Habari ya leo rafiki
na msomaji wa mtandao wa Fikra za Kitajiri. Hongera kumaliza salama mwaka 2019 na
kuanza vyema mwaka 2020.
Kama kawaida kila tunapoanza mwaka tunajiwekea malengo
kwa ajili ya kuboresha kila sekta ya maisha yetu. Katika mwaka huu nimejiwekea
lengo la kusoma na kuchambua vitabu 30 na vyote nitakushirikisha maarifa muhimu
kwa ajili ya kubadilisha maisha yako. Karibu tusafiri wote katika kipindi hiki
cha mwaka 2020.
Pia katika kipindi
hiki, mtandao wa Fikra za Kitajiri umedhamiria kuunganisha wafamilia wake kwa
kuanzisha kundi la WhatsApp ambalo litatumika kama darasa la kujifunza maarifa
mbalimbali yanayolenga kuboresha maisha yetu. Kupata fursa hii ya kuwa sehemu
ya kundi hili nitumie ujumbe kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com na
utaunganishwa na kundi hili ndani ya muda wa kipindi cha wiki mbili kuanzia
sasa.
Kumbuka kuwa, Lengo letu
kubwa tunapoingia kwenye mwaka 2020 ni kuendelea kuweka bidii kwa kadri ya
uwezo wetu kwa ajili ya kuifanya Dunia kuwa mahala pazuri pa kuishi. Kumbuka ili
Dunia iwe mahala pazuri pa kuishi ni lazima lianzie katika maisha yako. Ukiwa
na maisha mazuri Dunia hii utaiona sehemu salama pa kuishi na ndivyo ilivyo kwa
jamii unayoigusa. Karibu tena katika makala ya uchambuzi wa kitabu cha wiki
hii.
Kama bado hujajiunga
na mfumo wetu wa kupokea makala za uchambuzi wa vitabu, tafadhali fanya hivyo KWA KUBONYEZA HAPA na
kujaza fomu kisha bofya “jiunge/subscribe”. Ni fursa ambayo itakuwezesha kupata
uchambuzi wa vitabu kwa lugha rahisi kupitia barua pepe yako.
Kitabu cha kwanza
katika mwaka huu ni “Hooked” ambacho kimeandikwa na mwandishi
Nir Eyal. Kwa ufupi katika kitabu
hiki mwandishi anatushirikia namna ambavyo mfanyabiashara wa karne ya 21 anavyopaswa
kuzalisha au kutoa huduma ambazo zinalenga kuteka akili na hisia za wateja bila
ya wao kutambua.
Mwandishi
anatushirikisha kuwa tafiti zinaonesha kuwa asilimia 79 ya wamiliki wa simu
janja wanatumia dakika 15 kupitia simu zao hasa kwenye kurasa za mitandao ya
kijamii kila baada ya kuamka. Kubwa zaidi moja ya tatu ya kundi hilo wapo
tayari wakose chakula au tendo la ndoa kwa mke wake kuliko kukosa simu yake
janja. Tafiti zinaonesha kuwa kundi hili linapitia simu zao kati ya mara 44
hadi 150 kwa siku nzima.
Jibu la haraka hapa tunagundua kuwa teknolojia
tunazotumia zimetugeuza kuwa watumwa au walevi sawa na yalivyo madawa ya
kulevya. Ulevi huu unakamilika kupitia msukumo/kichocheo cha kuangalia simu
kila mara. Ni msukumo wa kuperuzi Facebook. Instangram, Youtube, Twiter au
WhatsApp kila baada ya dakika kadhaa.
Tabia za kila siku zinajengwa na mazoea ya
vitu vidogo vidogo ambavyo vinatokea katika maisha ya mhusika pasipo uelewa
wake (vinatokea bila kushirikisha mfumo wa ubongo wa mhusika). Matokeo yake ni
kwamba kwa kutumia mfano huo wa simu janja maisha ya mhusika yanakuwa
yanaendeshwa na watengenezaji wa teknolojia husika bila yeye kujitambua. Mfano,
mmiliki wa Facebook anakuendesha wewe kila mara pasipo wewe kujitambua huku
yeye akifanikiwa kuingiza hela nyingi kupitia kwenye biashara ya matangazo katika
mtandao wake huo wa kijamii.
Hivyo, katika karne hii ya 21, Kampuni nyingi
zimegundua kuwa ili ufanikishe kuuza biashara yako kwa mafanikio makubwa huna
budi ya kuwa na bidhaa ambayo inabadilisha mfumo wa akili na hisia ya mhusika
pasipo yeye kujitambua. Ni lazima bidhaa hiyo imfanye mhusika kutamani kubofya
ili aone kinachojiri kila mara. Bidhaa hizo zinaunganishwa na hisia pamoja na
mahitaji ya kila siku ya mwanadamu. Mwisho, wake ni kwamba mhusika anajikuta
amejenga tabia mpya katika maisha yake bila yeye kujigundua kuwa yupo kwenye
ulevi/uteja wa bidhaa husika. Tabia hiyo mpya inaambatana na msukumo/vichocheo kutoka
ndani mwake kiasi ambacho anajikuta anatekeleza au kutumia bila kuhitaji
kukumbushwa kufanya hivyo sawa na ilivyo kwa uteja (addiction) mwingine.
Karibu ushirikiane nami kujifunza machache
kati ya mengi ambayo tunashirikishwa katika kitabu hiki:
1. Tabia
mpya zinajengwa kupitia mzunguko wa hatua nne ambazo ni:
a) Kichocheo (Trigger) – Kianzilishi cha tabia. Vichocheo vinagawanyika
kati ya kichocheo kutoka ndani (Internal) na kichocheo kutoka nje (External).
Katika kujenga tabia mpya mhusika anaanza kuitikia vichocheo kutoka nje kama
vile picha, linki ya tovuti, barua pepe au alama ya “App” kwenye compyuta au
simu janja. Baada ya mhusika kuitikia vichocheo kutoka nje na kutumia vichocheo
hivyo mara kwa mara vinatafsiriwa kwenye akili yake na hatimaye anajikuta anaitikia
sauti ya ndani (vichocheo vya ndani) inayomtaka kuingia kwenye tovuti au
mtandao wa kijamii husika bila ya utashi wa akili yake.
b) Tendo (Action) – Baada
ya mhusika kuona kichocheo kutoka nje kinachofuata ni kushawishika kuchukua
hatua. Mfano, mtu unapoona linki ya tovuti au barua pepe kwenye simu yako
unashawishika kuifungua ili kuona inahusu nini.
c) Zawadi (Reward) –
Baada ya kufungua link husika na kuvutiwa na kilichomo ndani yake kwa kuwa
kinakidhi hisia zake, mhusika anakuwa na hamu ya kutembelea tovuti husika mara
kwa mara.
d) Uwekezaji – Ili
kukidhi hamu yake kuhusiana na tabia mpya, mhusika sasa anafanya kila awezavyo
kuhakikisha anafanikiwa kupata bidhaa husika kila mara. Mhusika yupo tayari
kuwekeza pesa (mfano kwa ajili ya kununua vifurushi), muda, mtaji wa kijamii au
nguvu za ziada. Hivyo, uwekezaji huu unalenga mhusika kurudia mara kwa mara
mzunguko huu na hatimaye mhusika kushirikisha wenzake kama sehemu ya kufurahi
kile anachofanya. Mfano, kwenye makundi ya kijamii kila mara mtu anapoweka
picha mpya anasubilia mwitikio wa marafiki kuhusu picha hiyo. Hali hiyo
itamfanya kila wakati atake kufungua data ili kuona marafiki wanasema nini
kuhusiana na picha husika.
2. Kampuni
nyingi zinaendelea kunufaika na Teknolojia ya Dunia kuwa Kijiji na zinatumia fursa
hiyo kubadilisha tabia zetu. Ni kutokana na hali hiyo kampuni hizi
zinatengeneza pesa nyingi kwa vile tayari zimeingia kwenye hisia na akili zetu.
Maisha yetu sasa yanaendeshwa na kampuni hizo kana kwamba sisi roboti bila ya
kujitambua kuwa tupo katika hali hiyo. Na kwa vile tayari bidhaa za kampuni
hizo zipo kwenye akili na hisia zetu, kampuni husika haziwekezi nguvu sana
kutangaza bidhaa zake bali sisi wenyewe kwa wenyewe tunatangaza bidhaa za
kampuni hizo bila kujitambua.
3. Bidhaa
zinazotengeneza tabia za watumiaji huwa zinabadilisha tabia za mtumiaji na
matokeo yake zinajiuza zenyewe. Hii ni kutokana na ukweli kwamba baada ya
mtumiaji kubadilika tabia anajikuta kwenye hali ya kuhitaji kutumia bidhaa
husika mara kwa mara katika maisha yake ya kila siku. Kusudi kubwa la
watengenezaji wa bidhaa husika ni kushawishi wateja watumie bidhaa zao, tena na
tena bila ya kuweka jitihada kubwa kwenye matangazo. Hali hii inatokana na
msukumo/kichocheo kutoka ndani mwa watumiaji mara baada ya kubadilisha tabia
zao. Mhusika anajikuta katika hali ya kutumia bidhaa husika kama sehemu ya
kupoteza muda au kusubiri ratiba flani katika majukumu yake ya siku. Mfano, ni
kawaida kukuta mtu yupo kwenye mitandao ya kijamii akiangalia yaliyojiri wakati
akiwa ampenga foleni benki au sehemu nyingine.
4. Bidhaa
zinazobadilisha tabia ya mtumiaji zinazasaidia wamiliki kuendelea kunufaika na
wateja wao kabla ya wateja husika kuhamia kwa wapinzani wa kibiashara. Kwa
maana nyingine ni kwamba mmiliki wa biashara unapofanikiwa kubadilisha tabia za
watumiaji wa bidhaa zako unakuwa umepunguza nguvu za wapinzani wako wa kibiashara
katika soko. Hii ni kutokana na ukweli kwamba baada ya mteja kubadilishwa tabia
ataendelea kuhitaji kutumia bidhaa zako ikilinganishwa bidhaa za wapinzani
wako. Mfano, katika soko kuna soda za Coca cola na Pepsi lakini kuna mteja
ambaye yeye anaamini Pepsi ni bora kuliko Coca kwa vile tu radha Pepsi
ilishabadilisha mfumo wake wa radha.
5. Kadri
wateja wanavyobadilishwa akili na hisia kutokana na matumizi ya bidhaa flani
wanajikuta hawajali tena kuhusu bei ya bidhaa husika. Kumbe, mmiliki wa bidhaa
kazi yake kubwa ni kuhakikisha bidhaa husika inakuwa sehemu ya maisha ya kila
siku kwa watumiaji. Baada ya kufanikiwa kufanya hivyo bidhaa husika inaweza
kuuzwa kwa bei ya juu na watumiaji wataendelea kutumia bidhaa husika bila
kujali badiliko la bei. Mfano, katika kampuni za mawasiliano, watumiaji wengi
wanaweza kuchagua kampuni ya mtandao wa simu wa Voda kwa kigezo tu cha kasi ya
mtandao. Kutokana na kigezo hicho wateja wataendelea kutumia mtandao husika
hata kama bei ya kifurushi itapanda.
6.
Bidhaa inayobadilisha tabia za watumiaji ina nafasi kubwa ya kukua katika soko
na kupendwa zaidi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kadri mteja mmoja
anavyokuwa mlevi/teja (addicted) wa bidhaa husika ndivyo anasambaza sifa za
bidhaa hizo kwa jamii inayomzunguka. Matokeo yake ni kwamba kadri bidhaa husika
inavyohitajika na watu wengi ndivyo inaliteka soko na hivyo kuzalisha faida
kubwa kwa mmiliki wa bidhaa.
7. Kwa
kifupi kama unahitaji kuzalisha bidhaa ambayo unalenga ibadilishe tabia na
hatimaye mazoea ya mtumiaji hakikisha unajibu maswali haya:-
ü Je
mtindo wa biashara yako unahitaji watumiaji wawe na tabia zipi?
ü Je
bidhaa yako unataka itatue matatizo yapi kwa watumiaji watarajiwa?
ü Je
wateja watarajiwa kwa sasa wanatatua vipi matatizo husika na ni kwa namna gani
bidhaa yako itawapatia suluhisho la kudumu?
ü Je
wateja watarajiwa watahitaji kutumia bidhaa yako kwa kiasi gani? Ni mara ngapi
wateja watarajiwa watahitaji kutumia bidhaa yako.
ü Je ni
mazoea yapi ambayo unahitaji wateja watarajiwa wawe nayo kama sehemu ya
kubadilisha tabia zao?
8. Tabia
zinajengwa na mhusika kutokana na mazoea ya kuitikia vichocheo mara kwa mara.
Vichocheo hivi kwa kufahamu au bila kufahamu vinamlazimisha mhusika kuchukua
hatua/kitendo ambayo ni sehemu ya pili katika mzunguko wa kujenga tabia mpya
kwa mhusika. Vichocheo hivi vinagawanyika sehemu mbili ambazo ni vichocheo
kutoka nje na vichocheo vya ndani. Vichocheo vya nje vinaambatana na taarifa
ambazo zinamshawishi mhusika hatua ipi achukue. Mfano, kama umeshika siku
ukasikia mlio wa sms moja kwa moja ubongo unakuelekeza kuwa unatakiwa kusoma
sms husika. Mfano mwingine, kama umezoea soda ya Cocacola katika pita pita zako
mtaani ukiona mtu anakunywa soda moja kwa moja akili na hisia zako zitatamani
kupata soda ya aina hiyo.
9. Vichocheo
vya nje vinagawanyika katika aina kuu nne kama zilivyoelezwa hapa chini. Ukiwa
mfanyabiashara ambaye unatamani bidhaa zako zibadilishe tabia za wateja wako
unatakiwa kuzifahamu hizo na namna ya kuzitumia katika biashara yako kwa ajili
ya kuteka akili na hisia za wateja wako.
ü Vichocheo vilivyolipiwa –
Kundi hili linahusisha matangazo ya biashara ambayo yanalenga kuvuta umakini wa
mtu kuchukua hatua kwenye bidhaa husika. Kundi hili ni muhimu kwa ajili ya
kuvuta wateja lakini linaambatana na gharama kwa mzalishaji wa bidhaa. Hivyo,
mzalishaji makini anatakiwa kulipia tangazo la kwa ajili ya wateja wapya na
kuhakikisha kuwa wateja hao wataendelea kutumia bidhaa zake sambamba na
kukaribisha wateja wapya kupitia matumizi ya bidhaa husika.
ü Vichocheo vinavyotokana kukubalika kwa
bidhaa husika – Vichocheo hivi vinatokana na jina (brand) ya
bidhaa husika au mtu husika kutokana na kukubalika katika vyombo vya usambazaji
wa taarifa. Mfano, tukitumia jina la msanii maarufu yeyote, siyo lazima yeye
alipie gharama ili nyimbo zake zipigwe kwenye vyombo vya mawasiliano.
Mfanyabiashara makini ili kutumia vichocheo vya aina hii unatakiwa kuhakikisha
bidhaa yako inakidhi mahitaji ya wateja ili bidhaa husika ijitangaze yenyewe.
ü Vichocheo vya kimahusiano – Mtu mmoja anamwambia mwenzake ubora
au umuhimu wa bidhaa au huduma husika. Vichocheo hivi vinaweza kuwa kuambiwa
kwa mdomo au kusoma kwenye mitandao ya kijamii au kusikiliza kwenye vyombo vya
habari. Hapa ndipo mfanyabiashara makini anatakiwa alenge zaidi hasa katika
zama hizi za mapinduzi ya teknolojia ya habari. Ni rahisi bidhaa au huduma kukua
kimiujiza (kasi) kama ina sifa za watu kuisambaza wao wenyewe.
ü Vichocheo vinavyomilikiwa – Kundi
hili linahusisha vichocheo ambavyo vinaonekana kwa macho ya watumiaji mara kwa
mara na vinashawishi watumiaji kuchukua hatua. Hivi ni vichochezi vyenye
hatimiliki. Mfano, jengo la biashara au alama ya programu katika simu yako.
pia, vichochezi katika kundi hili vinamtaka mtumiaji kujiunga na huduma husika
kwa ajili ya kupata taarifa za kila mara kupitia barua pepe au mtandao husika.
Mfano mzuri katika kundi hili ni huduma za mitandao ya kijamii kama Facebook, Instangram
au WhatsApp.
10. Aina
ya pili ya Vichocheo ni Vichecheo vya ndani. Aina hii ya vichocheo inatokana na
mhusika kutawaliwa na aina ya kwanza ya vichocheo. Katika hatua hii vichocheo
vya nje vinakuwa moja kwa moja vimeteka akili, mawazo, hisia na mfumo wa fikra
za mhusika kwa ujumla wake. Vichocheo hivi vinamsukuma mhusika kuchukua hatua
bila ya ufahamu wake. Na mara nyingi mhusika anachagua vitendo ambavyo kwake
yeye anachukulia kama tulizo la nafsi pindi anapokuwa kwenye hali ya msongo wa
mawazo, upweke, hasira au uchovu. Mfano, mtu anachagua kunywa pombe kama sehemu
ya kupoteza mawazo, mvutaji sigara anavuta ili kupoza hamu ya sigara au mtu
anakunywa soda aipendayo kama sehemu ya kupoza kiu. Pia, vichocheo vya ndani
vinatumika kama sehemu ya mhusika kuchukua hatua chanya katika maisha. Mfano,
mtu anajihisi maumivu ya mwili moja kwa moja atatamani kutumia dawa ambayo
itamrudisha kwenye hali yake ya kawaida. Hivyo, Mfanyabiashara makini unahitaji
kuhakikisha bidhaa au huduma unayoweka kwenye soko iwe na sifa za kumteka mteja
mtarajiwa kiakili, kihisia na kifikra.
11. Lengo
kubwa la mzalishaji wa bidhaa au mtoa huduma linatakiwa kuwa kuzalisha bidhaa
au huduma ambayo inatatua hitaji la mteja huku ikimfanya mteja aendelee
kuitumia kila mara kama sehemu ya tulizo la nafsi yake. Ili kufanikisha lengo
hilo wazalishaji wa bidhaa au huduma wanatakia kufahamu vichocheo vya ndani vinavyowakabili
wateja wao katika soko. Kwa maana nyingine wanatakiwa kufahamu matatizo ya
wateja ambayo yatatatuliwa na bidhaa au huduma husika. Ili kufanikisha hilo,
mzalishaji wa bidhaa anatakiwa kutambua maumivu au changamoto za wateja kihisia
zaidi kwa maana tatizo husika linaambatana na hisia zipi za wateja watarajiwa
kuliko kujikita kwenye ubora wa bidhaa au huduma pekee.
12. Katika
kuhakikisha kuwa bidhaa au huduma inakuwa na vichocheo kwa wateja watarajiwa,
mfanyabiashara anatakiwa kujibu maswali yafuatayo:-
ü Je
wateja tarajiwa wa bidhaa au huduma yako wana sifa zipi?
ü Je wateja
tarajiwa kwa sasa wanajihusisha na nini? Wana tabia zipi?
ü Ainisha
vichocheo vitatu ambavyo vinaweza kusababisha wateja tarajiwa kuchukua hatua ya
kutumia bidhaa au huduma zako.
ü Ainisha
kichocheo kimojawapo kati ya hivyo ambacho unahisi kitawashawishi zaidi wateja tarajiwa.
ü Tengeneza
uhusiano uliopo kati ya kichocheo cha ndani na tabia unayokusudia wateja tarajiwa
wawe nayo katika mazoea yao ya kila siku.
ü Jiulize
je ni sehemu zipi ambazo ni sahihi kwako kuweka matangazo (vichocheo vya nje)
kiasi ambacho yatawafikia wateja tarajiwa kwa idadi kubwa?
ü Jiulize
ni kwa namna gani unaweza kuunganisha vichocheo vya nje na vichocheo vya ndani
ili mteja tarajiwa abadilike kutokana na vichocheo vya nje.
ü Jiulize
ni njia ipi sahihi ya kumfikia tarajiwa kwa kutumia vichocheo vya ndani (je ni
kwa njia ya barua pepe, TV, Mitandao ya kijamii, au ubunifu wako mpya?)
Haya ni machache ambayo nimekushirikisha
katika sehemu hii ya kwanza ya uchambuzi wa kitabu hiki. Uchambuzi wa kitabu
chote utapatikana kuanzia mwishoni mwa wiki hii (tarehe 5 Januari, 2020) kwa
gharama ya Tshs. 5,000.00. Weka oda yako
sasa. Nakutakia mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu sahii kwa ajili
ya kubadilisha maisha yako.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe: fikrazatajiri@gmail.com
|