Habari ya leo rafiki
na msomaji wa mtandao wa Fikra za Kitajiri. Naamini unaendelea vyema kiafya,
kiroho na kiakili kwa ajili ya kuboresha Dunia hii kuwa mahala pazuri pa
kuishi. Kumbuka kuwa lengo la Dunia kuwa mahala pazuri pa kuishi ni lazima
lianzie katika maisha yako. Ukiwa na maisha mazuri Dunia hii utaiona sehemu salama pa
kuishi na ndivyo ilivyo kwa jamii unayoigusa. Karibu tena katika makala ya
uchambuzi wa kitabu cha wiki hii.
Kama bado hujajiunga
na mfumo wetu wa kupokea makala za uchambuzi wa vitabu, tafadhali fanya hivyo KWA KUBONYEZA HAPA na
kujaza fomu kisha bofya “jiunge/subscribe”. Ni fursa ambayo itakuwezesha kupata
uchambuzi wa vitabu kwa lugha rahisi kupitia barua pepe yako.
Kitabu cha wiki hii ni
“How
to Get Rich - Jinsi ya kuwa Tajiri”
ambacho kimeandikwa na tajiri nguri na mwanasiasa Donald J. Trump. Linapotajwa jina la Trump naamini hakuna haja ya
kumuelezea ni nani kutokana na mafanikio ambayo amepata katika ulimwengu wa
utajiri sambamba na mafanikio ya kisiasa. Kwa yule ambaye hamjui basi naomba
atambue kuwa kitabu cha leo kiliandikwa na Rais wa Marekani ambaye hadi sasa
yupo madarakani. Pia, naomba atambue kuwa kitabu hiki kimeandikwa na tajiri
mkubwa katika ardhi ya Marekani na Dunia nzima kwa ujumla.
Mwandishi anatushirikisha kuwa aliamua kitabu
hiki kukipa jina hilo kwa kuwa hilo ndilo swali ambalo amekuwa akiulizwa mara
nyingi. Kuwa anaulizwa swali hilo mara kwa mara kwa kuwa yeye ni bilionea. Kwa maana,
mtengeneza mikate ataulizwa namna ya kutengeneza mkate na tajiri anaulizwa
namna ya kutengeneza pesa hadi kufikia utajiri.
Karibu ushirikiane nami kujifunza machache
kati ya mengi ambayo tunashirikishwa katika kitabu hiki:
1. Kufanikiwa
kibiashara ni lazima ufahamu mambo mengi. Mwandishi anatushirikisha kuwa
mafanikio ya kibiashara ni lazima ufanye kazi na watu wa kila aina, taaluma/uzoefu
tofauti au umri tofauti. Ili ufanikiwe kupata kile unachohitaji kutoka kwao
huku ukitimiza matakwa yao ni lazima uwe na uelewa wa mambo mengi. Ukiwa mtendaji
mkuu unatakiwa katika kila kitengo cha biashara ufahamu vitu muhimu ambavyo
vinatekelezwa na kitengo husika. Ili ufanikishe adhima hiyo ni lazima ufanye
kazi kama Jenelali wa Jeshi, kwa maana kila maamuzi unayofanya yana umuhimu
kwako na watu unaofanya nao kazi.
2. Kadri
unavyokua kibiashara hakikisha unajenga timu ya ushindi kuputia watua
unaowaajiri. Mwandishi anatushirikisha kuwa unapokuwa tajiri unakuwa na miradi
mikubwa ambayo ili iendeshwe kwa faida ni lazima uwe na wafanyakazi bora
kitaaluma na kiutendaji. Wanyakazi hawa ni lazima wakurahisishie usimamizi wa
miradi kwa kuwa hauwezi kusimamia kila mradi kutokana na wingi wa miradi
uliyonayo. Ukiwa na wafanyakazi bora utakuwa na usimamizi au uendeshaji mzuri
na vivyo hivyo ukiwa na usimamizi mzuri utakuwa na wafanyakazi bora. Kanuni ya
kujifunza hapa ni kwamba “fanya kazi na mwajiriwa ambaye anatambua wajibu wake
na hakikisha unamtimizia matakwa yake”.
3. Hakikisha
husibweteke kutokana na mafanikio unayopata kiasi cha kupoteza dira ya picha
kubwa ya mafanikio. Mwandishi anatushirikisha namna ambavyo alipoteza dira
baada ya kufanikiwa kiuwekezaji. Matumizi katika vitu vidogo vidogo au starehe
za hapa na pale ni chanzo kikubwa kwa watu kupoteza dira ya mafanikio. Hivyo,
kadri unavyokuwa kibiashara unatakiwa kuendelea kuishi misingi ya maisha ambayo
ulijiwekea awali. Kwa maana nyingine unatakiwa kabla ya kuwa tajiri uwe na
mpango wa namna utakavyokuza utajiri wako na kuainisha utajiri huo utautumia
kufanikisha au kutekeleza yapi katika maisha yako.
4. Hakikisha
haupotezi kasi kadri unavyofanikiwa kibiashara. Mwandishi anatushirikisha kuwa
watu wengi wanashindwa kufikia kwenye kilele cha mafanikio kwa kuwa wanapoteza
kasi njiani. Na wengi wanapoteza kasi kwa kuwa wanaridhika na mafanikio
wanayopata na hivyo wanapunguza kuwekeza nguvu katika ubunifu wa kufanya kazi
zaidi au kuboresha yale waliyofanikisha. Ushauri ni kwamba katika kila hatua
jifanyie tathimini ili kutambua sehemu za kuboresha na kuendelea kukua zaidi
kibiashara.
5. Kuwa
na msaidizi bora. Mwandishi anatushirikisha kuwa timu ya ushindi katika mchezo
wa utajiri inaanzia nyumbani kwako. Hivyo, omba Mungu akupatio Mke au Mme bora
ambae mtakaa meza moja na kujadiliana mipango ya maendeleo. Pia, pale
mnapobahatika kuwa na watoto hakikisha mnawalea katika misingi ambayo
itawezesha wawe na uelewa mpana wa kusimamia miradi yenu. Kwa kifupi ni kwamba
kila mmoja ndani ya familia anatakiwa ashiriki katika kuhakikisha gurudumu la
mafanikio linasonga mbele.
6. Endelea
kufanya kazi kwa bidii kuliko yeyote katika biashara yako. Mwandishi
anatushirikisha kuwa ni vigumu wafanyakazi wako kufanya kazi kwa bidii kama
wewe mwenyewe haujishughulishi ipasavyo. Ili kufikia malengo ni lazima ujibidishe
kwa kadri uwezavyo kuliko mtu yeyote kwenye kampuni ili uwe mfano kwa kila
mmoja ndani ya timu yako. Lengo la kufanya kazi kwa bidii ni kuona kampuni zako
zinakua siku hadi siku. Hapa ndipo unatakiwa kuitazama biashara sawa na kiumbe
hai, kuwa ni lazima ilishwe na lazima iendelee kupumua na ni lazima ikue zaidi
ili izalishe faida unayotaka. Hivyo, hakikisha unatafisri namba zinazoingia na
kutoka katika biashara yako.
7. Kila
mwajiriwa mpya ni sawa na kucheza kamali kuna kupata na kukosa. Mwandishi anatushirikisha
kuwa mchakato wa kutafuta mwajiriwa mpya unaanzia kwa kupokea wasifu (CV) za
wanaoomba kazi, baada ya hapo ni kufanya mahojiano na mwisho ni kumpa ajira
yule ambaye amekuwa bora katika vigezo vya kampuni. Hata hivyo, ukweli ni
kwamba sio kile kinachoonekana kwenye michakato yote hiyo ndo kitapima ubora wa
mfanyakazi husika. Kwa uzoofu wapo wafanyakazi ambao uonekana wa hovyo kwenye
mchakato wa kuomba kazi lakini baadae kiutendeji wanakuwa bora zaidi na kinyume
chake ni sahihi. Fundisho, ni lazima uhakikishe unalinda wafanyakazi wako ambao
wako bora ili kuepukana na kukimbiwa na wafanyakazi kila mara.
8. Kuwa
na fikra pana na endelea kuishi kama mfalme. Mwandishi anatushirikisha kuwa ni
kupitia fikra vitu vinaumbika. Vitu vinavyoumbwa vinaweza kuwa kwenye upande
chanya au upande hasi. Katika safari ya utajiri ni lazima fikra zako zilenge
kutengeneza utajiri zaidi. Hata hivyo, kadri unavyotengeneza utajiri zaidi ni
lazima maisha yako yaendane na utajiri ulionao, unatakiwa kuishi maisha ya
kitajiri lakini mara zote katika maisha hayo hakikisha milango ipo wazi kwa
kila mwenye uhitaji wa kukufikia kwa ajili ya msaada au mawazo,
9. Tengeneza
pesa kupitia mchezo unaopenda zaidi katika maisha ya kila siku. Mwandishi anatushirikisha
kuwa kila mtu ni mpenzi wa mchezo flani. Ni kutokana na mapenzi hayo watu wengi
wanapoteza fedha na muda kwa ajili ya kufuatilia mchezo wanaoupenda. Katika safari
ya utajiri ni sahihi kuendelea kuwa mpenzi michezo lakini fikiria zaidi ni kwa
jinsi gani unaweza kutengeneza pesa kutokana uhusika wako kwenye mchezo husika.
Hata kama hautatengeneza faida kubwa lakini utaendelea kuburudika/kufurahia
kupitia michezo husika. Na hilo ndilo kusudi la maisha – kuwa na furaha
maishani. Mfano, Trump mwenyewe kutokana na kupenda mchezo wa Golf aliamua
kuanzisha klabu za michezo hiyo ambazo pia zinamwingizia kipato.
10. Tengeneza
brendi ya jina lako kadri unavyofanikiwa kibiashara. Mwandishi anatushirikisha
kuwa jina lako ni kitu muhimu kama utaliendeeleza katika kila unachofanya. Kwa kuzingatia
hilo majengo yake yote au uwekezaji kwenye sekta mbalimbali amekuwa akitumia
jina lake. Faida kubwa ya kutumia jina lako ni kujitangaza na kukuza jina hilo
katika jamii inayokuzunguka. Unavyokuza thamani ya jina lako kuna malipo ndani
yake ambayo yanaambatana na kila mtu ambaye atahitaji kutumia jina hilo katika
biashara zake. Hata hivyo, ili kulinda ubora au thamani ya jina lako ni lazima
uhakikishe unatoa huduma au kila unachofanya unakitekeleza kwa viwango na ubora
wa hali ya juu.
11. Kufanikiwa
kibiashara ni matokeo ya kujiamini. Mwandishi anatushirikisha kuwa sifa kubwa
ya mjasiliamali ni kujiamini kuwa unaweza kufanikisha chochote kile ambacho
umedhamiria kufanya. Kujiamini huko kunatokana na msukumo wa ndani ambao upo
imara katika kila changamoto ambazo utakumbana nazo katika safari ya mafanikio.
Msukumo huu ndo utakuunganisha na dili za kibiashara au kuvuta muhimu katika
maisha yako. Kumbuka kuwa binadamu wa kawaida anatumia asilimia 5 tu ya sehemu
ya ubongo katika maisha yake ya kila siku. Kupitia matumizi sahihi ya msukumo
wa ndani tunaweza kutumia sehemu ya asilimia 95 na kupata matokeo makubwa sana.
12. Mara
zote kuwa na mtazamo chanya sambamba na kutegemea kupata kilicho bora lakini
tayari kupokea matokeo ya aina zote. Mwandishi anatushirikisha kuwa kutegemea
kilicho bora kwenye kila unalofanya ni hatua ya awali ya kufanikiwa. Hata hivyo,
mara nyingi katika uhalisia kuna kupanda na kushuka – ni lazima unapotazamia
juu ya nyakati bora ufikirie pia namna ya kupambana na nyakati ngumu kwenye
kila unachofanya. Kwa kutazamia nyakati ngumu katika mipango yako kunapunguza
maumivu au kuepuka kujutia mara baada ya nyakati hizo kutokea.
13. Jifunze
kuongea mbele za watu na mara zote hakikisha unafikisha ujumbe sahihi kwa
wanaokusikiliza. Mwandishi anatushirikisha kuwa kadri unavyotengeneza utajiri
kuna watu wengi ambao wanahitaji kusikiliza namna ambavyo umefanikiwa
kibiashara. Kumbuka kuwa wapo wengi ambao wapo tayari kulipia kwa ajili ya
kuingia kwenye semina zako au kununua vitabu kwa ajili kufahamu namna ambavyo
unatengeneza pesa kiasi cha kufikia utajiri ulionao. Kumbe, ili ufanikiwe
katika upande huo ni lazima ujifunze mbinu za kuongea na hadhira. Mbinu moja
wapo ambayo mwandishi ametushirikisha ni kuhakikisha hadhira (watazamaji au
wasikilizaji wako) unawapa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya kusikia kutoka
kwako na wewe pia kujifunza kutoka kwao.
14. Hakikisha
tabia zako zinaendana na matamanio ya mafanikio uliyonayo. Maana nyingine ni
kwamba unahitaji kuhakikisha video yako inaendane audio. Ni lazima uwe tayari
kubadilika kitabia. Kufanikiwa na kibiashara ni lazima kuanzie na mabadiliko
ndani mwako. Kama unahitaji kuwa tajiri lakini haupo tayari kufanya yale ambayo
matajiri wanafanya hakika hilo sio hitaji bali ni ndoto ya mchana. Unahitaji kujenga
tabia za kuthubutu, kuondoa uoga na kujikita kwenye fikra chanya. Kwa ujumla ni
lazima uwe tayari kuachana na tabia zote mbaya ambazo hazichangii chochote
kwenye safari ya kufikia utajiri wa hitaji lako.
15. Jifunze
kusoma vitabu kwa ajili ya kujifahamu kwa undani wewe ni nani na kuifahamu pia
jamii inayokuzunguka. Kwa maana nyingine jifunze saikoloji, falsafa na vitabu
vya mafanikio mbalimbali. Epuka kukaa bila kuwa na kazi yoyote unayofanya kwa
kufanya hivyo unamkaribisha Shetani maisha mwako. Huo muda ambao hauna cha
kufanya utumie kwa ajili ya kujifunza maarifa mapya katika maisha yako. Kumbuka
kuwa msitari mmoja unaousoma kwenye makala au kitabu unaweza kubadilisha maisha
yako kwa ujumla.
16. Kuwa
na muda wa kutafakari angalau masaa matatu kila siku. Mwandishi anatushirikisha
kuwa ni katika kipindi cha utulivu mtu anaweza kutafakari mambo ambayo
ametekeleza katika siku husika. Pia, katika kipindi hicho ndipo mtu anapima
hatua zake kuelekea kwenye picha kubwa aliyonayo katika maisha yake. Ni katika kipindi
hiki unatakiwa kusoma na kutafakari kuhusu maisha yako.
17. Kuwa
mshauri binafsi wa masuala yako ya kifedha. Mwandishi anatushirikisha kuwa
utajiri unatengenezwa kupitia maamuzi sahihi ya masuala ya pesa. Unaweza kutumia
washauri wanaojihusisha na huduma za ushauri wa masuala ya pesa. Mwandishi
anashauri kuwa ni muhimu kuhakikisha unajitegemea kwa maana ya kujifunza kwa
vitendo katika sekta nzima ya fedha zako. Watu wengi wamepoteza mali nyingi na
pengine kufisilika kutokana na kusikiliza mawazo mabaya kutoka kwa washauri wa
masuala ya kifedha. Kumbe, ni muhimu kujitegemea zaidi katika maamuzi ya
kifedha na hata pale ambapo utahitaji ushauri hakikisha umefanya utafiti binafsi
kabla ya kutekeleza ushauri husika. Hapa ndipo unatakiwa kusoma makala,
majarida na hata magazeti ya biashara kwa ajili ya kujifunza zaidi kuhusiana na
pesa na uwekezaji wake.
18. Wekeza
kwa kadri uwezavyo lakini hakikisha unawekeza sehemu ambayo unafahamu
uendeshaji wake. Kumbuka kuwa tunapozungumza kuhusu kuwekeza tunazungumzia
pesa, na pesa ndio pumzi ya kuendeleza biashara zako ili ziendelee kukua zaidi.
Pia, unatakiwa kufahamu kuwa hauwezi kuwa tajiri kama hauwekezi pesa unayopata.
Kumbuka kuwa pesa inatakiwa izalishe pesa zaidi. Kwa kutambua hilo, unatakiwa
utumie akili zaidi katika kila sehemu ambayo umeamua kuwekeza. Husifanye maamuzi
ya uwekezaji kwa kurupuka kwani kwa kufanya hivyo unaweza kujiingiza kwenye
hasara na kupoteza kile ulichonacho.
19. Kuwa
na mkataba wa makubaliano unaolinda mali zako. Mwandishi anatushirikisha kuwa
katika maisha ya mahusiano yapo mengi yanaweza kujitokeza mbele ya safari kiasi
ambacho unaweza kupoteza uwekezaji wako wote. Ili kuepukana na tatizo hilo ni
vyema mali unazomiliki zilindwe na mkataba wa makubaliano maalumu ili kujua nani
anamiliki ni nini na kwa utaratibu upi.
20. Ondoa
au epuka madalali katika dili za biashara unazofanya. Mwandishi anatushirikisha
kuwa madalali au watu wa kati kwa ujumla wao wanatumia nafasi hiyo kwa ajili ya
kujinufaisha. Kundi hili linahusisha wanasheria, washauri wa sekta mbalimbali
na madalali kwa ujumla wao. Kama unahitaji kufanikiwa ni lazima uwe tayari
kupata taarifa ambazo watu wa kati wanakuwa nazo katika kila dhamira unahitaji
kutekeleza. Hii ni kutokana ukweli kwamba kundi la watu hawa lipo tayari
kukugeuza kuwa mtaji kwa ajili ya kufanikisha malengo yao.
21. Wafundishe
watoto wako thamani ya pesa katika hatua zote za ukuaji wao. Watoto wako ndio
warithi wa mali mnazotengeneza hivyo bila kuwashirikisha hakika mali hizo
hazitokuwa endelevu. Kumbe, unatakiwa ushirikishe kila hatua kwenye usimamizi
wa mali zako ili watambue thamani ya pesa na umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii.
Wanatakiwa watambue kuwa pesa haipatikana kirahisi na hivyo haipaswi kutumika
ovyo ili mradi tu kwa kuwa ipo mfuko au benki. Wanapotambua thamani ya pesa
wanakuwa na nafasi kubwa kumiliki pesa nyingi maishani mwao.
22. Jifunze
kufanya makubaliano ya biashara. Mwandishi anatushirikisha kuwa kukua kibiashara
kunahusisha kufanya makubaliano na makundi mbalimbali. Mara zote katika
makubaliano ya kibiashara lenga sehemu zote kufanikiwa kwa maana husiangalie
upande wako tu. Unatakiwa kuangalia utafanikiwa vipi bila kuumiza upande
mwingine. Hivyo, unatakiwa kubadilika kulingana na matakwa ya unaofanya nao
makubaliano japo bila kuathiri matakwa ya kampuni yako.
Haya ni machache niliyojifunza kutoka katika
kitabu hiki, nimeona nikushirikishe kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Jiunge
na mtandao wa Fikra za Kitajiri kwa KUBONYEZA HAPA.
Endelea
kusambaza makala hizi kwa kadri uwezavyo ili ndugu, jamaa na marafiki wanufaike
kwa kujifunza maarifa mbalimbali kutoka kwa waandishi wa vitabu. Kumbuka
umepata makala hii bila malipo yoyote hivyo hakikisha na wewe unaisambaza bure.
(Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share
link). Nakutakia mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe: fikrazatajiri@gmail.com
|