Mambo Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha So Smart But….: How Intelligent People Lose Credibility and How They Can Get It Back (Jinsi Watu Wenye Akili Wanavyopoteza Uaminifu na Jinsi ya Kuurejesha)

Habari ya leo rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya 24 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi wa vitabu nikiwa na lengo kubwa la kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako kuyatumia ili ubadilishe kila sekta ya maisha yako.

Uamzi wa kubadilisha maisha yako upo mikononi mwako na hivyo kama mpaka sasa haujajifunza kitu chochote katika makala hizi nakushauri husiendelee kupoteza muda wako na badala yake ufanye mambo ambayo umezoea.

Ili uendelee kunufaika na makala za mtandao huu BONYEZA HAPA na ujaze fomu utakuwa umejiunga na mtandao wa fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa na mtandao wa fikra za kitajiri moja kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.

Kabla ya kuendelea kushirikisha uchambuzi wa kitabu cha leo nitumie muda huu kuomba radhi kwa kuchelewa kukutelea uchambuzi huu ndani ya wiki iliyoisha jana. Hii imetokana na sababu zilizo nje ya uwezo wangu kwa kuwa mazingira niliyopo kwa sasa hayana nishati ya umeme ya uhakika.

Kitabu cha wiki hii ni So Smart But…..kutoka kwa mwandishi ALLEN N. Weiner. Mwandishi wa kitabu hiki amebobea katika tasnia ya mawasiliano na kwa muda mrefu amejihusisha katika utoaji wa semina mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa kocha kwa watu mbalimbali katika masuala ya mawasiliano na uzungumzaji. Semina zake mara nyingi zimejikita katika kuwafundisha watu namna wanavyoweza kuboresha ushawishi, hamasa binafsi pamoja na uaminifu bora kwa jamii inayowazunguka.

Mwandishi huyu alipata msukumo wa kuandika kitabu hiki mara baada ya kuona kuwa watu wengi wana taaluma mbalimbali kiasi ambacho wamefikia hatua ya kutambuliwa kama watu maarufu katika taaluma zao. Pamoja na watu hawa kufikia viwango vya juu vya taaluma, ajabu ni kwamba ni wachache kati ya watu hawa ambao wanaweza kujieleza mbele za watu na kueleweka. Wengi wao wanahitaji msaada katika mbinu za mawasiliano ili kufikisha ujumbe wanaokusudia. Tunafahamu fika kuwa bila mawasiliano mwanadamu hawezi kufanikisha jambo lolote na hii ndio sababu kubwa mwandishi wa kitabu hiki kuwaandikia watu kwa ajili ya kuwashirikisha misingi mikuu ya mawasiliano.

Karibu tujifunze wote machache niliyojifunza kutoka kitabu hiki:

1. Watu kadri wanavyokuwa na uzoefu wa kazi/biashara ndivyo inafikia hatua wanahisi kuwa kuna mtu juu yao ambaye hapendi kile wanachofanya. Mtu huyu anaweza kuwa ni bosi wako au mshindani wa biashara. Hata hivyo hisia hizo zinasababishwa na watu kutokufahamu mbinu za mawasiliano kwa kutumia lugha ya mwili. Zaidi ya asilimia sitini ya mawasiliano katika jamii uwasilishwa kwa mfumo husio wa maongezi ambao unahusisha lugha ya mwili. Mwandishi anatushirikisha kuwa unaweza kupata matinki ya mtu anayewasilisha kwa kusoma namna ambavyo anashirikisha viungo vya mwili wake katika kufikisha kuwasilisha ujumbe. Bahati mbaya ni wafanyakazi wachache sana ambao wanatambua mbinu hii ya mawasiliano na hivyo wengi wao wameshindwa kueleweka pindi wanapojieleza au pengine wameshindwa kuwaelewa wafanyakazi wenzao au waajiri wao.

2. Ni rahisi watu kutambua kiwango cha uaminifu/heshima yako kwa kuangalia lugha yako ya mwili (jinsi unavyoonekana kwa ujumla), mpangilio wa sauti yako pamoja na mpangilio wa maneno yako. Hivi ni vitu vitatu muhimu ambavyo vinamtambulisha mtu yeyeto pindi anapowasilisha mada yake kwa mtu mwingine au watu wengine. Na hapa ni muhimu kufahamu kuwa mwonekano wako pamoja na mpangilio wa sauti kwa pamoja vinachangia asilimia tisini ya kueleweka kwako ikilinginishwa na asilimia kumi tu ya mpangilio wa maneno. Muhimu, hapa unatakiwa kufahamu kuwa unahitaji kujitambulisha haraka kwa kutumia lugha ya mwili wako (mwonekano wako) pamoja na kuhakikisha kuwa unatoa sauti yenye kila chembe ya kujiamini kwa kadri uwezavyo.

3. Ili ueleweke kwa urahisi unahitaji vizingatia vitu vifuatavyo kwa ajili ya kuboresha mwonekano wako; i) matumizi ya nafasi yako pindi unapojieleza ii) matumizi bora ya kushikana mikono na wengine iii) matunmizi ya muda – zingatia kutumia vyema muda uliopewa iv) mwonekano wa uso wako v) matumizi ya viungo vyako vya mwili – fahamu namna ya kutumia kila kiungo cha mwili wako vi) zingatia mfumo wa mavazi yako pamoja na unene wa mwili wako; na matumizi bora ya mapambo ya nafasi.

4. Unapowasilisha mada yako vitu vifuatavyo vitakusaidia kuboresha mpangilio wa sauti yako; i) kiwango cha sauti yako – kuzungumza kwa sauti ya juu ili kila mmoja asikie; ii) mpangilio wa sauti – kupanda na kushuka kwa sauti kwa kutegemea kila sehemu unayozungumzia iii) kasi ya sauti yako iv) urefu wa sentensi zako v) matumizi fasaha ya lugha vi) zingatia rafudhi ya lugha husika vii) zingatia matumizi sahihi ya misamihati viii) zingatia matamushi sahihi ya misamihati ix) fahamu kwa kina mantiki ya kile unachowasilisha x) hakikisha unaongozwa na takwimu kuliko blah blah; na xii) hepuka kurudiarudia maneno mara kwa mara.

5. Fahamu kuwa unaendelea kuchunguzwa na wasikilizaji wako hata baada ya kumaliza wasilisho lako. Hapa mwandishi anatushirikisha kuwa ni muhimu kila mmoja afahamu kuwa wasikilizaji huwa wana tabia ya kuchunguza vitu vidogo kutoka kwa mtu anayewasilisha hata kama amemaliza kuongea. Mfano, wanaweza wakachunguza jinsi unavyotembea, namna ulivyokaa na hata namna unavyowasikiliza wengine.

6. Kuna njia tano za kukuwezesha kugundua kama unaeleweka kwa mada unayowasilisha na njia hizo ni; i) chanzo cha mada – fahamu kwa kina chimbuko la mada yako na namna unavyotakiwa kutumia lugha ya mwili kuiwasilisha; ii) ujumbe – fahamu nini hasa unataka wasikilizaji wasikie/wapate kutoka kwako; iii) chunguza sehemu ambapo wasilisho lako linafanyikia; iv) chunguza mtazamo wa wawasikilizaji – hii itakusaidia kutambua kama unaongea jamii unayohitaji hama vinginevyo; na v) nyakati – tambua mada unayowasilisha kama inaendana na nyakati zilizopo.

7. Watu wengi wana taaluma ambazo zimewafanya kujichanganua kama wataalam wabobevu katika sekta flani. Hata hivyo, ni wachache ambao wanaweza kuelezea kwa ufanisi kile wanachofahamu kwa jamii inayowazunguka. Hii inatokana na ukweli kwamba wengi wanashindwa kutafsri yale wanayofahamu katika taalamu zao kwenye mazingira halisia ya jamii inayowazunguka. Kutokana na hali hii wengi wanakosa uaminifu kwa jamii inayowazunguka ikiwa ni pamoja na mabosi wao au wafanyakazi wenzao.

8. Uaminifu wa mawasiliano yako kazini au jamii inayokuzunguka unapimwa kwa kuzingatia baadhi ya misingi kama ilivyoorodheshwa hapa; i) epuka kuongea maneno mengi ambayo hayatekelezeki – chagua maneno machache ya kuongea na hakikisha unaishi maneno yako; ii) mara zote jikite kwenye mantiki ya mada unayowasilisha – epuka porojo; iii) kuwa na uwezo wa kueleza mambo magumu katika lugha rahisi; iv) kuwa na mawazo mbadala mengi kwa ajili ya kukuza pato la mwajiri wako au kupunguza upotevu wa rasimali; v) mahusiano mema na wenzako – fanya kazi kama timu; vi) uwezo wa kuingilia kati na kushauri pale ambapo mambo hayaendi sawa; vii) uwezo wa kufanya majukumu yako kwa haraka; viii) kuwa mtu wa kufikiria kwa haraka; ix) kuwa mwandishi mzuri; x) jifunze kuwa msilikazaji mzuri; na xi) uwezo wa kujiamini kwa kile unachofanya. Misingi hii kwa ujumla, inalenga kumfanya kila mmoja wetu kuwa na picha kubwa katika majukumu ya kazi pamoja na mahusiano yake na jamii inayomzunguka.

9. Kuna mbinu tano ambazo unaweza kutumia kwa ajili ya kueleza na mada yako na ukaeleweka kwa ufasaha. Moja, ni kueleza mada yako ufupi lakini ukigusa maeneo yote muhimu. Mbili, ni kueleza mada yako kwa mapana zaidi. Tatu, ni kueleza mada yako kwa kina huku ukielezea kwa mapana kila eneo la mada yako – hapa unahitaji kuweka wazi uhakika wako kwenye mada husika. Nne, unahitaji kuainisha kwa mapana matokeo (faida au madhara) tarajiwa kutokana na kutekeleza/kutotekeleza ushauri wako. Tano, onyesha maono yako juu ya fursa/changamoto zilizopo katika mada unayowasilisha – hapa unahitaji kuonesha matumaini yako hasa chanya kwa siku zijazo endapo ushauri wako utazingatiwa. Mbinu hizi zinaweza kutumiwa kwa pamoja au kwa kuchagua baadhi yake pale ambapo mtu anakusudia kuwasilisha mada yake na akaeleweka vizuri kwa walengwa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba endapo utazingatia mbinu hizi kila mmoja atasema kuwa unafahamu malefu na mapana juu ya mada unayowasilisha na pia unafahamu matokeo tarajiwa endapo ushauri wako utachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwa na maono juu ya mada husika.


10. Baada ya kuwasilisha mada yako kwa ufasaha unahitaji kufahamu mbinu za kuchukua maswali na kuyajibu kwa ufasaha ili kukidhi mahitaji ya waulizaji. Mbinu hizi ni pamoja na i) kwanza unatakiwa kuhakikisha unaandika maswali yote na kila mtu aliyeuliza; ii) elewa kiini cha swali – tambua muulizaji anahitaji kufahamu nini; iii) tambua swali lina makusudi gani – kuna baadhi ya maswali yanalenga kukupima ufahamu wako juu ya mada husika; iv) jibu kwa ufasaha kuhakikisha ulefu wa majibu yako unaendana na ulefu wa swali uliloulizwa; na v) epuka kurudirudia – jibu moja kwa moja ulichoulizwa. Mwandishi anatushirikisha kuwa endapo kila mmoja atafuata mbinu hizi katika kujibu maswali atafanikiwa kujijengea heshima kutoka kwa wasikilizaji wake.

11. Unapotakiwa kuwasilisha mada yako ndani muda mfupi unatakiwa kuzingatia sehemu kuu tano za mada yako. Kwanza, ndani ya muda mfupi ainisha sehemu ya tatizo/fursa – hapa eleza kwa ufupi tatizo/fursa iliyopo. Mbili, ainisha kwa ufupi visababishi – hapa unahitaji kueleza chanzo cha tatizo au fursa husika. Tatu, ainisha madhara ya tatizo husika. Nne, eleza kwa ufupi ni nini suluhisho la tatizo husika – njia za kufuata kwa ajili ya kutatua tatizo. Tano, eleza nini kifanyike kwa ajili ya kutatua tatizo husika – toa maoni yako yanayolenga kumaliza tatizo. Sehemu hizi tano zinalenga kumwezesha mwajiriwa/mfanyakazi kurahisisha mada yake ili ionekane nyepesi kwa mwajiri wake hata kama mada husika ni ngumu.

12. Watu wengi uaminifu kwa vile wanashindwa kutambua tamaduni za jamii wanazofanyia kazi. Mwandishi anatushirikisha kuwa tamaduni za sehemu husika wakati mwingine zinaweza kuonekana ni mambo ya kizamani lakini yana mchango mkubwa katika kujenga uaminifu kwa mtu yeyote. Hii ni kutokana na ukweli kwamba pale ambapo utafanya tukio ambalo linaenda kinyume na tamaduni au hitifaki za sehemu husika moja kwa moja utaonekana mtu wa hovyo na hivyo kujishushia heshima yako.

13. Watu wengi wana akili lakini wanashindwa kuona vitu katika maono ya picha kubwa. Mwandishi anatushirikisha kuwa ni wafanyakazi wachache sana ambao wanakuwa na mtazamo wa picha kubwa katika mazingira ya kazi zao kwani walio wengi wanaishia kutazama picha ya mahitaji na majukumu yao tu. Ili kujitofautisha na watu wa namna hii mwandishi anatushirikisha kuwa kila mmoja anatakiwa kuwa na picha kubwa ambayo inajumuisha (a) maono ya taasisi au kiwanda (b) maono ya uongozi wa taasisi (c) maono ya idara (d) maono ya timu au wafanyakazi wenzako na (e) maono yako binafsi. Hapa utagundua kuwa wafanyakazi wengi huwa wanatanguliza maono binafsi na kusahau maono mengine.

14. Kila mfanyakazi mwenye malengo ya kudumisha uaminifu wake hana budi kuwa na maono ya ngazi tatu. Ngazi ya kwanza inajumuisha maono ya karibu yako – hii inajumuisha maono juu yako mwenyewe kwa maana ya unahitaji kuwa mtu wa aina gani, yapi unahitaji kuyakamilisha katika maisha yako kupitia kazi unayofanya. Ngazi ya pili inajumuisha maono ya kati – haya ni maono yako juu ya wafanyakazi wenzio au waajiriwa wako. Katika ngazi hii unatakiwa uwe na upeo wa kutambua mahitaji ya wanaokuzunguka kutoka kwako – nini hasa mchango wako kwa wale wanaokuzunguka. Ngazi ya tatu ni maono ya mbali – haya yanajumuisha ndoto zako. Ngazi hii inajumuisha mchango au mawazo yako ambayo unayatoa kwa taasisi au kampuni yako kwa ajili ya uendelevu wake. Kama mwajiriwa mwenye uaminifu unahitaji kuonesha ngazi za maono haya kupitia yale unayosema (mchango wako wa maneno), unayofanya (mchango wako wa vitendo) na jinsi unavyojihusisha na majukumu yako (kiwango cha ufanisi wako katika majukumu yako).

15. Wafanyakazi wengi katika ngazi za uongozi wa juu wanakosa uaminifu kwa vile wanashindwa kuwa na uwezo wa kuhimili misukosuko inayowakabili katika kazi zao. Hapa mwandishi anatushikisha kile ambacho mabosi wengi wanashindwa kutimiza kwa vile wengi wanakuwa ni waoga wa kusimamia maamuzi yao. Hili ni kosa ambalo linapoteza heshima kwa bosi yeyote yule kwa watu wake wa chini kwa vile ataendelea kuonekana hana msimamo katika maamuzi yake. Muda wote kama bosi watu wa chini yako wanahitaji wa kuone katika misingi ambayo haibadiliki mara kwa mara.

16. Watu wengi wanashindwa kueleweka kwa vile hawajui namna ya kuunda sentensi katika muuondo unaokubalika. Kwa ujumla ujumbe wowote ambao unatolewa kwa njia ya maandishi au maongezi ni lazima uhusishe muunganiko wa maneno ambayo kwa pamoja yanaunda sentensi ambazo nazo zinaunda haya za mada husika. Kwa mantiki hii kila neno katika stori na kila sentensi kwenye stori husika zinaunda mtiririko wa maana kwa msomaji au msikilizaji. Hivyo kila mwandishi au mzungumzaji hana budi kuzingatia utumiaji wa maneno na muunganiko wa sentensi zilizokamilika katika kila haya ya stori yake.

17. Njia nyingine ambayo inawafanya watu wengi washindwe kueleweka ni namna wanavyopangilia sentensi zao zenye maana hasi na chanya. Sehemu hii inahusisha mbinu za sentensi ipi kati ya chanya au hasi itangulie kwenye maongezi au maandishi ya mtoa stori. Mfano tazama sentensi kama hizi 1. “kazi yako ni nzuri japo kuna vitu unatakiwa kuviboresha”; 2. Kuna vitu unatakiwa kuviboresha japo unafanya kazi nzuri. Katika sentensi ya pili msikilizaji/msomaji atachukua maana ya mwisho ya sentensi na kuelewa kuwa anafanya kazi nzuri wakati katika sentensi ya kwanza msikilizaji/msomaji ataelewa kuwa pamoja na kufanya kazi vyema bado ana sehemu ambazo anahitaji kuboresha. Kama mwandishi au mtoa mada kwa njia ya maongezi ni lazima uwe tayari kutambua ni sehemu ipi kati ya sentensi chanya na hasi itangulie katika stori yako kwa ajili ya kufikisha ujumbe uliokusudiwa.

18. Watu wengi wanashindwa kuaminika katika jamii inayowazunguka kwa vile wanaishi katika falsafa ya kuamini kuwa wanafahamu kila kitu. Mwandishi anatushirikisha kuwa huu ni ugonjwa mwingine ambao unapoteza heshima kwa watu wengi kwa vile wanashindwa kufahamu kuwa katika maisha kila mtu anahitaji kujifunza kila siku kutoka kwa wanaomzunguka. Mtu anapoonekana kuwa yeye anafahamu kila kitu ni mara chache sana atachukulia kwa ukaribu maoni ya watu wanaomzunguka na hivyo kusababisha hasieleweke kwa jamii inayomzunguka.

19. Watu wengi wanapoteza heshima zao kwa vile wanatumia maneno ambayo yanaifanya jamii inayowazunguka hisipende matendo yao. Ni kawaida kusikia kusikia misemo kama “haijalishi kama wananipenda hama la cha msingi ni lazima waniheshimu”. Kiongozi anayetumia kauli kama hizi anakuwa sio mtu wa watu na badala yake anatumia mabavu kufanikisha majukumu yake kwa watu waliopo chini yake. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika jamii ni lazima kwanza uwekeze kwenye mtaji wa kijamii kwa maana yakujiweka karibu na watu wa karibu yako. Hii ni pamoja na kujihusisha kwenye matukio ya kijamii ambayo waajiriwa au jamii inayokuzunguka wanajihusisha nayo katika nje ya saa za kazi.

20. Watu wengi wenye taaluma za juu wamepoteza uaminifu/heshima kutokana na tabia mbaya wanazoishi katika jamii inayowazunguka. Mwandishi anatushirikisha kuwa tabia ya mtu ni utambulisho wa mhusika kwa jamii inayomzunguka. Unaweza kuwa na taaluma ya juu sana lakini kama hauna tabia njema kamwe hauwezi kupata heshima kwa jamii inayokuzunguka.

Haya ni machache ambayo nimeweza kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.

Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.

Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.

Born to Win ~ Dream Big 

Augustine Mathias Bilondwa

Namba ya Simu:      +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com


Mambo Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha Strong Mothers, Strong Sons: (Mama Bora, Mtoto wa Kiume Bora; Mwongozo kwa Akina Mama katika Kuwakuza Vyema Watoto wa Kiume)

Habari ya leo rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya 23 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi wa vitabu nikiwa na lengo kubwa la kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako kuyatumia ili ubadilishe kila sekta ya maisha yako.

Uamzi wa kubadilisha maisha yako upo mikononi mwako na hivyo kama mpaka sasa haujajifunza kitu chochote katika makala hizi nakushauri husiendelee kupoteza muda wako na badala yake ufanye mambo ambayo umezoea.

Ili uendelee kunufaika na makala za mtandao huu BONYEZA HAPA na ujaze fomu utakuwa umejiunga na mtandao wa fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa na mtandao wa fikra za kitajiri moja kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.

Kabla ya kuendelea kushirikisha uchambuzi wa kitabu cha leo nitumie muda huu kuomba radhi kwa kuchelewa kukutelea uchambuzi huu ndani ya wiki iliyoisha jana. Hii imetokana na sababu zilizo nje ya uwezo wangu kwa kuwa mazingira niliyopo kwa sasa hayana nishati ya umeme ya uhakika.

Kitabu cha wiki hii ni Strong Mothers Strong Sonskutoka kwa mwandishi Meg Meeker, M.D. Mwandishi Meg Meeker ni daktari wa binadamu na mzungumzaji/mhamasishaji mashuhuri kwenye masuala ya afya pamoja na uhusiano kati ya wazazi na watoto. Dr. Meg Meeker ni mama wa watoto watoto watatu ambapo kati yao wawili ni wa kike na mmoja ni wa kiume. Mwandishi ana uzoefu wa maisha ya ndoa kwa vile amefanikiwa kuishi na mme wake kwa zaidi ya miaka 30. Dr. Meg Meeker pia ni mwandishi wa Kitabu cha Strong Fathers, Strong Daughters ambacho anashirikisha nafasi ya baba katika kumuandaa mwanae wa kike ili awe mtoto bora na hatimaye mama bora kwa familia yake.


Mwandishi anatushirikisha kuwa shauku kubwa ya kuandika kitabu hiki ilitokana na uzoefu wake katika jamii kuwa akina mama wengi na watoto wao wa kiume wameingia kwenye mahusiano mabaya ya kutoelewana kwa vile hawatambui wajibu wao katika malezi ya watoto wa kiume. Mwandishi anatushirikisha kuwa mara nyingi akina mama wamekuwa na hasira na jinsia ya kiume kutokana na matendo maovu au manyanyaso ambayo wamewahi kutendewa na wanaume katika maisha yao. Hali hii imewafanya kupitisha hasira zao kwa watoto wao wa kiume pasipo wao kuelewa na matokeo yake watoto wanaanza kubadilika na kuwachukia mama zao. Hii inapelekea mtoto kubadilika kitabia kiasi ambacho hataki kusikiliza ushauri wa mama au baba.

Mtoto wa kiume anapokuwa katika hali kama hii inakuwa ni hatari zaidi kwake kutokana na ukweli kwamba; watoto wa kiume wana uwezekano wa kuwa na ulemavu wa kujifunza (kushindwa kujifunza) mara sita zaidi ikilinganishwa na watoto wa kike, ni mara tatu zaidi ya kujiunga kwenye vikundi vya madawa ya kulevya na mara nne zaidi ya kutambuliwa kama watoto wenye msongo wa mawazo.

Pia, watoto wa kiume wapo kwenye hatari kubwa ya kutawaliwa na tabia za wizi, ngono, ulevi, kukojoa kitandani, kujihusisha na makosa ya jinai na wapo kwenye asilimia kubwa ya kukumbwa na ajali za barabarani.  Yamkini ni akina mama wachache ambao wanafahamu kuwa wao ni nguzo namba moja katika kumkinga mwanae wa kiume dhidi ya tabia chafu na hatimaye kumkuza mwanae katika ili awe baba bora wa familia. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mama ana muda mwingi wa kuwa karibu na mtoto ikilinganishwa na baba. Katika kitabu hiki mwandishi anatoa mwongozo kwa akina mama kwa ajili ya kufanikisha malezi bora kwa watoto wa kiume.

Karibu tujifunze wote machache niliyojifunza kutoka kitabu hiki:

1. Wewe ni mtu wa kwanza wa kumuonyesha upendo. Mara nyingi ni kawaida kuona kuwa upendo wa mama kwa mtoto wake wa kiume haupimiki kwani mwanae ni zaidi ya mme wake. Ni kutokana na ukweli huu, katika kipindi cha ukuaji wa mtoto wa kiume, mama ana wajibu wa kuonesha kila aina ya upendo kwa mwanae na pengine akina mama wengi huwa wanatamani kuwa upendo huo uwe wa milele japo kutokana na maumbile ya kisayansi mtoto wa kiume anapopata mwenzi wake upendo wake kwa mama huwa unapungua. Katika kipindi hiki cha ukuaji mtoto wa kiume mara zote anaendelea kujifunza kutoka kwa mama yake ikiwa ni pamoja kuhitaji kila aina na faraja, furaha, hamasa na amani kutoka kwa mama yake. Hali hii inampa msingi bora katika maisha yake ya baadae dhidi ya mwenza wake na wanawake wote kwa ujumla na kinyume chake ni sahihi. Hii inatokana na ukweli kwamba akina mama wana muunganiko wa hisia mkubwa kwa watoto wao ikilinganishwa na akina baba.   

2. Mama hakikisha unampenda mwanao hata katika kipindi ambacho unaona tabia zake haziridhirishi. Mwandishi anatushirikisha kuwa mama ana nafasi ya kumrudisha mwanae wa kiume katika misingi ya tabia njema kama ataendelea kuonesha hali ya upendo kwa mwanae. Mara zote katika kumlea mtoto wa kiume mama unatakiwa kufahamu kuwa watoto wa kiume siyo wepesi wa kuzungumza matatizo yanayowakabili hivyo njia ya pekee ni kuhakikisha unamfahamu mwanao kwa undani zaidi. Wazazi wengi wameharibikiwa na watoto wao wa kiume kwa vile wametekeleza pindi wanapoona wamejiingiza katika makundi ya tabia mbaya. Kumbe wazazi wanasahahu kuwa katika kipindi hiki mzazi hasa mama anatakiwa kuonyesha upendo wa hali ya juu kwa mwanae wa kiume ikiwa ni pamoja na kumsaidia kuepukana na tabia mbaya au changamoto zinazomkabili. Hapa unatakiwa kukumbuka kuwa upendo wa mama kwa mwanae haupimiki wala kulinganishwa kulingana na hali iliyopo. Hii ndio njia pekee ya mtoto wako kuona kuwa anapendwa na ana wajibu wa kulipa upendo huo kwa wazazi wake kwa gharama yoyote.

3. Mama anapaswa kumfundisha mwanae misingi mitano ya fadhila ambayo ni (i) ujasiri – uwezo wa kufanya kitu kwa haki pasipo kujali wengine wanasema nini juu yake (ii) kiasi – uwezo wa kufanya vitu kwa kiasi pasipo kutawaliwa na tamaa za mwili (iii) haki – kufanya vitu pasipo kuvunja sheria au kuwaumiza wengine (iv) busara – uwezo wa kuishi maisha ya staha na tahadhari katika matendo, na (v) hekima – kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi makini pale inapotakiwa. Hivi ni vipaji ambavyo kila mama anapaswa kuhakikisha mwanae wa kiume anavipata kwani vipaji hivyo ni msingi wa mtoto kutambua yeye ni nani hasa katika kuishi maisha ya usafi wa moyo pamoja na kutambua kusudi la maisha yake. Na kadri mtoto atavyofundishwa vipaji hivi akiwa bado mdogo ndivyo atakuwa katika maisha ya furaha. Na hapa mtoto anatakiwa kufundishwa juu ya upendo kwa wengine kwa maana ya kwamba baada ya kupendwa na yeye anatakiwa kutambua wajibu wa kupenda wenzake na jamii kwa ujumla.

4. Mama mara zote kumbuka kuwa maneno mabaya unayonena kwa mwanao yaanacha makovu yasiyoponyeka. Kama ambavyo tumezoea kusikia sentensi ya “maneno uumba”, ndivyo mwandishi anatushirikisha kuwa endapo mtoto mara nyingi ataambiwa misamihati mibaya kama vile wewe ni mkorofi, mgomvi, mwizi, mchoyo, mjinga, mpumbavu na mengineyo ndivyo atakuwa akiamini kuwa hizo ndizo tabia zake halisi. Kutokana na ukweli huu mama ana nafasi ya kumjenga mtoto wa kiume kutoka kwenye tabia hasi kwa kumnenea misamihati yenye kumtia moyo mtoto ili abadilishe tabia zake kwa kadri anavyoongezeka umri.

5. Mama unahitaji kukumbuka kuwa una wajibu wa kumfundisha mwanao wa kiume misamihati ya hisia. Hapa tunafundishwa kuwa mama ana nafasi kubwa ya kutambua hisia za mtoto wa kiume kuliko ilivyo kwa baba mtoto. Hii ni pamoja na kutambua nyakati za furaha, hasira, msongo wa mawazo, huzuni au kuumizwa ambazo mwanae anapitia. Kutokana na ukweli huu, mwandishi anatushirikisha kuwa mama anapaswa awe mwalimu kwa mwanae wa kiume katika kumfundisha namna bora ya kutumia misamihati ya hisia. Hii ni pamoja na kumfundisha mwanae kutambua hisia zinazomkabili, jinsi ya kuonesha/kukabiliana na hisia husika pamoja na kumfundisha hatua zipi achukue kwa kila hisia pasipo kuumiza nafsi yake na jamii inayomzunguka. Mtoto ambaye amefundwa katika misingi hii ana nafasi kubwa ya kukabiliana na misukosuko ya mazingira yanayomkabili bila kukata tamaa.

6. Mama una nafasi kubwa ya kutatua hisia za mwanao wa kiume hasa ambazo zinapelekea aishi maisha ya huzuni unaosababishwa na historia ya maisha ya familia. Katika familia nyingi ni kawaida kukuta watoto wanateseka hasa kutokana na matendo ya wazazi wao ambayo pengine huwa yanapelekea wazazi kutalikia. Mwanandishi anatushirikisha kuwa watoto wa kiume mara nyingi huwa wanaumizwa na matendo ya baba zao kutokana na tabia mbaya za baba kiasi ambacho huwa wanaishi katika maisha ya upweke pamoja na kutokujiamini. Mama ana nafasi kubwa ya kuwajengea uwezo wa kukabiliana na tabia hii kwa kutumia maongezi ya mara kwa mara na mtoto wake. Katika maongezi haya mama anatakiwa afahamu chanzo halisi cha hisia zinazomkabili mwanae na hatimaye aanze kumsaidia kuepukana nazo kwa kadri awezavyo. Zoezi hili unatakiwa kulifanya mtoto angali bado mdogo.

7. Mara zote epuka kumkanya mwanao kwa kumpiga na badala yake unatakiwa umpe uelewa wa kwa nini hatakiwi kurudia makosa aliyofanya. Unapomuelewesha mtoto kwa njia hii inamsaidia kutambua kuwa alichofanya sio sahihi na hakikubaliki katika jamii. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mtoto wa kiume katika umri mdogo anakuwa hana uwezo wa kujidhibiti dhidi ya hisia zake kama vile hasira ambazo mara nyingi huwa zinamfanya apigane na wenzake. Hivyo, ili kuachana na tabia hii mtoto anahitaji kufundishwa kuwa anaweza kuishi na wenzake kwa upendo na anapotambua hili huwa inamjenga kisaikolojia na hivyo inakuwa sio rahisi kurudia makosa yake.

8. Tofauti kati ya mtoto wa kiume na mtoto wa kike ni kwamba watoto wa kike ni wazungumzaji wazuri wakilinganishwa na watoto wa kiume. Kutokana na ukweli tunashirikishwa kuwa watoto wa kiume ni wasiri wa matatizo yanayowakabili jambo ambalo hupelekea kugundua matatizo waliyonayo wakati yamekuwa sugu. Mwandishi anatushirikisha kuwa mama ana nafasi kubwa ya kutambua matatizo anayopitia mwanae wa kiume kwa kuhakikisha amejenga utaratibu wa kufanya mahojiano na mwanae mara kwa mara. Ili kufanikisha zoezi hili mama anatakiwa kujifunza kuwa msikilizaji badala ya kuwa mwongeaji. Kadri atakavyomsikiliza mwanae ndivyo atamfahamu kwa undani na hatimaye pindi mwanae anapokuwa katika hali tofauti inakuwa rahisi kumgundua mapema.

9. Ulimwengu umebadilika kiasi ambacho kuna kila aina ya uozo kama vile mapenzi ya jinsia moja kwa wanaume. Mwandishi anatushirikisha kuwa watoto wengi wa kiume wameangukia kwenye uozo wa namna hii kwa vile wazazi wengi hawana utaratibu wa kuwafahamu kwa undani watoto wao. Hali hii imepelekea watoto kugunduliwa wakati ambao tayari wameshaharibiwa. Kama mama ni lazima ufahamu kwa undani mwanao anapendelea michezo ya aina gani, sehemu anazopendelea kwenda, mapito yake wakati wa kwenda au kutoka shule pamoja na kuwafahamu kwa undani marafiki zake. Pia, mara nyingi unatakiwa kufahamu kuwa mtoto atabadilisha hobi kwa kadri siku zinavyoongezeka hivyo kadri anavyobadilisha hobi zake ndivyo unatakiwa kufahamu hobi zake mpya. Kwa ufupi; mama kwa kushirikiana na baba mna wajibu wa kumlinda mtoto dhidi ya maovu ya dunia hii na njia pekee ya kufanya hivyo ni kufahamu yapi anapendelea na yapi hapendelei.

10. Mambo ambayo yanakwamisha ukaribu wa mtoto na mama yake ni pamoja na ubize wa kufuatilia TV, kuchati kwenye mitandao ya kijamii, kuwa mkali pindi mtoto anapohitaji kuwa karibu na wewe au kumkatisha mtoto wakati anapokueleza jambo flani. Mwandishi anatushirikisha kuwa mama unahitaji kufahamu kuwa kadri mtoto wa kiume anavyokatishwa au kukosa muda wa kuwa karibu na wewe ndivyo itakuwia vigumu kumfahamu mwanao. Kama kweli unahitaji kuwa mama bora kwa mwanao wa kiume huna budi kuhakikisha unatenge muda wa saa moja kila siku kwa ajili ya mazungumzo na watoto wako hasa wa kiume. Saa moja au dakika chache kila siku zinaweza kubadilisha maisha ya mwanao kwa ujumla endapo umezitumia bila ya kuwa na mwingiliano wa majukumu mengine.

11. Kumbuka kuwa aibu kwa mwanao ni chanzo cha kutofahamu matatizo yanayomkabili. Mwandishi anatushirikisha kuwa kadri mtoto wa kiume anavyoongezeka umri ndivyo anapitia mabadiliko makubwa ya kimwili na tabia ikiwa ni pamoja na kuingia kwenye mahusiano. Muda huu mama unahitaji kuwa shupavu kumweleza ukweli juu ya mahusiano na watoto wa kike ili atambue mahusiano yapi yanamfaa. Hata hivyo ni akina mama wachache wenye ujasili wa kuzungumza na watoto wao wa kiume masuala ya kimahusiano hasa kwa kuzingatia tofauti za jinsia. Pamoja na tofauti hizo bado mama unatakiwa kutafuta lugha nzuri ya kumfunda mwanao kwenye masuala ya mahusiano pamoja na undani wa mapenzi.

12. Mama mpe hamasa mwanao kushiriki mazoezi ya viungo. Mazoezi ni njia nzuri ya kumfanya mwanao wa kiume hasiwe na muda wa kufanya au kuangalia vitu vya hovyo kwenye mtandao wa intaneti. Mwandishi anatushirikisha kuwa kadri kijana wa kiume anavyokaa bila mazoezi ya viungo ndivyo anavyokuwa anatengeneza nguvu ambazo ni sawa na bomu ambalo litalipuka wakati wowote. Na mara nyingine bomu hilo huwa linalipuka kwenye matumizi mabaya ya nguvu zake ikiwa ni pamoja na kujihusisha kwenye masuala ya ngono, ulevi au madawa ya kulevya. Kutokana na ukweli huu mama huna budi ya kuhakikisha mwanao ana ratiba ambayo haimpi muda wa kukaa kizembe pasipo kuwa na shughuli anayojihusisha nayo.   

13. Kuna muda ambao mama mwanao wa kiume atakutangazia uadui kati yake na wewe. Mara nyingi ugomvi huu huwa unaanza katika kipindi cha kubarehe kwa vile mtoto anakuwa katika hali ya kulinda maovu yake ili yaonekane ni kitu cha kawaida kwa mama yake. Hii inatokana na mabadiliko ya tabia anayopitia katika ukuaji wake. Hata hivyo, katika nyakati hizi mama hautakiwi kukata tamaa dhidi ya mwanao kwani ndani ya uadui huo kuna tumaini ndani yake endapo hautanyosha mikono dhidi ya mwanao. Katika hali hii, mama unatakiwa kwanza ufahamu mazingira anayopitia mwanao ikiwa ni pamoja na kutambua kuwa hata kama akisema kuwa hufahi kuwa mama yake bado haina maana kuwa ameondoa penzi lako kwake.

14. Watoto wa kiume wana tofauti ya kimaumbile na kimajukumu ikilinganishwa na mama zao. Mama anatakiwa kutambua kuwa mtoto wa kiume anafahamu tofauti iliyopo dhidi ya mama yake hata akiwa na umri mdogo wa miaka miwili. Kutokana na tofauti hizi kadri mtoto wa kiume anavyoongezeka umri ndivyo ukaribu wake na mama unavyozidi kupungua. Matokeo yake ni kwamba kadri umri unavyoongezeka ndivyo mtoto wa kiume anahitaji afanye maamuzi yake pasipo kuingiliwa na mama yake akidhania kuwa yeye ni mwanaume na anaweza kufanya jambo lolote bila ya ridhaa ya mtu mwingine. Kutokana na ukweli mama unahitaji kutambua tofauti hizi za asili na kuhakikisha unatafuta njia nzuri za kuendelea kumfunda mwanao katika hali tulivu.

15. Kuna umri ambao mama unahitaji kumfanya mwanao aondoe hisia zake kwako. Mara nyingi tumezoea kusikia msemo wa “mtoto wa mama”, hapa ndicho mwandishi anatushirikisha kuwa kama mtoto wa kiume ataendeleza hisia zake kwa mama itamuwia vigumu kudumu na mwenza wake katika maisha yake ya baadae. Hivyo, kama mama unatakiwa kumuongoza mwanao katika kipindi hicho cha mpito kwa ajili ya kufanikisha maisha yake ya baadae ili hatimaye mwanao awe baba bora wa familia yake.

16. Mama ni faraja kwa mwanae wa kiume. Hii haijalishi mwanao ana umri gani kwani katika kila hatua mtoto wa kiume anahitaji faraja kutoka kwa mama yake. Hata katika nyakati ambazo atakuwa ameoa bado mtoto wa kiume anahitaji faraja ya mama yake. Hii inatokana na ukweli kwamba katika ukuaji, mtoto wa kiume kuna mambo mengi ya kipekee ambayo uyapata kutoka kwa mama kiasi ambacho hawezi kuyapata sehemu yoyote ile. Kwa ufupi ni kwamba mama afananishwi na mtu mwingine na hivyo huu ni muunganiko tosha wa faraja ya mama kwa mtoto wa kiume katika kipindi chote cha maisha ya wawili hawa.

17. Wewe ni sehemu pakee ambayo mwanao wa kiume atapa msingi/mizizi imara. Kumbuka kuwa kama nyumba imejengwa juu ya msingi imara daima itadumu na kinyume chake ni kwamba kama nyumba imejengwa juu ya msingi dhaifu haiwezi kudumu. Pia, tunaweza kusema kuwa mama ni mhusika mkuu wa kuandaa mizizi imara ya mwanae wa kiume. Kumbuka kuwa kama mmea hauna mizizi imara hauwezi kustawi wakati wa dhoruba kama jua kali au wakati wa upepo mkali. Mwandishi anatushirikisha kuwa mama ni muhusika mkuu wa kumuandaa mwanae wa kiume ili apate kila aina ya mafanikio katika jamii inayomzunguka pasipo kujali changamoto atakazokabiliana nazo.

18. Mama ana nafasi kubwa ya kumfanya mtoto wa kiume atambue kusudi la maisha yake. Kumbuka kuwa watu wengi wapo jinsi walivyo kutokana na mchango mkubwa wa makuzi na malezi waliyopata katika enzi za ukuaji wao. Kwa maana hii, mama ana nafasi kubwa ya kumuongoza mwanae ili atambue wajibu wake katika ulimwengu huu. Mara nyingi baba huwa ni rahisi kumuongoza mwanae katika kazi zile ambazo sana sana zinahusisha matumizi ya nguvu ambazo pia utegemea majukumu ya baba. Lakini kwa upande wa mama wewe una nafasi kubwa ya kumuandaa mwanao katika ulimwengu wa kiakili, kiroho na kijamii. Hii haimaanishi kuwa baba hapaswi kujihusisha katika kumuandaa mwanae katika sekta hizi bali ukweli huu unatokana na maumbile ambayo akina mama wamejaliwa kuwa na hisia nyingi ikilinganishwa na akina baba. Hivyo mama una wajibu wa kutumia hisia zako kuhakikisha unamfunda mwanao kuwa hakuja duniani humu kwa bahati mbaya bali amekuja kukamilisha kazi ya wito wake. Hivyo kama mama bora hakikisha unamsaidia mwanao atambue vipaji vyake na namna ya kutumia vipaji hivi ili maisha yake yawe na msaada kwa jamii inayomzunguka.

19. Mfundishe mwanao misingi ya maisha kama vile kukubalika, kusamehe na kuvumilia. Kama ambavyo tunafahamu kuwa katika ulimwengu huu siku zote mambo hayawezi kwenda kama tunavyotarajia kwani kuna nyakati mambo yataenda kinyuma na matarajio. Mama unahitaji kumfunda mwanao wa kiume ili siku zote afahamu wazi juu ya ukweli huu na hatimaye abadilike kulingana na hali iliyopo. Hii ni pamoja na kumfundisha mwanao kuwa na roho ya kusamehe na kusahau kwa ajili ya kutoa nafasi ya kuanza upya katika maisha yake.

20. Mfundishe mwanao wa kiume kuwa kuna nguvu kubwa kuliko viumbe vyote kwa maana ya elimu ya dini. Mwandishi anatushirikisha kuwa mtoto wa kiume anahitaji kujifunza juu ya uwepo wa Mungu kutoka kwa mama yake. Mfanye mwanao aisome sura ya Mwenyezi Mungu kutoka kwenye uso wako. Kama wewe ni furaha muda wote mtoto atajua kuwa Mwenye Mungu ni mwingi wa furaha na hatimaye mtoto huyu naye atatamani kuwa na furaha kama Mungu alivyo. Kumbuka kuwa kama wewe unabadilika badilika mara kwa mara ndivyo mwanao atatafsri kuwa na Mungu yupo katika hali kama hiyo. Hapa una jukumu la kumfundisha mwanao kadri atavyokuwa anaoongezeka umri juu ya ukamilifu wa Mungu.

21. Kadri mwanao anavyoongezeka umri unahitaji kumsaidia kujibu maswali juu ya uwepo wa Mwenyezi Mungu. Kutokana na asili ni kawaida kukuta kuwa watoto wanauliza hivi Mungu yupo? Je Mungu anafanana je? Je mungu anapenda watoto? Mungu anakaa wapi? Haya ni baadhi ya maswali ambayo mara nyingi kila mtoto anatamani kufahamu kwa ajili kumfahamu Mungu kwa undani. Kama mzazi unahitaji kutumia muda wako kumpa majibu ya maswali kwa kadri atakavyokuwa anakuuliza. Majibu ya maswali haya yanamjengea msingi imara mwanao kwenye misingi ya imani na hatimaye kumfahamu na kumtumikia Mwenyezi Mungu.


Haya ni machache ambayo nimeweza kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.

Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.

Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.

Born to Win ~ Dream Big 

Augustine Mathias Bilondwa

Namba ya Simu:      +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com

Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com

Mambo Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha A Brief History of Humankind (Historia Fupi ya Mwanadamu)

Habari ya leo rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya 22 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi wa vitabu nikiwa na lengo kubwa la kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako kuyatumia ili ubadilishe kila sekta ya maisha yako.

Uamzi wa kubadilisha maisha yako upo mikononi mwako na hivyo kama mpaka sasa haujajifunza kitu chochote katika makala hizi nakushauri husiendelee kupoteza muda wako na badala yake ufanye mambo ambayo umeyazoea.

Ili uendelee kunufaika na makala za mtandao huu BONYEZA HAPA na ujaze fomu utakuwa umejiunga na mtandao wa fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa na mtandao wa fikra za kitajiri moja kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.

Kabla ya kuendelea kushirikisha uchambuzi wa kitabu cha leo nitumie muda huu kuomba radhi kwa kuchelewa kukutelea uchambuzi huu ndani ya wiki iliyoisha jana. Hii imetokana na sababu zilizo nje ya uwezo wangu kwa kuwa mazingira niliyopo kwa sasa hayana nishati ya umeme ya uhakika.

Kitabu cha wiki hii ni A Brief History of Humankindkutoka kwa mwandishi Yuval Noah Harari. Mwandishi ametumia anatumia kitabu kwa ajili ya kutushirikisha matukio muhimu katika historia ya mwanadamu. Kupitia kitabu hiki utagundua kuwa kadri nyakati zinavyobadilika ndivyo mwanadamu amekuwa akipitia kwenye mabadiliko mengi ya kimwili, kiakili na kimaendeleo. Mabadiliko haya yamepelekea binadamu kukabilia na mazingira kwa mbinu tofauti kulingana na changamoto anazokabiliana nazo kwa wakati husika.

Kwa ujumla, tunafahamu kuwa hapo zamani yapata miaka bilioni 13.5 iliyopita muunganiko wa maada (matter) na nishati kwa uwepo wa muda (time) flani na nafasi (space) kwa pamoja viliunda umbo ambalo lijulikanalo ‘big bang’. Historia ya tukio hili ndiyo inatupa sayansi ya fizikia (Physics).

Miaka 300,000 tangu kuumbwa kwa umbo hilo; maada na nishati vilianza kuunda maumbo yaliyojulikana kama atomi (atoms) ambazo kwa pamoja ziliunda molekuli (molecules). Historia ya tukio hili ndiyo inatupa sayansi ya kemia (Chemistry).  

Miaka bilioni 3.8 iliyopita katika sayari ya ijulikanayo kama Dunia, molekuli ziliungana kuunda maumbo yajulikanayo kama viumbe. Historia ya tukio hili ndio inatupa sayansi ya biolojia (biology).

Yapata miaka 70,000 iliyopita, viumbe katika kundi/aina (species) ya Homo sapiens (hili ndilo jina la kisayansi la binadamu) walianza kuunda miundo ya kipekee ijulikanayo kama tamaduni. Hatimaye maboresho ya matukio ya tamaduni katika nyakati tofauti ndiyo yakatupa msamiati wa neno “Historia”. Hapa ndipo tunaanzia kwa ajili ya kuona historia ya mwanadamu.
Kwa ujumla historia ya mwanadamu inagawanyika katika makundi matatu ambayo ni (a) mapinduzi ya utambuzi (Cognitive revolution) ambayo yalianza yapata miaka 70,000 iliyopita, (b) mapinduzi ya kilimo (agricultural revolution) ambayo ni yapata miaka 12 elfu iliyopita na (c) mapinduzi ya kisayansi (scientific revolution) ambayo yalitokea yapata miaka 500 iliyopita. Kwa kifupi kitabu hiki kinaelezea namna ambayo mapinduzi haya kwa pamoja yalivyoathiri maisha ya mwanadamu na mazingira yanayomzunguka kwa ujumla.

Karibu tujifunze wote machache niliyojifunza kutoka katika kitabu hiki:

1. Historia ya mwanadamu inaanzia katika kipindi ambacho mwanadamu alikuwa ni mnyama hasiye na manufaa. Historia ya mwanadamu inaanzia katika kipindi ambacho mwanadamu aliishi katika koo ambazo alikaa katika familia za msituni sawa na wanyama wengine kama sokwe mtu, nyani, tembo na wengineo. Katika kipindi hiki mchango wa mwanadamu katika kuboresha mazingira yanayomzunguka haupo kabisa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba katika kipindi hiki mwanadamu aliyategemea mazingira yamtunze kwa asilimia mia moja pasipo yeye kujishughulisha. Hii inajumuisha yeye kuishi kwenye mapango pamoja na kutegemea mizizi na matunda kama chakula chake. Jambo muhimu la kukumbuka ni kwamba kinachomtofautisha mwanadamu na wanyama wengine ni uwezo wake mkubwa wa kufikiri. Na hii ni sifa ya kipekee ambayo inawaunganisha wanadamu wote pasipo kujali rangi au matabaka yao. Sifa hii ndio ilimwezesha mwanadamu kuanza maisha ya kuboresha mazingira kutoka kwenye kula vyakula vibichi mpaka kwenye ugunduzi wa moto.

2. Kadri nyakati zilivyopita ndivyo ubongo wa mwanadamu uliboreshwa kupitia vinasaba na hivyo kupitishwa kizazi kimoja hadi kingine. Katika sayansi kupitia jeni (genes) vizazi vipya vinarithishwa ubongo ulioboreshwa na hatimaye kufanikisha maisha ya mwanadamu kuboreshwa kizazi kimoja hadi kingine. Ni kupitia sayansi hii tunaona mwanadamu alivyoanza ugunduzi katika mazingira yake ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya kujisitiri (nguo), usafiri (uvumbuzi wa magari na boti) na mawasiliano. Uvumbuzi huu kuna ukweli kuwa umewezeshwa na uwepo wa lugha ya mawasiliano kwani tofauti na mawasiliano/sauti za wanyama wengine lugha ya wanadamu inaweza kuundwa katika maneno ambayo kwa pamoja yanaunda sentensi na sentensi hizo zinawezesha mazungumzo kati ya mtu mmoja na mwingine na hatimaye kwa pamoja wanaafikiana juu ya mada husika. Pia, lugha ya mwanadamu ina upekee wa kuweza kuongelea juu ya vitu ambavyo mwanadamu hajawahi kuona, kugusa au kunusa.

3. Hatuwezi kufahamu asili, historia na saikolojia yetu pasipo kufahamu kwa undani maisha ya chimbuko letu ambalo kwa imani ni Adam na Hawa. Katika historia hii tunafahamu kuwa mwanadamu alipitia katika kipindi cha kutangatanga kwa kutegemea nyama, matunda na mizizi. Baadae mwanadamu akaingia katika kipindi cha kutegemea kilimo na ufugaji na kipindi hiki wanasaikolojia wanasema kuwa ni kilikuwa na mchango mkubwa kwenye masuala ya kijamii na saikolojia ya mwanadamu wa sasa. Mpaka sasa tunazungumzia mapinduzi ya viwanda, teknolojia ya habari na mawasiliano kama sehemu ya mafanikio ya mwanadamu ambayo amepitia tokea kuumbwa kwake. Hata hivyo pamoja na maendeleo haya mwandishi anatushirikisha kuwa bado binadamu wa sasa pamoja na kuwa umiliki wa rasilimali fedha, vitendea kazi na kila kitu lakini bado binadamu huyu hana furaha na mazingira yake ikilinganishwa na binadamu wa enzi za kutegemea mazingira kwa asilimia mia.

4. Mtawanyiko wa watu katika maeneo mengi hasa ambayo yamezungukwa na maji hapo awali ilikuwa vigumu kwa mwanadamu kufikia maeneo hayo. Ili kufikia maeneo hayo na kuweza kuyageuza mwanadamu alijifunza ujuzi wa kutengeneza boti ambazo zilimwezesha kufika kwenye maeneo ya visiwa vingi kama Madagascar na bara la Australia. Kadri mwanadamu alivyozidi kufungua makazi mapya katika katika maeneo yaliyofichika ndivyo pia alianza uharibifu wa mazingira ikiwemo kusababisha kutoweka baadhi ya viumbe kama wanyama wakali na mimea. Kutoweka kwa viumbe hawa pia kulichangiwa na mabadiliko ya asili ya tabianchi katika maeneo mengi ikiwa ni pamoja na tabia za viumbe husika hasa kwenye uwezo wao wa kuzaliana na muda wa kubeba mimba.

5. Mapinduzi ya kilimo na ufugaji yalilenga kuongeza shibe ya chakula hasa mizizi, nafaka, matunda na wanyama wa kufugwa kwa ajili ya uhakika wa nyama. Mazao mengi yaliyolimwa enzi hizo hadi sasa yanalisha idadi kubwa ya watu ni pamoja na mazao ya nafaka kama ulezi, mtama, mahindi na viazi mviringo. Wanazuoni kwa pamoja wanakubaliana kuwa mapinduzi ya kilimo yalikuwa ni hatua moja mbele katika historia ya mafanikio ya mwanadamu. Hii inadhihirisha namna ambavyo mwanadamu ameweza kuendelea kwa kutumia uwezo wa ubongo wake kutokana sheria ya asili ya kupitisha jeni (genes) nzuri pekee kutoka kizazi kimoja cha mwanadamu hadi kingine. Kadri uzalishaji ulivyoongezeka ndivyo na idadi ya watu iliongezeka kutokana na ukweli kwamba wakati wa shibe watoto wa kike wana nafasi kubwa ya kupevuka mapema na hivyo kuzaa mapema ikilinganishwa na wakati wa chakula kisichotosheleza.

6. Mapinduzi ya kilimo na ufugaji yalimwezesha mwanadamu kuanzisha makazi ya kudumu na hivyo kuepuka kuhama hama kwa ajili ya kutafuta chakula. Matokeo yake ilikuwa ni kuanzisha kazi za usanifu wa majengo kwa kutumia mawe na matope kwa ajili ya kujisitiri. Hii ilianzisha jamii nyingi kuanza kuishi katika familia zaidi na kuepuka maisha ya kuishi kama kundi moja. Hatua hii ilimwezesha mwanadamu aendeleze ugunduzi hasa uliojikita katika kuboresha mazingira yake pamoja na kuboresha mfumo wa kilimo na ufugaji. Mfano, mwanadamu alianza kujenga nyumba kwa ajili ya kuishi pamoja na kuanza kutumia wanyamakazi kwa ajili ya kuongeza ukubwa wa eneo linalolimwa pamoja na kuongeza uzalishaji wa mazao. Ni katika kipindi hiki pia mwanadamu alianza kujiwekea akiba kutokana na kutokuwa na uhakika wa misimu inayofuatia katika uzalishaji wa mazao. Uzalishaji wa mazao na mifugo kadri ulivyoongezeka ndivyo mwanadamu alianza kuwekeza kwenye ugunduzi wa vyombo vya usafirishaji na hatimaye kukua maeneo ya biashara ambayo yalikuwa katika miji na hatimaye kuwa majiji.

7. Kadri uzalishaji ulivyoongezeka ndivyo tabaka ya watawala (machifu) pamoja na dini zilivyoongezeka. Hii ilipelekea kuanzishwa kwa watawala katika sehemu mbalimbali na hivyo suala la kujilinda dhidi ya watawala wengine likaanza kupewa nafasi. Hii ilipelekea uhitaji wa kutunga sheria na kuhakikisha kila mwanajamii ndani ya utawala wake analinda na kutii sheria husika. Sheria hizi zilianzisha matabaka ya watala na wataliwa na hivyo uwepo wa watendewa kazi na watumishi. Mara nyingi sheria hizi zilizirithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine na hivyo kulazimisha umuhimu wa kutunza kumbukumbu muhimu kwa mwanadamu. Hii ilipelekea mwanadamu kuanza kuwekeza kwenye mifumo yauwekaji wa kumbukumbu kwa kutumia mfumo wa maandishi na hivyo kuwalazimisha wanadamu kuanza kujifunza kusoma na kuandika. Hatimaye hii ilipelekea mwanadamu kuanzisha mawasiliano kwa njia ya namba hivyo kupelekea kuanzishwa kwa mahesabu kwa ajili ya sayansi.

8. Historia haineshi uwepo wa usawa katika makundi ya mwanadamu. Mwandishi anatushirikisha kuwa historia ya mwanadamu inaonesha kuwa yalikuwepo makundi wa watu wa ngazi ya juu, kati na chini. Watu wa ngazi ya juu walineemeka na matunda ya uzalishaji kutoka kwa watu wa tabaka la chini na kati. Hii ilipelekea kuanzishwa kwa tabaka la watumwa ambalo lilitumikishwa kufanya kazi zote kwa ajili ya watu wa tabaka tawala. Hii iliendelea kuweka matabaka mengi katika jamii, mfano matabaka kati ya, wanaume na wanawake, watu weupe na weusi au matajiri na masikini. Kwa ujumla chanzo cha matabaka haya ilikuwa ni uongo ambao uliwekwa na watu wachache kwa ajili ya kujinufaisha wao wenyewe huku wakiendelea kuwakandamiza wengine.  

9. Baada uonevu wa muda mrefu kati nusu ya karne ya 20 wanazuoni walianzisha kampeni za kuwa binadamu wote ni sawa. Kampeni hizi ziliambatana na uenezaji wa dini katika maeneo mengi. Kampeni hizi zilionyesha kuwa kila tamaduni katika jamii husika ilikuwa na thamani yake, miiko na tamaduni hizi zinabadilika kulingana na nyakati. Pamoja na kwamba mwanadamu amekuwa na lengo la kutengeneza jamii moja kubwa yenye tamaduni zinazofanana, jitihada hizo zimekuwa zikigonga mwamba kwani kila anapokaribia kwenye lengo ndivyo tamaduni nyingine kubwa zinaibuka. Jitihada hizi zinahusisha nguvu ya dini, lugha na siasa katika kuunganisha watu wa matabaka mabalimbali.

10. Kuanzishwa kwa matumizi ya madini ya dhahabu kama kitu chenye thamani kwa ajili ya kubadilisha na bidhaa/huduma nyingine kulileta mabadiliko makubwa katika historia ya maendeleo ya mwanadamu. Hapa ndipo sarafu ya dhahabu ilipoanza kuamua nguvu ya uchumi kwani ilikuwa ni msingi wa kuuza na kununua. Matokeo yake ikawa ni kukinzana kwa wafuasi wa dini kubwa mbili kati ya Wakatoliki na Waislamu hasa kutokana na utofauti wa sarafu zilizotengenezwa na pande hizo mbili kwa wakati huo. Sarafu iliwezesha ukuaji wa uchumi katika maeneo mengi kwani iliweza kuondoa mapungufu ya biashara ya kubadilishana bidhaa kwa bidhaa au huduma na huduma.

11. Fedha ni zaidi ya sarafu au noti za benki kwani kwa ujumla fedha inahusisha thamani ya kila ya kitu ambacho watu wapo tayari kutumia kwa ajili ya kupata kitu kingine na hatimaye kufanikisha kubadilishana vitu na huduma nyingine. Kwa maana hii fedha inawezesha watu kulinganisha thamani ya bidhaa/huduma. Kwa maana hii fedha katika mfumo wa sarafu au noti ni sehemu ndogo ya thamani ya fedha zilizopo kwani fedha nyingi ipo katika mfumo wa namba na wala sio keshi (noti au sarafu). Fedha inafanya kazi katika mfumo wa fikra ambao watu wamejiwekea juu ya fedha na mfumo huo umejengwa juu ya msingi wa uhaminifu kati ya pande mbili husika. Kwa ujumla katika historia ya maendeleo ya mwanadamu fedha ilikuwa na mchango mkubwa wa kuwaunganisha watu kutoka pande mbalimbali pindi walipofanya biashara.

12. Fedha ilifanikisha uwepo wa Himaya mbalimbali katika historia ya maendeleo ya mwanadamu. Kwa ufupi Himaya ni aina ya Serikali yenye utawala, wataliwa, mipaka pamoja na tamaduni zake ambazo utumika kama utambulisho wa Himaya husika. Watawala wa Himaya hizi wengi wao walikuwa na mfumo wa uongozi wa kidektaita japo zipo nyingine ambazo ziliongozwa kwa mfumo wa kidemokrasia. Mfano wa Himaya za kidemokrasia ni kama Himaya ya Uingireza. Kwa ujumla Himaya hizi zilikuwa na mchango mkubwa katika historia ya mwanadamu kwani zilisaidia kuwaleta pamoja watu tofauti na hatimaye watu hawa wakafanya kazi chini sheria za Himaya yao.

13. Tukiacha mchango wa fedha pamoja na Himaya katika kuunganisha watu, Dini pia ilikuwa na mchango mkubwa wa kuunganisha watu matabaka, koo, sehemu na rangi tofauti. Tofauti na dini ya siku hizi ambayo kwa kiasi imekuwa ni chanzo cha kuwatengenisha watu kulingana na imani zao, katika historia ya mwanadamu dini ilikuwa na mchango mkubwa kwani ilifundisha watu kuwa watiifu wa sheria zilizopo pamoja na watu wenye mamlaka. Mchango mkubwa wa dini ulikuwa wa kufundisha watu kuwa kuna nguvu kubwa iliyoko juu yenye mamlaka kuliko wanadamu wote. Pia, kupitia mafundisho hayo watu walihamasishwa juu ya umuhimu wa kuishi maisha ya upendo, amani na usawa pasipo kujali matabaka wala rangi zao kwani Mungu ni mmoja na Mungu ni Upendo. Kwa maana hii hauwezi kutaja maendeleo ya mwanadamu pasipo kutaja mchango wa dini ya Ukristu na Uislamu.

14.  Biashara ya bidhaa na huduma, Himaya na Dini kwa pamoja vilitoa mchango mchango mkubwa wa ukuaji wa uchumi wa mwabanadamu. Mwandishi anatushirikisha kuwa Mtawala Costantine wa Himaya ya Roma baada ya kugundua kuwa Himaya yake ilikuwa na watu wenye matabaka na imani tofauti aliamua kuchagua Ukristu kuwa dini ya Himaya yake. Hapa ndipo tunaona kuwa Himaya ya Roma ilifanikiwa kuwa Himaya yenye nguvu kubwa kiuchumi kwa muda mrefu kwa vile watu wake walikuwa chini ya msingi wa Imani moja.

15. Hatuwezi kuzungumzia historia ya maendeleo ya binadamu pasipo kuangalia mchango wa Mapinduzi ya Sayansi (The Scientific Revolution). Mapiinduzi ya Sayansi kwa kiasi kikubwa yamebadilisha uso wa Dunia hii pamoja na viumbe vyote vilivyomo kiasi ambacho mtu aliyekufa kabla ya mapinduzi haya akifufuka kwa sasa anaweza kuuliza kuwa hapa peponi au kuzimu. Hii ni kutokana na mabadiliko makubwa ambayo mwanadamu ameyafanya kupitia ugunduzi wa kisayansi na hatimaye kufanikisha uwepo wa vitu vipya katika mazingira yanayomzunguka ikiwa ni pamoja na maendeleo katika afya ya mwanadamu. Mapinduzi haya yameambatana na ongezeko la binadamu katika Dunia. Siri kubwa ya mapinduzi ya kisayansi imekuwa ni uwekezaji mkubwa wa rasilimali katika tafiti mbalimbali. Kutokana na ukweli huu mataifa ambayo yamewekeza sana kwenye tafiti yamefanikiwa kupiga hatua kubwa kiuchumi na hatimaye kufanikisha mabadiliko ya maisha ya mwanadamu na mazingira yake.

16. Fedha imekuwa na mchango mkubwa katika kujengeka kwa Himaya nyingi lakini pia fedha hizo zimekuwa ni chanzo cha kuanguka kwa baadhi ya Himaya. Mwandishi anafafanua kwa kueleza kuwa katika Himaya nyingi kadri uchumi ulivyoongezeka ndivyo na idadi ya watu ilivyoongezeka mara dufu na matokeo yake uchumi wa Himaya husika uliendelea kudumaa na pengine kushuka kabisa. Kinyume na siku za nyuma kwa sasa fedha imetengenezwa kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa ni kipindi cha nyuma kwa vile siku hizi kuna uwezekano wa kutumia kipato chako cha siku zijazo katika matumizi au mipango yako ya sasa (mikopo ya muda mrefu). Msingi wa mafanikio haya umetokana na uaminifu katika nyakati zijazo, kwa maana nyakati zijazo zinaaminiwa kuwa zitakuwa na rasilimali za kutosha kwa ajili ya kuwezesha watu wote kuishi maisha mazuri pasipo kuumizana mmoja baada ya mwingine.

17. Mapinduzi ya mtaji (capitalism) yamefanikisha mapinduzi katika sekta ya viwanda na hivyo kubadilisha sura nzima ya maisha ya mwanadamu na mazingira yake. Hata hivyo ni lazima tukumbuke kuwa ili viwanda viendelee kuzalisha ni lazima pawepo malighafi na nishati. Hivyo endapo malighafi na nishati vikiisha viwanda hivi havitakuwa na msaada katika maendeleo ya mwandamu. Hata hivyo mwanadamu ameendelea kuwa mbunifu kwa wa ajili ya kuepuka upungufu wa malighafi na nishati ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa panakuwepo mbadala wa nishati au malighafi katika uzalishaji wa bidhaa za viwandani.

18. Mapinduzi ya viwanda yameambatana na uharibifu wa mazingira na hivyo kusabisha kutoweka kwa viumbe wa baharini na nchi kavu. Mwandishi natushirikisha kuwa kadri maendeleo yalivyozidi kushika kasi ndivyo uso wa dunia umeendelea kupoteza ukijani wake na kugeuzwa sehemu ya mavumbi na majumba. Uharibifu huu umepelekea mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaendelea kuhatarisha afya na uhai wa mwanadamu.

19. Pamoja na maendeleo ambayo yameshuhudiwa katika miaka 500 iliyopita bado mwanadamu wa sasa ameendelea kuishi maisha yasiyo na furaha ikilinganishwa na binadamu wa kale. Hii ni kutokana na ukweli kwamba furaha ya mwanadamu ina uhusiano mkubwa na hisia zake juu ya yeye mwenyewe pamoja na mazingira yake. Mara nyingi katika jamii watu wameshindwa kuwa na furaha kwa kuhusisha mahitaji yao na furaha. Kwa maana nyingine watu wamekuwa wanaishi maisha ya sasa kwa huzuni wakitegemea kuwa wakipata vitu flani katika maisha yao ndipo wataishi maisha ya furaha. Huu ni ushahidi tosha kuwa kuna uwezekano mkubwa binadamu wa kale ambaye alitegemea mazingira kwa kila kitu aliishi maisha ya furaha ikilinganishwa na binadamu wa sasa.

20. Binadamu kama viumbe wengine wanaoongozwa na sheria za asili. Pamoja na maendeleo ambayo mwanadamu amefanikiwa kuyapata katika historia yake bado kuna mipaka ya asili ambayo itaendelea kumuongoza yale anayofanya. Pamoja na uvumbuzi wa kompyuta na mwendelezo wa mwanadamu kutaka kuumba vitu bado kuna akili ambayo ipo juu ya uwezo wake. Ndio maana binadamu amefanikiwa kutengeneza roboti na anaendelea na tafiti za kuunganisha kompyuta na mfumo wa fikra za binadamu lakini bado hakuna dalili kuwa binadamu atafanikiwa kugundua chanzo halisi cha uhai.

Haya ni machache ambayo nimeweza kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Hakika nilichokushirikisha hapa ni sawa na robo ya kile ambacho mwandishi anatushirikisha kwa ajili ya ukuaji wa kiroho. Kwa maana hii nakushauri usome nakala ya kitabu hiki kwa ajili ya kujifunza mengi zaidi. Kupata nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.

Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.

Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.

Born to Win ~ Dream Big 

Augustine Mathias Bilondwa

Namba ya Simu:      +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com