Habari ya leo rafiki
na msomaji wa mtandao wa Fikra za Kitajiri. Karibu tena katika kitabu chetu cha
pili katika kipindi cha mwaka 2020 kati ya vitabu 30 ambavyo nimepanda kuvisoma
na kukushirikisha uchambuzi wake.
Pia katika kipindi
hiki, mtandao wa Fikra za Kitajiri umedhamiria kuunganisha wafamilia wake kwa
kuanzisha kundi la WhatsApp ambalo litatumika kama darasa la kujifunza maarifa
mbalimbali yanayolenga kuboresha maisha yetu. Kupata fursa hii ya kuwa sehemu
ya kundi hili nitumie ujumbe kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com na utaunganishwa na kundi hili ndani ya muda wa kipindi
cha wiki mbili kuanzia sasa.
Bado naendelea
kukumbusha kuwa, Lengo letu kubwa mwaka 2020 ni kuendelea kuweka bidii kwa
kadri ya uwezo wetu kwa ajili ya kuifanya Dunia kuwa mahala pazuri pa kuishi. Kumbuka
ili Dunia iwe mahala pazuri pa kuishi ni lazima lianzie katika maisha yako.
Ukiwa na maisha mazuri Dunia hii utaiona sehemu salama pa kuishi na ndivyo
ilivyo kwa jamii unayoigusa. Karibu tena katika makala ya uchambuzi wa kitabu
cha wiki hii.
Kama bado hujajiunga
na mfumo wetu wa kupokea makala za uchambuzi wa vitabu, tafadhali fanya hivyo KWA KUBONYEZA HAPA na kujaza
fomu kisha bofya “jiunge/subscribe”. Ni fursa ambayo itakuwezesha kupata
uchambuzi wa vitabu kwa lugha rahisi kupitia barua pepe yako.
Kitabu cha pili katika
mwaka huu ni “Sale Like Crazy” ambacho kimeandikwa na mwandishi Sabri Suby. Sabri Suby ni mwanzilishi
na mmiliki wa kampuni ya King Kong nchini Australia. King Kong ni Wakala wa
Masoko ya Mtandao (Digital Marketing Agency) ambayo katika kipindi cha miaka
minne iliweza kutengeneza dolla za kimarekani (USD) milioni 4 (zaidi ya bilioni
nane).
UTANGULIZI: KWA NINI MAARIFA YALIYOMO NDANI YA KITABU HIKI
NI MUHIMU KATIKA NYAKATI ZA SASA
Mwandishi
anatushirikisha kuwa tafiti zinaonesha kuwa asilimia 96 ya biashara zote huwa
zinakufa kabla ya kutimiza miaka kumi toka kuanzishwa kwake. Kati ya hizo,
takribani asilimia 80 huwa zinakufa ndani ya miaka miwili toka kuanzishwa
kwake. Hata hivyo, asilimia 4 ya biashara ambazo zinaweza kumudu kuendelea
baada ya miaka 10 haimaanisha kuwa zinafanya vizuri katika kutengeneza faida
kwa wamiliki.
Mwandishi anatushirikisha kuwa biashara nyingi
zinashindwa kukua zaidi ya miaka kumi kutokana na wamilikiwa kushindwa kutumia
mbinu sahihi za kuiendeleza biashara husika. Mbinu namba moja ni kuhakikisha
biashara inajiendesha kwa faida kwa maana uwezo wa wa biashara kuendelea kuzalisha
mapato. Kwa maneno rahisi, biashara iwe na uwezo wa kuzalisha fedha za kutosha katika
hali ambayo itawezesha uendelevu na ukuaji wa biashara. Hii ni kutokana na
ukweli kwamba fedha zinazozalishwa na biashara ndo uhai, hewa au chakula cha
biashara husika kuendelea kukua zaidi.
Biashara nyingi zinakufa katika kipindi cha
awali toka kuanzishwa kwake kwa kuwa waanzilishi wengi wa biashara wanakuwa
hawana elimu ya misingi ya bisashara. Mfano, biashara nyingi zinaanzishwa
kutokana ujuzi wa mwanzilishi wa biashara katika biashara anayoanzisha. Kwa
maana, Mpishi anaamua kuanzisha mgahawa, Mwanasheria anaanzisha Kampuni ya
huduma za kisheria au daktari anaanzisha biashara ya huduma za afya. Kubwa, ni
kwamba waanzilishi wote hao hawana misingi ya kuendesha biashara husika na
matokeo yake ni kwamba biashara zinakufa au zinadumaa.
Kutokana na waanzilishi wengi kushindwa kuwa
na misingi sahihi ya biashara wanajikuta biashara zinakuwa ni kazi ya mmiliki
(job) badala ya kuwa sehemu ya kuzalisha fedha kwa mmiliki wakati huo huo
ikimpunguzia muda wa kufanya kazi. Mfano, biashara nyingi katika jamii ni zile
ambazo mmiliki hawezi kutoka kwenye biashara kila siku na hivyo kufanya hivyo
anakuwa ni mtumwa wa biashara husika.
Katika kitabu hiki mwandishi anashirikisha
mfumo halisi wa mauzo ambao yeye binafsi ameutumia kukuza biashara nyingi
kutoka kwenye biashara za kawaida hadi kwenye za mabilioni. Mbinu hizi
amezitumia kusaidia wafanyabiashara wengi kuepukana na karaha ya kufanya kazi
zaidi masaa 80 kwa wiki hadi 32 huku wakiwa hawana msongo wa mawazo wa kupata
wateja wapya. Hali hii imewawezesha wamiliki wa biashara hizo kuwa na biashara
ambazo wanaweza kutengeneza zaidi ya asilimia 700% ikilinganishwa na kiasi cha
fedha walichokuwa wanatengeneza awali katika biashara husika.
Karibu ushirikiane nami kujifunza machache
kati ya mengi ambayo tunashirikishwa katika kitabu hiki:
1. Kama
unahitaji kuwa bilionea huna budi kuhakikisha unakuwa na fikra/mawazo za
kibilionea. Tena unatakiwa na fikra za bilionea ambaye unatafuta utajiri
mwenyewe na si kutegemea hela za kurithi au bahati na sibu. Unahitaji kufahamu
namna ambavyo mabilionea namna ambavyo wanafanya maamuzi yao kuhusiana na
maisha ya kawaida pamoja na maamuzi ya kibiashara. Kwa kifupi, unatakiwa
kufahamu sehemu ambazo mabilionea wanawekeza muda na rasilimali
zao.
Mwandishi anatushirikisha kuwa baada kufanya
tafiti kwa muda mrefu kuhusiana na maisha ya watu wenye mafanikio ya kifedha
amegundua kuwa, watu hawa wanawekeza sana kwenye vitu ambavyo vina mrejesho
chanya (positive return). Watu hawa wanajali sana rasilimali ambazo hazirejereshwi
(non-renewable resource) kuliko kitu chochote. Kwa kifupi, wanajali sana muda
wao na wanautumia kwenye kazi ambazo zinazalisha kipato zaidi. Moja, ya sababu
ambazo zinapoteza muda ni kukua kwa teknolojia ya habari ambayo inawafanya watu
kila baada ya dakika kadhaa watamani kufungua simu au kompyuta zao kujua
kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii au kwenye barua pepe. Matajiri wengi
hawatumi mitandao kijamii au barua pepe kwa hasara badala yake wanaitumia kwa
ajili ya kutengeneza pesa zaidi.
2. Maisha
yetu yamejaa usumbufu wa kila aina na ni usumbufu huo ambao unawafanya watu
wengi kuwa bize muda wote. Kumbe, ili kuwa bilionea unahitaji kujiepusha kazi
ambazo zinakupotezea mtiririko wa fikra na kujikita kwenye kazi muhimu pekee. Pia,
biashara ili ikue zaidi unatakiwa uwe na timu kubwa kwa maana ya kupanua wigo
wa biashara kutoka kwenye kufanywa na mtu mmoja (mmiliki) kwa kufungua matawi
zaidi. Uwezo wa kuuza bidhaa/huduma yako ndio unaamua ukuaji wa bidhaa/huduma
husika. Hivyo, ukuaji wa biashara yako utategemea na uwezo wako wa kutafuta
masoko kwa ajili ya wateja wapya. Kubwa kuliko, biashara yako inatakiwa kuwa na
mfumo ambao utawezesha biashara kukua kwa haraka katika kipindi cha muda mfupi.
Kwa kutaja tu baadhi sifa za mfumo huo ni kama:
ü Wateja
wanapaswa kukimbilia bidhaa/huduma zako na sio wewe kuwakimbilia;
ü Uwe
na utabiri na uthabiti ambao unatoa fursa mpya, wateja wapya na mapato zaidi;
ü Unaongea
na wateja watarajiwa wengi zaidi kuliko wezo wako wa kuwahudumia. Maana yake ni
kwamba mahitaji ya bidhaa/huduma zako ni wa kiwango cha juu;
ü Uwepo
wa mfumo wa moja kwa moja ambao unawezesha upatikanaji wa wateja wapya kwa
kutumia nguvu kidogo zaidi; na
ü Una
una muda wa kutosha kwa ajili ya kufanya kazi muhimu pekee ambazo zinakuwezesha
kutengeneza kipato zaidi.
3. Sifa
kubwa ambayo mfanyabiashara yeyote anatakiwa kuwa nayo ni kutambua kuwa bidhaa/huduma
yake ni kwa ajili ya kutatua matatizo ya wateja. Tafsiri yake ni kwamba
fedha zinatengenezwa kwa kuwa na uwezo wa kumshawishi mteja atambue thamani ya
bidhaa/huduma zako katika kutatua changamoto zake. Kumbe, ili kutengeneza pesa
zaidi unatakiwa kutambua maumivu, hamu, hofu, tumaini na hitaji la mteja wako
katika kutumia bidhaa/huduma zako. Pale unapokidhi hitaji la mteja moja kwa
moja bei ya bidhaa zako inakuwa sio changamoto tena kwa kuwa wateja wapo tayari
kulipia gharama yoyote endapo wana uhakika wa kupata kile wanachotaka.
4. Hakikisha
unafahamu kanuni ya Vilfredo Pareto ya 80/20% na namna ya kuitumia katika
biashara yako. Pareto aligundua kuwa 80% ya uchumi wa nchi
upo mikononi mwa 20% ya idadi ya watu. Pareto aligundua pia kuwa kanuni hii
inafanya kazi katika sehemu nyingi za maisha ya mwanadamu. Mfano, asilimia ya
20 ya pembejeo inazalisha 80% ya mazao; 20% pekee ya wafanyakazi wanazalisha
80% ya matokeo; 20% ya wateja wanaleta 80% ya mapato na zaidi na zaidi. Kwa
ujumla unatakiwa kufahamu kuwa katika biashara 20% ya kazi zinazohusiana na
biashara inazalisha 80% ya matokeo yote. Kumbe, mmiliki makini wa biashara
unatakiwa kujikita kwenye 20% ya kazi ambazo zinaingiza pato la 80% ya biashara
yote. Asilimia 80 ya kazi zinazobakia inabidi uamue kutafuta watu wa kuifanya
kwa ajili yako. Unachotakiwa kufanya kama mmiliki wa biashara ni kuanisha kazi
ambazo zinaingiza pato kubwa kwenye biashara na kujikita kwenye usimamizi wa kazi
hizo kwa ufasaha.
5. Thamani
ya muda wako inapatikana kwa kugawanya kiwango unacholipya dhidi ya idadi ya
masaa unayofanya kazi. Mfano, kama kwa wiki unafanya kazi masaa 40
na unaingiza 1,000,000.00; thamani ya muda wako kwa saa ni 25,000.00. Hivyo,
ili kuongeza thamani ya muda wako unatakiwa kuangalia ni kazi zipi ambazo
unaweza kuzipunguza ili zifanywe na wasaidizi wako. Kwa kufanya hivyo utakuwa
umepunguza masaa ya kazi na kuongeza pato lako kwa wiki.
6. Mmiliki
wa biashara jukumu lako namba moja ni kuhakikisha unakuza mauzo ya
bidhaa/huduma. Hivyo, muda, nguvu na umakini wako unatakiwa kuuwekeza sana
kwenye usimamizi wa mauzo kuliko kitu chochote kile. Unatakiwa kuwa mbobevu wa
mauzo ya bidhaa yako kuliko mtu yoyote yule ambaye unafanya nae kazi. Hakikisha
unawekeza muda wako kwenye shughuli ambazo zinahusiana na mauzo ya
bidhaa/huduma. Hata hivyo, hii hainamanishi kuwa kazi zote zinazohusiana na
mauzo ufanye mwenyewe bali lengo ni kukupa angalizo la kuhakikisha chochote
kinachofanyika kuhusiana na mauzo unakuwa na uelewa wa kutosha.
7. Tambua
kuwa mbobevu katika mauzo haina uhusiano na kiwango cha elimu, historia yako au
kalama ulizonazo. Kuuza ni sanaa na sayansi ambayo kila mtu anaweza kujifunza
na kufanikiwa kwa kiwango kikubwa. Mwandishi anatushirikisha kuwa ili ufanikiwe
kuwa muuzaji bora kwanza unatakiwa kuishinda sauti yako ya ndani ambayo imekuwa
ikikuambia kuwa hauwezi. Muhimu, unahitaji kujidhibiti wewe mwenyewe kuliko
unavyotakiwa kuwadhibiti wengine. Nidhamu binafsi katika safari ya kuwa muuzaji
bora ni nyenzo muhimu ambayo itakutofautisha na washindani wako kwenye soko. Hii
ni kutokana na ukweli kwamba nidhamu hiyo ndiyo itakusukuma: kuamka mapema kila
siku, kuwa na bidii ya kazi, kuepuka mambo yasiyo ya muhimu katika maisha yako
na kuwa na nidhamu kwenye matumizi ya pesa. Mwandishi anatushirikisha kuwa, ili
ufanikiwe katika hilo unatakiwa uwe na wigo mkubwa wa sababu zinazokusukuma
kufanikiwa kimauzo.
8. Siri
kubwa ya kufanikiwa ni kimauzo ni kuhakikisha unatangaza namna ambavyo
bidhaa/huduma zako zitamnufaisha mteja tarajiwa. Mwandishi
anatushirikisha kuwa watu hawajari ubora wa bidhaa au uimara wa kampuni yako
pale ambao unawaelezea juu ya bidhaa/huduma zako kwa mara ya kwanza. Watu
wanahitaji kusikia kutoka kwako namna ambavyo bidhaa/huduma zako zitawasaidia
kutatua matatizo/changamoto walizonazo. Kumbe, ili ufanikiwe kimauzo
haupaswi kutangaza bidhaa bali tangaza namna ambavyo unatatua changamoto za
wateja kupitia bidhaa/huduma unazotoa. Pia, badala ya kuuza mlango kwa
mlango au mtu kwa mtu ili ufanikiwe kimauzo siri nyingine ni kwamba
unatakiwa kuwa na uwezo wa kuandika matangazo ambayo yatavuta wateja wa
bidhaa/huduma zako. Uwezo wa kuandaa ujumbe wa bidhaa/huduma
zako na jinsi zinavyosaidia wateja kutatua changamoto zao ni sifa ya kipekee
katika kufanikisha mauzo. Matangazo/ujumbe wako unatakiwa uwe na sifa za kuvuta
wateja wapya sambamba na uwezo kufanikisha mauzo masaa yote katika masaa 24 ya
siku katika siku 7 za wiki. Hapa, sasa unakuwa umetengeneza mfumo wa moja kwa
moja wa kufanikisha mauzo ya bidhaa/huduma zako.
9. Wekeza
kwenye matangazo ya kulipia sawa na ilivyo uwekezaji wa hisa, dhamana au nyumba
za biashara. Mwandishi
anatushirikisha kuwa kama wewe ni muuzaji na unategemea kuongeza mauzo bila ya
kuwekeza kwenye matangazo hakika unajidanganya. Mwandishi anatushirikisha kuwa
katika teknolojia ya sasa ili upate jamu (wingi wa watu) wanaofuatilia bidhaa/huduma
zako ni lazima uwe tayari kununua jamu hiyo. Wingi wa watu unanunuliwa sawa na
ilivyo kwenye manunuzi ya bidhaa nyinginezo unazonunua ‘super market’. Na sehemu ambazo mwandishi anatushirikisha kuwa
bidhaa/huduma yako inaweza kufikia wateja tarajiwa zaidi ya mamilioni ndani ya
muda mfupi ni kupitia ukurasa wa Kijamii wa Facebook na Mtandao wa Google. Muuzaji
makini ni lazima uhakikishe unawekeza fedha nyingi kwenye matangazo ya facebook
na Google ili kupata wateja wapya wa bidhaa/huduma zako.
Haya ndio machache ambayo nimekushirikisha katika sehemu ya utangulizi wa kitabu. Husikose nakala yako yenye uchambuzi wa kitabu kizima jumapili ya wiki ijayo. Nakala nzima itapatikana kwa Tshs. 10,000/= tu.
|