Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa
ajili ya kuyaboresha maisha yako. Karibu katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI
kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya kumi na
tano katika kipindi cha mwaka 2017 naenedelea kukushirikisha uchambuzi wa
vitabu nikiwa na lengo kubwa la kukupa maarifa kwa ajili ya kubadilisha kila
sekta ya maisha yako.
Kama mpaka sasa haujafanikiwa kujifunza
kitu chochote katika makala hizi za uchambuzi wa vitabu nakushauri husiendelee
kupoteza muda wako na badala yake ufanye mambo ambayo umeyazoea.
Kujiunga na mtandao wa fikra za
kitajiri BONYEZA HAPA na
ujaze fomu ili uendelee kunufaika na makala za mtandao wa fikra za kitajiri.
Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala za mtandao wa fikra za kitajiri moja
kwa moja kwenye barua pepe yako.
Kitabu
cha wiki hii ni “Brain Rules” kutoka kwa mwandishi John Medina. Mwandishi
John Medina ni mtaalamu mbobevu wa elimu ya viumbe (biologist) na amejikita
sana kwenye sehemu ya mfumo wa ubongo. Katika kitabu hiki mwandishi
anatushirikisha kanuni kumi na mbili ambazo kila mtu anaweza kutumia kwa ajili
ya kuboresha maisha yake katika sehemu ya kazi/biashara, mahusiano au sehemu ya
masomo.
Kwa
ujumla mwandishi anatushirikisha kuwa mfumo wa ubongo ni sehemu ya hali ya juu
katika viuongo vya mwanadamu kiasi kwamba sehemu ndiyo inapima ufanisi wa kila
mtu. Ufanisi huu unatofautiana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kulingana namna
ambavyo kila mmoja amezoesha akili yake katika matukio ya maisha ya kila siku. Kwa
maana hii mfumo wa ubongo ni teknolojia ya mawasiliano yenye ubora wa hali ya
juu kuliko technolojia yoyote ile katika ulimwengu huu.
Hata
hivyo, watu wengi wameshindwa kutumia teknolojia hii ya hali ya juu kuboresha
maisha yao kutokana na ukweli kwamba watu wengi hawafahamu namna ambavyo mfumo
wa ubongo unavyofanya kazi. Mbaya zaidi ni kwamba katika jamii mfumo wa elimu
ya msingi au sekondari hauwafundishi watu namna ambavyo wanaweza kutumia mfumo
wa ubongo kwa ajili ya kupata mafanikio mwakubwa sana.
Karibu
tujifunze wote machache niliyojifunza kutoka kwenye sheria kumi na mbili za
ubongo ambazo mwandishi anatushirikisha katika kitabu kitabu hiki:
1. Kuna
uhusiano mkubwa kati ya mazoezi na utayari wa akili kufanya kazi. Mwandishi
anatushirikisha kuwa mwili wa mwanadamu umeumbwa kiasi kwamba unaweza kutembea
maili 12 kwa siku. Katika mzunguko huo mwili unaweza kufanya kazi mbalimbali
ambazo zinatofautisha dunia ya kizazi kimoja hadi kingine. Kwa ujumla unaweza fupisha
maana hii kwa kutumia maneno haya “wakakamavu ndo wanaishi – survivor of the
fittest”. Ukweli huu unadhihirishwa na maendeleo ya mwanadamu toka enzi za
kutegemea asili (matunda na mizizi) mpaka kuwa mzalisha na mboreshaji wa
mazingira. Hii yote ni kazi ya ubongo ambayo imefanikisha uwepo wa vifaa vya
kurahisisha utendaji kazi na mawasiliano.
2. Mazoezi
ni njia mojawapo ya kumwezesha mtu kuishi maisha marefu. Mwili uliojengeka kwa
mazoezi ni nadra sana kushambuliwa na magonjwa nyemerezi, hivyo, kama unahitaji
kuishi maisha marefu huna budi kuishi maisha ya mazoezi kwa ajili ya uimara wa
mwili pamoja na akili. Jibu la ukweli huu ni rahisi kwa kadri unavyofanya
mazoezi ndivyo unaifanya misuli iwe imara na hivyo kupelekea kupunguza hatari
ya magonjwa ya moyo. Pia, utafiti unaonesha kuwa watu ambao wameishi maisha ya
mazoezi wana faida ya kuwa na utimamu wa akili kwa muda mrefu na hivyo ni
rahisi kwao kufikiria na kuchanganua mambo haraka. Mazoezi yanapunguza hatari
ya kupatwa na magonjwa kwa kiwango cha zaidi ya 60%.
3. Mazoezi
yanasaidia kuimarisha afya ya watoto. Mwandishi anatushirikisha kuwa watoto
ambao wanajihusisha na mazoezi wana afya bora ikilinganishwa na watoto
wanaofungiwa ndani muda wote. Kadri watoto wanavyokuwa na afya imara ndivyo
inakuwa rahisi kufanya vyema katika masomo yao. Hii ni kutokana na ukweli
kwamba watoto ambao ni wakakamavu mara nyingi huwa na afya imara, wasikivu na
wanaojiamini katika yale wanayofanya.
4. Ubongo ni asilimia 2 tu ya sehemu yote ya
mwili wa binadamu lakini sehemu hii inatumia karibia asilimia 20 ya nishati
yote inayohitajika na mwili. Njia pekee ya kufanikisha seli za mwili ziendelee
kufanya kazi yake zikiwemo seli za ubongo ni mzunguko wa damu kuendelea
kusambaa sehemu zote za mwili. Kadri unavyofanya mazoezi unawezesha damu iweze
kuzunguka haraka na kwa kasi na hivyo kufanikisha usambazaji wa hewa ya
oksijeni pamoja na kuondoa sumu kwa njia ya jasho.
5. Kuna
njia mbili za kukabiliana na changamoto za mazingira yetu. Njia ya kwanza ni
kuwa na nguvu zaidi na njia ya pili ni kuwa na uwelevu/akili zaidi. Njia ya
pili ni nzuri zaidi kwa vile inatuwezesha kutawala ulimwengu huu kwa kutumia
nguvu kidogo huku tukitumia ubongo wetu. Na hii ndiyo njia pekee
inayotutofautisha sisi pamoja na viumbe wenye ukaribu na sisi kama vile Gorila.
Uwezo wa kuchanganua mambo kwa kutumia picha ya vitu husika akilini mwetu ni
nyenzo muhimu ambayo imeendelea kutofautisha kizazi cha mwanadamu na viumbe
wengine na ni kupitia uwezo huu mwanadamu ameendeleza uumbaji wa kila aina kwa
ajili ya kuboresha utendaji kazi katika mazingira yanayomzunguka.
6. Ubongo
ni kiumbe hai na hivyo unahitaji haki zote za kuwa hai ili uendelee kuishi. Haki
kubwa kabisa ya kuwa hai si nyingine zaidi ya kuhitaji kuboreshwa kutoka chini
kwenda juu kithamani (evolution) kupitia kwenye sheria ya asili ya kuchagua. Kiumbe yeyote anayeishi ni lazima apate
chakula baada ya kula ili kiumbe huyo aendelee kuwepo siku zijazo ni lazima
pawepo kuzaliana kwa ajili ya kupitisha tabia moja kwenda kizazi kingine. Hivi ndivyo
ubongo wa mwanadamu umekuwa ukiendelea kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Hapa utagundua
kuwa ubongo unaboreshwa kutoka kwenye ubongo wa kutegemea asili mpaka kufikia
kwenye ubongo wa kutaka kuishi mwezini.
7. Kutokana
na mfumo wa ubongo kusukwa tofauti ndiko kunapelekea watu wawe na vipaji
tofauti. Ndiyo maana utakuta kuna mchezaji kama Christiano Ronaldo ambaye
amefanikiwa katika soka lakini ukimpeleka katika mpira wa kikapu hawezi kufikia
mafanikio ya Michael Jordan. Mwandishi anatushirikisha kuwa huu ni ukweli ambao
unatofautisha kazi za uumbaji wa vitu kati mwanadamu mmoja na mwingine. Habari njema
ni kwamba ubongo unaweza mfumo wa ubongo unaweza kusukwa upya kutokana na
mazoea ya kazi unayofanya. Ni kutokana na ukweli huu mwanadamu anahimarika kila
siku kutokana na kazi ambayo amezoea kuifanya mara kwa mara kwa vile ubongo
unazoea kile ambacho kinafanyika mara kwa mara.
8. Seli
za ubongo ndani mwake zina vinyuzi vidogo ambavyo uitwa neurons. Vinyuzi hivi vinafanya kazi sawa na nyaya za umeme ambapo
katika mfumo wa ubongo vinasaidia kusafirisha taarifa moja kutoka kwenye ubongo
kwenda kwenye viungo vingine vya mwili. Kabla ya taarifa kutumwa kwenye viungo
vya mwili ni lazima kwanza ubongo uzitafsri na ndipo unaagiza sehemu ya mwili
husika kuchukua hatua. Ubongo unafanya kazi kiasi ambacho unaweza kufanyia kazi
taarifa moja na kuacha nyingine kwa kutegemea matokeo tarajiwa kwa taarifa
husika. Hapa unatakiwa kujenga utamaduni wa kuufundisha ubongo wako kufanyia
kazi taarifa zenye matokeo chanya tu.
9. Ubongo
ni sawa na msuli kwa maana ya kwamba kadri unavyotumiwa mara kwa mara ndivyo
unaimarika zaidi. Ni mara nyingi tumeona namna ambavyo watu wenye mazoezi
wanavyokuwa na misuli iliyotuna zaidi ikilinganishwa na watu wengine. Na mfumo
wa utendaji kazi wa ubongo ndivyo ulivyo kwa maana ya kwamba kadri unavyotumiwa
zaidi ndivyo unaimarika zaidi kwa kuongeza uwezo wa kufikri na kuchanganua
mambo kwa haraka. Hivyo ni lazima uwe tayari kuufundisha ubongo wako kufikria
njee ya boksi.
10.
Kadri ubongo unavyotumia muda mwingi
kwenye kichochezi au chanzo cha taarifa ndivyo taarifa husika itatafsiriwa na
kufanyiwa kazi na hatimaye kujidhihirisha kwenye ulimwengu wa nje. Hii ni sifa
inayopelekea ufanisi wa ubongo kufanikisha mambo mapya kupitia kujifunza mara
kwa mara. Kwa sifa hii kila mtu anaweza kuwa ufanisi katika kila sekta ya
maisha yake kwa kutumia muda mwingi kufikiria na kujifunza yale ambayo yana umuhimu
katika kufikia mafanikio anayokusudia.
11.
Mara nyingi vipaumbele vyetu vinatokana
na kumbukumbu, hobi pamoja na ufahamu wetu. Tunatumia historia kuhisi namna
ambavyo tunaweza kufanikisha matokeo yale tunayowaza. Kwa ufupi ni kwamba kila
aina ya mazingira tuliyozoea yana mchango katika matukio ya maisha yetu ya kila
siku. Pia, tamaduni na makuzi tuliyokulia yana nafasi kubwa ya kutambulisha jinsi
tulivyo katika kudhibiti hisia zetu.
12. Ubongo unaweza kufanyia kazi moja kwa
ufasaha na kutoa jibu moja kati ya zuri au baya na si vyote kwa pamoja. Hapa mwandishi
anatufundisha kuwa neurons za ubongo zinafanya kazi katika mfumo unaotoa matokeo
ya upande mmoja kwa wakati husika pasipo kujali kama wema au ubaya wa matokeo
husika. Kwa maana hii, tunafundishwa kuwa hatuwezi kuwa wenye furaha na huzuni
kwa wakati mmoja, hatuwezi kukimbia na kutembea kwa
wakati mmoja au hatuwezi kuwa hofu na kujiamini kwa wakati mmoja. Ni lazima
tukio moja lipewe nafasi kwa wakati husika badala ya tukio kinzani.
13. Hisia zinawezesha ubongo kujifunza. Hapa
mwandishi anatufundisha kuwa hisia ni chanzo cha ubongo kujifunza na hivyo
hisia zetu ndo zinaamua ni wapi akili zetu zimejikita zaidi katika maisha yetu
ya kila siku.
14. Ubongo una sehemu maalum kwa ajili ya
kutunza kumbukumbu ya matukio. Mwandishi anatufundisha kuwa yale yanayopewa
kipaumbele kwa kurudiwa mara kwa mara katika maisha ya muhusika ni rahisi sana
kukumbukwa na hatimaye kuwa desturi ya maisha ya kila siku. Kwa maana hii ni
wazi kuwa imani yetu katika vitu au matukio kwenye ulimwengu huu ni matokeo ya
kujifunza sisi wenyewe au kufundishwa kutoka kwa watu wengine wanaotuzunguka. Hii
ni kutokana na ukweli kwamba tulikuja ulimwenguni humu tukiwa watupu kwa maana
ya ubongo wetu ulikuwa wazi japo kadri umri ulivyosogea ndivyo tulijifunza au
kufundishwa zaidi juu ya mema au mabaya ya dunia hii.
15. Kumbukumbu ni nyenzo muhimu ya
kuboresha maisha ya mwanadamu. Nyenzo hii inashikilia mahusiano, maarifa na
uchumi wa kila mwanadamu kutokana na ukweli kwamba kumbukumbu inamwezesha
mwanadamu hasipotezee muda wa kurudia kujifunza kila siku matukio ambayo yamekuwepo
toka mwanadamu aumbwe. Hapa mwandishi anatukumbusha kuwa pasipo kuwa na kumbukumbu
imara ni lazima muhusika ajikute kwenye hali ya kurudia makosa yale yale kila
mara.
16. Taarifa nyingi zinazoingia kwenye
ubongo sehemu kubwa hazifanyiwa kazi na hivyo zinasahaulika ndani ya muda mfupi
na zile ambazo zinapewa kipaumbele zina nafasi ya kukumbukwa. Njia pekee ya
kuepuka kupoteza taarifa muhimu ni kujenga utamaduni wa kutembea na kijitabu
kidogo kwa ajili ya kuhifadhi taarifa muhimu ili ziendelee kupewa kipaumbele
zaidi. Hapa mwandishi anatushirikisha kuwa hauwezi kurudia kitu ambacho hauna
kumbukumbu zake hivyo ni muhimu kuimarisha mfumo wa kumbukumbu.
17. Usingizi ni sehemu ya kupumzisha na
ubongo kwa ajili ya kutoa nafasi ya kufikiria vyema zaidi. Pale tunapolala sio
kwamba ubongo nao unalala bali unapunguziwa majukumu kwenye baadhi ya viungo
vya mwili. Tendo hili linatoa nafasi kwa ubongo kufikiri vyema na hii inatoa
nafasi kwa ubongo kutunza nguvu kwa ajili ya kazi ya baadae. Katika muda huu wa
mapumziko neurons zinapata nafasi ya kurudia matukio ya mkanda wa matukio
yote kwa siku husika. Hivyo ni wazi kuwa unapokosa muda wa kutosha kwa ajili ya
usingizi ndivyo na ufanisi wako wa kufikiri na kutenda kazi unavyokuwa duni.
18. Ubongo wenye msongo wa mawazo hauwezi
kujifunza kwa urahisi. Ufanisi katika masomo au utendaji kazi unatofautiana
kati ya mtu mwenye msongo wa mawazo na yule ambaye yuko huru. Pia, msongo wa
mawazo unaweza pelekea matatizo ya moyo kushindwa kufanya kazi yake kwa
ufasaha.
19. Watu wengi katika jamii ya sasa
wanakosa muda wa kutoa malezi bora kwa watoto wao kwa vile wanabanwa na
majukumu ya kazi zao. Kwa ujumla watoto wanajikuta katika hali ya msongo wa
mawazo kwa vile watu wa kuwapa ushauri hawako karibu nao muda mwingi. Kadri msongo
wa mawazo unavyozidi kwa watoto hawa matokeo yake ni kwamba ubongo wao unajazwa
na hofu, vitu hasi, hasira, visasi na hatimaye ubongo wa namna hii una ubunifu
wa chini sana.
20. Mwanafunzi wa kwanza kabisa ambaye
anatakiwa kupewa nafasi ya kujifunza ni mzazi. Mwandishi anatushirikisha kuwa
elimu ya sasa inamlenga mtoto wa kuanzia miaka mitano au sita. Katika umri kama
huu mtoto anapofika shuleni anakutana na mwalimu ambaye ni mpya kabisa katika
mazoea ya mtoto, hali hii inaweza kumfanya mtoto hasiwe na mafanikio kama hana
msingi mzuri wa malezi kutoka kwa wazazi. Hivyo, kama mzazi ni lazima ujifunze
mara kwa mara namna ambavyo utamjenga mwanao katika maisha ya kujiamini katika
kila hali inayomzunguka.
21. Tumia milango yako yote ya fahamu
katika kila tukio linalokukabili. Mfano, tumia masikio kusikia, macho kuona, ngozi
kuhisi, pua kunusa na ikibidi ulimi kuonja pindi unapochanganua hali ya tukio. Milango
hii ya fahamu kila mmoja kwa mfumo wake wa neurons unatuma taarifa kwenye
ubongo na hatimaye ubongo kwa haraka unatafsiri tukio husika kwa pamoja. Kwa vile
ubongo unatafsiri taarifa kwa kutegemea uzoefu wa muhusika hivyo taarifa moja
inaweza kuwa tafsiri mbili tofauti kwa watu wawili. Hapa tunajifunza kuwa njia
bora ya kujifunza kwa urahisi ni kuhakikisha tunahusisha milango yetu yote ya
fahamu kwa ajili kumbukumbu zaidi.
22. Ni rahisi sana kujifunza kwa kutumia
picha kuliko maneno. Ubongo unajifunza mengi kutokana na mchoro au picha kuliko
ilivyo kwenye maneno. Mwandishi anatushirikisha kuwa hatuna budi ya kutengeneza
mchoro au picha akilini mwetu juu ya yale tunayowaza au kutamani katika maisha
yetu. Picha inaleta uhalisia wa kitu au tukio katika ulimwengu wa nje. Kwa maana
hii mfumo wa fahamu wa kuona ni mfumo mama ambao unaweza kuutumia kuamsha
mifumo ya fahamu mingine.
23. Binadamu ameumbwa katika hali ambayo
inampendelea kuitawala dunia hii. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mfumo wa
ubongo unamwezesha kila mmoja kujifunza vitu vipya na kutumia vitu hivi katika
maisha yake ya kila siku. Kwa maana hii tunaweza kujifunza vitu vipya au
kuboresha vitu vipya kwa kutumia neurons za ubongo.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi niliyojifunza kutoka kwenye kitabu hiki. Kupata
nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com