Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa
ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI
kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya 25 katika
kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi wa vitabu nikiwa na
lengo kubwa la kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako kuyatumia ili ubadilishe
kila sekta ya maisha yako.
Uamzi wa kubadilisha maisha yako upo
mikononi mwako na hivyo kama mpaka sasa haujajifunza kitu chochote katika
makala hizi nakushauri husiendelee kupoteza muda wako na badala yake ufanye
mambo ambayo umezoea.
Ili uendelee kunufaika na makala za
mtandao huu BONYEZA HAPA na
ujaze fomu utakuwa umejiunga na mtandao wa fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na
mtandao huu utapata makala zinazochapishwa na mtandao wa fikra za kitajiri moja
kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “Leading Quietely” kutoka
kwa mwandishi Joseph L. Badaracco Jr. Mwandishi wa kitabu hiki ni Profesa
katika Chuo Kikuu cha Havard. Katika majukumu ya kazi yake Profesa Badaracco
amejihusisha na majukumu ya uongozi kama Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa
Majukumu ya Wamiliki wa Chuo. Pia mwandishi wa kitabu hiki ameandika vitabu
mbalimbali juu ya mazingira/misingi ya biashara, uadilifu na uongozi.
Kwa
ujumla mwandishi anatushirikisha kuwa ni kawaida katika jamii kusikia majina ya
watu wakubwa ambao watu wengi wanawatumia kama mashujaa wao (role models). Pamoja
na kwamba mashujaa hawa huwa wanaimbwa na kusifiwa kutokana na matendo yao
lakini nyuma ya ushindi wao huwa kuna watu wengi ambao matendo yao hayasifiwi
au kufahamika. Kwa bahati mbaya watu hawa wanatumia nguvu na maarifa mengi kwa
ajili ya kampuni/taasisi wanazofanyia kazi bila ya kupewa thamani halisi ya
mchango wao na pengine kazi zao ndizo zinapelekea watu wengine kupewa tuzo za
utendaji kazi bora.
Hata
hivyo, mwandishi anatushirikisha kuwa kundi la watu hawa katika jamii ni kubwa
sana na kwa asilimia kubwa ni kundi hili ndo linabadilisha dunia na kuifanya
kuwa mahala pazuri pa kuishi. Juhudi za kundi hili zinahusisha majukumu ya
wafanyakazi au watu wa kawaida katika kila siku ya maisha yao. Kitabu hiki
kinatoa mwongozo wa maisha ya viongozi wasiofahamika kwa watu wengine lakini
matendo yao ni yamenufaisha watu wengi katika jamii inayowazunguka.
Karibu
tujifunze wote machache niliyojifunza kwenye hiki:
1. Viongozi
wasiowavuma muda wote wanaishi katika tumaini jema pindi wanapotimiza majukumu
yao. Katika hali hii viongozi hawa wanahakikisha wanafanya kazi kwa weledi na
ubunifu wa hali ya juu kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi wa hali
ya juu. Mwandishi wanawalinganisha watu katika kundi hili kama chombo katika
taasisi/kampuni/jamii ambacho kazi yake kubwa ni kufikri juu ya changamoto
zilizopo na namna bora ya kubaliana nazo kabla hazijawa na madhara.
2. Viongozi
wasiovuma wanafahamu na kuthamini mchango wa ushindi/matukio madogo madogo
katika maisha yao ya kila siku. Kwa mantiki hii viongozi katika kundi hili
wanahakikisha kila siku wanatumia muda wao vizuri kwa ajili ya kuhakikisha kila
siku inatengeneza ushindi kwa ajili ya kesho. Kwa kutambua thamani ya ushindi
mdogo mdogo viongozi hawa wanahakikisha kila siku wanafanya vitu ambavyo ni
sahihi na hivyo kuepuka kufanya makosa ya mara kwa mara.
3. Viongozi
wasiovuma wanatambua kuwa hawafahamu kila kitu na hivyo wanatumia muda wao
kijifunza kutoka kwa wengine. Kutokana na ukweli huu viongozi hawa wanakuwa na
mashujaa wao ambao mara nyingi ujifunza vitu vingi kutoka kwao. Hii ni nyenzo
muhimu inayotumiwa na viongozi hawa kwa ajili ya kujifunza majukumu ya kazi yao
lakini pia kufahamu majukumu na mahitaji ya watu wanaowaongoza.
4. Viongozi
wasiovuma wanatumia muda wao kwa ajili ya kutafakari juu ya mambo
yasiyofahamika katika utendaji kazi wao. Kutokana na sifa hii viongozi hawa
wanaweka mambo yasiyofahamika katika makundi mawili. Kundi la kwanza
linajumuisha mambo ambayo hayafahamika katika mazingira yao lakini tayari
yamejukalina kuwa yapo. Kundi hili linaweza kujumuisha matukio kama mabadiliko
ya tabianchi, magonjwa, mabadiliko ya soko n.k. Viongozi wazuri wanatumia muda
wao kuweka tahadhari katika bajeti zao kwa ajili ya mabadiliko katika kundi
hili.
Kundi la pili
linajumuisha mambo/matukio yasiyofahamika kwa ujumla katika mazingira ya
mhusika na hivyo matukio haya hayawezi kutabiliwa wala kuhisiwa namna
yanavyoweza kutokea. Viongozi wasiovuma wanajiwekea umakini mkubwa katika
makundi haya yote ili pale yanapotekea yasiathiri utendaji wa kazi wao.
5. Viongozi
wasiovuma wanaishi kwa kutambua kuwa tunaweza kuelewa maisha yetu kwa kuangalia
matukio yaliyopita lakini pia kwa kuishi maisha ya sasa ambayo yanaongozwa na
maono ya matukio yajayo. Kwa ujumla falsafa hii ni nzuri kwa mtu yeyote
kutokana na upekee wake wa kuangalia maisha katika pande mbili za matukio ya
yale yaliyopita na maono chanya katika matukio yatarajiwayo. Kutokana na
falsafa hii kila mmoja anaweza kujifunza kutokana na matukio yaliyopita na hivyo
matukio hayo yakatoa mwongozo wa kuweka maono kwa ajili ya matukio ya baadae.
Pia, kwa falsafa hii tunaweza kujibu maswali ya kwanini matukio flani yanatokea
au hayatokei katika historia ya maisha mwanadamu.
Soma: Mambo Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha A Brief History of Humankind (Historia Fupi ya Mwanadamu)
6. Viongozi
wasiovuma wanafanyia kazi matukio yanayoonekana kuwa na athari mbaya kwa siku
zijazo dhidi ya taasisi au kampuni wanazofanyia kazi. Mwandishi anatushirikisha
kuwa watu wengi wana uwezo wa kuona matukio katika ulimwengu wa kesho japo ni
wachache sana ambao wanawekeza kwenye kufanyia kazi maono yao kwa ajili ya kuboresha
matukio hayo. Watu wengi pamoja na kuona maono ya matukio ya ulimwengu wa kesho
wanakaa kimya pasipo kufanya jitihada zozote mpaka pale matukio husika
yanapojidhihirisha katika maisha yao.
7. Viongozi
wasiovuma wapo tayari kujitoa sadaka kwa manufaa ya wengine. Mwandishi
anatushirikisha kuwa viongozi wasiovuma wana kariba ya kufanya kazi kwa msukumo
wa kutekeleza kile ambacho wanaamini ni sahihi pasipo kujali athari za matokeo
ya maamzi yao katika maisha yao ya kila siku hata kama ni kutoa uhai wao kwa
ajili ya wengine. Kwa mantiki hii viongozi hawa wanaongozwa na roho ya upendo
katika kuhakikisha wanafanya matendo mema yanayonufaisha wanajamii bila kujali
hata kama kuna wachache wanaumizwa na matendo yao.
8. Watu
wengi wameshindwa kujitoa maisha yao kwa wengine kwa vile wanaongozwa na
ubinafsi. Mwandishi anatushirikisha kuwa pamoja na kwamba wapo viongozi ambao matendo
yao yanaongozwa na kisingizio cha kufanya kazi kwa faida ya wengine lakini mara
nyingi ukichunguza matendo yao kwa undani utagundua kuwa wengi wao wanafanya
yale wanayofanya kwa ajili ya manufaa yao binafsi.
9. Viongozi
wasiovuma wanaongozwa na mawazo/fikra pana ambazo ni mchanganyiko wa maono
walinayo katika kila sekta ya maisha yao. Mwandishi anatushirikisha kuwa
viongozi wa aina hii hawafanyii kazi sehemu mmoja ya maisha yao na kuridhika
bali kila mara wanakuwa na kiu ya kuendelea kuwa bora zaidi katika sekta ya
maisha yao. Kutokana na ukweli huu, viongozi hawa wana kila sababu ya
kufanikiwa katika kila aina ya changamoto wanazokutanazo kwenye maisha yao ya
kila siku.
10. Viongozi wasiovuma wanaongozwa na
vitendo kuliko maneno. Mwandishi anatushirikisha kuwa mara zote viongozi hawa
wanajisikia faraja kutokana na matokeo ya vitendo vyao na hivyo kila wakati
maisha yao yapo kivitendo zaidi. Hata hivyo changamoto kubwa ambayo inawakabili
viongozi wasiovuma ni namna watakavyofanikisha mlinganyo wa matendo kwa ajili
ya manufaa binafsi na manufaa ya wote. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kama
mhusika hayupo makini anawezakujikita kwenye manufaa binafsi na kusahau upande
mwingine au kinyume chake pia ni sahihi.
11. Viongozi wasiovuma kabla ya kutoa jibu wanatumia
muda kutafakari athari za kile walichoulizwa ikilinganishwa na majibu yao.
Kutokana na hali hii kila jibu linalotoka kinywani mwao ni lazima kwanza
lichambuliwe kwa kina ili kupima athari zake kwenye jamii inayowazunguka au
athari zake kwenye misingi ya taaluma zao. Na hapa mara zote viongozi wa aina
hii wapo tayari kwa jambo lolote lile ikiwa wanalazimishwa kufanya jambo ambalo
ni kinyume na misingi ya kazi au falsafa zao.
12. Viongozi wasiovuma wanatumia mbinu za
kuchelewesha muda kwa weledi (delaying tactics) kama njia ya kupunguza au
kuhamisha puresha kutoka kwa wasimamizi wao wa kazi. Hivyo viongozi hawa
wanatumia muda huo mfupi kwa ajili ya kurekebisha matatizo au changamoto ambazo
kwa wakati huo ni kizuizi katika ufanisi wa utendaji kazi wao. Mfano, ni
kawaida kwa viongozi hawa kutoa majibu kama “naomba unipe muda nilifanyie
kazi”, “nipo kwenye kikao nitakutafuta nikitoka”, “kwa sasa nimebanwa na
majukumu naomba niifanye kazi hii kesho” n.k. Hata hivyo, viongozi hawa ili
wasionekane wababaishaji ni lazima wawe makini na ahadi wanazotoa kwa ajili ya
kutimiza kile walichotakishwa.
13. Viongozi wasiovuma wanatenga muda kwa
ajili ya kuwekeza kwenye mahusiano mema na jamii na jamii inayowazunguka. Hii
inawasaidia viongozi hawa kuwa na mtaji wa kijamii wa kutosha ambao wanaweza kuutumia
nyakati wanapokabiliwa na matatizo katika sehemu zao za kazi. Mtaji huu ndio
njia pekee inayomwezesha mhusika kujenga heshima na uaminifu kwa wafanyakazi
wenzake na jamii inayomzunguka kwa ujumla.
14. Viongozi wasiovuma wanatoa maisha yao
kwa ajili ya manufaa ya taasisi, familia au jamii zinazowazunguka. Hapa
mwandishi anatushirikisha kuwa muda wote viongozi hawa wanaishi katika misingi
ya falsafa za maisha yao na hivyo hawapo tayari kwa jambo lolote ambalo lipo
kinyume na misingi hii. Kwa kufanya hivi, mara zote viongozi hawa wanaweka
mbele maslahi ya taasisi zao au watu wao wa karibu kuliko maslahi binafsi na
hivyo hali hii inapelekea wawe tayari kulipa gharama yoyote kwa ajili ya
kufanikisha ajenda waliyonayo kwa maslahi ya taifa au taasisi.
15. Viongozi wasiovuma wanaongozwa na dira
ya kufanikisha kusudi la maisha yao. Mwandishi anatushirikisha kuwa viongozi wa
kweli katika kila tukio la matendo yao muda wote wanaongozwa na ile hamasa ya
kuona wametimiza kusudi la maisha yao. Kutokana na ukweli huu, viongozi hawa
wanajisikia amani rohoni mwao pale wanapoona maisha yao yanatimiza kusudi la
uwepo wao duniani humu. Hapa ndipo kila mwenye kuhitaji kuwa kiongozi ni lazima
kwanza ajiulize maswali ya yeye ni nani na kwani nini aliumbwa. Hapa ndipo
mwanafalsa nguli Aristotle anatushirikisha kuwa ili uishi kusudi la maisha yako
ni lazima maisha yako yatawaliwe na wema. Na maisha haya ya wema yanajengwa na
misingi minne (4) ambayo ni busara, haki, ujasiri na uvumilivu. Hivyo misingi
ni muhimu kwa kila kiongozi pasipo kujali ni ngazi ya nafasi yake katika
taasisi, kampuni au jamii.
16. Matunda ya viongozi wasiovuma yanategemeana
na mazingira ya utendaji kazi katika sehemu husika. Mazingira ya utendaji kazi
yanajumuisha vikwazo/vizuizi kutokana na matumizi ya teknolojia, sheria/kanuni
pamoja na itifaki/tamaduni za sehemu husika. Kutokana na ukweli huu vikwazo
hivi vinaendelea kuwabana viongozi wengi ili wasivuke mipaka katika matendo
yao. Hata hivyo, teknolojia ni nyenzo muhimu kwa kila kiongozi kwa ajili ya
kufanikisha jitihada zake kwa urahisi. Hapa ndipo viongozi wanahitaji kutumia
muda mwingi kwa ajili ya kujielimisha juu matumizi ya teknolojia mpya vinginevyo
wataonekana wanafanya mambo kizamani.
17. Kukua kwa teknolojia kumesababisha
uwepo wa makundi ya kitaaluma na hivyo watu wanalazimika kuchagua ni taaluma
ipi wawekeze nguvu zao. Hatua hii inapelekea watu kufahamu vitu vichache kwa
kina zaidi katika taaluma walizochagua. Hata hivyo viongozi wasiovuma pamoja na
kwamba wana taaluma zao wanajitahidi kufahamu mambo ya muhimu nje ya taaluma
zao. Hatua hii inapelekea viongozi hawa wafahamu mambo mengi ambayo ni muhimu
katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili kwa utandaji kazi wao wa kila
siku.
18. Viongozi wasiovuma wanatumia
ugumu/changamoto zinazowakabili kama sehemu ya kujifunza vitu vipya. Mwandishi anatushirikisha
kuwa sifa moja waliyonayo viongozi wasiovuma ni ile hali ya kutokata tamaa hata
kama wanakabiliwa na nyakati ngumu. Kila nyakati zinazowakabili wanatambua kuwa
zina milango ya fursa ndani mwake na hivyo wajibu wao mkubwa ni kuhakikisha
watafuta fursa hizo kwa ajili ya utatuzi wa changamoto husika.
19. Viongozi wasiovuma mara nyingi
wanatafuta namna ambavyo wanaweza kupindisha sheria kwa ajili ufanisi wa kazi. Tunafahamu
kuwa kila kiongozi anatakiwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria japo kuna
mazingira ambayo yanapelekea kutafuta namna unavyoweza kucheza na sheria na
hatimaye ukapata matokeo tarajiwa kwa haraka zaidi. Hatua hii sio tu inasaidia
kufanikisha mambo kwa haraka bali pia inaweza kusaidia kulinda pande mbili
dhidi ya migogoro isiyokuwa na ulazima.
20. Viongozi wasiovuma wanaongozwa na
busara kutatua changamoto zinazowakabili. Kama ambavyo tumeona kuwa busara ni
moja ya misingi ya uongozi ndivyo mwandishi anatukumbusha kuwa kuna nyakati
ambazo viongozi watajikuta katika changamoto za kisheria dhidi yao. Kiongozi anapokuwa
kwenye hali kama hii mara nyingi kwanza wanaongozwa na busara ambayo inawapa
ujasiri wa kukabiliana na changamoto zilizopo dhidi yao. Kwa ufupi mwandishi
anatushirikisha kuwa hatupaswi kukimbia au kukubaliana na kesi dhidi yetu bali
kama viongozi tunatakiwa kutafuta njia salama ya kutatua kesi husika.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com