NENO LA SIKU_JANUARI 29/2022: Je! Wewe Ni Mzazi/Mlezi Mwenye Kiu ya Kukuza Wanao Kimaadili? Fahamu Jinsi Mtoto Anavyobadilika Kitabia!
📝Hongera rafiki yangu kwa kupata kibali cha kuendelea na majukumu yako ya siku hii ya leo. Ni jambo la heri kuona tupo salama na tumefanikiwa kuendelea kusukuma gurudumu la kufanikisha ndoto muhimu za maisha yetu.
📝Katika neno la siku ya leo nitaangazia wajibu wa wazazi/walezi au mtu ambaye anakusudia kuwa na familia yenye watoto au wewe ambaye kwa namna moja au nyingine majukumu yako ya kila siku yanahusisha kujumuika na watoto wa rika tofauti.
📝Uendelevu wa jamii au taifa lolote, msingi wake ni idadi ya watoto wanaokua katika kila rika kwa kuzingatia misingi bora ya maadili. Jamii au Taifa ambalo misingi ya maadili inaporomoka ni wazi kuwa maendeleo ya jamii au taifa hilo yapo hatarini.
📝Ukweli huu unatokana na msingi kuwa maadili yanaunda sifa za utu ambazo hutuongoza kufanya maamuzi na hukumu juu ya kile tunachofikiri ni sawa au si sahihi katika maisha ya kila siku.
📝Kwa kuwa watu wana uzoefu tofauti, maadili yanaweza kutofautiana kati ya mtu na mtu, jamii na jamii au taifa na taifa. Hata hivyo, pamoja na tofauti hizo katika jamii au taifa moja ni lazima pawepo tunu zinazoongoza watu wake. Tunu hizo ndizo zinaunda msingi wa maadili kwa wananchi wa taifa husika.
📝Pamoja na uwepo wa tunu hizo, maadili hutakiwa kuanza kufundishwa katika ngazi ya kwanza ya utawala ambayo ni ngazi ya familia ambako walimu ni wazazi au walezi na watoto ndo wanafunzi.
📝Wazazi au walezi wana jukumu kubwa la kuhakikisha kwanza wao wenyewe wanaishi maadili mema na wanatumia muda mwingi kuwa karibu na wanao kwa ajili ya kurekebisha tabia zao kulingana na hatua za ukuaji wanazopitia.
📝Hata hivyo, tunaishi katika Ulimwengu ambao idadi ya watoto wenye maadili yasiyofaa inaongezeka kila siku. Ukuaji wa teknolojia unaendelea kuzalisha kizazi ambacho asilimia kubwa ya kizazi hicho hakina maadili mema.
📝Ukuaji wa teknolojia na miundombinu ya kijamii umepelekea wazazi au walezi kukosa muda wa kutosha kuwa karibu na watoto wao.
📝Pia, ukuaji wa teknolojia hasa teknolojia ya mawasiliano unaendelea kuzalisha kizazi ambacho kinajifunza maadili kutoka kwenye TV, filamu au mitandao ya kijamii.
📝Ni kutokana na hayo, kila kukicha wazazi wanazidi kukosa muda wa kuwa karibu na watoto wao na baadhi wanachagua kutafuta watu wa kutekeleza jukumu la malezi kwa watoto tena watoto wachanga ambao wanahitaji misingi bora ya malezi.
📝Waswahili husema; “Samaki mkunje angali mbichi”, kila hatua ya ukuaji wa mtoto ni hatua muhimu katika kuamua maadili ya mtoto husika katika kipindi cha utu uzima.
📝Hivyo, kadri jamii inavyozidi kuwa na idadi kubwa ya kizazi kisichojitambua, mtu wa kwanza kulaumiwa ni mzazi kwa maana ameshindwa kutekeleza jukumu lake la malezi.
📝Hata hivyo, wazazi au walezi wengi wanashindwa kutekeleza jukumu lao la msingi kutokana na kutokujua nadharia (theory) mbalimbali za maendeleo na ukuaji wa watoto. Wanafalsafa mbalimbali wameweza kuelezea nadharia mbalimbali kuhusiana na hatua za ukuzaji wa tabia kwa mtoto.
📝Je! Wewe ni miongoni mwa wazazi au walezi ambao wangependa kujifunza kuhusu nadharia za maendeleo na ukuaji wa watoto? Kama ndivyo, hakikisha unapata nakala yako ya kitabu cha MAISHA YENYE THAMANI.
📝Katika kitabu hiki utajifunza nadharia za Wanafalsafa tano tofauti ambao kila mmoja ameelezea jinsi binadamu anavyojifunza tabia mpya katika kila hatua ya ukuaji wake. Nadharia hizi ni muhimu katika kipindi cha sasa ambacho wazazi au walezi tunaangaika kutafuta mbinu bora za kurejesha maadili kwa kizazi chetu.
📝Kwa nini kila mmoja wetu anatakiwa kuweka mkazo wa kuboresha maadili ya watoto? Suala la maadili mema ya watoto ni la kila mmoja kwenye jamii kutokana na ukweli kwamba maadili sahihi huwezesha watoto:-
Kujenga akili yao
Kutofautisha kati ya mema na mabaya
Kubadili mtazamo juu yao wenyewe na Ulimwengu unaowazunguka
Ni msingi wa tabia njema katika kipindi chote cha ukuaji
Kusaidia kuepuka ushawishi mbaya kutoka kwa makundi ya watoto wenzao
Ni msingi wa utatuzi wa changamoto za kimaisha
Husaidia watoto kuongeza uwezo wa kujiamini
Husaidia watoto kukua katika misingi ya kufikiria mahitaji ya wengine katika jamii.