Habari ya leo rafiki na
msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Nimatumaini yangu kuwa upo vizuri na
unaendelea kupambana kwa ajili ya kuyaboresha maisha yako. Leo ninakuletea
uchambuzi wa kitabu cha The Power of the First Step. Pia niendelee
kukumbusha kuwa kwa mwaka huu nimejipanga kurahisisha maisha yako ya usomaji wa
vitabu kwa kuhakikisha kila mwisho wa wiki (ijumaa) nakuletea uchambuzi wa
kitabu kimoja ili kupitia vitabu hivi pamoja tuweze kuyaboresha maisha yetu.
Ili uwe kwenye mfumo wangu wa kupata makala za uchambuzi wa vitabu pamoja na makala za hamasa ya kuyaishi ndoto za maisha yako unachotakiwa kufanya ni rahisi tu kwa kujaza fomu iliyopo mwishoni mwa makala
hii.
Karibu tujifunze wote mambo muhimu 20 niliyojifunza kwenye kitabu hiki ambacho kimeandikwa na mwandishi Shemeji Melayeki. Mwandishi wa kitabu hiki ni muhitimu wa shahada ya Uchumi wa Kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine ambapo alihitimu mwaka 2012. Shemeji Melayeki ni mwandishi wa vitabu, mzungumzaji kwenye semina na makongamano, mwimbaji wa nyimbo za kiroho, mfanyabiashara na mtaalamu mwelekezi kwenye fani alizobobea. Katika kitabu hiki mwandishi anatuhamasisha na kutushirikisha umuhimu wa kuanza kufanya mara moja na kuepuka ugonjwa wa kuhairisha mambo kwa kuanza kuchukua hatua ya kwanza. Karibu tujifunze wote:-
1.
Kila mtu ana ndoto kubwa ya maisha yake
jinsi gani anavyotaka yawe. Katika kufikia ndoto zetu kuna aina tatu za makundi
ya watu ambayo ni; (a) Kundi la watu wanaoamua kuchukua njia tofauti za
kutafsiri ndoto zao katika vitendo (b) Kundi la watu wanaoamua kuishi na ndoto
zao pasipo kuzifanyia kazi yoyote na hatimaye ndoto hizi zinafifia siku hadi
siku na (c) Kundi la mwisho ni la watu ambao wameamua kujiondoa kabisa katika
mbio za maisha yenye ndoto na hatimaye kuishi maisha yasiyo kuwa na tumaini la
baadae.
2.
Wengi wetu tumekuwa na ndoto nyingi
kama vile kumiliki ndege binafsi, kumiliki biashara na kampuni kubwa, kusafiri
duniani kote, kumiliki mashamba makubwa, kuwa baba/mama bora, kuishi maisha
yenye furaha na ya kumjua Mungu, kuwa mtu hodari katika taaluma yako n.k.
Lakini katika kuziendea ndoto hizi mara nyingi tumekutana na hali inayopelekea tunajikuta kwenye kauli kama "hauwezi kuzitekeleza", "hauwezi kufanikiwa", "hauna uwezo wa
kufanya hivyo", "utawezaje kuwa mtu wa namna hiyo wakati katika ukoo wako hakuna
ambaye aliwahi kufanya hivyo?" na kauli nyingine nyingi. Kauli hizi ambazo
usababisha mabishano ya nafsi ndani kwa ndani na hatimaye upande mmoja
unatakiwa kuushinda mwingine ili kuziishi ndoto zetu au kuachana nazo kabisa.
3.
Watu wengi wameshindwa kutimiza ndoto
zao kutokana na tabia kuchelewa/kusita kuchukua hatua (procrastination). Na hii
inasababishwa na hofu ya kuchukua hatua ya kwanza. Kama unataka kuishi ndoto za
maisha yako lazima uwe tayari kuishinda hofu hii ambayo imepelekea maisha yako yawe
jinsi yalivyo sasa. Na sababu kubwa inasababisha hofu kwa walio wengi ni swali ambalo linakuwa kwenye fikra zao la kuwa "itakuwaje endapo sitafanikiwa?" Ili uishinde kauli hii
tekeleza yale yanayokuogopesha pindi unapoyawaza badala ya kuogopa kushindwa
kwani hata ukishindwa utakuwa umejifunza kitu.
4.
Hatua ya kwanza inatoa hamasa na nguvu
za kuendelea kuchukua hatua za ziada badala ya uzembe. Ili kuchukua hatua ya
kwanza mwandishi anatufundisha kuwa kuna aina tatu za ujasiri (a) ujasiri wa
kuanza kuchukua hatua (b) ujasiri wa kuvumilia mara baada ya kuchukua hatua na
(c) ujasiri wa kumaliza vizuri hatua ulizoanza kuchukua. Ili kufikia ndoto zako
ni lazima uwe tayari kuvaa ujasiri wa aina zote.
5.
Safari ya maili milioni inaanza na
hatua moja. Hapa mwandhishi anatuamasisha umuhimu wa kuchukua hatua ya kwanza
pasipo kuogopa urefu wa safari katika kuzitimiza ndoto zetu. Pasipo kuogopa
urefu wa safari yako ni lazima uwe tayari kuanza hatua ya kwanza.
6.
Ili kuchukua hatua unahitaji kwanza
kuwa na imani thabiti juu ya jambo ambalo unaenda kulitekeleza. Na hapa ndipo
imani yako inatakiwa ijengwe kwenye misingi ya ushindi badala ya kufikiria
kushindwa. Pia, unatakiwa ufikirie kuwa maisha ni sawa na mchezo au mtihani
ambao unaenda kufanya pasipo kuwa na uhakika wa ushindi.
7.
Mwandishi anatufundisha kuwa Mungu ndo
anaongoza hatua zetu. Hivyo tunapoomba Mwenyezi Mungu kuongoza hatua zetu ni
lazima tuwe tayari tumeanzisha hatua za kuendea ndoto zetu vinginevyo hakuna
maana ya kuomba tukiwa bado tunaogopa kuchukua hatua kwani Mungu hatotuongoza
popote.
8.
Hatua ya kwanza itakufanya uzinduke
kutoka kwenye hali yako ya awali na kuanza maisha mapya. Hii ni sheria ya asili
ambayo mwanasayansi Isac Newton aliifafanua kwa kusema “kitu chochote
kitaendelea kuwa katika hali yake ya utulivu au kuendelea kuseleleka endapo
hakuna msukumo au nguvu yoyote itakayotumika juu ya kitu hiko”. Hivyo hata wewe
husipokuwa tayari kuchukua hatua utaendelea kuwa jinsi ulivyo miaka nenda rudi.
Pia unapoanza kuchukua hatua kumbuka kuwa unaweza endelea kupiga hatua za ziada
endapo hautoruhusu vikwazo vikuzuie au kukata tamaa.
9.
Mwandishi anatushirikisha kuwa nia ya
kutuhamasisha kuchukua hatua ni kutokana na ukweli kwamba unapochukua hatua ya
kwanza utapata uzoefu na hata pale utakaposhindwa kufikia lengo tayari utakuwa
umejifunza kitu. Pia, baada ya hatua ya kwanza unafungua milango ya fursa
nyingi ambazo kwa sasa huzioni.
10. Ili ufanikiwe katika maisha lazima uwe tayari
kujiona mjinga. Hii nikutokana na ukweli kwamba kadri utakavyoanza kuchukua
hatua kuna mambo mengi yanayokuzunguka yatasababisha ujione kama vile kila kitu
ni kipya kwako na pia wewe utatakiwa kuwa mtu wa tofauti pale inapobidi. Kwanza
jamii inayokuzunguka haitakuelewa, wakosoaji watakuwa wengi na mengine mengi
kwa vile jamii inasubilia wewe ushindwe. Unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha
unajua njia unayoiendea na kusimama imara katika kila hatua unayopiga.
11. Kitu
muhimu katika kuanza hatua ya kwanza ni ubora wa ndoto yako. Je ni kubwa kiasi
gani? Je itakupa changamoto kiasi gani? Baada ya kuwa na ndoto iliyo bora
unapoanza kuchukua hatua ya kwanza husiogopeshwe na kiasi cha fedha ulichonacho
mfukoni au kwenye akaunti ya benki wala hali ya yako ya maisha kwa wakati huo
bali la muhimu ni kwa kiasi gani una dhamira ya kutimiza ndoto yako. Hivyo
unatakiwa kuwa tayari kufumba masikio kwa sauti za ndani na nje ya nafsi na
kuanza mara moja pasipo kungoja.
12. Ili uhirusu imani yako ifanye kazi kuwa
tayari kuonekana mwendawazimu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kadri
unavyoanza kuchukua hatua yapo mambo mengi ambayo unatakiwa kuongozwa na imani
kuliko mazoea ya jamii. Kadri utakavyofanya vitu tofauti na mazoea ya jamii
ndivyo utaonekana mtu wa hajabu na wengi wao watakuona kama wewe ni kichaa.
Fumba macho endapo unaamini upo kwenye njia salama na piga hatua na mwisho wake
jamii itakuelewa baadae.
13. Unapoanza kuchukua hatua husikubali
kudanganjwa na mtu kuwa kwa sasa hakuna tena uvumbuzi bali ongozwa na kauli
kuwa dunia bado imejaa fursa kutokana na uasili wake wa milele. Hakikisha
unatumia urithi wa asili ambao kila mmoja wetu amepewa na Muumba kwa ajili ya
kuitawale dunia.
14. Dunia ipo kwa ajili ya wale
wanaothubutu na hawa ndio wenye thamani ya maisha yao hapa duniani. Kwa maana
nyingine kama unataka maisha yako yawe na thamani lazima uwe tayari kuishi
kusudi la maisha. Mwenyezi Mungu alikuwa ukiwa mtawala na wala sio mtawaliwa na
umeumbwa ukiwa kichwa na wala sio mkia. Hivyo basi, hakikisha unakuwa
mzalishaji kwa kutumia talanta uliyonayo ndani mwako, husikubali talanta hiyo
ipatwe na kutu kwa vile una uoga wa kuthubutu. Zinduka na anza sasa.
15. Mwandishi anatushirikisha kuwa ili
upate zaidi ni lazima uwe tayari kutoa zaidi. Anza kutoa yale uliyonayo ndani
mwako, nenda hatua za ziada ambazo hujawahi kufikia, tumia vipaji na nguvu
ulizonazo kwa ajili ya kuhakikisha unatekeleza ndoto zako. Kabala haujaanza
kuchukua hatua kamwe hauwezi kujua nguvu, vipaji na thamani ya maisha yako kwa
wengine. Kadri utakavyopiga hatua moja baada ya nyingine ndivyo utakavyogundua
kuwa umekuwa unajikwamisha mwenyewe kwa kuchelewa kuchukua hatua.
16. Husiishie kusoma makala za namna hii au vitabu
na kuhamasika kwa muda halafu baada ya hapo ukarudi kwenye hali ya maisha yako
ya awali. Hakikisha unaanza mara moja kwa kujiwekea mipango maalumu ya
kubadilisha sehemu ya maisha yako ambayo kwa muda imekuwa kikwazo kwako
kuchukua hatua.
17. Baada ya kuchukua hatua ya kwanza ili
ufanikiwa lazima uwe tayari kuendeleza hatua zako. Hapa chukulia mfano wa
mwanariadha wa mbio ndefu kama anataka kushinda ni lazima awe tayari kuendelea
kukimbia pasipo kujali upinzani ulipo mbele yake. Hata wewe, hakikisha
changamoto unazokutana nazo unazitumia kama chachu ya mafanikio yako. Jiulize
kwani nini unakutana na changamoto husika na fundisho lipo unaweza kulipata
kwenye kila changamoto unayokutana nayo.
18. Maisha yako yapo mikononi mwako na wewe
ndio muhusika mkuu wa maisha yako. Huna sababu ya kutafuta miujiza nje ya uwezo
wako kwa kuwa tayari miujiza ipo ndani mwako. Cha msingi kuhakikisha unaiamisha
miujiza hii ilianze kutekeleza kusudi la Muumba.
19. Wanamafanikio ni wale ambao wana ndoto
na wanatambua kuwa wamepewa talanta (vipaji) ambazo zinahitaji kutumika na
katika maisha yao ya kila siku wanatumia vipaji hivi ili kufikia ndoto zao. Kwa
mtazamo huu wanamafanikio wapo tayari kusherekea ushindi kutokana na vitu
vidogo vidogo katika maisha yao ya kila siku.
20. Wanamafanikio ni wale ambao wanatambua
kuwa ili kutumia talanta walizopewa ni lazima wawe tayari kujifunza kwa
vitendo, uzoefu na kupitia wanamafanikio waliowatangulia. Hapa ndipo tunaona
umuhimu wa kusoma vitabu, makala na majarida kwa ajili ya kuendelea kuwasha
moto ndani mwetu ambao utaendelea kutusukuma kuchukua hatua. Je unataka kuishi
kusudi la maisha yako?? Chukua hatua yako ya kwanza leo hii!
Haya ndiyo niliyojifunza katika
kitabu hiki. Ni matumaini yangu kuwa ukiyafanyia kazi yatabadilisha maisha yako
kwa ujumla. Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale
unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa
mahali pazuri pa kuishi. Nakutakia
mapambano mema.
Ili kupata makala za namna
hii kwa mfumo wa barua pepe BONYEZA HAPA
Karibuni kwenye fikra
tajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.
Born to Win~Dream Big
A.M.
Bilondwa
0786881155
fikrazatajiri@gmail.com
0786881155
fikrazatajiri@gmail.com