Mambo Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha Little Red Book of Selling (Kijitabu Chekundu Cha Mauzo)

Habari ya leo rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya 20 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi wa vitabu nikiwa na lengo kubwa la kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako kuyatumia ili ubadilishe kila sekta ya maisha yako.

Uamzi wa kubadilisha maisha yako upo mikononi mwako na hivyo kama mpaka sasa haujajifunza kitu chochote katika makala hizi nakushauri husiendelee kupoteza muda wako na badala yake ufanye mambo ambayo umeyazoea.

Ili uendelee kunufaika na makala za mtandao huu BONYEZA HAPA na ujaze fomu utakuwa umejiunga na mtandao wa fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa na mtandao wa fikra za kitajiri moja kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.

Kitabu cha wiki hii ni Little Red Book Of Sellingkutoka kwa mwandishi Jeffrey Gitommer’s. Mwandishi ni mzungumzaji/mhamasishaji mashuhuri kwenye masuala ya biashara hasa upande wa mauzo na amefanikiwa kuandika vitabu vingi vya mauzo na mafanikio kwa ujumla.

Kwa ujumla katika kitabu hiki anatushirikisha mambo muhimu katika tasnia ya mauzo ambayo analenga kuboresha ujuzi wetu katika kupata, kulinda na kuridhisha wateja wetu katika sehemu ya soko tuliyopo. Katika kitabu hiki tunaongozwa na ujumbe kuwa kama wateja “watakupenda, watakuamini, wana na tumaini na wewe na hatimaye wakawa na uhakika na wewe” kwa vyovyote vile ni uwezekano wa kuendelea kununua biadhaa/huduma zako. Hii ni kutokana na ukweli kwamba pindi wateja wanapokupenda inapelekea wawe na uaminifu kwako na uaminifu unapelekea wanunue kutoka kwako na wanaponunua kutoka kwako kwa pamoja mnakuwa na mahusiano ambayo yanapelekea mzunguko wa mauzo.   

Ujumbe mwingine ambao mwandishi anatupa kama angalizo kwenye tasnia ya mauzo ni kwamba wateja hawataki kuuzwa kwa maana ya kutapeliwa bali wanahitaji kununua. Hapa ndipo kila muuzaji ni lazima kwanza apate jibu la kwa nini watu wananunua? Hili ni swali muhimu la kuzingatia kabla ya kuanza kuweka malengo ya mauzo japo wauzaji wengi huwa wanakosea na kujiuliza ni kwa jinsi gani nitauza? Hauwezi kufanikiwa katika jibu la swali la pili kwa maana ni kwa jinsi gani nitauza kama haujapata jibu la kwa nini watu wananunua. Hivyo msingi mkubwa wa mauzo yenye mafanikio ni kufahamu kwa nini watu huwa wananunua.

Mwandishi anatushirikisha majibu ya swali kwa nini watu wananunua ambayo ameyapata baada ya kuwahoji watu kwa muda mrefu:-
     i.    Watu wananunua kwa vile wanampenda muuzaji;
    ii.    Wananunua kwa vile wanafahamu kile wanachotaka kununua;
   iii.    Wanaona utofauti wa muuzaji/kampuni ikilinganishwa na wauzaji wengine;
   iv.    Wanaona thamani katika bidhaa/huduma wanayonunua;
    v.    Wanamuamini, wanatumaini na kuwa na uhakika na muuzaji;
   vi.    Wanajisikia kuwa huru pindi wanaponunua;
 vii.    Wanajisikia bidhaa/huduma zinakidhi mahitaji yao;
viii.    Bei ni ya kawaida japo sio lazima iwe bei ya chini;
   ix.    Wana uhakika kuwa bidhaa/huduma itaongeza uzalishaji wao;
    x.    Wana uhakika kuwa bidhaa/huduma itaongeza faida yao; na
  xi.    Wana uhakika kuwa muuzaji anawasaidia kufikia malengo yao huku nae akifikia mahitaji yake.

Hapo unaweza kuona kuwa wengi wetu tumekuwa tukikosea kwa kumfikiria mteja upande mmoja tu wa bei kumbe mteja naye ana mahitaji yake zaidi ya kuangalia bei. Mwandishi anatushirikisha kuwa hiyo ndo misingi muhimu ambayo kila muuzaji anatakiwa kuwa nayo kwa ajili ya kuboresha mauzo ya huduma/bidhaa zake. Ukiwa na misingi hii utafanikiwa kuwa muuza bora kipindi cha maisha yako yote.

Karibu tujifunze wote machache niliyojifunza kutoka kitabu hiki:

1. Kinachowatoutisha watu au taasisi katika viwango vya mauzo ni namna ambavyo wanatumia mbinu za mauzo. Mbinu za mauzo ni nyingi lakini ni vyema kila muuzaji akafahamu kuwa ili uwe muuzaji bora ni lazima uzingatie mbinu hizi hapa (a) Kwanza kabisa ujiamini kuwa unaweza (b) Andaa mazingira ya kukuwezesha kuwa muuzaji bora ikiwa ni pamoja na kuchagua kundi la marafiki wanaokufaha (c) Pata muda kujifunza na kuhakikisha siku yako unaipangilia vizuri (d) Kuwa na majibu ambayo unahisi wateja watakuuliza maswali (e) Kuwa mtu mwenye thamani huku ukitafuta fursa mpya mara kwa mara (f) Kuwa mtu wa vitendo na mara sote husiogope kushindwa (g) Chunga sana matumizi yako ikilinganishwa na uwekezaji au akiba yako (h) Jenga tabia njema na muda wote kuwa macho kwa ajili kuliteka soko; na (i) Wapuuze watu wanaokubeza.

2. Tenga muda maalum kwa ajili ya kupitia malengo yako ya mauzo kwa kila siku. Mwandishi anatushirikisha kuwa ni vyema kila siku uwe na muda kuangalia namna ambavyo siku yako itakwenda na muda huu ni vyema ukawa ni wa asubuhi na mapema kabla watu hawajaamka kwa ajili ya utulivu. Pia kila siku unatakiwa kutenga muda kwa ajili ya kufanya tathimini namna ambavyo umefanikisha malengo ya siku husika. Hapa unatakiwa kuongozwa na nidhamu ya hali ya juu yenye chimbuko la hamasa kutoka ndani mwako pasipo kusubiria kusukumwa na mwajiri wako au mtu yeyote. Hii ni kutokana na ukweli kwamba hakuna mtu ambaye atakuja kukutunuku digrii ya mafanikio, digirii ya mafanikio unajitunuku mwenyewe kwa kuongozwa na bidii katika kazi. Ndiyo bidii katika kazi ndo nyenzo ambayo itakufanya jamii inayokuzunguka ione kuwa wewe ni mtu mwenye bahati. Bahati inatafutwa hivyo hakikisha unaitafuta bahati yako.

3. Anza kwa kujilaumu mwenyewe kutokana na kiwango cha mauzo yako badala ya kulaumu mfumo au serikali, mazingira au watu wanaokuzunguka. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wengi wanafikia hatua ya kulaumu waajiri wao, serikali, watu wao wa karibu au hata pengine wateja kabla ya kujiuliza wao wanahusika vipi kwenye kiwango cha mauzo yao. Kwa ujumla kiwango cha mauzo yako kinategemea na (a) Imani yako – Je unajiamini kuwa unaweza kuuza kwa kiwango kile unachokusudia? (b) Mazoea ya kazi yako – Je unaenda kazini ukiwa umechelewa na unafunga mapema jioni lakini bado unategemea kuwa na kiwango kikubwa cha mauzo? (c) Hisia mbaya juu yako – Je unahisia mbaya juu ya bidhaa/huduma au una wasiwasi wa bei zako? (d) Tabia mbaya kama ulevi/utaji wa sigara ukiwa kazini (e) Hautimizi ahadi kwa wateja au pengine unatimiza kinyume na makubaliano. Hizi baadhi ya sehemu muhimu ambazo unatakiwa kujitathimini kwa ajili ya kuboresha kiwango cha mauzo yako.

4. Siku mbaya au nzuri unaiandaa mwenyewe kila unapoamka asubuhi. Ni kawaida kusikia mtu anakuambia kuwa leo sina mudi ya kufanya au leo siku yangu imekwenda vibaya. Mwandishi anatushirikisha kuwa ukifanya tathimini siku ambayo unadai kuwa imekwendea vibaya utagundua kuwa kwa asilimia kubwa ubaya wa siku hiyo wewe ndo umechangia kwa kiasi kikubwa hasa kutokana na fikra/mtazamo wako kwa siku husika. Mfano, ni kawaida kwa watu walio wengi kuwa na uzalishaji mdogo kwenye siku za jumatatu na ijumaa kutokana na mitazamo yao juu ya siku husika.

5. Je unaongozwa na falsafa zipi? Falsafa zinazaa mtazamo, mtazamo unaleta vitendo na vitendo vinaleta matokeo na hatimaye matokeo yanaleta mtindo wa maisha yako. Kama haupendi mtindo wa maisha yako ni lazima kwanza unagalie falsafa zinazokuongoza na hatimaye uzibadilishe falsafa hizo kwa ajili ya kufikia mtindo mpya wa maisha. Watu wa mauzo mara nyingi wanafanya kosa kubwa la kutazama sehemu ya vitendo kabla ya kuangalia kwanza falsafa zinazowaongoza. Kwa kifupi falsafa ni vile vitu ambavyo una imani juu yake na katika maisha yako umeviweka kama mwongozo wako kwenye kila sekta ya maisha yako. Kwa maana hii falsa zinatofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine.

6. Kuwa na mtazamo wa NDIYO. Mwandishi anatushirikisha kuwa mtazamo wa ndiyo ni nyenzo muhimu ya kukabiliana na kila aina ya mazingira au tukio kwa muuzaji yeyeto yule. Hii ni kutokana na ukweli kwamba ukiwana mtazamo wa ndiyo utakuwa tayari kufanya kazi hata kwenye mazingira ambayo wenzako wanaona kuwa hayawezekani. Mtazamo huu unakufanya ujione kuwa kila kitu au tukio linaanza na NDIYO hata kama ni HAPANA hivyo kukujengea msingi imara wa kuona kuwa kila jambo linaweza kutekelezwa endapo utaweka jitihada.

7. Kazi ya kesho inaandaliwa usiku wa leo. Mwandishi anatushirikisha kuwa kama unataka kuwa muuzaji bora ni lazima uwe tayari kuindaa siku yako wakati watu wengine wamelala au wanaangalia TV usiku. Husikubali kupoteza muda wako kwa kuangalia michezo au filamu ambazo hazikuongezei kitu katika tasnia ya kazi yako na badala yake tumia muda huo kupangilia vyema kazi zako kwa ajili ya siku inayofuatia. Hapa unatakiwa kufahamu kuwa kadri unavyoharibu muda wako kwenye TV au siku hizi kwenye mitandao ya kijamii ndivyo unakubali kutumiwa na watu wengine kutimiza malengo yao ya mauzo.

8. Je wewe ni mshindi au mlalamikaji? Mwandishi anatushirikisha kuwa kama kweli unataka kuwa msshindi katika kazi zako za mauzo ni lazima kwanza uepuke tabia ya kuwa mlalamikaji. Hakikisha jukumu la ushindi unaliweka chini ya mamlaka yako ili hata pale unaposhindwa ujiulize wewe mwenyewe kwa nini umeshindwa na sio kulalamikia wengine. Hii ni kutokana na ukweli kwamba dhana ya ulalamikaji inakufanya ujitoe kwenye uhusika wa jambo au tukio na badala yake unamuachia mtu mwingine kama ndo amesababisha. Pia, unatakiwa kukumbuka kuwa hakuna mtu anayejitambua atapenda kukaa na mtu mlalamikaji. Kwa maana hivyo kadri unavyokuwa mlalamikaji unazidi kujiwekea mbali na watu wenye mchango chanya katika maendeleo ya kazi yako.

9. Utambulisho wako (self branding) ni nyenzo muhimu kwa wateja wako. Kadri watu wanavyokufahamu zaidi ndivyo watavutiwa kufanya biashara na wewe. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wengi kwenye tasnia ya mauzo wanafanya makosa ya kupigania utambulisho wa bidhaa/huduma zao kuliko wanavyoweka jitihada za kutambulisha majina yao wenyewe. Ili kuachana na makosa haya unahitaji kujitambulisha kwanza ili ufahamike kwa wateja wako na kadri wateja wanavyofahamu utambulisho wako ni rahisi kuvutiwa na yale unayofanya ikiwa ni pamoja na kampuni, bidhaa au huduma zako. Katika kujitambulisha unahitaji kujipambanua kama mtu mwenye kupigania kutatua matatizo ya wanajamii inayokuzunguka, unahitaji kujenga picha ya tofauti kwa wateja wako, unahitaji kujenga imani kwa wateja wako na unahitaji kuonekana mbunifu kupitia yale unayofanya. Muhimu tambua kuwa katika tasnia ya mauzo ni lazima utambue kuwa “si yule unayemfahamu bali ni yupi anakufahamu” hivyo unahitaji kujitangaza kwa hali na mali.

10. Thamani ya bidhaa zako pamoja na mahusiano yako na wateja ni sifa mbili muhimu za kuongeza kiwango cha mauzo yako na wala sio bei ya bidhaa/huduma zako. Watu wengi wanachanganya maana ya thamani kwa mteja kuwa ni kama vile punguzo la bei, bidhaa za bure zinazoambatana na kitu unachonunua, nyongeza n.k. Ukweli ni kwamba thamani kwa mteja ni vile vitu vinavyofanyika kwa mteja au mteja mtarajiwa kwa ajili ya faida yake pasipokutegemea wewe utafaidika na nini. Kwa maana hii ni lazima kwanza utangulize thamani kwa mteja wako na hatimaye faida itakufuata yenyewe. Hii ni pamoja na kutoa elimisho juu ya bidhaa au biashara yako kupitia makala, mitandao ya kijamii au semina za bure huku ukiacha namba zako za mawasiliano kwa ajili ya wateja watarajiwa. Kutokana na ukweli huu watu hawangalii bei bali wanaangalia thamani yako na huduma zako kwani kadri thamani inavyozidi kuwa kubwa ndivyo na wateja hawangalii kiwango cha bei.

11. Acha kuwa na fikra za kuwa biashara yako ni kuuza bidhaa/huduma kwa wateja na badala yake fikiria kuwa biashara yako ni kuuza thamani kwa wateja wako. Kumbuka kuwa unapouza thamani bei inakuwa sio kipimo cha mauzo yako na badala yake kinachoamua kiwango cha mauzo ni thamani unayotoa. Pia, kumbuka kuwa sio wateja wote watanunua kwa kuangalia thamani kwani tafiti zinaonyesha kuwa asilimia 30 – 40 ya wateja wananunua kwa kuangalia bei ya chini ikilinganishwa na asilimia 60 – 70 ya wateja wanaotangulizwa thamani kwanza.

12. Kiwango cha mauzo yako kina uhusiano mkubwa na jitihada unazoweka kwenye kujenga mtandao na wateja wako. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kadri unavyozidi kuwa na mtandao mkubwa ndivyo unaongeza idadi ya marafiki na idadi ya marafiki ina mchango chanya kwenye kiwango cha mauzo yako. Hapa unahitaji kutumia majukwaa au matukio mbalimbali kwa ajili kupanua mtandao wako. Unaweza kutumia mitandao ya kijamii, maonyesho mbalimbali kama maonyesho ya biashara, nanenane, mkusanyiko wa watu kwa ajili ya michezo na matukio mengineyo.

13. Kiwango cha mauzo yako kinategemea na idadi ya wateja au wateja tarajiwa ambao unaweza kuwashawishi. Mwandishi anatushirikisha kuwa kuna uhusiano mkubwa katika ya mauzo na uwezo wa kushawishi wateja wako. Pia, unapofanya ushawishi ni lazima utambue kuwa ni kundi lipi katika jamii unalilenga kwa ajili ya kufanya biashara na wewe. Mfano, itakuwa haina maana kumshawishi mtoto wakati unajua kuwa mtoa maamzi ni baba au mama. Itakuwa haina maana kumshawishi mwajiriwa wa kampuni kwa ajili ya bidhaa au huduma zako wakati unajua kabisa kuwa mtoa maamuzi ni bosi wake.

14. Kufanikiwa katika kuwashawishi wateja kunategemea na namna ambavyo unauliza au kujibu maswali pindi unapokutana na wateja watarajiwa. Mwandishi anatushirikisha kuwa kabla ya kufanya ushawishi na wateja ni lazima kwanza upangilie vyema maswali na majibu ili vyote kwa pamoja vimushawishi mtu kufanya biashara na wewe. Muda wote uliza maswali ambayo yatakutifautisha na wapinzani wako wa kibiashara, uliza maswali ambayo yatamfanya mteja aone thamani katika bidhaa/huduma yako, uliza maswali ambayo yatamfa mteja aone fursa mpya katika biashara zake au maswali ambayo yanampa shauku ya kuendelea kukusikiliza. Kumbuka kuwa kama mteja mtarajiwa hajashawishika ni kwa sababu na wewe haukuwa na ushawishi hivyo endelea kujifunza mbinu za kushawishi.

15. Kama unaweza kumchekesha mteja mtarajiwa kuna uwezekano mkubwa wa kumshawishi anunue kutoka kwako. Mwandishi anatushirikisha kuwa mteja unapomgusa hisia zake kiasi cha kuweza kutabasamu au kucheka basi fahamu kuwa umefanikisha hatua ya kwanza ya mahusiano mazuri kati yako na yeye. Hivyo katika kutafuta wateja wapya unahitaji kuongozwa na ucheshi wa maneno pamoja na lugha ya mwili. Hata hivyo ni lazima utambue kuwa mcheshi katika mauzo inachukua muda ikitegemea na namna mhusika anavyowekeza kwenye kujifunza kuwa mcheshi.

16. Tumia ubunifu kujitofautisha na wengine hatimaye kuliteka soko. Kama ambavyo tumeona kuwa watu wapo tayari kulipia thamani, ni kupitia ubunifu utafanikiwa kutoa thamani kubwa kwa wateja wako. Ubunifu unategemea na namna ambavyo unatumiwa kichwa chako kwa maana ubongo wako – unahitaji kujenga tabia ya kufikiri kwa ajili kuwa mbunifu, mtazamo wako – ukiwa na mtazamo hasi daima hauwezi kuwa mbunifu, namna unavyotazama mazingira yako – kuna fursa kila sehemu inayokuzunguka na jinsi unavyojitazama mwenyewe – kama haujiamini kamwe hauwezi kuwa mbunifu. Ili kuwa mbunifu unahitaji kusoma zaidi kwani kadri unavyosoma makala na vitabu mbalimbali ndivyo unajifunza ubunifu zaidi.

17. Kama muuzaji unahitaji kuchanganua hali hatarishi na kuipunguza kabla kufanya biashara na mteja wako. Kadri utavyopunguza hali hatarishi kwa wateja wako ndivyo itakuwa rahisi kuwavuta watu wengi kufanya biashara na wewe. Hii ni kutokana na ukweli kwamba watu wanahitaji bidhaa/huduma ambazo sio hatarishi (risk free products or services). Hali hatarishi unahitaji kuzichangunua kwa kuangalia ubora wa bidhaa/huduma zako, thamani halisi ya huduma zako, ukweli katika kile unachomuhubiria mteja wako, matumizi au matokeo tarajiwa baada ya kununua bidhaa/huduma zako n.k.

18. Shuhuda wa bidhaa au huduma zako ana nafasi ya kuwashawishi watu wengi kuliko wewe. Kuna msemo kuwa ukimfukuza mteja mmoja kutokana na uzembe au uongo wako katika huduma zako unakuwa umefukuza wateja zaidi ya kumi.  Ndicho mwandishi anachotushirikisha hapa kuwa unatakiwa kuhakikisha kila mteja unayefanya naye biashara huna budi kumridhisha. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kadri mteja anavyoridhika na huduma/bidhaa zako ndivyo atavyowaleta wateja wengine wapya.

19.  Kuwa macho muda wote kwa ajili ya kufanya mauzo. Kamwe husikubali kutoka kwenye lengo lako kubwa pasipokujali sehemu uliyopo, kila sehemu na kila wakati hakikisha upo tayari kwa ajili ushawishi wa wateja watarajiwa. Hapa muda wote unatakiwa kuongozwa na hamasa tano ambazo ni (i) hamasa ya ushindi (ii) hamasa ya kujiamini wewe pamoja na bidhaa/huduma zako (iii) hamasa ya kutegemea matukio chanya kuliko matukio hasi (iv) hamasa ya kufanikiwa na (v) hamasa ya maamuzi chanya.

20.  Jiuzulu nafasi yako kama meneja mkuu wa ulimwengu. Mwandishi anatushirikisha kuwa mpaka kufikia hapa umepata nyenzo muhimu za kukusukuma katika tasnia ya mauzo lakini kuna jambo moja la kuzingatia. Kuna matukio mengi yanatokea na mengine yataendelea kutokea katika ulimwengu huu lakini kabla ya kuyashabikia jiulize yanachangia nini katika maisha yako. Kamwe husikubali kutekwa kwenye matukio ya watu wengine, unahitaji kuandaa matukio yako mwenye ili yaweteke ambao bado hawajajitambua. Sanaa ya kuuza inahitaji nidhamu ya hali ya juu hasa nidhamu binafsi. Unahitaji kuachana na ushabiki ambao hauna tija kwako.

Haya ni machache ambayo nimeweza kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.

Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.

Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.

Born to Win ~ Dream Big 

Augustine Mathias Bilondwa

Namba ya Simu:      +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com


onclick='window.open(