Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri.
Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya kufikia ndoto za maisha yako. Rafiki siku kadhaa
zimepita bila kukushirikisha maarifa ninayojifunza kwenye vitabu mbalimbali
hali ambayo imetokana na mwitikio mdogo wa usomaji wa makala ninazowashirikisha
kupitia barua pepe kwa wale ambao wamejiunga na mtandao huu. Ninakusudia
kufanya mabadiliko ambayo yatafanikisha kuendelea na watu wachache ambao ni
wasomaji wazuri wa makala ninazowashirikisha kupitia mfumo wa barua pepe.
Hata hivyo, kila ninapofungua mfumo wa
barua pepe pamoja na orodha ya wasomaji wa mtandao wa Fikra za Kitajiri najikuta
kwenye hali ya kuona kuwa nina deni la kuhakikisha nafanya jambo litakalopelekea
makala za uchambuzi wa vitabu zinakuwa endelevu kwa faida ya wale wanaojifunza
kutokana na makala hizo. Kwa ajili ya maboresho zaidi, naomba kupata
maoni/ushauri au shuhuda kwa namna ambavyo makala hizi zimekuwa msaada kwako
(tuma maoni/ushauri/ushuhuda kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com).
Kama bado haujajiunga na mtandao huu, BONYEZA HAPA na
jaza fomu kisha bofya “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu. Kwa
kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja
kwenye barua pepe.
Kijitabu
cha leo ni “A Note From A Friend” kutoka kwa mwandishi Anthony Robins. Anthony
Robins ni mwandishi, mshauri na mhamasishaji mahili katika kusaidia makundi
mbalimbali kwenye jamii kufikia ndoto za maisha yao. Kupitia kitabu hiki Robins
anatushirikisha dondoo muhimu ambazo kila mtu angependa kuzipata kutoka kwa
rafiki yake wa karibu. Dondoo hizi zinatoa faraja kwa wale ambao wanahitaji
ukumbusho kuhusu misingi mikuu ya ukweli wa maisha na namna ya kukabiliana na
changamoto za kila siku katika kufikia maisha ambayo mhusika anahitaji.
Karibu
tujifunze machache kati ya mengi ambayo Robins anatushirikisha katika kitabu hiki:
1. Njia rahisi ya kufikia furaha
ya maisha yako ni kuwasaidia wanaokuzunguka kufikia furaha ya kweli ya maisha
yao. Mwandishi anatushirikisha kuwa mara nyingi tunaishi maisha ya kichoyo
ambayo yanajikita kwenye hitaji la nafsi zetu na kusahau kuwa nafsi zetu zipo
kwa ajili ya ukamilisho wa maisha ya jamii inayotuzunguka. Kumbe ili kuwa na
furaha ya kweli katika maisha ya kila siku mwandishi anatushirikisha kuwa ni
lazima tuyatoe maisha yetu kwa ajili ya wengine. Kadri unavyojitoa kwa ajili ya
watu wenye uhitaji mkubwa ndivyo wanafarijika zaidi na kutambua kuwa wanapendwa
na jamii inayowazunguka.
2. Geuza changamoto zinazokukabili
kuwa fundisho na zawadi ya maisha kwa wengine sambamba na kupata furaha ya
kweli. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika maisha ni kawaida kupitia katika
nyakati za changamoto. Changamoto hizi zinapelekea mhusika kuwa kwenye mawimbi
ya kimaisha kwa maana ya kupanda na kushuka katika kila sekta ya maisha yake.
Hata hivyo, changamoto hizo pale zinapochukuliwa kama mlango wa somo la maisha
zinageuzwa kuwa fundisho kwa mhusika ikiwa ni pamoja na kuwa zawadi kwa jamii
inayomzunguka kupitia shuhuda mbalimbali na hivyo kuwa sehemu ya ukamilifu wa
furaha ya kweli katika maisha.
3. Kila
mwanadamu ana nguvu kubwa ndani yake na nguvu hiyo inao uwezo wa kubadilisha
kila sekta ya maisha ya mwanadamu pale tu inapotumiwa ipasavyo. Mwandhishi
anatushirikisha kuwa ni nguvu hii ambayo inaweza kumzawadia kila mmoja miujiza
ya kila aina katika maisha. Nguvu hii inapotumiwa ipasavyo itampa mhusika kila
aina ya mafanikio kuanzia mafanikio ya kiafya, kiuchumi, kimahusiano na hata
kiroho. Hata hivyo, ni wachache sana ambao wameweza kuitumia nguvu hii na hao
ndio ambao wamefanikiwa kimaisha. Mwandishi anatushirikisha kuwa hatua ya
kwanza ya kuitumia nguvu iliyopo ndani mwako ni kubadirisha fikra na mtazamo
wako na hatimaye kujiamini kuwa unao uwezo wa kutimiza kila ndoto uliyonayo
katika maisha.
4. Siri
kubwa ya mafanikio ni kufanya kazi kwa ajili ya kuwasaidia watu wanaokuzunguka.
Ni lazima uwe tayari kuongeza thamani vitu au hali inayokuzunguka kwa faida ya
jamii. Ni lazima uwe tayari kuwasaidia watu waishi ndoto za maisha yao kwa
maana ya kuwabadilisha kutoka kwenye maisha waliyozoea kuelekea kwenye maisha
ya kweli/ukamilisho kwani kila mwanadamu ameumbwa kwa ajili ya
kutimiza/kufanikisha kitu katika uhai wake. Hata hivyo, mwandishi
anatushirikisha kuwa hauwezi kusaidia wengine kubadilika kama wewe haupo tayari
kubadilika. Kumbe, ni lazima uishi ndoto za maisha yako na ndipo ujitoe zawadi kwa
ajili ya wengine.
5. Kuwa
na fikra chanya bila kuchukua hatua hakutoshi kukufikisha kwenye ndoto za
maisha yako. Mwandishi anatushirikisha kuwa kila mmoja ana ndoto za kuwa na
maisha bora yenye familia ya upendo, mafanikio kiuchumi, kiroho na hata kugusa
maisha ya wengine katika hali chanya. Hata hivyo, ni wachache wanaofanikisha
ndoto za matamanio yao kwa kuwa wengi wanaishia hatua ya kuwa na fikra pasipo
kuchukua hatua za makusudi zinazolenga kufanikisha ndoto hizo. Kumbe, ili
ufanikishe fikra zako ni lazima uwe na mkakati wa muda mrefu ambao ndani yake
kuna shughuli zinazonapaswa kutekelezwa hatua kwa hatua kila siku ya maisha yako.
Mkakati huu ni lazima ulenge kukubadirisha kifikra, mtazamo, mazoea pamoja na
matendo ambayo yamekuwa yakikuzuia katika kila sekta ya maisha yako. Kumbuka,
katika kila hali unapaswa kufikiria zaidi namna ya kutatua kila changamoto
kuliko kufikiria kukwamishwa na changamoto hizo.
6. Historia
haina nafasi katika mafanikio yako. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wengi
wanashindwa kuchukua hatua kwa vile walijaribu wakashindwa katika kipindi cha
nyuma. Hivyo, wengi wanaishia kusema SIWEZI. Kauli hii ni moja kati ya kauli
kandamizi ambazo zimedumaza maisha ya maelfu ya watu katika jamii nyingi. Kumbe,
katika kila hali unahitaji kutambua kuwa historia haina uhusiano na maisha yako
ya sasa au ya baadae endapo upo tayari kuchukua hatua stahiki za kukabiliana na
vikwazo au tabia kandamizi ambazo zimeyafanya maisha yako yawe jinsi yalivyo
kwa sasa. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika mabadiliko yoyote ya kimaisha
ni lazima uanze na kujiuliza ni yapi unaweza kufanya kwa wakati huo kwa ajili
ya kufanikiwa na sio kuangalia matukio yaliyopita.
7. Kiwango
cha uvumilivu ndio kinatofautisha kati ya waliofanikiwa na waliokata tamaa.
Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wengi wanakuwa wepesi wa kukata tamaa kwa
vile wanaishia kujaribu njia moja au zaidi na pale njia hizo zisipofanikiwa
wanaamua kuacha kabisa na kujisemea kuwa hawana bahati. Kumbe, ili ufanikiwe
kimaisha unahitaji kwanza kutambua ni nini unataka katika maisha yako na
kuhakikisha kila siku unachukua hatua madhubuti kwa nguvu zako zote pasipo
kukata tamaa hata kama matokeo yanakuwa hayaridhishi. Kumbuka, kila hatua
unayochukua inakupa uzoefu zaidi na uzoefu huo ndio silaha inayo kutofautisha
na wale wanaokata tamaa. Ni kutokana na uzoefu huo kila mara unaboresha kile
unachofanya kwa kuzingatia makosa au changamoto zinakuwa sehemu ya kujifunza
katika njia ya mafanikio. Husikubali kupoteza dira kwa vile jamii
inayokuzunguka haikubaliani na wazo lako kwani ni wewe pekee ambae unatambua maono
na lengo kubwa unalohitaji kufanikisha kupitia wazo hilo.
8. Uoga
wa kushindwa au kupoteza ni kikwazo kikubwa cha kufikia ndoto au malengo ya
maisha yako. Ukweli ni kwamba katika maisha ya kila siku tunakatishwa tamaa na
watu wanaotuzunguka kwani mara nyingi tunaambiwa kauli kama vile: haiwezekani,
sio rahisi kufanikisha hilo, huwezi kupata faida, utafilisika, utaibiwa na
kauli nyingine kama hizo. Kumbe, silaha kuu ambayo unahitaji kuwa nayo ni
kuamini kuwa hata kama kwa sasa hali inaonekana haiwezekani – wewe una nguvu ya
kipekee na upo tayari kuhakikisha unabadirisha kisichowezekana kuwa
kinachowezekana. Kwa nguvu hiyo na ujasili wa aina hiyo ni lazima ufike
unakotaka kufika kwani upo tayari kuchukua hatua bila kuogopa changamoto.
9. Uwezo
wa kufanya maamuzi sahihi na kwa muda muhafaka ndio kipimo cha mafanikio. Mwandishi
anatushirikisha kuwa nguvu ya maamuzi ndio injini ya mabadiliko. Ni kutokana na
ukweli huu, katika maisha tunatakiwa kutambua kuwa hatuwezi kubadirisha au
kuzuia matukio yasiyo rafiki kwa maisha yetu ya kila siku. Hata hivyo, tuna
uwezo wa kudhibiti fikra, imani, hisia na vitendo vyetu kuhusiana na matukio
hayo. Kila sekunde ya maisha yetu tunajikuta kwenye mtihani wa kufanya chaguo
sahihi au kuchukua vitendo sahihi kati ya mbadala iliyopo. Kumbe, kila mmoja na
ana nguvu ya kufanya maamuzi na maamuzi anayofanya katika kila tukio ndio
yanaamua mafanikio au kutofanikiwa katika maisha. mapya.
10. Upo jinsi ulivyo kutokana na maamuzi
uliyochagua kutumia muda mwingi katika kufikiria, kuhisi, kujishughulisha,
kula/kunywa, kuamini au kujifunza katika maisha yako ya kila siku. Kumbe,
tunahitaji kujifunza kuwa mafanikio tunayohitaji tunayaandaa au kuyaharibu
wenyewe kutokana na maamuzi tunayofanya katika kila sekunde ya maisha yetu.
Kama tunahitaji kubadilika ni lazima kwanza tujifanyie tathimini inayolenga
kutambua vikwazo vinavyotuzuia na hatimaye kuanza kuchukua hatua mpya
zinazolenga kutuondoa kwenye tabia za zamani na kuingia kwenye mabadiliko. Na
hapa ndipo tunakiwa kufanya maamuzi ya dhati ambayo yatafanikisha mabadiliko ya
moja kwa moja. Ni lazima kutambua ni sadaka ipi tupo tayari kutoa kupitia muda,
mapenzi, nguvu, rasilimali na hata kazi zetu kwa ajili ya kuhakikisha tunaingia
kwenye ulimwengu mpya wa mafanikio bila kukata tamaa au kufikiria kurudi nyuma.
11. Maamuzi maamuzi maamuzi – maamuzi
sahihi. Mwandishi anatushirikisha kuwa njia pekee ya kubadilisha maisha yako ni
kufanya maamuzi sahihi na maamuzi hayo ndio yatakufanya uonekane una bahati
sana baada ya kufanikiwa. Hapa mwandishi anatushirikisha kuwa maamuzi sahihi ni
yale ambayo yatakulazimisha kuachana na mbadala zote na kubakiwa na njia ambayo
umejiridhisha kuwa itakufikisha kwenye mafanikio ya kweli. Na hakikisha kila
siku fikra zako zinajikita kwenye maamuzi uliyofanya. Ili kufikia kilele cha
mafanikio unayohitaji mwandishi anatushirikisha kuwa ni lazima:-
- Utambue au kuchagua ni nini hasa unahitaji kufanikisha;
- Uchukue hatua stahiki kwa muda muhafaka;
- Fanya tathimini ya mara kwa mara ili kutambua kama hatua unazochukua zinafanya kazi au hazitekelezeki kwa ajili kufanikisha lengo kuu;
- Endelea kufanya maboresho ya hatua unazochukua;
- Kuwa mvumilivu bila kukata tamaa wala kuyumbishwa mpaka pale utakapofanikiwa.
12. Kuna nguvu kubwa inayodhibiti au kuamua
nguvu ya maamuzi yako nayo si nyingine bali ni IMANI. Ukweli ni kwamba imani
yako ndio inaamua: ni yapi unaweza kufanikisha na yapi hauwezi kufanikisha;
yapi unaweza kufanya na yapi hauwezi kufanya; yapi utatazama na yapi
hayataonekana machoni pako; hisia zipi zikutawale na zipi uachane nazo; sehemu
zipi uwekeze na sehemu zipi husiwekeze na mengine mengi. Unapojenga imani kwenye
tukio au hali yoyote ile moja kwa moja unafanya ubongo wako ufungue au kufunga
milango kuhusiana na tukio au hali husika. Kumbe, imani ulizonazo kukuhusu wewe
mwenyewe na yale unayoweza kufanikisha ndicho kipimo cha mafanikio unaweza
kufikia katika maisha. Muhimu ni kuhakikisha unabadilisha imani ulizonazo ili
ziendene na ndoto za maisha yako.
13. Je IMANI ni nini hasa katika maisha
yetu ya kila siku? Mwandishi anatushirikisha kuwa imani ni kuwa na UHAKIKA juu
ya hali au tukio linalosadikika. Unapokuwa na uhakika juu ya hali au tukio
unakuwa umefungua mlango wa kubadilisha hali/tukio kutoka kwenye hali ya
kusadikika hadi kwenye hali ya uhalisia. Kwa maana nyingine imani inawezesha
kuumbika kwa vitu ambavyo awali havikuwepo kwenye maisha yako. Kumbe tunapokosa
UHAKIKA wa matukio au mafanikio ndani mwetu moja kwa moja tunajiondoa kwenye
ushindani kupitia imani tulizonazo. Athari ya kutokuwa na uhakika ndani mwetu
ni kushindwa kutumia nguvu kubwa iliyopo ndani mwetu ambayo ina uwezo wa
kutenda miujiza ya kila aina katika maisha yetu.
14. Msingi wa imani ni wazo kwa maana imani
zinajengwa na mawazo. Kwa maana hiyo ili tuwe na uhakika wa matukio au hali
tunazotarajia katika maisha yetu ni lazima tuanze na tathimini ya mfumo wa
mawazo yetu. Ni kutokana na ukweli huu sisi zao la yale tunayowaza muda mwingi
kwani mawazo hayo ndiyo yanajenga imani tulizonazo na hatimaye imani hizo ndizo
zinatupa uhakika wa yale tunayoweza kufanikisha katika maisha. Kumbe, kama
tunahitaji kubadilisha imani tulizonazo ni lazima kwanza tubadilishe mfumo wa
mawazo ambao pia ni lazima uende sambamba na kubadilisha matendo au uzoefu
ambao umepelekea tuwe na mawazo ya aina hiyo.
15. Watu wengi wanahitaji mabadiliko lakini
wanaofanikiwa kubadilika ni wachache. Mwandishi anatushirikisha kuwa njia rahisi
ya kufanikiwa kubadilika kiujumla ni kunabadilisha fikra zako ikiwa ni pamoja
kuhakikisha fikra zako zinatawaliwa na mambo ambayo ni muhimu katika kufikia mabadiliko
unayohitaji. Mwandishi anatushirikisha kuwa unaweza kuwa na hisia za uzuni kwa
kumbuka/kufikiria tukio ambalo lilikuhuzunisha siku za nyuma. Vivyo hivyo,
unaweza kuwa na furaha kwa kufikiria au kuwaza tukio ambalo lilikufurahisha.
Ndivyo, ilivyo hata kwenye mabadiliko ya kweli, kwa maana kama unahitaji
kubadilisha maisha yako ni lazima ujikite kwenye mawazo na fikra ambazo
zitapelekea kufanikisha mabadiliko unayohitaji katika maisha. Ni kutokana na
ukweli huu, unatakiwa kuhakikisha unajikita kwenye yale yaliyopo ndani ya uwezo
wako wa kufanya/kudhibiti na kuachana na yaliyo nje ya uwezo wako.
16. Njia nzuri ya kuendelea kwenye fikra
muhimu kwa ajili ya mafanikio unayohitaji ni kujenga utaratibu wa kujiuliza
maswali kila mara. Maswali sahihi yana majibu sahihi juu ya kile tunachohitaji
kukamilisha katika maisha yetu. Je maswali sahihi ni yapi? Mwandishi
anatushirikisha kuwa maswali sahihi ni yale ambayo hayana malalamiko na badala yake
yanajikita kwenye kutafuta majibu juu ya changamoto zinazotukabili. Hata
maandiko yanasema “Omba na mtapewa” – hivyo maswali ni mojawapo ya njia
inayosaidia kufikia kwenye matumizi ya kweli ya ile nguvu iliyopo ndani mwetu.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba kila unapojiuliza maswali sahihi unapata
majibu ambayo yanakupa mtazamo mpya kuhusiana na tatizo lililopo mbele yako. Unahitaji
kuwa na muda wa kijiuliza maswali pale unapoianza siku asubuhi mara baada ya
kuamka na usiku kabla ya kulala.
17. Hisia zina nafasi kubwa juu ya
mwonekano wa kila mmoja wetu – mfano, kama unatawaliwa na hisia za huzuni mara
nyingi utaonekana kuwa mtu wa huzuni machoni pa jamii inayokuzunguka. Hata
hivyo, hisia zinatokana na matendo tunayojihusisha nayo katika maisha yetu ya
kila siku. Kwa maana nyingine kuna uhusiano mkubwa kati ya vitendo vya mwili na
hisia zako. Kumbe, kama unahitaji kutawala hisia mbaya ndani mwako huna budi
kutawala matendo ya mwili wako. Badilisha namna unavyotembea, unavyoongea,
unavyocheka, unavyokaa na kila tendo ambalo unatamani uwe nalo kulingana na
mafanikio unayotaka. Hakika nguvu kubwa iliyopo ndani mwako itakufanya
ubadilike na kuingia kwenye hisia na mawazo ya mafanikio zaidi. Hapa ndipo
unahitaji kuwa na watu ambao unatamani kufikia mafanikio yao (role models).
18. Zungumza lugha ya mafanikio. Kumbuka
kuwa maneno unayonena dhidi ya nafsi yako yana athari kubwa katika mafanikio
kutokana na ukweli kwamba maneno yanaumba. Maneno tunayonena mara kwa mara
yanaathiri mfumo wa fikra na hivyo jinsi tulivyo (kihisia na kivitendo) ni
matokeo ya maneno tunayonena dhidi ya nafsi zetu. Mfano, kama ukisema nina
hasira sana, moja kwa moja hisia za hasira zitakutawala na matokeo yake
utafanya vitendo vinavyoendana na hisia hizo. Somo kubwa hapa mwandishi
anatufundisha kuwa mara zote tunakiwa kuwa makini na maneno au misamihati
tunayotumia dhidi ya nafsi zetu. Chagua misamihati ambayo inakupa tulizo la
nafsi kulingana na hali inayokukabili au chagua misamihati inachochea kutumia
nguvu kubwa iliyopo ndani mwako katika kufikia mafanikio unayotaka.
19. Tumia misamihati ambayo inajenga picha
bora katika mfumo wako wa akili. Mwandishi anatushirikisha kuwa kila misamihati
tunayotumia katika maisha yetu ya kila siku inajenga picha chanya au hasi
katika akili zetu. Picha hizo ni alama ambazoo zinatafsiliwa kwa ajili ya
kutupa nguvu ya kuumba au kubomoa. Mfano, tafsili sentensi hizi: (a) Maisha ni
mapambano; na (b) Maisha ni mchezo. Sentensi ya kwanza inakufanya siku zote
uyaone maisha ni sehemu ya kupambana kana kwamba upo vitani siku zote. Kumbuka katika
uwanja wa vita hakuna furaha hivyo maisha yako daima hayawezi kuwa na furaha. Sentensi
ya pili inaonesha umuhimu kufurahia maisha kwa kuona mema yaliyomo ndani yake. Kumbuka
mchezo ni kati ya matukio ambayo kila mmoja anaburudika. Hivyo, kwa kuyatazama
maisha katika picha hiyo mhusika atakuwa na mengi ya kufurahia kwenye kila
hatua maisha yake.
20. Kumbuka kila nyuma ya misamihati
unayotumia kuna imani ndani yake. Mwandishi anatushirikisha ubaya au uzuri wa
misamihati tunayotumia ni kuendena na imani zinazotuongoza kwenye maisha yetu. Kumbe,
tunachohitaji kufahamu ni kwamba misamihati inaunda imani na imani hizo ndizo
zinakuwa mwongozo wa maisha yetu katika njia chanya au hasi kulingana na
misamihati husika.
21. Tambua kuwa katika maisha hakuna mwenye
alama ya bahati nzuri au mbaya. Mwandishi anatushirikisha kuwa mafanikio ya namna
yoyote ile yanaanza na mhusika kutambua ni nini hasa anahitaji kufanikisha na kisha
kuweka malengo ya kufika kule anakokusudia. Hapa ndipo unapaswa kujiwekea lengo
la kuwa bora kuliko wote katika tasnia uliyoichagua. Hata hivyo, unahitaji
kukumbuka kuwa kuweka lengo tu hakutoshi kwani ni lazima lengo hilo liwe na
vitendo madhubuti vinavyomlazimisha mhusika kuchukua hatua kila mara. Kumbe,
kila mara unahitaji kujikumbusha kuwa hakuna bahati kwani bahati inatengenezwa
na mhusika kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa kwenye tasnia alioichagua.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Lengo langu ni kuona kila kitabu
ninachokushirikisha kinawaafikia watu zaidi ya elfu moja. Nisaidie kusambaza
ujumbe wa kitabu hiki kwa ndugu na marafiki kwa kadri uwezevyo. Kumbuka umepata
ujumbe wa kitabu hiki bila malipo yoyote sasa kwa nini husindwe kuwashirikisha
wengine bila gharama yoyote. Wote tumeumbwa ili kuibadirisha dunia hii kuwa
mahali pazuri pa kuishi hivyo kuwa sehemu ya kuleta mabadiriko hayo (Unaposambaza
makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link). Nakutakia
mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com
|