Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri.
Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa
FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa
ni wiki ya 38 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi
wa vitabu mbalimbali kwa ajili ya kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako
kuyatumia ili ubadilishe kila sekta ya maisha yako.
Makala hizi za uchambuzi wa vitabu
zimekuwa zikikufikia kila wiki kwa kadri ambavyo napata muda wa kukushirikisha
kile ninachojifunza kutoka kwenye vitabu vya maarifa mbalimbali. Ni matarajio
yangu kuwa muda ninaotumia kushirikisha uchambuzi wa vitabu umekuwa wa msaada
mkubwa kwako katika kubadilisha maisha yako. Hata hivyo, mtandao huu bado
unahitaji maoni/ushauri au shuhuda kwa namna ambavyo umekuwa wa msaada kwako au
namna ambavyo unahitaji makala hizi ziboreshwe zaidi (tuma
maoni/ushauri/ushuhuda wako kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com).
Ili uendelee kunufaika na makala za
mtandao huu BONYEZA HAPA na
ujaze fomu kisha bonyeza “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu.
Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja
kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kijarida
cha wiki hii ni “Starting Your Own
Business” kutoka
kwa EY. EY ni shirika linalotekeleza shughuli zake kwenye mataifa mbalimbali na
hivyo ni shirika la kimataifa linalojihusisha na utoaji wa huduma za ushauri
kwenye mambo ya viwango, kodi, miamala na shauri mbalimbali kwenye sekta ya
biashara na masoko ya mitaji.
Linapokuja
suala la kuanzisha biashara hasa kwa wajasilimali wadogo changamoto zimekuwa ni
nyingi ambazo baadhi kwa kutaja huwa ni kukosekana kwa mtaji wa kuanzisha
biashara husika, uhakika wa kushindana kwenye soko na uhakika wa wazo bora la
biashara. Kupitia kijarida hiki tunashirikishwa dondoo muhimu za kuzingatia wakati
wa kuanzisha biashara yako ili uweze kukabiliana na changamoto hizi na hatimaye
biashara yako iweze kuwa na mafanikio.
Karibu
tujifunze wote machache niliyojifunza kwenye hiki:
1. Tambua hamasa/shauku yako. Mwandishi
anatushirikisha kuwa kuanzisha biashara ni sawa na kuanzisha familia kutokana
na ukweli kwamba unahitaji kuwekeza muda, kufanya kazi kwa bidii pamoja na uwekezaji
wa kifedha. Vyote hivi vinahitaji dhamira ya kweli kutoka ndani mwako hivyo
kama hauna hamasa/shauku ya kutosha juu biashara husika itakuwa vigumu sana
biashara nhiyo kukua. Kwa kifupi ni kwamba unahitaji una pendo wa hali ya juu
kwenye biashara yako.
2. Tafsiri wazo lako kwenye mpango
wa biashara. Mpango wako wa kibiashara unakuwa ni dira ya kukuongoza kwa ajili
ya kufikia mafanikio unayohitaji. Mpango huu unapaswa kuonesha malengo ya
baadae ikiwa ni pamoja na hatua utakazofuata kwa ajili ya kufikia malengo
husika. Pia mpango huu kama umeandaliwa vyema unaweza kutumika kwa ajili ya
kukuza mtaji kutoka kwa wafadhiri au taasisi za kifedha ikiwa ni pamoja kutumia
mpango huu kwa ajili kusambaza bidhaa zako kwenye soko.
3. Hakikisha mpango wako wa kibiashara
una sehemu kuu nne. Sehemu ya kwanza ni maelezo ya utangulizi – sehemu hii
inatoa picha ya kampuni au biashara yako ufupi; sehemu ya pili ni makadirio ya
kifedha – hii ni sehemu kwani inaonesha namna ambavyo fedha zitaingizwa na
kuzalisha faida. Sehemu hii ndiyo inatazamwa zaidi na wafadhiri au taasisi za
kifedha kama unahitaji kukopeshwa mtaji. Sehemu ya tatu ni utawala/uendeshaji
wa biashara yako – hapa unahitaji kuonesha aina ya watu ambayo wanatakiwa kwa
ajili ya kuendesha biashara kwa ufanisi; na sehemu ya nne ni mkakati wa kuingia
kwenye soko – sehemu hii inaonesha mbinu ambazo utatumia kuingiza bidhaa/huduma
zako kwenye soko.
4. Kabla ya kuanzisha biashara hakikisha unafanya
tafiti juu ya wazo lako la biashara ili uwe na taarifa sahihi zinazoendana na
nyakati pamoja na sehemu husika. Taarifa hizi unaweza kuzipata kupitia semina
za biashara, sehemu za masoko/biashara zinazozunguka eneo husika, maonyesho ya
biashara, sehemu za viwandani au kwenye mitandao ya kijamii.
5. Tambua
wapinzani wako wa karibu kwenye soko. Kwanza unahitaji kutambua kuwa washindani
wako kibiashara sio maadui wako bali ni sehemu ya kujifunza mbinu zipi
zimefanikiwa na zipi zimeshindwa kufanya kazi. Hii itakusaidia kuboresha mbinu
zako kwa ajili ya kutoa huduma ambayo imeboreshwa ikilinganishwa na wapinzani
wako. Taarifa za wapinzani wako unaweza kuzipata kupitia kwenye mitandao,
semina za biashara, tafiti mbalimbali kuhusu bidhaa/huduma zinazotolewa na
wapinzani wako.
6. Tambua
umuhimu wa kutumia mindao ya kijamii kama vile facebook na twitter kwa ajili ya
kupata taarifa sahihi kuhusu bidhaa/huduma unayokusudia kuitoa. Mitandao ya
kijamii ni sehemu isiyo rasmi kwa ajili ya kufanya tafiti mbalimbali
zinazolenga kuboresha bidhaa/huduma unayokusudia kuitoa kulingana na wazo lako
la biashara. Pia unaweza kutumia mitandao ya kijamii kufahamu mahitaji ya
wateja katika soko linalokuzunguka.
7. Tafuta
mwalimu/mshauri wako wa kibiashara. Mshauri wa biashara ni mtu muhimu kwa mtu
anayeanzisha biashara kwa kuzingatia kuwa mshauri anakuwa tayari ana uzoefu wa
kutosha katika sekta ya biashara. Msahauri huyu anahitaji kumpa mwanga pamoja
na mwongozo mjasiliamali anayeanza safari yake ili akabiliane na mawimbi ya
kibiashara. Ushauri huu utakusaidia kuepukana na makosa ya kibiashara ambayo
yanaweza kupelekea upoteze mtaji wako.
8. Tafuta
mashindano ya wajasiliamali kupitia kwenye wazo bora la biashara ambayo unaweza
kuyatumia kwa ajili ya kushindanisha mpango wako wa kibiashara. Mbinu hii
inaweza kukusaidia kupata mtaji pale unapofanikiwa kushinda. Pia, kuwa macho
kuangalia mipango ya serikali ambayo inatoa michango ya kimtaji au elimu au
udhamini kwa wajasiliamali chipukizi katika kupata mitaji kupitia mikopo yenye
riba nafuu.
9. Kusanya
mtaji wa kutosha kwa ajili ya kuanzisha biashara yako. Hii ni changamoto ambayo
inawafanya wajasiliamali wengi washindwe kusonga mbele kutokana na changamoto
ya kukosa mtaji. Hata hivyo, kama una nia ya kweli haupaswi kukata tamaa kwani
kuna njia nyingi za kupata mtaji. Njia mojawapo ambayo kila mtu anaweza
kuitumia ni kuwa na nidhamu ya fedha kwa kuhakikisha kuwa kila shilingi
inayoingia mkononi mwako unatenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kufanikisha
uwekezaji wako. Kumbuka kuwa unaweza kuanza na biashara ya mtaji mdogo ambao
unaumudu kwa ajili ya kukuza mtaji. Kuwa tayari kufanya biashara yoyote hata
kama ni kuuza matunda, mkaa, n.k.
10. Njia nyingine za kupata mitaji ni
kupitia kwenye mikopo ya vijana, sapoti ya kiuwekezaji kutoka kwa wawekezaji
wakubwa, mikopo ya taasisi za kifedha au michango kutoka kwa ndugu na marafiki.
11. Siri ya kufanikiwa kibiashara ni
kuanzisha biashara pasipo kujali ukubwa wa biashara husika. Mwandishi anatushirikisha
kuwa unapoendelea kuahilisha kuanzisha biashara yako kutokana na changamoto za
kimtaji ndivyo unapoteza fursa ya kujifunza mengi kuhusu biashara. Unahitaji kuanzisha
biashara hata kama ni ndogo kwa ajili ya kufahamu undani wa biashara na jinsi
ya kukabiliana na changamoto zake.
12. Tengenza mkakati wa kukuza biashara
yako. Baada ya kuanzisha biashara hata kama ni ndogo changamoto iliyopo mbele
yako ni namna ya kukuza biashara husika. Hii ni kutokana na ukweli kwamba
ukuaji wa biashara ni ufunguo wa fursa mpya na mafanikio ya mjasiliamali. Kama biashara
ilikuwa inaendeshwa na mtu mmoja sasa unahitaji kufikiria kuongeza idadi ya
watendaji kwa ajili ya kufikia wateja wapya au kuongeza bidhaa/huduma mpya. Hii
itakusaidia kukupunguzia mzigo pamoja na kupata muda wa zaida wa kukuza bishara
husika.
13. Toa ajira kwa ajili ya kuongeza timu ya
wafanyakazi. Hakikisha unakuwa makini katika kuajiri ikiwa ni pamoja na
kuzingatia vigezo/sifa za aina ya watu unaowaajiri. Hakikisha waajiriwa wako
wanakuwa ni sehemu ya biashara yako ili kupitia utendaji wao biashara izidi
kukua zaidi.
14. Pia, hakikisha timu yako ina watu wa
kada mbalimbali kama vile watu wa teknolojia ya mawasiliano (IT), sheria,
masoko, utawala, wahasibu au kada nyinginezo kwa kutegemea aina ya biashara
yako. Unahitaji kuhakikisha kila mmoja kwenye timu anafahamu dira ya biashara
yako na kila mmoja ashiriki kufikia maono ya biashara hiyo. Hii itakusaidia
kuongeza mawazo mapya kutoka kwa waajiriwa wako na hivyo kuongeza wigo wa kutanua
biashara yako.
15. Shirikisha timu yako ya wafanyakazi
mpango wako wa biashara wa awali. Nia ya kufanya hivi ni kuangalia ni mbinu zipi
zimefanikisha maenedeleo ya biashara husika na mbinu zipi ambazo hazikufanya
kazi kwa tija zaidi. Pia hatua hii itakufanikisha kuangalia kama kuna mikakati
ambayo haijafanyiwa kazi na kwa sasa ikifanyiwa kazi itapelekea ukuaji wa
biashara kwa tija zaidi.
16. Fanya kazi na watu makini na wenye
taaluma sahihi. Watu hawa kila mmoja anatakiwa afahamu wajibu wake na pale
inapotakiwa kushauri atoe ushauri wa kitaaluma ambayo utapelekea ufanisi wa
biashara. Pia kila mmoja anatakiwa ajione kuwa sehemu ya umiliki wa biashara
husika. Hali hii itakufanya uwe na timu ya watu wenye kariba/lengo moja na
hivyo kuwa na nafasi kubwa ya kukuza biashara yako.
17. Jenga utamaduni wa kutuza (reward)
ubunifu wa mawazo mapya yanayotolewa na timu yako. Hali hii itawafanya
wafanyakazi wako wawe na hamasa ya kutafuta mbinu mpya za uzalishaji au
usambazaji wa bidhaa.
18. Muda wote kuwa macho kwenye
bidhaa/huduma zako kwa kuendelea kuzalisha kwa viwango vya hali ya juu. Hali hii
itakufanya uendelee kuwa juu ya washindani wako kibiashara na hivyo kuendelea
kuliteka soko. Pia, unahitaji kuendelea kufanya tafiti za kama kuna njia
mbadala ya kuwaridhisha wateja kupitia bidhaa zako kwa mbinu tofauti za
uzalishaji na usambazaji wa bidhaa/huduma.
19. Wekeza kwenye teknolojia mpya ya
uzalishaji au usambazaji. Muda wote lenga kwenye teknolojia ambayo ni rahisi na
inaweza kupunguza muda pamoja na gharama za uzalishaji au usambazaji wa
huduma/bidhaa zako. Hii itakusaidia kuzalisha/kusambaza kwa muda mfupi na kwa
gharama nafuu na hivyo kuokoa muda na fedha kwa ajili ya kuwekeza sehemu
nyingine.
20. Tengeneza mitandao na taasisi sahihi. Tasisi
hizi ni sehemu ya kupata taarifa za ndani ambazo ni muhimu kwa ajili ya fursa
mpya za uwekezaji. Tasisi hizi zinaweza kuwa taasisi za kifedha kama benki,
taasisi za masoko ya mitaji (soko la hisa), taasisi za bima na mashirika ya
serikali.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
|
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com