Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa
ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI
kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya 27 katika
kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi wa vitabu mbalimbali
kwa ajili ya kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako kuyatumia ili ubadilishe kila
sekta ya maisha yako.
Ni matumaini yangu kuwa makala hizi
zimekuwa na msaada mkubwa kwako kwa kadri ambavyo umekuwa ukiachukua hatua za kubadilisha
maisha yako. Hata hivyo, makala hizi haziwezi kubadilisha chochote kama umekuwa
mtu wa kusoma na kutokufanyia kazi yale unayojifunza.
Ili uendelee kunufaika na makala za
mtandao huu BONYEZA HAPA na
ujaze fomu kisha bonyeza “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao wa
fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa
humu moja kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “Ho To Negotiate
Better Deals” kutoka
kwa mwandishi Jeremy G. Thorn. Katika kitabu
hiki mwandishi anatushirikisha jinsi tunavyoweza kutumia mbinu za kufanya majadiliano
ya dili kubwa za kibiashara kwa kujiamini ili hatimaye tufanikiwe kupata/kuuza
bidhaa/huduma kwa bei nzuri.
Katika
biashara yoyote ile majadiliano kwenye bei ya bidhaa/huduma ni muhimu kutokana
na ukweli kwamba bei ya awali huwa inalenga kunufaisha upande mmoja. Kupitia
majadiliano haya pande zote mbili zitakubaliana bei ya mauziano na hatimaye
ushindi kwa kila upande utategemea na uwezo wake kwenye kufanya majadiliano. Hata
hivyo, ni lazima kukumbuka kuwa dili nzuri za biashara zinaharibiwa na uwezo
mdogo wa majadiliano kwa mhusika.
Mbinu
hizi za majadaliano tukiachana na matumizi yake kwenye ulimwengu wa biashara
tunatakiwa kufahamu kuwa ni mbinu hizi hizi pia zinatumika katika makubaliano
ya aina yoyote ile kati ya pande mbili. Yanaweza kuwa makubaliano kwa ajili ya
kuomba kazi, kuongezewa mshahara, makubaliano ya amani au makubaliano kwenye
mahusiano.
Mbinu
za majadiliano zipo wazi kwa kila mtu kwani kila mtu anaweza kujifunza mbinu
hizi nakuzitumia kwa faida yake katika maisha yake ya kila siku. Kupitia kitabu
hiki mwandishi anatushirikisha sifa na mbinu muhimu ambazo unatakiwa kuwa nazo
kwa ajili ya kufanya majadilino ya kibiashara kwa faida yako.
Karibu
tujifunze wote machache niliyojifunza kwenye hiki:
1. Watu
wengi wanashindwa kufanya majadiliano ya dili za kibiashara kwa vile wanakandamizwa
na tamaduni za sehemu husika au fikra hasi. Tamaduni hizi mara nyingi zinapelekea
watu wengi kuwa na uoga wa kufanya majadiliano ambao mara nyingi hugawanyika
katika sehemu kuu tatu ambazo ni uoga wa kushindwa, uoga wa kukataliwa na uoga
kutokueleweka. Mwandishi anatushirikisha kuwa kama unahitaji kufanya vyema
kwenye makubaliano ya kibiashara kwanza kabisa unahitaji kuondoa hofu, uoga
pamoja na imani za kijamii na hatimaye ujivike roho ya ujasiri. HUSIOGOPE
KUVUNJA BEI AU KUSIMAMIA BEI UNAYOHITAJI.
2. Tambua
kuwa mara zote bei ya kwanza huwa sio nzuri kibiashara. Mwandishi anatushirikisha
kuwa kama unahitaji kununua bidhaa/huduma kubwa kibiashara ni lazima utambue
kuwa bei inayotolewa awali juu ya bidhaa/huduma husika sio rafiki kwako wewe. Hapa
unahitaji kufanya makubaliano ya kibiashara (kuvunja bei) mpaka kufikia hatua
ambayo bei husika itapungua angalau kwa asilimia 10 – 20. Kufanikisha zoezi
hili unahitaji kuwa mvumilivu, mtulivu wa akili, jasiri, udhibiti hisia zako na
kuweka msimamo wako wa bei ambayo upo tayari kutoa. Hizi ni baadhi ya sifa
muhimu ambazo unahitaji kuwa nazo kwa ajili ya kumudu makubaliano ya dili bora
za kibiashara.
3. Anzisha
majadiliano juu ya makubaliano ya kibiashara kama kweli umejiandaa na kama
haujajiandaa ni vyema ukasubiri muda ambayo utajisikia kuwa upo tayari. Mwandishi
anatushirikisha kuwa watu wengi wanashindwa kufanya makubaliano ya dili kubwa
za kibiashara kwa vile wanaingia kwenye makubaliano ya bei kichwa kichwa pasipo
kuwa na taarifa muhimu juu ya bidhaa/huduma iliyopo sokoni. Kumbe basi hapa
tunashauriwa kuwa kitu cha kwanza unachotakiwa kufanya ili ufanikishe makubaliano
ya kibishara unahitaji kuifahamu kwa kina bidhaa/huduma husika na namna ambavyo
unaweza kuitumia katika mazingira ya kazi yako.
4. Fahamu
kuwa sio kila sehemu unaweza kufanya makubaliano ya kibiashara. Mwandishi anatushirikisha
kuwa makubaliano ya kiabiashara yanabadilika kutoka sehemu moja hadi nyingine
au kutoka kabila moja hadi jingine. Kutokana na ukweli huu unahitaji kubadilisha
mbinu zako za makubaliano ya kibiashara kwa kutegemea sehemu ulipo au nani unahitaji
kufanya naye biashara.
5. Fahamu
kuwa mara zote wauzaji wa bidhaa/huduma wanalenga bei ya juu ambayo ina faida
kubwa. Lengo kubwa la mfanyabiashara au mtoa huduma ni kuona anatengeneza faida
ikiwezekana hata mara mbili ikilinganishwa na bei halisi ya bidhaa/huduma yake.
Kutokana na ukweli huu mfanyabiashara au mtoa huduma anawalenga wateja ambao
wana uzoefu wa makubaliano ya biashara ambao kwa vyovyote vile atawauzia kwa
bei ya chini. Lakini pia anawalenga wateja ambao hawana uzoefu na makubaliano
ya kibiashara ambao mara nyingi wanauziwa kwa bei ya juu. Dhana hii unaweza
kuilewa vizuri ukiangalia mbinu wanazotumia machinga kuuza bidhaa zao mitaani. Machinga
wanachofanya ni kutaja bei ya juu zaidi ili mteja ataje bei aliyonayo, kama
hauna uzoefu utataja bei inayokaribia ile aliyokutajia na hivyo kujikuta
unanunua bidhaa kwa bei ya juu sana.
6. Kumbuka
kuwa haupotezi chochote pale ambapo utauliza kama unaweza kulipia kwa bei uliyonayo.
Mwandishi anatushirikisha kuwa suala la makubaliano ya kibiashara sio tu kwa
dili kubwa za biashara bali hata kwenye manunuzi ya bidhaa za kila siku. Kutokana
ukweli huu, mwandishi anatushirikisha kuwa mara zote epuka kununua
bidhaa/huduma kwa kuangalia bei iliyoorodheshwa na badala yake uliza kama
unaweza kupunguziwa bei kwa kila bidhaa husika. Kumbuka kuwa pamoja na
kuorodhesha bei ya kila bidhaa, mfanyabiashara anakuwa na ukomo wa bei ya chini
kabisa kwa kila bidhaa ambayo huwa ni siri yake hivyo kama haujatoa bei uliyonayo
mfanyabiashara atakuuzia kwa bei ya juu.
7. Kumbuka
kuwa kila makubaliano ya biashara ni lazima yawe na muundo wake. Kuna miundo ya
aina mbili ambayo unaweza kutumia kulingana na aina ya makubaliano ya biashara
unayofanya. Muundo wa kwanza ni ule unaolenga kunufaisha pande mbili (win-win
negotiation) na muundo wa pili ni ule unaojikita kwenye ushindani (competitive
negotiation). Muundo huu wa pili unalenga kunufaisha zaidi upande mmoja
(win-lose negotiation). Kuchagua ni muundo upi utumike katika makubaliano ya
kiabiashara itategemeana na mtu unayefanya nae biashara ameanzisha muundo upi. Mfano,
kama muuzaji hajatoa nafasi kwako kwa ajili ya majadiliano kwa vyovyote vile
utatumia muundo wa aina ya pili. Katika hali kama hii unaweza kukubali dili
husika kwa bei iliyotolewa au ukatoa bei yako na kupendekeza endapo muuzaji
atajifikiria akutafute kwa ajili ya kukamilisha biashara.
8. Heshima
na uaminifu kati ya pande mbili ni nyenzo muhimi katika kukamilisha makubaliano
ya biashara hasa katika muundo unaonufaisha pande zote. Ili kila mmoja anufaike
na biashara husika ni athamini utu wa mwenzake lakini pia awe na uaminifu kwa
kile anachohitaji kupata kutoka kwa mwenzake.
9. Unapojiandaa
kwa ajili ya kuanza makubaliano ya dili za kibiashara unahitaji kujiuliza
maswali ya kwa nini, nani, kipi na lini? Maswali haya yanatoa nafasi kwako
kutafakari juu ya msingi wa majadaliano yenu ya kibiashara na sababu kuu ya kwa
nini mnafanya makubaliano husika, kwa faida ya nani, juu ya bidhaa/huduma ipi
na lini mnatakiwa kukamilisha biashara husika. Hapa utagundua kuwa baada ya
majadiliano yenu mnatakiwa kila mmoja awe amefahamu jinsi mtakavyofanikisha kukamilisha
biashara husika na masharti yapi yanatakiwa kutekelezwa kabla ya kukabidhiana
bidhaa/huduma.
10. Fahamu ni lini unatakiwa kusema HAPANA
au NDIYO juu ya biashara husika. Hii ni pande zote zinazohusika kwenye
makubaliano ya biashara, iwe ni muuzaji au mteja unahitaji kutambua ukomo wako
wa bei ya chini au bei juu ambayo upo tayari kutoa au kupokea. Pale ambapo
unaona kuwa makubaliano hayaendani na mahitaji au uwezo wako huna budi ya
kuachana na biashara husika ili kuokoa muda wa kufanya mambo mengine.
11. Chagua timu yako makini kama
makubaliano ya biashara yanafanywa na watu wa taaluma mbalimbali. Mwandishi anatushirikisha
kuwa ni kawaida makubaliano juu ya dili kubwa za biashara kuwashirikisha watu
wa kada tofauti kwa ajili ya kila mmoja kushughulikia upande wa taaluma yake. Kutokana
na hali hii, kama kiongozi wa timu unahitaji kuhakikisha unachagua watu ambao
wanafahamu nini wanatakiwa kufanya na wana uzoefu wa kutosha katika makubaliano
ya dili kubwa za kibiashara. Baada ya kupata timu ya wataalamu hakikisha kila
mmoja unampa majukumu yake na mamlaka aliyonayo wakati wa zoezi la makubaliano
ya dili za kibiashara.
12. Kabla ya kuingia kwenye makubaliano ya
dili za kibiashara tumia muda wako kuwafahamu kwa kina wapinzani wako. Hapa mwandishi
anatushirikisha kuwa kama umebahatika kufahamu watu ambao wanagombea dili
husika hakikisha unatumia muda wako kufahamu nguvu na mapungufu waliyonayo. Pia,
kama wewe ni mnunuzi/muuzaji mtarajiwa unahitaji kufahamu kwa kina uwezo wa
muuzaji/mnunuzi ili kuondoa nafasi ya kushutukizwa katikati ya makubaliano ya dili
za kibiashara. Mara zote kumbuka kuwa kadri unavyomfahamu kwa kina mpinzani
wako ndivyo unakuwa na nafasi kubwa ya kushinda makubaliano ya dili ya
kibiashara husika.
13. Katika makubaliano ya dili za
kibiashara daima unahitaji kukumbuka kuwa kila sentensi inayotoka kwako ni
lazima iwe ina masharti ndani mwake dhidi ya muuzaji/mnunuzi kwa kutegemea nafasi
yako. Mfano, kama wewe ni mnunuzi unaweza kutumia sentensi kama “endapo
utapunguza bei yako kwa asilimia 10 tunaweza kupunguza masharti ya kutufikishia
mzigo” au “kama utakuwa tayari kufikisha mzigo mpaka kwenye anuani yetu basi
sisi tupo tayari kutoa kiasi hiki cha bei”. Sentensi zote mbili zinatoa
masharti ambayo muuzaji wa bidhaa anapaswa kuyatafakari kwa ajili ya kuboresha
bei ya bidhaa yake.
14. Mara zote kama wewe ni muuzaji kumbuka
kutangaza bidhaa yako kwa bei ya juu japo ukumbuke kuwa bei husika ni lazima
iwe halisi ikinganishwa na thamani ya bidhaa/huduma. Mwandishi anatushirikisha
kuwa kati majadiliano ya dili za kibiashara mara zote ni rahisi kushusha bei ya
bidhaa/huduma lakini ni vigumu kupandisha bei zaidi ya bei iliyotolewa awali. Kutokana
na ukweli huu, kama wewe unahitaji kuuza bidhaa/kutoa huduma ni lazima bei yako
ya awali iwe juu ili pale itakaposhushwa uendelee kuwa kwenye sehemu ya faida. Vivyo
hivyo, kama wewe ni mnunuzi unahitaji kutaja bei chini kabisa japo yenye
uhalisia ili kupitia majadiliano wote mfikie bei ambayo kila upande utaridhika.
15. Kumbuka kuweka wazi masharti ya ziada
wakati wa makubaliano ya dili za kibiashara. Mwandishi anatushirikisha kuwa
wakati wa makubaliano wa dili za kibiashara ni sehemu pekee ambapo unahitaji
kuweka wazi masharti yako. Mfano, kama wewe ni mnunuzi unahitaji kutaja
masharti juu ya bidhaa husika kuhusiana na vifungashio, mwaka wa kutengenezwa,
namna na lini mzigo unatakiwa uwe umefika, nani atahusika na gharama za
usafirishaji, bima endapo mzigo hautafika salama n.k. Haya masharti ambayo
yatakulinda wewe dhidi ya muuzaji kwani yanakuwa ni sehemu ya mkataba wa
mauziano kati yako na muuzaji.
16. Kuwa mwepesi wa kumsoma mwenzako
unayefanya nae makubaliano ya dili za kibiashara kwa ajili ya kugundua uelekeo
wake. Mwandishi anatushirikisha kuwa wakati wa zoezi la makubaliano ya dili za
kibiashara unahitaji kuwa macho muda wote kwa ajili ya kusoma hisia/ishara za
yule unayetaka kufanya nae biashara. Hii ni pamoja na kumsoma dimina ya uso
wake kwa kile anachozungumza pamoja na kuangalia lugha ya mwili muda wote
mazungumzo yanavyoendelea. Kama makubaliano yanafanyika kupitia mtandao unaweza
pia kujua hisia zake kupitia mtiririko wa mawasiliano yenu.
17. Tumia lugha ambayo una uhakika kuwa
pande zote mnaelewana kwa ufasaha. Mwandishi anatushirikisha kuwa endapo unafananya
biashara na mtu ambaye sio wa kabila au taifa lako unahitaji kuhakikisha
unachagua maneno rahisi ili kila mmoja wenu aweze kushiriki makubaliano ya
biashara husika. Hapa unahitaji kujifunza mbinu za kuongea na kusikiliza ikiwa
ni pamoja kuongea kwa taratibu ili upande wa pili upate maana ya kile
unachowasilisha.
18. Baada ya kufanya majadiliano ya muda
mrefu na wote mkakubaliana kwenye masharti ya kukamilisha dili husika sasa
unahitaji kuwa makini pindi mnapokamilisha majadiliano yenu. Huu ni muda ambao
kila mmoja anajifunga kwa kile ambacho ameahidi kutekeleza kwa ajili ya
kukamilisha dili husika. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika hatua hii ni
muhimu kutiliana saini za makubaliano kwa ajili kulinda matakwa ya kila mmoja. Hivyo,
kila upande hauna budi ya kusoma mkataba husika ili kujiridhisha kama umeweka
yale yaliyokubaliwa wakati wa majadiliano.
19. Ili kupata matokeo mazuri kutoka kwenye
makubaliano ya dili ya biashara husika unahitaji kuwa na nguvu ya kushawishi
upande wa pili katika biashara husika. Nguvu inapatikana kupitia ujasiri wako,
nguvu uliyonayo kwenye soko au ikibidi ujasiri wa kuondoka kwenye makubaliano
huku ukiwa umeacha masharti yako ili endapo watajisikia kuyakamilisha
wakutafute kwa ajili ya kukamilisha biashara husika.
20. Kabla ya kutia sahihi mkataba wa
makubaliano jidhirishe kupitia kwa mwanasheria wako kama mkataba husika
unatekelezeka kisheria. Mwandishi anatushirikisha kuwa mikataba ya makubaliano
inatofautiana kutoa sehemu moja hadi nyingine au taifa moja na jingine. Kutokana
na tofauti hizi, inabidi kupitia mwanasheria wako mjiridhishe kama yale
mliyokubaliana yanatekelezeka kisheria kwa mjibu wa sera, sheria za taifa
husika au sera za kampuni yako.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com