NENO LA SIKU_JANUARI 31/2022: Maisha Ni Mafupi Sana! Amua Sasa Kuishi Kwa Faida Kulingana na Misingi ya Asili
๐Ni siku nyingine ambayo tumezawadiwa ili tupate kuendelea kuwa bora zaidi ya jana. Hongera rafiki na mfuatiliaji wa masomo yangu kwa kufanikiwa kuifikia siku hii ambayo inaongeza idadi ya siku za uhai wako hapa duniani.
๐Ni siku ambayo naamini unaendelea kuitumia katika kutimiza majukumu yako muhimu. Kupitia siku ya leo tumeongezewa muda wa kuendeleza jitihada za kuishi kwa faida ya nafsi zetu, jamii na mazingira yanayotuzunguka.
๐Karibu tutafakari kupitia makala ya siku ya leo ambayo ni mwendelezo wa tafakari kuhusu maisha haya tunayoishi. Katika makala ya leo nitapenda ufanye tathimini ya maisha yako kwa kipindi ambacho umefanikiwa kuishi hadi sasa. Jiulize maswali muhimu yanayolenga kukurudisha kwenye historia ya maisha yako.
๐Piga picha ya kipindi chote ambacho umepitia toka ulivyofikia umri wa kuweza kutambua mema na mabaya. Kwa maana, yaone matukio uliopitia katika maisha kama mfululizo wa matukio yanayounda filamu halisi ya maisha yako.
๐Kupitia filamu ya maisha yako, jiulize maswali ya tafakari ambayo yanalenga kuhoji kila tukio katika filamu hiyo. Kama ni matukio ya mateso, jiulize chanzo cha mateso hayo na ulifanya nini ili kuepuka mateso husika. Kama ni matukio yanayosisimua hisia za mwili wako hasa hisia za furaha, jiulize ni matendo gani yaliyopelekea furaha hiyo na hitimisha kwa kulinganisha na hali ya sasa.
๐Endelea kupitia kila tukio kwenye filamu ya maisha yako! Jiulize ni matendo gani ambayo enzi hizo yaliwezesha kujiona mtu mwenye thamani japo yawezekana thamani hiyo haionekani kwa sasa. Jiulize ni watu gani muhimu ambao wamewezesha ufanikiwe kufikia hatua ya mafanikio uliyonayo! Je! Watu hao bado wana nafasi katika maisha ya sasa? Pia, jiulize watu ambao kwa njia moja au nyingine unajutia kukutana nao, kwa kuwa, kupitia wao kuna matukio ambayo unaona kwa kiasi yameharibu mtiririko wa matukio katika filamu ya maisha yako.
๐Husichoke endelea kupitia filamu ya maisha yako! Jiulize ni matendo gani ambayo yamekufanya mtu yule unayemuona kuwa ni wewe wa sasa bila kujali kama unajikadiria katika viwango vya juu au kuna kitu ambacho unaona lazima kifanyike ili ujivunie kuishi kwako hapa duniani.
๐Jiulize ikiwa ungepewa nafasi ya kurudi nyuma na kurekebisha, ni matukio yapi ambayo hungependa yawe sehemu ya filamu ya maisha yako na yapi husingetamani yaonekana kabisa kwenye historia yako. Jiulize ni matukio yapi ambayo unaona yameweka msingi wa maisha yako.
๐Kupitia filamu ya maisha yako jiulize ni matukio yapi ambayo unatamani yaonekane katika maisha yako ya kesho. Jiulize hatua zipi muhimu ambazo unatakiwa kuchukua ili kuunda msingi imara wa maisha yako ya kesho.
๐Hitimisha kwa kujiuliza kama leo ingekuwa siku yako ya mwisho kuishi hapa duniani historia ya matukio katika filamu ya maisha yako ingekuhumu kuelekea upande wa mema (upande wa Malaika) au mabaya (upande wa Ibilisi). Jiulize watu wangesema nini katika maombolezo ya msiba wako. Jiulize nani ambaye angelia au ni wangapi ambao wangelia zaidi kwa kuhuzunishwa na kifo chako. Kilio ambacho kinatokana na matendo mema uliyowatendea enzi za uhai wako. Jiulize ni watu wangapia ambao wangesherekea kusikia habari za kifo chako kutokana na unyama uliowatendea.
๐Tumia tafakari hii kurekebisha matukio ya filamu ya maisha yako. Amua sasa kuishi maisha yanayojikita kwenye uwanda mpana wa matendo mema dhidi ya nafsi yako, watu wengine na mazingira yanayokuzunguka. Amua sasa kuishi kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo. Amua sasa kuibadilisha filamu ya maisha yako ili iwe na matukio yanayovutia dhidi ya nafsi yako na watu wote. Nakutakia kila lenye heri katika kuishi kwa faida kuanzia sasa.
PATA NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI
Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.
Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.