Habari ya leo msomaji wa
mtandao wa Fikra za Kitajiri.
Naamini unaendelea vizuri na mapambano yanaendelea kwa ajili ya kuhakikisha kesho inakuwa bora zaidi.
Leo
hii naendelea kukushirikisha funguo 365 za hekima kutoka kwenye kitabu cha Mike Murdock. Katika Makala hii nakushirikisha funguo za mwezi Julai na lengo langu ni kumaliza funguo zilizobakia kabla ya mwezi Januari 2020.
Karibu tujifunze wote funguo za hekima ambazo mwandishi anatushirikisha katika sehemu hii:
Julai 1 (182): Mbegu
yako itadhihirisha tabia ya udongo. Kumbuka tunafahamu kuwa katika hali ya
kawaida, udongo wenye rutuba unatoa mbegu zenye ubora wa hali ya juu. Vivyo
hivyo katika maisha ya kawaida matunda yako katika jamii yatadhihirisha tabia
zako.
Julai 2 (183): Zawadi
tatu za Mwenyezi Mungu ni Kusamehe, Urafiki na Matumaini katika maisha ya
baadae. Hakikisha zawadi hizo zinakuwa sehemu ya maisha yako ya kila siku.
Jifunze kusamehe, hakikisha unakuwa rafiki mwema na hakikisha unakuwa na
tumaini bora katika maisha yajayo.
Julai 3 (184): Uadilifu
hauwezi kuthibitishwa bali kinachofanyika ni kuutambua tu. Hivyo katika jamii
unahitaji kuwa na vipimo vyako kuhusu uadilifu katika maisha yako ya kila siku.
Julai 4 (185): Tatizo
unalotatua linadhihirisha zawadi ambazo utapokea katika maisha yako. Kumbuka
kuwa tunapata tuzo kwa kutatua changamoto zilizopo katika jamii tunamo ishi.
Ukitatua tatizo dogo utapokea zawadi zinazoendana na udogo wa tatizo hilo na
kinyume chake ni sahihi.
Julai 5 (186): Watu
hawakumbuki unachosema bali wanakumbuka hisia walizopata kulingana na maneno
yako. Kabla ya kutamka neno lolote jiulize litapokelewa vipi na jamii
unayoilenga. Ni bora kunyamaza kuliko kutamka neno lenye hisia hasi kwa wengine.
Julai 6 (187): Lengo
la adui ni kubadilisha haiba au mwonekano wako katika jamii inayokuzunguka.
Hakikisha haumpi nafasi adui kujua undani wako kwani kufanya hivyo unamwongezea
nafasi ya kufahamu mapungufu yako.
Julai 7 (188): Wakati
utafunua yale ambayo hawezi kufunuliwa katika mahojiano. Kupitia mahojiano
unaweza kuongea lolote kuhusu maisha yako lakini ni muda pekee amabo unaweza
kudhihirisha ukweli wa kile ulichosema.
Julai 8 (189): Ubora
wa udongo unaamua ubora wa mbegu. Ukiwa na udongo bora utapata mbegu bora na
kinyume chake ni sahihi. Vivyo hivyo, mafanikio katika maisha yanategemea na
matendo yako.
Julai 9 (190): Mapenzi
ya Mungu ni tabia sio mahali. Chochote ambacho kinakamilisha tabia njema katika
jamii kinadhihirisha uwepo wa Mungu. Hivyo, tenda mema kwa kadri uwezavyo kwani
kufanya hivyo unatumia hazina/kalama ambayo umepewa na Mungu.
Julai 10 (191): Ufanye
wakati ujao uwe mkubwa sana kwani jana imeshapotea. Ishi leo kwa ajili ya kesho
kwani ya jana hayana nafasi tena. Muhimu ni kuhakikisha unatumia ya jana
kuepuka makosa katika matendo ya leo na hatimaye kuboresha maisha yajayo.
Julai 11 (192): Ubora
wa maswali yako hudhihirisha ubora wa uvumbuzi wako. Husikubali kuridhika na
hali inayokuzunguka badala yake katika kila hali jiulize ni kipi unachoweza
kufanya ili kuboresha hali husika.
Julai 12 (193): Umaarufu
ni pale unapopendwa na watu lakini furaha ni pale unapojipenda mwenyewe.
Jiulize je yale unayofanya yanamchango chanya katika kukamilisha furaha yako au
yanalenga kutafuta umaarufu tu.
Julai 13 (194): Marafiki
wa kweli wana maadui wanaofanana. Kumbuka msemo kuwa ndege wanaofanana huruka
pamoja. Kama ni urafiki wa kweli ni lazima muwe mnashirikiana na kutatua
changamoto zinazowakabili na kufanya hivyo mnatengeneza maadui. Kumbuka wapo
ambao hawapendi urafiki au mahusiano yenu.
Julai 14 (195): Pale
unapopenda kitu ndani yake kuna matamanio japo pale unapoheshimu kitu ndani
yake kuna uthamani. Hivyo, tofauti katika ya kupenda na kuheshimu ni matamani
na thamani. Tanguliza thamani katika kile unachopenda ili kudumisha upendo huo.
Julai 15 (196): Ubora
wa mbegu yako unaamua ubora wa mavuno. Mara zote katika maisha fikiria zaidi
kuboresha mbegu ambazo ni sawa na msingi wa nyumba ili kuwa na mavuno bora au
nyumba imara. Tatizo ni kwamba asilimia kubwa katika jamii inahitaji mavuno
bora bila kuwekeza kwenye kuboresha ubora wa mbegu ambazo katika maisha
tunaweza kusema ni matendo au tabia yako.
Julai 16 (197): Kazi
za Mwenyezi Mungu haziendani na hitaji lako bali maarifa uliyonayo kuhusu yeye.
Jiulize je umewekeza kiasi gani katika maarifa yanayolenga kufunua makuu ya
Mwenyezi Mungu katika maisha yako.
Julai 17 (198): Ni
heri kutokuwa na kitu chochote ambacho Mwenyezi Mungu hajataka uwe na nacho.
Yawezekana umeomba sana bila majibu na pengine umekata tamaa, kumbe unahitaji
kutambua kuwa Mungu ana makusudi ya kutokupa kile unachoomba.
Julai 18 (199):
Msimu wa tafiti sio msimu wa kutangaza bidhaa. Kumbuka kila msimu una matukio
yake hivyo unahitaji kuhakikisha yale unayofanya yanaendana na msimu husika. Kuna
wakati wa kupanda na wakati wa kuvuna hivyo husilazimishe kuvuna wakati wa
kupanda.
Julai 19 (200): Awaye
yoyote katika shida ni mlango wako wa kutokana na shida. Shida zako zinamalizwa
kwa kutatua shida zinazowakabili wengine katika jamii au mazingira
yanayokuzunguka.
Julai 20 (201): Vita
ni ushuhuda kuwa adui yako amefahamu kesho yako. Hakikisha unaifanya mipango
yako kuwa siri ili kuepuka mapambano na adui wasiopenda upige hatua katika
maisha yako ya baadae.
Julai 21 (202): Yale
unayosikia hudhihirisha yale ambayo upo tayari kubadilisha katika jamii yako.
Chochote ambacho umedhamiria kufanya katika maisha yako ni lazima utumie muda
mwingi kupata taarifa zake. Unatahiji kuwa na taarifa za kutosha kuhusu
changamoto ambazo unakusudia kutatua.
Julai 22 (203): Mbegu
inayoondoka mikononi mwake kamwe haiondoki katika maisha yako badala yake
inaingia katika maisha yako ya baadae ambapo huwa inaongezeka zaidi au inazaa
matunda. Kumbe unapoendelea kuishikilia mbegu uliyonayo itaendelea kudumaa
jinsi ilivyo na hakuna siku itazaa matunda.
Julai 23 (204): Kuna
njia mbili za kuongeza hekima nazo ni: kupitia makosa au kupitia kwa
walimu/washauri. Jifunze kutokana na makosa au jifunze kutoka kwa wengine ambao
unaweza kuwa kujifunza kwa kusoma maarifa mbalimbali au watu ambao unatamani
kuwa kama wao (role models). Mfano, ningekuwa mchezaji wa mpira ningetamani
mara zote nifanye vitu anavyofanya Ronaldo au Messi hivyo ningetumia muda
mwingi kujifunza kuhusu uwezo wao.
Julai 24 (205):
Macho yaliyochoka ni nadra kuona yajayo. Na kama macho yako hayawezi kuona
yajayo hauna tumaini la baadae katika maisha. Na kama hauna tumaini katika
maisha ya baadae ni vigumu sana kupata mafanikio katika kila sekta ya maisha
yako.
Julai 25 (206): Wanaoridhika
na madhaifu yako wanaweza kuwa maadui katika kufikia malengo yako. Kumbe
unatakiwa kujiuliza kama wanaokusifia wanafanya hivyo kwa kumaanisha au
wanafanya kwa lengo la kukudumaza husipige hatua zaidi. Husiridhike na hatua
ulizofikia bali endelea kuboresha zaidi kwa kupunguza madhaifu yaliyopo.
Julai 26 (207): Yupo
mtu ambaye mara zote anakuangalia na yupo tayari kubariki kazi ya mikono yako.
Kumbe katika kila tendo unalofanya katika maisha yako unapaswa kukumbuka kuwa
ipo nafsi inakuangalia na unaweza kubarikiwa au kulaaniwa kupitia tendo hilo.
Julai 27 (208):
Hauwezi kushinda kile ambacho haupo tayari kukichukia. Hivyo, kama kuna tabia
au matendo ambayo huyapendi katika maisha yako, hatua ya kwanza ya kubadilisha
tabia au matendo hayo ni kuyachukia.
Julai 28 (209): Chochote
unachojaribu kuishi bila mafanikio ni kwa sababu haujakipa thamani inatakiwa.
Kumbe ili ufanikishe chochote katika maisha ni lazima kwanza ukithamini. Kwa
maana hiyo tunafakiwa kupata vitu ambavyo vimepewa thamani katika maisha yetu.
Julai 29 (210): Kutoa
zaka sio malipo ya deni bali ni kukubali kuwa ni sehemu ya majukumu yako. Hakikisha
unalipia zaka kulingana na taratibu za Imani yako.
Julai 30 (211): Utii
usio wa kawaida unafungua upendeleo usio wa kawaida. Muhimu ni kujiuliza kuwa
utii wako unahusiana na nini. Pia hapa unatakiwa kutofautisha utii na uoga.
Watu wengi wanakuwa waoga kwa kudhania kuwa kufanya hivyo wanatii mamlaka
iliyopo juu.
Julai 31 (212):
Kamwe husilalamike kuhusu hali ya sasa kama haupo tayari kuibadilisha kwa ajili
ya mafanikio katika maisha ya baadae. Kumbuka kuwa kesho iliyo bora inatokana
na mabadiliko katika mfumo wa maisha leo.
Sehemu
hii niliyokushirikisha leo ina funguo za hekima kutoka kwa Mike Murdock ambazo ni katika Julai. Nitaendelea kukushirikisha funguo zilizobakia kwa kadri nitakavyokuwa napata muda. lengo ni kumaliza funguo zote 365 kabla ya mwezi Januari ili funguo hizi uanze kuzitumia katika kipindi cha mwaka 2020. Kupata nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha tuma ujumbe wa kuomba kitabu hiki
kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Endelea kusambaza makala hizi
kwa kadri uwezavyo ili ndugu, jamaa na marafiki wanufaike kwa kujifunza maarifa
mbalimbali kutoka kwa waandishi wa vitabu. Kumbuka umepata makala hii bila
malipo yoyote hivyo hakikisha na wewe unaisambaza bure. (Unaposambaza makala
hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link). Nakutakia
mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com
|