Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa Fikra za Kitajiri.
Rafiki naamini kuwa
unaendelea kupambana kwa ajili ya kuhakikisha kesho yako inakuwa bora zaidi ya
sasa. Ni lazima upambane kwa maana ya kufanya kazi kwa ubunifu na weledi ili
kuhakikisha unatimiza ndoto za maisha yako.
Naendelea kutimiza ahadi
yangu kwako ya kuhakikisha kila ninapopata muda nakushirikisha kile
ninachojifunza kupitia uchambuzi wa vitabu ninavyosoma. Ni mategemeo yangu kuwa
Makala hizi za uchambuzi wa vitabu zimekuwa msaada mkubwa kwako katika
kubadirisha sekta mbalimbali za maisha yako. Naomba kupata shuhuda sambamba na
maoni juu ya makala hizi zilivyogusa maisha yako namna ambavyo kwa pamoja tunaweza
kupanua wigo na kufikia wanufaika wengi zaidi.
Kama bado haujajiunga na
mtandao huu, BONYEZA HAPA na jaza fomu kisha
bofya “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu. Kwa kujiunga na
mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja kwenye barua
pepe.
Kitabu
ninachokushirikisha leo hii ni “Automatic
Millionaire” kutoka kwa mwandishi maarufu David Bach. Mwandishi anatumia kitabu hiki kutushirikisha namna ambavyo kila
mmoja anaweza kutengeneza utajiri katika maisha yake hapa duniani. Mwandishi
anatushirikisha kuwa kitabu hiki kinalenga kumsaidia msomaji kutengeneza
njia/mpango wa moja kwa moja (Automatic) wa kuwa milionea.
Lengo
kubwa ambalo mwandishi anakusudia kupitia kitabu hiki ni kuhakikisha msomaji
anapata elimu muhafaka kuhusu “fedha” kwani elimu hii imekosekana kwa watu
wengi. Hii ndio sababu asilimia kubwa katika jamii ni masikini kwa kuwa hawana
msingi sahihi kuhusu somo la fedha hasa namna ya kuitengeza na namna ya
kuitumia kutengeneza fedha zaidi.
Hata
hivyo mwandishi anatoa tahadhari kuwa “siri/misingi
ya kuwa tajiri ipo wazi kwa kila mmoja” na pengine hata wewe unayesoma
makala hii unafahamu misingi hiyo. Pamoja na kwamba siri hizo zipo wazi lakini
wengi wameshindwa kufikia utajiri wa ndoto zao kwa vile hawatumii misingi hiyo
katika maisha yao ya kila siku. Hivyo, kitabu hiki sio kwa wale wanaotaka
utajiri wa haraka haraka kwa maana kulala masikini na kuamka tajiri bali
kinalenga kuweka mfumo wa moja kwa moja (automatic) wa kufikia UHURU WA KIFEDHA AU UTAJIRI WA KWELI.
Kwa
ufupi, kitabu hiki kimejengwa juu ya falsafa kuwa:-
- Kuwa tajiri sio lazima uwe na pesa nyingi;
- Sio lazima uwe na nidhamu juu ya fedha zako (najua hii itakuchanganya kama mimi maana tunafahamu kuwa siri mojawapo ya kuwa tajiri ni kuwa na nidhamu ya fedha);
- Sio lazima ujiajiri mwenyewe ili kuwa tajiri kwani unaweza kuendelea kuajiriwa na ukawa milionea;
- Kwa kutumia kile mwandishi anachokiita “The Latte Factor”, unaweza kutengeneza pesa nyingi kupitia pesa kidogo ulizonazo;
- Matajiri wanaendelea kuwa matajiri kwa kuwa wana utaratibu wa kujilipa kwanza;
- Wamiliki wa nyumba za biashara wanaendelea kuwa matajiri wakati wapangaji wanaendelea kuwa masikini; na
- Zaidi ya yote unahitaji mfumo wa moja kwa moja (automatic system) ili husikwame katika kufikia utajiri wa ndoto zako.
Karibu
ushirikiane nami kujifunza machache kati ya mengi ambayo mwandishi
anatushirikisha katika kitabu hiki:
1. Njia pekee inayokuhakikishia
kufikia utajiri wa ndoto zako ni kuweka mfumo wa moja kwa moja wa mipango yako
yote ya kifedha. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika maisha kuna majukumu
mengi ambayo kila siku mhusika anajishughulisha nayo. Ni kutokana na majukumu
hayo watu wengi wanashindwa kufikia mipango waliyojiwekea kwa vile pengine
wanasahau au wanashindwa wajigawe vipi. Kumbe, mwandishi anatushirikisha kuwa
kupitia mfumo wa moja kwa moja (automatic system) unakuwezesha kupata muda wa
kuendelea na majukumu yako bila ya kuwa na wasiwasi juu ya pesa yako. Hivyo, mfumo huu unafaa kwa vile utakufanya
husiwe na msongo wa mawazo na hivyo utakuwa na maisha halisi unayotamani kuwa
nayo kwa maana ya maisha yenye furaha.
2.
Watu wengi wanaigiza maisha ya utajiri wakati maisha
waliyonayo ni ya kimasikini. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika jamii watu
wanaishi maisha ambayo watu wanaowazunguka wanadhania kuwa wana maisha mazuri kumbe
ukitembelea akaunti zao hazina kitu na wala hawana kitega uchumi chochote
ambacho kina uhakika. Kumbe, kama unahitaji kuwa tajiri wa moja kwa moja
unapaswa kuishi maisha yako bila kujali mtazamo wa jamii inayokuzunguka. Fanya
kile ambacho kipo kwenye mpango wako wa utajiri bila kujali macho/maneno ya
wanaokuzunguka.
3. Kama unahitaji kuwa tajiri
hakikisha unajilipa kwanza katika kila shilingi inayoingia mikononi mwako. Somo
kubwa hapa ni kwamba ni lazima uweke mfumo wa moja kwa moja ambao utawezesha
kila shilingi inayoingia mkononi mwako inawekezwa kwa ajili ya kesho yako.
Hivyo, kabla ya kufanya mgawanyo wa kila fedha unayopata kupitia vyanzo
mbalimbali ni lazima ujilipe kwanza kwa kutenga asilimia flani ya pato lako kwa
ajili ya uwekezaji. Na hapa ndipo mwandishi anatushirikisha kuwa ni vyema
ukafungua akaunti maalum ya uwekezaji ili asilimia flani ya pesa unayopata
iingie moja kwa moja kwenye akaunti hiyo hata kabla ya kuingia mikononi mwako.
Hali hii itakuwezesha kugawanya kiasi cha pesa kinachoingia mikononi mwako bila
kugusa kiasi kilichowekezwa kwenye akaunti ya uwekezaji.
4. Siri nyingine ya kuwa tajiri
nikutofanya manunuzi ya aina yoyote ile kwa mkopo. Katika siri hii una chaguzi
mbili ambazo ni kununua kwa pesa taslimu (cash) au kutonunua kabisa. Pamoja na
siri ni kuhakikisha unanunua bidhaa iliyotumika lakini ikiwa bado ina ubora
badala ya kununua bidhaa mpya – mfano kununua gari kutoka kwa mtu badala ya
kwenda kununua “show room”. Pale
unaponunua kwa mkopo unajiweka kwenye hatari ya kuingilia matumizi ya pato lako
kabla hata halijaingia mkononi mwako. Pia, unaponunua kwa mkopo kuna hatari ya
kupandishiwa bei zaidi ya ile ambayo ungelipa kwa fedha taslimu. Aidha,
unaponunua bidhaa iliyotumika inakuwezesha kupata punguzo katika bei
ikilinganishwa na bei halisi ya bidhaa husika dukani.
5. Kama unahitaji kuwa tajiri ni
lazima uipende pesa yako kwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima. Hii ni pamoja
na kuhakikisha pesa ambayo ingetumika kwenye matumizi ya ovyo inatumika kufanya
mambo ya maana kwa maana yale yanayochangia kukuza utajiri wako. Na ni siri hii
mwandishi ndiyo anatushirikisha kuwa unahitaji kutumia “The Latte Factor” kwa maana pesa ambayo ungetumia katika matumizi
yasiyo ya lazima; moja kwa moja inatumika kukuza utajiri wako (angalia pointi
Na. 8). Kumbe unahitaji kutambua kuwa sio pato lako linalokufanya uwe tajiri
bali nini ufanya kutokana na pato lako bila kujali kama una kipato kikubwa au
kidogo kiasi gani. Utajiri ni maamuzi ambayo yapo akilini mwako yanasubiria
uchukue hatua.
6. Unatahitaji
kuwa na mfumo wa moja kwa moja na siyo kuwa na nidhamu ya pesa. Mwandishi
anatushirikisha kuwa hakuna kitu kigumu kama kuwa na nidhamu juu ya matumizi ya
pesa ambayo ipo mikononi mwako kutokana na vishawishi katika ulimwengu wa sasa.
Ili kufanikisha siri hii, mwanishi anatushirikisha kuwa ili uepukane na
matumizi ya ovyo ni lazima utengeneze mfumo wa moja kwa moja ambao utakufanya
husiwe na pesa mkononi kwa ajili ya matumizi ambayo hayana tija katika kufikia
utajiri wa ndoto zako. Kumbe siri zote hizi zinatukumbusha nguvu ya maamuzi na
umuhimu wa kuchukua hatua stahiki katika maisha ya kila siku. Hakika hauwezi
kufa masikini endapo umezitendea haki siri hizo.
7. Je
unahitaji kuwa tajiri? Naamini jibu lako ni ndio kama ndo hivyo basi mwandishi
anatushirikisha kuwa ni lazima uhakikishe matumizi yako yanakuwa madogo
ikilinganishwa na kipato. Kumbuka kuwa baada ya kutoa asilimia kwa ajili ya
uwekezaji (kujilipa) matumizi yako ni lazima yaendane na kiasi kinachobakia.
Kama matumizi yanazidi kipato chako hakika utajiri utakuwa ni ndoto kwako.
Mwandishi anatushirikisha kuwa kama unahitaji kuwa tajiri unahitaji kutenga
angalau asilimia 15 hadi 20 kwa ajili ya kujilipa kwanza kabla ya kuanza kulipa
matumizi mengineyo. Watu wengi wanashindwa kuwekeza kwa vile wanapoteza fedha
ambayo inaonekana kuwa ni ndogo katika vitu vidogo vidogo ambavyo si vya muhimu
katika maisha ya kila siku. Kumbe, unahitaji kutambua kuwa katika safari ya
utajiri hakuna pesa ndogo kwani unayoiona kuwa ndogo ikutumiwa vyema thamani
yake inaongezeka.
8. Je
upo tayari kuwa tajiri? Kama jibu ni ndiyo basi angalia ni matumizi yapi ya
fedha ambayo kila siku unafanya lakini si ya lazima au yanaweza kupunguzwa kwa
kununua kwa bei pungufu. Baada ya kutambua sehemu ambazo unaweza kuokoa pesa
basi hakikisha unajiwekea utaratibu wa kuwekeza hicho kiasi kidogo cha pesa
kila siku ya maisha yako bila kuacha kufanya hivyo. Hakika utaona maajabu ndani
ya mwaka wa kwanza. Maajabu haya yanatokana na muujiza wenye nguvu unaoitwa
ongezeko la riba (interest) kwa kila shilingi inayowekezwa. Mfano, kama umewekeza
1,000/= kila siku kwenye benki ambayo ongezeko la riba ni asilimia 10. Baada ya mwaka mmoja kiwango ulichowekeza
kitakuwa ni 1,000X30X12+1,000X0.1X30X12 = 396,000.00. Bila kuongeza
uwekezaji wowote hela hii ambayo kitaani inaitwa “buku” iliyowekezwa kwa mwaka mmoja tu katika kipindi cha
miaka 10 itakuwa imeongezeka kama ifuatavyo: 396,000.00+396,000.00X0.1X10 = 792,000.00. Fikiria kama umeendelea
kuweka buku kila siku ndani ya miaka 10 utakuwa na shilingi ngapi kwani hapo tumepigia
hesabu ya buku ile ya mwaka wa kwanza tu ikiwekezwa kwa kipindi cha miaka 10.
Naamini mpaka hapo rafiki yangu umeona nguvu ya buku halisi kuliko ile ambayo
umekuwa ukiambiwa na muhindi. Unaweza kupunguza matumizi kwenye vocha, soda,
sigara, chakula, bia, mishikaki, bodaboda, chips n.k hizo nimekusaidia tu
baadhi.
9. Mfumo
wa bajeti sio njia sahihi ya kukuwezesha kuwa tajiri. Mwandishi anatushirikisha
kuwa ni mara nyingi tumeambiwa kuwa ili uwe tajiri ni lazima uishi kwa
kuzingatia bajeti. Ukweli ni kwamba ni vigumu mno kuishi kwa bajeti na nyakati
nyingine inaweza kusababisha ugomvi ndani ya familia kwa sababu mmoja anaweza kumdu
kuishi kwa bajeti husika wakati mwenza wake hawezi kabisa. Mwandishi
anatushirikisha kuwa watu wengi wanashindwa kutumia pesa kulingana na mahitaji
ya bajeti yao kwa kuwa mfumo huu wa bajeti unamfanya mhusika kuwa mtumwa na
hivyo anakosa uhuru. Kumbuka kuwa tunatafuta utajiri ili kuwa na maisha yenye
furaha zaidi ya tuliyonayo sasa na maisha utumwa kamwe hayawezi kuwa na furaha
ndani mwake. Kumbe suruhisho la bajeti ni kuhakikisha wewe mwenyewe unaidhibiti
pesa yako na sio pesa ikuchanganye kiasi cha kufanya matumizi ambayo hayana uhalisia.
Bila kujali pesa ipo mfukoni au benki haupaswi kuitumia kwenye vitu ambavyo
havina tija na badala yake fanya manunuzi pale ambapo umekusudia kufanya hivyo.
10. Unaweza kupata utajiri kwa njia sita
tofauti ambazo ni: (a) unaweza kushinda kupitia mchezo wa bahati na sibu; (b)
unaweza kuoa au kuolewa na tajiri; (c) unaweza kushinda kesi ambayo itakufanya
uwe tajiri – kama ipo; (d) unaweza ukarithi utajiri wa ndugu zako; (e) unaweza
kuishi kwa bajeti – japo tumeona ni kazi ngumu; na (f) unaweza kupata utajiri
kwa kujilipa kwanza. Kati ya njia zote hizo mwandishi anatushirikisha kuwa
utajiri wa kweli ambao unatangenezwa na mhusika, njia ya kujilipa kwanza ndio
njia sahihi ambayo itakufikisha sehemu unayotaka kufika. Hata hivyo, njia hii
sio njia mpya kwani kama ni msomaji wa vitabu au mhudhuriaji wa semina utakuwa
umeisikia mara kwa mara. Sasa jiulize maswali haya: a) Je unajua kiasi gani
unatakiwa kujilipa kwanza? b) Je unatambua ni sehemu ipi sahihi ya kuwekeza
pesa hiyo unayojilipa? c) Je ni kweli kwa sasa unajilipa kwanza? na d) Je una
mfumo wa moja kwa moja wa kujilipa kwanza?
11. Mwandishi anatushirikisha kuwa kama
majibu ya maswali yote hapo juu ni NDIYO basi unastahili hongera kwa kuwa
tayari upo kwenye safari ya kuwa tajiri. Kama majibu yako baadhi au yote ni HAPANA
basi na wewe husikate tamaa kwa kuwa ndio maana unasoma makala kama hii kwa
ajili ya kubadirisha mfumo wa maisha yako. Ukweli ni kwamba watu wengi
hawajilipi kwanza japo wanahitaji kuwa matajiri jambo ambalo ni gumu mno labda
kama utajiri huo waupate kwa zari tu. Maana halisi ya kujilipa kwanza ni
kuhakikisha kila shilingi inayoingia mkononi mwako unatenga asilimia yake
kulingana na mpango wako wa kufikia utajiri na pesa hiyo unaiwekeza kwenye
akaunti maalumu ya uwekezaji. Mwandishi anatushirikisha kuwa kama unahitaji
kuwa tajiri hakikisha unajilipa asilimia 15 hadi 20 ya pato lako. Kama kiasi
hicho ni kikubwa kwa kuanzia unaweza kuanza na asilimili 5 kwa ajili ya
kujijengea nidhamu ya kujilipa kwanza.
12. Tunapima masaa halisi unayofanyia kazi
kwa ajili yako na wategemezi wako kwa kuangalia kiasi unachowekeza kwa kujilipa
kwanza. Mwandishi anatushirikisha kuwa kila tunachofanya iwe kazini au kwenye
biashara ni kwa faida ya mhusika mwenyewe na wategemezi wake. Je ni kwa kiasi
gani unatumia muda mwingi kufanya kazi kwa ajili yako na wategemezi wako?
Majibu ya swali hili yanapatikana kwa kugawanya kiwango ulichojilipa kwanza
dhidi ya masaa uliyofanya kazi. Mfano, chukulia ndani ya mwezi mmoja una masaa
240 ya kazi na umejilipa 50,000. Hivyo, masaa ambayo umefanya kazi kwa faida
yako na wategemezi ni sawa na 50,000/240 ambayo kwa kukadiria ni masaa 208
ndani ya mwezi mmoja. Kumbuka kama haukutenga chochote ni sawa na kwamba mwezi
mzima umeupoteza bila kujilipa wewe na wategemezi wako.
13. Fikiria kati ya makundi haya na chagua
moja ambalo linakufaa: (a) husijilipe kwanza, tumia zaidi ya pato lako, kopa
hela kwa ajili ya matumizi na endelea kuishi kwa mshahara husiyounga mwezi hadi
mwezi. Kwa dalili hizo wewe ni mtu ambaye kila siku utakuwa umepinda kiuchumi
na msongo wa mawazo juu; (b) njia ya umasikini – endelea kusoma kuhusu kujilipa
kwanza bila kuchukua hatua, endelea kutumia kila kinachoingia mikononi mwako
bila kuwekeza chochote huku ukiendelea kujisemea ipo siku ntakuwa tajiri bila
kuweka mpango wowote; (c) njia ya kuwa mtu wa pato la kawaida – jilipe kwanza
kati ya asilimia 5 hadi 10 ya pato lako; (d) Njia ya kuwa mtu mwenye kipato cha
juu – jilipe kwanza kati ya asilimia 10 hadi 15; (e) njia ya utajiri – jilipe
kwanza kati ya asilimia 15 hadi 20; na (f) njia ya utajiri kiasi kwamba unaweza
kustaafu umri wako ukiwa mdogo – jilipe kwanza angalau asilimia 20 na
kuendelea. Njia zote zipo kwa ajili yako na hivyo kuwa masikini wa kupindukia
au tajiri/milionea ni maamuzi yaliyopo mkononi mwako.
14. Weka mfumo wa moja kwa moja wa kujilipa
kwanza. Mwandishi anatushirikisha kuwa baada ya kuamua kujilipa kwanza kwenye
kila shilingi inayoingia mkononi mwako sasa unahitaji kutengeneza mfumo wa moja
kwa moja wa kujilipa ili pesa hiyo husishawishike kuipangia matumizi pale
inapoingia mikononi mwako. Mwandishi ametushirikisha mbinu mbalimbali ambazo tunaweza
kuzitumia kwa ajili ya kuwa na mfumo wa makato wa moja kwa moja kwa kiasi
ambacho tumeamua kujilipa kwanza. Hata hivyo, njia hizo nimeona kuwa katika
mazingira ya nchi yetu yawezekana hazipo hasa kwa wale ambao wamejiajiri. Somo,
kubwa ni kwamba iwe umeajiriwa au umejiajiri utaratibu wa kujilipa kwanza
unawezekana kabisa katika mazingira yetu. Kubwa ni kuwa na nidhamu ya
kutekeleza kile ambacho umekusudia kujilipa katika pato lako. Kwa yule ambae yupo tayari kufanya hivyo nitafungua
group la WhatsApp la “JILIPE KWANZA”. Tuma ujumbe kwenye namba +255 786 881 155
ukiomba kuunganishwa kwenye kundi hilo na nitakupa masharti ya kundi.
15. Kumbuka hakuna kesho, mwaka kesho au
nyakati zilizo bora zaidi ya sasa. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wengi
wanafanya makosa kwa kujisemea kuwa kwa sasa mambo yangu hayajakaa sawa hivyo
ngoja kwanza yakikaa sawa ndo nitaanza kutenga asilimia ya kujilipa kwanza.
Ukweli ni kwamba kama unahitaji kuwa tajiri ni lazima ufanye maamuzi magumu na
wakati sahihi wa kufanya maamuzi hayo ni sasa. Anza sasa na hakikisha kila
mwezi unatenga asilimia uliyojipangia kwa ajili ya kujilipa kwanza. Pia,
hakikisha kila shilingi inayoingia mkononi mwako unajilipa kwanza bila kujali
ni nyingi au kidogo. Hakika kwa kufanya maamuzi hayo hautojutia hata siku moja.
16. Wekeza pesa unayojilipa kwenye akaunti au
ambayo ina ongezeko la riba. Mwandishi anatushirikisha kuwa sifa kubwa ambayo
matajiri wanayo ni kuifanya pesa iwafanyie kazi badala ya wao kuifanyia kazi. Hata
nyakati ambazo wanakuwa wamelala pesa yao inakuwa inawafanyia kazi – huo ndio
utajiri wa kweli. Njia mojawapo wa kufanikisha hilo ni kuwekeza pesa sehemu
ambayo ina ongezeko la riba au thamani. Mfano, unaweza kuwekeza kwenye dhamana
za serikali (Government bond), Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja (UTT), fixed
account au kununua hisa. Lengo la kuwekeza katika sehemu hizo ni kwa ajili ya
kupata muujiza wa uwekezaji unaotokana na “Ongezeko la Riba”. Kumbuka kuwa njia
ya utajiri inayotafutwa hapa sio ya kulala masikini na kuamka tajiri bali ni
njia ya kutafuta utajiri kwa mpango maalum ambao ni wa muda mrefu. Ni kutokana
na muda huo ndipo utashangaa maajabu ya “ongezeko la riba” (angalia Na. 8).
17. Unaweza kuwekeza pesa unayojilipa kwenye mchanganyiko
wa makundi haya ya uwekezaji: (a) fedha taslimu (cash); (b) dhamana za
serikali; (c) hisa za makampuni (stocks); (d) uwekezaji wa mapato (miradi
mbalimbali); na (e) ukuaji wa uwekezaji (kujikta kwenye uwekezaji mkubwa zaidi).
Hata hivyo, mchanganyiko huo wa uwekezaji utategemea nyakati mbalimbali ambazo
unapitia kama vile: (i) kipindi cha maandalizi (kukusanya mtaji); (ii) kipindi
cha kutengeneza pesa; (iii) kipindi cha maandalizi ya kustaafu; na (iv) kipindi
cha kustaafu. Katika kila kipindi mahitaji yako na malengo ni tofauti hivyo
unahitaji mchanyiko mzuri wa makundi tofauti ya uwekezaji. Pia, mchanganyiko
huo wa makundi ya uwekezaji (fedha taslimu, dhamana za serikali na hisa)
utategemea na umri wako kwa wakati huo.
18. Mchanganyiko wa uwekezaji unaouchagua
(angalia Na. 17) unatakiwa kuzingatia hatari za uwekezaji. Hivyo, uwekezaji
wako unapaswa kuwa katika muundo wa umbo la piramidi (pembe tatu iliyogeukia
juu). Kwa maana kuanzia chini ya piramidi kwenda juu yake hatari za uwekezaji
zinaongezeka zaidi. Hii inamaanisha kuwa katika kipindi cha maandalizi
(kukusanya mtaji) unahitaji kuwekeza pesa unayojilipa kwenye sehemu yenye
usalama zaidi ambayo katika umbo la piramidi inakuwa ni kama msingi wa umbo. Mfano,
kwa hapa kwetu unaweza kuwekeza kwenye Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja au kwenye Akaunti
Maalum ya Uwekezaji – saving account). Kadri mtaji unavyoongezeka ndivyo
unahitaji kuchukua hatari zaidi kiuwekezaji kwa kupanda ya piramidi. Lengo la
kuwa na mchanganyiko wa uwekezaji ni kuepuka kuweka mayai yote katika kapu
moja.
19. Baada ya kujilipa kwanza sasa unatakiwa
kutenga hela kwa ajili ya dharura. Mwandishi anatushirikisha kuwa hakuna mwenye
uhakika na matukio ya baadae katika maisha yake. Ni kutokana na ukweli huo kama
“Automatic Millionaire” unatakiwa utenge fedha kwa ajili ya dharura. Lengo la
kufanya hivyo ni kulinda fedha unazojilipa zisijekutumika kwa ajili ya dharura
katika maisha yako ya baadae. Mwandhishi anashauri kuwa kiasi unachotenga
kinatakiwa angalau kiwezeshe kukidhi mahitaji yako yote katika kipindi cha kuanzia
miezi mitatu na kuendelea. Fedha hizi ni kwa ajili ya dharura kama vile kufukuzwa
kazi, umepata uremavu, magonjwa au kuunguliwa na nyumba. Baada ya kuchagua
kiasi unachotakiwa kutenga kwa ajili ya dharura sasa unatakiwa kukiwekeza
kwenye akaunti maalum ambayo pia ina ongezeko la riba na kama unaweza hakikisha
kinaingizwa kwenye mfumo wa makato ya moja kwa moja.
20. Miliki nyumba na hakikisha haidaiwi kodi kwa
maana kodi ya Serikali. Mwandishi anatushirikisha kuwa hatua kubwa katika
safari ya kuelekea kwenye utajiri ni kuhakikisha unamiliki nyumba unayoishi.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba pesa unayotoa kwa ajili ya kulipia kodi hakuna
siku hata moja ambayo itakuwezesha umiliki nyumba yako. Hii ni pesa ambayo ni
lazima kila mwisho wa mwaka au mwezi uitoe kwa mwenye nyumba na mwisho wa pango
haumiliki chochote. Mfano, kama unakaa
kwenye nyumba ambayo kodi ni Tshs. 200,000.00 kwa mwezi. Kwa mwaka ni Tshs.
2,400,000.00 ambayo katika kipindi cha miaka kumi ni Tshs. 24M. Pesa hii ni
nyingi kiasi kwamba ingekuwezesha kumiliki nyumba yako bila kujali ukubwa wake.
21. Wekeza kwenye nyumba za biashara kama
njia ya kutengeneza utajiri zaidi. Mwandishi anatushirikisha kuwa baada ya
kumiliki nyumba unayoishi sasa unatakiwa kumiliki nyumba za biashara ili pesa yako
ianze kukufanyia kazi. Kubwa ni kwamba nyumba ya biashara ni: (a) uwekezaji
ambao mtaji wake uonaongezeka thamani kila kukicha; (b) unapata faida kutokana
na uwepo wa wapangaji – malipo ya kodi; na (c) unaweza kuitumia kama dhamana
kwa ajili ya kupata fedha za wengine zikufanyie kazi. Faida hii ya tatu
inahusiana na kukopa benki ambapo unapewa fedha za wateja wengine ili uzitumie
kwa ajili ya kuwekeza zaidi.
22. Hakikisha unamaliza madeni yasiyo na
faida kama tayari unayo. Hii ni sambamba na kuhakikisha unakimbia mikopo yote
ya hasara ambayo umekuwa ukifanya bila kutambua athari ya mikopo hiyo kwenye
safari yako ya utajiri. Unahitaji kubadirisha tabia ya kununua kwa mkopo bila
kujali ukubwa wa mkopo husika. Mwandishi anatushirikisha kuwa mikopo mingi huwa
inasababishwa na wahusika kuishi maisha ya kuigiza kwa kutaka waonekane wapo
vizuri kuliko uhalisia wa kipato chao. Kumbe, baada ya kufahamu kuhusu siri hii
unachotakiwa kufanya ni kuishi kulingana na uwezo wa pato lako. Matajiri huwa
hawaishi maisha ambayo hayapo kwenye akaunti zao. Katika jamii wengi ambao
unadhania kuwa ni matajiri ukiuliza wanamiliki nini kwenye akaunti utagundua
kuwa hawana chochote zaidi ya nguo, viatu au gari la kifahari wanalotembelea.
23. Kumbuka kurudisha kwa jamii. Mwandishi anatushirikisha
kuwa mbinu zote zilizoshirikishwa hapa zinalenga kukusanya utajiri ambao kila
mmoja anatamani kuwa nao. Hata hivyo, maisha mengine ni lazima yaendelee kwa
maana haupaswi kuwa mchoyo kwenye jamii inayokuzunguka. Kumbuka unabarikiwa
zaidi kadri unavyotoa kwa wale wenye uhitaji. Tunahitaji kutambua kuwa
tunatafuta utajiri si tu kwa ajili ya kuwa na uhuru wa kifedha bali kwa ajili
ya kuendelea kuishi maisha yenye furaha ambayo yanaguswa na maisha ya jamii
inayotuzunguka. Kumbe, kuwa tajiri kisiwe kigezo cha kutokuwa na hisia dhidi ya
maisha ya wale ambao hawajabahatika kuwa matajiri badala yake tumia utajiri
wako kuifikia jamii zaidi kwa kadri uwezavyo. Utajiri wako uwe nyenzo ya kubadirisha
dunia hii kuwa mahala pazuri pa kuishi kwa viumbe vyote.
Haya ni machache ambayo nimebahatika
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Kwa ambao wamehamasika ushauri wangu ni kwamba husiishie
kuhamasika bila kuchukua hatua. Hakikisha unachukua hatua ya kwanza
kwa kuanzisha mpango wa kujilipa kwanza. KARIBU KWENYE KUNDI
LA “JILIPE KWANZA” ambapo kwa
pamoja tutaianza safari ya kuwa MILIONEA.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com
|