Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri.
Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa
FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa
ni wiki ya 29 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi
wa vitabu mbalimbali kwa ajili ya kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako
kuyatumia ili ubadilishe kila sekta ya maisha yako.
Ni matumaini yangu kuwa makala hizi
zimekuwa na msaada mkubwa kwako kwa kadri ambavyo umekuwa ukichukua hatua za
kubadilisha maisha yako. Hata hivyo, makala hizi haziwezi kubadilisha chochote
kama umekuwa mtu wa kusoma na kutokufanyia kazi yale unayojifunza.
Ili uendelee kunufaika na makala za
mtandao huu BONYEZA HAPA na
ujaze fomu kisha bonyeza “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao wa
fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa
humu moja kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kupata
uchambuzi wa kitabu cha The Rules of Money (Kanuni 107 za Kutengeneza pesa na
kuwa tajiri) BONYEZA HAPA
Kitabu
cha wiki hii ni “Procrastinate on
Purpose” kutoka
kwa mwandishi Rory Vaden. Rory Vaden
ni mwanaharakati wa mafanikio ambaye anaongozwa na nidhamu binafsi na uadilifu
katika kutimiza majukumu yake. Mwandishi huyu ni mkufunzi (kocha), mzungumzaji
wa kimataifa na mshauri ambaye amejikita kwenye maono ya kuwaongoza watu ili
waishi maisha yaliyojikita kwenye msingi wa nidhamu binafsi. Mwandishi anatumia
uzoefu alionao katika biashara zake kuwashirikisha mamia ya watu ili wafikie
mafanikio ya ndoto zao.
Muda
ni rasilimali ambayo watu wotu wote tumepewa sawa. Yaani kila mtu kwa siku
anapewa masaa 24 ambayo ni sawa na dakika 1,440 ambazo ni sawa na sekunde
86,400. Hivyo, kila kukicha kila mmoja ambaye yu hai anapewa sekunde hizo ndani
ya masaa 24 na yeye ndo mwamuzi mkuu wa nini afanye katika kila sekunde.
Tunasema
muda ni rasilimali kutokana na ukweli kwamba yale tunayofanya katika kila
sekunde ya maisha yetu ndiyo yanaamua nafasi ya mafanikio yetu. Kutokana na
muda kutumiwa visivyo katika makundi ya watu kwenye jamii ndio maana tunaweza
kutofautisha mafanikio ya watu ndani ya jamii moja. Wale wanaotumia muda wao
kufanya mambo ya maana wamefanikiwa kupiga hatua kubwa ya mafanikio katika
maisha yao ikilinganishwa na wale ambao wanatumia muda wao kufanya mambo ya
hovyo.
Hata
hivyo watu wengi wameendelea kulalamika kuwa muda hautoshi kwa ajili ya
kukamilisha majukumu yao siku pengine kwa vile hawajatambua njia nzuri ya
kupangilia vizuri muda wao. Mwandishi Rory Vaden anatumia kitabu hiki
kutushirikisha njia bora ambazo kila mtu anaweza kutumia kwa ajili ya kuboresha
matumizi ya muda wake.
Karibu
tujifunze wote machache niliyojifunza kwenye hiki:
1. Tofauti
kubwa iliyopo kati ya watu waliofanikiwa na watu wa kawaida ni uwezo mkubwa wa
kufikiri walionao watu wenye mafanikio ikilinganishwa na watu wa kawaida.
Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wenye mafanikio makubwa wanatambua na
kuishi msingi huu “ili uweze kutoa matokeo makubwa unahitaji kufikiri nje ya boksi”. Kutokana
uwezo wa kuishi msingi huu, watu wenye mafanikio wanatumia kila sekunde ya
maisha yao kwa ajili ya kuzalisha matokeo makubwa kwenye majukumu yao ya kila
siku.
2. Kukosekana
kwa vipaumbele ni mfumo mpya wa kupoteza muda. Mfumo huu hauna tofauti na watu
wanaopoteza muda kutokana na uzembe au uvivu wa kufanya kazi. Mfumo huu
umesababisha kupoteza muda mwingi wa kuzalisha katika sehemu za kazi kama vile
viwandani, ofisi za serikali au sekta binafsi na matokeo yake ni upotevu wa
rasilimali muda ambayo inapelekea kampuni au serikali kukosa mapato ya kutosha.
Hali hii inapelekea mtu kujiona kama vile kadri anavyozidi kupigana kufanya
kazi ndivyo anazidi kurudi nyuma au ndivyo kazi zinazidi kuwa nyingi zaidi.
Watu wa namna hii wanafanya kazi kwa presha kubwa kwa ajili ya kukamilisha
majukumu yaliyopo mbele yao huku muda wote maisha yao yakitawaliwa na msongo wa
mawazo wa kujiuliza ni lini watapata muda huru kwa ajili ya kufurahia maisha
yao.
3. Epuka
ubize wa muda wote ambao hauna tija au tija yake ni ndogo. Mwandishi
anatushirikisha kuwa ni kawaida watu wengi kusema wapo bize muda wote na
matokeo yake ni kwamba ukifanya tathimini ya ubize wao utagundua kuwa
uzalishaji walionao ni wa kawaida na pengine upo chini zaidi. Watu hawa siyo
kweli kuwa wapo bize bali wanashindwa kupangilia majukumu ya kazi zao na
matokeo yake ni kushindwa kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili. Watu
wenye mafanikio hawasemi kuwa wapo bize muda wote bali wanatambua namna ya
kucheza na vipaumbele vya ratiba zao za kila siku na hatimaye kupelekea watu
hawa kuwa na uzalishaji wa juu na hivyo wana matokeo mazuri katika maisha yao.
4. Epuka
neno “mlinganyo/usawa (balance)”. Mwandishi anatushirikisha kuwa kama unahitaji
kutumia muda wako vizuri ni lazima kwanza ufahamu kuwa kuna wakati utahitaji
kutumia muda mwingi kwa ajili ya kukamilisha kazi uliyoipanga ili kwa baadae
ikuletee matokeo mazuri. Kuna muda utahitaji kulala masaa machache kwa ajili ya
kukamilisha jukumu ulilonalo au kuna wakati utapaswa kufanya kazi bila malipo.
5. Watu
waliofanikiwa wanafurahia majukumu ya kazi zao. Mwandishi anatushirikisha kuwa
watu wa kawaida wana fikra kuwa ipo siku ambayo watakuwa na muda wa kupumzika ili
wafurahie maisha. Hii ni fikra ambayo watu waliofanikiwa wanapingana nayo kwa
vile wao kila wanachofanya ni furaha na faraja katika maisha yao ya kila siku.
Hapa ni muhimu kutambua kuwa unatakiwa kuishi leo kana kwamba kesho hautakuwepo
kwa maana ya kwamba hautakiwi kuairisha furaha ya leo kwa ajili ya kesho. Kwa
maana hii kazi inatakiwa kuchukuliwa kwa mtazamo wa kuwa kazi ni sehemu ya
maisha ya kila siku na ni chanzo cha furaha katika maisha ya kila mmoja. TUMIA
MUDA WAKO KUFANYA MAMBO YANAYOKUFURAHISHA.
6. Fahamu
kuwa watu wenye mafanikio makubwa wanahitaji kulipwa kutokana na matokeo ya
kazi zao. Mwandishi anatushirikisha kuwa hii ni tofauti kubwa kati ya watu
wenye mafanikio mkubwa na watu wa kawaida. Watu wa kawaida mara nyingi
wanahitaji kulipwa kulingana na muda wanaotumia kazini na wala hawajali kipi
wanazalisha pindi wanapokuwa kazini. Kwa ujumla watu wenye mafanikio wanafanya
kazi kubwa kwa sasa wakitegemea kupata faida baada ya matokeo ya kazi
waliofanya kuonekana. Watu waliofanikiwa hawafanyi kazi kwa ajili ya malipo
bali wanafanya kazi kwa ajili ya kutoa matokeo mazuri kwenye jamii
inayowazunguka na matokeo hayo ndiyo yanarudisha mshindo nyuma (feedback) kwa
muhusika kama malipo ya kazi yake.
7. Watu
wengi wanaendelea na falsafa ya zama ya “kutunza muda” na kusahau kuwa kamwe
muda hautunzwi badala yake mhusika anapaswa kudhibiti matendo yake kwenye kila
sekunde ya muda wake. Mwandishi anatushirikisha kuwa hakuna namna yoyote ile
mtu ataweza kutunza muda kama anashindwa kuwa na nidhamu binafsi ya matendo
yake. Kwa maana hii kila mtu ni muhusika mkuu wa kuamua ni kipi kifanyike au
kisifanyike kwenye kila sekunde ya muda alionao. Unaweza kuamua kufanya vitu
vyenye matokeo mazuri pekee au unaweza kuamua kufanya mambo ya hovyo. Hapa ndipo
watu wanaachana na kuanza kuona makundi ya watu waliofanikiwa kimaisha na wengine
wanaangaika kimaisha lakini wote kila siku wanapewa muda sawa. Kwa ufupi ni
kwamba “KAMA UNASHINDWA KUJIDHIBITI MWENYEWE KAMWE HAUWEZI KUTUMIA VYEMA MUDA
WAKO”.
8. Njia
ya kwanza ya kudhibiti matendo yako ni kutenga majukumu yako kwa vipaumbele.
Hakikisha majukumu yako kwa siku nzima unayagawanya katika makundi manne ambayo
kwa ujumla yanaitwa “time management
matrix”. Kundi la kwanza ni majukumu ambayo ni MUHIMU na ni ya HARAKA,
kundi la pili ni majukumu ambayo ni MUHIMU lakini SIO YA HARAKA, kundi la tatu
ni majukumu ambayo SIO YA MUHIMU lakini YANA UHARAKA na kundi la mwisho ni
majukumu ambayo SIYO MUHIMU na SIYO YA HARAKA. Makundi haya kwa ujumla yanatoa
nafasi kwa mhusika kufikiria juu ya kipi ni cha muhimu kufanyika na kwa muda
upi kifanyike. Kwa maana nyingine makundi haya yanatuhitaji kutekeleza majukumu
yetu kwa mtiririko wa umuhimu na uharaka wake. Hii ni tofauti na falsafa ya
zamani ya kutunza muda ambayo ililenga mtu kufanya kazi kwa haraka na presha
kubwa ili aendane muda uliyopo.
9. Wanamafanikio
wanatambua kuwa kadri wanavyotenga muda wa kutosha kwa ajili ya
kufuatilia/kukamilisha majukumu waliyonayo kwenye kila sekta ya maisha yao
ndivyo wanapata matokeo makubwa kwenye husika. Mfano, kwa wastani watu wengi
katika jamii wanapambana kwa ajili ya kufanikisha maisha yao katika sekta sita
ambazo ni Kazi, Familia, Imani, Fedha, Afya/Utimamu wa mwili na Kijamii. Mafanikio
yako katika kila sekta yatategemea na muda unaotenga kwa siku au wiki kwa ajili
ya kujiendeleza kwenye kila sekta. UTAVUNA KULINGANA NA UNACHOPANDA.
10. Watu waliofanikiwa zaidi wana uwezo wa
kuongeza/kupanua muda wao. Unaweza kujiuliza kuwa wanaweza vipi kuongeza muda?
Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wenye mafanikio pamoja na kufanya vitu kwa
mtiririko wa umuhimu na uharaka wake, watu hawa wana uwezo wa kufanya mambo
yenye matokeo makubwa na yanayoweza kudumu kwa muda mrefu. Uwezo wa kuongeza
muda unatokana na ufanisi wa utendaji kazi ambao unapelekea kuwekeza muda
mwingi kwenye kazi ambazo zinawapa muda wa kutosha kwa ajili ya kufanya kazi
nyingine siku zijazo. Kwa maana nyingine ni kwamba watu wenye mafanikio makubwa
sio tu wanaangalia umuhimu na uharaka wa jambo kwa wakati uliopo pekee bali
wanaangalia umuhimu wa jambo husika kwa siku zijazo. Hivyo, watu wenye
mafanikio makubwa wanajiuliza ni kwa namna gani matumizi ya muda wao kwa sasa
yatabadilisha maisha yao ya baadae.
11. Ruhusa
ya kwanza ya kuongeza muda; AMUA
KUPOTEZEA AU KUSEMA HAPANA. Mwandishi anatushirikisha kuwa kama unataka
kutunza muda wako vizuri ili utumike kwa ajili ya kufanya vitu vyenye manufaa
ni lazima uwe na nguvu ya kupotezea au kusema hapana kwa baadhi ya vitu ambavyo
havina tija katika maisha yako. Hapa unahitaji kuwa jasiri wa kukataa kuwa kila
sio linalokuja kwenye fikra zako au mbele yako lazima lifanyiwe kazi au sio
kila anayekuja utimize haja zake. Hakikisha unafanya vitu ambavyo kamwe
hautojutia kwa nini umefanya mara baada ya matokeo ya vitu hivyo
kujidhihirisha.
Baadhi ya tabia
ambazo unapaswa kuachana nazo mara moja ni mabishano, kufanya kazi za wengine
ambazo sio lazima ufanye wewe, epuka kupoteza muda kwa kuangalia TV, epuka
kupoteza muda kujibu emails au chati za kwenye mitandao ya kijamii ambazo
hazina tija, epuka vikao visivyo na tija, epuka kazi za kujitolea ambazo
zimepitiliza, epuka kufanya kazi mbili kwa mkupuo, epuka kutoa maelezo marefu
n.k. Tabia hizi zinapoteza muda ambao ungeutumia kwa ajili ya kuwa karibu na
familia yako au kufanya mambo mengine ambayo ni muhimu.
12. Ruhusa
ya pili ya kuongeza muda; WEKAZA
MUDA WAKO KUPITIA MAAMUZI YAKO YA FEDHA. Mwandishi anatushirikisha kuwa
maamuzi yako ya fedha unayofanya kwa sasa yana mchango mkubwa wa kuamua hatima
ya kipato chako na muda wako kwa siku zijazo. Watu wenye mafanikio kabla ya
kufanya matumizi yoyote ya pesa ni lazima wajiulize thamani ya fedha hiyo kama ingewekezwa
sehemu ambayo inatoa asilimia flani kama faida kwa mwaka na je baada ya miaka
kadhaa fedha hiyo ingelipa thamani sawa na hicho ambacho wanahitaji kuitumia
kwa sasa?. Swali hili linamfanya mtu mwenye mafanikio atafakari gharama na
faida ambazo atazikosa kwa kuamua kutumia kiasi cha fedha husika kwa sasa
badala ya kuiwekeza ili baada ya miaka kadhaa apate ongezeka la thamani ya
fedha husika. Kutokana na msingi huu unatakiwa kufahamu kuwa kila shilingi
unayoitumia kwa sasa ina athari kubwa kwenye nafasi yako ya kifedha kwa miaka
ijayo. Hapa unaweza ukajitathimini kwenye matumizi yako ya fedha ambayo siyo ya
lazima kama ununuzi wa vocha, magazeti, uvutaji wa sigara, ulevi au matumizi
ambayo hayapo kwenye bajeti yako. MUDA UNA THAMANI ZAIDI YA PESA KUTOKANA NA
UKWELI KUWA MUDA UKITUMIWA VIZURI UNATENGENEZA PESA AMBAZO ZITAENDELEA
KUJITENGENEZA ZENYEWE.
13. Tumia njia ambazo zinasaidia kupunguza
muda wa utendaji kazi. Kama ambavyo tumeona katika ruhusa ya pili hapo juu kuwa
shilingi ya leo kwa kesho itakuwa na thamani kubwa kama imewekezwa, ndivyo
mwandishi anatukumbusha pia juu ya matumizi ya muda wetu katika kazi zetu za
kila siku. Kama kuna uwezekano wa kutumia teknolojia ambayo imeboreshwa katika
kazi yako hakuna haja ya kuendelea kutumia teknolojia ya zamani ambayo
inasababisha upoteze muda mwingi ambao ungeutumia kufanya mambo mengine. Mfano,
kama kazi inaweza kufanywa na mashine hakuna haja ya kung’ang’ania kufanya hizo
kwa kutumia mikono. Nguvu iliyopo katika kufanya kazi kwa teknolojia ni kwamba
itakusaidia kufanya kazi masaa yote na siku zote saba za wiki kulingana na
teknolojia pamoja na kazi husika. Mfano, mauzo kwa kutumia mtandao, mhusika
anaweza kuuza hata kama amelala.
14. Ruhusa
ya tatu ya kuongeza muda; ONGEZA
MUDA WAKO KWA GATUA MADARAKA/KAZI AMBAZO ZIPO JUU YA UWEZO WAKO AU SIO ZA
KIWANGO CHAKO. Mwandishi anatushirikisha kuwa ni muhimu kufanya tathimini
ya majukumu ya kazi zako za kila siku na kisha ukajiuliza kama kuna ulazima wa
kazi zote kufanywa na wewe. Chagua kazi ambazo unaona unaweza kumfundisha wa
chini yako ili azitekeleze kwa niaba yako na kukufanya hivyo utakuwa umetunza
muda ambao utautumia kufanya mambo mengine.
Pia,
sehemu nyingine ambayo unahitaji kugatua madaraka ni zile ambazo zipo nje ya
taaluma yako. Badala ya kukomaa na kazi
ambayo hauna utaalamu wa kutosha ni vyema ukamtafuta wa kuifanya kazi hizo kwa
ufanisi zaidi huku wewe ukiwa unatekeleza majukumu mengine. Mfano, ni kawaida
kukuta kuwa wafanyabiashara wa kawaida wanatumia muda mwingi kutekeleza majukumu
yote ya biashara kuanzia kazi za uhasibu, sheria, mipango n.k. Mwandishi anatushauri
kuwa kama unahitaji kuwa na mafanikio makubwa ni lazima uwe tayari kuamini kuwa
kazi yako inaweza kufanywa na mtu yeyote kwa viwango unavyohitaji.
15. Ruhusa
ya nne ya kuongeza muda; ONGEZA MUDA WAKO KWA KUKUBALI KUAIRISHA MAMBO PALE
INAPOBIDI. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wenye mafanikio sio
tu wanafanya kwa mtiririko wa umuhimu, uharaka na umuhimu wa vitu husika kwa
siku zijazo bali pia wanaangalia ni upi muhafaka kwa ajili ya kufanya kazi
husika. Watu waliofanikiwa wanafahamu kama endapo kuna ulazima wa kazi husika
kukamilishwa kwa sasa au kusubirishwa kwa baadae kwa kutegemea umuhimu wake kwa
wakati husika. Kwa ujumla mwandishi anatushirikisha kuwa kila kazi au maamuzi
unayofanya ni lazima kwanza usome alama za nyakati. Kama alama za nyakati
haziruhusu kazi/maamuzi husika kufanyika kwa wakati huo hakuna haja la
kulazimisha kukamilisha/kufanya maamuzi badala yake ni vyema ukasubiria kwa
makusudi mpaka pale hali itakapokuwa vizuri.
16. Watu wenye mafanikio wanajua nguvu
iliyopo kwenye kusubiria mpaka dakika ya mwisho katika fursa husika. Mwandishi
anatushirikisha kuwa watu waliofanikiwa wantambuwa kuwa dakika ya mwisho kwenye
fursa husika ndio muda kutengeneza faida kubwa. Kutokana na ukweli huu,
wanamafanikio wanatumia pindi wanaposubirisha kazi/fursa kama ambavyo tumeona
kwenye ruhusa ya nne ya kuongeza muda wanasubiria mpaka dakika ya mwisho ambayo
ndo fursa husika inakuwa imeiva. Hii ndio siri ambayo watu wenye mafanikio
wanaitumia kutengeneza pesa nyingi kwa vile wanakuwa na taarifa sahihi kuhusu
fursa husika na hawana hofu pindi wanaposubiria ili fursa husika ikomae. KILA
KITU KINABADIRIKA HASA KWENYE SOKO LA ULIMWENGU WA SASA HIVYO UNAHITAJI
KUFAHAMU NYAKATI ZIPI NI SAHIHI KUKALIMISHA KAZI/MAAMUZI ULIYOYASUBIRISHA KWA
MAKUSUDI ILI KUEPUKA GHARAMA YA KUFANYA MAAMUZI YA HARAKA.
17. Fahamu kuwa matajiri hawalipii bili za
kodi mwanzoni bali wanasubiria mpaka siku za mwisho wanazotakiwa kulipia. Siri
hii ndio mwandishi anatushirikisha kwa ajili ya kufahamu nguvu iliyopo katika
kusubilia mpaka dakika ya mwisho. Matajiri wanafahamu kuwa katika muda wanaosubilia
kulipa wanawezakutumia fedha husika kwa ajili kukamilisha fursa endapo itajitokeza
ndani ya muda husika. Kwa kufanya hivi wanafanikiwa kuongeza muda ambao
unazalisha muda zaidi kwa ajili ya kukamilisha kazi za siku zaijazo.
18. Ruhusa
ya tano ya kuongeza muda; ONGEZA
MUDA WAKO KWA KUTULIZA AKILI KATIKA NYAKATI MUHIMU. Mwandishi anatushirikisha
kuwa kuna nyakati ambazo utatakiwa kufanya kazi mara mbili zaidi ya ulivyozoea
kwa ajili ya kuhakikisha unakamilisha jukumu lililo mbele yako. Hii ni pamoja na
kuhakikisha kuwa rasilimali zote unazielekeza kwenye jukumu husika kwa kadri
zinavyotakiwa mpaka pale ambapo utaona kuwa umefanikisha kukamilisha jukumu
hilo. Katika hatua hii unahitaji kutambua kuwa baada ya kuairisha fursa/kazi
kwa makusudi sasa ni muda ambao upo kwenye dakika ya mwisho ambayo ukizembea
kidogo tu unakosa kila kitu na hivyo kusubilia kwako hakutakuwa na faida bali ni
hasara. Hapa unahitaji kuongeza muda wako kwa kuhakikisha unafanyia kazi ambayo
ni kipaumbele kwa wakati na si vinginevyo. Hakikisha haurusu mwingiliano wa
vitu vingine ambavyo vinaweza kukupoteza kwenye kipaumbele chako.
19. Tengeneza mtiririko wa vipaumbele. Somo
kubwa katika kitabu hiki ni kuona kuwa msomaji anaweza kuongeza muda wake wa
kesho kwa kadri awezavyo kupitia majukumu anayofanya kwa sasa. Mwandishi anatushirikisha
kuwa ili ufanikishe zoezi la kuzalisha muda ni lazima uhakikishe unakuwa na
vipaumbele ambavyo vina muunganiko wa matukio kiasi kwamba kukamilika kwa
kipaumbele kimoja kunapelekea kuanza kwa kipaumbele kingine. Pia, kipaumbele
kimoja kisaidie kuongeza muda kwa ajili ya kipaumbele kinchofuatia.
20. Baada ya kuondoa tabia au kazi ambazo
zimekuwa zikipoteza muda wako sasa unatakiwa kuongeza uzalishaji wako. Hapa unahitaji
kutengeneza utamaduni au falsafa ambazo zitakuongoza katika kipindi chako chote
ili hatimaye uzidi kuongeza muda wako kwa ajili ya kufanikiwa katika kila sekta
ya maisha ya maisha yako. Kama wewe ni mwajiri unahitaji kuhakikisha unaishi
misingi uliyojifunza hapa ili kila mmoja chini yako ajifunze kutoka kwako kwa
ajili ya kuongeza ufanisi utendaji kazi.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com