Habari ya leo rafiki
na msomaji wa mtandao wa Fikra za Kitajiri. Naamini unaendelea vyema kiafya,
kiroho na kiakili kwa ajili ya kuboresha Dunia hii kuwa mahala pazuri pa
kuishi. Kumbuka kuwa lengo la Dunia kuwa mahala pazuri pa kuishi ni lazima
lianzie katika maisha yako. Ukiwa na maisha mazuri Dunia hii utaiona sehemu
salama pa kuishi na ndivyo ilivyo kwa jamii unayoigusa. Karibu tena katika
makala ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii.
Kama bado hujajiunga
na mfumo wetu wa kupokea makala za uchambuzi wa vitabu, tafadhali fanya hivyo KWA KUBONYEZA HAPA na
kujaza fomu kisha bofya “jiunge/subscribe”. Ni fursa ambayo itakuwezesha kupata
uchambuzi wa vitabu kwa lugha rahisi kupitia barua pepe yako.
Kitabu cha wiki hii ni
“Raising
Great Kids” ambacho kimeandikwa na waandishi Dr. Henry Cloud na Dr. John
Townsend. Wawili hawa wanatumia kitabu hiki kwa ajili ya kutushirikisha
mbinu mbalimbali za malezi wa watoto.
Waandishi hawa wanatushirikisha kuwa linapotajwa
suala zima la malezi ya watoto kwa ujumla mambo manne yanaguswa ambayo ni;
a)
Ustawi
wa Watoto – Kila mzazi anatamani kuona mtoto wake anakuwa vyema
huku akiepuka makucha ya Dunia na kuwa na maadili mema katika maisha yake yote.
b)
Jamii
inayomzunguka mtoto – Makuzi ya mtoto ni matokeo ya jamii
inayomzunguka kuanzia mazingira ya nyumbani, shuleni, majirani,
kanisani/msikitini na hata marafiki zake.
c)
Ustawi
wa wazazi – Mafanikio ya mtoto katika kuwa na malezi bora
ni jawabu la mafanikio ya mzazi hasa kwenye suala zima la kuwa na ndoa bora. Hii
ni kutokana na ukweli kwamba mzazi anaathirika kwa upande chanya au hasi
kutokana na maendeleo ya mtoto wake. Akiwa na maadili mema ni furaha kwa wazazi
na kinyume chake ni sahihi.
d)
Kuhusu
uimara au mafanikio ya dini – Mafanikio katika kuishi
misingi ya dini ni jawabu kuwa watoto wanaishi misingi bora. Hii ni kutokana na
ukweli kwamba maadili ya mtoto yanadhihirisha namna anavyozingatia misingi
mikuu ya dini yake.
Hivyo, kufikia malezi bora waandishi hawa
wanatushirikisha kuwa ni lazima misingi mikuu ya malezi ifuatayo izingatiwe na
kila mzazi:-
a)
Thamani
ya Upendo – Upendo ni msingi mkuu wa mahusiano. Hakuna
namna ambayo mzazi utafakiwa kumlea mwanao kama hauna upendo wa dhati naye.
Kadri watoto wanavyokua wanahitaji kuhisi na kuona kuwa wanapendwa na wazazi
wao. Kumbuka kuwa upendo ndio sheria kuu ya Mungu ambayo inatutaka kupendana
sisi kwa sisi, hivyo, mtoto naye anahitaji hilo lakini pia anatakiwa
kufundishwa umuhimu wa kuwa na upendo.
b)
Thamani
ya Ukweli – Upendo pekee hautoshelezi kwani maisha ndani
ya familia ili yawe yenye mafanikio ni lazima pasiwepo uongo ndani ya
wanafamilia. Watoto wanahitaji kujua umuhimu wa kuwa wakweli na kuambiwa ukweli
katika kipindi cha ukuaji wao.
c)
Nafasi
ya Tabia – Kazi ya malezi ya mzazi kwa mtoto ni jukumu la
muda tu kwani kuna umri ambao mtoto ataanza maisha ya kujitegemea. Katika
kipindi hicho cha kujitegemea ataongozwa na maadili ambayo msingi wake ni
malezi aliyopata kutoka kwa wazazi. Maadili hayo ndizo tabia atakazokuwa nazo katika
kila sekta ya maisha yake.
d)
Uelewa
kuhusu dhambi, matendo ya kitoto na kumjua Mungu. Duni
imejaa uovu wa kila aina na uovu huo unawasubiri watoto wa jinsia zote
kudumbukia katika dhambi hizo. Mzazi ndo wa kumkinga mtoto dhidhi ya makucha
mabaya ya dunia katika kipindi chote cha ukuaji wake. Vivyo hivyo, Dunia imejaa
mema ambayo Mungu anakusudia kila kiumbe kilichoumbwa kipate kuyafurahia. Mzazi
wajibu wako ni kumuandaa mtoto wako aangukie kwenye mema ya Dunia katika
kipindi cha maisha yake. Tunaamini kuwa kila mtoto ameumbwa kwa sura ya
Mwenyezi Mungu, hivyo mzazi una wajibu wa kuhakikisha sura hiyo haipotei katika
maisha ya mwanao katika kipindi cha ukuaji wake.
e)
Thamani
ya Uhuru – Wapo wazazi wanaoamini katika kuwadhibiti
watoto kwa kufungia ndani na wapo ambao wanaamini katika kuwapa uhuru watoto
wao. Jambo la muhimu ni kutambua kuwa kama mzazi unatakiwa kuwapa misingi wanao
ambayo itawawezesha kujidhibiti wenyewe na maisha yao kwa ujumla.
f)
Umuhimu
wa uwepo wa Mwenyezi Mungu katika maisha yao – Mtoto
anapaswa kumjua Mungu, kumuheshimu, kumpenda, kuogopa kwenda kinyume na matakwa
yake na hata kuishi amri zake katika maisha yake ya kila siku. Mzazi huo ni
wajibu wako wa kuhakikisha mtoto anakua kiroho kadri anavyokua kimwili.
g)
Malezi ni Mchakato – Mchakato
wa malezi unaanzia tangu pale mimba inapotungwa na kuendelea katika kipindi cha
miaka kadhaa katika ukuaji wa mtoto. Pia, mzazi unatakiwa kutambua kuwa malezi
yanabadilika mara kwa mara kulingana na ukuaji wa mtoto.
Karibu ushirikiane nami kujifunza machache
kati ya mengi ambayo tunashirikishwa katika kitabu hiki:
SEHEMU
YA KWANZA: KUMKUZA MTOTO MWENYE MAADILI
1. Kila
mzazi anataka kuwa na mtoto mwenye maadili mema hata hivyo ni wazazi wachache
ambao wanasaidia watoto kupata maadili hayo. Waandishi wanatushirikisha kuwa
wajibu mkubwa wa kuitwa mzazi ni kuhakikisha unawasaidia watoto wako wawe na
maadili mema, tabia njema au wawe watoto wema kwa ujumla wake. Wajibu
unaambatana na majukumu ambayo wewe mzazi unatakiwa kuyatimiza katika kila muda
unaokuwa na watoto wako. Majukumu ya kuwa mlezi ni pamoja na kuhakikisha mtoto
anafundishwa misingi ya kiroho, tamaduni, upendo kwa jamii inayomzunguka na
viumbe vinavyomzunguka, umuhimu wa kufanya kazi sambamba na kufahamu wajibu
wake kama mtoto.
2. Kila
mzazi anatamani kumuona mtoto wake akikua kutoka hatua moja hadi nyingine
katika kila sekta ya maisha yake. Shuleni anatamani kuona mtoto anatoka hatua
moja hadi nyingine kimasomo. Kazini anatamani kuona mtoto wake anatoka nafasi
moja hadi nyingine. Vivyo hivyo, katika mahusiano kila mzazi anatamani kuona
mtoto wake akiwa na mahusiano yanaozalisha ndoa bora. Ndivyo ilivyo kwenye
sekta ya kiroho, kiuchumi, kitabia na kwenye urafiki na wenzake. Kwa bahati
mbaya sio watoto wote wanakua kulingana na mategemeo ya wazazi. Hapa ndipo kila
mzazi anaona kuwa alitimiza wajibu wake na mengine yaliyobakia ilikuwa nafasi
ya mtoto mwenyewe. Hata hivyo, mzazi analaumiwa na jamii kuwa hakutimiza wajibu
wake. Waandishi wanatushirikisha kuwa wajibu ni kwa wote kwa maana mzazi na
mtoto lakini mzazi ndo anatangulia kwanza na baadae mtoto anafuata.
3. Lengo
kubwa la mzazi katika malezi kwa watoto ni kuwa na watoto wenye maadili au
tabia njema. Tabia njema zinaambatana na uhuru wa mtoto katika yale anayofanya,
uwezo wa kujiamini, uwezo wa kutatua changamoto zinazomkabili, uwezo wa
kujitegemea kwa kutimiza wajibu wake katika kazi, uadilifu, maadili mema na
kuishi misingi ya kiroho. Kwa ujumla tabia ni ule uwezo wa namna ya kutumia
vipaji vyetu kulingana na matakwa ya Muumba wetu. Na ni katika kipindi cha
utoto ndipo mzazi unatakiwa kujenga misingi ya tabia njema kwa mtoto wako. Hapa
ndipo jukumu kubwa la mzazi lilipo, kuhakikisha anamjengea misingi bora mtoto
wake ili misingi hiyo izae tabia tabia njema katika maisha yake ya baadae.
4. Katika
hatua za malezi ya mtoto, mzazi anatakiwa kuhusisha mbinu mbili za za kulea
ambazo ni (a) kunfundisha ujuzi na maarifa muhimu kwa mtoto na (b) kutumia
uzoefu wa vitendo. Mwandishi anatushirikisha kuwa ili mtoto awe na misingi bora
ya tabia njema ni lazima ashirikishwe kwenye majukumu mbalimbali ambayo
yanamjenga kujifunza kwa vitendo. Ukweli ni kwamba ni rahisi kujifunza kwa vitendo
kuliko kutumia nadharia. Mfano, hauwezi kuendesha baiskeli kwa kutegemea kusoma
mbinu za kuendesha baiskeli kwenye kitabu badala yake ni lazima ujifunze kwa
vitendo ambavyo vitahusisha kuanguka hadi pale ambapo utaweza kuendesha kwa
ufasaha. Vivyo hivyo, tabia njema katika mtoto kwenye kila sekta ya maisha yake
zinajengwa kwa kumhusisha mtoto kupitia vitendo katika maisha ya kila siku
ndani ya familia. Mfano, kwa kutaja tu baadhi mtoto anatakiwa kushiriki kwa
vitendo katika kufanya kazi za nyumbani, kazi za kujenga uchumi, matendo ya
huruma na matendo ya kiroho.
5. Kadri
mtoto anavyokua ni lazima ufundishwe kuwa na NEEMA ndani mwake. Waandishi
wanatushirikisha kuwa neno neema linatafsiriwa “kuwa tayari kwa wengine”. Neno
hili linajumuisha matendo kama vile: Upole, huruma, msamaha, fadhira, shukrani,
uelewa, utoaji, upendo na msahada. Haya yote ni lazima mtoto afundishwe katika
kila hatua za ukuaji wake. Mzazi hapa lengo lako ni kutaka mwanao atambue kuwa
maisha yake si kwa ajili yake tu bali ni kwa ajili ya jamii inayomzunguka.
Tafsri pana ni kwamba mtoto anatakiwa kufahamu kuwa maisha yanategemeana.
6. Pia
mtoto ni lazima afundishwe kuwa tabia njema zinahusisha kuwa mkweli katika
maisha yake. Waandishi wanatushirikisha kuwa neno ukweli linatafsiriwa kama
kuwa mwaminifu dhidi ya nafsi yako na mwenye kuaminiwa na jamii inayokuzunguka.
Kwa tafsiri pana ni kwamba mtoto anatakiwa kufahamu mipaka yake katika kile
anachofanya au matamanio yake. Kutokana na tafsiri hiyo, ukweli katika maisha
unajumuhisha: maadili mema, matarajio, maamuzi, hukumu dhidi ya wengine, tabia,
nidhamu, uadilifu na uaminifu. Mtoto anatakiwa kutambua umuhimu tabia zote hizo
katika maisha yake akiwa mtoto na hata katika kipindi cha utu uzima.
7. Changamoto
kubwa kwa mzazi ni namna gania atawezesha kumpa mtoto matendo ya neema na
ukweli kwa wakati mmoja. Matendo haya ni muhimu kwa kuwa kila linapotajwa neno
malezi ni lazima lihusishwe na upendo kwa watoto (matendo ya faraja/neema)
sambamba na mipaka kwa watoto (ukweli). Mfano, ni kawaida mtoto mara zote
anathamini kucheza kuliko kitu chochote katika maisha yake. Kama mzazi haupaswi
kumkatisha tamaa mwanao kwenye michezo anayopendelea zaidi lakini pia haupaswi
kusahau kuwa mtoto anatakiwa kutimiza majukumu yake mengine ya kila siku. Hivyo,
huna budi kutumia sentensi ambazo zinamtia moyo na kumhamasisha kwanza kutimiza
jukumu husika kabla ya kwenda kucheza. Mfano, tumia sentensi kama “natambua
kuwa unahitaji kwenda kucheza na ni vigumu kusubiria lakini nahitaji kwanza
ukamilishe “home work” uliyopewa shuleni au ukamilishe kwanza kazi hii….”.
8. Tabia
au matendo yoyote ambayo unataka mwanao awe nayo ni lazima utumie muda mwingi
kumfundisha, kumsahihisha, kumhamasisha, kumpa changamoto na hata kumkanya. Kama
mzazi/mlezi huna budi kutenga muda kila siku kwa ajili ya kuhakikisha mwanao
anafundishwa kile ambacho unatamani awe nacho katika maisha yake ya baadae.
Pia, unatakiwa kutafuta watu maalum wa kumfundisha mwanao ujuzi/maarifa ambayo
yapo nje ya uwezo wako. Mfano, kama ana kipaji cha kuimba tafuta watu ambao
watamsaidia kukuza kipaji hicho kadri anavyokua kiumri. Vivyo hivyo, kama ni
mpenzi wa michezo, hakikisha anapata mwongozo sahihi wa kukuza kipaji chake
katika mchezo husika.
9. Ukuaji
wa mtoto ni sawa na mti. Mti baada ya kupandwa ni lazima umwagiliwe au
kupaliliwa pamoja na kuhakikisha matawi yasiyofaa yanaondolewa ili kubaki
matawi bora. Hata hivyo, unaweza kupanda mti na husifanye chochote na mti huo
utaendelea kukua tu na mwisho wake hautapata kile ulichotamani. Ndivyo ilivyo
kwa mtoto, ukuaji ni lazima uendelee bila kuzingatia kuwa anajengewa tabia
zipi. Waandishi wa kitabu wanashauri kuwa mzazi/mlezi una wajibu wa kuhakikisha
una muda wa kutosha kwa ajili ya kuwa karibu na watoto na hata pale ambapo
haupo ni lazima ufuatilie tabia zao. Lengo ni kuhakikisha kuwa tabia mbaya
zinadhibitiwa katika kipindi cha ukuaji wa mtoto. Hii ni kutokana na ukweli
kwamba katika hatua za ukuaji watoto wanajifunza mengi kutoka kwenye Dunia
inayowazunguka. Kumbuka kuwa Dunia hiyo ndo imejaa mabaya na mazuri.
10. Katika
hatua za ukuaji hakikisha mtoto anajenga uwezo katika: namna kukamilisha au
kueleza mahitaji; kukabiliana na madhaifu yake; kukabiliana na hatari za
maisha; kudhibiti maumivu ya kimaisha; kukabiliana na huzuni katika maisha;
kudhibiti hasira; uwezo wa kutoa maoni au kujieleza; kukuza kipaji chake;
kujiamini na uwezo wa mahusiano kijinsia. Ukiangalia vipengele vyote hivyo
vinalenga kumjenga mtoto katika kukuza uwezo wake kwenye mahusiano na jamii ya
watu wanaomzunguka. Kwa kifupi mzazi una nafasi kubwa ya kumjenga mtoto ili
katika maisha yake ya baadae awe mtu wa kujiamini na kujitegemea. Na hauwezi
kufanikisha lengo hilo kama hauna muda wa kutosha wa kuwa karibu na mtoto wako.
11. Chochote
unachomfundisha mtoto wako unatakiwa kutambua kuwa inachukua muda hadi mtoto
aelewe na kuweka yale anayofundishwa kwenye mfumo wa kumbukumbu zake. Husitegemee
kuwa kile unachomfundisha mtoto atakielewa hapo hapo na kuanza kukitekeleza
katika maisha yake. Hapa ndipo wazazi/walezi wengi wanapokosea na matokeo yake
wanatumia adhabu za mara kwa mara kwa watoto. Hali hii inapelekea watoto
wanakuwa na uoga au wasiwasi wakati wa kujifunza. Kumbe, mzazi/mlezi unatakiwa
kutambua kuwa mtoto kujifunza ni mchakato ambao unahusisha hatua 5 ambazo ni:
ü Mfundishe
mtoto kuhusu ukweli au kile ambacho unataka awe nacho – watoto hawaelewi
chochote hivyo wanatakiwa kufundishwa kuhusu kanuni, mila, wazo au tabia;
ü Wape
muda wa kuvuka mipaka au ukomo wa uwezo wao kuhusu tabia husika – Mtoto
anapofundishwa kitu kipya katika maisha yake hawezi kukitekeleza kwa ufasaha
hivyo ni lazima apewe muda wa kujifunza kutokana na makosa;
ü Msaidie
mtoto kubadilisha makosa yake ili yaendane na kile alichofundishwa – mtoto
anapokosea kutimiza alichofundishwa kuna hisia zinajengeka katika akili yake.
Mzazi wajibu wako ni kutumia sentensi zenye upendo ndani yake ili aondokane na
hisia hizo na hatimaye hamasa ya kujifunza iendelee;
ü Msaidie
mtoto kutambua ukweli katika kile anachojifunza – baada ya mtoto kuhamasishwa
sasa mzazi/mlezi unatakiwa kumsaidia katika hatua za kujifunza maarifa mapya au
tabia kwa kuwa karibu nae ili utambue sehemu anazokwama na mwisho umrekebishe;
na
ü Mhamasishe
mtoto kurudia tena vitendo vinavyoendana na kile alicofundishwa – mtoto
anavyorudia mara kwa mara inamsaidia tabia husika kuwa sehemu ya maisha yake.
Haya ni machache niliyojifunza kutoka katika sehemu ya kwanza ya kitabu hiki. Kupata nakala ya uchambuzi wa kitabu hiki lipia Tshs. 10,000 na utatumiwa nakala tete kwa njia ya barua pepe. Kama bado haujajiunga na Mtandao wa huu, jiunge kwa KUBONYEZA HAPA.
Tuma pesa yako kwa njia ya M-pesa au Airtel Money kupitia namba zifuatazo:-
M – Pesa tumia namba: 0763 745 451 (Augustine Mathias Mugenyi)
Airtel Money tumia namba: 0786 881 155 (Augustine Mathias Mugenyi)
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe: fikrazatajiri@gmail.com
|