UCHAMBUZI WA KITABU The Rules of Money: How to Make It and How to Hold on to It (Kanuni za Pesa: Jinsi ya Kuzitengeneza na Jinsi ya Kuendelea Kutengeneza Pesa Zaidi)

Habari ya leo rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea vizuri katika mapambano ya kuboresha maisha yako kwa kuhakikisha kila siku unakuwa bora zaidi kupitia ushindi mdogo mdogo. Leo hii ninakuletea uchambuzi maalumu wa kitabu cha The Rules of Money ambacho kimeandikwa na mwandishi mahiri na tajiri Richard Templar.

Kupitia kitabu hiki mwandishi anatushirikisha kanuni 107 za pesa ambazo kupitia uchambuzi huu nitakushirikisha kanuni zote ili uanze kuzitumia kwa ajili ya kutengeneza pesa zaidi na zaidi katika mchezo huu wa fedha. Kwa ujumla katika kitabu hiki tunafundishwa kuwa pesa hawezi kununua furaha au mapenzi yako bali pesa inaweza kununua kila aina ya vitu na hivyo kukuwezesha kumiliki kila aina vitu unavyohitaji. Lakini katika yote ni muhimu kukumbuka kuwa furaha ya kweli juu ya matumizi ya pesa yako inatengenezwa na wewe mwenyewe kutoka ndani mwako.

Kanuni hizi zimegawanyika katika makundi saba na kila kundi lina kanuni zinazokuhusu wewe na pesa yako. Kila kanuni imegusa kwa namna ambavyo unaweza kutengeneza pesa na hatua zipi unatakiwa kufuata kwa ajili ya kupata za ndoto yako. Kwa kina katika kila kundi nimekuchambulia kwa kina kanuni moja baada ya nyingine ili kukufikishia kile ambacho mwandishi ametushikisha kwa ajili ya kukuwezesha ufahame kanuni hizi kwa urahisi lakini pia uwe tayari kuzitumia kwa ajili ya kutengeneza pesa zaidi na hatimaye upate uhuru wa kifedha.

Katika makala hii ninakushirikisha kanuni kumi (10) kama sehemu ya utangulizi wa uchambuzi wa kanuni zote mia na saba (107) na kama unahitaji uchambuzi wa kanuni zote maelekezo ya namna ya kuzipata yapo mwishoni mwa makala hizi.

Karibu tujifunze wote kwa haya machache niliyokuchambulia katika kanuni kumi (10) za mwanzo;

SEHEMU YA KWANZA: FIKRI KITAJIRI (THINKING WEALTHY)
Mwandishi katika sehemu hii ya kwanza anatushirikisha kanuni ambazo kwa pamoja zina nia ya kutufumbua macho dhidi ya fikra, hisia au imani zetu dhidi ya fedha. Kwanza tunatakiwa kufahamu kuwa fedha ni dhana ambayo inaambatana na imani nyingi kulingana na sehemu ulipo. Kwa asili fedha inabebeshwa kila aina ya imani kwani ambao wanasema fedha ni mbaya au ni nzuri, ni vibaya kupenda pesa au ni vyema kupenda pesa na imani nyingine nyingi. Kwa ujumla unakiwa kufahamu kuwa imani ulizonazo juu ya pesa zina athari hasi au chanya dhidi ya nafasi yako kwenye uhuru wa kifedha. Jinsi unavyofikiria dhidi ya pesa inaweza kuwa chanzo cha wewe kuendelea kuwa masikini au kutofanikiwa katika yale unayofanya. Hivyo katika sehemu hii ya kwanza mwandishi anatushirikisha kanuni ambazo zinatoa mwongozo wa namna ya kufikri kitajiri na hatimaye kujenga msingi imara wa safari ya utajiri.  

1. Kanuni ya Kwanza: Kila mtu anaweza kuwa na fedha anazozitaka, ni suala la yeye kujiweka sawa kwenye kanuni za kutengeneza fedha. Kuwa na pesa ni haki ya kila mmoja bila kujali rangi, kabila, umri, historia ya wazazi wake au utaifa wake. Kila siku inafungua mlango kwako kwa ajili ya kutumia fursa zilizopo ili kuweza kutengeneza pesa unazotaka na hivyo ni muhimu kwako kujifunza mbinu wanazotumia matajiri kutengeneza pesa zaidi na mbinu hizo zipo wazi kwa kila mmoja. Kitu pekee kinachoweza kukukwamisha ni wewe mwenyewe na mtazamo wako juu ya upatikanaji wa fedha. Kanuni hii ndio kanuni kuu ya kutengeneza pesa na kanuni nyingine zinahusu wewe kujijengea misingi ya ya kuendelea kutengeneza pesa zaidi na ziadi.

2. Kanuni ya Pili: Kuwa Na Maana Yako Juu Ya Neno “Utajiri”. Katika kanuni hii mwandishi anatushirikisha kuwa utajiri unaanza na wewe kufafanunua nini maana ya utajiri kwa mtazamo wako. Nini hasa unataka kupata ili ukishapata vitu hivyo ndo uone kuwa umekuwa tajiri. Hivyo kabla haujaanza safari ya utajiri anza kwa kuadaa orodha ya yale yote unayoyataka katika maisha yako ya utajiri. Hapa haupaswi kujifunga kwa kutengeneza picha finyu bali unatakiwa kuwa na fikra pana ambazo pengine zinakufanya uziogope kwa sasa.

3. Kanuni ya Tatu: Tengeneza Lengo Lako. Baada ya kuwa na maana yako ya utajiri ambayo ni sawa na kilele cha safari yako hivyo unapaswa kutengeneza lengo kubwa ambalo litakuwa ni njia ya kuelekea kwenye kilele hicho.  Hapa unapaswa kuweka muda ambao unategemea kufikia kilele cha utajiri wako, eleza njia zipi zitatumika kufikia utajiri huo, ainisha changamoto ambazo ambazo unahisi zinaweza kukukwamisha na hatimaye kuwa na mpango wa kupambana na changamoto hizo. Lengo linatakiwa liwe linatekelezeka, lenye uhalisia na linatoka ndani mwako.

4. Kanuni ya Nne: Lifanye Lengo Lako Kuwa Siri. Unapoanza safari ya kuishi lengo kubwa ulilojiwekea ina maana kuwa unaanza maisha mapya ambayo yatakufanya uwe mtu wa tofauti ikilinganishwa na maisha yako ya zamani. Hivyo katika maisha haya mapya wapo wengi ambao hawatafurahia jinsi unavyobadilika kutokana na chuki zao au wivu kwa vile unaelekea kwenye maisha ya tofauti na wao. Kwa hali kama hii unatakiwa malengo uliyojiwekea yawe siri yako ili husikatishwe tamaa na maneno ya jamii inayokuzunguka.

5. Kanuni ya Tano: Watu Wengi Ni Wavivu Kufikia Utajiri Wao. Hakuna njia nyingine ya kuwa tajiri zaidi ya kufanya kazi kwa bidii. Ni lazima uwe tayari kufanya kazi kwa nguvu zako zote kuhakikisha unafanikisha malengo uliyojiwekea. Hakikisha unaamka asubuhi na kuanza kutekeleza majukumu yako ya kila siku na hata pale unapoenda kulala fanya hivyo ukiwa katika picha kubwa ya lengo kubwa la maisha yako.

Husitegemee kuwa tajiri kwa fedha za kurithi, fedha za bahati na sibu au fedha za kuokota. Watu wengi wanataka utajiri lakini hawapo tayari kujibidisha ili wafikie utajiri huo, hawapo tayari kujifunza, hawapo tayari kufanya kazi, hawapo tayari kutoa sadaka kwa ajili ya kuupata utajiri na mbaya zaidi wengi wana fikra hasi kuwa ili uwe tajiri ni lazima uende kwa wachawi au utajiri ni kwa ajili ya wateule wachache. Utajiri wa kweli hauko hivyo bali ni lazima uandaliwe kwa kutumia misingi na mifumo ambayo inakuhusisha wewe kama mhusika mkuu wa safari hii. Hii nikutokana na ukweli kwamba matajiri wote wana sifa kubwa ya kufanya kazi za ziada kiasi kwamba kazi wanazofanya kwa siku ni zaidi ya zile tunazofanya kwa mwezi mzima.

6. Kanuni ya Sita: Jifanyie Tathmini Ambayo Ni Ya Kweli. Ili uwe tajiri ni lazima ujifanyie upekuzi kwanza. Katika upekuzi huu unatakiwa kufahamu ni tabia zipi ambazo zimekufikisha hapo ulipo na hatimaye weka mikakati ya kukabiliana na tabia ambazo zinakukwamisha. Kaa chini na fikiria ni tabia zipi ambazo ukianza kuzifanya zitapelekea utajiri wako uongezeke na anza mara moja kuzifanyia kazi. Kuwa mkweli kwenye matumizi ya pesa yako, muda, marafiki na manunuzi yako.  Kisha jenga tabia ya kutenga kiasi cha fedha kwenye kila shilingi inayoingia mkononi mwako kwa ajili ya uwekezaji wa muda mfupi na muda mrefu. 

7. Kanuni ya Saba: Fahamu Imani/Kauli Zako Kuhusu Pesa Na Vyanzo Vya Kauli Hizo. Katika jamii tunazoishi kuna kila kauli juu ya fedha na utajiri kwa ujumla. Wapo wanaoamini kuwa pesa ni chanzo cha maovu yote, utajiri ni kwa wateule tu, matajiri ni watu wabaya, warafi, wachoyo, wachawi kwa maana ya kwamba hauwezi kuwa na fedha na kwa wakati huo huo ukawa msafi wa roho, ni afadhari kuwa maskini na kauli nyinginezo. Je wewe imani/kauli zako juu ya fedha na utajiri ni zipi? Pata muda wa kutafakari na hatimaye jipe imani/kauli mpya ambazo zitakupeleka kwenye mtazamo mpya juu ya pesa na utajiri.

8. Kanuni ya Nane: Fahamu kuwa Utajiri ni Mchakato na sio zawadi. Katika kutafuta utajiri ni lazima ujitoe kufanya kazi kwa bidii ili fedha zifuatie kama zawadi kwa bidii na ubunifu katika utendaji kazi wako. Kadri unavyofanyakazi kwa bidii na ubunifu ndivyo unavyopata pesa zaidi.

9. Kanuni ya Tisa: Andaa sababu zinazokusukuma kuwa tajiri. Hakikisha unaandaa sababu za kwa nini unataka kuwa tajiri. Eleza nini utafanyia pesa zako pindi ukiwa na pesa za ndoto yako, chagua ni starehe zipo utakuwanazo pindi ukiwa tajiri, sehemu zipi utapenda kutembelea, vitega uchumi vipi utapenda kuwa navyo n.k. Hapa unatakiwa kuandaa sababu ambazo zitakufanya uridhike na kufurahia utajiri wako badala ya kuja kuangamizwa na utajiri wako. Pia andaa orodha ya vitu ambavyo hautakuwa tayari kufanya kupitia utajiri wako ili kesho na keshokutwa uongozwe na hiyo kuepuka matumizi mabaya ya fedha zako.

10. Kanuni ya Kumi: Fahamu kuwa Pesa zinatengeneza Pesa. Tumia pesa zako kuhakikisha zinatengeneza pesa nyingine zaidi na zaidi. Ndio maana matajiri wanaendelea kuwa matajiri wakati masikini nao wanaendelea kuwa masikini. Hivyo kwa kutumia kanuni hii unatakiwa kutumia pesa kidogo ulizonazo sasa kwa ajili ya kuzalisha pesa zaidi na zaidi kwani hiyo ndo njia pekee ya kuwa tajiri. Hakikisha unatenga kiasi cha pesa katika pato lako kwa ajili ya kuwekeza ili kiasi hicho ndo kitumike kama mbegu ya kuzalisha pesa nyingine. Kama ilivyo kwa mkulima au mfugaji hawezi kula mbegu au mifugo yake yote na akategemea kuzalisha zaidi shambani au mifugo kuongezeka ndivyo ilivyo kwenye fedha. Uamzi upo mikononi mwako kati ya kuchagua kuwa masikini au kuwa kati ya matajiri.

Uchambuzi wa kina wa kanuni zote (107) umeandaliwa kwa mfumo wa pdf na unapatikana kwa gharama ya Shilingi za Kitanzania (TSHS) elfu tano tu (5,000/=). Uchambuzi wa kanuni zote una jumla ya kurasa 39 na ni kitabu ambacho unaweza kusoma kwenye simu yako ya mkononi kama ni simu janja (smart phone) au kwenye kompyuta mpakato (pc).

Kupata uchambuzi wa kanuni zote tuma pesa yako kwa njia ya M-pesa au Airtel Money kupitia namba zifuatazo:-

M – Pesa tumia namba: 0763 745 451 (Majina ni Augustine Mathias)
Airtel Money tumia namba: 0786 881 155 (Majina ni Augustine Mathias)

Baada kutuma pesa hiyo nitumie ujumbe kwenye namba ya airtel (0786 881 155) ukiwa na barua pepe yako ili nikutumie uchambuzi wa kanuni hizi moja kwa moja kwenye mtandao wako.

Karibu kwenye mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI ili upate elimu isiyokuwa na mwisho.

Born to Win~Dream Big 

Augustine Mathias Bilondwa

Namba ya Simu:      0786881155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com


onclick='window.open(