Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha The Power of the First Step (Nguvu ya Hatua ya Kwanza)

Habari ya leo rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Nimatumaini yangu kuwa upo vizuri na unaendelea kupambana kwa ajili ya kuyaboresha maisha yako. Leo ninakuletea uchambuzi wa kitabu cha The Power of the First StepPia niendelee kukumbusha kuwa kwa mwaka huu nimejipanga kurahisisha maisha yako ya usomaji wa vitabu kwa kuhakikisha kila mwisho wa wiki (ijumaa) nakuletea uchambuzi wa kitabu kimoja ili kupitia vitabu hivi pamoja tuweze kuyaboresha maisha yetu. 

Ili uwe kwenye mfumo wangu wa kupata makala za uchambuzi wa vitabu pamoja na makala za hamasa ya kuyaishi ndoto za maisha yako unachotakiwa kufanya ni rahisi tu kwa kujaza fomu iliyopo mwishoni mwa makala hii.

Karibu tujifunze wote mambo muhimu 20 niliyojifunza kwenye kitabu hiki ambacho kimeandikwa na mwandishi Shemeji Melayeki. Mwandishi wa kitabu hiki ni muhitimu wa shahada ya Uchumi wa Kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine ambapo alihitimu mwaka 2012. Shemeji Melayeki ni mwandishi wa vitabu, mzungumzaji kwenye semina na makongamano, mwimbaji wa nyimbo za kiroho, mfanyabiashara na mtaalamu mwelekezi kwenye fani alizobobea. Katika kitabu hiki mwandishi anatuhamasisha na kutushirikisha umuhimu wa kuanza kufanya mara moja na kuepuka ugonjwa wa kuhairisha mambo kwa kuanza kuchukua hatua ya kwanza. Karibu tujifunze wote:-

1. Kila mtu ana ndoto kubwa ya maisha yake jinsi gani anavyotaka yawe. Katika kufikia ndoto zetu kuna aina tatu za makundi ya watu ambayo ni; (a) Kundi la watu wanaoamua kuchukua njia tofauti za kutafsiri ndoto zao katika vitendo (b) Kundi la watu wanaoamua kuishi na ndoto zao pasipo kuzifanyia kazi yoyote na hatimaye ndoto hizi zinafifia siku hadi siku na (c) Kundi la mwisho ni la watu ambao wameamua kujiondoa kabisa katika mbio za maisha yenye ndoto na hatimaye kuishi maisha yasiyo kuwa na tumaini la baadae.


2. Wengi wetu tumekuwa na ndoto nyingi kama vile kumiliki ndege binafsi, kumiliki biashara na kampuni kubwa, kusafiri duniani kote, kumiliki mashamba makubwa, kuwa baba/mama bora, kuishi maisha yenye furaha na ya kumjua Mungu, kuwa mtu hodari katika taaluma yako n.k. Lakini katika kuziendea ndoto hizi mara nyingi tumekutana na hali inayopelekea tunajikuta kwenye kauli kama "hauwezi kuzitekeleza", "hauwezi kufanikiwa", "hauna uwezo wa kufanya hivyo", "utawezaje kuwa mtu wa namna hiyo wakati katika ukoo wako hakuna ambaye aliwahi kufanya hivyo?" na kauli nyingine nyingi. Kauli hizi ambazo usababisha mabishano ya nafsi ndani kwa ndani na hatimaye upande mmoja unatakiwa kuushinda mwingine ili kuziishi ndoto zetu au kuachana nazo kabisa.

3. Watu wengi wameshindwa kutimiza ndoto zao kutokana na tabia kuchelewa/kusita kuchukua hatua (procrastination). Na hii inasababishwa na hofu ya kuchukua hatua ya kwanza. Kama unataka kuishi ndoto za maisha yako lazima uwe tayari kuishinda hofu hii ambayo imepelekea maisha yako yawe jinsi yalivyo sasa. Na sababu kubwa inasababisha hofu kwa walio wengi ni swali ambalo linakuwa kwenye fikra zao la kuwa "itakuwaje endapo sitafanikiwa?" Ili uishinde kauli hii tekeleza yale yanayokuogopesha pindi unapoyawaza badala ya kuogopa kushindwa kwani hata ukishindwa utakuwa umejifunza kitu.

4. Hatua ya kwanza inatoa hamasa na nguvu za kuendelea kuchukua hatua za ziada badala ya uzembe. Ili kuchukua hatua ya kwanza mwandishi anatufundisha kuwa kuna aina tatu za ujasiri (a) ujasiri wa kuanza kuchukua hatua (b) ujasiri wa kuvumilia mara baada ya kuchukua hatua na (c) ujasiri wa kumaliza vizuri hatua ulizoanza kuchukua. Ili kufikia ndoto zako ni lazima uwe tayari kuvaa ujasiri wa aina zote.

5. Safari ya maili milioni inaanza na hatua moja. Hapa mwandhishi anatuamasisha umuhimu wa kuchukua hatua ya kwanza pasipo kuogopa urefu wa safari katika kuzitimiza ndoto zetu. Pasipo kuogopa urefu wa safari yako ni lazima uwe tayari kuanza hatua ya kwanza.

6. Ili kuchukua hatua unahitaji kwanza kuwa na imani thabiti juu ya jambo ambalo unaenda kulitekeleza. Na hapa ndipo imani yako inatakiwa ijengwe kwenye misingi ya ushindi badala ya kufikiria kushindwa. Pia, unatakiwa ufikirie kuwa maisha ni sawa na mchezo au mtihani ambao unaenda kufanya pasipo kuwa na uhakika wa ushindi.

7. Mwandishi anatufundisha kuwa Mungu ndo anaongoza hatua zetu. Hivyo tunapoomba Mwenyezi Mungu kuongoza hatua zetu ni lazima tuwe tayari tumeanzisha hatua za kuendea ndoto zetu vinginevyo hakuna maana ya kuomba tukiwa bado tunaogopa kuchukua hatua kwani Mungu hatotuongoza popote.


8. Hatua ya kwanza itakufanya uzinduke kutoka kwenye hali yako ya awali na kuanza maisha mapya. Hii ni sheria ya asili ambayo mwanasayansi Isac Newton aliifafanua kwa kusema “kitu chochote kitaendelea kuwa katika hali yake ya utulivu au kuendelea kuseleleka endapo hakuna msukumo au nguvu yoyote itakayotumika juu ya kitu hiko”. Hivyo hata wewe husipokuwa tayari kuchukua hatua utaendelea kuwa jinsi ulivyo miaka nenda rudi. Pia unapoanza kuchukua hatua kumbuka kuwa unaweza endelea kupiga hatua za ziada endapo hautoruhusu vikwazo vikuzuie au kukata tamaa.

9. Mwandishi anatushirikisha kuwa nia ya kutuhamasisha kuchukua hatua ni kutokana na ukweli kwamba unapochukua hatua ya kwanza utapata uzoefu na hata pale utakaposhindwa kufikia lengo tayari utakuwa umejifunza kitu. Pia, baada ya hatua ya kwanza unafungua milango ya fursa nyingi ambazo kwa sasa huzioni.

10.  Ili ufanikiwe katika maisha lazima uwe tayari kujiona mjinga. Hii nikutokana na ukweli kwamba kadri utakavyoanza kuchukua hatua kuna mambo mengi yanayokuzunguka yatasababisha ujione kama vile kila kitu ni kipya kwako na pia wewe utatakiwa kuwa mtu wa tofauti pale inapobidi. Kwanza jamii inayokuzunguka haitakuelewa, wakosoaji watakuwa wengi na mengine mengi kwa vile jamii inasubilia wewe ushindwe. Unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha unajua njia unayoiendea na kusimama imara katika kila hatua unayopiga.


11. Kitu muhimu katika kuanza hatua ya kwanza ni ubora wa ndoto yako. Je ni kubwa kiasi gani? Je itakupa changamoto kiasi gani? Baada ya kuwa na ndoto iliyo bora unapoanza kuchukua hatua ya kwanza husiogopeshwe na kiasi cha fedha ulichonacho mfukoni au kwenye akaunti ya benki wala hali ya yako ya maisha kwa wakati huo bali la muhimu ni kwa kiasi gani una dhamira ya kutimiza ndoto yako. Hivyo unatakiwa kuwa tayari kufumba masikio kwa sauti za ndani na nje ya nafsi na kuanza mara moja pasipo kungoja.

12. Ili uhirusu imani yako ifanye kazi kuwa tayari kuonekana mwendawazimu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kadri unavyoanza kuchukua hatua yapo mambo mengi ambayo unatakiwa kuongozwa na imani kuliko mazoea ya jamii. Kadri utakavyofanya vitu tofauti na mazoea ya jamii ndivyo utaonekana mtu wa hajabu na wengi wao watakuona kama wewe ni kichaa. Fumba macho endapo unaamini upo kwenye njia salama na piga hatua na mwisho wake jamii itakuelewa baadae.

13.  Unapoanza kuchukua hatua husikubali kudanganjwa na mtu kuwa kwa sasa hakuna tena uvumbuzi bali ongozwa na kauli kuwa dunia bado imejaa fursa kutokana na uasili wake wa milele. Hakikisha unatumia urithi wa asili ambao kila mmoja wetu amepewa na Muumba kwa ajili ya kuitawale dunia.

14. Dunia ipo kwa ajili ya wale wanaothubutu na hawa ndio wenye thamani ya maisha yao hapa duniani. Kwa maana nyingine kama unataka maisha yako yawe na thamani lazima uwe tayari kuishi kusudi la maisha. Mwenyezi Mungu alikuwa ukiwa mtawala na wala sio mtawaliwa na umeumbwa ukiwa kichwa na wala sio mkia. Hivyo basi, hakikisha unakuwa mzalishaji kwa kutumia talanta uliyonayo ndani mwako, husikubali talanta hiyo ipatwe na kutu kwa vile una uoga wa kuthubutu. Zinduka na anza sasa.


15. Mwandishi anatushirikisha kuwa ili upate zaidi ni lazima uwe tayari kutoa zaidi. Anza kutoa yale uliyonayo ndani mwako, nenda hatua za ziada ambazo hujawahi kufikia, tumia vipaji na nguvu ulizonazo kwa ajili ya kuhakikisha unatekeleza ndoto zako. Kabala haujaanza kuchukua hatua kamwe hauwezi kujua nguvu, vipaji na thamani ya maisha yako kwa wengine. Kadri utakavyopiga hatua moja baada ya nyingine ndivyo utakavyogundua kuwa umekuwa unajikwamisha mwenyewe kwa kuchelewa kuchukua hatua.

16. Husiishie kusoma makala za namna hii au vitabu na kuhamasika kwa muda halafu baada ya hapo ukarudi kwenye hali ya maisha yako ya awali. Hakikisha unaanza mara moja kwa kujiwekea mipango maalumu ya kubadilisha sehemu ya maisha yako ambayo kwa muda imekuwa kikwazo kwako kuchukua hatua.

17. Baada ya kuchukua hatua ya kwanza ili ufanikiwa lazima uwe tayari kuendeleza hatua zako. Hapa chukulia mfano wa mwanariadha wa mbio ndefu kama anataka kushinda ni lazima awe tayari kuendelea kukimbia pasipo kujali upinzani ulipo mbele yake. Hata wewe, hakikisha changamoto unazokutana nazo unazitumia kama chachu ya mafanikio yako. Jiulize kwani nini unakutana na changamoto husika na fundisho lipo unaweza kulipata kwenye kila changamoto unayokutana nayo.

18.  Maisha yako yapo mikononi mwako na wewe ndio muhusika mkuu wa maisha yako. Huna sababu ya kutafuta miujiza nje ya uwezo wako kwa kuwa tayari miujiza ipo ndani mwako. Cha msingi kuhakikisha unaiamisha miujiza hii ilianze kutekeleza kusudi la Muumba.

19. Wanamafanikio ni wale ambao wana ndoto na wanatambua kuwa wamepewa talanta (vipaji) ambazo zinahitaji kutumika na katika maisha yao ya kila siku wanatumia vipaji hivi ili kufikia ndoto zao. Kwa mtazamo huu wanamafanikio wapo tayari kusherekea ushindi kutokana na vitu vidogo vidogo katika maisha yao ya kila siku.

20.  Wanamafanikio ni wale ambao wanatambua kuwa ili kutumia talanta walizopewa ni lazima wawe tayari kujifunza kwa vitendo, uzoefu na kupitia wanamafanikio waliowatangulia. Hapa ndipo tunaona umuhimu wa kusoma vitabu, makala na majarida kwa ajili ya kuendelea kuwasha moto ndani mwetu ambao utaendelea kutusukuma kuchukua hatua. Je unataka kuishi kusudi la maisha yako?? Chukua hatua yako ya kwanza leo hii!


Haya ndiyo niliyojifunza katika kitabu hiki. Ni matumaini yangu kuwa ukiyafanyia kazi yatabadilisha maisha yako kwa ujumla. Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi. Nakutakia mapambano mema.

Ili kupata makala za namna hii kwa mfumo wa barua pepe BONYEZA HAPA

Karibuni kwenye fikra tajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.

Born to Win~Dream Big

A.M. Bilondwa
0786881155
fikrazatajiri@gmail.com



Karibu Ujiunge na Mtando wa Fikra za Kitajiri

* indicates required

onclick='window.open(