Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri.
Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa
FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa
ni wiki ya 31 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi
wa vitabu mbalimbali kwa ajili ya kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako
kuyatumia ili ubadilishe kila sekta ya maisha yako.
Ni matumaini yangu kuwa makala hizi
zimekuwa na msaada mkubwa kwako kwa kadri ambavyo umekuwa ukichukua hatua za
kubadilisha maisha yako. Hata hivyo, makala hizi haziwezi kubadilisha chochote
kama umekuwa mtu wa kusoma na kutokufanyia kazi yale unayojifunza.
Ili uendelee kunufaika na makala za
mtandao huu BONYEZA HAPA na
ujaze fomu kisha bonyeza “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao wa
fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa
humu moja kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “Healing Your Family
History” kutoka
kwa mwandishi Rebecca Linder Hintze. Rebecca ni mwandishi wa vitabu, mhamasishaji
na mzungumzaji maarufu ambaye amejikta katika kuielimisha jamii ili iishi
maisha ya mafanikio kwenye masuala ya kifamilia, mahusiano kati ya wazazi na
watoto na maisha ya ndoa.
Mwandishi
ameandika kitabu hiki mara baada ya kuona kuwa watu wengi wanaishi ndani ya minyororo
ambayo imetokana na mazoea ambayo wamerithishwa kutoka kwa watangulizi wao. Watu
wengi wamekuwa wakifanya vitu kwa mazoea pasipo kuwa na majibu sahihi ya kwa
nini wanafanya yale wanayofanya. Hii ni kutokana na ukweli kwamba tabia zinarithishwa
kutoka kizazi kimoja hadi kingine na endapo tabia hizo ni mbaya inakuwa ni
chanzo cha kuendelea kudidimiza wahusika kizazi na kizazi.
Kila
familia ina imani na mila ambazo zinarithishwa kizazi na kizazi kwenye familia
husika. Imani hizi zinawezakuhusiana na mtazamo wa familia kwenye masuala ya
imani, afya, fedha, na maisha ya jamii inayowazunguka. Imani hizi pamoja na
mila potofu zinaweza kuwa ni kuta ambazo zimekuwa zikiwazuia wanafamilia
kufikia mafanikio yanayotaka katika maisha yao.
Njia
pekee ya kukabiliana na imani/mila potofu ni lazima mhusika aweze kutambua
imani ambazo zimekuwa sehemu ya maisha yake huku zikiendelea kumsogeza nyuma
kimafanikio. Hatua hii ni muhimu kwa ajili ya kuvunja ukuta ambao umekufanya
uwe kama ulivyo kwa sasa na hivyo njia pekee ya kusonga mbele ni kufuata hatua tano
ambazo mwandishi ametushirikisha katika kitabu hiki kwa ajili ya kuachana na makovu
ambayo yamekuumiza kwa muda.
Karibu
tujifunze wote machache niliyojifunza kwenye hiki:
1. Mama
na baba katika familia wana nafasi kubwa ya kuwabadilisha watoto wao ili
wakulie kwenye misingi ya imani na mila sahihi. Hii ni kutokana na ukweli
kwamba mama na baba ni wahamasishaji na walimu wa kwanza kabisa katika
kubadilisha ubongo wa watoto wao. Wazazi ndio wahusika wakuu kwenye kumfundisha
mtoto namna avyotakiwa kuhishi yeye kama yeye, mtazamo wake kwenye jamii na
dunia inayomzunguka kwa ujumla. Yamkini ni wazazi wachache ambao wamewekeza
kwenye kujifunza namna bora ya kumlea mtoto katika misingi ya imani na mila
sahihi na matokeo yake ni kwamba vizazi vinaendelea kuangamia kwa minyonyoro ya
imani za ukoo au jamii zilizotangulia.
2. Kama
wazazi mnatakiwa kuficha madhaifu yenu kwa watoto wenu pale inapotokea
mmekorofishana. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wengi wameishi kwa kuumizwa
na historia za mafarakano ya wazazi wao kiasi ambacho na wao wanashindwa kudumu
ndani ya familia zao. Ni kawaida kukuta kuwa wazazi ambao walipeana taraka na
vizazi vyao navyo havidumu kwenye maisha ya ndoa. Kumbe kinachosababisha ni
minyororo ambayo inafunga wahusika ndani ya familia bila ya wao kutambua. Matokeo
yake ni kwamba muda wote mtu anakaa ndani ya ndoa akiwaza kuwa ipo siku
yaliyotokea kwa wazazi wao yatatokea na kwake pia.
3. Sisi
ni zao la watangulizi wetu kwa maana ya mababu/mabibi zetu. Mwandishi anatushirikisha
kuwa japo tafiti za kisayansi hazijaweza kudhihirisha kama hisia zinarithishwa
kutoka kizazi kimoja hadi kingine kupitia jeni (genes) bado kuna dalili zinaonesha
kuwa wajukuu wana sifa za kihisia zinazofanana na mababu/mabibi zao. Kulingana na
ukweli huu upo uwezekano mkubwa wa watoto kurithi hisia kutoka kwa watangulizi
wao na endapo wamerithi hisia ambazo sio nzuri zitaendelea kuwakandamiza katika
maisha yao. Habari njema ni kwamba kila mmoja anaweza kuamua kuachana na hisia
hizo ambazo zimekuwa kandamizi kwenye maisha yake.
4. Sisi
ni zao la hisia zetu. Tupo jinsi tulivyo kutokana na namna ambayo tunakabiliana
na hisia zetu. Mfano, kama unatawaliwa na hisia za hofu ni wazi kwamba maisha
yako yatakuwa ya hofu na kama unatawalia na hisia za kutokukubalika ni wazi
kwamba itakuwa ni nadra kukubalika kwenye jamii. Mwandishi anatushirikisha kuwa
hatuwezi kuponya makovu ya historia ya familia zetu kama hatuwezi kudhibiti
hisia zetu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba hisia ndizo zinatusukuma kufanya
yale ya muhimu au yale ambayo yamekuwa yakitukandamiza muda wote. Na hapa ni
lazima tutambue kuwa ili ufanikiwe kuvunja minyororo ambayo imekufunga ni
lazima uwe tayari kuisikiliza sauti yako ya ndani (roho au wewe wa ukweli)
kwani hiyo ni sauti pekee ambayo itakuongoza hatua kwa hatua.
HATUA YA KWANZA – TAMBUA NI TABIA ZIPI
UNAHITAJI KUBADILISHA
5. Kwa
asili familia zote zinapitisha mila kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Mila hizi
zinajumuisha zile ambazo zinamuongoza mtoto kwenye namna ya kuwapenda wengine,
kujithamini, kujiheshimu na kuwaheshimu wengine, namna ya kufanikiwa pamoja na
kuwasaidia watu wanaomzunguka. Hata hivyo zipo mila nyingine ambazo zinapelekea
mtoto ashindwe kujiamini, awe mtu wa visasi, mchoyo, mwizi na mtundu. Katika uponyaji
wa makovu ya kihistoria ndani ya familia, mwandishi anatushirikisha kuwa ni
lazima kwanza tutambue mila ambazo zimekuwa zinatuzuia kusonga mbele pasipo
uelewa wetu kwani mila hizo ndizo chanzo cha kushindwa kupenda/kupendwa, kufanikiwa,
kukua kiroho au kutambua kusudi la maisha yetu.
6. Sikiliza
na kujifunza kutokana na imani zilizopo ndani ya ukoo wenu. Mfano, ni kawaida
kukuta koo ambazo hazina uhuru wa kifedha zinakuwa na kauli mbaya dhidi
matajiri. Wengi katika koo hizi utakuta wanakuambaia matajiri ni watu wabaya au
wachoyo, hivyo kutokana na kauli kama hizo ni vigumu sana wanafamilia
kufanikiwa kifedha. Unahitaji kusikiliza kutoka kwa ndugu zako pamoja na
kuisikiliza sauti yako ya ndani ili hatimaye uweze kutambua kauli ambazo
zimakuwa zinakukwamisha kupiga hatua. Kauli kama “ni bora kuwa masikini kuliko kuwa tajiri kwani utajiri utaninyima amani,
sisi familia yetu huwa ni watu wa kukosa, wanaume/wanawake sio kuaminiwa, mapenzi
ni maumivu na mahusiano yanaumiza hivyo ni bora ya kuwa peke yangu” ni
baadhi ya kauli ambazo haupaswi kujisemea maishani mwako.
7. Jichunguze
ni imani/mila zipi umeifadhi katika akili yako ya ndani (subconscious mind)
ambazo zimekuwa zikikuzuia kusonga mbele. Katika koo nyingi kuna imani kuwa maisha
ya furaha na heshima yanapatikana pale mtu anapokuwa na fedha nyingi, anamiliki
magari na majumba, anapokuwa msomi wa juu sana na mengine mengi. Imani kama
hizi zinaendelea kuwazuia wengi kuishi maisha ya furaha na heshima kwa vile
wanajiona kuwa hawastahili kuwa na furaha au heshima kwa vile hawana fedha au
elimu ya kutosha.
8. Futa
mila/imani potofu kwenye mfumo wako wa kumbukumbu. Binadamu ana mfumo wa
kuhifadhi kumbukumbu kama ilivyo kompyuta hivyo unachotakiwa kufanya baada ya
kugundua imani/mila ambazo zimekukwamisha kwa muda ni kuhakikisha uzifuta
kwenye mfumo wa kumbukumbu huku nafasi yake ukiijaza na imani/mila ambazo
zitakuwezesha kusonga mbele.
HATUA
YA PILI – KUDHIBITI HUKUMU NA HOFU
9. Kutokana
na imani/mila potofu ulizonazo umekuwa mtu hukumu vitu ambavyo sio sahihi. Katika
hatua ya kwanza tumeona hukumu za moja kwa moja kama vile matajiri ni wachoyo
au watu wabaya, mimi ni mtu wa kukosa na nyinginezo; hukumu hizi zimekufanya
ushindwe kuufahamu ukweli na hivyo muda wote umekuwa ukiuishi uongo. Sasa unahitaji
kuangalia katika historia ya familia yako na kuchambua hukumu ambazo mmekuwa
mkiishi kama sehemu ya maisha na hatimaye uanze kuachana nazo mara moja. Hapa unahitaji
kujiuliza maswali kama Je nawahukumu vipi wenzangu?, Je nawahukumu wengine kwa
mwonekano wao?, Je nawahukumu wengine kwa dini zao? Je nawahukumu wengine kwa
vipato vyao au rangi zao? na Je nafsi yangu naihukumu vipi katika kila sekta ya
maisha yangu.
10.
Zipo imani/mila ambazo tumerithishwa
kutoka kwa watangulizi wetu na bahati mbaya imani/mila hizi zimetujaza hofu. Hii
ni kutokana na ukweli kwamba hofu au woga wa kukataliwa au kutokukubalika
tumerithi kutoka kwa wazazi kupitia makuzi na malezi. Hofu hii imeendelea kutufanya
tukose uthubutu wa kuchukua hatua na matokeo yake ni kushindwa kufikia
mafanikio tunayotamani kupata. Mwandishi anatushirikisha kuwa kama unahitaji
kuponya makovu ya historia ya famili ni lazima kwanza tufahamu ni hofu zipi
ambazo zimetokana na imani/mila zetu na hatimaye tuanze kuzishinda hofu hizo.
11.
Migogoro mingi ya familia inatokana na
hisia za kuhamishia tatizo kwa mwenza wako pasipo kufanya tathimini ya wapi
wewe unakosea. Mwandishi anatushirikisha kuwa familia nyingi zimekulia katika
utamaduni wa kusukumizia tatizo kwa mwingine kwani hakuna ambaye anakubali
kuhusika kwenye tatizo linalowagombanisha. Pia, tatizo jingine linalosababisha
mafarakano ndani ya familia ni ile mila/dhana ya kwamba furaha yako
imeshikiliwa na mwenza wako. Kumbuka kuwa mwenza wako ni mwanadamu kama wewe
hivyo ni vigumu kukupa furaha unayotarajia kutoka kwake.
HATUA
YA TATU – CHUKUA HATUA ACHA KUISHI MAISHA YALEYALE
12. Kuwa tayari kuachana na maisha
uliyozoea na kuanza kuisha maisha mapya (escape your comfort zone). Hapa mwandishi
anatushirikisha kuwa ili uishi maisha mapya kwanza kabisa unatakiwa uanze
kujifunza upya na kuachana na imani/mila ambazo awali zilikudanganya. Unahitaji
kuutafuta ukweli na hatimaye uanze kuuishi ukweli huo. Tatizo kubwa ni kwamba
watu wengi hawapo tayari kubadilika kwa vile ni rahisi kuishi maisha waliyozoea
badala ya kuingia kwenye maisha mapya. Hata hivyo wale wachache ambao wanaamua
kukabiliana na ugumu wa maisha mapya ndo hao hao ambao wanafanikiwa katika
jamii inayozunguka. Hii ni kutokana na ukweli kwamba watu wapo tayari kuendelea
kwenye imani/mila kandamizi kwa vile tayari zimekuwa sehemu ya maisha yao na
hii inawafanya wawe na hofu ya kuanza maisha mapya.
13. Tambua ni matakwa yapi unayohitaji
katika maisha yako na bado hayajakamilishwa katika familia yako. Mwandishi
anatushirikisha kuwa ni kawaida kila mwenza ndani ya familia kuwa na mahitaji
anayotaka yakamilishwe na mwenza wake na pengine matakwa hayo hayakamilishwi. Matakwa
haya yanajumuisha mahitaji muhimu kama vile mavazi, chakula, maradhi, faraja
kwa wenza au watoto wao pamoja na ukuaji wa kiroho. Baada ya kutambua matakwa
yapi hayajakamilika, sasa unatakiwa kutathimini imani/mila ulizonazo dhidi ya
matakwa hayo ambayo muda wote umekuwa ukiona kuwa wewe au mwenza wako
mnapungukiwa. Chukua hatua ya kuanza kukabiliana na mila hizo. Mfano, kama
katika makuzi yako umewahi kuambiwa kuwa hata
ufanye kazi kwa bidii kiasi gani kamwe hauwezi kuwa na pesa ya kutosha – hii ni imani ambayo itakufanya
maisha yako yote uhangaike kufanya kazi kwa bidii pasipo kupata pesa za
kutosha. Kubadilisha imani hii unatakiwa kufahamu kuwa msingi wa kupata pesa
unazotaka ni kufanya kazi kwa bidii na si vinginevyo.
14. Safisha hisia zote ambazo zimekufanya
uwe mtumwa wa makovu uliyopata katika enzi za ukuaji wako pasipo wewe kufahamu.
Mwandishi anatushirikisha kuwa katika hatua za ukuaji watu wengi wamekutana na
mazingira/matukio hatarishi kutoka kwenye familia zao au jamii zinazowazunguka.
Matukio hayo yamewafanya waishi maisha ya utumwa kwa kutumi vijibwana ambavyo
vipo ndani mwao hila wao hatambui kuwa ni watumwa wa matukio hayo. Matukio hayo
yanaweza kuwa ugomvi wa wazazi, kunyanyaswa, kubakwa, kutishiwa na mengine
mengi. Haya ni matukio ambayo yanamfanya mhusika awe na hisia hasi muda wote wa
maisha yake na hisia hizo zinakuwa kizuizi cha yeye kusonga mbele. Sasa unahitaji
kufanya tathimini ya kila tukio katika enzi za ukuaji wako na kuona athari yake
ni ipi katika maisha yako ya sasa.
15. Njia bora ya kusonga mbele na kuchukua
hatua ni kuanzisha matendo ya kuwasaidia wengine wenye uhitaji wa ujuzi ulionao.
Mwandishi anatushirikisha kuwa kadri mtu anavyojitoa kwa ajili ya kuwasaidia
wengine kwa moyo wa dhati ndivyo na milango yake inavyofunguka na hatimaye
kufanikisha mahitaji yake. Kwa ujumla tunaweza sema kuwa tunajazwa baraka katika
ulimwengu huu kutokana na jinsi tunavyojitoa kutumia kalama zetu kwa ajili ya
kuwasaidia wengine.
HATUA YA NNE – ITAFUTE HAZINA YAKO
16. Ipo hazina kubwa ndani mwako tena yenye
thamani ambayo haijatumiwa ipasavyo. Ili uitumie vyema hazina iliyopo ndani
mwako unahitaji kuanza kupingana na imani/mila kandamizi ambazo zimekuzuia kwa
muda sasa. Hapa unatakiwa kuweka misingi ambayo itakuwa mwongozo wako katika
maisha mapya. Misingi hii ni lazima iwe na sifa za kukuongoza katika ukuaji
wako kwenye kila hatua ya maisha yako. Kumbuka kuwa ukuaji ndio maisha na pale
unapoacha kukua ni sawa na kwamba unajichimbia kaburi. Pia, tambua kuwa ili uendelee
kukua kwenye kila sekta ya maisha yako unahitaji kujifunza kila mara na
hatimaye utumie mafundisho hayo kwa ajili ya kutunisha hazina yako.
17. Anza kujifunza kutokana na makosa. Mwandishi
anatushirikisha kuwa njia mojawapo ya kuponya makovu ya historia ya familia ni
kuanza kutazama makosa kama sehemu ya kujifunza. Makosa ambayo umekuwa ukifanya
mara kwa mara unahitaji kuyaangalia kwa sura ya kujifunza kitu kutoka kwenye
makosa hayo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba makosa haya yametuzuia kwa muda
sasa kufikia kwenye hazina kuu ambayo ipo ndani mwetu. Hivyo, kuanzia sasa
tunapaswa kuangalia upande chanya kwenye kila kosa ambalo tunafanya, jiulize ni
kipi naweza kujifunza kutokana na kosa husika. Hili ni zoezi gumu lakini pale
unapofanikiwa ni rahisi kurudisha furaha na amani ambayo umeipoteza kwa muda
sasa. Hii pia inaambatana na uponyaji unaotokana na kubadilisha madhahifu yetu
kwenda kwenye uimara kwenye kila sekta ya maisha yetu.
18. Ifanye familia yako kuwa mahali sawa na
peponi kwa maana ya kuhakikisha familia yako ni sehemu yenye furaha na amani
muda wote. Huu ni uponyaji ambao utamgusa kila mwana familia na hivyo uponyaji
huu utadumu kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine. Hakikisha kila mmoja
ndani ya familia atambue kuwa mwanadamu anaweza kutenda makosa lakini kukosea
sio mwisho wa safari bali kila kosa lina somo ndani yake. Hakikisha kila
mwanafamilia anatambua umuhimu wa kupendana na kuwajali wengine badala ya
kuangalia nafsi yake pekee.
19. Watazame wanaokuzunguka kwa jicho la
Mungu anavyowatazama. Wote tunafahamu kuwa Mwenyezi Mungu ni mwema kwa watu
wote na kwake kila mmoja anamtazama kwa jicho la upendo ndani mwake. Haijalishi
umekosea kiasi gani mbele za Mwenyezi Mungu anaendelea kukukaribisha kwa ajili
ya toba ili uendelee kufurahia ukuu wake. Mwandishi anatushirikisha kuwa
uponyaji wa kuwatazama wengine kwa jicho la Mungu ni uponyaji wa aina yake kwa
kuzingatia kuwa unapowatazama wengine kwa jicho la kimungu daima utawapenda,
utawapa faraja na amani. Hii itakusaidia ujifunze vitu vingi kutoka kwa wenzako
na hivyo kuendelea kupanua hazina yako.
HATUA
YA TANO – KARIBISHA UWEPO WA ROHO MTAKATIFU
20. Kila mwanadamu ameumbwa na kupewa mwili ambao ndani yake umewekewa pumzi
ya uhai ambayo ndiyo roho. Mwili muda
wote unamsukuma mhusika kwenye mambo ya kidunia wakati roho kazi yake kubwa ni
kumuunganisha mhusika na nguvu ya ajabu (Mungu). Kadri mtu anavyoujua ukweli
ndivyo anajitambua kuwa yeye ni nani kwa maana kujitambua kimwili na kiroho na
hivyo anakuwa na nafasi kubwa ya kuuishi ukweli. Mtu anayeishi ukweli ni yule
anaye ongozwa na matendo ya roho mtakatifu badala ya kuongozwa na matendo ya
mwili. Mtu huyu ambaye anaongozwa na roho mtakatifu muda wote ataishi maisha ya
furaha na amani kimwili na kiroho na hivyo mafanikio yatamfuata kwenye kila
sekta ya maisha yake.
21. Binadamu wote tumepewa uwezo wa
kufikiri, kuchanganua mambo na kubadilisha vitu kwa kadri tupendavyo. Huu ni
uwezo wa kipekee ambao unatutofautisha na wanayama wengine. Uwezo huu wote
tumepewa sawa japokuwa tunatofautiana jinsi ambavyo tunautumia kwa ajili ya
faida yetu. Ili ufanikiwe kutumia uwezo huu ni lazima uongozwe na roho kwani ni
roho pekee ndo anatuongoza kwenye mabadiliko ya kweli badala ya kuzama kwenye
matamanio ya mwili.
22. Kuwa na muunganiko na roho kupitia njia
ya sara. Mwandishi anatushirikisha kuwa sara ni njia pekee ya kuboresha
muunganiko wa mhusika na roho. Mfumo huu wa sara unafanya kazi kwa rika zote
pasipo kujali umri wa mhusika kinachotakiwa ni imani ya kweli inayoambatana na
matamanio ya kupata kile ambacho unaomba.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com