Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa
ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI
kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya 21 katika
kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi wa vitabu nikiwa na
lengo kubwa la kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako kuyatumia ili ubadilishe
kila sekta ya maisha yako.
Uamzi wa kubadilisha maisha yako upo
mikononi mwako na hivyo kama mpaka sasa haujajifunza kitu chochote katika
makala hizi nakushauri husiendelee kupoteza muda wako na badala yake ufanye
mambo ambayo umeyazoea.
Ili uendelee kunufaika na makala za
mtandao huu BONYEZA HAPA na
ujaze fomu utakuwa umejiunga na mtandao wa fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na
mtandao huu utapata makala zinazochapishwa na mtandao wa fikra za kitajiri moja
kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “The Power Of Now” kutoka
kwa mwandishi Eckhart Tolle.
Mwandishi
ametumia zaidi ya miaka kumi akitafuta ukweli wa yeye ni nani na kwanini yupo
duniani humu. Katika kipindi hiki mwandishi ameweza kufanya mahojiano na watu
wa kada mbalimbali kama vile wanasayansi, madaktari, wanasaikolojia,
wafanyabiashara na viongozi wa dini. Hii imemsaidia kugundua kuwa mpaka sasa
maana halisi ya ubinadamu ni kuchukua hatua kwa ajili ya maendeleo na
mabadiliko katika kila hatua ya maisha yake. Mabadiliko na maendeleo haya ndiyo
yanapelekea mabadiliko ya dunia na hatimaye tunaiona dunia jinsi ilivyo lakini
kumbe dunia na vilivyomo ni matokeo ya jinsi tulivyo.
Hivyo
kwa ujumla katika kutafuta ukweli wa wewe ni nani unahitaji kupata majibu ya
maswali mawili (a) Je sisi ni watu wa aina gani? na (b) Je dunia tuliyomo ina
asili gani?. Majibu yetu katika maswali haya ndio yanayopima kiwango na ubora wa
mahusiano yetu na familia, marafiki, waajiri au waajiriwa wetu au jamii nzima
kwa ujumla.
Katika
mabadiliko na maendeleo ya mwanadamu inafikia hatua ya kilele cha
mabadiliko/maendeleo na hapa ndipo mwanadamu anakuwa kwenye hatua ambayo
jitihada zake zimechanua matunda katika kila sekta ya maisha yake. Matunda haya
yanajumuisha ukuaji wa kiroho, upendo, uvumilivu, kijitambua kimwili, uwezo wa
kuchanua mambo, mawasiliano na uwezo wa hiari.
Karibu
tujifunze wote machache niliyojifunza kutoka kitabu hiki:
1. Kila
mwanadamu anaishi katika pande mbili ambazo ni upande wa yeye na upande wa
nafsi. Nafsi inapoendelezwa na kufikia kiwango cha kilele cha mabadiliko
inakuwa imefikia hatua ambayo mwanadamu anajitambua kuwa yeye ni nani na kwanini
yupo hapa duniani. Katika hatua hii mtu anakuwa anajua kusudi la maisha yake
hapa duniani na hivyo anakua amefanikiwa kiroho. Katika hatua hii pia binadamu
haendeshwi na matamanio ya mwili bali anaongozwa na roho katika kila anachofanya.
2. Mwanadamu
anapokuwa hajajua kusudi la maisha yake anakuwa ni sawa na ombaomba ambaye siku
zote anakalia boksi kuomba vicenti vya hela kumbe ndani ya hilo boksi kuna kila
kitu cha thamani. Kila mmoja ndani yake ana mbegu za kufanya mambo makubwa huku
akiongozwa na roho lakini kutokana na kwamba watu wengi hawatambui kusudi la
maisha yao wanaishia kufanya vitu vya kawaida kwa ajili ya kuridhisha tamaa za
mwili. Mwandishi anatushirikisha kuwa kama haujatambua kusudi la maisha yako
kwa maana ya kufikia kilele cha ukuaji wa kiroho wewe ni ombaomba ambaye unahitaji
kujitambua kuwa haupaswi kuwa ombaomba kwani ndani mwako kuna kila kitu cha
thamani.
3. Unapofikia
kilele cha ukuaji wa kiroho unakuwa katika hali ambayo hauna mateso wala
maangaiko ya duniani. Wale wanaofikia hatua hii wanakuwa katika muunganiko wa
kudumu na nguvu ya ajabu (supernatural power) ambayo ina nguvu na mamlaka
kuliko vitu vyote. Nguvu hiyo ya ajabu ndiyo wewe halisi na ndio mbegu ambayo
kila mmoja amepewa tangu enzi za kuumbwa kwake. Kinyume chake ni kwamba
unapokosa muunganiko huu unakuwa katika hali ya kufanya vitu bila ya kujitambua
wewe ni nani na kwanini uliumbwa na matokeo yake unaishia kufanya vitu
nusunusu.
4. Ili
kuishi katika wakati uliopo unahitahiji kujua nguvu ya hali ya kuwa (state of
being) au unaweza kusema nguvu ya Mungu. Kwa imani, kila mtu kwa imani yake
pasipokujali kama ana imani katika Mungu au miungu wote tunatambuwa kuwa kuna nguvu
ya ajabu kuliko vitu vyote na nguvu hii ndio inatuongoza kuelekea kwenye kilele
cha mafanikio. Ili uishi wakati uliopo ni lazima ufahamu kwa undani maana
halisi kwako kuwa nguvu hiyo ni ipi na inafanyaje kazi katika maisha yako ya
kila siku. Zaidi unatakiwa kutambua kuwa nguvu hii ya ajabu kwa asili ni ya milele
na milele zaidi ikilinganishwa na maisha ambayo yana mwanzo (kuzaliwa) na mwisho
(kufa). Hii ina maana kuwa ukuaji wa kiroho unaambatana na ufahamu nguvu wa hii
ya ajabu na kuishi nayo milele.
5. Ukuaji
wa kiroho unaambatana na ukombozi wa fikra. Kutofautisha vitu kwa fikra/akili
yako pasipo kuongozwa na roho kunasababisha uwepo wa kizuizi kati yako wewe na
nafsi yako, kati yako wewe na jamii inayokuzunguka, kati yako wewe na
asili/mazingira yanayokuzunguka au kati yako wewe na Mungu. Hii inapelekea
uishi katika maisha yanayojikita kwenye umimi badala ya kutambua kuwa sisi sote
ni sawa kwa kuwa tumeunganishwa na roho mmoja. Maisha haya ya umimi yanapelekea
tunashindwa kuufahamu ukweli kwa kuwa kila tunachokifanya tunafanya kwa
kuongozwa na fikra/akili zetu.
6. Fikra
zinaweza kukuangamiza au kuwa nyenzo muhimu ya kukuongoza kufanya makubwa. Unahitaji
kuzitawala fikra/akili zako badala kukubali zenye zikutawale. Ugonjwa mkubwa
ambao umewamaliza watu wengi kuliko ugonjwa wa aina yoyote ile ni ugonjwa wa
kukubali kutumiwa na fikra zako. Watu wengi wanaendeshwa na fikra zao kutenda
mambo ya ovyo badala kutumia muda mwingi kuwekeza kwenye vitu muhimu vya
kufikiria ili hatimaye fikra hizo zitoe matokeo chanya katika kila
wanachofanya. Hii ni kutokana na ukweli kwamba fikra/akili ni chombo cha juu
katika kufanikisha maendeleo na ustarabu wa mwanadamu japo chombo hicho
kisipotumiwa vyema matokeo yake anguko kwa muhusika.
7. Kama
hauwezi kupumzisha kichwa kwa muda ili kisiendelee na kufikri basi wewe bado
unatumiwa na fikra. Hii ina maana kuwa umekuwa ukiishi katika fikra za
kutawaliwa na matukio ya nyuma na uwoga wa maisha ya baadae badala ya kuishi
katika wakati uliopo. Ili uzitawale fikra ni lazima utambue kuwa kuna ufahamu
wa juu zaidi ya fikra ambao unaweza kuutumia kutawala kila aina fikra zinazoingia
kichwani mwako. Huu ndio ukombozi wa kweli wa fikra ambao ndio ukuaji wa kiroho
halisi. Hapa unahitaji kuisikiliza sauti yako ya ndani. Naamini kabla ya
kufanya tukio lolote hasa kwa matukio mabaya kila mtu huwa kuna sauti
inamuuliza maswali juu ya tukio husika – hii ndiyo sauti ambayo unatakiwa kuisikiliza
yale inayokuelekeza. Pindi utapofanikiwa kutawala fikra za kichwa chako daima
utakuwa na amani ya ndani na hii ndio amani halisi ambayo kila mtu anatakiwa
kuwa nayo – kwa kifupi nikwamba amani hii inakufanya husiwe kwenye mabishano
kati yako wewe na nafsi yako.
8. Njia
nzuri ya kutawala fikra/akili zako ni kufanya tajuhudi. Katika zoezi hili
utafanikiwa kupumzisha kichwa chako kutoka kwenye zoezi la kufikiri hivyo
kutengeneza nafasi ya wazi katika mfumo wa fikra au tunaweza sema muda wa
mapuziko. Katika muda huu utajisikia amani rohoni na ni zoezi ambalo ukilifanya
mara kwa mara litakupa muunganiko halisi kati yako na nafsi yako na kati yako
na nguvu ya ajabu (roho). Zoezi hili linaweza kuwa gumu kwako mwanzoni lakini
kadri unavyolifanya mara kwa mara ndivyo utalimudu na hatimaye kulifurahia. Hili
ni zoezi ambalo unaweza kufanya katika matendo ya kila siku kwa kuhakikisha
kuwa akili yako yote inakuwepo kwenye tukio husika. Mfano, kama unatembea
hakikisha akili yako yote ipo kwenye kila hatua unayopiga hii ni pamoja na
kudhibiti namna unavyopumua ili kila hatua yako iwe na muunganiko wa pumzi
unayovuta na kutoa.
9. Mfumo
wa fikra/mawazo ndio zawadi pekee ambayo inamtofautisha mwanadamu kutoka kwenye
viumbe wengine bila ya mfumo huu mwandamu angekuwa sawa na wanyama wengine. Fikra/mawazo
ni nyenzo ambayo kila mwanadamu anahitaji kuiboresha ili kusudi kila wakati
aweze kudhibiti mazingira yake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha fikra zote
zainatawaliwa na ufahamu wake. Hii kutokana ukweli kwamba kuna tofauti kati ya
kufikiri na ufahamu; kufikiri ni chembe ndogo ya ufahamu. Hii ina maana kuwa
mawazo/fikra haziwezi kuwepo pasipokuwepo ufahamu. Kwa maana hii hiyo kama
hauwezi kudhibiti fikra zako wewe ni sawa na wanyama wengine.
10.
Tofauti kati ya fikra na akili ni
kwamba akili ina muunganiko wa hisia za mwili ndani yake wakati fikra zenyewe hazina
muunganiko huo. Kwa maana hii hisia zinaanza pale akili na mwili vinapoungana. Ndio
maana utakuta kuwa hisia zinaambatana na msisimko/mihemko ya mwili. Hivyo, hisia
ni mwitikio wa mwili kwa akili ya mhusika. Kwa maana hii, kama unataka
kukabiliana na mihemuko/msisimko au hisia za mwili wako unahitaji kwanza
kukabiliana na akili yako. Mara nyingi watu wanatawaliwa na hisia kwa vile
wanaruhusu nguvu ya hisia itawale akili yao. Hii inatokea kwa vile wakati huo
wa mabishano kati ya mwili na fikra mhusika anashindwa kuishi wakati uliopo na
matokeo yake anatawaliwa na hisia. Kwa ujumla kutawaliwa na hisia ni matokeo ya
kushindwa kujitambua wewe ni nani katika mantiki zaidi ya jina na umbile lako
kwa maana ya kushindwa kujitambua wewe ni nani katika macho ya kiroho.
11. Upendo, furaha na amani ni zaidi ya hisia
kwani vyote kwa pamoja vinaunda utatu ambo unamuunganiko na nguvu ya ajabu
(nguvu ya roho). Kwa maana hii kama una muunganiko na nguvu ya hii moja kwa
moja utaishi maisha yenye amani, upendo na furaha muda wote. Na hapa unatakiwa
kutofautisha furaha na raha – raha inakuwa ni ya muda mfupi na mara nyingi ni
matokeo kutoka nje kwa maana ya kwamba inaletwa na uwepo wa vitu flani. Hivyo,
ni kawaida vitu vinavyokupa raha leo hii kesho vitakusababishia huzuni na
maumivu. Lakini furaha ni ya kudumu na chimbuko lake linaanzia ndani mwako.
12. Upendo ni chimbuko la ndani tofauti na
matamanio ya muda mfupi. Kama tulivyoona kuwa raha inakuwa ya muda mfupi ndivyo
pia matamanio yalivyo. Watu wengi wanaishi katika ulimwengu wa matamanio
wakidhani kuwa ni ulimwengu wa upendo. Ndio maana katika jamii tunashuhudia mafarakano
ya mara kwa mara kwa kuwa wengi wanaongozwa na matamanio na matokeo yake
matamanio hayo yanageuka kuwa chuki za kudumu. Jambo muhimu la kujifunza hapa
ni kwamba kama unaishi katika upendo wa kutoka ndani mwako kamwe upendo huo
hauwezi kugeuka kuwa chuki kwani upendo wa kweli unaongozwa na roho na hauna
mabadiliko bali ni wa kudumu.
13. Amani kwa binadamu ni jambo ambalo ni
ndoto za alinacha kama mwanadamu ana muunganiko na Mungu. Mwandishi anatushirikisha
kuwa mwanadamu anapokuwa katika muunganiko na Nguvu ya ajabu ni muda wote
atakuwa mwenye amani katika matendo yake. Hata hivyo watu wengi wanaishi katika
ulimwengu wa giza na hivyo kamwe hawawezi kuwa na amani maishani mwao. Katika maisha
ya namna hii muda mwingi mwanadamu anajutia matendo yake jambo linalomuweka
mbali na Baraka za Muumba na hivyo kuendelea kuishi katika maumivu. Maumivu haya
yanagawanyika katika sehemu mbili ambazo ni maumivu unayotengeneza kwa wakati
uliopo na maumivu yanayotokana na matukio katika historia yako.
14. Sehemu kubwa ya maumivu ya mwanadamu
yanatokana na yeye kushindwa kutawala mawazo/fikra zake. Maumivu haya ni
matokeo ya kutawaliwa na nguvu za kimwili (hisia) badala ya nguvu za Roho kwa
maana ya kutawaliwa na maovu kuliko mema. Kiwango cha maumivu haya kati ya
binadamu mmoja na mwingine kinategemeana na utofauti wa ukuaji wa kiroho kwa
maana ya uwezo wa kuishi maisha ya wakati uliopo. Tunahiji kuishi ukamilifu wa wakati
uliopo huku tukikumbatia uwepo wa nguvu ya Roho kuliko kuishi maisha yenye
maumivu ya matukio yaliyopita na uoga wa maisha ya baadae.
15. Unaweza kuishi katika hisia za maumivu ya
mwili kwa muda mfupi au mrefu kwa kutegemea jinsi ambavyo unabeba hisia hizo. Maumivu
ya mwili kwa mtu mmoja yanaweza yasimuhumize kwa takribani asilimia 90 wakati
mwingine maumivu hayo yatamuumiza kwa asilimia mia. Hii inatoa picha kuwa
kinachotofautisha maumivu ya mwili ni kutokana na wahusika wanavyoishi maisha
ya ukamilifu wa nyakati. Kama unaongozwa na Roho daima maumivu ya mwili
hayatakusumbua sana ikilinganishwa na yule ambaye anaongozwa na fikra zake
mwenyewe. Katika ulimwengu wa kiroho maumivu yanachukuliwa kuwepo kwako ajili
ya kutumiwa kufikia kusudi la maisha yako ili kupitia shuhuda zako watu wengi
wapate kujitambua wao ni nani na kwa nini wapo duniani humu.
16. Chanzo kikubwa cha hofu ni kutokuwa na
hakika na matukio yajayo katika maisha yako. Hofu hii mara nyingi inakuja
katika hali tofauti kulingana na aina ya tukio tarajiwa, mfano hofu inawezakusababishwa
na kutokuridhishwa, wasiwasi, woga, mvutano
na kadhalika. Kwa maana hii watu wengi wanatawaliwa na hofu kwa vile wanaishi
maisha ya baadae katika nyakati za sasa hivi. Hivyo ni sahihi kusema kuwa hofu
mara nyingi inakuwa katika makundi kama; hofu ya kupoteza, hofu ya kushindwa,
hofu ya kuumizwa, hofu ya kuangamizwa, hofu ya kusalitiwa, hofu ya kifo na
kadhalika. Mara nyingi mtu anayeishi kwa kutawaliwa na fikra muda wote huwa
anaona kifo kipo karibu yake na matokeo yake hofu hii ya kifo inaharibu kila
sekta ya maisha ya mhusika.
17. Maisha ya watu wengi yanatawaliwa na
umimi ambayo maisha yanakuwa ni ya kuridhisha hisia zako au katika saikolojia
msamiati sahihi wa kutumia ni maisha ya kuridhisha “EGO”. Kwa maana hii
unapoishi kwa ajili ya kuridhisha ego unaishi maisha ya kuridhisha mwili na
matokeo yake muda wote maisha hayo huwa yametawaliwa na matendo ya giza. Maisha
ya namna hii huwa yanaleta faraja, raha au amani ya muda mfupi na mara zote huwa
ni maisha yenye kufikiria kuwa nikipata hiki nita…., mfano nitakuwa na furaha
pindi nikiwa na fedha nyingi. Lakini mara zote hata pale unapopata kile
ulichohitaji unajikuwa bado kuna ombwe kubwa la kujazwa ili upate furaha ya
kudumu.
18. Kama unahitaji kuachana na maisha
yaliyotawaliwa na ego (maisha yenye kuhitaji kuridhisha matamanio ya mwili)
kwanza kabisa unahitaji kuchambua au kufanya tathimini ya kina kwa ajili ya
kujua chanzo cha matamanio hayo. Baada ya kutambua chanzo maisha yasiyoongozwa
na ufahamu wako unahitaji kuishi maisha mapya ambayo yanaongozwa na ufahamu
wako lakini pia kuishi maisha yaliyojengwa kwenye misingi ya wakati uliopo.
19. Kila kitu kinatokana na nguvu ya wakati
uliopo au wakati wa sasa. Mambo yanayooneka ni historia yalikuwa ni matukio ya
nyakati zilizokuwepo wakati huo na mambo yanaotarajiwa kuwepo siku zijazo yana
nyakati zake za sasa wakati ukifika. Katika mawazo ya kibanadamu sio rahisi
kuelea saikolojia hii, lakini unachohitaji kufahamu hapa ni kwamba wakati wa
sasa umeundwa na wakati uliopita na wakati wa kesho unaundwa na wakati wa sasa.
Lakini vyote hivi kwa pamoja unahitaji kuvihishi katika maisha yanayoongozwa na
roho.
20. Maisha yanayotawaliwa na yaliyopita na
yale yanayokuja kwa pamoja na yanaondoa uwepo wa nguvu ya Roho katika maisha ya
mhusika. Katika kuishi maisha ya Usasa au nyakati zilizopo mara nyingi
unahitaji kujiuliza maswali kama Ni kipi kimekosekana kwa sasa? au Kama sio
sasa ni lini? Maswali haya kwa pamoja yanahitaji majibu yanayotolewa kwa kuongozwa
na maono ya kiroho kuliko maono ya kibanadamu.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Hakika nilichokushirikisha
hapa ni sawa na robo ya kile ambacho mwandishi anatushirikisha kwa ajili ya
ukuaji wa kiroho. Kwa maana hii nakushauri usome nakala ya kitabu hiki kwa
ajili ya kujifunza mengi zaidi. Kupata nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com