya watu ndani ya jamii moja. Wale wanaotumia muda wao kufanya mambo ya maana wamefanikiwa kupiga hatua kubwa ya mafanikio katika maisha yao ikilinganishwa na wale ambao wanatumia muda wao kufanya mambo ya hovyo.

Hata hivyo watu wengi wameendelea kulalamika kuwa muda hautoshi kwa ajili ya kukamilisha majukumu yao siku pengine kwa vile hawajatambua njia nzuri ya kupangilia vizuri muda wao. Mwandishi Rory Vaden anatumia kitabu hiki kutushirikisha njia bora ambazo kila mtu anaweza kutumia kwa ajili ya kuboresha matumizi ya muda wake.

Karibu tujifunze wote machache niliyojifunza kwenye hiki:

1. Tofauti kubwa iliyopo kati ya watu waliofanikiwa na watu wa kawaida ni uwezo mkubwa wa kufikiri walionao watu wenye mafanikio ikilinganishwa na watu wa kawaida. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wenye mafanikio makubwa wanatambua na kuishi msingi huu “ili uweze kutoa matokeo makubwa unahitaji kufikiri nje ya boksi”. Kutokana uwezo wa kuishi msingi huu, watu wenye mafanikio wanatumia kila sekunde ya maisha yao kwa ajili ya kuzalisha matokeo makubwa kwenye majukumu yao ya kila siku.

2. Kukosekana kwa vipaumbele ni mfumo mpya wa kupoteza muda. Mfumo huu hauna tofauti na watu wanaopoteza muda kutokana na uzembe au uvivu wa kufanya kazi. Mfumo huu umesababisha kupoteza muda mwingi wa kuzalisha katika sehemu za kazi kama vile viwandani, ofisi za serikali au sekta binafsi na matokeo yake ni upotevu wa rasilimali muda ambayo inapelekea kampuni au serikali kukosa mapato ya kutosha. Hali hii inapelekea mtu kujiona kama vile kadri anavyozidi kupigana kufanya kazi ndivyo anazidi kurudi nyuma au ndivyo kazi zinazidi kuwa nyingi zaidi. Watu wa namna hii wanafanya kazi kwa presha kubwa kwa ajili ya kukamilisha majukumu yaliyopo mbele yao huku muda wote maisha yao yakitawaliwa na msongo wa mawazo wa kujiuliza ni lini watapata muda huru kwa ajili ya kufurahia maisha yao.

3. Epuka ubize wa muda wote ambao hauna tija au tija yake ni ndogo. Mwandishi anatushirikisha kuwa ni kawaida watu wengi kusema wapo bize muda wote na matokeo yake ni kwamba ukifanya tathimini ya ubize wao utagundua kuwa uzalishaji walionao ni wa kawaida na pengine upo chini zaidi. Watu hawa siyo kweli kuwa wapo bize bali wanashindwa kupangilia majukumu ya kazi zao na matokeo yake ni kushindwa kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili. Watu wenye mafanikio hawasemi kuwa wapo bize muda wote bali wanatambua namna ya kucheza na vipaumbele vya ratiba zao za kila siku na hatimaye kupelekea watu hawa kuwa na uzalishaji wa juu na hivyo wana matokeo mazuri katika maisha yao.

4. Epuka neno “mlinganyo/usawa (balance)”. Mwandishi anatushirikisha kuwa kama unahitaji kutumia muda wako vizuri ni lazima kwanza ufahamu kuwa kuna wakati utahitaji kutumia muda mwingi kwa ajili ya kukamilisha kazi uliyoipanga ili kwa baadae ikuletee matokeo mazuri. Kuna muda utahitaji kulala masaa machache kwa ajili ya kukamilisha jukumu ulilonalo au kuna wakati utapaswa kufanya kazi bila malipo.

5. Watu waliofanikiwa wanafurahia majukumu ya kazi zao. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wa kawaida wana fikra kuwa ipo siku ambayo watakuwa na muda wa kupumzika ili wafurahie maisha. Hii ni fikra ambayo watu waliofanikiwa wanapingana nayo kwa vile wao kila wanachofanya ni furaha na faraja katika maisha yao ya kila siku. Hapa ni muhimu kutambua kuwa unatakiwa kuishi leo kana kwamba kesho hautakuwepo kwa maana ya kwamba hautakiwi kuairisha furaha ya leo kwa ajili ya kesho. Kwa maana hii kazi inatakiwa kuchukuliwa kwa mtazamo wa kuwa kazi ni sehemu ya maisha ya kila siku na ni chanzo cha furaha katika maisha ya kila mmoja. TUMIA MUDA WAKO KUFANYA MAMBO YANAYOKUFURAHISHA.

6. Fahamu kuwa watu wenye mafanikio makubwa wanahitaji kulipwa kutokana na matokeo ya kazi zao. Mwandishi anatushirikisha kuwa hii ni tofauti kubwa kati ya watu wenye mafanikio mkubwa na watu wa kawaida. Watu wa kawaida mara nyingi wanahitaji kulipwa kulingana na muda wanaotumia kazini na wala hawajali kipi wanazalisha pindi wanapokuwa kazini. Kwa ujumla watu wenye mafanikio wanafanya kazi kubwa kwa sasa wakitegemea kupata faida baada ya matokeo ya kazi waliofanya kuonekana. Watu waliofanikiwa hawafanyi kazi kwa ajili ya malipo bali wanafanya kazi kwa ajili ya kutoa matokeo mazuri kwenye jamii inayowazunguka na matokeo hayo ndiyo yanarudisha mshindo nyuma (feedback) kwa muhusika kama malipo ya kazi yake.

7. Watu wengi wanaendelea na falsafa ya zama ya “kutunza muda” na kusahau kuwa kamwe muda hautunzwi badala yake mhusika anapaswa kudhibiti matendo yake kwenye kila sekunde ya muda wake. Mwandishi anatushirikisha kuwa hakuna namna yoyote ile mtu ataweza kutunza muda kama anashindwa kuwa na nidhamu binafsi ya matendo yake. Kwa maana hii kila mtu ni muhusika mkuu wa kuamua ni kipi kifanyike au kisifanyike kwenye kila sekunde ya muda alionao. Unaweza kuamua kufanya vitu vyenye matokeo mazuri pekee au unaweza kuamua kufanya mambo ya hovyo. Hapa ndipo watu wanaachana na kuanza kuona makundi ya watu waliofanikiwa kimaisha na wengine wanaangaika kimaisha lakini wote kila siku wanapewa muda sawa. Kwa ufupi ni kwamba “KAMA UNASHINDWA KUJIDHIBITI MWENYEWE KAMWE HAUWEZI KUTUMIA VYEMA MUDA WAKO”.

8. Njia ya kwanza ya kudhibiti matendo yako ni kutenga majukumu yako kwa vipaumbele. Hakikisha majukumu yako kwa siku nzima unayagawanya katika makundi manne ambayo kwa ujumla yanaitwa “time management matrix”. Kundi la kwanza ni majukumu ambayo ni MUHIMU na ni ya HARAKA, kundi la pili ni majukumu ambayo ni MUHIMU lakini SIO YA HARAKA, kundi la tatu ni majukumu ambayo SIO YA MUHIMU lakini YANA UHARAKA na kundi la mwisho ni majukumu ambayo SIYO MUHIMU na SIYO YA HARAKA. Makundi haya kwa ujumla yanatoa nafasi kwa mhusika kufikiria juu ya kipi ni cha muhimu kufanyika na kwa muda upi kifanyike. Kwa maana nyingine makundi haya yanatuhitaji kutekeleza majukumu yetu kwa mtiririko wa umuhimu na uharaka wake. Hii ni tofauti na falsafa ya zamani ya kutunza muda ambayo ililenga mtu kufanya kazi kwa haraka na presha kubwa ili aendane muda uliyopo.

9. Wanamafanikio wanatambua kuwa kadri wanavyotenga muda wa kutosha kwa ajili ya kufuatilia/kukamilisha majukumu waliyonayo kwenye kila sekta ya maisha yao ndivyo wanapata matokeo makubwa kwenye husika. Mfano, kwa wastani watu wengi katika jamii wanapambana kwa ajili ya kufanikisha maisha yao katika sekta sita ambazo ni Kazi, Familia, Imani, Fedha, Afya/Utimamu wa mwili na Kijamii. Mafanikio yako katika kila sekta yatategemea na muda unaotenga kwa siku au wiki kwa ajili ya kujiendeleza kwenye kila sekta. UTAVUNA KULINGANA NA UNACHOPANDA.

10. Watu waliofanikiwa zaidi wana uwezo wa kuongeza/kupanua muda wao. Unaweza kujiuliza kuwa wanaweza vipi kuongeza muda? Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wenye mafanikio pamoja na kufanya vitu kwa mtiririko wa umuhimu na uharaka wake, watu hawa wana uwezo wa kufanya mambo yenye matokeo makubwa na yanayoweza kudumu kwa muda mrefu. Uwezo wa kuongeza muda unatokana na ufanisi wa utendaji kazi ambao unapelekea kuwekeza muda mwingi kwenye kazi ambazo zinawapa muda wa kutosha kwa ajili ya kufanya kazi nyingine siku zijazo. Kwa maana nyingine ni kwamba watu wenye mafanikio makubwa sio tu wanaangalia umuhimu na uharaka wa jambo kwa wakati uliopo pekee bali wanaangalia umuhimu wa jambo husika kwa siku zijazo. Hivyo, watu wenye mafanikio makubwa wanajiuliza ni kwa namna gani matumizi ya muda wao kwa sasa yatabadilisha maisha yao ya baadae.

11. Ruhusa ya kwanza ya kuongeza muda; AMUA KUPOTEZEA AU KUSEMA HAPANA. Mwandishi anatushirikisha kuwa kama unataka kutunza muda wako vizuri ili utumike kwa ajili ya kufanya vitu vyenye manufaa ni lazima uwe na nguvu ya kupotezea au kusema hapana kwa baadhi ya vitu ambavyo havina tija katika maisha yako. Hapa unahitaji kuwa jasiri wa kukataa kuwa kila sio linalokuja kwenye fikra zako au mbele yako lazima lifanyiwe kazi au sio kila anayekuja utimize haja zake. Hakikisha unafanya vitu ambavyo kamwe hautojutia kwa nini umefanya mara baada ya matokeo ya vitu hivyo kujidhihirisha.

Baadhi ya tabia ambazo unapaswa kuachana nazo mara moja ni mabishano, kufanya kazi za wengine ambazo sio lazima ufanye wewe, epuka kupoteza muda kwa kuangalia TV, epuka kupoteza muda kujibu emails au chati za kwenye mitandao ya kijamii ambazo hazina tija, epuka vikao visivyo na tija, epuka kazi za kujitolea ambazo zimepitiliza, epuka kufanya kazi mbili kwa mkupuo, epuka kutoa maelezo marefu n.k. Tabia hizi zinapoteza muda ambao ungeutumia kwa ajili ya kuwa karibu na familia yako au kufanya mambo mengine ambayo ni muhimu.

12. Ruhusa ya pili ya kuongeza muda; WEKAZA MUDA WAKO KUPITIA MAAMUZI YAKO YA FEDHA. Mwandishi anatushirikisha kuwa maamuzi yako ya fedha unayofanya kwa sasa yana mchango mkubwa wa kuamua hatima ya kipato chako na muda wako kwa siku zijazo. Watu wenye mafanikio kabla ya kufanya matumizi yoyote ya pesa ni lazima wajiulize thamani ya fedha hiyo kama ingewekezwa sehemu ambayo inatoa asilimia flani kama faida kwa mwaka na je baada ya miaka kadhaa fedha hiyo ingelipa thamani sawa na hicho ambacho wanahitaji kuitumia kwa sasa?. Swali hili linamfanya mtu mwenye mafanikio atafakari gharama na faida ambazo atazikosa kwa kuamua kutumia kiasi cha fedha husika kwa sasa badala ya kuiwekeza ili baada ya miaka kadhaa apate ongezeka la thamani ya fedha husika. Kutokana na msingi huu unatakiwa kufahamu kuwa kila shilingi unayoitumia kwa sasa ina athari kubwa kwenye nafasi yako ya kifedha kwa miaka ijayo. Hapa unaweza ukajitathimini kwenye matumizi yako ya fedha ambayo siyo ya lazima kama ununuzi wa vocha, magazeti, uvutaji wa sigara, ulevi au matumizi ambayo hayapo kwenye bajeti yako. MUDA UNA THAMANI ZAIDI YA PESA KUTOKANA NA UKWELI KUWA MUDA UKITUMIWA VIZURI UNATENGENEZA PESA AMBAZO ZITAENDELEA KUJITENGENEZA ZENYEWE.

13. Tumia njia ambazo zinasaidia kupunguza muda wa utendaji kazi. Kama ambavyo tumeona katika ruhusa ya pili hapo juu kuwa shilingi ya leo kwa kesho itakuwa na thamani kubwa kama imewekezwa, ndivyo mwandishi anatukumbusha pia juu ya matumizi ya muda wetu katika kazi zetu za kila siku. Kama kuna uwezekano wa kutumia teknolojia ambayo imeboreshwa katika kazi yako hakuna haja ya kuendelea kutumia teknolojia ya zamani ambayo inasababisha upoteze muda mwingi ambao ungeutumia kufanya mambo mengine. Mfano, kama kazi inaweza kufanywa na mashine hakuna haja ya kung’ang’ania kufanya hizo kwa kutumia mikono. Nguvu iliyopo katika kufanya kazi kwa teknolojia ni kwamba itakusaidia kufanya kazi masaa yote na siku zote saba za wiki kulingana na teknolojia pamoja na kazi husika. Mfano, mauzo kwa kutumia mtandao, mhusika anaweza kuuza hata kama amelala.

14. Ruhusa ya tatu ya kuongeza muda; ONGEZA MUDA WAKO KWA GATUA MADARAKA/KAZI AMBAZO ZIPO JUU YA UWEZO WAKO AU SIO ZA KIWANGO CHAKO. Mwandishi anatushirikisha kuwa ni muhimu kufanya tathimini ya majukumu ya kazi zako za kila siku na kisha ukajiuliza kama kuna ulazima wa kazi zote kufanywa na wewe. Chagua kazi ambazo unaona unaweza kumfundisha wa chini yako ili azitekeleze kwa niaba yako na kukufanya hivyo utakuwa umetunza muda ambao utautumia kufanya mambo mengine.

Pia, sehemu nyingine ambayo unahitaji kugatua madaraka ni zile ambazo zipo nje ya taaluma yako.  Badala ya kukomaa na kazi ambayo hauna utaalamu wa kutosha ni vyema ukamtafuta wa kuifanya kazi hizo kwa ufanisi zaidi huku wewe ukiwa unatekeleza majukumu mengine. Mfano, ni kawaida kukuta kuwa wafanyabiashara wa kawaida wanatumia muda mwingi kutekeleza majukumu yote ya biashara kuanzia kazi za uhasibu, sheria, mipango n.k. Mwandishi anatushauri kuwa kama unahitaji kuwa na mafanikio makubwa ni lazima uwe tayari kuamini kuwa kazi yako inaweza kufanywa na mtu yeyote kwa viwango unavyohitaji.

15. Ruhusa ya nne ya kuongeza muda; ONGEZA MUDA WAKO KWA KUKUBALI KUAIRISHA MAMBO PALE INAPOBIDI. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wenye mafanikio sio tu wanafanya kwa mtiririko wa umuhimu, uharaka na umuhimu wa vitu husika kwa siku zijazo bali pia wanaangalia ni upi muhafaka kwa ajili ya kufanya kazi husika. Watu waliofanikiwa wanafahamu kama endapo kuna ulazima wa kazi husika kukamilishwa kwa sasa au kusubirishwa kwa baadae kwa kutegemea umuhimu wake kwa wakati husika. Kwa ujumla mwandishi anatushirikisha kuwa kila kazi au maamuzi unayofanya ni lazima kwanza usome alama za nyakati. Kama alama za nyakati haziruhusu kazi/maamuzi husika kufanyika kwa wakati huo hakuna haja la kulazimisha kukamilisha/kufanya maamuzi badala yake ni vyema ukasubiria kwa makusudi mpaka pale hali itakapokuwa vizuri.

16. Watu wenye mafanikio wanajua nguvu iliyopo kwenye kusubiria mpaka dakika ya mwisho katika fursa husika. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu waliofanikiwa wantambuwa kuwa dakika ya mwisho kwenye fursa husika ndio muda kutengeneza faida kubwa. Kutokana na ukweli huu, wanamafanikio wanatumia pindi wanaposubirisha kazi/fursa kama ambavyo tumeona kwenye ruhusa ya nne ya kuongeza muda wanasubiria mpaka dakika ya mwisho ambayo ndo fursa husika inakuwa imeiva. Hii ndio siri ambayo watu wenye mafanikio wanaitumia kutengeneza pesa nyingi kwa vile wanakuwa na taarifa sahihi kuhusu fursa husika na hawana hofu pindi wanaposubiria ili fursa husika ikomae. KILA KITU KINABADIRIKA HASA KWENYE SOKO LA ULIMWENGU WA SASA HIVYO UNAHITAJI KUFAHAMU NYAKATI ZIPI NI SAHIHI KUKALIMISHA KAZI/MAAMUZI ULIYOYASUBIRISHA KWA MAKUSUDI ILI KUEPUKA GHARAMA YA KUFANYA MAAMUZI YA HARAKA.

17. Fahamu kuwa matajiri hawalipii bili za kodi mwanzoni bali wanasubiria mpaka siku za mwisho wanazotakiwa kulipia. Siri hii ndio mwandishi anatushirikisha kwa ajili ya kufahamu nguvu iliyopo katika kusubilia mpaka dakika ya mwisho. Matajiri wanafahamu kuwa katika muda wanaosubilia kulipa wanawezakutumia fedha husika kwa ajili kukamilisha fursa endapo itajitokeza ndani ya muda husika. Kwa kufanya hivi wanafanikiwa kuongeza muda ambao unazalisha muda zaidi kwa ajili ya kukamilisha kazi za siku zaijazo.

18. Ruhusa ya tano ya kuongeza muda; ONGEZA MUDA WAKO KWA KUTULIZA AKILI KATIKA NYAKATI MUHIMU. Mwandishi anatushirikisha kuwa kuna nyakati ambazo utatakiwa kufanya kazi mara mbili zaidi ya ulivyozoea kwa ajili ya kuhakikisha unakamilisha jukumu lililo mbele yako. Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa rasilimali zote unazielekeza kwenye jukumu husika kwa kadri zinavyotakiwa mpaka pale ambapo utaona kuwa umefanikisha kukamilisha jukumu hilo. Katika hatua hii unahitaji kutambua kuwa baada ya kuairisha fursa/kazi kwa makusudi sasa ni muda ambao upo kwenye dakika ya mwisho ambayo ukizembea kidogo tu unakosa kila kitu na hivyo kusubilia kwako hakutakuwa na faida bali ni hasara. Hapa unahitaji kuongeza muda wako kwa kuhakikisha unafanyia kazi ambayo ni kipaumbele kwa wakati na si vinginevyo. Hakikisha haurusu mwingiliano wa vitu vingine ambavyo vinaweza kukupoteza kwenye kipaumbele chako.

19. Tengeneza mtiririko wa vipaumbele. Somo kubwa katika kitabu hiki ni kuona kuwa msomaji anaweza kuongeza muda wake wa kesho kwa kadri awezavyo kupitia majukumu anayofanya kwa sasa. Mwandishi anatushirikisha kuwa ili ufanikishe zoezi la kuzalisha muda ni lazima uhakikishe unakuwa na vipaumbele ambavyo vina muunganiko wa matukio kiasi kwamba kukamilika kwa kipaumbele kimoja kunapelekea kuanza kwa kipaumbele kingine. Pia, kipaumbele kimoja kisaidie kuongeza muda kwa ajili ya kipaumbele kinchofuatia.

20. Baada ya kuondoa tabia au kazi ambazo zimekuwa zikipoteza muda wako sasa unatakiwa kuongeza uzalishaji wako. Hapa unahitaji kutengeneza utamaduni au falsafa ambazo zitakuongoza katika kipindi chako chote ili hatimaye uzidi kuongeza muda wako kwa ajili ya kufanikiwa katika kila sekta ya maisha ya maisha yako. Kama wewe ni mwajiri unahitaji kuhakikisha unaishi misingi uliyojifunza hapa ili kila mmoja chini yako ajifunze kutoka kwako kwa ajili ya kuongeza ufanisi utendaji kazi.

Haya ni machache ambayo nimeweza kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.

Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.

Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.

Born to Win ~ Dream Big 

Augustine Mathias Bilondwa

Namba ya Simu:      +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com


onclick='window.open(