Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa
ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI
kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya 24 katika
kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi wa vitabu nikiwa na
lengo kubwa la kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako kuyatumia ili ubadilishe
kila sekta ya maisha yako.
Uamzi wa kubadilisha maisha yako upo
mikononi mwako na hivyo kama mpaka sasa haujajifunza kitu chochote katika
makala hizi nakushauri husiendelee kupoteza muda wako na badala yake ufanye
mambo ambayo umezoea.
Ili uendelee kunufaika na makala za
mtandao huu BONYEZA HAPA na
ujaze fomu utakuwa umejiunga na mtandao wa fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na
mtandao huu utapata makala zinazochapishwa na mtandao wa fikra za kitajiri moja
kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kabla
ya kuendelea kushirikisha uchambuzi wa kitabu cha leo nitumie muda huu kuomba
radhi kwa kuchelewa kukutelea uchambuzi huu ndani ya wiki iliyoisha jana. Hii
imetokana na sababu zilizo nje ya uwezo wangu kwa kuwa mazingira niliyopo kwa
sasa hayana nishati ya umeme ya uhakika.
Kitabu
cha wiki hii ni “So Smart But…..” kutoka
kwa mwandishi ALLEN N. Weiner. Mwandishi wa kitabu hiki amebobea katika
tasnia ya mawasiliano na kwa muda mrefu amejihusisha katika utoaji wa semina
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa kocha kwa watu mbalimbali katika masuala ya
mawasiliano na uzungumzaji. Semina zake mara nyingi zimejikita katika
kuwafundisha watu namna wanavyoweza kuboresha ushawishi, hamasa binafsi pamoja
na uaminifu bora kwa jamii inayowazunguka.
Mwandishi
huyu alipata msukumo wa kuandika kitabu hiki mara baada ya kuona kuwa watu
wengi wana taaluma mbalimbali kiasi ambacho wamefikia hatua ya kutambuliwa kama
watu maarufu katika taaluma zao. Pamoja na watu hawa kufikia viwango vya juu
vya taaluma, ajabu ni kwamba ni wachache kati ya watu hawa ambao wanaweza
kujieleza mbele za watu na kueleweka. Wengi wao wanahitaji msaada katika mbinu
za mawasiliano ili kufikisha ujumbe wanaokusudia. Tunafahamu fika kuwa bila
mawasiliano mwanadamu hawezi kufanikisha jambo lolote na hii ndio sababu kubwa mwandishi
wa kitabu hiki kuwaandikia watu kwa ajili ya kuwashirikisha misingi mikuu ya
mawasiliano.
Karibu
tujifunze wote machache niliyojifunza kutoka kitabu hiki:
1. Watu
kadri wanavyokuwa na uzoefu wa kazi/biashara ndivyo inafikia hatua wanahisi
kuwa kuna mtu juu yao ambaye hapendi kile wanachofanya. Mtu huyu anaweza kuwa
ni bosi wako au mshindani wa biashara. Hata hivyo hisia hizo zinasababishwa na
watu kutokufahamu mbinu za mawasiliano kwa kutumia lugha ya mwili. Zaidi ya
asilimia sitini ya mawasiliano katika jamii uwasilishwa kwa mfumo husio wa
maongezi ambao unahusisha lugha ya mwili. Mwandishi anatushirikisha kuwa
unaweza kupata matinki ya mtu anayewasilisha kwa kusoma namna ambavyo
anashirikisha viungo vya mwili wake katika kufikisha kuwasilisha ujumbe. Bahati
mbaya ni wafanyakazi wachache sana ambao wanatambua mbinu hii ya mawasiliano na
hivyo wengi wao wameshindwa kueleweka pindi wanapojieleza au pengine
wameshindwa kuwaelewa wafanyakazi wenzao au waajiri wao.
2. Ni rahisi
watu kutambua kiwango cha uaminifu/heshima yako kwa kuangalia lugha yako ya
mwili (jinsi unavyoonekana kwa ujumla), mpangilio wa sauti yako pamoja na
mpangilio wa maneno yako. Hivi ni vitu vitatu muhimu ambavyo vinamtambulisha
mtu yeyeto pindi anapowasilisha mada yake kwa mtu mwingine au watu wengine. Na
hapa ni muhimu kufahamu kuwa mwonekano wako pamoja na mpangilio wa sauti kwa
pamoja vinachangia asilimia tisini ya kueleweka kwako ikilinginishwa na
asilimia kumi tu ya mpangilio wa maneno. Muhimu, hapa unatakiwa kufahamu kuwa
unahitaji kujitambulisha haraka kwa kutumia lugha ya mwili wako (mwonekano
wako) pamoja na kuhakikisha kuwa unatoa sauti yenye kila chembe ya kujiamini
kwa kadri uwezavyo.
3. Ili
ueleweke kwa urahisi unahitaji vizingatia vitu vifuatavyo kwa ajili ya
kuboresha mwonekano wako; i) matumizi ya nafasi yako pindi unapojieleza ii)
matumizi bora ya kushikana mikono na wengine iii) matunmizi ya muda – zingatia kutumia
vyema muda uliopewa iv) mwonekano wa uso wako v) matumizi ya viungo vyako vya
mwili – fahamu namna ya kutumia kila kiungo cha mwili wako vi) zingatia mfumo
wa mavazi yako pamoja na unene wa mwili wako; na matumizi bora ya mapambo ya
nafasi.
4. Unapowasilisha
mada yako vitu vifuatavyo vitakusaidia kuboresha mpangilio wa sauti yako; i) kiwango
cha sauti yako – kuzungumza kwa sauti ya juu ili kila mmoja asikie; ii)
mpangilio wa sauti – kupanda na kushuka kwa sauti kwa kutegemea kila sehemu
unayozungumzia iii) kasi ya sauti yako iv) urefu wa sentensi zako v) matumizi
fasaha ya lugha vi) zingatia rafudhi ya lugha husika vii) zingatia matumizi
sahihi ya misamihati viii) zingatia matamushi sahihi ya misamihati ix) fahamu
kwa kina mantiki ya kile unachowasilisha x) hakikisha unaongozwa na takwimu
kuliko blah blah; na xii) hepuka kurudiarudia maneno mara kwa mara.
5. Fahamu
kuwa unaendelea kuchunguzwa na wasikilizaji wako hata baada ya kumaliza
wasilisho lako. Hapa mwandishi anatushirikisha kuwa ni muhimu kila mmoja
afahamu kuwa wasikilizaji huwa wana tabia ya kuchunguza vitu vidogo kutoka kwa
mtu anayewasilisha hata kama amemaliza kuongea. Mfano, wanaweza wakachunguza
jinsi unavyotembea, namna ulivyokaa na hata namna unavyowasikiliza wengine.
6. Kuna
njia tano za kukuwezesha kugundua kama unaeleweka kwa mada unayowasilisha na
njia hizo ni; i) chanzo cha mada – fahamu kwa kina chimbuko la mada yako na
namna unavyotakiwa kutumia lugha ya mwili kuiwasilisha; ii) ujumbe – fahamu nini
hasa unataka wasikilizaji wasikie/wapate kutoka kwako; iii) chunguza sehemu
ambapo wasilisho lako linafanyikia; iv) chunguza mtazamo wa wawasikilizaji –
hii itakusaidia kutambua kama unaongea jamii unayohitaji hama vinginevyo; na v)
nyakati – tambua mada unayowasilisha kama inaendana na nyakati zilizopo.
7. Watu
wengi wana taaluma ambazo zimewafanya kujichanganua kama wataalam wabobevu
katika sekta flani. Hata hivyo, ni wachache ambao wanaweza kuelezea kwa ufanisi
kile wanachofahamu kwa jamii inayowazunguka. Hii inatokana na ukweli kwamba
wengi wanashindwa kutafsri yale wanayofahamu katika taalamu zao kwenye
mazingira halisia ya jamii inayowazunguka. Kutokana na hali hii wengi wanakosa
uaminifu kwa jamii inayowazunguka ikiwa ni pamoja na mabosi wao au wafanyakazi
wenzao.
8. Uaminifu
wa mawasiliano yako kazini au jamii inayokuzunguka unapimwa kwa kuzingatia baadhi
ya misingi kama ilivyoorodheshwa hapa; i) epuka kuongea maneno mengi ambayo hayatekelezeki
– chagua maneno machache ya kuongea na hakikisha unaishi maneno yako; ii) mara
zote jikite kwenye mantiki ya mada unayowasilisha – epuka porojo; iii) kuwa na
uwezo wa kueleza mambo magumu katika lugha rahisi; iv) kuwa na mawazo mbadala
mengi kwa ajili ya kukuza pato la mwajiri wako au kupunguza upotevu wa
rasimali; v) mahusiano mema na wenzako – fanya kazi kama timu; vi) uwezo wa
kuingilia kati na kushauri pale ambapo mambo hayaendi sawa; vii) uwezo wa
kufanya majukumu yako kwa haraka; viii) kuwa mtu wa kufikiria kwa haraka; ix)
kuwa mwandishi mzuri; x) jifunze kuwa msilikazaji mzuri; na xi) uwezo wa
kujiamini kwa kile unachofanya. Misingi hii kwa ujumla, inalenga kumfanya kila
mmoja wetu kuwa na picha kubwa katika majukumu ya kazi pamoja na mahusiano yake
na jamii inayomzunguka.
9. Kuna
mbinu tano ambazo unaweza kutumia kwa ajili ya kueleza na mada yako na
ukaeleweka kwa ufasaha. Moja, ni kueleza mada yako ufupi lakini ukigusa maeneo
yote muhimu. Mbili, ni kueleza mada yako kwa mapana zaidi. Tatu, ni kueleza
mada yako kwa kina huku ukielezea kwa mapana kila eneo la mada yako – hapa unahitaji
kuweka wazi uhakika wako kwenye mada husika. Nne, unahitaji kuainisha kwa
mapana matokeo (faida au madhara) tarajiwa kutokana na kutekeleza/kutotekeleza
ushauri wako. Tano, onyesha maono yako juu ya fursa/changamoto zilizopo katika
mada unayowasilisha – hapa unahitaji kuonesha matumaini yako hasa chanya kwa
siku zijazo endapo ushauri wako utazingatiwa. Mbinu hizi zinaweza kutumiwa kwa
pamoja au kwa kuchagua baadhi yake pale ambapo mtu anakusudia kuwasilisha mada
yake na akaeleweka vizuri kwa walengwa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba endapo
utazingatia mbinu hizi kila mmoja atasema kuwa unafahamu malefu na mapana juu
ya mada unayowasilisha na pia unafahamu matokeo tarajiwa endapo ushauri wako
utachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwa na maono juu ya mada husika.
10. Baada ya kuwasilisha mada yako kwa
ufasaha unahitaji kufahamu mbinu za kuchukua maswali na kuyajibu kwa ufasaha
ili kukidhi mahitaji ya waulizaji. Mbinu hizi ni pamoja na i) kwanza unatakiwa
kuhakikisha unaandika maswali yote na kila mtu aliyeuliza; ii) elewa kiini cha swali
– tambua muulizaji anahitaji kufahamu nini; iii) tambua swali lina makusudi
gani – kuna baadhi ya maswali yanalenga kukupima ufahamu wako juu ya mada
husika; iv) jibu kwa ufasaha kuhakikisha ulefu wa majibu yako unaendana na
ulefu wa swali uliloulizwa; na v) epuka kurudirudia – jibu moja kwa moja
ulichoulizwa. Mwandishi anatushirikisha kuwa endapo kila mmoja atafuata mbinu
hizi katika kujibu maswali atafanikiwa kujijengea heshima kutoka kwa
wasikilizaji wake.
11. Unapotakiwa kuwasilisha mada yako ndani
muda mfupi unatakiwa kuzingatia sehemu kuu tano za mada yako. Kwanza, ndani ya
muda mfupi ainisha sehemu ya tatizo/fursa – hapa eleza kwa ufupi tatizo/fursa
iliyopo. Mbili, ainisha kwa ufupi visababishi – hapa unahitaji kueleza chanzo
cha tatizo au fursa husika. Tatu, ainisha madhara ya tatizo husika. Nne, eleza
kwa ufupi ni nini suluhisho la tatizo husika – njia za kufuata kwa ajili ya
kutatua tatizo. Tano, eleza nini kifanyike kwa ajili ya kutatua tatizo husika –
toa maoni yako yanayolenga kumaliza tatizo. Sehemu hizi tano zinalenga
kumwezesha mwajiriwa/mfanyakazi kurahisisha mada yake ili ionekane nyepesi kwa
mwajiri wake hata kama mada husika ni ngumu.
12. Watu wengi uaminifu kwa vile wanashindwa
kutambua tamaduni za jamii wanazofanyia kazi. Mwandishi anatushirikisha kuwa
tamaduni za sehemu husika wakati mwingine zinaweza kuonekana ni mambo ya kizamani
lakini yana mchango mkubwa katika kujenga uaminifu kwa mtu yeyote. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba pale ambapo utafanya tukio ambalo linaenda kinyume na
tamaduni au hitifaki za sehemu husika moja kwa moja utaonekana mtu wa hovyo na
hivyo kujishushia heshima yako.
13. Watu wengi wana akili lakini
wanashindwa kuona vitu katika maono ya picha kubwa. Mwandishi anatushirikisha
kuwa ni wafanyakazi wachache sana ambao wanakuwa na mtazamo wa picha kubwa
katika mazingira ya kazi zao kwani walio wengi wanaishia kutazama picha ya
mahitaji na majukumu yao tu. Ili kujitofautisha na watu wa namna hii mwandishi
anatushirikisha kuwa kila mmoja anatakiwa kuwa na picha kubwa ambayo
inajumuisha (a) maono ya taasisi au kiwanda (b) maono ya uongozi wa taasisi (c)
maono ya idara (d) maono ya timu au wafanyakazi wenzako na (e) maono yako
binafsi. Hapa utagundua kuwa wafanyakazi wengi huwa wanatanguliza maono binafsi
na kusahau maono mengine.
14. Kila mfanyakazi mwenye malengo ya
kudumisha uaminifu wake hana budi kuwa na maono ya ngazi tatu. Ngazi ya kwanza
inajumuisha maono ya karibu yako – hii inajumuisha maono juu yako mwenyewe kwa
maana ya unahitaji kuwa mtu wa aina gani, yapi unahitaji kuyakamilisha katika
maisha yako kupitia kazi unayofanya. Ngazi ya pili inajumuisha maono ya kati –
haya ni maono yako juu ya wafanyakazi wenzio au waajiriwa wako. Katika ngazi
hii unatakiwa uwe na upeo wa kutambua mahitaji ya wanaokuzunguka kutoka kwako –
nini hasa mchango wako kwa wale wanaokuzunguka. Ngazi ya tatu ni maono ya mbali
– haya yanajumuisha ndoto zako. Ngazi hii inajumuisha mchango au mawazo yako
ambayo unayatoa kwa taasisi au kampuni yako kwa ajili ya uendelevu wake. Kama mwajiriwa
mwenye uaminifu unahitaji kuonesha ngazi za maono haya kupitia yale unayosema
(mchango wako wa maneno), unayofanya (mchango wako wa vitendo) na jinsi
unavyojihusisha na majukumu yako (kiwango cha ufanisi wako katika majukumu
yako).
15. Wafanyakazi wengi katika ngazi za
uongozi wa juu wanakosa uaminifu kwa vile wanashindwa kuwa na uwezo wa kuhimili
misukosuko inayowakabili katika kazi zao. Hapa mwandishi anatushikisha kile
ambacho mabosi wengi wanashindwa kutimiza kwa vile wengi wanakuwa ni waoga wa
kusimamia maamuzi yao. Hili ni kosa ambalo linapoteza heshima kwa bosi yeyote
yule kwa watu wake wa chini kwa vile ataendelea kuonekana hana msimamo katika
maamuzi yake. Muda wote kama bosi watu wa chini yako wanahitaji wa kuone katika
misingi ambayo haibadiliki mara kwa mara.
16. Watu wengi wanashindwa kueleweka kwa
vile hawajui namna ya kuunda sentensi katika muuondo unaokubalika. Kwa ujumla
ujumbe wowote ambao unatolewa kwa njia ya maandishi au maongezi ni lazima
uhusishe muunganiko wa maneno ambayo kwa pamoja yanaunda sentensi ambazo nazo
zinaunda haya za mada husika. Kwa mantiki hii kila neno katika stori na kila
sentensi kwenye stori husika zinaunda mtiririko wa maana kwa msomaji au
msikilizaji. Hivyo kila mwandishi au mzungumzaji hana budi kuzingatia utumiaji
wa maneno na muunganiko wa sentensi zilizokamilika katika kila haya ya stori
yake.
17. Njia nyingine ambayo inawafanya watu
wengi washindwe kueleweka ni namna wanavyopangilia sentensi zao zenye maana
hasi na chanya. Sehemu hii inahusisha mbinu za sentensi ipi kati ya chanya au
hasi itangulie kwenye maongezi au maandishi ya mtoa stori. Mfano tazama
sentensi kama hizi 1. “kazi yako ni nzuri japo kuna vitu unatakiwa kuviboresha”;
2. Kuna vitu unatakiwa kuviboresha japo unafanya kazi nzuri. Katika sentensi ya
pili msikilizaji/msomaji atachukua maana ya mwisho ya sentensi na kuelewa kuwa
anafanya kazi nzuri wakati katika sentensi ya kwanza msikilizaji/msomaji
ataelewa kuwa pamoja na kufanya kazi vyema bado ana sehemu ambazo anahitaji
kuboresha. Kama mwandishi au mtoa mada kwa njia ya maongezi ni lazima uwe
tayari kutambua ni sehemu ipi kati ya sentensi chanya na hasi itangulie katika
stori yako kwa ajili ya kufikisha ujumbe uliokusudiwa.
18. Watu wengi wanashindwa kuaminika katika
jamii inayowazunguka kwa vile wanaishi katika falsafa ya kuamini kuwa
wanafahamu kila kitu. Mwandishi anatushirikisha kuwa huu ni ugonjwa mwingine
ambao unapoteza heshima kwa watu wengi kwa vile wanashindwa kufahamu kuwa
katika maisha kila mtu anahitaji kujifunza kila siku kutoka kwa wanaomzunguka. Mtu
anapoonekana kuwa yeye anafahamu kila kitu ni mara chache sana atachukulia kwa
ukaribu maoni ya watu wanaomzunguka na hivyo kusababisha hasieleweke kwa jamii
inayomzunguka.
19. Watu wengi wanapoteza heshima zao kwa
vile wanatumia maneno ambayo yanaifanya jamii inayowazunguka hisipende matendo
yao. Ni kawaida kusikia kusikia misemo kama “haijalishi kama wananipenda hama
la cha msingi ni lazima waniheshimu”. Kiongozi anayetumia kauli kama hizi
anakuwa sio mtu wa watu na badala yake anatumia mabavu kufanikisha majukumu
yake kwa watu waliopo chini yake. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika jamii
ni lazima kwanza uwekeze kwenye mtaji wa kijamii kwa maana yakujiweka karibu na
watu wa karibu yako. Hii ni pamoja na kujihusisha kwenye matukio ya kijamii
ambayo waajiriwa au jamii inayokuzunguka wanajihusisha nayo katika nje ya saa
za kazi.
20. Watu wengi wenye taaluma za juu wamepoteza
uaminifu/heshima kutokana na tabia mbaya wanazoishi katika jamii inayowazunguka.
Mwandishi anatushirikisha kuwa tabia ya mtu ni utambulisho wa mhusika kwa jamii
inayomzunguka. Unaweza kuwa na taaluma ya juu sana lakini kama hauna tabia
njema kamwe hauwezi kupata heshima kwa jamii inayokuzunguka.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com