Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa Fikra za Kitajiri.
Naamini unaendelea vizuri na mapambano ya
kila siku kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Kama nilivyokuahidi wiki
iliyopita kukushirikisha mwendelezo wa funguo 365 za hekima kutoka kwa
Mwandishi Mike Murdock, leo hii nakushirikisha kuanzia ufunguo 32 hadi
ufunguo wa 90 (Mwezi Februari & Machi).
Kama bado hujajiunga kwenye mfumo wetu wa
kupokea makala za uchambuzi wa vitabu, tafadhali fanya hivyo KWA KUBONYEZA BONYEZA HAPA na
kujaza fomu kisha bofya “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu. Ni
fursa ya bure ambayo utaendelea kupata uchambuzi wa vitabu kwa lugha rahisi
kupitia barua pepe yako.
Karibu
ushirikiane nami kujifunza machache kati ya mengi ambayo mwandishi
anatushirikisha katika katika sehemu hii ya pili ya mwendelezo wa kitabu hiki:
Februari 01 (32): Mara
zote katika maisha utakumbukwa kwa vitu viwili: Matatizo unayotatua au matatizo
unayosababisha. Jiulize kama umekuwa na maisha ya kutafutia suluhu matatizo au
umekuwa mtu wa kusababisha matatizo katika jamii inayokuzunguka. Tathimini
unayoifanya ijikite kwenye maeneo ya kijamii, kimazingira, kiuchumi, kisiasa na
kiutamaduni.
Februari 02 (33): Mwenyezi
Mungu huwa hafanyi rejea ya makosa yako ya nyuma kwa ajili ya kuamua maisha
yako ya baadae. Hivyo, kama kuna makosa au uzembe umefanya katika maisha
yaliyopo kuanzia sasa huna budi kutambua kuwa hayana nafasi ya kuamua maisha
yako yajayo.
Februari 03 (34): Hatua
yoyote kuelekea kwenye mafanikio mara zote inazalisha furaha rohoni. Kumbe,
kila hatua yenye mwelekeo sahihi katika maisha ina nafasi kubwa kwa kuwa hatua
1000 ni lazima zianzie hatua ya kwanza. hivyo, sherekea ushindi mdogo mdogo katika
maisha ya kila siku kwani ushindi huo unakupeleka kwenye mafanikio unayotamani.
Februari 04 (35): Ukiendelea
kusisitiza juu fursa ambayo Mwenyezi Mungu hakukupatia, utanyanganywa fursa
ambayo alikupatia. Muhimu ni kushikilia fursa iliyopo mikononi mwetu ili
kupitia fursa hiyo fursa zaidi zifunguke.
Februari 05 (36): Ushahidi
wa uwepo wa Mwenyezi Mungu hadi sasa unazidi mashaka ya kutokuwepo kwake.
Jiulize unaamini nini juu ya uwepo wa Mwenyezi Mungu katika maisha yako ya kila
siku.
Februari 06 (37): Kamwe
husilalamikie yale ambayo unayaruhusu katika maisha yako ya kila siku. Binadamu
tofauti na viumbe wengine amepewa uwezo wa kufikiria na kufanya maamuzi yaliyo
sahihi katika matukio ya maisha yake ya kila siku. Hivyo, yale ambayo unayapa
nafasi na unaona sio sahihi mamlaka yapo mikononi mwako kuachana nayo badala
kuendelea kulalamika.
Februari 07 (38): Nenda
sehemu ambayo unakubalika zaidi kuliko sehemu ambayo unavumiliwa. Tambua ni
sehemu zipi katika kila sekta ya maisha yako unakubalika zaidi na baada ya kuzitambua
sehemu hizo hakikisha unazitumia kama kalama uliyopewa na Mwenyezi Mungu kwa
faida ya jamii inayokuzunguka.
Februari 08 (39): Siku
moja yenye heri ni bora zaidi ya siku elfu moja za maumivu. Mara zote katika
maisha lenga kuwa na maisha yenye heri kuliko maisha ya huzuni. Kutokana na
ukweli huu, kila mmoja anatakiwa kuishi maisha mema ambayo hayasababishi
maumivu kwa wengine.
Februari 09 (40): Mara
zote penye ugumu kuna muujiza wa kutoka kwenye ugumu huo. Tambua kuwa magumu
yanayokukabiri ni ya muda tu na tafuta muujiza uliojificha ndani ya ugumu huo.
Tumia muujiza huo kubadilisha maisha ya jamii inayokuzunguka.
Februari 10 (41): Kilichovunjika huwa
bora zaidi wakati wa kuunganishwa. Kubali kuvunyika katika maisha ili pale
unaposimama upya ujifunze mengi kutokana na kuvunjika kwako.
Februari 11 (42): Mafanikio
kwa kifupi ni kuwa ni Baraka zaidi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya
kukamilisha kazi yake katika maisha yako. Kumbe, kila mara tunatakiwa kuishi
kwa ajili ya ukamilisho wa kusudi la Muumba ambalo amekusudia kwa kila binadamu
katika maisha yake hapa Duniani.
Februari 12 (43): Saa
moja ya uwepo wa Mungu katika maisha yako itakufunulia mapungufu katika mipango
yako. Tenga muda kwa ajili ya kuwa na muunganiko na muumba wako kulingana na
Imani yako ili katika muunganiko huo upate kutafakari juu ya malengo yako
katika kila sekta ya maisha yako.
Februari 13 (44): Hasira
ni chanzo cha kupata ufumbuzi wa tatizo. Mara zote kumbuka kuwa hisia za hasira
ziishie katika kupata muhafaka/upatanisho wa tatizo na sio kwenye ugomvi na
mafarakano.
Februari 14 (45): Mara
zote utayari wa kufikika unatoa nafasi ya kubadilika. Katika jamii husikubali
kuishi kana kwamba wewe ndo una majibu ya kila kitu; kuwa tayari kusikiliza ili
ujifunze kutoka kwa wanaokuzunguka.
Februari 15 (46): Kamwe
husitoe muda zaidi kwa wakosoaji kuliko unavyofanya kwa marafiki. Katika kila
unachofanya kumbuka kuwa wapo watu ambao watajifanya wanajua zaidi na wapo
tayari kukuambia kuwa hautofanikiwa. Watu wa aina hiyo watakukatisha tamaa na
mwisho wake utashindwa kutekeleza kusudi lako. Kuwa makini na watu wa aina
hiyo.
Februari 16 (47): Utayari
wa kufikika mwanzo huwa ni zawadi baadae inakuwa ni mtihani na mwishowe inakuwa
ni thawabu. Kuwa tayari kufikika na jamii inayokuzunguka ili upate thawabu
ambazo zinakusubiria. Kumbuka kuwa tunafakiwa kwa kutatua matatizo ya jamii
inayotuzunguka.
Februari 17 (48): Usumaku
unaotokana na ufadhili/huruma yako mar azote ni bora kuliko kumbukumbu za akili
yako. Kubwa ni kuendelea kutambua kuwa hatuishi kwa faida yetu bali tunaishi
kwa faida ya wengine na katika kuishi huko ndivyo tunapata mafanikio ya
kimaisha.
Februari 18 (49): Pale
unapokubali kupoteza kilichopo tayari katika mikono yako ndivyo na Mungu anasitisha
Baraka alizokusudia katika maisha yako. Tunakumbushwa kuthamini kile
tunachomiliki ili kupitia umiliki huo tufungue milango ya Baraka zaidi.
Februari 19 (50): Kamwe
husiandike upya theolojia yako (misingi binafsi ya maisha yako) kwa ajili ya
kuruhusu mambo ya ovyo. Hakikisha misingi au kanuni binafsi za maisha
unazoamini zinakupeleka kwenye mafanikio ya kimaisha kuliko kwenye anguko la
kimaisha.
Februari 20 (51): Mara
zote changamoto huwa zinajitokeza pale unapokaribia kwenye ushindi. Kumbe
zinapojitokeza changamoto unahitaji kutambua kuwa ushindi unakaribia. Badala ya
kukimbia changamoto hizo hakikisha unazitatua kwa ajili ya kufikia hatua
iliyopo mbele zaidi.
Februari 21 (52): Kamwe
husikuze ugumu katika maisha badala yake unatakiwa utafute njia rahisi ya
kupambana na ugumu huo. Jiulize je umekuwa mtu wa kuyafanya maisha yako yawe
magumu zaidi? Kama ndivyo hivyo unahitaji kuachana na tabia ambazo zinapelekea
maisha yako yawe magumu kiasi hicho.
Februari 22 (53): Kumbukizi
zinakufanya uwe mtumwa kuliko udhalimu wa aina yoyote ile. Fanya tafakari juu
ya kumbukizi ambazo unazipa nafasi katika maisha yako na amua sasa kuachana na
zile ambazo zinahatarisha maisha yako.
Februari 23 (54): Umuhimu
wako haupo katika mfanano na wenzako bali katika pointi za msingi ambazo
unatofautiana nao. Kumbe, kuwa na fikra tofauti na jamii inayokuzunguka siyo
dhambi bali ni chanzo cha kufanya vitu kwa weledi na ubunifu katika maisha yako
ya kila siku.
Februari 24 (55):
Unachoweza kuvumilia hauwezi kukibadilisha. Kumbe katika maisha kila mara
tunahitaji kujiuliza kama yale tunayovumilia yana mchango chanya au hasi katika
kufikia mafanikio ya matamanio yetu.
Februari 25 (56): Majira
ya maisha yako yatabadilika kila mara unapotumia Imani yako. Hakikisha Imani
uliyonayo katika kila sekta ya maisha yako inakupeleka kwenye mabadiliko ya
maisha ambayo yapo kwenye njia sahihi.
Februari 26 (57): Pale
unapo omba Mungu muujiza mara zote atakupatia maelekezo ya kufanya ili kupata
muujiza husika. Unakiwa kujifunza kuwa hakuna muujiza ambao utatokea katika
maisha yako bila ya wewe kujishughulisha katika uumbaji wa muujiza huo. Timiza
wajibu wako na Mungu atakupatia miujiza mingi ambayo inasukubiria.
Februari 27 (58): Mara
zote tambua kuwa chochote kinachokosekana katika maisha yako kipo hivyo kwa
kuwa hakijathamaniwa ipasavyo. Hii inamaanisha kuwa kinachothaminiwa katika
maisha yako ya kila siku kinapata nafasi ya kuumbika kwenye uhalisia wake.
Februari 28 (59): Mwitikio
wako kwenye cheo au ukuu unatoa picha ya unyenyekevu ulionao. Mara nyingi
tumezoa kusikia msemo kuwa “pata cheo au pesa tujue tabia zako halisi”. Kumbe
kwa mujibu wa ufunguo huu wa hekima, cheo au pesa havitakiwi kukutoa kwenye
tabia yako iliyozoeleka.
Machi 01 (60): Heshima
ni mbegu ya maisha marefu au urafiki wa kweli. Fanya tathimini ya maisha yako
ili kugundua kama matendo yako yanakupa heshima unayostahili au yanakupunguzi
heshima katika jamii inayokuzunguka.
Machi 02 (61):
Maneno yako ni mbegu ya hisia ulizonazo katika kila siku ya maisha yako. Je ni
maneno yapi ambayo yanatoka kinywani mwako au unayonena dhidi ya nafsi yako.
Kumbuka maneno yana nguvu kubwa ya kuumba hivyo ni rahisi kuwa na hisia hasi
kutokana na maneno yako.
Machi 03 (62):
Marafiki uleta tulizo/faraja na maadui uleta mabadiliko. Kumbe, unahitaji
kuwatumia maadui zako kwa ajili ya kubadilisha sehemu muhimu za sekta ya maisha
yako. Fanya tathimini kugundua maadui wa maisha yako na kuhakikisha unatafuta
dawa ya kudumu ya kubadilika kutoka kwenye himaya ya maadui hao.
Machi 04 (63): Chocho
unachomiliki sasa kinaweza kutumika kuunda chochote unachotamani katika maisha
yako ya baadae. Kumbe husidharau unachomiliki sasa hata kama ni kidogo kiasi
gani. Hakikisha hicho unachomiliki kinaboreshwa siku hadi siku kwa ajili ya
kufikia mafanikio makubwa ya matamanio yako.
Machi 05 (64): Kukosa
utashi wa kumwamini mtu mwema utakufanya upoteze fursa nyingi kuliko kumwamini
mtu mbaya. Jiulize mara nyingi unaandamana na watu wa aina gani katika maisha
yako ya kila siku.
Machi 06 (65):
Chochote chema/kizuri kinachukiwa na chochote kibaya. Hii ni sharia ya asili
kuwa wema na ubaya kamwe haviwezi vyote kukaa pamoja. Hivyo, kumbuka kuwa
ukitenda mema utachukiwa na wengi wenye nia mbaya dhidi yako.
Machi 07 (66): Ndoto
isiyo ya kawaida inahitaji mwalimu/mshauri asiye wa kawaida kwa ajili ya
kutimiza ndoto hiyo. Kumbe husiogope ukubwa wa ndoto ulizonazo badala yake
hakikisha kila ndoto yako unakuwa na mshauri au kocha au mtu ambaye ni mfano
bora (role model) kwa ajili ya kutimiza ndoto yako.
Machi 08 (67): Kile
kinachokuhuzunisha ni ishara juu ya jukumu ambalo Mungu amekupa ukamilishe.
Kumbe kila changamoto katika maisha yako ya kila siku kuna siri ambayo Mungu
anakusudia uitumie kubadilisha jamii inayokuzunguka.
Machi 09 (68): Kila
mazingira yana kanuni au miongozo ya kuingia au kutoka ndani yake. Hivyo,
mazingira yoyote au katika kila hali unahitaji kujua kanuni au miongozo ya
kuingia au kutoka katika mazingira husika.
Machi 10 (69): Ukuu
sio kipimo cha kuwa mkamilifu bali namna unavyokabiliana na mapungufu uliyonayo.
Kumbe, mara zote ni muhimu kutambua kuwa binadamu si mkamilifu, hivyo, fahamu
mapungufu yako ni katika sekta zipi na hakikisha unayafanyia kazi kwa ajili ya
kuimarika kila mara.
Machi 11 (70): Kila
tendo la utiifu/nidhamu linafupisha umbali wa muujiza unaosubilia utokee katika
maisha yako. Kumbe tunatakiwa kufahamu kuwa nidhamu binafsi ni nyenzo muhimu ya
kukufikisha kwenye matamanio ya maisha yako.
Machi 12 (71): Mwitikio
wako katika neno la Mungu hutoa picha ya namna ambavyo unamheshimu muumba wako.
Jiulize ni mara ngapi neno la Mungu limekuwa likikujia katika akili yako na
namna ambavyo umekuwa ukilifanyia katika maisha yako ya kila siku.
Machi 13 (72): Tatizo
linalokusumbua zaidi katika maisha yako ndilo tatizo ambalo Mungu anakusudia
ulitatue katika jamii inayokuzunguka. Jiulize ni tatizo lipi ambalo limekuwa
likikusumbua na hakikisha unafutia njia sahihi za kulitatua na kuhakikisha
jamii inayokuzunguka inanufaika na njia hizo.
Machi 14 (73): Mashitaka
ya uongo ni hatua ya mwisho kuelekea kwenye anguko. Jitahidi kuepuka uongo
unaolenga kukandamiza haki za jamii inayokuzunguka. Harakati zako za maisha
ziende sambamba na kujali maisha ya jamii inayokuzunguka.
Machi 15 (74): Miujiza
inatokea kwa kasi kama ilivyo kasi ya majanga katika maisha. Kumbuka kuwa kadri
unavyosubilia miujiza katika maisha yako ndivyo na majanga nayo yatatokea
katika maisha yako japo si sehemu ya matamanio yako. Muhimu ni kuhakikisha
unaandaa mazingira ya kuwezesha muujiza unaoutaka katika maisha yako.
Machi 16 (75):
Tofauti kati ya UMUHIMU na SIYO MUHIMU ni ADUI katika matukio ya maisha ya kila
siku. Kumbe yale yote ambayo siyo ya muhimu katika maisha yetu tunatakiwa
kuchukulia katika mtazamo wa adui wa maisha yetu.
Machi 17 (76): Pale
watu waovu wanapokaa mbali na maisha yako ndivyo na maovu yanaacha kutokea
katika maisha yako. Kumbe, mara zote tunatakiwa kuwa mbali na makundi ya watu
waovu ili kuepusha uovu katika maisha yetu.
Machi 18 (77): Imani
ni mbegu ya ukamilisho wa kalama au Baraka za maisha yako na Imani hii ndio
huwezesha ukamilisho wa ahadi za maisha yako. Chochote unachohitaji katika
maisha yako ni lazima utangulize Imani kuwa ukamilisho wake unawezekana. Imani pia
itakuwezesha kukamilisha ndoto ambazo zinaonekana kukuogopesha kila
unapozitafakari.
Machi 19 (78): Utovu
wa nidhamu ni gharama kuliko nidhamu. Katika maisha unahitaji kuwa na nidhamu
kwa jamii inayokuzunguka sambamba na kuwa nidhamu binafsi. Pia unatakiwa kuwa
na nidhamu kwenye malengo binafsi ili malengo hayo yapate kukamilika katika
maisha yako.
Machi 20 (79): Adui
ambaye siyo wa kawaida anahitaji hekima zisizo za kawaida kukabiliana nae. Kumbe
unahitaji kubadilisha mbinu kulingana na aina ya adui unayekabiliana. Usiendelee
kutumia mbinu zile zile kwa maadui wenye sifa tofauti huku ukitegemea kupata
matokeo tofauti.
Machi 21 (80): Kile
unachozungumza sio kama kile ambacho wengine wanakumbuka. Kumbe ni muhimu kuwa
na matendo bora kwa ajili ya kutengeneza historia nzuri ya maisha yako. Tengeneza
kumbukiza bora ya maisha yako ili historia au matendo yako yaongee kuliko
maneno yako.
Machi 22 (81): Kamwe
husijadili changamoto zako na mtu ambaye ana uwezo wa kuzitatua. Eleza
changamoto zako kwa mtu ambaye unaamini anaweza kukusaidia kupata suluhu ya
changamoto hizo. Kumbuka, kuwa changamoto zako ni siri ya maisha yako hivyo
kueleza kwa mtu ambaye hana uwezo wa kukusaidia ni sawa na kusambaza siri zako
kwa jamii.
Machi 23 (82): Furaha
ni tuzo la Kimungu kwa kugundua kusudi la Kimungu katika hali au tukio husika. Kumbe
kila tukio katika maisha yako unahitaji kutafakari kusudi lake kiroho zaidi ili
ndani ya hali au tukio husika upate furaha ndani yake.
Machi 24 (83): Mwenyezi
Mungu kamwe huwa hajibu kwenye maamivu badala yake anajibu harakati zako za
kukabiliana na maumivu hayo. Kumbe sara zako zinatakiwa kuambatana na harakati
za kupambana/kukabiliana na maumivu yanayokukabili.
Machi 25 (84): Pale
unapojihusisha na ndoto ya Mwenyezi Mungu dhidi ya nafsi, yeye atakulipa kwa
kujihusisha na ndoto ulizonazo katika maisha yako. Tambua kusudi la maisha yako
ili Mungu akuongoze katika mikono salama kadri unavyopambana kuishi kusudi hilo
katika maisha ya kila siku.
Machi 26 (85): Kazi
ya kweli ya hekima ni agizo. Kumbe pale tunapokuwa na hekima, tunapata maagizo ya
namna ya kukabiliana na kila tukio kwenye maisha yetu ya kila siku. Kwa kufanya
hivyo maisha yetu yataepukana na misukosuko ya maisha na hivyo kuishi maisha ya
ukamilisho.
Machi 27 (86):
Wenye busara/hekima kamwe huwa hawajadili yale ambayo wanahitaji wengine
wasahau. Unahitaji kuwa na kifua kikubwa kwa ajili ya kuhifadhi mambo ambayo
unaona hayana tija kuendelea kujadiliwa kuhusiana na maisha yako au jamii
inayokuzunguka.
Machi 28 (87): Ugomvi
huwa ni jaribio la kulinda mahusiano. Katika mahusiano angalia yapi
yanayowagombanisha na jiulize kwa nini huwa ugomvi huo unatokea mara kwa mara. Epuka
kurudia makosa yale yale kwa ajili kulinda mahusiano yanu.
Machi 29 (88):
Uthibitisho wa upendo ni shauku/hamu ya kufurahishwa. Kubwa katika upendo ni kuendelea
kuwa na hamu ya kufurahishwa na hali au matukio yanayokufurahisha katika kila
siku ya maisha yako. Kukosa hamu hiyo ni kiasharia cha mwisho wa upendo katika
maisha yako.
Machi 30 (89): Maumivu
ni uthibitisho wa kwenda kinyume na matakwa. Hapa ni lazima kukumbuka kuwa
hatujaumbwa kwa ajili ya mateso. Mateso tunayopata katika maisha yetu mara
nyingi tunayatengeneza wenyewe bila kujua au kwa kujua lakini hatujali. Mara nyingi
maumivu mengi katika maisha yetu yanatokana na tulizo la matamanio ya mwili. Tulizo
hili huwa linadumu kwa muda mfupi hila kwa baadae athari yake huwa ni mateso ya
muda mrefu.
Machi 31 (90): Madeni
huwa ni uthibitisho wa tamaa. Mara nyingi tamaa huwa zinapelekea watu wengi
kuingia kwenye madeni makubwa. Athari ya madeni hayo ni kukosa utulivu katika
maisha kutokana na msongo wa mawazo unaotokana na madeni hayo.
Katika
sehemu hii ya pili nimekushirikisha funguo 90 za hekima kati ya funguo 365
ambazo mwandishi Mike ametushirikisha katika kitabu hiki. Panapo majaliwa
tukutane wiki ijayo kwa ajili ya funguo zinazofuatia katika siku 365 za mwaka
kutoka kwa mwandishi wa kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha tuma ujumbe wa kuomba kitabu hiki
kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Endelea kusambaza makala hizi kwa kadri
uwezavyo ili ndugu, jamaa na marafiki wanufaike kwa kujifunza maarifa
mbalimbali kutoka kwa waandishi wa vitabu. Kumbuka umepata makala hii bila
malipo yoyote hivyo hakikisha na wewe unaisambaza bure. (Unaposambaza makala
hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link). Nakutakia
mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com
|