Mambo Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha The Seven Principles For Making Marriage Work (Kanuni Saba za Kuijenga Ndoa Imara)

Habari ya leo rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya kumi na sita katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi wa vitabu. Lengo kubwa la kufanya hivyo ni kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako kuyatumia kubadilisha kila sekta ya maisha yako.

Uamzi wa kubadilisha maisha yako upo mikononi mwako na hivyo kama mpaka sasa haujafanikiwa kujifunza kitu chochote katika makala hizi za uchambuzi wa vitabu nakushauri husiendelee kupoteza muda wako na badala yake ufanye mambo ambayo umeyazoea.

Kujiunga na mtandao wa fikra za kitajiri BONYEZA HAPA na ujaze fomu ili uendelee kunufaika na makala za mtandao wa fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa na mtandao huu moja kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.

Kitabu cha wiki hii ni The Seven Principles For Making Marriage Workkutoka kwa waandishi John M. Gottman akishirikiana na Nan Silver. John M. Gottmann ni mwanasaikolojia na mtafiti wa masuala ya familia na ndoa. Wawili hawa kwa pamoja wameshirikiana kuandika vitabu mbalimbali kwa ajili ya kuboresha maisha ya ndoa na familia kwa ujumla.

Katika kitabu hiki waandishi hawa wanatushirikisha kanuni saba ambazo wanandoa kwa pamoja wanaweza kuzitumia kwa ajili ya kuboresha na kuendeleza maisha ya ndoa ambayo imejengwa kwenye msingi wa furaha.  

Karibu tujifunze wote machache niliyojifunza kutoka kitabu hiki:

1. Furaha katika maisha ya ndoa haitokani na pesa, akili nyingi au umiliki wa rasilimali za aina yoyote ile. Waandishi wa kitabu wanatushirikisha kuwa chanzo cha ndoa nyingi kuishi maisha yasiyo ya furaha ni wanandoa husika kuishi maisha ya fikra hasi pamoja na hisia mbaya zinazojengwa juu ya mwenza wake. Hivyo, ili ndoa iwe na maisha yenye furaha ni lazima kwanza wanandoa waheshimiane, wanyenyekeane, waelewane na kusikilizana katika maisha yao ya kila siku. Kwa maana hii msingi mkubwa wa ndoa yenye mafanikio ni kila mmoja kuwa na hisia juu ya mweza wake na wala sio pesa au umiliki wa rasilimali.

2. Ndoa ni sehemu ya kuongeza siku za kuishi. Waandishi wa kitabu hiki wanatushirikisha kuwa utafiti unaonyesha kuwa wanandoa ambao wameishi pamoja kwa muda wa maisha yao wanaishi kati ya miaka minne hadi nane ikilinganishwa na wale ambao wametalikiana. Hii ni kutokana na ukweli kwamba ndoa zenye msongo wa mawazo na kila aina ya misukosuko ni chanzo cha miili ya wanandoa kuwa na upungufu wa kinga za mwili dhidi ya maradhi mbalimbali.

3. Mawasiliano kati wenza au familia ni chanzo cha kutatua migogoro na maisha yenye furaha ndani ya familia. Mawasiliano ni chanzo kikubwa cha mapenzi ya dhati kati ya mke/mme na mwenza wake na wanandoa ambao hawana mawasiliano ya mara kwa mara si rahisi kudumu kwa muda mrefu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mawasiliano ni chanzo cha kusikilizana na kufahamu mahitaji ya mwenza wako ili kuboresha maisha ya ndoa yako.

4. Urafiki kati ya wanandoa unasaidia kukuza ndoa imara na yenye furaha. Waandishi wanatushirikisha kuwa ni muhimu wenza katika ndoa kuishi maisha ya urafiki na katika urafiki huu wenza hawa wanatakiwa kutambua mapungufu ya kila mmoja. Pia, kila mmoja anatakiwa kufahamu vipaumbele vya mwenzake na kwa pamoja kila mmoja atumie jitihada za kumridhisha mwenza wake ili atomize vipaumbele vyake. Hivyo, ni muhimu wanandoa wakaishi maisha ya urafiki yenye kila aina ya vichocheo vya mapenzi.

5. Chanzo cha ndoa nyingi kuanguka ni kukosa unyenyekevu kati ya wenza. Waandishi wanatushirikisha kuwa dhumuni kubwa la maisha ya ndoa ni wawili (mme na mke) kusaidiana kwa ajili ya kila mmoja kufanikisha ndoto za mwenza wake. Katika maisha ya namna hii wawili hawa wanatakiwa waishi maisha yenye kusudi moja kwa ajili ya kufanikisha kukuza familia yao kwa misingi bora. Endapo wanandoa watakosa misingi hii ni wazi kuwa ndoa yao itakuwa kwenye malumbano ya mara kwa mara ambayo yatapelekea ndoa yao kupoteza mwelekeo.

6. Tabia za kukosoa, vitendo vinavyoambatana na lugha ya mwili, kujiona wewe hauna kosa bali mwenye makosa ni mwenzi wako, kuongea kwa jazba, kuwa na kumbukumbuku za matukio mabaya kati yenu na malalamiko ya kila wakati ni sababu kuu kati ya nyingi zinazosababisha kuvunjika kwa ndoa nyingi. Waandishi wanatushirikisha kuwa ni vyema kila mmoja katika maisha ya ndoa atambue wajibu wake na pale inapotokea kuna kutoelewana ni lazima kila mmoja atambue ni wapi amekosea yeye kama yeye kabla ya kumlaumu mwenzake.

7. Kwa asili mwanaume ndo nguzo ya familia na utafiti unaonesha kuwa ukweli huu unajidhihirisha kwa zaidi ya asilimia 85 za ndoa katika jamii nyingi. Hii inaonyesha wazi kuwa mwanaume na mwanamke ni viumbe vyenye maumbile tofauti. Mfano, wanawake wameumbwa kwa ajili ya kufanya kazi ambazo zinawezesha kupumzika kwa muda mrefu hasa kwa mama anayenyonyesha ili kuruhusu homoni za maziwa ziwezeshe maziwa kuzalishwa kwa wingi. Kwa upande wa mwanaume yeye kimaumbile anaweza kufanya kazi kwa muda mrefu kwa kuzingatia maumbile ya misuli yake.

8. Katika maisha ya ndoa ni lazima kila mmoja amfahamu mwenza wake kwa undani zaidi. Hii ni kanuni ya kwanza ambayo waandishi wanatushirikisha kwa ajili ya kuboresha familia zetu. Hapa tunashirikishwa kuwa kama unataka kuboresha familia yako ni vyema kuhakikisha unafahamu mwenza wako anapendelea nini, mwenza wako anakabiliwa na tatizo lipi, hofu zake, matukio muhimu katika historia ya mwenza wako, anasongwa na mambo yapi kwa muda husika n.k. Baada ya kumfahamu mwenza wako ndani na nje unatakiwa kutumia vitu hivyo kuamsha vichocheo vya mapenzi kwa njia yoyote ile ikiwa ni pamoja na kuwa na muda wa utani na kufurahi. Mfano, unaweza kutumia nyimbo au filamu ambazo mwenza wako anapendelea na kuhakikisha unazitumia kwa ajili ya kuamsha hisia zake za mapenzi.

9. Wanandoa wanapopata mtoto inaweza kuwa mwanzo wa mafarakano wa familia husika. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mara baada ya kupata mtoto wanandoa wanakuwa na majukumu mapya ambayo mara nyingi yanapelekea mapenzi ya wawili hawa yaamie kwa mtoto. Njia pekee ya kuendelea kupendana na kila mmoja kutimiza majukumu yake kwa mwenza wake ni kuhakikisha wanandoa wanafahamiana kwa undani ili hata pale mabadiliko yanapojitokeza kila mmoja atafute namna ya kurudi kwenye msitari.

10. Rutubisha hisia na matamanio yenu ndani ya ndoa. Waandishi wanatushirikisha kuwa ni muhimu kwa wanandoa kuhakikisha kila siku hisia zao zinakuwa hai hii ni pamoja na kukumbuka historia za enzi za uchanga wa penzi lenu la dhati. Hata hivyo ni muhimu kila mwanandoa kuhakikisha kila siku anatafuta njia za kumchangamsha mwenza wake ili muda wote wawili hawa wawe kwenye furaha yenye chimbuko la kutoka rohoni.   

11. Mtazamo chanya juu ya mwenza wako na mahusiano yenu ni nyenzo muhimu ya kuepuka mambo mabaya ndani ya mahusiano. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mtazamo chanya juu ya mwenza wako ni tiba ya mafarakano ndani ya ndoa. Kadri unavyokuwa na mtazamo chanya juu ya familia na mwenza wako ndivyo kila kukicha mwenza wako unamuona mpya. Hii ni pamoja na kuhakikisha mnaishi maisha ya shukrani kwa kila tukio linalotokea kwenye maisha yenu.

12. Ndoa nyingi zimevunjika kutokana na kukosa muda wa wenza kuwa pamoja. Sehemu pekee ya kufahamu mahitaji ya mwenza wako ni kuwa na muda wa pamoja ambao mnaweza kuongea pamoja. Utafiti unaonyesha kuwa ndoa nyingi zimebomoka kwa vile wanandoa husika wamekosa vionjo vya penzi ambavyo awali vilifanya penzi lao liwe hai muda wote. Ili kuepuka mtego huu ni muhimu kwa wanandoa kutenga muda wa kusikilizana kwa ajili ya kukumbusha vitu muhimu katika maisha yao na hivyo kuhuisha akaunti ya penzi lao.

13. Ukaribu wa wanandoa sio tu unasaidia kuboresha uaminifu wa wanandoa bali pia ni chanzo cha kuamsha hisia za mapenzi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kadri wanandoa wanavyokuwa karibu muda mwingi ndivyo wanasaidiana majukumu ya kazi zao. Katika kusaidiana majukumu haya ndivyo kila mmoja anaonyesha thamani yake kwa mwenzi wake.

14. Kukua kwa teknolojia ya habari na mtandao kumepelekea wanandoa wengi kukosa utulivu wa akili pindi wanapokuwa pamoja. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wanandoa wengi wamemezwa na mitandao ya kijamii hivyo pindi wanapokuwa pamoja kila mmoja yupo bize na simu yake akiendelea na kuchati. Hali hii inaendelea kupoteza amani ndani ya ndoa nyingi kwa vile kila mmoja hana muda wa kumsikiliza mwenza wake. Ili kuepukana na hatari hii waandishi wanatushauri kuwa ni vyema kutenga muda wa kupitia mitandao ya kijamii, emails na ujumbe mfupi wa simu. Hakikisha muda ambao umeutenga kwa ajili ya mwenza wako au watoto wako hauna mwingiliano wa mambo mengine.

15. Mwanaume hasitumie madaraka yake kama nguzo ya familia kuhakikisha kuwa maamuzi ndani ya ndoa anafanya peke yake bali ushirikiano uwe msingi wa maamuzi ya wanandoa. Kanuni hii ni kwa ajili ya kuhakikisha kuwa maamuzi yanayofanywa yanamfurahisha kila mmoja ndani ya ndoa. Daima epuka maamuzi ambayo yanamfa mwenza wako hasijisikie vizuri juu utekelezaji wa maamuzi yako. Maamuzi endapo yanafanywa kwa kushirikiana yanapunguza migongano kwa wanandoa na hivyo kuboresha urafiki wa wenza hawa.

16. Migogoro ndani ya ndoa inagawanyika katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni ile migogoro ambayo inajitokeza mara kwa mara ndani ya wenza. Katika kundi hili wanandoa mara nyingi wanaishi ndani ya migogoro hii kipindi kirefu cha maisha yao. Mfano, katika ndoa ya Jane na Smith; Jane anataka tendo la ndoa lifanyike mara kwa mara wakati Smith yupo tayari hata mara moja kwa wiki. Pia, migogoro hii inahusisha majukumu ya kazi kwa wenza ambayo yanapelekea kila mmoja kuona kuna upungufu kwa mwenzake katika kutimiza majukumu yake ya ndoa.

Kundi la pili la migogoro ni ile ambayo inasuruhishika (solvable problems). Migogoro ya aina hii pamoja na kwamba inatatuliwa mara nyingi inawaachia makovu wanandoa. Mfano, migogoro hii inaweza kuwa uaminifu kwa wanandoa au kutotimiza majukumu ya ndoa. Migogoro hii hisipotatuliwa mara nyingi inageuka kuwa migogoro sawa na ile ya kundi la kwanza.

17. Njia mojawapo ya kutatua migogoro kwa wanandoa ni kupeana thamani ya kipekee kama ambavyo thamani anayopewa mgeni ndani ya familia. Mfano, unaweza kutembelewa na mgeni ambaye kwa bahati mbaya akaharibu kitu – hauwezi kumkemea mgeni kwamba kwa nini umeharibu kitu hiki? Badala yake utasema hakuna shida hiyo itarekebishwa. Waandishi wanatushirikisha kuwa ni muhimu kutumia kauli kama hizo kwa mwenza wako pale ambapo unaona amefanya kitu kinyume na utaratibu.

18. Pia, wanandoa wanaweza kutatua migogoro kwa kuhakikisha kuwa utatuzi wa migogoro unafanyika na wawili hawa kwa kutumia njia laini ambazo hazimuumizi mwenza wake. Mara nyingi tumezoea kuona ugomvi kwa wanandoa kama sehemu ya kutatua migogoro yao, waandishi wanatushirikisha kuwa njia hiyo inapaswa kuepukwa kwani sio tu inasababisha hofu kwa mwenza bali makovu yake ni ya muda mrefu na hivyo kusababisha maisha ya ndoa hisiyo na furaha.

19. Baadhi ya migogoro kwa wanandoa ambayo chimbuko lake ni matatizo ya kifedha kwa wanandoa ambayo pia utegemea mtazamo wa wanandoa juu ya fedha. Waandishi wanatushirikisha kuwa migogoro ya namna hii inaweza kutatuliwa kwa kuhakikisha wanandoa wanapanga kwa pamoja juu ya matumizi ya fedha zao. Pia, ni muhimu kufanya kazi kama timu ili kufahamu majukumu ya kila mmoja katika kufikia malengo ya kifedha kwa wanandoa.

20. Zaidi ya asilimia 67 kwa wanandoa inaonyesha kuwa wanawake mara baada ya kupata mtoto wanakuwa na mabadiliko ya ghafla kwenye kutimiza majukumu ya penzi kwa wenza wao. Hali hii inapelekea na wanaume kubadilika mara baada ya kuona hali ya kutoridhishwa na wenza wao. Hali hii kwa wanawake inasababishwa mara nyingi na mabadiliko ya majukumu yao ambayo kwa wakati huo wanakuwa na jukumu la kulea mtoto ambalo uambatana na kukosa muda wa usingizi wa kutosha. Waandishi wanatushirikisha njia nyingi za kukabiliana na hali hii kwa ajili ya kuboresha ndoa kama zilivyoainishwa hapa chini;
  • Katika kipindi cha maandalizi ya kupata mtoto wanandoa wanapaswa kutumia muda mwingi kufikiria majukumu yao mapya na jinsi ya kukabiliana nayo kama timu moja;
  • Baba awe sehemu ya kumuhudumia mtoto kwa kadri awezavyo kuliko kumuachia mama majukumu yote;
  • Baba apate muda wa kucheza na mtoto kwa ajili ya kumpa mama muda wa kukabiliana na majukumu mengine;
  • Kila mmoja hasisahau wajibu wake kwa mwenza wake; na
  • Kama baba mpe mama muda wa kupumzika.
 21. Kuridhishana kupitia tendo la ndoa ni kiungo muhimu cha kuboresha maisha ya ndoa. Kutokana na tafiti zilizofanyika zinaonesha kuwa kimaumbele wanaume wana hamu ya kufanya tendo la ndoa mara kwa mara ikilinganishwa na wanawake. Tendo hili la ndoa linaboreshwa na matendo ya kimahaba kwa wenza katika majukumu yao ya kila siku na hivyo ni vyema wanandoa wakatenga nafasi ya kipekee sawa na majukumu yao mengine kwa ajili ya tendo la ndoa. Waandishi wanatushirikisha njia zifuatazo kwa ajili ya kulifanya tendo la ndoa liwe na thamani na la kimahaba kwa wanandoa;
  • Kuwa na maana yenu ambayo ina uhusiano mkubwa kati ya mahaba na tendo la ndoa katika maisha yenu ya kila siku;
  • Jifunze jinsi ya kuzungumzia tendo hili pasipo kusababisha kumtoa kwenye hamu mwenzio katika maisha yenu ya ndoa;
  • Kuwa na muda wa kuchati/kuzungumza juu ya maisha yenu ya kimahaba. Mfano mnaweza kuwa na muda wa kukumbushana juu matendo yenu ya kimahaba yaliyopita; na
  • Jifunze namna ya kuanzisha, kukubali au kukataa kufanya tendo la ndoa pasipo kumuumiza mwenzio.
 22.  Ndoa haipo tu kwa ajili ya kutekeleza majukumu yenu, kufanya tendo la ndoa au kulea watoto bali ndoa ni jumuiko ambalo ili lidumu ni lazima wanandoa waione ndoa kama sehemu ya kutimiza matakwa ya Mwenyezi Mungu. Waandishi wanatushirikisha kuwa ni muhimu wana ndoa kufahamu kusudi la maisha yao katika kutekeleza majukumu yao ya ndoa kila siku. Hivyo ndoa imara ni lazima ijengwe kwenye msingi wa tamaduni na imani zinazowaongoza wanandoa.

Haya ni machache ambayo nimeweza kukushirikisha kati ya mengi niliyojifunza kutoka kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.

Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.

Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.

Born to Win ~ Dream Big 

Augustine Mathias Bilondwa

Namba ya Simu:      +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com




onclick='window.open(